Tuesday, December 1, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA KUMI NA NNE

 DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



SEHEMU YA KUMI NA NNE!!
"Lakini Ally mpenzi wangu nimefanyaje?" Salma aliuliza kwa masikitiko makubwa huku akionekana kuumia baada ya kusukumwa.
"Unajifanya hujui siyo tena usiniite mpenzi wako kuanzia hivi sasa, we wa kunifanya mimi mtumwa wa ngono hadi umesababisha nisioe wakati natakiwa kuwa na familia sasa hivi" Ally alifoka.
"Ally nakupenda ndiyo maana nimefanya hivyo hadi nikazaa na wewe" Salma akaongea huku akilia.
"Weee tena ishia hapo hapo" Ally alimkaripia huku akimuongeza teke la mguu Salma.
"Ally nikatae ila ukae ukijua Hamida siyo mtoto wa mume wangu bali ni damu yako, ndiyo maana hata alipozaliwa kaka yako alikutania umefanana naye miguu ila ukweli ile ni damu yako kabisa" Salma aliongea huku akilia, Ally alipuuza maneno ya Salma akaondoka eneo akimuacha akilia ingawa kuna jambo lilikuwa likiisumbua akili baada ya kusikia maneno hayo.



****


"  "Ally huyu mtoto kafanana na wewe hiyo miguu balaa ingawa ana sura ya mama yake na baba yake" Shafii aliongea huku akicheka.
"Haaaa! Shemeji nawe waanza kwahiyo waataka sema kafanana na babaye na Ally pamoja nami" Salma alisema huku akimtazama Shafii.
"Ndiyo hivyo ahemeji" Shafii alisema.
"Wewe Chumbio waleta zako sasa huoni kama hiyo miguu ni ya mama yake kabisa, wamefanana tazama kucha hizo uache msifia mdogo wako" Hamis aliongea na kusababisha wati wote wacheke humo ndani.
"Bonoeza usichukie basi masihara ni jadi yetu tangu twacheza michezo ya kitoto, hongera bwana kwa kupata binti mrembo huyo na urembo wake unaonekana tangu akiwa mtoto" Shafiu aliongea huku akimpa mkono wa pongezi rafiki yake kipenzi.
"shukrani Chumbio rafiki wa tangu utotoni" Hamis aliitikia huku akicheka
"sasa Bonoeza hapo inabidi ufuge mbwa na bunduki ununue mapema maana wajanja wataanza kuja kutoa salamu sana kumbe wataka wampate malkia hapa" Shafii alisema na wote waliopo nyumbani kwa Hamisi wakacheka " Maneno aliyoambiwa na Salma ndiyo yalivuta kumbukumbu yakamkumbusha siku hiyo ambayo Hamida alikuwa ndiyo kaletwa nyumbani baada ya kuzaliwa katika hospitali ya Ngamiani, alizidi kukumbuka zaidi na hapo akakumbuka tukio jingine kabisa baada ya kumuona Hamida akiwa na miaka mitano tu tangu azaliwe na siku hiyo alikuwa akibadilishwa nguo na mama yake Salma, siku hiyo alimuona Hamida akiwa ana mwili unaofanana wake sana. Ally alikumbuka zaidi juu ya siku hiyo na akawa anajifikiria kwa umakini haswa ndipo akajikuta anaamini lakini siyo kwa asilimiia zote yale maneno aliyoambiwa na Salma.
"Dah nimefanyishwa dhambi mbaya ya kuzini na mke wa mtu bila kujijua" Alky aliongea huku akikata mitaa na alionekana ni mwenye majuto makuu juu ya jambo hilo ingawa hakutegemea kama atalifanya, alitembea huku uelekeo wake maalum ukiwa haujulikani kwani alikuwa anazurura mitaani tu.
"ni bora nilale nje kuliko kulala kwenye mali haramu niliyokuwa nimekabidhiwa na nikajikuta nimeipokea bila kujijua, ni bora nisifanye kazi niwe masikini kuliko kuitumia hii elimu niliyosomeshwa kwa kutumia fedha haramu zilizosababisha mwanadamu mwenzangu amwage damu kwa manufaa ya wengine. Shahada nimeipata kwa pesa zilizotokana na damu ya mwenzangu kumwagika, nawachukia Shafii, Hamid, Hassan, Hussein, Falzal, Hamisi pamoja  mke wako Salma aliyetoa kitu kichafu ili aangamizwe kiumbe asiye na hatia. Hisan Shelukindo pia mwanaharamu mkubwa wewe umekuwa na maisha mazuri kwa ukatili wenu  huo" Ally aliongea kwa hasira akiwa tayari ameshafika Sahare kwa kutembea tu bila hata mpangilio; alihisi uchovu kwa kutembea siku hiyo nzima na akakaa katika baraza la maduka ambayo yalikuwa ndiyo yamekamilika ujenzi wake lakini bado hayajafunguliwa. Alijiona ni mmoja wa wenye makosa kwa kutumia sehemu ya mali iliyotokana na  njia haramu ingawa hakujijua, alijikuta hata akilengwa na machozi na hatimaye alianza kulia kimya kimya hadi pale alipochoka akainuka kwenye baraza hiyo.
"Bora uwe masikini utaabike kuliko uwe tajiri kwa njia isiyo ya halali bila kujijua, inauma sana" Ally alisema kwa uchungu huku akinyanyuka tena barazani hapo na kuanza kutembea kama ilivyokuwa awali, alitembea akawa anafuata uelekeo wa nyumbani kwa baba yake hadi alipofika akaingia ndani na moja kwa moja akaenda kujitupa sebuleni akalala usingizi mzito bila hata kuwa amekula kitu chochote siku hiyo.

   Asubuhi ya siku iliyofuata aliamka akajisafisha mwili wake akatoka hadi nje, akamuona dereva wa gari za baba yake akiwa yupo barazani akipata kifungua kinywa akamsabahi kisha akawa anaelekea getini.
"Kaka unaelekea wapi nikutoe maana gari zipo hapa" Dereva wa baba yake alimuambia.
"unaweza ukapumzika kaka mkubwa" Ally alimuambia dereva wa gari ya baba yake kisha akatoka nje akawa anaelekea ilipo barabara ya Mombasa, alitembea hadi akipoifikia hiyo barabara akamuita dereva wa pikipiki akaja mara moja.
"Mpirani kaka" Ally alimuambia dereva wa pikipiki ambaye alimchangamkia akamuambia apande tu bila hata kutaja bei, Ally alipanda hiyo pikipiki na safari ikaanza ambapo ilichukua dakika kumi na tano kwa mwendo wa pikipiki akawa ameshafika Mpirani akampa dereva yule pesa yake kisha akaingia mtaani na akatembea hadi mahali ambapo nyumba zipo moja moja na hatimaye akaifikia nyumba kubwa ambayo ipo kama gofu tu ikiwa ipo katikati ya shamba kubwa  ikionekana  kuwa ipo peke yake mbali na makazi ya watu wengine. Nyumba hiyo ilionekana kutolewa milango na baadhi ya madirisha baada ya kukaa siku nyingi bila kutumiwa kama makazi ya watu na eneo zima lenye kuizunguka nyumba hiyo lilikuwa  na majani mengi yaliyoonekana hayaku punguzwa kwa muda mrefu.
Ally aliingia ndani ya nyumba hiyo iliyoezekwa kwa bati  lililochakaa na sakafu ya chini ilionesha kuwa ni ya udongo mwekundu  ambao hutumiwa kukandika kuta za nyumba za udongo, ilikuwa ni nyumba kubwa yenye  vyumba takribani vinne na sebule ambayo ndani ina kuta za udongo zilizowekwa plasta kwa nje. Sebule kubwa ya nyumba hiyo ilikuwa na usafi mkubwa kupitiliza ambao ulimshangaza sana Ally na vyumbani kulikuwa kuna nyuzi nyingi za buibui kiasi kwamba haiwezekani hata kidogo mtu wa kawaida kuingia humo ndani bila hata kusafisha hizo nyuzi za buibui, Ally aliangalia kila chumba akawa anakumbuka matukio tofauti ambayo yalikuwa yakifanyika hasa kipindi ambacho anaishi katika nyumba hiyo ambayo kwa sasa imetekelezwa na mwenyewe.
"Ni historia nisiyoweza kuisahau na ni mazingira yasiyoweza kusahaulikavkwa mtu kama mimi na natamani niyarudie niishi kama nilivyokuwa awali huenda amani ya moyo wangu itarejea kama ilivyokuwa awali" Ally aliongea akiwa amesimama katika mlango wa chumba ambacho ndiyo alikuwa akikitumia kipindi akiishi katika nyumba hiyo.
Akiwa amesimama hapo alisikia sauti ya mtu akipiga uruzi kutoka nje ya nyumba hiyo na ikamlazimu atoke aende kutazama ni nani huyo, alipokuwa akikaribia mlango wa kutokea mlango wa nyumba hiyo alikutana na kijana wa kisomali aliyekuwa akifanana sana na mtu ambaye alikuwa anamjua ila jina lilikuwa limemshamtoka kichwani mwake. Kijana huyo alikuwa amevaa kanzu nyekundu  iliyomka vyema na kofia ya rangi ya kahawia, Ally alipomuona huyo kijana alizidi kuvuta kumbukumbu juu ya alipomuona lakini hakukumbuka chochote.
"habari yako kijana" Ally alimsabahi yule kijana.
"salama tu, shikamoo" Yule kijana aliitikia.
"Marhaba sijui ni nani mwenzangu" Alky aliitikia kisha akamuiliza swali yule kijana.
"naitwa Fahmi ni mjukuu wa mzee mmoja maarufu wa kiarabu anayeitwa  Muburaka" Yule kijana alieleza.
"Mzee Mubaraka huyuhuyu baba yake Faimu waliyehamia kijiji cha Bwagamacho" Ally alisema.
"Ndiyo huyo huyo na mimi ni mtoto wa Faimu" Fahmi alieleza.
"ok ok karibu bwana leo nimekuja kuzuru makazi yetu ya zamani" Ally alieleza.
"Asante sana, mimi huwa ni sehemu yangu ambayo napenda kukaa huwa inanikumbusha mengi sana hii na nikiwa na huzuni basi huwa nakuja kukaa hapa ndiyo maana unapaona pasafi sana hasa upande wa sebule hii" Fahmi alieleza.
"Ok kijana ndiyo maana nilitaka nishangae imekuwaje mpaka pawe  hivi, karibu tukae sote na mimi leo nimependelea sana kukaa humu" Ally alimuambia huku akimpa mkono Fahmi ambaye aliupokea akiwa na tabasamu pana usoni.
"umefanana sana na baba yako hadi mkitabamu mpo hivyohivyo, hakika mungu kawajalia tabasamu pana kijana" Ally alimwambia Fahmy na kusababisha Fahmy atabasamu.
"asante anko, napenda nikuite anko kama hutajali" Fahmi alimuambia  Ally.
"si vibaya waweza kuniita hivyo tu kwani umeonesha heshima kubwa sana kwangu kijana" Ally alisema.
"asante sana nafurahi kuongea na wewe" Fahmi alisema.
"hata mimi pia, vipi baba yako hajambo?" Ally aliongea huku akitabasamu kisha akamuuliza juu ya hali ya baba yake, swali hilo lilimfanya Fahmi aondokwe na uso wa tabasamu usoni mwake ingawa alilazimisha tabasamu hilo lirudi katika uso wake.
"Baba yupo uarabuni kwa sasa na huko ndipo alipojenga maisha yake" Fahmi alijibu huku akilazimisha tabasamu usoni mwake.
"ohoooo! Mpe hongera sana rafiki yangu aliyenijali sana yule" Ally aliongea huku akitabasamu.
Maongezi yao yaliendelea hadi ilipotimu adhuhuri Fahmi akaaga akaondoka na akamuahidi Ally angerejea akiwa na ugeni mkubwa sana kama angekuwepo hapo. Alky alimpa ahadi ya kuwepo eneo kwa siku nzima hivyo angemkuta, hakuutambua ugeni huo ulikuwa ni ugeni gani na laiti angeutambua angetamani hata auone muda huo lakini haikuwezekana. Ally aliendea kukaa hapo hadi ilipofika muda wa alasiri akaja kijana mwingine akiwa na chombo cha chakula akampatia, yule kijana alimuambia chakula hicho kilikuwa kimeagizwa aletewe na Fahmi.  Ally alishukuru sana akakila chakula chote kutokana na njaa  ambayo tayari ilishaanza kushambulia tumbo lake, baada ya kumaliza kula alitoa shukrani kwa ubinadamu aliofanyiwa na yule kijana
aliyetumwa pia akamwambia apeleke shukrani za dhati kwa Fahmi kwa kumjali namna hiyo.
Baada ya kijana yule kuondoka Ally aliendelea kukaa hapo akikumbuka mambo mbalimbali kipindi akiishi  ndani ya nyumba hiyo kabla hajahama, mambo mengine ya furaha na upendo na alivyokuwa akiishi na shemeji yake ambaye alimjali yalimpa tabasamu kila akiyakumbuka ila alipokumbuka wema aliofanyiwa na kaka yake alijikuta anasonya tu kwani hakuupenda hata kidogo huo wema wake na wala hadi muda hakuona umuhimu wake.
"Shetani katumia ushetani kunifanikishia malengo yangu, hadi sasa sioni umuhimu wa mimi kufikia haya malengo ikiwa kuna mwenzangu kateseka kwasababu ya huyo shetani. Kakimbia kwao kwasababu ya huyo shetani. Shetani huyu kanisaidia ili na mimi anitumbukize katika ushetani"Ally aliongea kwa hasira  kisha akanyanyuka akasema, "namchukia maana bila yeye mimi nisingetumiwa kama mtumwa wa ngono na yule malaya aliyekubuhu kwa umalaya tangu yupo kigori. aaargh! Nawachukiaaa!" Ally aliongea kwa hasira kisha akapiga ngumi ukutani na kupelekea sehemu ya plasta iliyowekwa juu ya ukuta wa udongo wa nyumba hiyo uanguke.
Chuki za waziwazi kwa  kaka yake ndiyo zilikuwa zimeutawala moyo wake na hakumpenda kama ilivyokuwa akimpenda hapo awali, hakuona umuhimu wa yeye kumuita kaka wakati kafanya mambo yasiyopendeza kwa mwanadamu yoyote mwenye moyo wa kibinadamu na siyo wa  kama aliokuwa nao kaka yake. Alitokea kuwachukia ndugu zake wote walioshiriki mpango ule hakuona faida ya kuwa na ndugu kama wao katika dunia hii, aliona ni bora angekuwa na undugu na jiwe kuliko kuwa na undugu na hao aliowaheshu kama kaka zake lakini hakuona ustahiki wao wa heshima hiyo aliyowapa.






               SURA YA NANE.
   Majira ya magharibi katika eneo hilo alilokuwepo Ally paliiingia ugeni mwingine ambao haukutia mguu katika eneo hilo kwa miaka kadhaa tangu walipoondoka, ugeni huo ulikuwa ni msafara wa magari mawili ya kifahari yenye thamani kubwa sana nchini Tanzania kwa kipindi chote. Magari hayo yalikatisha katika majani baada ya barabara ya kuingia eneo hilo kuwa imeota majani kila sehemu.  Ally aliposikia mingurumo ya gari hiyo wala hakujishughulisha kwenda kuangalia zaidi ya kutulia vilevile sehemu ya dirishani ya sebule hiyo alipokaa katika eneo ambalo  dirisha limetolewa, aliposikia hatua za mtu akiingia hapo ndani yeye alielekeza machp mlangoni tu na hadi mtu huyo anaingia tayari alikuwa ameshamuona na ni mtu kati ya watu anaowaheshimu akiwa amebeba mikeka inayotengenezwa kwa ukindu maarufu kama majamvi kwa wakazi wa jiji la Tanga
"Ally kumbe huku" Sauti ya mtu huyo ilimsemesha na hapo Ally akainuka akamfuata.
"ndiyo baba nipo huku, shikamoo" Ally alimuamkia baba yake baada tu ya kumjibu swali alilouliza.
"marhaba tumekutafuta sana mchana wa leo ili uje huku maana kuna jambo muhimu sana" Mzee Buruhan alisema.
"sawa baba nipo tayari hakuna kilichoharibika" Ally aliongea huku akimpokea  baba yake majamvi.
"yatandike hapo chini kwa ajili ya wageni watakaokuja maana mzee Mahmud kasema kuna ugeni utafika hapa kwa ajili ya jambo hili tuliloitiwa hapa.
"sawa baba" Ally alitii amri akaanza kuyatandika majamvi chini kama alivyoambiwa na baada ya muda akawa amemaliza.
"vizuri sasa tumsubiri mzee mwenzangu anakuja sasa hivi na nimeambiwa nisiwaruhusu ndugu zako kuingia mpaka yeye afike" Msee Buruhan  aliongea huku akienda kuketi dirishani alipokuwa ameketi Ally awali, Ally naye aliungana naye kwenda kukaa alipokuwa  awali.
Baada ya dakika tano mlio wa pikipiki ulisikika nje ya nyumba hiyo ikija na kisha baada ya dakika moja ikaondoka, muda huo huo mzee Mahmud alionekana akiingia mlangoni akiwa amebeba taa nne kubwa za kuchaji baada ya pikipiki hiyo kuondoka.
"vipi kila kitu tayari?" Mzee Mahmud aliuliza.
"ndiyo kila kitu tayari mzee mwenzangu" Mzee Mahmud alijibu.
"vizuri basi, Ally hujambo mwanangu" Mzee Buruhan alipongeza kisha akamjulia hali Ally.
"Sijambo baba shikamoo" Ally alijibu kisha akamsalimia.
"Marhaba mwanangu vizuri kwa kuwepo hapa, ngoja nianze kazi" Mzee Buruhan aliongea kisha akaanza kutamka maneno yasiyoeleweka akawa anazunguka eneo zima lenye mikeka halafu akafanya hivyo kwenye kila pembe ya ukuta hadi akamaliza sehemu zote na alipomaliza kufanya hivyo aliwasha taa alizokuja nazo akazitundika ukutani kwenye kila kona.
"Sasa hao wanaweza kuingia wakae upande wa kushoto na uwaambie wasiongee mpaka niwaambie mimi, Ally kaa pembeni yangu"  Mzee Mahmud aliongea kisha akakaa chini, mzee Buruhan alitoka nje na baada ya muda akarejea akiwa pamoja na Shafii,Salma, Hamida na Jamal.
Shafii aliongozwa na Jamal hadi eneo wanalotakiwa wakae na alishushwa kwenye kiti akakalishwa kitako, baada ya wote kukaa chini kwenye jamvi waligeuka wakawa wanamtazama mzee Mahmud kujua kinachofuata.
"Bado ugeni mmoja uingie, wageni karibuni" Mzee Mahmud aliongea huku akitazama mlangoni na kupelekea watu wote watazame mlangoni, ugeni ulioingia hapo ulikuwa ni watu  wanaowajua ambapo wengine walishtuka baada ya kuuona ugeni huo ambao haukueleweka umefika hapo kwa usafiri gani kwani walionekana tu wapo mlangoni.
Wa kwanza kuonekana mbele ya macho yao alikuwa ni Zalabain akiwa amevaa joho jeusi  na kofia nyupe ambaye alitambulika kwa Ally na Shafii pamoja na mzee Mahmud, Ally alimtambua Zalabain  kama Fahmi aliyekuwa naye hapo hadi muda wa adhuhuri na hakumfahamu kwa vingine kabisa. Shafii alimtambua huyo mtu kama mbaya wake baada ya kuiona sura yake siku aliyokufa mganga Sauti ya radi na alimkimbia, alipomuona alishtuka sana alitamani hata ardhi ipasuke atumbukie asionekane eneo hilo kwani alishuhudia ukatili wa Zalabain hivyo alimuogopa. Wageni wengine walioingia eneo hilo walikuwa ni Bi Farida na Zayina wakiwa wamevaa nguo za thamani kubwa walizopata wakiwa katika ulimwengu wa majini, Shafii alipowaona alijikuta akijawa na furaha akataka kutamka neno ila ishara ya baba yake ikimkataza kutozungumza ikamfanya atulie.
"Karibu Zalabain mwana Zaif mjukuu wa Zulain mfalme wa himaya ya majini ya  Majichungu, karibu uketi upande ule wa pili ukiwa na wageni wenzako" Mzee Mahmud alisema huku akitabasamu na kusababisha Zalabain atabasamu pia, Zalabain na mama yake pamoja na dada yake walienda kukaa mwingine kabisa pembeni ya upande aliopo Shafii.
"Sasa basi nimewaita hapa ili tuweze kutatua tatizo ambalo lingemsababishia mzee mwenzangu hapa asibakiwe na hata muhomili mmoja ndani ya dunia hii, utatuzi wa tatizo hilo utaanza kuonekana tu ikiwa ukweli wote utakuwa utakuwa hadharani" Mzee Mahmud alisema kisha akamwangalia Shafii akamwambia, "Shafii napenda uanze kuongea ukweli kuanzia unaanza kumpenda Bi Farida na ulivyompata hadi ukamuoa, tafadhali narudia tena tafadhali ukweli ni muhimu katika kila kitu".
Baada ya mzee Mahmud kumaliza kuongea alimpisha Shafii ili aeleze ukweli wake wote, Shafii naye hakuwa na jinsi zaidi ya kueleza ukweli wote juu ya suala hilo ili apate  nafuu ya matatizo yake kwa jinsi anavyoamini na kwa jinsi alivyoambiwa na mzee Mahmud. Shafii alianza kwa kusafisha koo lake kisha akasimulia, "Kwanza napenda nitangulize msamaha kwa hichi nitakachokusimulia ikiwa kitakuwa kimemkwaza yoyote kwani si kizuri, nilikuwa ni mtoto mtiifu sana kwa wazazi wangu kwa kipindi ambacho bado sikuwa nimepevuka kutokana na malezi ya kimaadili aliyonilea baba yangu kwa  kipindi hicho. Ndiyo muda huo huo mke wangu mama Zayina alikuwa angali binti mdogo hata kuvunja ungo bado ingawa alikuwa akitajwa ni mmoja kati ya mabinti wenye uzuri ambao haukuwahi kutokea katika kijiji chetu cha Bwagamacho Baada ya Farida kuanza kupevuka ndipo uzuri huo wa umbo na kila kitu ulianza kuonekana na kipindi hicho na ndiyo wavulana wa rika langu wakaanza kumfuata lakini waliambulia kukataliwa na binti huyo na hata wengine walishtakiwa kwa wazazi wao baada kumtongoza, jambo hilo lilinitisha na kunifanya nishindwe kwenda kumuambia kwa kuhofia ukali wa baba yangu kama akijua. Nilimpenda sana tena sana lakini nilihofia kupigwa sana na baba yangu kama nilivyoshuhudia wenzangu wakifanyiwa hivyo na baba zao baada tu ya mashtaka kuletwa nyumbani juu ya kumtongoza Farida. Baada ya miaka miwili kupita ndipo nilipoanza kupata ujasiri wa kumtongoza ingawa nilikuwa nina uoga kwa mbali, kutongoza kwangu kuligonga mwamba na hata nilipomueleza rafiki yangu kipenzi Hamis ambaye ni kaka yake juu ya suala hilo aliniambia yupo tayari kumsaidia ikiwa tu na yeye nitamsaidia kufanikisha jambo analolitaka.
"Jambo gani wataka nikusaidie  Bonoeza" Nilimuuliza Hamis.kwa kutia jina la utani ambalo hakuwa analipenda kabisa kwa kipindi hicho.
"Shafii waanza sasa nimesema hilo jina silitaki nitaacha kusaidia nikamjaze sumu dada yangu umkose" Hamis alinijia juu baada ya kumtajia hilo jina.
"Hamis nisamehe rafiki yangu niambie shida yako sasa" Nilimuomba radhi na nikawa tayari kuisikiliza hiyo shida yake kwani ndiye rafiki yangu wa shida na raha.
"rafiki yangu hii ni aibu sana hasa kwa vijana wa rika langu na nimeificha ila kwakuwa wewe ni rafiki yangu wa muda mrefu nimeamua nikueleze ili unisaidie na wewe  nikusaidie, kiufupi nampenda sana Salma yule mtoto mzee Rajabu ila mdomo wangu ni mzito kutamka neno hili kwake na ninabaki nikiungua ndani kwa ndani tu" Hamis alinieleza tatizo lake ambalo nilikuwa nipo tayari kumsaidia tu ili nipate moyo wa dada yake  kipenzi, tatizo lake lilikuwa ni dogo tu kwani  hata Salma alikuwa akimpenda vilevile na ishara zote niliziona ila tu wote hawakuwa na ujasiri huo. Nilimsaidia hadi akampata Salma na mimi akaanza harakati za kunisaidia lakini hazikuzaa matunda kabisa kwani msimamo wa Farida bado ulikuwa ni uleule na hata alipomtumia Salma katika suala hilo ilikuwa vilevile na yeye alizidi kunipa moyo kuwa nitampata ingawa nilianza kukata tamaa juu ya suala hilo.  Niliendelea kumbembeleza Farida lakini sikuchoka kwani niliamini yeye alikuwa akinipenda mimi pia na kama angekuwa hanipendi basi angelikuwa amenishitaki siku nyingi nyumbani kwetu juu ya kumsumbua kwangu lakini hakufanya hivyo, hakika sikutambua kama kaanza kukomaa kiakili na jambo kama hilo hakuwa na haja tena kulisema kwani ingeonekana ni akili za kitoto. Niliendelea kujipa moyo nikijua ipo siku nitampata na sikutambua kama mawazo yangu ni sawa na kuchemsha mawe nikitegemea yatachemke kutokana na upendo mzito nilionao kwake, sikutambua kama najipa matumaini hayawezekani kutokea hivihivi kama kubadilika kwa majira ya mwaka kutoka kiangazi hadi vuli. Nilichojali ni kupata jibu sikujali itachukua muda gani hadi niwe naye, niliendelea kusumbuka katika kumueleza kila siku lakini niliambulia patupu na nikawa natembea na matumaini ya kumpata tu kichwani mwangu. Matumaini yangu yaliishi katika moyo wangu lakini baadaye yalikufa baada ya muda wa miezi kadhaa tu na nikajikuta nikiumia moyoni, kufa  kwa matumaini yangu kulikuwa ni baada ya kuingia kikwazo katika kumpata Farida...



*Hatimaye akubali kufunguka

*usikose kujua alichofunguka.

No comments:

Post a Comment