Wednesday, December 2, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA KUMI NA TANO

RIWAYA: DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE




SEHEMU YA KUMI NA TANO!!
Niliendelea kujipa moyo nikijua ipo siku nitampata na sikutambua kama mawazo yangu ni sawa na kuchemsha mawe nikitegemea yatachemke kutokana na upendo mzito nilionao kwake, sikutambua kama najipa matumaini hayawezekani kutokea hivihivi kama kubadilika kwa majira ya mwaka kutoka kiangazi hadi vuli. Nilichojali ni kupata jibu sikujali itachukua muda gani hadi niwe naye, niliendelea kusumbuka katika kumueleza kila siku lakini niliambulia patupu na nikawa natembea na matumaini ya kumpata tu kichwani mwangu. Matumaini yangu yaliishi katika moyo wangu lakini baadaye yalikufa baada ya muda wa miezi kadhaa tu na nikajikuta nikiumia moyoni, kufa  kwa matumaini yangu kulikuwa ni baada ya kuingia kikwazo katika kumpata Farida...


****


Nakumbuka vizuri kijijini kwetu waliingia wageni ambao walipatiwa eneo ambalo baadaye  walilinunua wakajenga makazi yao ya kudumu, wageni hao walikuwa ni wenye asili ya tofauti na watu walioko kijijini
kwetu kwani wao walikuwa na asili ya uarabu lakini siyo wang'avu kabisa na ninaweza kuwaita wasomali pia. Walikuwa ni mke na mume  pamoja na kijana wao mmoja ambaye ni makamo yetu, wageni wenyewe walioingia katika kijiji chetu walikuwa ni Mzee Mubaraka mkewe pamoja na mtoto wao wa pekee Faimu. Kuja kwa huu ugeni ndiyo kikwazo kikuu cha kumpata Farida kilichokuwa kinaniumiza akili, kikwazo hiki sikuweza kukibaini hapo awali kwani Faimu hakuonekana kama atakuja kuwa kikwazo katika kumpata Farida.
Ndani ya mwezi mmoja wa kwanza tangu Faimu awasili pale kijijini kweti tayari wavulana wa rika letu walishaanza kumchukia kwani alikuwa kikwazo kwao kikubwa cha kuwapata wasichana hao, uzuri wa sura, umbo na hata muonekano mwingine alionao Faimu ulifanya awe midomoni mwa wasichana wa karibia kijiji kizima na kila msichana alikuwa na ndoto za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Faimu na kupelekea kuwa na ushindani mkubwa katika kumpata.
Mabinti hawa walibuni mbinu mbadala ya kufanya waweze kuwa chaguo la wazazi wa Faimu kwani kipindi hicho mzazi akimpenda binti basi hufanya mipango ili aweze kuwa  mkwewe, sasa basi ili waweze kuwavutia wazazi wa Faimu walikuwa wakienda mara kwa mara nyumbani kwa mzee Mubaraka wakitumia njia ya  kumsaidia kazi mke wa mzee Mubaraka ili waonekane ni mabinti watiifu. Mbinu hiyo ya mabinti wa kijijini kwetu haikujulikana na mzazi yoyote zaidi ya kuona ni tabia njema tu ya mabinti zao  katika kuwakirimu wageni ili tu nao wakipata mabinti waje kuwakirimu, hakika ukarimu ndiyo ulikipamba kijiji chetu  na ndiyo maana hila hiyo haikugundulika kwa wazazi zaidi ya kubainika na wavulana tu wa kawaida waliozidisha chuki sana kwa Faimu.
Ulipotimia mwaka mmoja tangu Faimu ahamie hapo tayari alikuwa anachukiwa na robo tatu ya wavulana wa kijiji hicho na marafiki zake wakuu tulikuwa ni mimi na Hamis tu, sisi pekee tulikuwa ni marafiki zake wakubwa kutokana na kuwa mcheshi sana kwetu. Katika kipindi hicho hakuwahi kumtambua Farida kwani tangu ahamie alisikia habari za Farida ila hakupata bahati ya kukutana naye ana kwa ana kutokana na kazi mbalimbali zinazomkabili  Farida, hata Farida naye kwa mujibu wa Hamisi alithibitisha kuwa hakuwa kumuona Faimu zaidi ya kusikia kuna mgeni kahamia ana urafiki na sisi.
Kusema uongo dhambi na pia kumsifia uzuri mwanaume mwenzio siyo vizuri  ila ukweli Faimu alikuwa mzuri sana hadi akafikia hatua baadhi ya kina mama wa kijijini wakaanza kumtaka  huku mabinti wengine walidiriki kupigana kisa yeye tu, ilifika kipindi wasichana uvumilivu ukawashinda wakamuambia ukweli na hadi wengine walitoroka majumbani mwao kipindi cha usiku wakaenda kuvamia chumbani kwake ili walale naye lakini bado alikuwa na msimamo wake kama mtu anayejitambua.
Siku moja tukiwa kwenye kijiwe chetu tukiongea nikiwepo mimi, Hamis na Faimu mcheshi wetu aliyetufanya tucheke  kila kukicha. Siku hiyo Farida alipita mbele ya macho yetu  na ndiyo hapo nikamuonesha Faimu nikamtambulisha ni shemeji yake ili tu amuheshimu na asije akampenda kwani nilishabaini mwenzangu wasichana kwake ni kama mbwa na yeye ni chatu wanamfuata wenyewe, nilipomuita Farida siku hiyo alikataa kuitika akaendelea kwani alikuwa ametumwa na baba yake.
Niliponyamaziwa mimi niliumia sana na ndipo Hamis akamuita  akaitika na akajongea pale tulipo kutokana na heshima aliyokuwa nayo kwake kama kaka yake, Farida alipofika macho yake yalikuwa  hayotoki usoni kwa Faimu hadi nikaanza kujisikia wivu ingawa nilijipa moyo baada ya Faimu kumtazama mara moja kisha akainamisha macho yake chini asimtazame tena.
"Farida mdogo wangu heshima wafunzwa  nyumbani ila hutaki itumia ukiwa upo nje ya nyumbani, Shafii si akuita mbona wamfanyia hivyo au hapaswi kukuita" Hamis alimuambua Farida ambaye alikuwa ameinamisha macho chini kwa aibu.
"apaswa niita kaka ila ntachelewa, baba kaniagiza kwa mzee Mubaraka nipeleke huu mzigo niwahi rudi" Farida aliongea huku akiangalia chini.
"Si vibaya akikusindikiza basi hebu nenda najua hutochelewa"  Hamis alimuambia Farida ambaye alikubali kutokana na heshima aliyokuwa nayo kwa kaka yake, nilimsindikiza Farida huku nikimchombeza  kuhusu ombi langu kwake na hata nilipozidi aliiua mada yangu na akawa ananiuliza juu ya Faimu na ikanibidi nimueleze kila kitu na kisha nikaendelea kumchombeza Hadi namsindikiza na kurudi kwa wenzangu sikuwa nimeambulia jibu la kuniridhisha moyo wangu ingawa niliporejea Faimu aliniuliza juu ya Farida niliamua kumdanganya.
"Kila kitu kipo kizuri rafiki na hapa alishindwa itika sababu  aona haya yupo kakaye" Nilimdanganya Faimu huku nilichojibiwa kikibaki kuwa siri moyoni mwangu na kwa Hamisi ambaye anajua kila kitu juu  ya kukataliwa kwangu.
"Shafii nipe mkono" Faimu aliniambia huku akitabasamu na mimi nilimpatia bila hata hiyana, Faimu alinipa mkono kwa ishara ya kutoleana pongezi halafu akaniambia, "hongera sana Shafii wajua kuchagua haswa  rafiki nikupe hongera".
Maneno ya Faimu yalinifanya nitabasamu ingawa moyoni nilijiona ni mjinga kwa kupewa sifa nisizostahiki kupewa na nilipata ahueni sana na nikawa na uhakika Farida ni wangu tu kwani niliyemuhofia hakuonekana kuwa na muda nae hivyo sikuwa na mpinzani kwani kijiji kizima nilishawapa vitisho vijana wenzangu kumfuata Farida nikiwaambia ni mali yangu. Baada ya siku hiyo urafiki wetu ulidumu kama kawaida ingawa ulikuja kuingia dosari miezi mitatu mbele kutokana  na taarifa aliyotuletea Salma ambaye alikuwa ni shemeji yangu kwa Hamis, siku hiyo nilijikuta nikipandwa na ghdhabu sana kutokana na taarifa hiyo kwani iliniuma mno tena iliniuma sana.
Salma alituletea taarifa ya kuwaona Faimu na Farida wakifanya jimai katika kichaka kilichopo kando ya mto ambao tunautumia kuchota maji ya matumizi ya nyumbani, Salma alieleza kuwa wote walikiri kuwa wanapendana na ndiyo chaguo la kila mmoja.
Iliniuma, iliniuma tena sana kupata taarifa hiyo kutokana na kumpenda sana Farida aliyekuwa hana upendo na mimi Nilitamani kumfanyia jambo la kwenda kumpiga Faimu na nimuonye juu ya kuachana na Farida lakini Hamisi alinizuia akiniambia sina mahusiano  na Farida na ningefanya hivyo na Farida akatangaza ningeumbuka sana. Maneno ya Hamis niliyaafiki na hapo ndipo tukaanza mikakati ya kumfanyia kitu kibaya Faimu, niliwashirikiaha wadogo zangu wote katika mpango huo kasoro Ally  ambaye sikumuamini kutokana na urafiki wake na Faimu ambao nilikuwa siuelewi. Hamid ,Haasan, Hussein na Falzal wote walikubali kumfanyia njama Faimu kwani wasichana waliokuwa na mahusiano  nao walikuwa wakimpenda Faimu hivyo jambo hilo liliwakera sana, tulianza kusuka mpango wa kumkamata Faimu akipita kuelekea kuchunga mbuzi wa kwao ili tumuue lakini mpango huo ulishindikana kwa namna ambayo haikueleweka.
Mara ya kwanza tulipanga tumuue akiwa machungani akichunga mbuzi lakini tulipoenda tulimkosa kwa siku mbili tofauti ambapo tulimuona ni yeye alikuwa amepeleka mbuzi machungani lakini tulipoenda tulikuta anayechunga mbuzi ni mzee ambaye hatumjui, mpango huo ulishindikana kwa mara nne mfululizo na hata yule mzee tunayemkuta tukimuuliza anasema ameondoka baada ya kuleta mbuzi huku machungani. Muda wa kurudisha mbuzi alikuwa akionekana ni yeye anarudisha hao mbuzi, tulipomfuata kwa urafiki wetu wa kinafiki na kumuuliza juu ya alipokuwa alituambia huwa anatoka kidogo tu akimuachia yule mzee ila anarudi. baadaye.
Mipango ya kumuua ilipokosa mafanikio ndipo tukatumia mbinu nyingine tofauti ya awali ingawa nayo haikufanikiwa, tuliamua kwenda waganga wa kijijini kwetu   ili tumuue kwa njia ya uchawi lakini cha ajabu waganga wote walisema hilo suala haliwezekani, mwishowe tukaamua kumuhadaa rafiki wa baba yetu kipenzi mzee Mahmud ili amuue kwani tuliamini yeye ndiyo mganga mwenye nguvu peke yake kijijini kwetu lakini baba yetu naye alikataa katakata akisema siyo kazi yake kufanya ubaya.
"wanangu mnalolitafuta nj kubwa sana tofauti mnavyofikiria, Faimu ni mwenye nyota kali sana hakuna mganga yeyote awezaye  kuizima na yasimkute matatizo labda  Muumba amnusuru. Pia siui bali naagua" Nayakumbuka maneno ya baba yetu ambaye ni sawa na baba yetu aliyepelekea uzao wetu  alivyotuambia
"Kaka twafanyaje sasa maana yule simpendi sana" Hamid aliongea tukiwa tunajadiliana nyumbani kwetu baada ya kutoka tu nyumbani kwako Baba yetu Mzee Mahumd.
"jamani sikilizeni, yabidi twende kwa baba yake Sauti ya radi wa pale Maforoni nafikiri tutaweza" Hussein alitoa wazo ambalo nililiafiki na nilipanga kwenda mwenyewe huko Maforoni, siku iliyofuata asubuhi na mapema nikaenda maforoni kwa kupitia njia ya mkato na nilitumia muda mfupi tu nikawa nimeshafika kutokana na kutumia baiskeli yenye uwezo mzuri. Nilifika nikapokelewa vizuri na yule mganga na nikamueleza tatizo langu lote, mganga huyo aliongea na walimu wake kwa muda mfupi kisha akaniambia "Kijana huyo mpinzani wako ana nyota kali sana na kumuua haiwezekani sema nakupa dawa moja utaenda mchanganyia huyo binti kwenye maji ya kunywa na akinywa yeye atakupenda wewe milele tu, huyo mbaya wako atakuwa hana nafasi tena".
Mganga alinipatia dawa hiyo ya unga na nilirejea kijijini haraka sana nikawaambia ndugu zangu nilipofikia kisha tukamuita Hamis na tukamuambia kila kitu, Hamis akasema tumuachie hiyo kazi ataimaliza na kweli tulimuachia hiyo akaifanya na matokeo yakaja mazuri sana.
Farida alianza kunipenda mimi akawa hamtaki Faimu jambo ambalo lilikuwa ni ajabu kwa Faimu ambaye alizidi kumfuata Farida na hatimaye alitukanwa sana mbele za vijana wengine na kusababisha vijana wazidi kumcheka. Faimu hakukoma alizidi kumfuatilia Farida na majibu yakawa ni yaleyale, na huo ndiyo ukawa mwisho wa penzi lao.
Nakumbuka mara mwisho Faiz alimfuata Farida kisimani akalazimisha penzi na matokeo yake yalikuwa ni mabaya, kwani Farida alipiga kelele za kuwa anabakwa na sisi tuliokuwa karibu tukamvamia na kuanza kumpiga na baadaye watu waliongezeka hasa vijana wanaomchukia ambayo walimpiga sana kisha akapelekwa kwa kiongozi wa kijiji. Wazazi wake waliitwa wakaelezwa juu ya hilo ambalo lilikuwa ni aibu kwao na jambo llililowakera, baada ya siku kadhaa kiongozi wa kijiji alimfukuza Faiz katika kijiji na ikawa ni furaha kwa vijana wa kijiji hicho pia huzuni kwa wasichana waliompenda kwani hakuwahi kuonekana hadi leo hii".

 Hadi anafikia kituo kueleza juu ya hilo tayari Bi Farida alikuwa analia kwa kwikwi baada ya kubaini jambo alilofanyiwa na Shafii, Zayina naye alisikitishwa sana uovu alioufanya baba yake. Zalabain hasira zilimpanda zaidi hadi macho yakawa mekundu lakini hakufanya lolote juu ya hilo kutokana na kuzuiwa na mzee Mahmud, hasira zilipomzidi Zalabaun machozi yalimtoka na akawa anatetemeka hadi midomo ikawa inacheza.
Upande wa mzee Buruhan hasira zilimpanda kwa ujinga wa mwanae lakini alipotaka kuongea Mzee Mahmud alimzuia kutokana na masharti aliyowapa, mzee Mahmud alitazama hali  za watu waliomo humo ndani na mwisho wake  akayatuliza macho yake yaliyozungukwa na ngozi iliyofunyaa kutokana na uzee kwenye uso wa mzee Buruhan. Alimtazama mzee mwenzake halafu akasema, "mzee mwenzangu nadhani unakumbuka zaidi kile kisa nilichokusimulia nikitumia mafumbo pia nikiongeza chumvi ili usijue na nilikuambia muendelezo wake utaujua sasa usikilize huo muendelezo wake leo. Nilitia chumvi kukuambia hakuna aliyejua usiri wa penzi la Giguna ambaye ndiye huyu Farida na Mufeji ambaye ni Faimu ila ukweli ni kwamba kuna mtu mwingine ambaye alikuwa anajua ambaye ninampa Nikuza ambaye ni mdogo wa mwisho wa Nukeze au Shafii mdogo huyo ukipenda muite Ally. Haya Ally tusimuulie kile unachojua katika uhusiano wa Farida na Faimu".
Ally aliposikia maneno hayo alimtazama sana kaka yake kwa chuki kisha akamtazama Bi Farida kwa huruma sana halafu akafunguka kile anachokijua, "Baada ya mimi kuanza kupevuka tu tayari Faimu alikuwa ni mwenyeji ndani ya kijiji chetu na alikuwa ni rafiki wa huyo firauni wa kizazi hiki, Faimu namkumbuka kama mtu aliyenizidi umri ambaye alikuwa anapenda kukaa na mimi na hakutumia udogo wangu kwake kuwa sababu ya kunitenga kama ilivyo hao ndugu zangu. Nilimpenda kutokana na uchangamfu wake na hata kunishauri mambo mengine katika umri huu wa upevukaji tofauti na wengine walioniacha nikacheze na  watoto wadogo walionizidi umri kwa kisingizio kuwa sijakua, katika kipindi hicho niliomba ushauri kwake pia baada ya huyu Salma niliyemuheshimu kuanza kunitaka kimapenzi na alinishauri vizuri nimkatae. Siku moja nakumbuka niliwakuta Farida na Faimu wakiwa wamekaa kihasara  sana niliyeambiwa ni shemeji yangu, iliniuma sana ila nilikuwa kawaida baada ya kujua juu ya uhusiano wao na nilipotambua kuwa hakuwa shemeji yangu kama nilivyoambiwa. Niliukubali uhusiano wao kwa mikono miwili na niliufanya siri yangu kutokana na kaka zangu kutonihusisha katika yao, hata Salma alipokuja kuniambia juu ya kubaini hilo nilimuambia wamependana hivyo uwaache ingawa yeye alisema anaenda kumuambia mchumba wake na mimi nilipuuzia tu kwani namjua huyo ni mmoja kati ya wasichana walioenda nyumbani kwa mzee Mubaraka ili tu aonekane na Faimu kwakuwa anamtaka. Siku moja ndipo huyuhuyu Salma aliyekuwa ananitaka aliniletea taarifa ya uhusiano mpya wa Farida na Shafii ambao umeanza , nilienda kumuuliza Faimu juu ya hilo na akanibainishia kuwa Farida hamtaki. Sikutaka kuamini moja kwa moja nikamfuata Farida mwenyewe kwani alikuwa ananiheshimu na mimi namuheshimu, sikujali ndugu yangu kumpata ila niliangalia yule aliyenijali zaidi hata ya ndugu anavyonijali akiumia mimi iliniuma pia kwani  nilimuheshimu sana.
"Farida umekuwa vipi? Si uliniambia wampemda Faimu wewe ni nini kimekupata?" Nilimuuliza Farida.
"Sikumpenda Faimu ila nilipotea njia ila sasa simronda(simtaki)" Farida aliniambia tena mwishoni akazidi kuniwekea msamiati wa kidigo akiniambia hamtaki.
"Farida kumbuka ulisema Faimu ndiyo chaguo  lako leo umehamia kwa kaka yangu tena" Nilimuambia Farida nikiwa hata simuelewi.
"haaaa! Ally aaambiwa mimi huyo Farida mchetu(binti) wa Jumanne  nimesema hivyo? Ally nampenda Shafii na sikumbuki Faimu nilimpenda vipi, niheshimu kama shemejio kwa kaka yako kama ninavyokuheshimu" Farida aliniambia neno hilo ambalo lilinichanganya na nikampelekea taarifa Faimu ambaye pia alionekana kuchanganywa ila zaidi yangu. Baada ya muda zilinijia taarifa za kutaka kumbaka Farida na nilienda kumshuhudia hiyo siku anayopigwa na roho iliniuma kutokana na jinsi alivyonipenda, baada ya kupona majeraha yake Faimu alikuja kuniaga akahama kijiji na sikumuona tena hadi leo hii na niliendelea kumuheshimu Farida kama alivyoniambia nimuheshimu. Baada ya...."

"Basi Ally ishia hapohapo kwa kusimulia unachojua juu ya kaka yako......Mzee mwenzangu umesikia hayo yanayosemwa nataka uujue muendelezo wa kisa chetu hadi mwisho. Salma wewe ueleze ukweli wote siku ya kwanza kumuona Faimu jua ukidanganya yatakayokupata shauri yako kuna nguvu kubwa hapa" Mzee Mahmud alimkatisha Ally kisha akamgeukia Mzee Buruhan akamuambua maneno machache, alipomaliz alimgeukia Salma akuambia asimulie na akamuonya juu ya usemaji  uongo.
Salma aliposikia hayo maneno alijifikiria kwa muda mfupi kisha akaanza kusema, "Baada ya Faimu kuwasili kijijini kwetu nilimuona ni mstarabu kumbe ni mshenzi kupi...". Salma alishindwa kumalizia kauli yake baada ya eneo alilokaa kutokeza shimo kubwa kwa nyuma na nguvu kubwa ya upepo ikawa inamsukuma kuangukia kwenye hilo, alipiga kelele akijua wenzake wameona kule alichokiona kumbe alikuwa amekiona yeye, Mzee Mahmud na Zalabain tu. Kelele zake ziliwashangaza wengine wote  waliomo humo kasoro waliiona kilichomtokea, Zalabain naye aliposikia kauli ya Salma hasirs zikampanda ila alishindwa kunyanyuka baada ya nguvu kubwa iliyopo hapo kumzuia.  Mzee Mahmud alinyoosha mkono akatamka maneno yasiyoeleweka na lile shimo likapotea, hali ya kawaida ikarudi kama awali huku Salma akawa anahema kwa uoga.
"Kwanini unakuwa mbishi binti si nimekuambia uache kusema uongo unadhani hii ni sehemu ya kudanganya, nimekuambia kuna nguvu nzito hapa au huelewi? Sasa rudia tena iwe mwisho wa maisha yako" Mzee Mahmud aliongea kwa hasira halafu akamgeukia Zalabain akamwambia, "Huna nguvu ya kufanya hivyo bila nguvu zilizopo hapa kukuruhusu kufanya unachotaka kufanya hivyo tulia kwanza usiendekeze hasira mbele ya nguvu kubwa".
"Haya endelea kusimulia na uwe mkweli" Mzee Mahmud alisema.
Salma aliposikia kauli ya mzee Mahmud hakuwa na ujanja zaidi ya kusimulia yaliyompata akiogopa kufa na aliongea, "Urafiki wangu na Farida ni wa siku nyingi sana na yeye alinijua kama wifi yake mapema kabla ya waru wote   kujua, hata shemeji Shafii alipoanza kumpenda alinisihi nimbembeleze ili akubali na mimi nilifanya hivyo lakini aliendelea kushikilia msimamo wake uleule wa kutokibali kuwa na Shafii. Nilijitahidi sana mwisho nikachoka nikaamua kuacha na nikawa namuonea huruma sana shemeji yangu kwa jinsi anavyoumia, baada ya muda kidogo kupita ndipo familia ya Faimu ilipoingia hapo kijijini kwetu na nilipomuona Faimu kwa mara ya kwanza nilijikuta nampenda na nilitaka kuwa naye kwani nilishazoea kukaa na kutembea na wanaume mbalimbali na nilianza haya hata kabla sijampata Hamis na nilipokuja kumpata nilitulia ila nilijikuta nikiirudia tabia yangu hiyo kwa mara  nyingine tena niliifanya kwa mara mbili tofauti. Mara ya kwanza nilianza kwa Faimu nikawa najipitisha sana kwao ili anuone nikijua nitamnasa tu kama nilivyonasa vijana wa hapo kijijini kumbe Faimu hakuwa kijana wa hivyo, uvumilivu uliponishinda niliamua kumuambia ukweli  lakini pia nilimkosa baada ya kukataliwa na akanitishia kumuambia Hamis.  Mara ya pili niliirudia tabia yangu kwa kumtaka Ally baada ua uzuri wake  kuonekana alipofikia kwenye balehe  lakini pia alinikataa nikajikuta nazidi kumsumbua nikijua nitampata tu kwani ni mtoto yule bado akili haijapevuka zaidi ya kupevuka mwili tu, nilipoona nakataliwa sikuchoka na niliamua kuanzisha mazoea ya kawaida naye.  Siku nilipokuja kuwafuma Farida na Faimu na wote wakakiri kuwa wana uhusiano ndiyo siku niliyoona ya kutumia sababu hiyo kwa njia mbili, kwanza ni kulipa kisasi cha kukataliwa na Faimu na pili ni kumteka Ally kiakili. Nilijua Ally ni bado ana akili za kitoto hivyo nilipanga nimuambie hii habari ili ajue ni jinsi gani nampenda hadi nikaamua kumuambia hiyo habari ili aamini moyo wangu upo kwake, pia nilitaka nimuambie mpenzi wangu juu ya usaliti wa rafiki yao kwao waweze kumfanyia kitu kibaya ili nimcheke na hata amkose Farida.





ITAENDELEA!!

No comments:

Post a Comment