Wednesday, December 16, 2015

SHUJAA SEHEMU YA KUMI NA MBILI





RIWAYA: SHUJAA


MTUNZI: Hassan O Mambosasa

SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



            ILIPOISHIA

"Hakika mimi ni kitwana mtoa burudani kwako Malkia ninayekuhusudu zaidi ya nafsi yangu, jukumu la kukupa burudani ewe malkia wangu uliye pekee ni langu na nitalifanya pasipo kungoja shukrani zaidi ya hifadhi ya moyo wangu katika Kasri la upendo wako. Nanena yatokayo moyoni yanayothibitika hata machoni, I love you Beatrice "  Moses aliamua kuweka hisia zake wazi kwa Beatrice huku mapigo yake ya moyo yakiwa juu kama ameshtuliwa na ndoto ya kutisha usingizini. Maneno hayo yalisababisha moyo wa Beatrice mshtuko wa furaha, kitendo cha yeye kutamkiwa neno hilo na kijana aliyempenda ilikuwa ni furaha kwake ingawa alikosa la kuongea kwa muda huo. Hata alipotaka kuongea  alikatishwa na sauti ya mama yake.

"Beatrice njoo upige picha mara moja" Mams Beatrice alimuita Beatrice akiwa umbali mfupi toka pale alipo. Beatrice alianza kumfuta mama yake huku Moses akiwa amesimama palepale.

"Moses baba na wewe njoo pia" Mams Beatrice alimuita Moses pia katika suala la kupiga picha. Moses aliitiiia wito huo kisha akamfuata Mama Beatrice alipo kwa ajili ya zoezi la kupiga picha.



ENDELEA NAYO ILI KUPATA UHONDO ULIOMO NDANI YAKE



SEHEMU YA KUMI NA MBILI!!

Walipiga picha mbalimbali wakiwa pamoja mithili ya watu wa karibu wa siku nyingi, Mama Beatrice alipomaliza kupiga nao picha aliamua kuongea na binti yake huku Moses akibaki peke yake baada ya kuwapisha mama na mwana  waongee. Aliamua kurudi pale alipokuwa amesimama awali na akiwa peke yake na uhuru wa moyo wake ukiwa upo juu, yote hii ni kutokana na yeye kutua mzigo aliokuwa ameubeba kwa muda wa siku kadhaa. Kitendo cha yeye kubainisha hisia zake kwa binti anayempenda ndio kilimfanya ajione kama ametua mzigo alionao, hadi muda huo watu walikuwa wamemaliza kula na ratiba ya sherehe ilikuwa bado haijafikia muda wa kuendelea na kitu kingine kutokana na muda uliotengwa kwa ajili ya kula kutoisha. Watu walianza kuongea mambo mbalimbali kubadilishana mawazo kwa waliokuwa wamezoeana na wenye ukaribu na hata wasio na ukaribu wengine walianza kubadilishana mawazo kutokana na kukaa karibu katika eneo moja. Soga mbalimbali zikipamba moto katika sherehe hiyo huku Moses alikuwa kasimama pale alipokuwa amesimama na Beatrice akiwa peke yake, rafiki yake Hilary alikuwa yupo na Irene muda huo. Bilauri ya kinywaji laini kisicho na kilevi ndiyo ilikuwa mkononi mwake kwa muda huo, eneo lililokuwa na watu alikuwa amelipa mgongo na alikuwa amesimama  eneo la wazi huku kichwa chake kikiangalia juu angani na macho yake  yakifaidi kuuona uzuri wa anga lililopambwa kwa nyota usiku huo.

"nyota yako haina haja ya kuiangalia angani kwani imeshang'aa siku ya leo katika macho ya kadamnasi yakiizima nyota iliyostahiki kung'aa" sauti ya kiume ilisikika kutoka nyuma yake na ikamfanya ageuke, Moses alipogeuka alikutana uso kwa uso na Andrew na alibaini kijana huyo ndiye aliyemwambia maneno hayo.

"nyota ya kwenye gofu kuwaka kwenye kasiri la kifalme hadi ikaishinda nyota  ya kifalme iliyopo eneo hilo, maajabu ya mwaka haya. Yaani mlughalugha na anachezea asivyoviweza mwache aumbuke maana haviwezi" Andrew aliendelea kuongea kwa dharau na maneno ya fumbo ya kumkejeli Moses ndiyo yalikuwa yanatoka katika kinywa chake, maneno hayo aliyatamka akiwa na tabasamu usoni mwake huku moyoni akiwa na uchungu sana. Moses alikaa kimya tu akimsikiliza huku nafsi yake ikimfurukuta kwa hasira aliyoidhibiti ili isimuongoze akafanya kitu kibaya, maneno ya Andrew yote aliyaelewa yanachomaanisha na aliamua kunyamaza kiume ili asionekane mtu asiye na akili pindi atakapozifuata hasira zake.

"mtu kama wewe una hadhi gani ya kucheza, kukaa meza na hata kukumbatiana na binti mrembo Beatrice. Wenye hadhi hizo ni sisi na sio kapuku kama wewe." Andrew alizidi kumsema vibaya kwa kumdharau kutokana na kuvaa vitu vya gharama kumzidi na alijiona ni mzuri kumzidi pia, hakika alidanganywa na kioo na hata kitendo kuvaa vazi la gharama ndilo lilimdanganya akajua anaongea na mtu mwenye hadhi ya chini na hata ya kumzidi.

"mali kama ile ni ya kukaa na watu kama sisi watoto wa vigogo na sio wewe mgoroko, sasa usijidanganye kama utampata mtoto kama yule mwenye..." Andrew alishindwa kumalizia kauli hiyo baada ya kuguswa begani na mtu akiyekuwa nyuma yake, alipogeuka alimuona dada yake akiwa amekunja sura kuashiria kutopendezwa na jambo fulani.

"what are you doing Andrew?(unafanya nini Andrew?) what am I told you young bro? (nilikwambia nini mdogo wangu).....Moses sorry kwa maneno ya mdogo wangu" Annie alitoa maneno ya kumlaumu Andrew kisha akamgusa Moses mkono baada ya kusogea karibu naye, Moses akiutazama mkono wa Annie uliomgusa kisha akautoa halafu akaondoka eneo hilo kwa hasira akipita sehemu iliyo jirani na Hilary alipo. Mwendo aliokuwa anatembea na sura yake ilivyo kwa muda huo ilikuwa ni ishara tosha kwa Hilary kumjua Moses kama hayupo sawa na anatatizwa na jambo kwa muda huo. Moses alifika hadi jirani na bwawa la kuogelea kisha akasimama ukingoni huku akiyaangalia maji, alichuchumaa chini huku akiwa kainamisha kichwa na hasira ndiyo zikawa zipo moyoni mwake. Hilary naye alikuwa tayari kashafika hadi eneo ambalo Moses yupo, alimkamata bega Moses kisha akamwambia "yaani ni miaka kadhaa tangu tumefahamiana na katika miaka hiyo yote nimeweza kukujua ukiwa na tatizo hata uwe na tabasamu usoni, tatizo nini bab".

"Man nadhani nimekuja huku kutukanwa sio kusherekea, yule jamaa mwenye macheni ya gold katoswa ndio anakuja kunikejeli mimi akijua ni wa chini sana" Moses aliongea kwa uchungu.

"Bab sikia jamaa yule hata pale alipocheza na  Bite alikuwa kalazimisha na kama asingemshika kinguvu angekuwa amepitwa kama wengine. Hivyo usihangaike nae maana ana maneno ya mkosaji na kuwa mtoto wa waziri isiwe ndio kigezo cha yeye kukukejeli wakati we una mawe na mali tena zako mwenyewe ulizoachiwa sio yule anaringia za baba" Hilary aliongea maneno yaliyomfanya Moses aondokwe na hasira.

"kuvaa vitu vya gharama vya kununuliwa na vya kununua kipi bora? Yaani Mwana we una ishu kibao alizokuachia mzee wako na zinakupa mkwanja daily. Achana na yule asiyejielewa" Hilary alizidi kumuambia Moses kisha akashika mkono akamuinua pale alipokuwa amechuchumaa, Moses muda huo alikuwa amerudi katika hali ya kawaida kama alivyokuwa awali kabla hajakutana na Andrew.


*****


Nyumbani kwa akina Moses hali ilikuwa tofauti na siku zote, ugeni wa watu wawili wenye ngozi nyeupe wakiwa wameongozana na Kennedy mjomba wake Moses  ndio ulioingia. Wageni hao ambao walitambulishwa kwa mlinzi kama wageni waliokuwa na shughuli za kiofisi na Kennedy, mlinzi hakuwa na hiyana na jambo hilo kutokana na kutokuwa na kauli yoyote zaidi ya kukubali. Wageni hao wakiwa pamoja na Kennedy waliingia  hadi kwenye maabara iliyopo ndani ya nyumba hiyo kisha wakapekua mafaili ya humo kwa kuyasoma moja moja hadi wakayamaliza.

"hakuna cha muhimu hapa cha kutuongoza" Mmoja wa wale wazungu aliongea na kupekelea wazungu hao watokee humo maabara kisha wakaelekea sebuleni, walipofika wakabaki wamesimama  kwa sekunde kadhaa bila kujua jambo lolote la kufanya.

"hebu twendeni chumbani kwake" Kennedy aliongea kisha akaanza kupiga hatua kuelekea chumbani kwa Moses, walifika kisha wakaingia  ndani ya chumba hicho cha kisasa mithili ya hoteli ya nyota ya tano. Huko walipekua kila sehemu na hawakuambulia chochote zaidi ya karatasi yenye ramani ambayo ilikuwa inajulikana na Kennedy.

"hii ramani ya nini?" Mzungu mmoja aliuliza kwa sauti ya chini.

"ni ya  kuonesha eneo ilipo hoteli mojawapo kati ya hoteli tano zilizopo chini ya Moses kwa sasa" Kennedy alijibu.

"je kuna mashine ya photocopy humu ndani maana hii ramani nina wasiwasi nayo" Mzungu yule aliuliza kwa mara ya pili.

"hebu twendeni chumbani kwangu mara moja" Kennedy aliongea huku akitoka nje na wageni wake walikuwa nyuma  yake wakimfuata, walifika chumbani kwa Kennedy kisha wakazitoa karatasi hiyo kivuli. Walizirudisha nakala halisi  za mahali walipozikuta kisha wakaondoka bila ya kuacha alama yoyote walipopita.


****


"mabibi na mabwana sasa umefika ule muda wa Beatrice kupokea zawadi kutoka kwa waaalikwa mbalimbali wa sherehe hii, hivyo wageni waalikwa wenye zawadi mbalimbali kwa ajili ya kumpongeza Beatrice kwa kuiona siku nyingine ya kuzaliwa kwake mnakaribishwa kutoa zawadi hizo. DJ wasidindikize watoa zawadi hao kwa muziki mwanana"  Mshereheshaji wa sherehe aliongea kuwajulisha waalikwa kinachofuata katika ratiba ya sherehe, muziki wa kuchangamsha watoaji wa zawadi wamiminike kutoa zawadi ndio uliokuwa ukipigwa kwa muda huo na mtaalamu wa kupangilia nyimbo katika sherehe mbalimbali. Watu mbalimbali walianza kumiminika kutoa zawadi wakisindikizwa na muziki. Utoaji huo wa zawadi ulianza kwa kutangulia watu wa karibu kisha wengine wakafuatia, Andrew na Annie nao hawakuwa nyuma katika suala la utoaji zawadi kwani nao walijiunga na wengine katika suala la utoaji zawadi. Waliongozana kwa kufuatana hadi waliposimama Beatrice na Moses, Andrew akiwa mbele ndiye aliyetangulia kumpa zawadi Beatrice iliyofungwa kwenye boksi lililonakshiwa na mapambo ya rangi nyekundu. Annie naye alifuata katika kumpatia zawadi halafu akakumbatiana na Beatrice kisha akamkumbatia Moses huku akifanya kitu ambacho hakikujulikana na mtu yoyote zaidi ya Moses, kitendo cha yeye kumkumbatia Moses ikikuwa ni mwanya wa yeye kutia kikaratasi katika mfuko wa shati alilovaa Moses akiwa na lengo la kufanikisha azma yake. Hadi muda wa kutoa zawadi unamalizika Moses hakuwa ameangalia karatasi hiyo aliyotiliwa mfukoni na Annie na alikuwa amebaki njia panda na mambo aliyofanyiwa na binti huyo ambaye kwake ni mkubwa kiumri hata kielimu. Mambo yote aliyokuwa anafanyiwa ilikuwa ni ishara tosha ya mtu yoyote kujua lengo la binti huyo kwa mwenye uzoefu wa wasichana ingawa mlengwa anayefanyiwa hakuwa akijua chochote kutokana na ugeni wa vituko hivyo vya wasichana, mawazo yote ya juu ya alichomwambia Beatrice yaliondoka na yakabaki ya  vituko vya Annie hadi akaonekana kwa Beatrice kama alikuwa na mawazo.

"Moses" Beatrice aliitia huku akishika mkono wa Moses hadi akamtoa Moses kwenye mawazo hayo.

"yes" Moses akiitika huku akimtazama Beatrice usoni.

"nakuona hauko sawa, nini tatizo?" Beatrice alimuuliza Moses akiwa anamfuata kwa macho ya udadisi.

"nipo sawa" Moses alimwambia.

"Mmmh! Please usinidanganye"  Beatice alimwambia.

"ok ok siwezi kukuficha juu ya jambo nililokuambia tulipomaliza kula ndiyo linalonitatiza, kukupenda ndio kunanifanya niwe na mawazo hivi. Narudia tena kusema I love you Beatrice" Moses aliongea  kuficha jambo linalomtatiza huku akimtazama Beatrice usoni ambaye alikuwa ameinama uso kwa aibu kutokana na jambo aliloambiwa, alishindwa hata kutoa jibu kumuambia ingawa moyoni alikuwa anashangilia kwa kutamkiwa anapendwa.

"Najua nitakuwa nimekuongezea mzigo mzito kwenye kichwa chako na kukufanya uongeze mambo ya kufikiri tena hili jambo lenye uzito ndio litakufanya uzidi kutafakari, you are queen of my heart Beatrice na sitaki nikuchoshe kwa kufikiri ikiwa bado una mambo mengi ya kufikiri juu ya maisha yako. Jambo langu hata ukiliweka kiporo nitasubiri zaidi na hata ukiliwekea kipaumbele katika kuliongea nitafurahi zaidi. Nakupa muda wa kufikiri zaidi my Queen" Moses alizidi kumuambia Beatrice kisha akampapasa kiganja cha mkono taratibu, hiyo ilimfanya Beatrice azidi kujiona wa pekee na mwenye bahati ndani ya dunia hii kwa kuguswa mkono na hata kupapaswa na mtu aliyepo katika moyo wake na kila upande wake katika maisha yake. Upendo wake kwa Moses ni wa kipekee kwani kila kiungo ndani ya mwili wake kilimsukuma kumpenda kijana hiyo, macho yake yalimsukuma kutamani kumtazama Moses kila anapomuona, pua yake ilimsukuma kunusa harufu asili ya mwili wa kijana huyo iliyochanganywa na uturi anaoutumia nayo aliipenda tangu  mara ya kwanza alipoinusa baada ya kukumbatiana naye. Masikio yake yalipenda kuisikia sauti yake kila siku, mdomo ulipenda kumbusu zaidi  tangu alipombusu kwa mara ya kwanza alipomkumbatia darasani. Kifua chake kilipenda kugusana na kifua cha Moses  tangu alipomkumbatia kwa mara ya kwanza. Yote hayo kutoa jibu papo hapo alikuwa anasita na hata kukataa hawezi maana hata mdomo wake ambao unamuhusudu ulibeba kiungo ambacho kina uwezo wa kukataa ikiwa mdomo utaruhusu kiungo hicho kifanye kazi yake. Ulimi ndicho kiungo ambacho kingemuwezesha kukataa lakini muda huo hakikuweza kutokana kuzuiliwa na moyo  wenye kubeba yazungumzwayo ambao unamuhusudu kijana huyo.  Hivyo alibaki amekaa kimya pasipo kujibu chochote kutokana na kuwa na wasiwasi kuongea neno lisilo sahihi kwa ampendaye, kila neno aliloiaka kuliongea aliliona halifai na kimya aliona ni bora kuliko kuongea jambo lisilofaa kwa ampendaye. Yote hiyo ilikuwa ni mitazamo yake ingawa aliweza kuongea neno lolote.  Muda huo wote alikuwa amezama kwenye fikra huku akichezea vidole vya mikono ya Moses  aliyekuwa akimpapasa kiganja cha huku macho kainamisha chini. Walikuwa mbele wakiwa wamezibwa na lundo la zawadi lililopo juu ya meza iliyopo mbele ya kiti walichokalia, kitendo wao kugusana mikono hakikuwa kimeonekana na mtu yoyote.

"mabibi na mabwana sasa umefika ule muda wa kufanya tukio la mwisho litakalofunga sherehe hii, tukio hilo ni kucheza muziki utakaofunguliwa na Beatrice pamoja na Moses. Sasa basi Moses na Beateice mnaombwa kusogea mbele ili mfungue muziki huo" Sauti ya Mshereheshaji ndiyo ilisikika na ndiyo ilimfanya Beatrice atoke katika mawazo juu ya jambo alilokuwa anaambiwa, Beatrice aliinuka huku akiwa amemshika mkono Moses kisha akatembea hadi mbele ya watu wote. Alisimama akawa anatazamana uso kwa uso na Moses wakisubiri muziki uanze kupigwa, muziki wa taratibu ndiyo uliyotumika kufungulia muziki huo na Beatrice na Moses ndio waliofungua kwa kucheza kwa namna ya kipekee na yenye kuvutia. Watu wengine walimiminika wawili wawili katika kuucheza muziki huo baada ya kuvutiwa na uchezaji wa wafunguzi wa muziki huo, baada ya muda mchezeaji wa santuri za muziki alibadilisha wimbo kwa makeke huku watu wakibadilisha aina ya uchezaji kuendana na muziki uliowekwa. Mnamo saa sita kamili ya usiku  sherehe ilifungwa rasmi na watu wote wakawa wapo katika harakati za kuondoka ili wawahi kufika na wengibe ambao ni marafiki wa karibu wa Beatrice pamoja na ndugu walilala hapo. Moses naye alikuwa anajianda kutoka ili aondoke akamsubiri rafiki yake kwenye gari.

"Moses unaitwa na mama" Ilikuwa ni sauti ya Victoria ikimuita Moses pindi alipotoka kuondoka na ikamfanya aongozane na Victoria hadi ndani, akipelekwa pale sebuleni alipoingia awali wakati anawasili katika sherehe hiyo. Hapo alimkuta Mama Beatrice akiwa amekaa kwenye kochi sambamba na Beatrice.

"Moses baba unaondoka?" Mama Beatrice alimuuliza

"ndiyo mama naondoka maana muda umeenda" Moses alijibu.

"sasa baba ndiyo hutuagi" Mama Beatrice alimwambia

"ooh! Samahani mama nilighafirika kidogo" Moses aliomba radhi.

"bila samahani baba, asante kwa kuifanya sherehe ya mwanangu iwe na furaha. Haya wasalimie" Mama Beatrice alimuaga Moses.

"haya" Moses aliitikia

"we dogo mbona mwenzio alitaka kututoroka," Victoria naye aliongea kwa kuweka utani.

"mmh! Nawe ushaanza sasa, Moses nisubiri kwenye parking please" Beatrice aliongea baada ya Victoria kutumbukiza utani na kusababisha Victoria acheke.

"haya jamani tutaonana Mungu akipenda, usiku mwema" Moses aliaga kisha akatoka sebuleni baada ya kupeana mkono na Mama Beatrice. Alienda hadi kwenye maegesho ya magari alipoacha gari yake, hapo alikuta gari aina ya landcruiser prado nyeupe ikiwa ipo jirani na gari yake. Gari hiyo hakuitilia maanani na alijua ni ya ya hapo nyumbani baada ya magari ya waalikwa kuondoka, alipokuwa analikaribia gari hilo ndipo akawaona Andrew na wenzake wakiwa wameiegemea.

"vipi unataka tukupe lifti maana hiyo BMW ni  ya watu na sasa hivi daladala hamna?" Andrew alimuuliza Moses kwa kejeli huku wenzake wakicheka.

"we mgoroko ongea basi kama unataka lifti" Mmoja wa marafiki za Andrew aliongea akijua Moses ni wa kawaida tu, Moses alibaki anawatazama huku hasira zikiwa zimempanda.

"tumpeni lifti jamani" Rafiki mwingine wa Andrew alidakia, Moses alijikuta akitaka kupigana nao lakini aliamua kuwaziba mdomo kwa namna ya kipekee, alitoa ufunguo wa gari kisha akqminya rimoti iliyopo kwenye ufunguo huo. Gari aina ya BMW nyekundu waliyosema ya watu ndiyo ilitoa mlio wa kuashiria ile ni rimoti yake.

"najivunia nina mali zangu na sijivunii mali za baba yangu, siwezi nikaja na gari ya kuendea sokoni kwenye sherehe kama hii wala sibishani na kapuku  kama wewe" Moses alimwambia  Andrew ambaye alikuwa kakaa kimya muda huo na dharau zote zikiwa zimemuisha. Hakutegemea Moses atakuwa amekuja na gari kama hiyo, alikuwa anaipenda gari hiyo na hata alipoingia eneo hilo alikiri mwenye hiyo gari ni mwenye uwezo ingawa hakutegemea kama itakuwa inamilikiwa na mtu aliyekuwa anamdharau. Alibaki kapigwa na butwaa huku Moses akiwa yupo mlangoni mwa gari baada ya kuondoka alipo Andrew,  Moses alipotaka kufungua kitasa cha mlango sauti ya kuitwa kwake na Beatrice ilisikika. Moses aligeuka akamuona Beatrice akija eneo alilopo, alisimama akimsubiri hadi alipofika karibu yake.

"yaani umeaga wote ila mimi hujaniaga" Beatrice aliongea kwa sauti ya chini ambayo haikusikika na wakina Andrew ambao walikuwa wanawatazama.

"sio hivyo" Moses aliongea akiwa anatazamana uso kwa uso na Beatrice. Beatrice alimtazama Moses kwa macho malegevu kisha akafanya tendo ambalo lilikuwa mwiba kwa Andrew alipoliona, alimbusu Moses kwenye papi za mdomo kwa sekunde kadhaa kisha akamuachia huku akiwa amegusanisha paji lake la uso na la Moses.

"I love you too" Beatrice alimwambia  Moses kwa hisia tena kwa sauti ya juu kidogo hadi Andrew akasikia kutoka pale alipo.




ITAENDELEA!!

No comments:

Post a Comment