Friday, December 4, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA MWISHO





     DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



SEHEMU YA MWISHO!!
 Vijana hao walifaniliwa kuwateka Ally na Jamadin na kuondoka nao ambapo njiani Ally alipigwa kisogoni akazirai akatupwa kando ya reli mita chache kutoka katika mzunguko wa Kwa Minchi majira ya usiku, kupotea kwa Jamadin na Ally nyumbani kwangu ilikuwa ni huzuni sana kwa mke wangu lakini kwangu mimi ilikuwa ni kawaida kwani nilikuwa najua kila kitu. Tulikusanyika nyumbani wanaume wote huku mimi nikionekana kulia sana na nilibembelezwa hadi nikanyamza ndipo tulipoanza kujadiliana kimaigizo nini cha kufanya, baada ya mjadala wanaume wote sita tulikubaliana tuongie mtaani kumtafuta Jamadin na Ally na wake wote wakakaa nyumbani kwangu wakimbembeleza Farida.


****




Tuliwaacha wake zetu na matumaini hewa ya kurudi wakiamini tulikwenda kumtafuta kumbe tulikwenda  kufanya kitu kingine tofauti na kumtafuta mtoto huyo, haikuwa safari ya kwenda kumtafuta Jamadin kama walivyokuwa wakifikiria bali tulikuwa tunaenda kumalizia shughuli yetu tuliyoambizana na mganga Sauti ya Radi ikamilike siku hiyo. Sehemu ya kwanza baada ya kutoka nyumbani kwangu ilikiwa  ni Kisosora  upande wa ufukweni mwa bahari ya Hindi jirani na kichaka kimoja, hapo tuliwakuta wale vijana wakiwa na Jamadin waliyemfunga kamba ngumu pamoja na kitambaa mdomoni ili asipige kelele. Walitukabidhi Jamadin kwani tulikuwa tushamalizana nao kila kitu na ilikuwa ni kuagana  baada ya kukabidhiana tu, hicho ndicho kilifanyika hapo na sisi tukaianza safari ya kuekea mpirani ambapo tulifika majira ya saa ya tano usiku tukiwa na asusa yetu. Ilipokaribia saa sita mganga alianza kuandaa mazingira ya kuanza ikiwa ni pamoja na shimo kubwa kuchimbwa katika eneo la sebule ambalo ndiyo hapa tumekaa, baada ya kazi hiyo kukamilika alituambia tulizunguke shimo hilo tukiwa na kisu mkononi kila mmoja ambavyo vilikuwa vimefungwa vipande vya kaniki nyekundu upande wa kwenye mpini wa kushikia. Mganga alianza kazi yake kwa kupiga manyanga huku akiimba nyimbo alizozitambua yeye na baada ya muda upepo mkali sana ulisikika ulivuma kama kimbunga kuizunguka nyumba tuliyomo, upepo huo uliendelea kuvuma hadi mlango mkubwa wa kuingilia sebuleni hapo uliokuwa umefungwa ulifunguka kwa nguvu sana. Ulikuwa ni upepo wenye kuogopesha lakini mganga alituambia tusitetereke na lile duara letu kulizinguka shimo tulilolichimba tuache uwazi upande unaotazamana na mlango, Hamis na Falzal ambao walikuwepo katika upande huo walijisogeza pembeni kwa kutusukuma sisi na sisi tulisogea ili waweze kutimiza maelekezo ya mganga ya kupisha njia. Upepo ule mkali uliendelea kuvuma na ulizidi kutuogopesha sana lakini tulijikaza kisabuni kama watoto wa kime, ulizidi kuvuma na hatimaye ukaingia ndani ukapita pale kwenye upenyo wa duara letu ukaingia hadi kati ya shimo tulilochimba ukajenga sura ya mtu kwa kutumia vumbi la kimbunga ambalo ndilo liliingia nalo. Kitendo cha kuona umbile la mtu katika upepo huo tulijikuta tukitamani kukimbia ilikuwa inaogopesha sana sana lakini mganga alitusihi tusikimbie na tufanye kile atakachotuambia, mganga kwa kitendo cha upesi alimwaga ile damu ya mwezini ya mwanamke kulizunguka shimo hilo  na ule upepp ukawa unajaribu kutoka ndani ya eneo lililozunguahiwa damu lakini ulishindwa kwani ulipokaribia mpaka wa ile damu ambayo ni ya Shemeji Salma ulirudi huku sauti isiyoeleweka kama ya popo aliyejeruhiwa ndiyo ikawa inasikika kutoka kwenye ule upepo. Mganga baada ya kuhakikisha ule upepo umeshindwa kuivuka ile damu ya Mwezini alituamrisha tuchome visu vyetu kwa pamoja katika sehemu ya kifua na ya mgongo ya umbo la mtu lililotengeneza na upepo huo kwa kutumia vumbi jingi lililosababishwa na huo upepo, wote kwa pamoja tulichoma visu vyetu kwemye huo upepo ambavyo vilitupa hisia ya kwamba tumetoboa kitu hadi makelele ya popo aliyejeruhiwa yakssikikakwa nguvu kwenye ule upepo kisha ukazama ndani ya shimo kwa mara moja. Hapo ndipo mganga akambeba Jamadin aliyekuwa kafungwa kamba akiwa anafurukuta aweze kutoka lakini alishindwa kutokana na kamba ngumu alizokuwa amefungwa, alimuingiza ndani ya shimo hilo kisha akaliingiza lile jeneza tulilolileta ndani ya shimo pamoja na chupa. Alimlaza Jamadin juu ya jeneza kisha akatuamuru kila mmoja amchanje mara sita kwa kutumia kisu alichonacho mkononi, sote tulifanya ambapo Jamadin alitoa ukelele wa maumivu lakini hatukumjali hata kidogo mpaka tulipomaliza kumchanja ndipo tulipoanza kuona ajabu jingine lilitokea katika mwili wa Jamadin baada ya yeye kutanua mdomo apige kelele tulipomaliza kumchanja lakini kelele hazikutoka zaidi ya kutoka mwanga mweupe ulioingia ndani ya chupa. Mganga aliifunga ile chupa kwa kukaza sana kifuniko halafu akaiweka ile chupa pembeni, alipomtazama Jamadin nasi tulimtazama ndipo tukaona ajabu jingine lililopo kwemye mwili wake ambalo awali hatukuliona. Shingoni mwa Jamadin tuliona amevaa mkufu wenye vito vyenye kuvutia ambavyo hatujawahi kuviona duniani na mpaka hii leo havijawahi kuonekana sehemu yoyote. Mganga aliniamuru niuvue ule mkufu shingoni mwa Jamadin niuvae mimi nami nikafanya hivyohivyo ambapo nilishuhudia maajabu mengine ambayo sikuwahi kuyashuhudia kwani ule mkufu nilipouvaa haukuonekana kifuani mwangu, kitendo cha kuvaa mkufu tu wenzangu wote vifuani mwao kulitokea mwangaza  wa kung'aa kisha ukafifia papo hapo tukabaki tukishangaa lakini mganga aliishia kutabasamu tu kisha akatueleza sasa tupo miongoni mwa watu matajiri duniani kutokana na nguvu ya mkufu huo hivyo tujipongeze kwa hilo. Kauli hiyo ulitufanya wote tufurahi sana kwani ndiyo ulikuwa mwisho wa kuteseka na kasumba iliyotukumba ghafla katika maisha yetu na sasa ni muda wa kufurahia maisha, baada ya hapo ule mwili wa Jamadin tuliuweka ndani ya lile jeneza jeusi na tuliliinfiza shimoni halafu zoezi la kufukia ndiyo lilifuata hadi likaisha. Mganga naye alifanya maajabu  yake eneo lile likawa kama halijachimbwa awali wala halikuwa na muonekano wa eneo lililochimbuliwa, baada ya zoezi hilo ndipo tulirudi mjini haraka sana na tulienda hadi kwa minchi tukamuokota Ally kwanj tulijua ni eneo gani ametupwa. Tulirudi naye nyumbani tukiwa hatuna Jamadin katika mikono yetu na hiyo ndiyo ilikuwa siku ya huzuni kwa Farida kwani alilia sana kutokana na hilo, kazi ya kumbembeleza ikawa kwetu sisi pamoja huku mioyoni mwetu  tukitambua wazi tunafanya unafiki kwani tunatambua ni kila kitu. Siku iliyofuata wasamaria wema walileta mwili wa Jamadin uliokotwa Kisosora na walikuwa na asilimia mia kuwa yule ni Jamadin lakini hakuna aliyekuwa anatambua kuwa Jamadin tulishampoteza na tukamzika mpirani, mazishi ya mwili wa  ulioletwa yalifanywa huku Farida akiwa na uchungu mwingi sana hadi nikawa namuonea huruma lakini ilishatokea. Baada ya muda taarifa hiyo ilishasahaulika kidogo ndipo siku moja tukiwa tushaanza kuingia katika mafanikio Ally kwa bahati mbaya alitusikia tukizungumza kuhusu hilo suala  tulilolifanya tukiwa  na Salma, siku hiyo Ally alitufokea sana lakini niliweza kumdhibiti baada ya ule mkufu kutokea kimaajabu kifuani mwangu kisha ukaachia mionzi yake iliyoenda kumuingia na kuanzia hapo akawa anatusikiliza sisi tu na si mwingine".

Simulizi ya Shafii iliishia ambapo ndiyo simulizi iliyokuwa imemvua nguo zote mbele ya kila mtu hapo ndani kwani ubaya waliouficha sasa uliluwa umeshagundulika, Bi Farida alimtazama Shafii kwa chuki za wazi baada ya kubaini upande wake wa pili wa maisha yake aliouficha kwa kipindi. Hakuna mwingine ambaye aliyekuwa ametarajia kama Shafii angeweza kufanya vile kwa mtoto asiye na hatia kama Jamadin, ilikuwa ni huzuni iliyojaa chuki za wazi baada ya kila mmoja kubaini uovu uliokuwa ukifanywa na Shafii kwa takribani miaka ishirini na sita iliyopita. Baada ya simulizi hiyo hata Mzee Mahmud aliyekuwa akiitambua simulizi hiyo alisikitika pia kila akimtazama  Shafii kwani alijua  alikuwa amefanya janga kubwa tofauti na yeye alivyokuwa anadhani, alibaki akimuangalia kwa sekunde kadhaa kisha akajikohoza ili kusafisha koo lake apate kuongea bila sauti yake kukwaruza.
"Shafii hivi unajua ni kitu ulichokifanya mpaka dhahama hii inawakumba wenzako na hadi sasa mliousuka  mpango huo mmebaki wewe na Salma tu kwani mliyemkosea tayari ameshawapoteza Falzal, Hassan na Hamis. Kwanini lakini unafanya mashindano na kiumbe  usiyemjua Shafii?" Mzee Mahmud alilalamika kisha akamtupia jicho Zalabain halsfu akamnyooshea kidole akasema, "umemuona huyu aliyeingia na Farida na Zayina? Ulijua utamuua siyo mlipouchimbia mwili wake hapa tulipokaa? Huyo ndiye Jamadin mwenyewe na hakufa kama mnavyofikiria, na ile chupa iliyofungiwa kitu kilichokuwa kinatoka mdomoni mwake ilifunguliwa  na huu mwili mliofukia ukatolewa akarudi kama awali. Hivi we mtoto unamjua ni nani huyu uliyekuwa unamfanyia ubaya huo? Loh! Nakuonea huruma sana kwa ujinga wako ulioufanya mwanangu.... Jamani ngoja nimkaribishe  mgeni mwingine ambaye sikuwaambia kama atakuwepo katika eneo hili aje awaeleze kuhusu asili ya Jamadin. Mzee Mubaraka karibu tafadhali" Mzee Mahmud alimlaumu sana Shafii kwa kitu alichokifanya na alitumia muda huo kumtambulisha Jamadin ambaye anajulikana alikufa mbele ya wote hapo ambapo wengine walishtuka sana walipolijua hilo, alitumia fursa hiyo kumkaribisha mgeni mwingine ambaye anajulikana hapo kama baba yake Faimu aliyekuwa lulu kwa warembo wa miaka mingi iliyopita ambao sasa hivi warembo hao walikuwa kina mama wanaoukimbilia uzee.
Ukaribisho wa Mzee Mahmud ulifafanya watu waangalie mlangoni ambapo walimuona mzee wa kiarabu mwenye ndevu nyingi aliyevalia kanzu safi ya rangi nyekundu na kofia akiingia ndani humo, alionekana ni mzee hasa lakini hapo alikuwa alitembea vizuri kama kijana wa kawaida tofauti na watu wengine waliomzoea. Mzee huyu hakuwa mwingine bali ni mzee Mubaraka ambaye baada tu ya kuingia alitoa salamu kwa wote na kupelekea kidevu chake kilichobeba ndevu nyrupe zilizosimama kama mwiba kicheze baada ya kinywa chake kufunguka. Salamu yake iliitikiwana watu wote na mzee huyu alienda moja kwa moja hadi kwa Zalabain akatoa salamu ya heshima kama wafanyavyo vijakazi wakifika kwa watukufu wa familia ya kifalme, salamu hiyo iliwashangaza sana watu wote kwani hawakuelewa kwanini mzee huyo alisalimia kwa salamu hiyo.
Iloonekana ni babu na mjukuu wake kwa jinsi walivyofanana lakini kusalimia kwa namna ile ndiyo kuliwapa swali jingine lisilo na libu katika vichwa vya watu wote waliopo eneo hilo, Mzee Mubaraka hakujali mishangao iliyowapata waliomo humo ndani yeye alienda kuketi jirani na mzee Mahmud.
"Naam mzee Mubaraka najua watambua suala lote uliloitiwa hapa sasa naomba ueleze asili yake jina lako na asili ya Faimu pamoja na Jamadin na vingine vyote" Mzee Mahmud aliongea huku akimtazama Mzee  Mubaraka usoni ambaye alitikisa kichwa kuashiria amekubaliana naye.
Mzee Mubaraka alipopewa ruhusa hiyo aliwatazama wote waliopo humo ndani kisha akasema, "kwa jina naitwa Mubaraka bin Yaktwash ni jini niliyezaliwa katika himaya ya majini ya Majichungu". Alikatisha kidogo kusimulia kisha akawatazama waliopo mule ndani ambapo wengine walionesha kushtuka kusikia taarifa hiyo, hakuwajali mshtuko wao na aliendelea, "Nimezaliwa miaka elfu mbili iliyopita katika himaya hiyo na nilipoanza kuwa kijana nilianza kufanya kazi nikiwa kama mtumishi wa ndani ya kasri la mfalme Zulain, nikiwa nina miaka mia tano tangu nizaliwe katika alizaliwa mtoto wa pekee wa mfalme wetu mtukufu aliyeitwa Zaif. Mtoto huyo nilikabidhiwa kuwa msaidizi wake hadi anakua mkubwa na alikuwa ni mtoto mwenye kupendwa sana na wanamajini wote wa himaya hiyo kwani alionekana aliwa mwerevu tangu yupo mdogo, Nilikuwa mlezi na msaidizi wake kwa muda wa miaka mingi sana hadi alipotimiza miaka elfu na mia tano mimi nikiwa nina miaka elfu mbili. Zaif kwa kipindi hicho alimuaga baba yake anakuja kufanya matembezi duniani na kukaa kwa muda kidogo ili aweze kuyaona maisha ya wanadamu yalivyo, alikubaliwa na baba yake kwa mikono miwili na akapewa angalizo la kuwa makini na wanadamu kwani siyo viumbe wazuri. Alikabidhiwa watumishi wawili na mmojawapo akiwa ni mimi na mwingine ni jini wa kike mwenye taaluma ya upishi katika kasri la mfalme, wote kwa pamoja tuliingia duniani kama wasafiri na tulifikia kijiji cha Bwagamacho ambapo nilijitambulisha kama Mubaraka na yule jini wa kike nilimtambulisha kama mke wangu na mtoto wa mfalme wetu mtakatifu nilimtambulisha kwa jina la Faimu nikimtaja ni mtoto wangu wa kumzaa.
Tuliyaanza maisha yetu ya happ kijijini karibu  kila mwanakijiji akidhani sisi ni wanadamu tena wa familia moja kasoro Mzee Mahmud hapa ndiye aliyeweza kubaini sisi ni majini ila hakuwa na neno na sisi baada ya kutubaini hatukuja kwa nia mbaya eneo hilo, maisha yetu yaliendele kwa amani hapo kijijini ambapo Faimu akiwa nje ya nyumba alikuwa akitupa heshima kama wazazi wake ila tulipokuwa ndani mbali na upeo wa mwanadamu yeyote tulikuwa tulimpa heshima kama mwana wa mfalme wetu mtukufu. Hadi Faimu anaanza kupendwa na wasichana hapo kijijini tayari tulikuwa tumeshabaini hilo suala na walipokuja kujitolea kufanya kazi tulikuwa tukiwacheka sana wanadamu kwa jinsi walivyo na papara ya kupenda tu, kwa Faimu ilikuwa ni burudani tu kwani alikuwa anajifunza mengi jinsi binadamu alivyo ambavyo yeye alikuwa hawajui zaidi ya kuwasikia. Aliishi maisha ya kibinadamu tu na alikuwa akiona fahari sana kubadilishana mawazo na wanadamu ingawa wa rika lake wengi walikuwa wanamchukia, hata alipokuwa na urafiki wa pamoja  kati yake na wanawadamu ambao ni Shafii na Hamis alikuwa akifurahi sana hata siri walizokuwa wakizificha aliluwa akizijua sana. Kipindi hicho alishajua uwepo wa Farida kwa kutumia nguvu zake za  kijini na alimpenda sana ingawa alitaka ajithibitishie kama anapendwa na hakuwa tayari kutumia uwezo wake kumuingilia na kumshawishi, alikuwa akitusimulia sisi watumishi wake ambao alitufanya kama washauri wake wakuu. Nasi tulimshauri asitumie nguvu bali ahakikishe anapendwa naye na kama hapendwi aache, ushauri huo alioufuata na akasubiria ziku ya kuonanana na Farida hadi ilipowadia. Hakumlazimisha Farida kuwa na mapenzi bali alikubali kwa hiyari na uhusiano ukaanza, huku huyu Ally akiwa mtu wa kwanza kubaini kwani ndiye aliyekuwa akipendwa hasa na Faimu kati ya wanadamu wote hapo kijijini. Uhusiano wake ulipovurugwa alionekana ni jinsi gani ameuzwa lakini hakutaka kutumia nguvu zake  kabisa na aliishia kumuomba penzi Farida kisimani akaambiwa anataka kubaka akapigwa sana akionekana hafai mwishowe akaondoka hapo kijijini baada ya kufukuzwa na hakuwa tayari kutumia nguvu zake  na hata mtukufu mfalme aliposikia alitaka kuwaangamiza wanadamu hao lakini kwa huruma ya mwanae akawaacha. Jambo ambalo wanadamu hawa hawakulitambua  ni kwamba dawa waliyompa Farida kila siku usiku ilikuwa  inapunguzwa na Faimu na hapo Farida hurudi katika akili na hukutana kimwili na Faimu kwa kipindi hicho chote huwa alikuwa anamjia kwa njia ya ndoto, hadi huyu bwana hapa anamposa Farida baada ya kumuweka chini yake kwa kutumia nguvu za kichawi tayari huo mchezo Faimu alikuwa anaendelea na ndiyo katika kipindi hicho akawa anamuona anaweweseka na hata alipokuja kuacha tayari Farida alikuwa ana ujauzito wa Faimu huyu bwana akidhani ni wake. Jamadin alipozaliwa Faimu alikuwa yupo makini sana katika kumlinda mwanae kuliko kitu kingine chochote pia alimpatia mkufu wenye kidani kinachoitwa Dainun ili umlinde na hadi hawa mabwana wanataka kumtoa kafara Jamadin kipindi hicho akiwa na miaka mitano hapa duniani na mmoja kwamujibu wa mila za kijini ambazo miaka mitano ya kwanza ya mtoto huhesabiwa ni mwaka mmoja .  Faimu alishajua hilo na alifika eneo hili akiwa na jazba sana. Alifanya hila ya kutengeneza upepo nje ili aharibu kazi yao kisha aliingia ndani akiwa yupo  kama kimbunga ndipo alipojikuta amenasa kwa kuzungushiwa damu ya hedhi ya mwanamke akawa hawezi kutoka kwani ina madhara sana kwake kama akiisogelea, hapo ndipo mabwana hawa wakamchoma kwa pamoja visu vilivyochovya kwenye damu ya hedhi  katika mwili  wake na kumfanya apate jeraha kubwa. Faimu aliishiwa nguvu na alizama chini ya ardhi mimi nikaja kumtoa nikampeleka kwa mtukufu mfalme ili apatiwe matibabu kwa jereha hilo, kuanzia siku hiyo Faimu alikuwa mtu wa kukaa kitandani kwani mkufu wenye Dainun ambao ni mali yake ndiyo ungeweza kumponya tu. Baada ya mwaka mmoja Faimu alifariki akitoa tamko mwanae ndiye aje kukaimu nafasi yake ya ufalme atapofariki baba yake, agizo jingine alilotoa ni kisasi chote kilipwe na mwanae tu. Kiongozi Zalabain au Faimu alipokuja kupatikana taji lilimkataa mpaka upatikane huu mkufu na kisasi kulipwe kwani hawa ndugu ndiyo chanzo kuzaliwa watoto waliodumaa katika himaya yetu kutokana na kutoonekana kwa usiku kwa  muda mrefu".
Mzee Mubarak alimaliza simulizi yake iliyomliza sana Bi Farida baada ya kusikia kuwa Faimu kwa muda huo ni marehemu, mzee Buruhan aliposikia hiyo habari hasira zilimzidi maradufu na akasimama wima huku akihema kwa nguvu.
"Mzee mwenzangu tulia basi walsu kidogo tumalizie" Mzee Mahmud alimsihi rafiki  yake.
"Sihitaji hata kuendelea kumuangalia huyu mwanaharamu na sina mtoto kama yeye ngoja niondoke nje mkimaliza mtanikuta" Mzee Buruhan alisema kwa jazna kisha akaanza kutembea kuelekea nje.
"Baba usifanye hivyo"  Shafii alilalamika kumsihi baba yake.
"kelele wee! Shaytwani mkubwa usiniite baba yako na sina mtoto kama wewe mtoto wangu ni Ally tu" Mzee Buruhan aliongea kwa ukali kisha akatoka nje akamuacha Shafii akilia kwa uchungu, muda huo huo Ally naye akainuka akamtazama Shafii kisha akamtazama na Salma halafu akamtazama Hamida kwa huruma sana.
"Salma naomba unipatie mwanangu niondoke naye" Ally aliongwa kwa ustarabu halafu akamuangalia Mzee Mahmud akamuambia, "Baba huyu mwanamke ni zaidi ya shetani yaani kanitumikisha kama mtumwa wa ngono kwa miaka mingi baada ya ule mkufu kunifanya niwapende na ushenzi wao, sijaoa wala kuwa na mke  na umri huu matokeo yake napata  mtoto kupitia huyu malaya tena mke wa mtu. Hebu muulizeni Hamida ni mtoto wa nani".
Ally alipoongea maneno hayo hadi Shafii aliweka mkono  kinywani kwa ujinga alioufanya Salma ambaye aliishia kuona aibu tu, aliinamisha kichwa chini kutokana na fedheha iliyomkuta hadi wanae wakawa wanamuona ni binadamu wa ajabu.
"Salma huyo Hamida ni mtoto wa nani?" Mzee Mahmud aliuliza taratibu huku akimuangalia Salma kwa Macho ya ukali sana, Salma alishindwa kujibu na akakaa kimya akiwa ameinamisha macho chini hadi alipokaripiwa.
"wa  A....A..Ally" Salma alijibu huku akitazama chini kwa aibu na kupelekea mwanae mkubwa Jamal asimame akawa anaenda alipo Ally ambapo ni jirani na mlango wa kutoka mje ili aondoke, Salma alimshikilia miguu mwanae lakini alijikuta akisukumwa kwa nguvu.
"Bora ningezaliwa na shetani kuliko wewe" Jamal aliongea kwa hasira halafu akatoka nje huku akilia kwa uchungu, Hamida naye alinyanyuka kisha akaanza kumtazama mama yake huku machozi yakimtoka kwa uchungu. Salma alipotaka kumkumbatia miguuni alimsukuma kwa nguvu halafu akaenda halipo Ally akawa anamtazama huku machozi yakimtoka, Hamida alimkumbatia baba yake kwa mara ya kwanza huku akilia na Ally naye alimpokea mwanae huku machozi yakimtoka kwa alichofanyiwa.
"Baba samahani naondoka humu nikiwa nina mwanangu, sina kaka humo" Ally alizungumza kwa hasira halafu akatoka nje akiwa na Hamida, Salma alipotaka kuwafuata alijikuta hawezi kuinuka kabisa.
"Shafii nadhani unakumbuka jana jioni nilikuambia  leo ndiyo utapata nafuu ya tatizo lako, sasa basi napenda utambue kuwa sikumaanisha litatuliwa basi nafuu yenyewe ndiyo hii ya kuwaona Bi Farida na Zayina ila si kukusaidia zaidi kutokana na udhalimu mlioufanya. Niliwaonya  msifanye hivyo tangu mnaenda kumuwekea dawa Farida lakini hukusikia kwa ubishi wako, sasa  mwanangu donda la kujitakia halihitaji pole  uguza bila msaada wala pole. Nadhani Zalabain Jamadin ana mengi  ya kuongea na wewe mkiwa wewe na Salma sasa mtazungumza naye wawili, mimi sisaidii madhalimu kama nyinyi" Mzee Mahmud naye aliongea kisha akanyuka akasema, "lengo langu ilikuwa kumnasua Ally maana naye angekumbwa na balaa  lisilomuhusu na nimefanikiwa sasa nawatakia mazungumzo mema na Zalabain".
Mzee Mahmud alitoka nje akazidisha machungu sana kwa Shafii ambaye alilia sana pia Salma naye alijuta kwa yote aliyokuwa akiyafanya kwani hakuwa na muda wa kurekebisha tayati alishachelewa kabisa.
Mzee Mubaraka, Bi Farida pamoja na Zayina nao walinyanyuka wakabakisha watu watatu tu waliobaki humo ndani na walianza kutembea kwataratibu kuufuata mlango ulipo.
"Mke wangu, mwanangu" Shafii aliita huku akinyoosha akiwa anazidi kulia sana kwani hakuwa anaweza hata kunyanyuka, maneno yake yalimfanya Bi Farida asimame kisha akamsonya kwa nguvu halafu akasema, "mkeo nani kwa ndoa ipi? Sina mume kama wewe".
Bi Farida alipimaliza kuongea hayo maneno alitoka nje kwa hasira akiwa amemshikilia Zayina aliyekuwa analia tu kutokana na kilio cha  baba yake lakini alimuacha apate  adhabu kwa uovu wake
Zalabain alipohakikisha mtumishi wake,mama na dada yake wametoka nje alimama wima akiwa na macho yaliyojaa ghadhabu sana akawasogelea Shafii na Salma, alimuangalia Salma kwa macho makali halafu akamsogelea karibu zaidi na kusababisha Salma atokwe na haja ndogo papo hapo.
"Wakati unatoa damu yako ya hedhi  iliyosababisha baba yangu afe mbona hukujikojolea, ulijua na mimi itaniua wakati mnanichanja na visu vyenu nilikuwa nina Dainun shingoni mwangu. Sasa leo zamu yako" Zalabain aliongea kisha akaushika shingo ya Salma akaiminya kwa nguvu hadi mishipa ikapasuka damu zikaanza kuvuja, alishika na kichwa akakivuta akakichomoa kabisa  halafu akamgeukia Shafii akamwambia "nipe".
Shafii kwa uoga aliokuwa nao aliposhuhudia Salma alivyouawa aliweka mkono kifuani mwanga ukatokea na hapo mkufu ukaonekana ukiwaka halafu ukazimika ghafla, kuzimika kwa mkufu kulimfanya Shafii ashangae sana akabaki akimuangalia Zalabain huku  akitetemeka.
"He! Ulijua hiyo Dainun itatoa mwanga uniue nayo, kwa taarifa yako nguvu kubwa ya Mzee Mahmud inaizuia hiyo isifanye kazi. Nipe!" Zalabain aliongea huku akimsogelea Shafii akiwa na jazba, Shafii hakuwa na ujanja aliivua Dainun akampatia Zalabain huku akitetemeka.
Zalabain aliichukua Dainun akaivaa shingoni mwake na kusababisha Dainun  ipige mwanga mkali ulioenda juu kisha ikaanza kung'aa, alitoa tabasamu kisha akanyooshea  Shafii kidole akamuambia, "umenipatia kimoja bado kingine tumalizane kabisa".
"Kipi?" Shafii aliuliza huku akitetemeka
"roho yako" Zalabain alijibu na macho yake yakaanza kutoa machozi ya damu tabasamu likawa limefutika usoni
"hapana" Shafii alisema huku aliweka mikono ishara ya kuomba msamaha lakini haikusaidia kitu kwani Zalabain alijigeuza kimbunga kikali kikamvaa Shafii kikawa kinamzungusha na kupelekea Shafii atoe mayowe ya maumivu yaliyosikika hadi nje, taswira mbaya ya kuruka kwa damu pembeni wakati akizungushwa ndiyo ilionekana na kisha vipande vya mifupa vvikaruka pembeni vikiwa na damu tupu. Muda huo tayari Shafii alikuwa ameaga dunia kutokana kupata mshahara kwa kile alichokifanya miaka mingi iliyopita.

****

Watu wote waliokuwa nje walisikia kelele za Shafii lakini hakuna hata oja aliyethubutu kumsaidia na makelele yalipotulia haukupita muda mrefu nyumba yote ikaanza kuporomoka yote kisha ardhi yake ikafunguka kifusi chote kikazama na huo ndiyo ukawa mwisho wa Shafii, watu waliona kitendo hicho walisikitika sana wengine walitokwa na machozi kwani ingawa  kafanya mabaya bado alikuwa na nafasi kwa baba yake na mtoto wake.
Kulipotulia kabisa Zalabain alitokea akiwa ana Dainun shingoni mwake akamchukua mama yake na dada yake pamoja na mtumishi wake wakaondoka, waliobaki walitafita nyumba za kulala hapo Mpirani usiku huo baada ya kushuhudia mwisho wa dhahama ya kujitakia


****



Miale ya Dainun iliyopiga angani ilisababisha mwangaza wa kawaida kurejea katika himaya ya Majichungu, ndelemo na vifijo kutoka kwa majini wa aina mbalimbali ndiyo  zilisikika na siku iliyofuata sherehe ilifanywa katika viwanja vya kasri la kifalme. Zalabain alivikwa rasmi taji la ufalme ambalo halikumkataa lilikaa kwenye kichwa chake vizuri kabisa, sherehe kubwa ilifanywa ilishuhudiwa na dada yake pamoja na mama yake wakiwa na furaha kama alivyokuwa yeye ana furaha.


MWISHO!!


NAPENDA NIMSHUKURU MWENYEZIMUNGU KWA KUNIJALIA AFYA NA UHAI HADI NAMALIZA HII RIWAYA, NAPENDA NIWASHUKURU WADAU WOTE MLIONIUNGA  MKONO KUANZIA MWANZO HADI SASA HIVI TUNAFIKIA TAMATI.
NAOMBA TUWE PAMOJA KWA RIWAYA ZINGINE ZINAZOFUATA.


MAONI YENU TAFADHALI

No comments:

Post a Comment