Friday, November 25, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA KUMI NA MBILI





RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________





         SEHEMU YA KUMI NA MBILI!!

               "Afuuu Nor unaanza sasa wakati mwenzako nimechoka sana kazi yako siyo ndogo" Jamila aliongea kisha akambusu Norbert kwa mara ya mwisho akamuambia, "haya mpenzi wahi".

      Norbert hakuchelewa alitoka upesi chumbani humo akimuacha Jamila ndani na alirudi katika chumba ambacho alikuwepo Josephine amelala, alipoingia ndani hakumkuta Josphine zaidi ya kusikia
maji yakiwa yanamwagika bafuni na kitandani aliikuta simu kama alivyoiacha. Norbert aliichukua simu yake akawasha kioo ili aingize namba zake za siri atoe loki, alipoingiza namba za siri kwenye simu yake picha ya Josephine ikaja kwenye kioo kwa ghafla ikitoa tangazo na mfano kwenye mfumo wa simu juuvya kuchezewa simu yake.

               "intruder selfie" Norbert aliongea huku akiitazama picha ya Josephine ambayo ilipigwa moja kwa moja na siku bila Josephine kujua.


****


       Intruder selfie ni picha inayopigwa kwa kamera ya mbele ya simu baada ya mtu kukosea kuingiza neno la siri au kukosea mchoro wa simu(pattern) ambao ndiyo hufunga simu kwa usalama zaidi, mara nyingi mchoro huwa upo kwenye simu za kisasa zenye mfumo wa android katika program zinahusika kufunga program zingine(appslock) hasa kwa programu ya ulinzi wa simu dhidi ya virusi maarufu kama CM security.

        Ulinzi wa namna hii ndiyo ulikuwepo kwenye simu ya Norbert ambayo alikabidhiwa na shirika la EASA aitumie kwa ajili ya shughuli za kijasusi, simu hii ilikuwa ni tofauti na simu zingine ambazo mpaka uweke programu maalum yenyewe kufanya hivyo. Hii ilikuwa ina mfumo wa moja kwa moja wa ulinzi wa  simu na ilikuwa imeundwa kwa ajili ya wapelelezi wa daraja za juu sana katika mashirika mbalimbali ya wapelelezi duniani, simu hii ilikuwa imetengenezwa na kampuni ya Samsung ya Korea ya Kusini kwa agizo maalum kutoka mashirika ya kijasusi duniani.

      Hadi hapo Norbert alishabaini Josephine ndiye aliyeichezea simu yake kipindi hayupo, picha ya Josephine iliyokuwepo juu ya kioo ilikuwa ni ushahidi tosha usiopingika. Norbert alisikitika tu alipoona hiyo picha ikiambatana na maandishi yaliyoandikwa 'someone tried to snoop on your phone'. Yaliyomjulisha juu ya uchezewaji wa simu hiyo akiwa hayupo, alipuuzia suala hilo kuliweka ndani ya fikra zake kwa muda  huo.

      Aliamua kufungua sehemu ya ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu yake baada ya kukuta ujumbe mpya umeingia kutoka kwa Moses, aliusoma ujumbe huo kisha akatikisa kichwa kuuafiki halafu akatizama ulipo mlango wa bafuni humo chumbani. Akili yake bado ilikuwa ipo imara ingawa muda huo mwili wake ulikuwa na uchovu sana kutokana na shughuli nzito aliyotoka kuifanya muda mfupi uliopita, uchovu wa mwili wake ulimfanya ajilaze kitandani huku akisikia uchovu mkubwa uliopo kwenye mgongo wake.

     Akili yake ilianza kurudi na kuwaza tukio la siku iliyopita hasa pale hospitali ya taifa ya Muhimbili alipokuwa akifuatilia upelelezi wa mauaji ya Jenerali Kulika, mchoro wa muuaji wa wanajeshi wote waliokuwa wakilinda nyumbani kwa mkuu wa majeshi huyo nao ulimrudia kwenye kichwa chake kwa sura ile anayoitambua ambayo mwanzo hakuwa ameitambua kutokana na kutodhania kwa huyo mwanamke anaweza kufanya kitu ksma hicho.  Hakika umdhaniaye siye kumbe ndiye na umdhaniaye ndiye kumbe siye, Norbert alibaki akiwa na hatiati juu ya mhusika huyo  na alijionya kuwa awe makiini kwani ashang'amua kuwa muuaji huyo anajua kwamba yupo nyuma yake akifuatilia nyendo zake.
Fikra za muuaji huyo zilipozidi kushambulia katika halmashauri ya kichwa chake aliamua kusimama wima kisha akajongea hadi lilipo dirisha la chumba, aliamua kuweka macho yake hapo dirishani yatalii eneo la barabarani kwenye makutano ya mtaa wa Aggrey na Jamhuri.

     Aliusngalia utulivu wa eneo hilo hasa nyakati kama hizo kutokana na barabara yake kutotumiwa  sana, utulivu wa mtaa huo ulizidi kuifanya akili yake iwe kwenye utulivu zaidi katika kulifikiria suala lililopo mbele yake ambalo ilikuwa ni wajibu alipatie ufumbuzi hata kabla hajaambiwa kufanya na bosi wake anayempa kazi. Hakika alitakiwa aongeze umakini zaidi hata anavyoongeza umakini wa kulinda mboni za macho akipita kwenye eneo lenye kimbunga chenye mchangayiko wa takataka na vumbi, alikuwa akigawiana kitu kimoja cha siri na muuaji huyo anayemtafuta na ameweza kumtambua kuwa huyo ndiye muuaji ambaye ni miongoni mwawauaji hao.

            "hebu" Norbert katika fikra zake alikumbuka kitu na hapo akaitoa simu yake akafungua sehemu ya ulinzi wa simu ya ambayo hupiga picha ya ghafla pamoja na kurekodi ikiwa tu itanasa sauti, alifungua katika mafaili yenye kuhifadhi picha pamoja na sauti akakuta faili la sauti likiwa na ukubwa wa megabaiti moja(1 MB). Alilitazama faili hilo kwa umakini pamoja na tarehe lililoingia na muundo wake, file hilo lilikuwa limerikodiwa muda ambao alikuwa chumbani kwa Jamila. Norbert aliligusa faili hilo kwa kidole gumba alifungue kisha akalifunga papo baada ya sauti ya mlango wa bafuni kusikika ukifunguliwa, alifunga sehemu ya ulinzi wa simu yake kwa haraka sana kisha akafungua video ya nyimbo ya msanii wa kitanzania ambayo ilikuwa ni mpya aliyoipakua mtandaoni ili aiangalie kutokana na kuwa mpenzi wa muziki.

     Josephine alionekana akitoka bafuni huku akiwa amejifunga taulo fupi  sana la rangi nyeupe lilioshia kwenye mapaja yake huku akitumia taulo jingine dogo kujifuta nywele zake, alipousikia huo muziki unaolia kwenye simu ya Norbertr alitabasamu kisha akamtazama ambaye aliinua macho yake kumtazama mara moja.

             "Yaani Norbert huo wimbo naupenda sana utanirushia kwenye simu yangu" Josephine aliongea  huku akiwa bado ameweka kichwa chake upande aweze kujifuta vizuri maji kwenye nywele zake.

           "nikurushie video au audio?" Norbert alimuuliza.

             "Zote zote halafu video sijaiona  kabisa" Josephine aliongea huku akijifungua taulo na kubakiwa hana kitu akaanza kujifuta maji.

            "video ndiyo hii naitazama" Norbert alijibu huku akimtazama Josephine ambaye hakuwa na kitu mwilini akiwa anajifuta maji, aliutazama mwil huo kuanzia juu hadi chini kisha akatikisa kichwa  huku akitabasamu.

             "weee! Usiniambie nipe na mimi niione....nini sasa Norbert mbona hivyo?" Josephine aliposikia juu ya video ya nyimbo hiyo alijikuta akipatwa na hamu ya kutaka kuitazama video hiyo, aliponyanyua uso wake kumtazama Norbert kwa mara nyingine alimuona akisanifu umbo lake na hapo ndipo alipomuuliza huku akiingiwa na aibu.

             "Wewe ni mrembo sana ndiyo maana siishi kukutazama" Norbert aliongea huku akimtazama Josephine kwa taratibu pana.

             "Norbert bwana na wewe" Josphine alisema huku akiinamisha macho chini kwa aibu akimuacha Norbert aendelee kuusanifu mwili wake huo.

            "ok, ngoja na mimi nikaoge tukale" Norbert aliongea huku akitembea hadi kitandani akaitupia simu kitandani, alivua nguo alizovaa kisha akavaa taulo  akaelekea mahali ulipo mlango wa bafuni akimuacha Josephine akiwa anajiweka sawa baada ya kumaliza kujifuta maji mwilini mwake.



****

       
     Upande mwingine maeneo ya  Kunduchi nyumbani kwa mkuu wa majeshi ya majini Luteni Jenerali Ibrahim, kikao kizito kilikuwa kimeandaliwa baada ya ripoti nzito kufika kwenye mikono ya wakubwa wa majeshi ya ulinzi na usalama kwa kupitia daktari aliyechukua vipimo vya damu katika mwili wa Jenerali Kulika pamoja na wale wanajeshi kwa namna ya siri baada  ya uchunguzi wa awali kuonesha vipimo walivyotilia shaka na baadhi ya wakubwa wa majeshi akiwemo Msemaji mkuu wa majeshi hayo.

       Mkutano huo uliendeshwa ndani ya chumba cha siri  katika nyumba hiyo chenye meza ambayo kila mhusika wa mkutano huo alikuwa amekaa kwenye kiti kinachoizunguka meza hiyo. Mkuu wa majeshi ya majini L.J Ibrahim, mkuu wa majeshi ya anga na nchi kavu M.J Belinda, Mkuu wa jeshi la kujenga taifa(JKT) Filipo Marwa, Dokta Bakari kutoka Muhimbili pamoja na Benson ambaye alihudhuria kama mwanausalama ambaye amekuwa akifuatilia vifo vya watu waliokufa kwa sumu ya Quantanise aliyeletwa kwa msaada wa ngazi za juu wa Kanisa la Kiluteri ambao walimkodi kutoka shirika la kijasusi Marekani CIA. Ripoti hiyo ilipofika L.J Ibrahimu ilizidi kumtia hasira haswa kutokana na uzito wake, kifo cha mkuu wake kilizidi kumfanya jazba ipande.

             "Jamani hii ni aibu kabisa kwa mtu kama Moses Gawaza mkurugenzi wa usalama wa taifa pia mwanasayansi wa kuaminika ndani ya nchi hii, ametengeneza sumu akisema ni ya kuulia wadudu waharibifu wa mimea tena akaifungua kwa sherehe kubwa na taifa lilimpongeza  kwa kuwa mkombozi wa wakulima kumbe ni muuaji aliyetumia  kivuli cha taaluma yake kuangamiza wengine hii ni too much Dokta Bakari hebu wape maelezo wa kila ulichokibaini wewe baada ya kukuambia ufanye uchunguzi kwa mara ya pili kwa siri" L.J Ibrahim aliunguruma kwa hasira kwenye mkutano huo, Dokta Bakari aliposikia ruhusa hiyo ya kueleza kuhusu ripoti hiyo alisimama akiwa mkononi ana faili lenye makaratasi yaliyobanwa vizuri.

              "Nashukuru ndugu Luteni Jenerali kwa kunipa wasaa huu, kabla ya kuanza uchunguzi huo nilianza kupitia tafiti za uchunguzi zilizotangulia katika vifo vinavyofanana na kifo na General pamoja na wanajeshi wengine wazalendo waliokuwa wakifanya kazi ya kumlinda General. Uchunguzi wa matukio ya awali inaonesha kuwa kifo cha Bishop Edson na Mufti kilisabAbishwa na kupasuka kwa mishipa ya damu na ule wekundu uliokuwa unaonekana juu ya ngozi ni damu kuviria juu yake kiasi kwamba miili yao ilianza kuvimba  juu ya ngozi kama lengelenge kubwa katika sehemu za mbalimbali na laiti ikitobolewa kidogo basi damu ilikuwa inavuja eneo lilipotobolewa" Dokta Bakari alieleza kisha akamtazama kila mmoja aliyepo humo ndani halafu akaendelea, "sasa turejee katika uchunguzi huu nilioubaini ambao ulinitia maswali sana kabla hata sijaanza kuchunguza, ripoti za chunguzi zilizopita zilieleza juu ya kuvuja kwa damu lakini sikuwahi kuhusika kwenye chunguzi hizo. Swali langu la kwanza nililojikuta najiuliza ni kwanini General alikuwa na alama ya kutobolewa na kitu chenye ncha kali nyuma ya shingo lakini sikupata majibu hadi pale nilipopima damu yake kwa umakini nikiwa nimebaki peke yangu katika chumba cha uchunguzi majira ya usiku wa manane, kwa mujibu wa taarifa za tafiti yangu nimebaini kwamba aliyotobolewa nayo ilikuwa ni sindano ambayo ilitobolewa kwa kutumia nguvu nyingi sana hadi sehemu ya plastiki ya sindano hiyo  ikabaki ndani ya ngozi baada ya kugonga pingili za shingo sehemu hiyo ya plastiki ni hii..."

      Dokta Bakari aliingiza mkono kwenye koti la mfuko wa koti la suti alilokuwa amelivaa akatoa mfuko wa nailoni wenye kipande kidogo cha plastiki lenye rangi ya bluu, aliwapatia M.J Belinda aliyekuwa pembeni yake ambaye alikiangalia kisha akampatia M.J Marwa. Mfuko huo ulizunguka kwa watu wote  humo ndani na hatimaye ukarudi mikononi mwa Dokta Bakari ambaye aliuweka mezani, alifungua karatasi kadhaa za faili hilo kisha akaendelea kusoma, "Plastiki hiyo nilipoichunguza nilikuta ina chembechembe za kemikali za Quantanise ambazo ninatambua kuwa ni sumu ya kuua wadudu waharibifu wa mimea iliyoipa sifa nchi yetu kwa kutengenezwa kwake, sikutaka kuamini kama sumu hiyo ndiyo imemuua General pasipo kufanya utafiti ikiingia kwenye mwili wa kiumbe hai inaleta athari gani. Ili kujua athari za sumu hii niliamua kumchukua panya albino(panya weupe) nikagusa mabaki ya sumu hiyo kwenye sindano ndogo ya kupima malaria kisha nikamchoma panya huyo, nilimuweka panya huyo kwenye sanduku la peke yake kisha nimtazame atakuwa na hali gani baada ya kumchoma. Panya aliishiwa nguvu ndani ya sekunde kadhaa na hatimaye ngozi yake ikaanza na kuwa nyekundu hadi alipokufa, hivyo basi hapo nikatambua athari za sumu ya Quantanise ambazo zilitokea katika mwili wa General na hiyo ndiyo chanzo cha kifo chake baada  ya sumu hiyo kuleta athari kwenye moyo"  Dokta Bakari alipomaliza kuongea aliketi kwenye kiti chake.

      L.J Ibrahim alisimama kwa mara nyingine akasema, "nadhani mmemsikia Dokta alivyosema juu ya uchunguzi wa kifo cha mkuu wetu ambacho kinafanana kwa kila kitu na kifo cha walinzi wake, sasa nyinyi wengine miongoni mwa wanajeshi wenzangu wenye uchungu na mkuu wetu ningetaka kusikia maoni yenu, naanza na Major general Marwa".
M.J Marwa aliposikia kauli ya L.J Ibrahim alisimama  akapiga saluti moja kisha akasema, " kwa mujibu wa maelezo ya Dokta hapa hakuna ubishi juu ya suala hilo chanzo cha kifo cha General ni Professa Moses Gawaza kwani hizo kemikali nakumbuka wakati anazizindua alisema ni hatari sana kwa binadamu na itatumika kwa uangalifu maalum hapa nchini  tena itatolewa kwa vibali maalum, sikuwahi kusikia kama kuna mkulima wa hapa nchini aliwahi kuchukua kibali akainunua zaidi ya kusikia sumu hiyo ilisafirishwa kwa meli kuelekea huko Ulaya zilipotoka oda za kuinunua. Hivyo basi kwa matumizi ya ndani ya nchi hii ni Moses anahusika kwani haipo kwenye mikono ya mwingine yoyote na pia muuaji ni mtu mwenye mbinu za kijasusi, Moses ndiye mhusika kwani yeye ana mbinu za kijasusi tukumbuke na ni kiongozi wa usalama wa taifa. Lazima atiwe nguvuni mara moja".
M.J Marwa alipoongea hivyo jazba tayari ilikuwa imempanda na hadi anakaa chini alikuwa alihema sana, L.J Ibrahim alimruhusu M.J Belinda naye aongee katika mkutano huo.

       M.J Belinda alipopata ruhusa ya kuongea alinyanyuka akatoa saluti kisha akasema, "Najua nitakuwa nipo tofauti sana na nyinyi nyote ila napenda niseme hivi, kabla ya kuanza kumtuhumu Moses ningependa tuwatuhumu na Special forces wa jeshi la polisi ambao walinivamia nyumbani kwangu wakataka kunichoma sindano yenye kimiminika chekundu ila niliwahi kuwatia nguvuni na wapo kwenye basement ya kambini. Hao  tumewabana na wamekiri kutumwa kuwaua wale wote walioshiriki operesheni fagio la chuma ambayo iliongozwa na General, mtu waliyemtaja anawatuma kwa ajili ya kazi hiyo ni Kamishna ambaye hawajamtaja jina lake. Sasa mnaposema muuaji Moses wakati yeye mwenyewe alishiriki Operesheni fagio la chuma na aliwatoroka hao Special force  bado haina ushahidi kwanza tuwahoji hawa niliowakamata na hiyo sindano ikapimwe na kama ni hiyo sumu wataje wameipata vipi. Mkuu hapo tutaweza kumpata Mhusika kirahisi kutengeneza sumu na kuwa jasusi haitoshi kumtuhumu kuwa ni muuaji". Alipomaliza kuongea alikaa chini akiwaacha wakubwa wenzake  wakitafakari maneno yake, Benson alikuwa kakaa kimya muda wote huo akiwasikiliza na hakuwa amenyanyua mdomo wake kuongea.

       Baada ya kimya cha muda wa dakika kadhaa kuvamia humo ndani hatimaye Dokta Bakari alinyoosha mkono, wote kwa pamoja walimtazama na hatimaye L.J Ibrahim ambaye ndiye mkubwa kuliko wakubwa wote waliopo na ndiye mwenye kauli kuu akamruhusu kuongea.

                  "Kwa maelezo ya meja jenerali Belinda ni wazi kuwa hiyo sindano aliyotaka kuchomwa ni ya Quantanise kwani hiyo sumu  ina rangi nyekundu nafikiri angeileta hiyo sindano tuifanyie ufafiti za kuhakiki" Dokta Bakari aliongea kisha akakaa chini, M.J Belinda aliposikia maneno ya Dokta Bakari alizamisha mkono wake katika mfuko wa kombati la kijeshi alilolivaa akatoa simu ya kisasa ambayo  alibonyeza kwenye kioo mara kadhaa akampatia Dokta Bakari huku akimuonesha kwenye kioo. Dokta Bakari aliangalia kioo hicho cha simu akapatwa na mshtuko sana na akaishika simu ya M.J Belinda akaweka vidole viwili kwenye kioo cha simu hiyo ya kugusa akavitanua ili kukuza(zoom) kile alichokiona hapo  kwenye kioo.

                    "Hii ni quantanise ikiwa kwenye injection container(bomba la sindano) means hao watu ni wanahusika" Dokta Bakari aliongea kisha akampatia simu L.J Ibrahim ambsye aliitazama akampatia M.J Marwa halafu ikapelekwa Benson kabla haijarudi  kwa mwenyewe M.J Belinda. Maneno hayo alipoyasikia L.J Ibrahim aliweka mikono kwenye uso wake kisha akajifikiria kwa sekunde kadhaa halafu akainuka kwenye kiti, aliwatazama wote waliomo mule kisha akasafisha koo lake huku akishusha pumzi ili ajiandae kusema jambo ambalo liljia kichwani kwa muda huo.

                    "Ok ok ni hivi Belinda utaongozana na Benson mkawahoji wale watuhumiwa halafu kikosi kingine cha makomandoo kitaemda kumtia nguvuni Moses kabla habari hizi hazijafika kwenye vyombo vya habari. Is that clear? Mimi ndiyo nitajua hatua gani atakayochukuliwa Moses kwani bado muuaji kwangu"L.J Ibrahim aliongea  akazidi kumshangaza M.J Belinda kwa uamuzi aliouchukua.

                    "Lakini mkuu hapo hatuna uhakika wa wa ushahidi kumtia Moses nguvuni Moses apewe adhabu kutengeneza chemical hiyo siyo saba..."
 
                    "Shut up Belinda nani mkuu kati ya mimi na wewe?! Si wewe mdogo kicheo sasa sikiliza amri zangu ninavyosema mimi ndiye mkuu kwa sasa, is that clear?!"M.J Belinda aliongea kwa kutoridhishwa na uamuzi wa mkuu wake lakini  alifokewa kwa nguvu sana L.J Ibrahim ambaye ni mkubwa kwake kicheo, alilazimika kukubali amri ya mkuu kwa kukamsa  huku akisema,"Mkuu!"

                      "Good! Sasa kazi ianze mara moja kuanzia muda  huu, kikosi cha kumkamata Moses kitateuliwa na wewe Belinda kutoka jeshi la nchi kavu. sitaki nisikie unadanganyika na hao watu uliowakamata kumbuka alama hiyo ya mabawa ya ndege yenye rangi ya silver iliyowekwa hapo kwenye mfuko wa kombati yako ya juu inamaanisha wewe ni komandoo tena kiongozi wa kikosi  cha makomandoo kuanzia hivi sasa baada ya General. Sasa ujinga huo sitaki kuusikia, Marwa hakikisha unatoa vijana wako watakaa mipakani wakishirikiana na wa jeshi l ardhini katika kuhakikisha huyu mtu hatoroki. Kikao kimevunjwa kwa sasa mpaka atakapopatikana Gawaza ndiyo tutakaa tena kikao kujadili" L.J Ibrahim aliondoka humo kwenye chumba cha mkutano huku kila mmoja akinyanyuka akiwa na fikra zake kichwani.


****


     Majira ya saa nne usiku Norbert alikuwa tayari ameshapata chakula cha jioni pamoja na  Josephine, muda huo walikuwa wamejilaza kitandani wakichezeana michezo ya hapa na pale mithili ya wapenzi wa siku nyingi.

      Walikuwa wamevaa nguo za kulalia wakifanya michezo hiyo mithili ya watoto na hatimaye wakaamsha wazungu waliolala kwa kila mmoja, joto la miili yao lilipanda kwa ghafla baada ya wazungu hao wasio hata na asili ya Ulaya kuamka. Hitaji la kuwalaza wazungu ndiyo lilifuata kwani hawakuwa na namna baada ya wazungu wa Josephine kuchachamaa zaidi wakihitaji kulazwa, ilikuwa ni wajibu wa Norbert kwa namna moja tu na hakuwa na namna nyingine itakayowafanya wazungu hao walale.

      Kuwalaza wazungu hao ilikuwa ni kama unamlaza mtoto, yaani uwalaze kwa namna ambayo wanataka kulala ndiyo watalala.

      Wazungu hao ambao tayari walikuwa wameshamtia  wazimu Josephine na alimkalia kwa juu Norbert aliyekuwa amelala cha huku akifungua uwazi wa mavazi maalum ya kulalia na kifua kika wazi. Alianza kuchezea lifua cha Norbert na akapeleka kinywa chake karibu na kinywa cha Norbert ambapo alipokewa na Norbert kisha akaanza kufanya utundu katika mwili wa Norbert, haikupita muda mrefu Norbert alimgeuza akamuweka yeye chini akaendelea na utundu wake kwenye mwili wa binti huyo ambao ulimfanya awe kama aliyepandwa na maruhani jinsi alivyokuwa akigaragara kwenye kitanda hiko akienda kushoto  na kulia huku akipiga makelele. Aliendelea na utundu wake kwa muda mrefu kisha akaanza tena mchezo mwingine usiohitaji musmuzi na wenye uwanja uliotengenezwa kwa bidhaa za zao la misitu, miguno ya Josephine ndiyo ilitawala ndani ya chumba hicho kwa muda wa masaa mawili. Saa sita usiku wa maneno ndiyo kelele hizo zilikoma baada ya wazungu wake kulala sasa akawa anatawaliwa na uchovu wa hali ya juu, alilala usingizi hapo kitandani akimucha Norbert akiwa anafikiria mambo mengine hadi alipopitiwa na usingizi.

    Majira ya saa kumi na moja alikuja kushtuka baada ya kusikia mlio wa simu yake ikilia kwa fujo, alijinyoosha kisha akatazama pembeni hakumuona Josephine badala yake alisikia sauti ya kunong'ona ikitokea ulipo wa mlango wa kuelekea bafuni  kisha sauti ya maji yakimwagika ikasikika baada ya yeye kuzima kengele ya simu aliyokuwa ameitega kila siku ikimkumbusha(reminder) juu ya jambo ambalo aliazimia kulifanya siku hiyo.

    Norbert aliamka kitandani kwa haraka kisha akakaa akafungua simu yake akaangalia sehemu ya kurekodi ilivyokuwa na akakutana kuna faili jingine la ziada likiwa limeongozeka kwenye simu yake, tabasamu la ghsfla lisiloashiria furaha lilimjia katika uso wake. Muda huo Josephine alitoka bafuni akiwa ameshika simu yake akamkuta Norbert akiwa amekaa kitandani, aliungana naye kitandani huku akionesha kutokuwa na wasiwasi wowote.

        "Network haipatikani mpaka bafuni siyo" Norbert aliongea huku akitabasamu.

             "Hamna nilienda kwenye sink kunawa ndiyo simu ikaita nikarudi kuichukua nikaenda nayo nikawa nanawa huku naongea nayo" Josephine aliongea huku akijisogeza karibu zaidi halafu akamkumbatia Norbert.

            "mapema yote hii nayo" Norbert alimuambia Josephine.

              "Norbert nawe nini sasa" Josphine aliuliza huku akitumbukiza mkono yake katika eneo lisilostahili kutimbukizwa mikono

     Norbert hakutaka ubishi aliamua kutimiza kile kilichokuwa kikimfanya Josephine aingize mikono katika eneo la milki yake asubuhi hiyo.



***


    MBEZI BEACH
 DAR ES SALAAM

    Muda ambao Norbert akiwa anajivinjari na ndiyo muda ambao gari la jeshi la wananchi wa Tanzania(JWTZ) liliingia  katika lango la nyumba hiyya kifahari baada ya mlinzi wa nyumba hiyo kulazimishwa afanye hivyo, ilikuwa ni range rover  ambayo makelele yake yalitosha kuwaamsha waliomo humo ndani. Breki za gari hiyo zilipofungwa kwa ghafla na kuleta makelele tayari wafanyakazi wa nyumba hiyo walikuwa wameshaamka, wanajeshi waliovaa sare za kijeshi walishuka ndani ya gari wakiongozwa na Afisa mteule daraja la pili ambaye alitoa amri kwa baadhi kuizunguka nyumba hiyi. Wengine wakiongozwa na Afisa mteule huyo waligonga mlango wakuingia ndani kwa nguvu hadi mfanyakazi wa ndani  alipofungua ndiyo wakaacha.

                       "Yuko wapi Dokta Hilary" Afisa mteule huyo alimuuliza mfanyakazi huyo ambaye alianza kutetemeka kwa uoga.

                      "ni mimi niwasaidie nini?" Sauti kutoka ndani ya nyumba  hiyo ilisikika na hapo wanajeshi wote wakaingia wakimsukuma msichana huyo wa kazi, waliingia ndani wakamkuta Dokta Hilary akiwa kasimama na mkewe Irene akiwa na mavazi ya  kulalia.

                      "Moses yupo wapi"Afisa mteule huyo daraja la pili ambaye alijulikana kutokana na kuvaa cheo mkononi kilicho na umbo kama la saa yenye alama ya mwenge alimuuliza Dokta Hilary huku wenzake wakimnyooshea bunduki kwa tahadhari.

                   "Sijui alipo" Dokta Hilary alijibu kwa kujiamini.

                     "Ok, mkamateni yeye mpaka atakapojileta Moses" Afisa mteule  huyo aliongea kuwapa amri wenzake, askari hao walisogea mbele ili wamtie nguvuni Dokta Hilary lakini walisita baada ya kusikika amri nyingine.

                   "SUBIRI!" Afisa mteule ambaye ndiye kiongozi wap alipaza sauti.


TUKUTANE TENA JUMAMOSI PANAPO UHAI




HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI














No comments:

Post a Comment