Monday, November 30, 2015

KOSA SEHEMU YA KUMI NA TATU


TEMBELEA:http://www.facebook.com/riwayamaridhawa




  KOSA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA

SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



 ILIPOISHIA

Nilienda sehemu yenye silaha nikachagua bastola za aina mbili pamoja na maboksi kadhaa ya risasi, kwa bunduki kubwa nilichukua bunduki aina ya UZI ya nchini Israel ambayo imeundwa na mwanajeshi wa kiyahudi anayeitwa Uziel Gal mwaka 1948. Bunduki hii ni moja  kati ya bunduki hatari duniani yenye uwezo kupiga risasi mfululizo kama ilivyo AK47, MP5 na nyinginezo, nilibeba risasi za kutosha na viwambo vya kuzuia sauti nikaenda kuviweka pale nilipoelekezwa.
"vipi visu hubebi?" Nurulayt aliniulixa huku anipatia visu sita vikubwa, nilivipokea visu hivyo bila ya kusema chochote nikaviweka kwenye gari kisha nikamtazama kama anaweza kuniambia la ziada.
"panda tuondoke" Nurulayt aliniambia nami nikazunguka mbele kwenye mlango wa pembeni ya dereva nikapanda.



ENDELEA NA MKASA HUU WENYE KUELIMISHA NA KUSISIMUA


SEHEMU YA KUMI NA TATU!!

Usukani wa gari hili ulikamatwa na Nurulayt na safari ya kuelekea pori la Chirinda ikaanza mara moja baada ya geti lililokuwa lipo humo ndani kufunguliwa na kifaa maalum, baada ya gari kutoka geti lile lilijifunga tena kama ilivyokuwa awali na tukawa tupo nie ya nyumba hiyo kwa upande mwingine kabisa. Ilikuwa ni majira ya saa tano kasoro za usiku barabara ilikuwa tulivu sana kuliko kawaida, tulikuwa tukipishana na magari machache tu njiani yaliyokuwa yanaitumia barabara kwa muda huo. Tulirudi hadi katikati ya jiji la Widhoek kuifuata barabara ambayp sikuijua inaitwaje hadi muda huo, Nurulayt aliifuata barabara hiyo kuelekea mashariki ya jiji la Widhoek kwa mwendo wa kasi sana. Alikuwa akiweka gia na kutoa gia nyingine huku akicheza na usukani kwa umakini sana na kusababisha gari hii iende mwendo mkali hadi ikawa inatoa mlio kama wa kulalamika kwa kuendeshwa  mwendo huo, gia tano za gari hii zilitumiwa ipasavyo na Nurulayt kama anaendesha gari ya mashindano hali iliyonisababisha nifunge mkanda mwenyewe kwani mwanzo sikuwa nimefunga mkanda. Baada ya muda mfupi tulikuwa tumeingia kwenye eneo la jangwa lisilo na majani wala nyumba za watu, tulipongia katila jagwa hilo ambalo nalijua kwa jina la Kalahari ndiyo mwendo wa gari  ulizidi . Nurulayt hakuonekana kujali sana kwa mwendo aliokuwa anautumia yeye ndiyo alizidi kukanyaga mafuta hadi mshale wa mngurumo  wa gari ukafika sehemu yenye alama nyekundu huku kengele ya hatari ikigonga kwa fujo.
"we mwanamke sikuwezi hata kidogo" Nilimuambia huku nikisikitika kwa mwendo aliokuwa anautumia Nurulayt
"kwanini unasema hivyo?" Nurulayt aliniuliza huku macho yake yakiwa makini kuangalia mbele.
"huu mwendo sijui upo mashindano ya formula 1" Nilimwambia kuhusu mwendo anaoutumia tena niliufananisha mashindano maarufu ya magari ya formula 1 yenye magari yanayooenda kwa kasi sana, maneno yangu yalimfanya Nurulayt atabasamu kisha akasema "we unataka tutembee mwendo wa harusini unafikiri tutafika leo Abdul yaani hapa hatujafika Botswana halafu tunaelekea Zimbabwe".
"Mh! Haya suka twende kazi" Nilimwambia kukatisha mazungumzo yetu kisha nikakaa kimya na sikuongea hadi Nurulayt alipopunguza mwendo akaingia kwenye sheli iliyopo pembezoni mwa barabara.
"vipi mafuta yamepungua?" Nilimuuliza.
"hayajapungua ila yanahitajika yaongezwe" Nurulayt alijibu huku akishuka kwenye gari baada ya gari kuliegesha gari jirani na mashine ya kujazia mafuta, Nurulayt alilipa pesa na gari ikajazwa mafuta hadi tenki lote likajaa kisha akarudi kwenye gari lakini hakukaa kwenye kiti cha dereva bali alikaa kwenye viti vya nyuma na kiti cha dereva kikabaki kitupu kama kilivyo.
"Nuru mbona unakaa huko mbona sikuelewi ?" Nilimuuliza huku nikigeuka nyuma nikamtazama.
"Abdul huelewi nini au mimi kuachia usukani kuja kukaa huku?" Nurulayt aliniuliza.
"ndiyo maana yake hicho ndicho nisichokielewa" Nilimwambia.
"Abdul hapa tupo karibu na West gate na West gate camp katika jangwa hili la Kalahari, mbele kidogo kiasi cha mita 500 kuna mpaka wa Trans Kalahari ambao unatenganisha nchi hii na Botswana na una ulinzi mkali. Sasa basi hatuwezi kuuvuka mpaka huo bila ya kuwa na mtu ambaye ni askari wa pale, nimetoka kwenye kiti cha dereva ili kumpisha askari niliyemkodi kwa ajili ya kutuvusha atuvushe" Nurulayt aliongea kunielewesha juu ya mpango wake ambao nilikuwa siujui kabisa.
"hapo sawa nimekuelewa" Nilimwambia kukubali kuuelewa mpango wake mzima alioupanga, maelezo yake yaliniridhisha na nikatazama mbele.
" sasa sikiliza" Nurulayt aliniambia huku akinivuta bega, niligeuka kumtazama ili  kumsikiliza nini anachotaka kuniambia.
"katika kazi kama hizi usipende kuwa muongeaji na muulizaji wa maswali sana, unatakiwa uwe kimya Abdul ingekuwa mwingine tayari ameshakupiga risasi" Nurulayt aliniambia huku akinitazama kwa umakini usoni, nilimsikiliza maneno yake kisha nikashusha  pumzi halafu nikasema "poa" nikageuka mbele. Baada ya muda takribani dakika kumi kupita mlango wa dereva ulifunguliwa na mtu mwenye mavazi ya kiaskari aliingia ndani ya gari  kisha akatutazama akasema, "samahani kwa kuchelewa".
Askari huyu aliwasha akaliingiza barabarani na safari ikaendelea wote tukiwa kimya bila ya kuongea chochote, baada ya dakika tano tulikuwa tumefika sehemu hiyo ya mpaka ambayo ilkuwa na ukaguzi wa magari yanayotoka na kuingia nchini Namibia. Mpaka huo ulikuwa na njia mbili ambayo moja yanapita magari yanayokwenda nje ya nchi na nyingine yanapita magari yanayoingia ndani ya nchi, tulipokaribia  eneo hilo yule askari aliwela gari kando akatuomba tumsubiri anarejea sasa hivi. Alishuka ndani ya gari akaenda kwenye ofisi zilizopo hapo mpakani, tulibaki tukiwa tunamsubiri na alirejea baada ya dakika takribani tatu kisha akaingia ndani ya gari safari ikaendelea tukawa tunaelekea kwenye mpaka kuvuka. Alipofika eneo la ukaguzi alitoa kadi na makaratasi akawaonesha askari ambao walimruhusu kupita bila hata kumuuliza  lolote, tuliendelea na safari tukivuka bango kubwa linalo  tukaribisha  nchini Botswana. Yule askari aliendesha gari kwa mwendo wa mita takribani 400 kisha akashuka akatuaga akikutakia safari njema, baada ya askari kuondoka Nurulayt alirudi  kwenye usukani kama kawaida na safari ikaendelea kwa mwendo ule ule wa kilevi. Baada ya saa moja tangu tuvuke pale mpakani tulitokea kwenye mji mdogo uliokuwa umechangamka sana, ilikuwa yapata saa saba za usiku na ilitubidi tuegeshe gari kando ya barabara ili tupumzike humo humo ndani ya gari kwa ajili ya usalama wa
vitu vyetu, tulilala usingizi wa mang'amng'am hadi kunakucha tukaendelea na safari yetu. Usukani wa gari kama kawaida ulikamatwa na Nurulayt na mwendo wa gari aliupunguza kwa sababu tulikuwa tumeingia katika makazi ya watu. Tulitembea kwa umbali wa kilomita kadhaa tukawa tumefika sehemu yemmnye barabara mbili ambayo moja inaelekea kushoto na nyingine inaelekea kulia, Nurulayt alipokaribia njia hizo aliweka gari pembeni na jirani na mgahawa aliweka breki ya mkononi huku akiliacha gari likiwa linawaka.
"twende tukanywe chai saa tatu hii" Aliniambia huku akiteremka garini nami nikamfuata bilab kuongea jambo lolote, tuliingia ndani ya mgahawa. Tulipata kifungua kinywa kwa pamoja na tulipomaliza  tulirudi garini na safari ikaendelea huku macho yangu yakiwa dirishani kuangalia mandhari ya nchi hii kwa upande wa sehemu wanazoishi watu wenye hali ya chini. Baina ya zile njia zilizokuwa zimegawanyika sisi tulifuata njia ya upande wa kushoto, tulienda kwa mwendo wa masaa kadhaa tukawa tumefika sehemu yenye mji mdogo uliochangamka sana.
"hapa panaitwa Maun ni sehemu iliyo karibu na hifadhi ya wanyama kwa upande wa kushoto na delta ya mto Okavango kwa upande huo huo" Nurulayt alinielezea  juu ya sehemu iliyokuwa ipo mbele yetu.
"ok" nilimuitikia kwa ufupi tu kisha nikakaa kimya nikimuacha Nurulayt acheze na usukani wa gari, Nurulayt naye hakuwa muongeaji sana  baada ya kunielezea hivyo alikaa kimya akaelekeza umakini  wake barabarani. Haikupita hata nusu saa tangu alivyonieleza hivyo usingizi mzito ulinichukua kutokana na uchovu nilionao uliotokana na kutolala usinfizi wa kutosha, nilikuja kuamka baada ya kusikia napigwa kibao huku jina langu likiitwa.
"Amka wewe tukale jioni hii"Nurulayt aliniambia nilipofumbua macho kumtazama, hapo nilibaini giza llishaanza  kuingia na tulikuwa tunaonana kupitia taa ndogo iliyopo ndani ya gari.
Nilipiga muayo mrefu kisha nikamtazama Nurulayt ambaye alionekana kuchoka sana.
"shuka bwana twende au wewe huhisi njaa?" Nurulayt aliniuliza baada ya kuona namtazama bila ya kushuka kwenye gari.
"hapa ni wapi?" Nilimuuliza bila hata  kujali maneno aliyoniambia.
"bwana hebu shuka huko  mwanaume una maswali kama mwanao, nahisi  kachukua tabia yako" Nurulayt aliongea huku akinisukuma nishuke. Muda huo  yeye alikuwa tayari ameshafungua mlango wa upande wake alikuwa anasubiri mimi tu nishuke, nilifungua mlango nikashuka chini kisha nikaenda hadi upande aliopo Nurulayt ili aniongoze kuelekea hiyo sehemu ya kwenda kula kwakuwa nilikuwa mgeni ndani ya eneo hilo.
"yaani wewe na mwanao mkikaa na mimi nahisi mtaniua maana mna maswali mengi kama polisi" Nurulayt aliendelea kuongea huku akinishika mkono kuelekea ndani ya nyumba moja yenye milango mikubwa ambayo ilikuwa ipo mbele yetu.
"huyo mtoto kachukua tabia zako mimi unanipakazia tu" Nilijitetea kimasihara na kusababisha Nurulayt anisukume begani kimasihara.
"Loh! Lione yaani mwanao nimekaa naye kwa miaka mitano tu lakini alipoanza kuongea kazi nilikuwa nayo ya kujibu maswali tu, na sasa nakutana na baba mtu habari ni hiyohiyo tu yaani kama mnanihoji vile" Nurulayr aliongea akiingia ndani nami nikamfuata, tulikuwa tumeingia kwenye mgahawa mdogo wenye watu wachache jioni hiyo. Nurulayt aliagiza chakula kama ilivyo kawaida yake halafu akaja kuketi meza moja nami, chakula kililetwa na kila mtu akawa anashughulika katika kulijaza tumbo lake. Hatukuongea hadi tulipotoka tularudi ndani ya gari, Nurulayt alienda kukaa kwenye kiti cha changu na mimi nikakaa kwenye usukani.
"tunaelekea wapi sasa, nahitaji nijue sio unaniachia usukani tu bila kusema cjochote" Nilimwambia Nurulayt.
"hapa tupo Nata kwenye njia tatu zinapokutana, fuata barabara inayoenda kusini mashariki hadi katika mji unaoitwa Francistown" Nurulayt aliniambia huku akikinyoosha kiti cha gari miayo ikimtoka mdomoni mwake, niliwasha  gari nikaingiza barabarani na safari ikaendelea kuutafuta mji wa Francis town nikiwa nimewasha taa za gari kwani nuru ya anga ilishaanza kupotea. Baada ya dakika thelathini tangu niingize gari barabarani Nurulayt alikuwa tayari yupo kwenye usingizi mzito sana na kama isingekuwa mkanda wa gari angekuwa kajigeuza ovyo hadi kufikia kuiparamia gia ya gari, siku hii niliendesha gari kwa mwendo wa kasi nikiomba tufike salama kwani sikuwa mwenyeji wa barabara ninayoitumia na alama za barabarani ndiyo kitu pekee kilichonisaidia kuniongoza katika barabara hiyo. Hadi inatimu saa nne ya usiku tayari nilikuwa nimeshafika katika mji wa Francistown uliopo kilomita 185 kutoka Nata nilipotoka, nilipofika hapo ndipo nikamshtua Nurulayt usingizini na nilimtaarifu tumefika tayari.
"ingia hiyo barabara inayoelekea kushoto na uende hadi utapokuta sheli yenye  supermarket" Nurulayt aliniambia maneno hayo alipomaliza alirudi tena kulala.
Niliingiza gari barabarani kwa mara nyingine nikawa naelekea barabara inayoenda kushoto kati ya barabara tatu zilizopo mbele yangu, barabara hizi kwa Tanzania ningezifananisha na makutano ya barabara ya Segera yanayokutanisha barabara tatu zinazoelekea Tanga mjini, Kilimanjaro na Mkoa wa pwani. Eneo la Nata  na hili la Francistown lilifanana kila kitu muundo wa makutano ya barabara zilivyo, niliamua kuwa makini na alama za barabarani kwani hizo ndizo zilikuwa msaada kwangu katika kuniongoza na barabara ya huku ili niweze kufika salama bila hata kupata ajali yoyote. Nilitumia kiasi cha dakika 45 nikawa nimefika katika sheli aliyonielekeza Nurulayt, hapo nilimuamsha tena na nikamtaatifu kuwa nimeshafika. Nurulayt aliamka kisha akatazama mazingira ya hapo kwenye sheli halafu akashuka akaniambia," sogeza gari sehemu ya kuwekea mafuta". Nilisogeza kama alivyoniambia kisha akaongea na na mhudumu wa hapo sheli, alipomaliza alichukua mpira wa kujazia mafuta akatia mafuta hadi mshale wa mafuta katika kioo cha plastiki kilichopo chini ya usukani kikaonesha tenki la gari limejaa. Alifanya malipo kisha akarejea ndani ya gari alipokuwa awali, alipokaa kwenye kiti nilimuangalia usoni nilitarajia aseme lipi juu ya hii safari.
"Mbona unaniangalia hivyo?" Nurulayt aliniuliza.
"nahitaji kujua nini kinachofuata Nuru" Nilimwambia huku nikiwa sijatoa jicho langu usoni mwake.
"ok ok ni hivi, nusu kilomita kutoka hapa kuna mpaka wa Ramekgwebana unaotenganisha Botswana na Zimbabwe. Hivyo inabidi uruke kiti cha nyuma kuna askari wa uhamiaji atakuja kutuvusha hapa kama tulivyovuka kule Trans kalahari border" Nurulayt alinipa maelezo ya mpango unaofuatia. Baada ya dakika kadhaa tangu anipe maelezo hayo  nilimuona askari wa  mmoja aliyebeba mkoba mkubwa mgongoni akija hadi kwenye gari letu usawa wa mlango wa dereva, alipofika niliamua kuruka  kiti nyuma kwani nilijua fika ndiye mtu tunayemsubiri. Yule askari alifungua mlango wa gari akaingia huku akiwa anahema  sana akiwa na mkoba wake  ambao aliupakata mapajani alipokaa kwenye kiti cha gari.
"mambo si mazuri huko" Askari aliongea huku akitutazama kila mmoja.
"vipi huko kuna nini?" Nurulayt aliuliza
"muda mfupi uliopita hapo mpakani walipita watu  wakiwa na  gari yenye mizigo mingi ambayo haikujulikana ni vitu gani, walipekuliwa wakakutwa na na unga na walipotaka kukamatwa wakaanzisha vita ndogo. Wamefanikiwa kukimbia  na gari lao la mizigo kuingia mpaka Zimbabwe kinguvu lakini waliishia msituni wa jirani na mpaka, na hivi ninavyokuambia wanafanya majibizano ya risasi na askari na mpaka mzima umemwagwa askari"  Yule askari alieleza sababu ya mambo kutokuwa mazuri huko mpakani.
"sasa itakuwaje?" Nurulayt aliuliza akionekana kuchanganyikiwa sana na maelezo hayo.
"njia pekee ya kuvuka pale mpakani ni kuvaa sare za kama hizi zangu na viatu" Aliongea yule askari huku akifungua mkoba mkubwa alioingia nao akatupatia sare za askari wa uhamiaji pamoja na viatu vya  kijeshi.
"mkivaa nguo za askari wa uhamiaji mtajulikana ni askari waliongezwa na makao makuu kwenda kupambana na hawa wasafirishaji madawa ya kulevya na mtaruhusiwa kupita. Badilisheni hapahapa" Yule askari alituambia.
"ok hamna shida ila wewe inabidi ushuke tubadilishe nguo kwani mimi ni mwanamke na huyu ni mzazi mwenzangu, hupaswi kuniona nikibadili nguo labda yeye kwakuwa hakuna asichokijua katika mwili wangu" Nurulayt alimuambia yule askari
"mh! OK hamna shida" Yule askari alinitazama kwa jicho la pembeni halafu akatabasamu akaonesha kukubaliana na maneno ya Nurulayt, alishuka  ndani ya gari kwa  haraka  na sisi tukabadilisha kwa haraka halafu tukamuita tulipomaliza kuvaa.
"Hapo safi kabisa yaani mpo kama askari wa uhamiaji, chukueni na hizi  bunduki mzishikilie ili wakituona wajue mnaingia kazini" Yule aliongea baada ya kutuona tukiwa tumevaa magwanda ya askari wa uhamiaji, alifungua ule mkoba tena akatoa bunduki mbili aina ya short gun akatupatia pamoja na mikanda ya risasi. Safari ya kuelekea kwenye mpaka wa Ramekgwebana iluanza na askari yule ndiye aliyekuwa dereva, gari letu lilipoingia barabarani alitoa king'ora cha kubandika akampatia Nurulayt ambaye alikiweka juu ya paa la gari. Mpakani tulifanikiwa kupita bila matatizo na kweli kulikuwa kuna maaskari wengi wakiwa na wana silaha kama hizi tulizokabidhiwa, safari yetu iliendelea na tukawa tumeingia kwenye pori lililopo mwanzaoni mwa nchi ya Zimbabwe. Furaha ilidhihirika machoni mwetu kwa kufanikiwa kukivuka kikwazo kile lakini furaha hii haikudumu kwani dosari kubwa iliingilia furaha hii, tukiwa tupo katikati ya pori usiku majira ya saa sita milio ya risasi ilianza kusikika na vioo vya  gari letu vikaanza  kupasuka.Yule askari ambaye ndiye aliyekuwa dereva wetu alitoa ukelele wa maumivu akiachia usukani wa  gari
 na gari likaingia pembeni ya barabara nusura ligonge mti baada ya  yeye kuwahi kukanyaga breki ya gari.


*Mmmh kunani tena?

*je watafanikiwa kupita salama?


ITAENDELEA!!

No comments:

Post a Comment