Monday, December 21, 2015

SHUJAA SEHEMU YA KUMI NA SABA









RIWAYA: SHUJAA


MTUNZI: Hassan O Mambosasa

SIMU:+255713776843
+255762219759



WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



SEHEMU YA KUMI  NA SABA!!




 Majuto siku zote huja baada ya kutenda jambo ambalo hukulijua matokeo yake na wala hukuweza kufikiri kama litakuja kutokea kwa namna ambayo hukuitarajia, haya ndiyo yalimjia Andrew baada ya kutuma mtu akampige Moses ili amtishe aachane na Beatrice na matokeo yake ni huyo  mtu kujeruhiwa naye na jambo hilo kugundulika na dada yake. Hakuwaa anatambua kama alikuwa analazimisha maji yapande badala ya kuyawekea mteremko ili yashuke, kupuuza mbinu ya dada yake na kuitumia mbinu yake mwenyewe katika  kumpata Beatrice ndiyo ilichangia. Yote haya ni kwa sababu alikuwa akimchukia Moses na hakutaka kuona kuna ukaribu baina yake ndiyo maana hakutaka awe shemeji yake, sasa dada yake amenuna na hataki hata kuongea naye na moyoni amejawa na majuto tu.
Hatua inayofuata baada ya kumkosea dada yake aliona ni kumkosa Beatrice, msichana aliyeamini ni wa maisha yake. Hakujua dada yake atachukua hatua gani baada ya ile mbinu yao ya awali waliyoipanga, akili yake ilimuambia Moses ndiye anayehitajika na dada yake lakini si kwa mbinu ile aliyoiasi hapo awali ambayo ilikuwa inamtendea haki dada yake na inamtendea haki na yeye pia. Mpango mzima umeenda mrama na sasa dada yake hajali juu ya suala lake la kumpata Beatrice na anajali juu ya kumpata Moses tu kwa njia yoyote, Andrew alitambua fika dada yake ambaye akili zake ni kama mwendawazimu akiudhiwa anaweza akamfanya Beatrice chochote kibaya katika vita ya kusaka penzi la Moses baada ya yeye kumfanyia Moses kitu kibaya katika harakati za kusaka penzi la Beatrice. Lawama ndiyo zilianza kuutafuna ubongo wake kwa muda huo na sasa  hata kitanda alichokilalia alikiona kinamsuta kwa jambo alilolifanya, moyo wake ulivurugukiwa na amani na alijiona amefanya kosa ambalo lingemgharimu  maisha yake. Mawazo yalizidi kumzunguka mithili ya nzi wanavyouzunguka mzoga uliooza, usiku huo hata kulala aliona hakufai zaidi ya kuzidi kumletea mawazo tu kwani kila alipojitahidi kuutafuta usingizi ili umpumbaze kwa muda apumzishe nafsi lakini hakuupata. Kila akikaa ndani ya chumba chake aliona kama hajatimia kwa mawazo yalivyomzonga na alihitaji kitu cha ziada ili kitulize mawazo aliyokuwa nayo ajione ametimia, kila alipofikiria hicho kitu alichokiacha miaka kadha iliyopita ndicho alijikuta akikihitaji kukipata tena ili atulize mawazo. Uamuzi wa pekee uliopita katika halmshauri ya kichwa chake ni kupata hicho kitu ili atulize akili zake vinginevyo mawazo  hayo yanayomzonga yangemnyima amani katika kichwa chake na hata moyoni mwake. Andrew aliamua kutoka usiku huohuo bila hata kumuaga yoyote hata mama yake, alitumia gari mojawapo kati ya gari zilizopo kwenye maegesho ya nyumba hiyo kuelekea  alidhamiria kwenda kupata kitu alichoona ni kitulizo cha mawazo yake katika ubongo wake. Mlinzi wa nyumba yao alifungua geti kulipisha gari aina ya altezza kutoka nje ambalo alikuwa analiendesha Andrew kuelekea getini, Andrew aliondoa gari kwa mwendo wa kasi hadi mlinzi alishangaa na makelele ya gari hiyo yaliwashtua Annie na mama yake waliokuwa ndani lakini walipotoka walikuta mlinzi ndiyo akimalizia kufunga geti na Andrew ameshatokomea.
Safari ya Andrew iliishia kwenye nyumba iliyokuwa mtaa wa pili ambao upo mbali kidogo na nyumbani kwao,  Andrew alifika kwenye geti la nyumba hiyo kisha akapiga honi halafu akaingiza gari ndani baada ya geti kufunguliwa. Alilipeleka hadi maegesho kisha akashuka baada ya kufunguliwa mlango na mmoja wa wafanyakazi wa hapo ndani, Andrew alishuka kwa haraka huku akionekana nafsi yake haitulii kutokana na mawazo aliyonayo.
"Yupo ndani?" Andrew alimuuliza mfanyakazi aliyemfungulia mlango.
"yupo pita tu" Mfanyakazi alimjibu, Andrew alienda hadi ndani ya nyumba kubwa iliyonakshiwa na mapambo ya gharama kisha akaingia ndani hadi sebuleni.
"kijana mpotevu naona leo umenikumbuka, leta mpya maana naona tangu mshua wako apate uwaziri ndiyo umetokomea moja kwa moja" alikaribishwa na sauti ya mtu  mwenye mwili wa kimazoezi akiwa amezungukwa na wasichana wakimkanda.
"kwanza nipatie kitu nina stress mzigo" Andrew aliongea huku akijibweteka kwenye kochi mojawapo yaliyopo hapo sebuleni.
"We malaya hebu mpe msokoto mmoja mdogo wangu wa hiyari" Yule mtu alimwambia mmoja wa wanawake waliokuwa wanamkanda amletee msokoto Andrew.
"Dogo hii kitu uliacha  naona sasa umeirudia" Yule mtu aliendelea kuongea.
" Komredi kuna jamaa kanipora tunda mdomoni nimemtumia mvua za rasharasha sista kashtuka kamaindi hataki kunisaidia nimpore jamaa tunda hataki" Andrew aliongea huku akipokea msokoto wa bangi kutoka kwa mwanamke aliyetumwa na Komredi.
"sasa huyo sista wako kinachofanya amaindi ni nini?" Komredi aliuliza huku akinyanyua bilauri ya pombe kali iliyopo kwenye meza ndogo.
"anamkubali yule lofa kuliko mtu mwingine" Andrew aliongea.
"mmh! Mbona kali hii malaya naye kapenda, tabia yake ya kugawa itaisha...Gota si unakumbuka siku ile tuliyomkuta kule Mikadi beach kwenye mwamba usiku kweli watu hubadilika" Komredi alimuambia Andrew kumkumbusha jambo lililomfanya avute kumbukumbu zaidi.
Andrew alikumbuka  siku ambayo alikuwa yupo na Komredi pamoja na baadhi ya kundi la wahuni la Komredi wakiwa wapo kwenye mambo yao katika ufukwe wa Mikadi beach, siku hiyo majira ya saa mbili usiku walimfuma Annie akifanya mapenzi na wanaume wawili kwa mpigo. Tukio hilo lilimuundhi Andrew sana na kusababisha ampore panga mmoja wa watu wa Komredi kisha akawakatakata watu waliokuwa wakufanya mapenzi na dada yake.
"Daaah! Nakumbuka siku ile si niliwacharaza mabeto wale mac****" Andrew aliongea baada ya kuvuta kumbukumbu huku akivuta bangi kisha akasema, "sista aliikuwa malaya yule yaani bila mshua kumuweka chini angekuwa kimboka anagawa yule". Andrew aliendelea kuvuta bangi kwa fujo hadi mawazo akayaona yapo kawaida tu.
"mshua wako alikuwa mtu wa karibu na rais katika kampeni za uchaguzi uliopita sasa unadhani angemuacha hivi na wewe angekuacha uendelee kupuliza hiyo kitu si mngemuharibia swahiba wake" Komredi aliongea.
"zima hiyo kitu kwanza, kuna bitch mmoja anaitwa Beatrice ni mtoto wa Bernard huyu muhaya yaani namkubali kichizi tatizo kuna fala kunipiga overtake. Huyu fala nahitaji azimwe kama moto kuhusu mshiko usihofu nipo tayari kurudi kwenye kupiga mzigo muda ukiwepo" Andrew aliongea kwa hasira huku macho yake yakiwa mekundu kutokana na moshi wa bangi.
"dogo kipindi cha nyuma umenifanya niwe kwenye ramani za jiji hili hadi sasa, we ni mtu wangu hiyo ishu bure wahuni wangu wanakupigia" Komredi alikubali kumfanyia Andrew  kazi yake bure kutokana na ukaribu waliokuwa nao kipindi cha nyuma  baada ya Andrew kuacha shule kutokana na uvutaji mkubwa wa bangi na utumiaji wa madawa ya kulevya, Andrew alitiwa nguvuni na baba yake ambaye alikuwa mbunge kisha akapata tiba ya kumuondoa na ualosto wa madawa pamoja bangi na ikawa ndiyo mwisho wa kuwa karibu na Komredi. Sasa amerudi kwa Komredi na amerudi katika uvutaji wa bangi aliouacha hapo awali na amepania jambo baya kwa Moses.

****

Ndani ya nyumba ya kizamani iliyopo katika sehemu iliyojitenga na makazi ya watu, ilikuwa ni majira ya saa tano usiku na humo ndani kulikuwa na mtu aliyening'inizwa kichwa chini miguu juu akipigwa magongo na watu ambao kwa mtazamo ungewajua kama ni majambazi kutokana na sura ngumu walizokuwa nazo. Kennedy alikuwa kasimama pembeni akiangalia mtu huyo aliyefunikwa uso anavyopigwa magongo na hao watu, kipigo kiliendelea kwa muda mrefu hadi yule mtu akawa amelegea kabisa na hana nguvu. Kennedy aliwaashiria wale watu wasimpige baada ya huyo mtu kuishiwa nguvu kisha akaenda kumfungua kitambaa cheusi walichomvalisha usoni, alikuwa ni Mponjo akiwa hawezi kuangalika mara mbili na mtu mwenye moyo mwepesi kwa jinsi alivyotapakaa damu usoni kutokana na kipigo kizito alichokuwa anapokea kutoka kwa hao watu.
"nani kakutuma?" Kennedy alimuuliza.
"ni do...go mmoja anayei...twa Gota" Mponjo  aliongea kwa tabu kisha akazirai hapo hapo.
"Mshusheni mkamtupe Tegeta jiranina nyumbani kwake" Kennedy alitoa amri kwa wale watu kisha akaondoka kwa haraka.


****

Andrew alirudi nyumbani kwao majira ya saa sita usiku akiwa anaendesha gari kama mwendawazimu hata alipoingia katika eneo la maegesho, aliminya mafuta kwa nguvu na kupelekea awaamshe mama yake na dada  yake waliokuwa wamelala ndani. Siku hiyo baba yake hakuwepo alikuwa kwenye mkutano bungeni Dodoma hivyo hapakuwa na mtu anayemuogopa,  aliposhuka ndani ya gari alimkuta mama yake akiwa yupo kwenye mlango wa kuingia ndani akiwa kakunja sura. Andrew hakumjali hata kidogo kutokana na akili zake kuwa zinaongozwa na bangi muda huo, alitembea hadi mlangoni akiwa ameinamisha uso wake chini.
"Andrew unatoka wapi? Na kwanini unaendesha gari hivyo?" Mama yake alimshambulia kwa Maswali akiwa amesimama katikati ya mlango, Andrew aliinua uso na kumtazama mama yake bila hata kusema chochote. Mama yake alipouona macho mekundu ya Andrew na sura ya jazba alipisha njia mwenyewe kwa hofu, Andrew alipopishwa njia alimpita bila hata kumsemesha akaingia ndani huko nako alikutana na dada yake na wakaishia kutazamana kwa macho ya chuki kila mmoja. Andrew alipitiliza chumbani kwake moja kwa moja akajifungia.

****

Asubuhi iliyofuata baada ya Beatrice kuondoka shule, Victoria aliamua kutumia gari aina ya toyota landcruiser kwenda nayo chuoni. Akiwa anatoka nje ya geti lao alikutana gari aina ya BMW ambayo ilitumiwa na Moses kuja katika sherehe ya kuzaliwa ya Beatrice ikiwa ipo nje ya uzio wa nyumba yao pembeni ya geti. Alipoliona alisimamisha gari akidhani ni Moses kisha akashuka hadi kwenye kioo cha dereva halafu akagonga kioo ili  amsalimie shemeji yake kwa mdogo wake, kioo kiliposhushwa alikutana na sura ya aliyekuwa shemeji yake na pia ni mjomba wa shemeji yake mwingine. Kennedy ndiye aliyekuwa yupo ndani ya gari hiyo akiwa na sura ya tabasamu, Victoria alishtuka kidogo alipomuona kisha tukio la siku iliyopita la Kennedy kumpiga Mponjo aliyemuumiza Moses likawa linapita kichwani mwake.
"vipi unashangaa kuniona mimi hapa" Kennedy aliongea huku akitabasamu mu, Victoria alibaki kaduwaa akiwa hana la kusema.
"Moses is my nephew(Moses ni mpwa wangu) hatakiwi kujua chochote iwe kujuana kwetu sisi au suala la mimi kuwahi kutembea na Annie, Victoria nadhani  umenielewa" Kennedy aliongea  akiwa anatabasamu vilevile.
"ndi..yo Tasu" Victotia alijibu kwa kubabaika kwani alitambua mtu anayeongea naye si mwenye roho ya kawaida hasa baada ya kushuhudia alichokiona siku iliyopita.
"ni hayo tu mrembo, so long" Kennedy alihitimisha maelezo yake kisha akaweka gia ya kurudi nyuma, alirudisha gari nyuma kwa kasi kisha akageuza akaondoka. Victoria alibaki kaduwaa kwa dakika kadhaa akiwa na uoga, alibaki hapo akijifkiria kisha akapuuzia maneno hayo halafu akaingia ndani ya gari akaondoka kuekekea chuo.

****


                                    TAWI DOGO
     EAST AFRICA SECURITY      AGENCY(EASA)
                             DAR ES SALAAM.

Norbert aliingia katika ofisi za mkuu wa EASA tawi la Dar es salaam baada ya kupokea simu ya kuitwa na CE, alipita kwa katibu Mukhtasi ambaye Norene kama ilivyo kawaida yake. Ofisini kwa katibu mukhtasi alimkuta Norene akiwa amekaa kwenye kiti akuendelea na kazi za kawaida. Norbert alienda hadi nyuma ya Norene kisha akamshika kiuno halafu akambusu shavuni.
"we Mwanaume leo ndiyo umejileta sio" Norene aliongea baada ya Norbert kuingia ofisinj kwake na kuanza kumfanyia uchokozi.
"bibie we ni sumaku mi chuma nitajiletaje bila wewe kunivuta" Norbert aliongea huku mikono yake ikiwa bado ipo kiunoni mwa Norene.
"kwahiyo nimekuvuta sio" Norene aliuliza huku akiinua kichwa juu kumtazama Norbert.
"we huoni hata mikono yangu imenasa kiunoni mwako kwenye nguvu kubwa ya sumaku, yaani kiunoni changu nacho  kinavutwa hapa sema nimekizuia ila nitazidiwa" Norbert aliongea kimasihara huku akijifanya kama kiuno chake kinavutwa kwenda mbele.
"looh! Jianaume kama beberu vile hebu toka zako" Norene aliongea huku akinyanyua kitabu kilichopo mezani ili ampige nacho Norbert kutokana na masihara yake, Norbert alirudi nyuma kwa haraka huku akicheka kisha akauliza, "kizee chako kipo?"
"siyo kizee sema kijana mwenye mvi, yupo anakusubiri" Norene aliongea.
"mmh! Kijana! Ujana wake umeujuaje au ushawahi kuupima nini?" Norbert aliongea kwa masikhara na kupelekea Norene akunje sura kisha akamrushia kitabu Norbert ambacho kilimkosa
"lione" Norene aliiongea baada ya kitsbu kumkosa Norbert.
"nimeuliza tu kwani kuna kosa?" Norbert aliongea huku akifungua mlango ulioandikwa CE halafu akaingia.
"N001 karibu" sauti ya mzee wa makamo mwenye mwili mkakamavu ilimkaribisha.
"asante CE"  Norbert alijibu huku akitoa heshima kwa CE.
"keti tafadhali" CE aliongea kisha akabonyeza kitufe kilichopo juu ya meza yake na kupelekea taa za ofisini kwake zizimike na kirusha picha ukutani ambacho hutumika kuonesha sinema kichukue nafasi ya kurusha picha katika ubao mweupe uliomo humo ofisini. Picha ya mzungu mwenye mwili mwembamba na kimo kirefu ilionekana kwenye ubao vizuri, CE alichukua fimbo na kuanza kuionesha hiyo picha.
"anaitwa Brown Mcdonald ni raia wa Uingereza mwenye mafunzo wa hali ya juu ya kijeshi aliyoyapata alipokuwa katika jeshi la Uingereza, pia ni kachero wa shirika la kipelelezi la Uingerza maarufu kama M16 aliyeasi na akajiunga na mafia wa Italy wenye mtandao wa kuuza madawa ya kulevya duniani. Karibu mashirika yote ya kipelelezi yanamtafuta kutokana na makosa tofauti ikiwemo  mauaji, uuzaji wa madawa ya kulevya na wizi wa vifaa mbalimbali vya kijeshi. Gaidi huyu ametoroka Ulaya na inasemekana yupo Ndani ya ukanda wa Afrika ya mashariki kutokana na kadi yake ya benki kutumika katika ATM za Barclays za jijini Dar es salaam, Kampala na Nairobi, kazi ya kumsaka ipo mikononi mwako vifaa vya kazi atakupatia Norene" CE aliongea kwa kirefu zaidi, Norbert alitikisa kichwa kukubaliana na CE.
"napenda nikutahadharishe kabisa kwamba katika kazi ya kumtafuta huyu mwanaharamu sitaki ulete umalaya wako wa kupenda kufungua zipu kila ukiona kizuri, inabidi uwe makini la si hivyo itakugharimu N001 na kazi haitofanikiwa. Narudia tena punguza umalaya muda wa kazi" CE alisisitiza.
"sawa mkuu" Norbery aliitikia.
"unaweza ukaenda ila usisahau kupita kwa Norene ukachukue vitendea kazi.
"sawa mkuu" Norbert aliinuka kisha akapeana mkono na CE halafu akatoka ofisini kwa CE, alirudi hadi ofisini kwa Norene kama alivyoelekezwa na CE.
"mzigo wako huo hapo nyuma ya kiti" Norene aliongea huku macho yakiwa kwenye kioo cha tarakilishi, Norbert alichukua sanduku aliloelekezwa kisha akamtekenya Norene halafu akambusu shavuni. Alichukua begi dogo lenye umbo kama mkoba wa kuhifadhia pesa halafu akaanza kuondoka ofisini humo.
"Nor" Norene alimuita na kumfanya asimame kumsikiliza, Norbert alirudi hadi pale alipo Norene kisha akamtazama Norene.
"kazi njema ila ukae utambue nakupenda" Norene alimuambia Norbert kisha akabadilishana naye shurubati ya kinywani mwake kwa dakika nzima.
"kila la heri" Norene alimuambia Norbert kisha akaendelea na kazi zingine, Norbert aliondoka bila kusema chochote zaidi ya kutabasamu.



ITAENDELEA!!

No comments:

Post a Comment