Monday, November 14, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA KWANZA




    RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843



SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA



ANGALIZO: KUTOKANA NA KUTAKA DHAMIRA YA RIWAYA HII IFIKE KWA JAMII NIMEAMUA KUTUMIA SEHEMU MBALIMBALI ZA KIJAMII HASA KIDINI KWA DINI ZOTE, NDUGU MSOMAJI NI MARUFUKU KUTOA COMMENT YOYOTE INAYOHUSU UDINI ILI KUHESHIMU DINI YA MWENZAKO




*****ANZA SASA**********


         SURA YA KWANZA
                (MFUNIKO)
    
   Mlio wa saa ya mezani ndiyo ulisikika ukileta bugudha katika kitanda walicholala wapendanao  majira ya asubuhi ikiashiria muda waliokuwa wanahitaji kuwa macho wakati bado usingizi unawazonga ndiyo huo umewadia, wa kwanza kushtuka alikuwa mwenye jinsia ya kiume ambaye baada ya kushtuka tu alinyanyua mikono juu kisha akaipeleka kushoto na kulia ili kunyoosha baadhi ya viungo halafu akamuangalia mpenzi wake aliyekuwa amelala usingizi.

     Alimuamsha taratibu sana kwa namna isiyoleta karaha kwa mpenzi wake halafu akampiga busu baada tu ya mpenzi wake kuamka, alinyanyuka kitandani akaelekea sehemu kilipo kioo cha kabati dogo la kuwekea vipodozi na uturi wa aina mbalimbali  wanaoutumia, mwanaume huyo alipofika hapo kwenye kioo alijiangalia kwa muda akakagua uso wake na aliporidhika akageuka upande wa kitandani akamuona mpenzi akiwa amekaa kitako huku sehemu kubwa ya mapaja yake ikiwa ipo wazi kutokana na kuvaa gauni fupi la kulalia. Mwanaume huyo alibaki akimtazama mpenzi kwa muda mrefu hadi mwanamke huyo akajua kwamba anatazamwa na mpenzi wake tena kwa mshangao.
 
        "Mbona unaniangalia hivyo jamani?" Mwanamke aliuliza huku akiangalia chini.

       "Yaani mke wangu kama ndiyo kwanza nakuona, kila siku wewe ni mpya ndani ya macho yangu kuanzia urembo  wako hadi...dah! Ngoja niache" Mwanaume huyo huyo aliongea huku akiachia tabasamu lililomfanya aonekane na mvuto zaidi kuliko hata ilivyokuwa awali.

       "Hata wewe nakuona ni mwanaume mpya kila saa ndiyo maana hata ukiwa unaendesha gari kuelekea kazini huwa siishi kukutazama machoni huku nikiwa nina tabasamu usoni mwangu mume wangu, Moses nakupenda sana mume wangu" Maneno hayo yalimtoka mwanamke huyo akiwa amesimama na kulifanya umbo lake tata na mapaja yaliyo jaa vionekane dhahiri ambapo laiti kama vikionekana mbele ya mwanaume mkamilifu yoyote basi lazima aingiwe na matamanio papo hapo, kifua chake kichanga kisichofunikwa na kitu kingine chochote zaidi ya gauni laini la kulalia ndiyo kilionekana na kilimfanya aonekane mrembo zaidi kwa Moses.

          "Hata mimi nakupenda pia Beatrice na sitaacha kukuonesha nakupenda na hata ikibidi nitumie misamiati mbalimbali ila ibebe ujumbe huo wa kuonesha jinsi gani ninavyokupenda mke wangu" Moses aliongea kisha akamkumbatia mke wake kwa mapenzi ya dhati.
 
      "Nafurahi sana kusikia unanipenda kama ninavyokupenda mimi mume wangu, nina suprise yako muda huu jana sikukuambia" Beatrice aliongea baada tu ya kuachiana na Moses huku uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu halafu akageuka akampa mgongo Moses, hiyo ilikuwa ishara tosha kwa Moses ambapo na yeye alimkumbatia mke wake kwa nyuma halafu akampiga busu sehemu ya juu ya sikio na kupelekea Beatrice asisimkwe mwili mzima.

        "My queen tell me( malkia wangu miambie)" Moses alimuambia Beatrice jirani kabisa na sikio lake tena kwa sauti ya chini huku akitoa muhemo hafifu, Beatrice aliposikia hiyo kauli ya Moses aliuchukua mkono wa kuume wa Moses akauweka tumboni mwake halafu akasema, "You guess what? (we unadhani nini?)"

       "Wooow! Don't tell me, I'll be crazy more than now(Wooow! Usiniambie, nitakuwa kichaa zaidi ya sasa)" Moses aliongea huku akiwa amepigwa na mshangao pamoja na tabasamu kubwa usoni mwake.

        "Nimenasa Moses na nimejua jana tu  na leo asubuhi ndiyo nilitaka ujue kama ulivyojua sasa hivi" Beatrice aliongea huku akimuegemea Moses kwa nyuma, kauli hiyo ilimfanya Mosea ambusu mara nyingi sehemu za shingoni, kwenye mashavu na mdomoni hadi Beatrice akaanza kupata msisimko mwili mzima.

          "Moses hapana siyo sasa hivi mume wangu, tutachelewa kazini twende tukaoge bwana" Beatrice alimuambia Moses ambaye alimuonesha kumuelewa na wote wakatoka wakaelekea bafuni.

 
  Baada ya nusu saa wapendanao hao walitoka pamoja wakiwa wanatumia gari moja wakaelekea kazini kama ilivyo kawaida yao katika siku za kazi, Beatrice alipelekwa mpaka kazini kwake posta kwenye jengo la Benjamin william mkapa ambalo ni makao makuu ya shirika la mfuko wa hifadhi ya jamii.

    Baada ya Moses kumshusha mke wake katika jengo analofanyia kazi aliimgiza gari barabarani akiwa na tabasamu kubwa usoni mwake kutokana na taarifa aliyoambiwa pindi alipoamka, baada ya dakika kumi na tano alikuwa tayari ameshafika katika jengo la maabara kubwa ya umoja wa mataifa iliyojengwa maeneo ya Magogoni jijini Dar es salaam  katika wilaya ya Ilala. Ilikuwa ndiyo eneo lake analofanyia kaziili kuweza kuficha utambulisho wake wa pili kama mkurugenzi wa idara ya usalama aliyeteuliwa na Rais Zuber Ameir baada tu ya kuingia toka apinduliwe rais muovu Filbert Ole aliyetaka kuuza rasilimali za nchi kwa wahalifu wa kimataifa waliokuwa chini Hilton maarufu kama eagle the don ambye kwa muda huo tayari alikuwa ni marehemu baada ya kuangamizwa katika OPERESHENI FAGIO LA CHUMA iliyokuwa ikifagia viongozi wote waovu ndani ya jamhuri ya muungano pamoja na vibaraka wao wote. Ulikuwa ni mwaka wa tatu umepita tangu operesheni hiyo imefanyika na kuleta mapinduzi makubwa kwa watanzania  baada ya kuondoshwa uongozi usiofaa kwa wananchi.

     Moses akiwa na furaha kubwa usoni alitembea huku akitabasamu na alikuwa akisalimiana na wanafanyakazi wenzake kama ilivyo kawaida ingawa siku hiyo uchamgamfu wake tofauti na ilivyo siku nyingine, ujauzito wa mkewe Beatrice ndiyo ulimfanya afurahi kuliko kitu chochote kwani alijua baada ya miezi kadhaa angeitwa baba  baada ya Beatrice kujifungua mtoto aliyekuwa amembeba katika tumbo lake. Kawaida ya wanaume wote walioko kwenye ndoa ambao huwa na ndoto za kuwa familia wakipata habari kama hiyo ni lazima wawe na furaha, ndiyo maana hata Moses alikuwa nafuraha vilevile baada ya kupata habari hiyo kutoka kwa mkewe.

     Aliingia ofisini kwake akiwa na furaha vilevile na aliketi kwenye kiti chake cha kuzunguka ambacho kilikuwa kimevishwa koti jeupe kwa nyuma ambalo hutumiwa sana na matabibu au watu wa maabara, sekunde kadhaa toka aketi kwenye kiti mlango wa ofisi yake ulifunguliwa na akaingia mtu aliyevaa mavazi ya kanisa la kiluteri akiwa na tabasamu pana sana usoni ambaye alipoonekana mbele ya macho ya Moses naye alijikuta akitabasamu baada ya kumbaini mtu huyo aliyehusika katika kuwaunganisha  wawe mwili mmoja yeye na Beatrice. 
  
   Alikuwa ni askofu wa kanisa la kiluteri dayosisi ya mashariki na pwani Dkt Edson David ambaye ni mtu aliyemheshimu sana kutokana na busara alizonazo pamoja na hekima katika kuongoza ibada mbalimbali katika kanisa lake, Moses alisimama kwenye kiti kwa heshima aliyonayo kwa askofu huyo na alimfuata akiwa na uso uliojawa furaha sana hadi akasababisha Askofu naye atabasasmu zaidi kama anaelekea kucheka kutokana na kuridhishwa na uchangamfu aliyooneshwa na Moses ambaye ni kijana aliyejizolea umaarufu nchini kutona na kazi yake ya sayansi.

       "Bwana yesu asifiwe baba askofu" Moses alioongea kwa uchangamfu huku akimpatia mkono Askofu Edson.

     "Ameen Bwama yesu asifiwe Professa" Askofu Edson alijibu kwa uchngamfu huku akitumia jina la cheo alichotunukiwa Moses baada ya kufanya mapinduzi makubwa katika sayansi nchini Tanzania kwa kuweza kugundua vitu mbalimbali ambavyo havikuwahi kugunduliwa na wanasayansi waliopita baada ya kufariki kwa Professa Lawrence Gawaza ambaye alikuwa ni baba yake mzazi.

        "Karibu sana baba" Moses alimkaribisha Askofu Edison akitumia jina la baba alilozoea kumuita kutokana na kumheshimu sana.
 
       "Asante mwanangu vipi mkeo hajambo?" Askofu Edson alishukuru kwa ukaribisho huo kisha akauliza hali ya mke wake Moses.

        "hajambo baba tunamshukuru Mungu miezi tisa baadaye tunatarajia na sisi kuongeza familia yetu" Moses alimuambia hali ya mkewe Askofu Edson kisha akamfunulia habari za ujauzito aliokuwa nao Beatrice, askofu aliposikia taarifa hiyo alitoa tabasamu kubwa kama ilivyo kawaida ambalo halitofautiani na kicheko.

         "hongera sana mwanangu hakika Yehova ametenda kazi yake ndoa yenu, apewe sifa kwa hilo. Bwana wa mabwana amewapa baraka itokaye kwake atukuzwe kwa hilo kama ilivyobainishwa na waraka wa pili wa Wakorinto 9:8 ambayo inasema,'na Mungu anaweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili kila wakati muwe na kila kitu kwa kiasi cha kutosha na ziada kwa ajili ya kazi njema'.

       Bwana asifiwe katika hilo mwanangu kwani amewapatia kila kitu katika maisha yenu kwa kwa ajili ya kazi njema iliyowaleta hapa duniani, ameweza kuwapa maisha mazuri mliyokuwa mkiyahitaji, ameweza kuwapa upendo katika mioyo yenu mliokuwa mnauhitaji kwenye ndoa yenu, ameweza kuwapa maisha yenya amani na upendo katika ndoa yenu, ameweza kuwapatia kile mnachokitafuta kutokana na jasho lenu, pia ameweza kuwajalia afya njema mliyokuwa mkiihityaji katika ndoa, pia ameweza kuwajalia kuongeza mwanakondoo mmoja kutokana na ndoa yenu ili akikua aweze kumsifu bwana kama mnavyomsifu nyinyi na pia amewajalia elimu na heshima ndani jamii yenu ambayo ndiyo mliyokuwa mkiihitaji. Hakika bwana ni muweza wa yote mwanangu, bwana asifiwe" Askofu Edson alihubiri neno baada ya kuambiwa habari njema ya ujuzito wa Beatrice na alizidi kumfungulia Moses juu ya neema za muweza yote kwa kuwajalia mambo mbalimbali katika maisha yao, mahubiri hayo yaliingia sawasawa katika moyo wa Moses ambaye alikuwa akinyoosha mikono kila pale mchungaji alipokuwa akihubiri na alitamka amen kwa kila uwezo wa muweza uliotajwa na Askofu Edson.

       "Amen" Moses alisema tena neno hilo baada ya mchungaji kufikia kituo cha mahubiri yake aliyoyahubiri kwa hisia huku akitetemeka.

        "Baada ya kumshukuru kwa kila jambo alilolitenda katika  maisha yenu pia na mimi kumshukuru bwana kwa kila jambo alilolitenda kwa maisha yangu hadi kuniwezesha mimi kufika eneo hili nikiwa na uzima pia nina afya njema, napenda niongee kile kilichonileta hapa mwanangu kwa uwezo wa mkuu wa majeshi na mwenye uweza kuliko majeshi yote ndani ya ulimwengu huu" Askofu Edsona alileta utangulizi wa maneno kabla hajanena kile kilichomleta katika ofisi ya Moses asubuhi ya siku hiyo, aliingiza mkono wake katika kanzu yake ya kiaskofu akatoa karatasi zilizokunjwa vizuri akampatia Moses huku akiwa na tabasamu usoni mwake kama ilivyo kawaida yake.

     Moses alizipokea karatasi hizo akazipitia kisha akamtazama Askofu Edfson akioneshwa hajaelewa juu ya kile kilichoandikwa katika karatasdi zile, aliamua kuzipitia kwa mara ya pili karatasi hizo kisha akaziweka juu ya meza akamtazama Askofu Edson kwa macho yanayoasharia anataka ufafanuzi juu ya kile akilichoandikwa katika katika karatasi zile.

     "Mwanangu kanisa kuu la kiluteri la nchini Ujerumani limetambua sana mchango wako kitaifa na hata kimataifa katika medani ya sayansi ndiyo maana ikakuteua wewe ushiriki katika mchango wa kiroho katika kulisaidia kanisa hili kwa jina la bwana kwani amekusaidia katika mambo mengi hivyo inabidi na wewe usaidie katika kutoa amchango wako katika asasi zinazoendeshwa na wanakondoo wa bwana. Hakika bwana amejitolea katika maisha yako basi nawe unatakiwa ujitolee katika kuendeleza asasi  za wanakondoo wa bwana walau kwa mchango mdogo uwezao kuutoa katika hili mwanangu, yapasa uwe na fadhila kwa kila wema alokutendea bwana katika maisha yako ya kila siku. Mwanangu wanakondoo wa nchini ujerumani kwenye kubwa ya kanisa la kiruteri duniani wamekumbwa na  na balaa kubwa la kufiwa kwa mazao yao mizabibu katika mashmba yao yaliyopo nchini Italia ambayo yamekuwa yakiendeshwa na asasi yao kubwa ya kidini nchini humo, kutokana na kutambua mchango wako wa kisayansi kimataifa na hata kitaifa  wameamua kukuletea ujumbe huo waliokuomba ili wapate dawa ya quantanise ambayo uliigundua mwezi uliopita ili iwe sulushisho kwa uharibifu wa zao linaloingizia asasi hii kubwa ya kanisa la kileteri kubwa sana duniani. Mwanangu kanisa hili la Evangelical lutheran la Ujerumani linaomba msaada  katika hili uwakomboe na janga hili kwa kuwatumia sehemu ya dawa yako" Askofu Edson alieleza kiini cha safari yake ilyomleta ofisini kwa Norbert ili aeleze shida inayo wasumbua kanisa kubwa la kiluteri duniani ambalo, maelezo hayo yalimfanya Moses ajifikirie kwa muda wa dakika kadhaa kisha akashusha pumzi ndefu akayachukua makratasi yale akayasoma kwa mara ya pili.

     Hakika maneno ya Askofu  Edson yalimuingia barabara katika mtima wake kwani alikuwa muumini mzuri wa kanisa  la kiluteri, uhudhuriaji wake wa  misa katika siku ya jumapili ulimfanya awe na moyo wa kuwasaidia waumini wenzake wa kanisa la kiruteri kwani walikuwa wamoja hivyo kusaidiana ni jambo muhimu.


    Alipomaliza kusoma karatasi zile alinyanyua macho akamtazama Askofu Edson kisha 
akamwambia,"nipo tayari baba katika kuwasaidia wanakondoo wa bwana"

    Maneno yake yalimfanya Askofu Edson aachie tabsamu lake linalofanana na kicheko kwa mara pili ambalo sasa hivi lilikuwa pana kulikuwa awali hadi mapengo yake ya sehemu za magego yakaonekana, kauli ya Mosaes ilimfanya atamke."Ubarikiwe mwangu kwa jina baba ubarikiwe ,ubarikiwe mwanangu kwa jina mwana  na ubarikiwe mwanagu kwa jina la roho mtakatifu".

          "Amin" Moses aliitikia huku akiachia tabasamu kutokana na kunogewa sana na neno la uzima alilokuwa anapewa na Askofu Edson.

      "Mwanangu haina budi nikuache uendelee kuutafuta mkate wa kila siku ambao amekuwekea bwana wa mabwana uutafute kwa njia nhii, amani ya bwana iwe nawe" Askofu Edson aliaga baada ya ujumbe aliouleta kupokelewa kwa mikono miwili na Moses ambaye alikuwa ni professa mwenye umri mdogo kabisa katika nchi ya Tanzania na akiwa amefanya maajabu mengi sana katika medani ya sayansi kama alivyofanya baba yake katika kipindi ch maisha yake ingawa aliitumia kinyume muda mwingine.

    Dakika kumi kupita tangu aondoke Askofu Edson, Moses alikuwa akipitia baadhi ya mafaili yaliyopo mezani iliaangalie kazi zilizokuwa zimeachwa kiporo aweze kuzimalizia, alipitia faili moja moja hadi akamaliza kisha kanyanyua mkonga wa simu ya mezani akbonyeza namba moja tu kisha kaweka sikioni akasikiliza milo wa simu ukiita hadi ikapokelewa.
 
        "Dokta Roshan namuhitaji ofisini kwangu mara moja" Aliongea maneno hayo kisha akakata simu akaurudisha mkonga mahala pake, alisubiri baada ya dakika moja na mlango wake ukafunguliwa akaingia kijana wa kihindi aliyepishana naye kiumri akiwa amevaa koti la kitabibu na miwani ikiwa ipo chini kidogo ya macho yake ikiwa imejenga mpaka kati ya pua na macho yake. Kijana huyo wa kihindi aliashiriwa na Moses aketi kwenye kiti naye akataii halafu akasema,"Yes Professor(ndiyo professa)"

         "Doctor two cointainer of Quantanise must remain here for community needs(Daktari vyombo viwili vya     Quantanise vinatakiwa vibaki hapa kwa matumizi ya jamii" Moses aliongea huku akimtazama Dokta Roshan kwa umakini.

           "Ok Professor(sawa Professa)" Dokta Roshan alitii amri ya Moses kwa heshima na utiifu.
 
           "you may go(unaweza kwenda)" Moses alisema na Dokta Roshan alinyanyuka kwenye kiti akatoka nje ya ofisi hiyo, Moses alichukua koti la kikazi akalivaa  na akabeba mafaili yaliyopo mezani kwake akatoka nje ya ofisi yake na akaufunga mlango akenda kuendelea na kazi kama ilivyo kawaida yake akiwa yupo ndani ya maabara hiyo ya Umoja wa mataifa



****

                                                              YOMBO,
                                               WILAYANI TEMEKE,       
                                                   DAR ES SALAAM.

 
    Upande huu jijini Dar es salaam kulikuwa kuna hali shwari sana ndani yake na watu walikuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida, ilikuwa ni katika mtaa unaoitwa     Bakwata jirani kabisa kabisa na makutano ya reli mbili za Tazara ambapo moja ilikuwa ikitokea bandarini na nyingine ikitokea katika kituo cha treni za abiria cha Tazara kilichopo mkabala na kiwanda cha kutengeneza mikate kinachokuwa kikimilikiwa na mfanyabiashara maarufu sana jijini Dar es salaam.

    Eneo hili la Yombo mtaa wa Bakwata jirani kabisa mwembe ambao hutumiwa na watu katika kucheza bao pamoja na kunywa kahawa kulikuwa na hali ya utulivu huku baadhi ya vijana wakiwa wapo na shughuli zao na wazee pia walikuwa wapo katika mizunguko takribani mitano wakiangalia wazee wenzao waliokuwa wanacheza bao. Kulikuwa na hali ya amani ambapo amani hiyo iliingia dosari katika namna isiyotarajiwa baada ya kupita mzee wa kanisa moja mgeni  maarufu sana maeneo hayo akiwa kaongozana na vijana wake wawili pamoja na mlinzi huku mbele yao kukiwa na kijana anayesukuma toroli kubwa lililosheheni nyama mbichi ambayo hupendwa kuitwa na vijana kwa jina la mbuzi katoliki na wengine wanaiita kitimoto. 

    Kijana huyo alionekama akiendesha mkokoteni huo kwa kasi bila ya kujali uwepo watu njiani na uzito wa mzigo wa mzee wa kanisa huyo mwenye lafudhi ya kichaga naye hakuisha katika kumuhimiza yule kijana afanye haraka, mkokoteni huo pamoja na msafara wa  mzee wa kanisa huyo ulikuwa ukitokea upande lilipo daraja la tingatinga na ulikuwa ukielekea upande uliopo miembe hiyo  ambapo yule kijana mwenye mkokoteni alionekana kutaka kupitiliza eneo hilo.

          "Aisee bwashee nimekuambia kata kona hapo kwenye huo muembe uingie ndani ndipo ilipo njia ya kuelekea nyumbani kwangu" Mzee wa Kanisa huyo ambaye anatambulika kwa kutozungumza na watu maeneo hayo alimkumbusha yule kijana baada ya kuonekana alitaka kupitiliza njia anayoelekzwa. yule kijana ilimbidi akate kwa upesi kwani angepitiliza ingekuwa ngumu kurudi nyuma kutokana na wingi wa mchanga uliopo eneo hilo na hapo ndipo alipotibua amani ya eneo hilo baada ya kusababisha kile kilichowaudhi wazee waliokuwa 
wanacheza bao. 

     Alikuwa amefanya kosa kubwa sana kwa kona yake aliyoikata kwa nguvu katika eneo hilo kutokana na kushurutishwa na aliyempa ajira ya kubeba mzigo wake ili aweze kupata ujira.
Kijana huyo alikuwa amezua makuu ambayo  laiti angelijua yangelitokea wala asingelikubali kubeba mizigo za mzee huyo wa kanisa  maarufu sana maeneo hayo kutokana na kuwa jeuri na kutozungumza na watu sana hasa waliokuwa wapo imani tofauti   sana na yeye kutokana tofuti za kiimani.
 
    Kona kali aliyoikata yule kijana ilisababisha majimaji yaliyokuwa yapo ndani ya nyama hiyo ambayo ilikuwa haijafunikwa vizuri kuwamwagikia wazee waliokuwa wamekaa makundi mawili wakiwa wanacheza mchezo wa bao huku wengi wakiwa wanakunywa kahawa wakibadilisha mawazo tofauti, wazee hao walimtazama kwa hamaki yule kijana kisha wakamuangalia yule mzee wa Kanisa ambaye alionesha kutojali kabisa juu ya suala hilo na ndiyo kwanza alimuhimiza yule kijana aendelee na safari baada ya kumuona yule kijana akiwa ameduwaa akiweka mikono ishara ya kuomba kwa wale wazee.
 
         "Aisee bwashee huu siyo mwisho wa safari mama Minaeli yupo nyumbani anasubiri mzigo kwa sjili ya Kipaimara cha mtoto wetu anayekuja kesho!! Twende mbele wewe" Mzee wa kanisa huyo aliongea kwa kufoka akimuhimiza yule kijana asonge.
 
          "We Kimaro ina maana huoni huyo kijana alichokifanya, katumwagia najisi ambayo na wewe unaona upuuzi tu" Mzee mmoja alilalamika huku akikunja uso kutokana na majimaji yaliyopo kwenye nyama hiyo kumwagikia.
 
       "mabwashee kwani akiwamwagia ndiyo mnakufa mpaka malalmike hivyo' Mzee wa Kanisa aliongea kwa dharau huku wale vijana aliokuwa nao wawili wakiwa wapo pembeni yake wakitazama tu.
 
      'Yaani wewe kimaro pamoja na hao wanao ni mna mwezi tu tangu mhamie naona sasa mwataka kutupanda kichwani sisi wenyeji wako uliotukuta" Mzee alimaka kwa sauti kisha kasimama juu akafunua shati lake akatoa  msime halafu akasema,"hizi ni dharau kabisa yaani  wewe mchaga kuja mwezi tu unatuletea jeuri hivi kiasi cha kudhalilika hivi tukajikoshe makosho saba".

      Mzee huyu aliwavamia Kimaro na wenzake na kusababohsa kutokea kwa vurugu kubwa sana, ambyo iliwafanya baadhi ya waumini wa dini kiislamu kulivalia njuga suala hilo.



****


                                                           GEREZA LA UKONGA,
                                                                        PUGU


   Mlango wa chuma wa gereza ulifunguliwa kwa nguvu na askari aliyeonekana alikuwa hajapenda kwenda  kumtoa mfungwa aliyekuwa ndani ya gereza ambaye kwa muda huo alikuwa tayari ameota ndevu nyingi sana kutokana kukaa gerezani kwa muda wa miaka kadhaa tu tangu ahukumiwe kifungo cha maisha, alikuwa ni adui mkubwa wa nchi ya Tanzania kutokana na maovu aliyoyafanya ambayo yalimstahiki hata apewe adhabu ya kifo kwa sheria kali za nchi nyingine tofauti na Tanzania. Mzee huyu ulipofunguliwa mlango alionesha kutojali ndiyo alijigeuza upande wa ukutani wa godoro alilolalia akionesha ni kiburi sana. Jambo hilo lilimuudhi sana askari aliyefungua mlango hadi akmfuata akampiga rungu la kwenye paja lilomfanya mzee huyo augulie maumivu kisha akamvuta kwa nguvu.

          "Pumbavu wewe unadhani hapa ni ikulu ulipoingia kwa kumwaga damu ya wenzako" Askari alimfokea huku akimsukuma nje mzee huyo ambaye alikuwa ameshika sehemu ya paja liyopigwa runmgu.

        "tena ongoza njia kabla sijakuongeza rungu la pili fisadi wa nchi wewe" Askari alimuambia kwaukali huku akimsukuma atangulie mbele.




*ndiyo mwanzo tuwe pamoja





ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment