Thursday, December 3, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA KUMI NA SITA





 DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE


SEHEMU YA KUMI NA SITA!!
Mara ya kwanza nilianza kwa Faimu nikawa najipitisha sana kwao ili anuone nikijua nitamnasa tu kama nilivyonasa vijana wa hapo kijijini kumbe Faimu hakuwa kijana wa hivyo, uvumilivu uliponishinda niliamua kumuambia ukweli  lakini pia nilimkosa baada ya kukataliwa na akanitishia kumuambia Hamis.  Mara ya pili niliirudia tabia yangu kwa kumtaka Ally baada ua uzuri wake  kuonekana alipofikia kwenye balehe  lakini pia alinikataa nikajikuta nazidi kumsumbua nikijua nitampata tu kwani ni mtoto yule bado akili haijapevuka zaidi ya kupevuka mwili tu, nilipoona nakataliwa sikuchoka na niliamua kuanzisha mazoea ya kawaida naye.  Siku nilipokuja kuwafuma Farida na Faimu na wote wakakiri kuwa wana uhusiano ndiyo siku niliyoona ya kutumia sababu hiyo kwa njia mbili, kwanza ni kulipa kisasi cha kukataliwa na Faimu na pili ni kumteka Ally kiakili. Nilijua Ally ni bado ana akili za kitoto hivyo nilipanga nimuambie hii habari ili ajue ni jinsi gani nampenda hadi nikaamua kumuambia hiyo habari ili aamini moyo wangu upo kwake, pia nilitaka nimuambie mpenzi wangu juu ya usaliti wa rafiki yao kwao waweze kumfanyia kitu kibaya ili nimcheke na hata amkose Farida.



****


Sikutaka kurudi nyuma katika azma hii ambayo niliiweka  na hapo ndipo nilipoona ni nafasi nzuri ya kuweza kujipa furaha niliyokuwa  naitaka, nilianza kutimiza azma hii kwa kumuambia Ally juu ya uhusiano wa Farida na Faimu nikijua na yeye ataumia akisikia kaka yake ameporwa tunda alilokuwa akilitaka kila siku ili aweze kulimiliki katika mkono wake. Tena nilijifanya naongea kwa hisia zaidi ili nimteke akili zaidi kwa kuamini huyu bado ni mtoto, nilimuambia lengo la kumuambia hiyo habari ni kutokana na jinsi gani nampenda na sipendi aumie akisikia kaka yake ameumia kwani na mimi nitaumia pia kutokana na jinsi ninavyompenda yeye. Nilizidi kuongea kihisia kwa kumuekeza ni jinsi gani namuamini mpaka ikafikia kumuambia hayo mambo kwani nilihisi  ndiyo mahali salama ya moyo wangu, nilijivika ujasiri tofauti na watoto wengine wa kike nikiwa naeleza hayo maneno ambayo nilijua kabisa kwa mtu kama Ally mwenye kusumbuliwa na mihemko ya upevukaji basi nitaweza kumpata kirahisi jambo ambalo lilikuwa kinyume na nilivyotarajia.
Baada ya kutua maneno yangu yote niliyokuwa nimeyapanga kinywani mwangu Ally alinitazama sana kisha akaniuliza, "hivi watu wakipendana na wenyewe wakiridhiana kuna haja ya kuwafuatilia?"
Nilimjibu, "hakuna haja ya kuwafuatilia".
Jibu langu hilo nilimjibu kirahisi tu kwani bado nilimuona mtoto na ana itikadi za kitoto hivyo sikuhofia kabisa kama ataongea neno jingine kwa jinsi anavyompenda kaka yake, nikiwa nasubiri ni nini atasema kifua chake kilipanda na kushuka kuashiria anashusha pumzi ili aongee kitu ambacho niliamini kabisa atakuwa ameguswa na maneno yangu.
"Sasa kama hakuna haja ya wafuatilia basi Farida na Faimu nao wamependana haina haja ya wafuatilia waache na mapenzi yao na pia usitegemee nitaumia kwa jinsi kaka yangu anavyolazimisha kupenda kwa Farida ikiwa hatakiwi. Tena ukirudia tena nitongoza kwa njia hii nitakushtaki kwa kaka ili amuambie Hamis wakujue tabia yako ambayo waifanya kwangu" Ndiyo maneno yaliyotoka kinywani kwa Ally baada tu ya kumuambia kuhusu hiyo habari hadi nikawa najiona kama nimepungua umri na umbo kutokana na maneno yake  jinsi alivyoniumbua.
Nilikubali kwa Ally nimeshindwa kwa  siku hiyo labda nijaribu kwa mbinu nyingine kabisa tofauti na ile ili niweze kumpata kwani alinivutia sana, niliamua sasa kwenda kuifanya njia yangu ya pili ya kwenda kumuambia Hamis ambayo ilifanikiwa  kwa kiasi kikubwa sana kwani alichukizwa sana na kusikia Faimu ana mahusiano na dada yake na taarifa hiyo ilifikishwa kwa Shafii na mipango hiyo ya kwenda kwa mganga ili kumkomoa Faimu ndipo ilipoanza".
Salma aliweka kituo kikuu katika kusimulia kwake na hadi muda huo mzee Buruhan alikuwa akimtazama kwa hasira sana kutokana na kuujua ukweli wa tabia yake, watoto wake nao walioneshwa kuwa na mshangao hasa wa tabia aliyokuwa anafanya mama yao kwani hawakutegemea kama ataweza mambo kama yale.
Upande wa Bi Farida baada ya Salma kumaliza kusimulia kilichompata tayari hasira dhidi ya shoga yake kipenzi zilikuwa zipo juu na mawazo ya urafiki nae yalikuwa yameshatoka kichwani mwake, alimtazama wazi kwa macho yaliyojaa chuki kuu  iliyoongezewa na machozi yenye uchungu kutokana na masikio yake kupata hiyo habari ya kuwa rafiki yake aliyempenda na kumuamini amekuwa akimzunguka kwa miaka mingi bila ya yeye mwenyewe ingawa alimuamini sana na kumthamini.
Ama kweli kikulacho kinguoni mwake kama waliozaliwa toka awali walivyonena na rafiki yako ndiye adui yako kama ambavyo waliozaliwa toka walivyotoa maana ya msemo wao huo waliounena, ama kweli rafiki anaweza  akawa siyo rafiki kama ambavyo Salma alivyokuwa akifanya kwa Farida haikustahiki aitwe rafiki kwani kafanya yasiyostahiki kufanywa na anayeitwa rafiki kwani ni usaliti  mkubwa sana alioufanya.
Baada ya kisa hicho mhusika wa aliyeita hapo familia zote ambaye ni mzee Mahmud alikuwa akimtazama kila mtu aliyepo eneo hilo katika uso wake ili kujua hali zao zipo vipi waliposikia simulizi hiyo, alizungusha shingo yake iliyozungukwa na ngozi iliyofunyaa kwa kila mmoja aliyepo eneo hilo huku akiwa mithili ya mtu anayechambua fikira za mtu zilizomo  ndani ya ubongo wake na mwishowe akayatuliza macho kwa rafiki yake kipenzi wa  tangu, ujana na hadi wanazeeka pamoja. Mzee Mahmud alimtazama rafiki yake hadi alipobaini katambua kama anamtazama ndipo akafungua kinywa chake, "mzee mwenzangu umesikia mambo ya watoto wetu hayo? Je una lolote la  kusema kabla sijaendelea na kinachofuata?"
Mzee Buruhan alipoulizwa hilo swali alimtazama Shafii kwa umakini kisha akamuuliza, "Shafii hivi Farida ni nani yako?"
"ni mke wangu baba" Shafii alijibu akiwa ameinamisha uso wake chini kutokana na aibu aliyonayo kwa baba yake  baada ya mabaya yake kubainika.
"Kwa kigezo kipi Farida mkeo we mwana? Aliridhia kwa moyo wake wakati unaenda kutoa posa au kizizi chako ulichokichukua huko Maforoni ndiyo kilimfanya aridhie?" Mzee Buruhan aliongea kwa ukali wa wastani na kusababisha Shafii atazame chini kwa aibu kutokana na kitendo alichokifanya kwani kilikuwa cha aibu sana tena amekieleza mbele ya watoto.
"Wajukuu samahanini sana kama nitakuwa nimekosea  na pia nitakuwa sijaongea kauli nzuri kwa mujibu wa maadili yetu mbele yenu nyinyi. Ila lazima niseme ukweli juu ya hili, alichokifanya huyu ambaye ni mjomba kwa wengine na pia ni baba kwa mwingine ambaye yupo hapahapa ni sawa na kumuingilia mwanamke akiwa amelewa hivyo ninaona alikuwa anabaka na hayupo katika ndoa. Sina la ziada mzee mwenzangu"  Mzee Buruhan aliongea maneno yaliyozidi kumuumiza Shafii na pia kumtia sibu mbele ya mtoto wake pamoja na wapwa zake, maneno hayo yalimfanya Zalabain azidi kuwa na hasira na mama azidi kulia kwani alikuwa amekosewa haswa na kosa kubwa lenye kujaza maudhi tele kwa kiumbe yoyote mwenye uhai na aliyejaliwa akili na matamanio.







               SURA YA TISA

   Mzee Mahmud naye alisikitika sana hulu akimtazama Shafii na Salma kwani alijua fika wamefanya ujinga mkubwa sana ambayo utawafanya waumie na wajute kwa muda mfupi tu na hawatapata bahati ya kuusafisha ujinga huo tena katika dunia hii kwani wakati wake ulipita wakati jambo hilo wanalifanya. Walikuwa wamepoteza muda wao mwingi katika matumizi mabaya yasiyofaa na walifanya kosa pasipo kusahau kubwa hawataweza kulisahihisha tena hilo kosa, kwani muda wake ulishapita tayari hivyo matumizi yao mabaya ya muda wao kipindi cha nyuma ndiyo yalimfanya mzee Mahmud awasikitie kila akiwaangalia.
Giza nje ya eneo hilo lilikuwa tayari lishaumeza mwangaza mdogo wa muda wa magharibi ambao waliukuta kipindi wanaingia eneo hilo, nuru yote ilishapotea tayari na kiza kizito kikawa kimelimeza eneo lote kwa nje kutokana na uwepo wa miti na mapori katika eneo la jirani na hiyo nyumba. Majira hayo yalimfanya mzee Mahmud aendelee na utaratibu aliouweka kwa haraka ili usiku mnene usiwakute wakiwa eneo  hilo, na kutokana na msjira hayo ilimbidi aseme "Shafii sasa endelea kusimulia ulipoanza mahusiano yako na Farida hadi mnaishi kwa pamoja".
Sauti ya mzee Buruhan ilifika mapema zaidi hata ya  robo sekunde tu tangu azungumze katika masikio ya Shafii ambaye naye alinyanyua kinywa chake na kusimulia, "Baada  ya Farida kuwepo katika mikono yangu na kuwa msichana nilikuwa nikikutana naye kimwili kupunguza mihemko ya ujana na pia nilifanya hivyo ili tu nikija kumkosa niwe tayari nimeshatumia mwili wake kwani hilo ni jambo la fahari sana kwa kijana kama mimi, sikuwa na imani na dawa hizo na niliamini dawa  niliyomfanya anipende itaisha tu kutokana na kiwewe cha kupendwa ghafla na sikuwa ninaamini kabisa kama nitakuja kuendelea kukaa naye. Nilianza kuingiwa na imani ya kuendelea kukaa naye baada ya Hamis kunishauri nipeleke posa nyumbani kwao nimuoe moja kwa moja kuliko kusababisha mimba mapema, jambo hilo nililikubali kwa mikono miwili na nikaona hiyo ndiyo njia inayofaa ili kumfanya Farida awe wangu kabisa na hata kama Faimu akija kujua ajue tayari amemkosa Farida na si mali yake tena. Kwa mara ya kwanza katika ujana wangu nilijivika ujasiri na kumueleza  baba yangu juu ya suala hili na yeye alifurahishwa na uamuzi wangu wa kwenda kuposa akiniambia tayari nilishakuwa mkubwa na hilo ndiyo jambo la maana nimeamua kama kijana anayejitambua, baba yangu alienda kumueleza mzee Jumanne ambaye ndiye baba mzazi wa Farida ambaye aliridhia kwa mikono miwil hilo suala kutokana na utiifu nilionao kwake hapo kijijini. Taarifa hiyo ilipelekwa kwa Farida ambaye alikubali na furaha yangu ikazidi na hapo ndipo nikazidi kuamini ile dawa ya mganga ambaye ni baba mzazi wa mzee Sauti ya radi ilifanya kazi na inaendelea kufanya kazi na wasiwasi wa kumoksa Farida sikuwa nao kabisa, baada ya muda mfupi baba yangu aliweka kila kitu sawa ndos ikafungwa  na tukayaanza maisha yetu katika nyumba ya baba yangu iliyokuwa ipo shambani kwake huku wazazi wa pande zote mbili wakituahidi kututafutia makazi yaliyobora kwa ajili yetu.  Maisha yetu na ndoa na Farida yalikuwa ya furaha kwa kipindi cha mwaka wa kwanza na katika kipindi hicho nilikuwa tayari nishaanza kufanya shughuli ili nipate kipato  kwa ajili ya familia yangu na mke wangu maisha yetu yaende mbele, mwaka wa pili wa ndoa yetu ulipoingia Farida alianza kuweweseka usiku na alipoamka asubuhi alikuwa mchovu sana  hali iloyozidi kunipa wasiwasi sana na ikanilazimu niende kwa baba mzee Mahmud akanipa dawa ambaye nilimpatia dawa ambayo ilimsaidia Farida sana akawa hapatwi tena na hali hiyo, baada ya Farida kupona hilo tatizo haikupita hata muda mrefu akashika ujauzito ambayo ulinifanya niwe na furaha  sana na hata wazazi wa pande mbili walijawa na furaha baada ya kuwapa taarifa hiyo. Furaha ya wazazi  baada ya Farida kupata ijauzito ilionekana wazi baada ya kutupatia zawadi iliyotufurahisha zaidi, wazazi wa pande zote  mbili walijenga nyumba kubwa hadi ikaisha bila sisi kutambua na walikuja kutukabidhi baada ya  kuwapelekea taarifa ujauzito na wakatuambia ndiyo sehemu ya pekee itayotufaa kuanzisha familia yetu. Nyumba yenyewe  ndiyo nyumba hii ambayo tumo wote hivi sasa ambayo ilitufanya mimi na mke wangu kuhama kule kijijini na kuja kuishi  hapa Mpirani nikiwa na mdogo wangu Ally, tuliyaanza maisha mapya kwa furaha sana na mdogo wangu Ally tayari alikuwa yupo shule ya msingi akiwa yupo ukingoni kumalizia elimu hiyo.
Miezi tisa ilipitimia Farida alijifungua mtoto wa kiume mwenye afya nzuri ambaye alizidi kuongeza furaha ya ndoa pamoja na furaha ya wazazi wetu ambao walikuja kututembelea na wakapata bahati ya kumuona huyo mtoto aliyelepekea furaha yetu izidi, mtoto huyo tulimpa jina la Jamadin ambalo ni jina la babu yangu mzaa mama ili jina hilo zuri lisiweze kupotea bila kupatikana mrithi  wake ndani ya dunia hii kama ilivyo kawaida ya jamii zetu kurithisha watoto wao majina ili tu jina liwepo na liendelee kuwepo. Jamadin alikuwa ni mtoto mchangamfu sana na  aliyefanya familia yetu  iwe na furaha kuputiliza, matendo yake ya tangu utoto yalikuwa ni yenye kufurahisha na ndiyo maana familia yetu ilizidi kuwa na furaha. Kipindi hicho tayari Ally alikuwa ameshamaliza elimu ya msingi na alikuwa anasubiri majibu ili aweze kuendelea na elimu ya sekondari ambayo ilikuwa ikionekana na hadhi kubwa kama mtu akiisoma, muda huo wa kusubiri majibu ndiyo muda ambao Ally alikuwa akiutumia kucheza na Jamadin hadi akawa amemzoea sana kuliko hata mimi niliyekuwa nashinda kwenye mihangaiko Makorora na kurejea nyumbani jioni sana. Baada ya mwaka mmoja kupita tayari Ally alikuwa sekondari na ndugu zangu wengine wote walikuwa wapo Tanga mjini tukifanya shughuli pamoja baada ya kuoa kila mmoja, furaha ya kuwa karibu na ndugu zangu ndiyo ilizidi maradufu kwani kazi tuliifanya kwa umoja na kuzidi kujiingizia kipato kwa ajili ya familia zetu ambazo  zilitegemea sana uchapaji  kazi wetu ili ziweze kujipatia chakula na mahitaji mengine muhimu. Kipindi hichi ndiyo Hamis naye alikuja kuungana nasi baada ya kumuoa Salma na alipata nyumba ya kukodisha Usagara  akakaa huko na tukawa tukifanya kazi pamoja, miaka miwili baadaye Ally akiwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Usagara ilibidi tumuhamishie nyumbani kwa Hamis ili awe karibu na shule asome vizuri. Tuliendelea kuchapa kazi kwa kipindi  hicho hadi tukawa na mafanikio kidogo yaliyoniwezesha kuhama Mpirani nikaja kuishi Chumbageni baada ya kuweza kukodi nyumba nzuri iliyoniwezesha kukaa vizuri na familia yangu. Ally alimaliza kidato cha nne alikuja kuungana na sisi Chumbageni na kuifanya familia yetu iwe na furaha zaidi kwani Jamadin alikuwa amekaa karibu  na Ally mtu anayeelewana naye sana.  Mwaka huo aliomaliza Ally kidato cha nne ndiyo mwaka ambao mambo yalibadilika kwa nna ya kustajabisha sana, vitega uchumi vyetu vilianza kuyumba na kupungua katika namna ya kustajabisha sana hadi ikafikia tukawa na kitega uchumi kimoja tu ambacho nacho kilitekea na moto katika mazingira ya kutatanisha. Hali hiyo ilitufanya tuanze kufanya kazi kama waajiriwa ili tuokoe familia zetu na tuweze kusogea hatua kadhaa kimaendeleo, tulifanya kazi na kulisha familia zetu pamoja na kulipa pango la nyumba na hakukuwa na pesa  nyingine yoyote iliyobaki tuseme tutatumia kuanzisha shughuli nyingine. Mambo yalipoanza kuzidi kuwa mabaya wote kwa pamoja tuliweka kikao nyumbani kwa Hamis na tukashauriana tuende kumuona mtaalam aliyetusaidia kumuondoa Faimu kijijini huenda akatusaidia cha kufanya ili tuweze kukomboka katika balaa hili, siku iliyofuata wote kwa pamoja tulienda Duga maforoni kwenda kuonana na mganga wetu aliyetufanyia dawa miaka kadhaa iliyopita. Safari hiyo ya kwa mganga ndiyo iliweza kubainisha tatizo la kukwama kwa mambo yetu, tulimkuta mtoto wake yule mganga ambaye ni Sauti ya radi ambaye alitutajia tatizo kubwa la kuharibika kwa shughuli zetu niliambiwa lipo kwangu na  tulihitaji utatuzi basi nikubaliane na sharti la kutoa kile kinachofanya kuwe na kssumba katika mipango yetu. Nakumbuka vizuri maneno ya mganga Sauti ya radi aliniambia, "mtoto unayelea ndiyo kikwazo cha kukwama kwa matatizo yenu na kama mkitaka mfanikiwe basi yule mtoto anatakiwa atolewe sadaka katika eneo alilozaliwa na baadaye utakuja kupata mtoto wa pili wa kike ndiye akikua utajri utazidi na hata wenzako watatajirika pia".
Kweli ilikuwa ngumu sana kukubali lakini nilipoelezwa juu ya nguvu kubwa za maajabu alizonazo yule mtoto kiasi kwamba ameweza  kutambua uchawi nilimuwekea mama yake hadi nikampata. Mganga alienda mbali akanitajia uajabu wa huyo kama siamini niende nikamkate kidogo mkononi mwake nijifanya ni bahati mbaya halafu niangalie kitakachotokea, siku hiyo nilirudi nyumbani nikiwa nimechanganywa na masharti ya mganga na nikaagana na wenzangu nikawaambia kesho tutajua cha kufanya kingine. Sikutaka kuamini mambo ya yule mganga nimtoe kafara mtoto wa pekee niliyekuwa naye wakati hata wa pili bado sijajaliwa, nilipingana na suala hilo lakini nilitaka nijaribu vile alivyoniambia mganga ili nione itatokea vipi. Majira ya alasiri siku hiyo nilikuja na mpira wa upepo wa ndani ya baiskeli nikawa na panda kipende cha mti kinatumika kutengeneza  manati, nilimuita Jamadin nikamuambia anishikie miandae mipira kwa ajili ya manati nataka kuipeleka shamba itumiwe na banu yake. Jamadin alinielewa mapema ingawa ndiyo kwanza alikuwa ana miaka mnne, alishika nilivyomuelekeza na nilianza kukata ule mpira wa baiskeli na nikajifanya nimekosea nikamkata na kiwembe na damu ilimtoka lakini alitulia kimya tu. Kitendo hicho kilinichanganua na nikajikuta naangalia pembeni nitafute walau kitambaa  nizuie damu isitoke, niliangaza macho pembeni nikakosa kitambaa na niliporudisha macho sehemu niliyomkata Jamadin nilijikuta nikishtuka hadi nikarudi nyuma kwa uoga. Jeraha lile nililomkata na kiwembe sikuliona na niliona hakukuwa na jeraha sehemu yoyote katika mkono wake, Jamadin yeye  alikuwa ananitazama kwa dharau tu nilivyokuwa natetemeka baada ya kutoona jeraha nililomkata na kiwembe.
"Uahajua ulichotaka jua?" Aliniuliza hivyo na nilipokaa kimya aliondoka bila kunisemesha chochote na hapo ndiyo ukawa mwanzo wa mimi kuanza kumuogopa yeye na pia nikajikuta nipo tayari kwa sharti alilonipa mganga Sauti ya radi. Siku iliyofuata nilienda kuonana na wenzangu mapema iwezekanavyo  na nikawaeleza juu ya kila kitu nilichokishuhudia na nilikuwa tayari kumtoa Jamadin kwani siyo mtoto wa kawaida, siku hiyo tulienda kwa sauti ya radi na tukaambiwa vitu vilivyokuwa vinahitajika kwa ajili ya kafara ya Jamadin. Ilihitajika jeneza dogo jeusi linalolingana na urefu wa Jamadin, damu ya mwisho wa mwezi wa mwanamke, chupa ya ujazo wa nusu lita yenye mfuniko na  kaniki nyekundu mita moja na visu saba.  Vitu vingine tuliambiwa  vitapatikana hapo kwa mganga na kafara hiyo ambayo ilipangwa kufanyika usiku wa kuamkia siku ya ijumaa ambayo ni keshokutwa yake na mikakati ya kumnasa Jamadin tuliambiwa ianze. Mganga Sauti ya radi alisema atatusaidia katika kumfunga  Jamadin asibaini kitakachokuja kutokea.  Baada ya kupewa hayo mahitaji wote tulienda kuyatafuta siku hiyohiyo ya jumatano na ilipofika jioni tulikuwa tumeshapata kila kitu, siku iliyofuata tulipanga mikakati ya kumnasa Jamadin katika mikono yetu bila yeyote kutambua ili twende tukamtoe kafara mipango yrtu ifanikiwe.
Ili kutimiza azma yetu ya mtoa kafara Jamadin tuliamua tumtumie Ally kwani ndiyo njia rahisi ya kumnasa Jamadin, siku hiyoida ya alasiri nilimuagiza Ally Makoroea kwa makusudi na Jamadin aliomba kwenda na nikamruhusu kwani  hiyo ndiyo njia ya kumnasa. Huko Makorora tulikuwa tumeandaa vijana wa kukodi waliokuwa wanatumia gari aina ya volkswagen tuliyomuazima tajiri mmoja wa jijini Tanga enzi hizo aliyeitwa Brown ambaye ni chotara kwa sasa ni Marehemu, tajiri huyu mwanae wa kiume ndiye alikufa kule Duga Maforoni wakati nyumba za kampuni ya Hamid  zilipoungua na pia mjukuu wake smbaye namtambua kwa jina la James alikufa mulemule. Vijana hao walifaniliwa kuwateka Ally na Jamadin na kuondoka nao ambapo njiani Ally alipigwa kisogoni akazirai akatupwa kando ya reli mita chache kutoka katika mzunguko wa Kwa Minchi majira ya usiku, kupotea kwa Jamadin na Ally nyumbani kwangu ilikuwa ni huzuni sana kwa mke wangu lakini kwangu mimi ilikuwa ni kawaida kwani nilikuwa najua kila kitu. Tulikusanyika nyumbani wanaume wote huku mimi nikionekana kulia sana na nilibembelezwa hadi nikanyamza ndipo tulipoanza kujadiliana kimaigizo nini cha kufanya, baada ya mjadala wanaume wote sita tulikubaliana tuongie mtaani kumtafuta Jamadin na Ally na wake wote wakakaa nyumbani kwangu wakimbembeleza Farida.



TUKUTANE KESHO KUHITIMISHA RIWAYA HII

1 comment:

  1. Baada ya kuona chapisho kwenye mtandao la Jenna kutoka USA akisema jinsi alivyosaidiwa na Dk. DAWN, niliamua pia kuwasiliana naye kwa msaada kwa sababu sikuwa na chaguo nilichotaka ni kumrudisha mpenzi wangu na furaha. Kwa mshangao mkubwa mpenzi wangu alifika nyumbani akiwa amepiga magoti kwamba nitafute nafasi moyoni mwangu kumsamehe, hakika nilistaajabu na kushtuka mpenzi wangu alipopiga magoti akiomba msamaha na mimi nimkubalie tena. Kweli nimepungukiwa na maneno, na sijui ni kiasi gani cha kukushukuru wewe Dr. DAWN. Wewe ni Mungu aliyetumwa kurejesha uhusiano uliovunjika, Na sasa mimi ni mwanamke mwenye furaha. mawasiliano yake ni Whatsapp +2349046229159
    dawnacuna314@gmail.com

    ReplyDelete