Tuesday, December 8, 2015

SHUJAA SEHEMU YA NNE





RIWAYA: SHUJAA

MTUNZI: Hassan O Mambosasa

SIMU:+255713776843...
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGI





  ILIPOISHIA

MASAA MAWILI BAADAE
KWENYE MBUGA YA KENYA WILD IMPALA

Mbuga hii iliyo jirani iliyo jirani na ziwa Victoria
kulikuwa na na handaki kubwa sana lililochimbwa
kilomita mbili kutoka ziwani, ndani ya Handaki hilo
kulikuwa na kundi la watu takribani sita wenye asili
ya barani Ulaya. Watu hao walikuwa wameizunguka
meza kubwa ya duara iliyotengenezwa kwa chuma,
meza hiyo ilikuwana urefu uliowafikia kiunoni mwao,
katikati ya meza hiyo kulikuwa na karatasi kubwa
lilioenea karibu meza nzima.

"nafikiri tutumie boti yenye uwezo wa kuzama kama
ilivyo Nyambizi" aliongea Obren ambaye alikuwa ni
mmoja kati ya watu waliokuwa wapo eneo hilo.

"ni njia sana nzuri, sasa tukatokee sehemu gani
iliyokuwa salama" aliongea mzungu mwingine kisha
akauliza swali.

" Calvin mbona rahisi hiyo, tutapita chini kwa chini
hadi katika pori la Rubondo lililopo katika kisiwa cha
Rubondo kisha hapo tutafanya mapumziko ya muda
kisha tutaendelea hadi Kagera" Campbel alijibu swali
hilo huku akielekeza kwenye ramani sehemu
wanazopitia.

"njia nzuri hiyo nadhani ramani itatusaidia kufika"
alisema Calvin

"ndio inasaidia na tukifika huko tutachukuliwa na
helikopta hadi kibaha halafu hapo tutakutana na
Tasi" aliongea Campbel.

"Obren, Calvin, Scott , Jameson na Christian
nadhani tupo pamoja sasa team mambas tuingie.
kazi!" alihitimisha Campbel kisha akanyoosha ngumi
mbele na kupelekea wenzake wote wanyooshe
ngumi na kukutanisha ngumi ya Campbel.

"kazii!" wote waliitikia kwa pamoja kisha wakatoka
kwenda kuchukua vitu vyao vya muhimu







 ENDELEA NAYO ILI KUPATA UHONDO ULIOMO NDANI
YAKE





SEHEMU YA NNE
Baada ya dakika kadhaa wote walirejea wakiwa
wamevaa mabegi ya mgongoni yenye rangi ya kahawia,
wote walielekea kwenye ngazi zilizopo ndani ya
handaki hilo zilizowapeleka mpaka sehemu yenye
bwawa kubwa lililotengenezwa kwa namna ya
kuvutia. Ndani ya bwawa hilo kulikuwa kuna boti ya
kisasa yenye rangi ya kijani ikiwa imeegeshwa
pembezoni mwa bwawa hilo, hadi muda huo tayari
walikuwa wameshafika jirani na boti hiyo ili
kujiandaa kuingia ndani yake. Waliingia kwa pamoja
ndani ya boti hiyo kisha wakaenda kuketi kwenye
viti vilivyomo humo ndani.

"anza safari" Campbel alimwambia nahodha wa boti
hiyo aliyekuwa yupo katika usukani mbele yao.
Nahodha wa boti hiyo alibonyeza kimojawao
miongoni mwa vitufe vingi vilivyopo mbele yake na
kupelekea boti hiyo ijifunike huku umbo lake likiwa
kama yai , alibonyeza tena kitufe kingine kisha
akashikilia usukani wa boti hiyo kwa mikono miwili. Boti
ilizama ndani ya bwawa hilo kuelekea chini kabisa
hadi lilipofika usawa wa bomba kubwa la duara
lenye uwezo wa kupitisha boti hiyo ambayo sasa ipo
katika umbile la nyambizi ya kivita ingawa ina umbo
dogo. Walipita ndani ya bomba hilo hadi kwenye mlango
wa kioo kuashiria ni mwisho wa bomba hilo. Hapo
nahodha alichukua simu ya kijeshi kisha akasema
"Captain B45 hapa. Tupo kwenye mlango, ninahitaji
ufunguliwe tupite". Alipomaliza kuongea alirudisha
simu sehemu yake kisha akashika kwa mkono
mmoja kwa nguvu huku mkono mwingine ukiwa
umeshika chuma kilicho na umbo kama gia ya gari.
Mlango wa kioo uliokuwa mbele yao ulifunguka
kupelekea maji yaingie huku nyuma ya boti hiyo
kukitokea kioo kingine kama cha awali kuzuia maji
yasiingie kwenye handaki, yule nahodha alisukuma
kile chuma kilicho na umbo kama gia ya gari na
kupelekea boti hiyo ianze kwenda kwa mwendo wa
kasi. Akiwa anatumia ramani iliyopo kwenye kioo
kilichopo chini ya usukani pamoja na dira iliyopo
mbele yake, aliweza kukiongoza chombo kuelekea
kusini magharibi mwa eneo walilolopo. Mwendokasi
wa boti hiyo uliwafanya wote waliomo humo ndani
watulie kutokana na kona kali zilizokuwa zikikatwa
na nahodha ili kukwepa miamba iliyomo ziwani.
Nahodha ilimbidi afanye kazi ya ziada katika
kucheza na usukani wa boti hiyo, hadi wanafika
kisiwa cha Rubondo tayari ilikuwa usiku wa manane
hivyo iliwalazimu kuinua boti juu ili wapumzike kwa
muda mfupi kisha waendelee.Waliifungua boti hiyi
ikawa wazi baada ya kuinua juu.

"kwanini tusiende kwenye kingo ya ziwa ile pale
tuka tukapumzike" aliongea Calvin huku akisimama
kwenye kiti chake baada ya kufungua mkanda

"unataka ufanywe kitoweo sio?" aliuliza Nahodha wa
boti hiyo.

"kivipi nahodha?" Calvin naye aliuliza

"hii sio bahari rafiki bali ni ziwa na kuna mamba
pembezoni mwake, sasa ukienda kule unajitafutia
kifo kwani wanakaa pembezoni" Nahodha wa
chombo chao alifafanua

"aaah! nafikiri ni kiumbe kidogo na hakitaweza
kushindana nguvu na mimi" Calvin aliongea kwa
dharau.

"rafiki ukae ukijua mamba wa pale ni wakubwa na
wenye uzito mkubwa sana, sasa suala kushindana
nao nguvu usijidanganye kabisa" Nahodha
alimwambia

"huyo hajui mamba zaidi ya kuwaona kwenye zoo
kawazoea kenge wa majini" Obren aliongea
kimasihara huku akicheka.

"ujue mamba wa humu ziwani wanafika urefu mita
sita na uzito wa tani moja, sasa kama unaweza
kushindana nao nguvu nikupe boti ndogo ya kujaza
na upepo uende" Nahodha alisema.

"aisee hao mamba wa Afrika kama ndio wapo hivyo
basi siendi, tupumzike hapahapa" Calvin kwa upole
huku akirudi kwenye kiti chake baada ya kusimama
kwa muda mrefu.

"sio mamba wa Afrika tu ndio wapo hivyo hata wa
dunia nzima ni wakubwa na uliowaona wewe ni
watoto, ushawahi kusikia ukubwa wa mamba aitwae
Lolong wa Ufilipino?" aliyepo jirani yake alimwambia

"ujue Scott yule mamba waliomkamata Wafilipino
nilijua ni wa uongo" Calvin alimwambia Scott

"sasa ndiyo ujue kuwa yule mamba ni wa ukweli na
haikuwahi kuonekana mamba mkubwa namna ile
kwa mujibu wa watafiti wa mambo ya wanyama"
Campbel naye alimwambia Calvin.

Walipumzika kwa
muda wa nusu saa huku
wakijadiliana mambo mabalimbali, mapumziko
yalipoisha nahodha alibonyeza kitufe na kupelekea
boti ijifunge kama awali kisha akawageukia wakina
Campbel.

"mikanda ni muhimu jamani" aliwaambia kisha
akabonyeza kitufe kingine na kupelekea boti hiyo
ianze kuzama taratibu, alikipeleka mbele kile chuma
kilicho na umbo kama gia ya gari. Boti ilianza
kwenda kwa mwendo mkubwa kama awali na
nahodha wake alizidi kuongeza umakini kuliko awali,
eneo lenye mawe mengi ndani ya ziwa hilo ndio
waliloingia na kupelekea nahodha akate kona kila
mara kuyakwepa mawe hayo. Hadi saa tisa usiku
inaingia tayari walikuwa wameshawasili Kagera
katika hifadhi ya Biharamulo iliyopo pembezoni mwa
ziwa Viktoria, kwa umbali wa mita kadhaa toka
kwenye kingo ya ziwa hilo kulikuwa na helikopta
kubwa ya kisasa aina ya AW139SAR ikiwa
imeegeshwa sehemu tambarare. Boti hiyo iliibuka
juu ya maji pembezoni mwa ziwa kisha ikajifuungua
halafu ikasogea hadi kando kabisa jirani na nchi
kavu, Campbel,Obren,Calvin,Jameson ,Scott na
Christian
ndiyo walioruka hadi nchi kavu kwa ukakamavu
huku nahodha akiwa amebaki ndani ya boti.
Kikosi hiki cha watu sita kilikimbia hadi ilipo
helikopta kisha kikaingia ndani pamoja na mizigo
yao, nahodha wa boti aliishia hapo kama wajibu
wake ulivyomtaka. Aliifunika boti halafu akaizamisha
ndani ya maji kama awali kisha akaondoka eneo
hilo, eneo ambalo boti hiyo iliibuka lilibaki tulivu
kama hakuna jambo lolote lilitokea.

"fungeni mikanda tafadhali" Rubani wa helikopta
aliwaambia vijana wa kazi aliotumwa kuja
kuwachukua ambao nao walitii bila kuweka walakini
wowote. Rubani alikinyanyua chombo chake kama
alivyotakiwa kufanya kisha akakiongoza kuelekea
mahali kilipotakiwa kuelekea, njiani watu wote
walikuwa kimya kusubiri mwisho wa safari ili
washuke. Mnamo alfajiri saa kumi na moja kasoro
helikopta hiyo iliwasili katika uwanja wa mpira
uliopo jirani na shule ya msingi iliyopo maeneo ya
kibaha, pembezoni mwa uwanja huo kulikuwa kuna
gari aina ya AUDI Q8 ikiwa imeegeshwa kwenye
kivuli cha mti wa mwembe. Pembeni ya mwembe
huo kulikuwa na range rover ya rangi ya kijivu.
Helikopta hiyo ilitua katika uwanja huo kisha milango
yake ikafunguliwa baada ya upanga wake kuacha
kuzunguka toka ilipozimwa, vijana sita wa kazi
walishuka wakakutana na Tasi akiwa amesimama
katika uwanja huo akiwasubiri

"karibuni" Tasi aliwaambia huku akiwapa mkono kila
mmoja.

"tushakaribia" Calvin aliongea kwa niaba ya
wenzake. Wote waliondoka hadi yalipoegeshwa
magari yaliyo jirani na uwanja huo kisha wakaingia
kwenye magari hayo, Tasi aliingia kwenye gari aina
ya AUDI Q8 akiwa na Campbel, Obren na Calvin
huku Jameson, Christian na Scott wakiingia kwenye
range rover wakiwa pamoja na dereva aliyekuja na
Tasi.
Msafara wa magari hayo mawili uliondoka uwanjani
hapo baada ya Helikopta iliyotua hapo uwanjani
kuondoka, msafara huu uliingia barabara ya
Morogoro kwa mwendo wa kasi ukielekea katikati ya
jiji.

****

Mnamo saa kumi na moja na nusu alfajiri Moses
alishtuka usingizini kama ilivyo kawaida yake,
aliinuka kitandani halafu akaelekea kwenye mahali
ilipo maliwato ndani ya chumba chake. Huko
alijisafisha vizuri kisha akatoka halafu akafanya
maandalizi kwa ajili ya shule, alipomaliza alitoka
hadi nje kwenye eneo la maegesho ya magari.
Aliingia kwenye gari analotumia kila siku kisha
akaliwasha, aliweka gia taratibu kisha akaachia breki
na kupelekea gari lianze kujongea kuelekea geti ambapo mlinzi tayari alikuwa ameshafungua geti ili
kuruhusu gari, akiwa amesimama pembeni ya geti
kama ilivyo kawaida yake.

"niaje kaka?" Moses alimsabahi mlinzi baada ya
kusimamisha gari alipofika usawa wa getini.

"poa dogo, za asubuhi?" Mlinzi aliitikia salamu huku
akimjulia hali.

"salama tu, hivi anko Kenne katoka saa ngapi
maana nimeona gari moja halipo"

"ametoka mida ya saa kumi alfajiri" Mlinzi alijibu.

"hakukwambia anapoenda"

"ameniambia anaelekea kazini kapata dharura"

"sawa kaka, wacha mi niwahi shule"

"poa dogo".

Moses aliondoa gari kwa mwendo wa kasi akielekea
barabara iendayo mtaa wa Warioba baada ya
kuagana na mlinzi wa nyumbani kwao..


 ****

Saa moja na nusu asubuhi walimu na wanafunzi wote wa shule ya Neema trust
walikuwa wamekusanyika katika eneo maalum la
kukusanyika wanafunzi kila siku asubuhi, haikuwa
kawaida kwa walimu wote kukusanyika hapo ifikapo
muda wa mstarini zaidi ya walimu wa zamu tu. Siku
hiyo shule nzuma ilikuwepo hapo kuashiria kuna
jambo muhimu na mkuu wa shule alikuwepo pia,
ratiba ya kila siku ya mstarini ilianza kisha mkuu wa
shule akasimama kuzunguka na wanafunzi wote.

"habari za asubuhi wanafunzi......natumaini wote
mmeamka salama na mpo na afya njema kama ilivyo
kawaida, dhumuni la kuwaita hapa ni kuwajulisha
juu ya ujio wa mwalimu mpya wa masomo ya Kemia
katika shule mwenye utaalamu wa hali ya juu katika
ufundishaji kutoka nchini Uingereza. Mwalimu huyu
atakuwa pamoja nanyi katika masomo hayo kwa
vidato vya nne, tano na sita kwa muda huu ambao
mwalimu wenu wa Kemia atakuwa likizo baada ya
kupata matatizo ya kifamilia. Napenda nimkaribishe
kwenu Dokta Jameson Share" alihitimisha mkuu wa
shule huku Dkt Jameson akisogea kusalimiana na
wanafunzi.

"habari za asubuhi wanafunzi na vijana wenzangu
kama mimi...........naitwa Dkt Jameson Share
nitakuwa nanyi katika masomo ya kemia katika
kidato vilivyotajwa na mkuu wa shule, hivyo
naombeni ushirikiano wenu kama wanafunzi" Dkt
Jameson alihitimisha na kupeleka shule nzima ipige
makofi.
Wanafunzi wote walitawanyika baada ya taratibu
zingine za hapo mstarini kuisha, waliingia
madarasani moja kwa moja kusubiri vipindi vianze.


 ****

Norbert Kaila ni mwandishi mashuhuri wa habari wa
nchini Tanzania pia ni mpelelezi wa shirika la EASA
(East Africa Security Agency) la Afrika ya mashariki,
kijana huyu alikuwa yupo katika pori la Hifadhi ya
Biharamulo kwa siku tatu zilizopita akifanya utafiti
kama mwandishi wa habari juu ya pori hilo. Kwa
muda wa siku tatu hizo alikuwa anaishi ndani ya
hema akiwa na askari mmoja aliyepewa na ofisi za
wanyama pori zilizo jirani na Hifadhi hiyo. Usiku uliopita
akiwa amelala katika hema lake alishtuliwa na ujio
wa helikopta katika pori hilo, ujio wa helikopta hiyo
ulimpa hamasa ya kutaka kujua ni nini kinaendelea.
Hivyo alitoka katika lake lilipo umbali wa mita
takribani mia tatu toka ilipo helikopta hiyo. Alitembea
kwa tahadhari hadi katikati ya miti iliyo jirani na
eneo hilo akiwa na kamera yake ya kipelelezi tofauti
na kamera yake ya kawaida. Ajibanza
hapo hadi aliposhudia ujio wa boti mfano wa
nyambizi iliyofika hadi ukingoni, hadi hapo aliweza kuoiga
picha kila anachokiona kwa msaada wa mwangaza
uliotoka katika taa ya helikopta na taa ya boti. Hadi
watu sita wanashuka kwenye boti ile alikuwa
amewaona na amewapiga picha, boti hiyo pia
alikuwa ameiona na ameipiga picha pia na helikopta
aliipiga vizuri akilenga namba zake zilizopo ubavuni.
Alipomaliza alibaki palepale hadi walipoingia ndani
ya helikopta kuondoka, na ile boti ilipozama chini.
Hapo alirudi kwenye hema kisha akajilaza pembeni
ya msimamizi wake kama ilivyokuwa awali. Hadi
asubuhi inaingia alikuwa macho na jua
lilipochomoza alikusanya vitu vyake kisha
akaondoka porini hapo akiwa na msaidizi aliyepewa.


 MZEE WA KAZI KAZINI




ITAENDELEA!!

No comments:

Post a Comment