Thursday, June 23, 2016

SHUJAA SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA

RIWAYA: SHUJAA


MTUNZI: Hassan O Mambosasa

SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA!
Taarifa ya kutoonekana kwa binti yake aliitoa upesi katika kituo cha polisi na suala hilo likaanza kufanyiwa kazi upesi, hadi saa tano usiku inaingia Mzee Bernard hakuwa amelala na wala hakuwa amekula kutokana na suala hilo. Alikuwa yupo nyumbani kwake na kundi kubwa la maaskari walikuwa wakifanya mahojiano na familia yake, mitambo ya kipolisi iliunganishwa na tarakilishi baada ya juhudi zote kugonga mwamba na zoezi la kutafuta mahali simu ilipo kwa kutumia GPS  (Global positioning system) ndiyo likafuata baada ya askari wa jeshi la polisi kubainishiwa simu ya Viktoria ilikuwa imeunganishwa na GPS.


"Hii hapa tumeipata kubwa" Askari aliyekuwa anashughulikia kutafuta simu kwa tarakilishi alisema kwa sauti kubwa, kila aliyesikia suala hilo alikimbia kwenye kioo cha tarakilishi ya jeshi la polisi.

****

"Msitu wa Mabwepande ndipo ilipo hiyo simu, nahitaji vijana wa haraka wa kwenda huko huenda ndipo alipotekwa" Askari mmoja alizungumza kumuambia mwenzake aliyekuwa yupo pembeni.
"Sir" Yule askari aliitikia huku akitoa saluti halafu akachukua simu ya upepo akatoa maagizo mara moja kituoni. Baada ya kutolewa kwa maagizo kituoni  msaskari waliendelea kumtia moyo Mzee Bernard kuhusu suala la kutafutwa mtoto wake lipo mikononi mwao na litashughulikiwa haraka ieezekanavyo. 
  Baada ya dakika kadhaa Inspekta John aliingia hapo nyumbani kwa mzee Bernard akiwa na sare za kazi, maaskari wote walimpigia saluti kwa kuwa ni mkubwa wao kisha wakatoa maelezo yao hadi walichokigundua juu ya kuonekana eneo ambalo simu hiyo ipo.
"aisee sasa sikilizeni inabidi mimi niende huko ili nikaungane nao nyinyi bakini hapa na msicheze mbali na Tarakilishi hiyo endeleeni kudodosa kila kitu na ikiwezekana mfanye mahojiano na mlinzi aliyemuona wakati anatoka ili tujue tutaanzia wapi, anzeni kazi sasa hivi tunaelewana?!" Inspekta John alitoa maagizo kisha akaondoka mara moja baada ya maagizo yake kutiliwa maanani na maaskari hao.

****
 
Ni afadhali hali ilivyokuwa kwa mzee Bernard na mkewe baada ya kutoonekana kwa Victoria jambo ambalo ni tofauti na kawaida yake, hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Beatrice maana kila kukicha alikuwa haishi kulia kutokana na suala hilo, alimpenda sana dada yake na kumkosa ilikuwa ni pigo kubwa sana kwake. Alilia kwa muda mrefu hadi akapitiwa na usingizi baada ya kichwa kuanza kumuuma, alikuja kushtuliwa na mlio wa simu ambayo aliipokea kwa pupa baada ya kumjua anayepiga hiyo simu ni nani.
"Moses dada yangu mimi weee!.......Dada kapotea Moses hajulikani ni wapi alipo na hata simu yake inapigwa inaita tu......Moses inauma sijui dada yangu kawakosea nini jamani.......sawa mpenzi............sitamuambia dady.........sawa baby love you too" Beatrice aliongea na Moses kisha akakata simu baada ya kuambiwa maneno yaliyomtia moyo kidogo, alitoka chumbani kwake akaenda sebuleni walipo wazazi wake na maaskari ambapo alikuta mlinzi wa getini akihojiwa juu ya kupotea kwa Victoria na yeye alitoa maelezo yote juu ya jinsi alivyoondoka na mtu aliyeondoka naye siku hiyo.
"unasema alifuatana na Annie na kila mtu alikuwa kwenye gari lake, hebu mpigie simu Annie aje hapa nyumbani haraka iwezekavyo tuweze kupata walau chochote kitakachotuwezesha kupata mwanga juu ya pa kuanzia" Mzee Bernard alitoa wazo ambalo liliafikiwa mara moja na maaskari.
"lakini Baba Vic huoni sasa hivi muda umekwenda na atakuwa yupo kwao, si wangeenda maaskari kufanya mahojiano naye huko nyumbani kwao ili tujue anachokijua yeye au na yeye amekumbwa na mkasa huu" Mama Beatrice alitoa wazo ambalo lilikuwa bora zaidi kuliko la mumewe na maaskari ndiyo walilitilia mkazo, muda huo taarifa ilitolewa kituoni na maaskari ya kuhitajika maaskari wengine wakafanye mahojiano na Annie nyumbani kwao kama akiwepo.
Askari aliyekuwa anacheza na tarakilishi naye alikuwa yupo kwenye kufanya kila linalowezekana kwa kutumia tarakilishi hiyo iliyofungwa mtambo maalumu hapo nyumbani kwao, muda huu askari huyo alikuwa akiitafuta namba ya Annie na alipoipata alishusha pumzi.
"Annie yupo salama nyumbani kwao" Aliwaambia maaskari wenzake pamoja na Mzee Bernard na familia yake.
"Tusubiri majibu ya hao askari wenzetu walipenda kufanya   mahojiano naye huko nyumbani kwao"Askari mwingine alipendekeza na kuungwa mkono na wote waliomo hapo kasoro Beatrice tu ambaye alionekana yupo makini na simu muda huo akiandika.
"Samahani mzee hivi ushawahi kuwa na ugomvi na mtu au kukosana na kijana yeyote kisa huyo binti" Askari mwingine aliyekuwa amekaa kimya muda wote alimuuliza mzee Bernard swali ambalo lilionekana halina maana kwa maaskari wengine ila kwa mzee Bernard lilikuwa na maana kubwa na likamkumbusha jambo ambalo alishalisahau kabisa.
"Nimekumbuka kitu hapa" Bernard alisema kisha akasafisha koo lake na kukaa vizuri akasema, "kuna kijana mmoja alishawahi kuwa na mahusiano na Victoria wakati akiwa akiwa shule na nilipokuja kubaini nilichukua jukumu langu kama baba na kijana huyo alipelekwa nje ya nchi na wazazi wake na siku moja baada ya sikukuu ya kuzaliwa ya Beatrice huyo kijana nilimuona uwanja wa ndege akiingia hapa Tanzania kwa mara ya kwanza tangu alivyoondoka ili kutenganishwa mbali na Victoria kama nilivyowaambia wazazi wake".
Maelezo hayo yaliwafanya maaskari watazamane kisha mmoja akauliza, huyo kijana anaitwa nani na ni mtoto wa nani?"
"Jina kusema kweli simtambui ila ni mtoto wa Gerald Geofrey huyu mwanasiasa" Mzee Bernard alitoa maelezo hayo yaliyowafanya askari wabaini kitu.
"Nahisi huyu kijana ndiye muhusika mkuu wa hili tukio" Mzee Bernard aliongezea.
"Mzee ukisema hivyo kisheria unakuwa na makosa kwani huna ushahidi wa kumtuhumu moja kwa moja kuhusu habari hii. Wacha tufanye uchunguzi wetu tutabaini nani ni muhusika wa hili sakata" Askari alimuambia Mzee Bernard

****

Wakati askari hao wakiendelea na kazi nyumbani kwa akina Beatrice katika hali ambayo hawakuitambua ni kwamba maongezi yao na hata mikakati yao vilikuwa vikisikiwa vilivyo upande mwingine na Moses ambaye alikuwa ameweka spika ya simu baada ya Beatrice kupiga simu na kuiacha ikiwa hewani wakati maongezi hayo yakiendelea. Pia alikuwa akiyarekodi kwa kutumia mfumo wa kurekodi uliokuwa kwenye simu yake hadi pale simu ilpokatika.
"Mtoto wa Gerald Godfrey aliyekuwa masomoni nje ya nchi, hebu ngoja" Moses alijisemea kisha akachukua simu yake ya mkononi akabonyeza baadhi ya namba akaiweka sikioni akaongea baada ya simu kupokelewa, "Phil eti yule mtoto mzee Gerald Godfrey aliyekuwa nje karudi hata miezi minne hana anaitwa nani?.......eeh! Huyohuyo......nitumie namba yake we si unajuana na mdogo wake....poa poa nimekupata" Moses alikata simu kisha akachukua madaftari akaenda kusoma.

****

    MSITU WA MABWEPANDE

Magari mawili ya polisi yaliyotoka katikati ya jiji la Dar es salaam yalisimama mbali kidogo na ulipo msitu kisha askari wenye silaha wakiongozwa na Inspekta John wakashuka wakawa wanaelekea upande ambao walikuwa wakielekezwa na askari wenzao waliopo nyumbani kwa mzee Bernard kwa njia ya simu. Askari hao walifika eneo ambalo ndiyo simu ya Viktoria ilipo wakakuta gari ambalo alilitumia Viktoria wakati anatoka nyumbani kwao likiwa lipo pembeni ya barabara linawaka.
"Wote wekeni silaha zenu tayari kwa lolote, na tunasogea kwa kulizunguka hilo gari tena kwa umakini" Inspekta John aliwaambia wenzake kisha akachomoa bunduki yake ya kisskaro aina ya revolver kiunoni akawa anasonga mbele mahali lilipo hilo gari tayari kwa lolote. Walipolikaribia wote walijificha wakasubiri kwa dakika kadhaa na walijitokeza baada ya kuona kupo kimya kisha wakalisogelea hilo gari bunduki zao zikiwa tayari kwa lolote.
Askari mmoja mwenye mipira ya kuvaa mkononi alifungua mlango na wengine wakaweka silaha zao tayari kwa lolote, mngurumo wa gari pamoja na kiyoyozi ndiyo vitu pekee vilivyowalaki baada tu ya kufungua mlango wa gari hilo ambao ulikuwa wazi.
"Wamelitelekeza gari hili sasa nyinyi kagueni gari lote kisha mchukue alama za mkono kama zitapatikana na ushahidi" Inspekta John aliongea.
"afandee!"Maaskari waliitikia na kuanza kupekua gari hilo mara moja wakiwa na vifaa maalum na mikononi wamevaa mipira, baada ya zoezi kukamilika walipeleka kila kitu walichokikuta kwa Inspekta John ikiwemo mkoba wa Victoria. Pia walipata alama za mikono zilizokuwa zipo kwenye pochi hiyo na usukani wa gari.
"Vizuri sana sasa mmoja aendeshe hilo gari  kuelekea kituoni atangulie mbele si tunafuata" Inspekta John alitoa maelezo hayo na maaskari wote walitii amri na msafara ukaanza mara moja kurejea mjini.

*****


      GUHO WAREHOUSE
            BUNJU
        DAR ES SALAAM


     Msafara wa magari mawili ulionekana ukiingia ndani ya eneo la Guho warehouse na kisha magari mengine mawili yakafuatia na kutimia msnne, watu waliogawanyika makundi mawili tofauti walishuka ndani ya magari hayo na wakaingia ndani ya ghala hilo. Watu hao waligawanyika makundi mawili vilevile wakakaa meza moja mkabala kwa kila mmoja, upande mmoja ulikuwa una sanduku kubwa la hela na upande mwingine ulikuwa na mzigo mkubwa uliokuwa upo ndani ya begi kubwa lenye matairi.
"mzigo?" Upande wenye sanduku kubwa la hela uliuliza.
"pesa?" Upande wenye begi kubwa la matairi nao uliuliza.
"fungua mzigo tuuone" Upande wenye pesa uliamuru
"fungua pesa tuzione" Upande wenye mzigo nao uliliamuru.
Wote kwa pamoja wakafungua kuhakikisha kama kila kitu ni halali kisha wakabadilishana, halafu viongozi wa misafara ya kila upande wakapeana mikono na hapo ndipo mchezo mchafu ulichipuka mithili ya mche unavyochipukia ardhini. Upande uliopokea mzigo uliwanyooshea bunduki watu waliopokea pesa ghafla na kisha sehemu zilizojificha za ndani ya ghala hilo wakaongezeka watu wengine wa ziada, watu waliokuja na mzigo na walijikuta wamewekwa kati baada tu ya kupokea pesa na kundi walilotakiwa kufanya nao biashara.
"nadhani mnatambua kabisa Komredi na Gotta hufanya zaidi kazi ya kuongeza kipato bila kutumia chochote na huwa tunafyeka wote tunaofanya nao biashara na kuchukua mizigo yote kama tunavyofanya kwenu hivi sasa. Buriani nyote" Mmoja wa vijana waliokuja na pesa ambaye ni kijana wa Komredi aliongea kwa majigambo huku akizunguka kila pande, kisha akajiandaa kufyatua risasi kuwaangamiza wote lakini alijikuta akipigwa risasi isiyojulikana ilitokea wapi na mlio wa bunduki aina ya shot gun iitwayo spac-12 ndiyo ulisikika. Moshi mzito ndiyo ulifuatia   hadi watu wakawa hawaonani na ulipokuja kuisha eneo walilosimama watu waliopokea pesa ambao walitakiwa wauliwe lilikuwa tupu na mfuniko wa shimo la chini ya ardhi ndiyo ulionekana upo wazi.
"Hakikisheni hawatoroki hao watu kwa namna yoyote ile, wafuateni humo chini walipoingia" Mmoja wa vijana wa Komredi aliongea kisha wengine wakisalia wakaondoka eneo hilo, wengine waliingia ndani ya mfuniko huo kuwafuata maadui zao.
Vijana wa komredi walioingia kwenye sehemu ya chini ya ghala hilo waliwatafuta maadui zao hadi wakajikuta wametokea sehemu nyingine iliyokuwa na mlango sehemu yenye shamba ambalo lilionekana kutolimwa kwa muda mrefu. Eneo walilotokea walikuta alama za matairi ya gari yanayoonekana dhahiri kuwa kuna gari lilikuwepo hapo muda si mrefu.
"shit! Wamekimbia tayari ingawa biashara imekamilika tusepeni hukuhuku kurudi kule itakuwa ni gundu" Mmoja wao alisema na wenzake wakakubaliana naye na wakaondoka eneo hilo.


****


      SIKU ILIYOFUATA
         


     Kutokana na habari ya huzuni iliyowakumba wanafamilia wa Mutashobya, marafiki wa karibu wa Beatrice pamoja na mpenzi wake walikuja kumuona hapo nyumbani kwao ili asijihisi mnyonge. Wanafunzi baadhi anaosoma nao Beatrice hadi muda huo walikuwa hapo nyumbani, Beatrice alikuwa ni mtu mwenye huzuni muda wote hadi pale alipomuona Moses kidogo ndiyo  kidogo akafarijika. Sebule ya nyumba hiyo ilijaa marafiki zake waliokuja kumuona, uhuru wa kutosha kwa marafiki hao ulikuwepo kwani mzee Bernard hakuwepo na mkewe alikuwa kajifungia chumbani. Muda wote huo Beatrice alikuwa yupo karibu na Moses na hata maongezi yalipokuwa yanaendelea alikuwa amemuegea Moses begani akiwa na uso usio na furaha
"Mose vipi mbona bibie kanuna huyo?" Hilary alitia utani wakati maongezi yakiendelea.
"Furaha ipo karibu utanunaje hivyo" Irene naye aliongezea ilimradi Beatride arejewe na furaha.
"shiiiiii! Subirini kwanza" Moses alisema na wote walinyamaza na mlango wa kuingilia sebuleni ulifunguliwa na Mama Andrew akiwa ameongozana na Andrew na Annie aliingia akasema, "hamjambo"
"Hatujambo shikamoo" wote waliitikia na Mama Andrew na wanae wakaketi, muda huohuo Mama Beatrice akafika hapo sebuleni.
"Karibuni jamani" Mama Beatrice aliwaambia
"asante za hapa"Mama Andrew alinyanyuka akakumbatiana na Mama Beatrice na Annie akakumbatiana naye huku akilia machozi ya uongo. Kilio hicho kilimfanya Mama Beatrice alie na akawa anabembelezwa na Mama Andrew huku Annie akizidisha kilio na kumfanya mama yake abembeleze wote wawili. Beatrice naye hakuweza kustahimili kuona kilio cha mama yake naye akaanza kulia kama vile kulikuwa na msiba na akawa ameegemea kifua cha Moses huku akilia kwa uchungu, Moses ilimbidi ambembeleze Beatrice bila hata kujali uwepo wa Mama yake karibu.

   Kubembelezwa kwa Beatrice na Moses ilikuwa ni sawa na mkuki mziti uliochoma moyo wa Andrew na Annie, ingawa Annie alikuwa akilia kilio cha uongo alijikuta akilia kweli na ikawa ni kazi ya kubembelezwa na mama yake na Beatrice ndiyo kwanza alizidisha kulia kila alipomuona mama yake analia kwa uchungu.  Chanzo cha kulia sana kwa Beatrice Moses alikigundua haraka iwezekanavyo na ikambidi ampe ishara  Hilary na marafiki wengine wote waende nje ili angalau asimuone mama yake anavyolia, kundi zima la marafiki wote wa Beatrice lliinuka na Moses naye akainuka akiwa amemkumbatia Beatrice ubavuni akiwa bado anambembeleza wakaelekea nje huku wakiwaacha Annie na Andrew wakiumia kwa jinsi walivyokuwa pamoja. Beatrice, Moses na marafiki zao wengine walielekea kwenye bustani ya nyumba hiyo wote kwa pamoja, huko Beatrice alibembelezwa hadi akatulia.
"My queen dada yako ni mzima na atapatikana acha suala hilo lishughulikiwe na litaisha, usihuzunike sana. Sawa baby" Moses alimuambia Beatrice ambaye alikuwa kifuani mwake huku akichezea nywele zake, Beatrice aliitikia kwa kichwa akizidi kujiweka huru kwenye  kifua cha Moses huku akionekana kudeka kabisa.
"Yaani hapo mkate umekutana chai wenyewe umelainika" Irene aliongea kwa kumbeza Beatrice aliyekuwa anadeka kwa Moses.
"afuu wewe lione huko unaanza" Beatrice alimwambia Irene huku kiaibu kutokana  na jinsi alivyotaniwa.
"Shem nikuulize kitu" Mmoja wa marafiki wa Beatrice alimuambia Moses.
"Uliza tu" Moses alimtoa hofu
"hivi shosti yetu huyo umemlisha nini maana ingekuwa mwingine huyo asingenyamaza ila kwako katulia tuli kama maji mtungini" Rafiki wa Beatrice na kufanya wengine wacheke
"Afu Lucy" Beatrice alisema huku akiunda sura yenye hasira ambazo hazikudumu na akajikuta akitabasamu akalalia kifua cha Moses kwa kudeka.

 ****

Baada ya mama Beatrice kunyamaza Andrew alitoka nje kwenye baraza la nyumba ya akina Beatrice akawa anatazama bustanini na kupelekea kumuona Beatrice akiwa amekumbatiwa na Moses na marafiki zake wakiwa wapo jirani naye. Jambo hilo lilimuuma sana akajikuta anapandwa na hasira hadi akajishika kiunoni sehemu ambayo ameweka silaha yake.
"Ukijaribu kufanya upumbavu huo  utataka vita isiyoisha wewe dogo, una vita na mimi usijiongezee vita nyingine" Sauti ya Annie ya kawaida ilisikika vyema kwa Andrew na ikamfanya aache kufanya anachokifanya akageuka akatazamana uso kwa uso na dada yake akiwa na bilauri mbili za shurubati.
"Your dog, one day I'll kill him (mbwa wako siku nitamuua)" Andrew aliongea kwa sauti ya chini yenye jazba haswa.
"even your bitch I'll chop her head off then I'll kill you( hata mbwa jike wako nitakikata kichwa chake halafu nitakuua) Annie aliongea kwa sauti ya chini yenye dharau haswa.
 "Annie dada yangu alishakufa siku nyingi ingawa namuhadaa mama yangu mimi ni dada yangu ila ukweli wewe ni kahaba aliyekubuhu siyo dada yangu hivyo kukuua na hata kukunajisi kwangu sio jambo la ajabu" Andrew alizidi kuongea kwa hasira kwa sauti ya chini.
"ohooo! Kabla hujaninajisi mimu jua wewe utaf...... na vijana wangu kabla sijakukata vipandevipande. You are not my young brother ila namuhadaa mama yangu ajue wewe firauni ni kaka kumbe siyo. mixiuuuuuuu" Annie naye alimtupia maneno makali mdogo wa damu kisa tu vita yao inayotakana na penzi la Moses na Beatrice, baada ya maneno hayo Annie alimkabidhi Andrew bilauri moja ya shurubati kwa kumsukumizia halafu akaondoka kuingia ndani.
"When I catch I'll rape you then your death will be next( Nitakapokukamata nitakubaka halafu kifo chako kitafuata)" Andrew aliyamtaka maneno hayo wakati Annie anagusa kitasa cha mlango, maneno hayo yalimfanya Annie amuangalie Andrew halafu akamsonya kwa nguvu akafungua mlango akaingia ndani.

****

"He! Kulikoni mbona unasonya hivyo hadi humu ndani tunakusikia?" Mama Andrew alimuuliza Annie baada tu ya kuingia humo ndani na kumfanya Annie ashtuke ingawa hakuonesha kama kashtuka.
"mama huyo mwanao mimi dada yake ananigeza bibi yake kwa jinsi anavyonitania" Annie alilalamika kwa maigizo na kumfanya mama yake acheke.
"si mnataniana wenyewe wala sihusiki maana na wewe unamgeza babu yako mkiwa nyumbani" Mama Andrew akiongea huku akicheka.
"shoga wanao wanapendana sana inaonekana hadi wanataniana hivyo?" Mama Beatrice alimuuliza Mama Andrew
"yaani shoga hawa wanapendana sana hadi nikiwaona wanataniana na kucheka huwa nafurahi sana" Mama Andrew alijibu huku akitabasamu na Annie naye akatabasamu


*Mh! Usilolijua usiku wa kiza

*Kisa kulinda wawapendao






MWENYE KUIHITAJI RIWAYA HII HADI MWISHO ANAWEZA KUWASILIANA NA MTUNZI KUPITIA NAMBA ZAKE HAPO JUU KWA NJIA YA UJUMBE MFUPI TU WA MANENO NA SI KUPIGA. HUKO UTAIPATA YOTE.



KWA RIWAYA ZAIDI LIKE UKURASA WETU WA FACEBOOK AMBAO NI:




      Riwaya Maridhawa
       Riwaya Maridhawa
      Riwaya Maridhawa
       Riwaya Maridhawa
        Riwaya Maridhawa

No comments:

Post a Comment