Friday, November 27, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA KUMI

DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE





SEHEMU YA KUMI!!
Laiti kama wanadamu tungalipewa uwezo wa kuona yaliyojificha katika mioyo ya wenzetu basi Bi
Farida angeliomba talaka mapema sana lakini Mungu muumba hakutupa uwezo huo wa kuona yaliyo katika mioyo ya wenzetu ndiyo maana Bi Farida hakutambua jambo linalimtatiza. Ama kweli moyo wa mtu ni kiza nene zaidi hata ya giza nene lililotanda kwenye pori nene  katika usiku mnene, mungu muumba alikuwa na maana yake sana kutuumba wanadamu kwa kuficha yaliyopo mioyoni kwani hadi muda huo tayari wanadamu tungekuwa tushafarakana kama tungebaini yaliyopo kwenye mioyo ya wenzetu.


****

"ngoja nikuwahishe ndani mume wangu ukanywe zile dawa na upumzike" Bi Farida aliongea huku akianza kuburuza kiti cha matairi cha mumewe huku akiita, "Jamali! Jsmali!".
"naam!" Sauti kutoka ndani ya chumba kimojawapo ilisikika ikiitika.
"njoo unisaidie kumuweka kitandani mjomba wako" Bi Farida alimuambia yule mtu aliyemuita huku akikisukuma kiti cha matairi kuelekea chumbani kwake, muda huo Shafii alikuwa bado ameuma akiweka maumivu yake ya kuigiza ili azidi kumchota mke wake akili ajue ni kweli ameumia.
"Sawa shangazi nakuja sasa hivi" Sauti ya Jamal ilisikika kisha mlango wa chumba kimojawapo ukafunguka na akatoka kijana aliyefanana sana sura na Hamis kaka yake Bi Farida na shemeji yake Shafii, Jamal alitembea upesi akamfikia shangazi yake akachukua kiti alichokalia Shafii akaanza kukiburuza yeye kukiingiza katika mlango wa chumba kimojawapo ambacho kimejitenga sana na vyumba vingine ndani ya nyumba hiyo, alipoingia ndani alikiburuza kiti hadi mahali kilipo kitanda cha kisasa kilichotengenezwa kwa mtindo wa kipekee na kunakshiwa kwa mapambo mbalimbali. Jamali alipofika hapo alimbeba mjomba wake kwa uangalifu akamlaza kitandani halafu akatoka chumbani kwa mjomba wake upesi kutokana na heshima aliyonayo kwao ambayo haimpasi kukaa humo ndani muda mrefu kama alikuwa tayari amemaliza kile kilichomfanya aitwe.
Bi Farida alichukua dawa za kutuliza maumivu akampatia mumewe pamoja na maji, Shafii alizinywa hizo dawa kisha akajilaza huku akiuma meno vilevile na baada ya muda alijifanya kapitiwa na usingizi ili kutuliza wahka aliyokuwa nao mkewe juu  yake kwani wasiwasi ulikuwa mkubwa sana kila akimuangalia anavyouma meno kwa hasira. Bi Farida baada ya kumuona Shafii kalala alimfunika na shuka vizuri halafu akambusu usoni, alitoka chumbani akaelekea sebuleni akamkuta Jamali anaongea na simu ya mezani ambapo alipofika tu mpwa wake huyo alisema, "eeh huyu hapa ongea naye".
Jamal alimkabidhi mkonga wa simu shangazi yake kisha akaenda kukae sebuleni kwenye kochi, Bi Farida alichukua mkonga wa simu akauweka sikioni na kuongea " ndiyo ni mama yake hapa.......hapana hajarudi nyumbani tangu muhula wa masomo ulipoanza.......nyinyi mnasema tulimtuma mtu aje kumfuata sisi hatukutuma ingawa ni kweli kulikuwa na matatizo huku nyumbani.....sawa toa taarifa ya kutoonekana kwake nyumbani wala chuoni".
Baada ya kuongea hayo maneno kwa njia ya simu aliikata simu kisha akaanza kulia kwa sauti ya chini kutokana na taarifa aliyopewa, Jamali aliinuka akaenda kumbembeleza  shangazi huku akimuuliza jambo lililomfanya alie.
"Jamal binamu yako hajaonekana chuo tangu siku ile ya msiba wa wajomba zako na huko chuoni kwao walikuja watu wakasema wametumwa na baba Zayina kumfuata arudi kwa ajili ya msiba jambo ambalo siyo la kweli kabisa" Bi Farida alieleza huku akilia kwa uchungu sana.
"Shangazi usilie sasa inabidi wewe ndiyo upange mkakati wa kumtafuta  kwani mjomba hali yake ndiyo hiyo unaiona na hii taarifa akipewa itamletea matatizo zaidi, naamini Zayina yupo salama tu na hajadhurika hivyo tuanze kumtafuta haraka iwezekanavyo bila hata kumuhusisha mjomba"Jamal alimuambia shangazi yake.
"Jamali mwanangu mimi jamani, sijui wamemkosea nini mpaka wamafanyie hivyo. Oooh! Yarrabi nisaidie mimi" Bi Farida alizidi kulalamika kwa sauti tofauti na awali.
"Shangazi sauti hiyo mjomba ataamka na asikie iwe mengine nafikiri unajua jinsi anavyompenda sana Zayina, hebu fikiria akiamka utamuweka katika hali gani kama akijua. Inabidi tutoe taatifa kwa wajomba wengine na baba  ila yeye tu asiambiwe ili wasaidie katika hili" Jamali aliongea kwa upole tena kwa kusihi hadi Bi Farida akatulia akawa anafuta machozi hadi aliponyamaza.
"Sawa nimekuelewa anko, ngoja nimpikie baba yako na shemeji Hassani ili tuje tujadili hili suala" Bi Farida alimuambia Jamali halafu akanyanyuka akaenda mezani alipoiacha simu yake ya mkononi akawapigia wahusika aliowahitaji katika kujadili hilo suala.

    Baada ya nusu saa Hamis na Hasaani walikuwa tayari wameshawasili nyumbani kwa Shafii na kikao cha watu wanne kikawekwa eneo la bustanini na wahusika wa kikao hicho wakawa ni Bi Farida, Hamis, Hassani na Jamali. Kikao kilianza kwa Bi Farida alifungua kikao kwa kueleza kils kitu juu ya taarifa aliyoipata kutoka kwa uongozi wa chuo kikuu cha Dar es salaam kisha akaeleza ushauri alioupata kutoka kwa Jamali wa kuwaita wao ili waweze kulitatua tatizo hilo.
"Umefanya vizuri sana mwanangu kwa kumshauri shangazi juu ya hili suala" Hamis alimpongeza Jamali kisha akaendelea, "dada hili suala kwa jinsi unavyolieleza ni zito sana na linahitaji tufikirie kwa kina haswa maana huyo mtu aliyemfuata Zayina akamwambia mnamuita nyumbani anajua nini anafanya na ametumia taarifa ya msiba huu kuwa ni njia ya kumnasa".
"Shemeji Hamis naungana na wewe  katika suala hili itakuwa huyu mtu ni adui namba moja wa kaka sasa inabidi huu msako tutume watu wenyewe wauendeshe kwani tukitumia vyombo vya dola itakuwa tunaharibu tu maana hatuwezi jua huyu mtu ana nguvu gani katika serikali. Kumbuka Zayina kusoma chuo kile tulifanya siri kwa wanafamilia tu kwani tunatambua mtu maarufu ana maadui sana ndiyo maana tukawaambia watu wengine kwamba Zayina anasoma Ulaya ili tuwapoteze njia ya kumtafuta, sasa tujiulize huyu mtu ana ni nani na ana lengo gani mpaka amejua Zayina alipo na akafanya hilo alilolifanya" Hassani naye aliongea kwa mara ya kwanza katika kikao hicho.
"Shemeji tayari mimi nishawaambia uongozi wa chuo kikuu cha Dar es salaam watoe taarifa juu ya suala hilo hivyo tayari lipo kwenye vyombo vya dola, sasa tufanyeje?" Bi  Farida aliongea
"Aaaah! Shemeji umekosea sana kufanya hivyo huoni huyo aliyemshikilia Zayina atazidi kuwa makini ili tusimjue" Hassani alimlaumu shemeji yake kwa kuwaambia uongozi wa chuo kutoa taarifa.
"Dada hapo umekosea sana kufanya hivyo kwani alichokuwa anaongea Shemeji hapa ni sahihi kabisa kukifanya katika suala hili kwani haitakiwi kuwashirikisha wanausalama inatakiwa tutumie pesa yetu mtoto apatikane" Hamis naye alimlaumu dada yake.
"Jamani nilikuwa nimechanganyikiwa haswa kutokana na kupokea taarifa hiyi, sasa tutafanyaje?" Bi Farida aliongea akionekana kutambua alichokifanya sicho katika kutoa taarifa ya kuwaambia uongozi wa chuo.
"Hukutakiwa kufanya hivyo dada" Hamis alimlaumu dada yake.
"Baba na mjomba hili suala limeshatokea na haliwezi kuwa halijatokea yaani tukubali Shangazi alikosea kuwaambia uongozi wa chuo kuto taarifa polisi lakini tusimlaumu kwa kufanya hivyo maana huo muda wa kulaumiana hamna, cha msingi ni kukaa na kujadili hilo  tufanye nini ili Zayina apatikane jamani" Jamali kwa mara ya kwanza aliongea baada ya kuwasikiliza wakubaa zake, maneno yake yalionekana kuwaingia mjomba wake na baba yake hadi wakakaa kimya kwa muda wakijifikiria halafu wakatazamana na wakapeana ishara ambayo hakuna yoyote aliyeiona.
"Sawa mwanangu nimekusikia tuachienu hili suala tulishughulikie naamini Zayina atapatikana ndani ya muda mfupi tu" Hamis huku baada ya kushusha pumzi, Hassan naye alikubaliana na maneno naye.
"nafikiri hili suala lipo kwetu na tutalifanyia kazi sasa naomba Kaka asijue juu ya hili" Hassani naye aliongea kisha akasimama pamoja na Hamis.
"Shemeji yupo wapi tukamjulie hali kidogo kwani kuja huku bila kumjulia hali si jambo jema" Hamis aliuliza
"Yupo chumbani kapumzika baada ya mgongo kushtuka, nafikiri atakuwa kashaamka twendeni mkamuone" Bi Farida aliwaambia  huku akinyanyuka kwenye akaelekea ndani, Hamis na Hassani walikuwa nyuma wakimfuata.
Wote kwa pamoja walielekea chumbani kwa Shafii ambapo walimkuta akiwa tayari ameamka.
"Karibuni jamani" Shafii aliwakaribisha
"Asante Chumbio" Hamis aliitikia ukaribisho huku akikumbushia jina la utani la Shafii, Hassani na Bi Farida wacheke.
"hilo jina husahau tu Bonoeza" Shafii naye aliongea huku akitia jina la utani la Hamisi nakupelekea wote wacheke humo ndani.
"Bonoeza siku hizi umelizoea si ulikuwa ukiitwa unarusha mawe kaka" Bi Farida naye aliongea huku akicheka na kupelekea wote humo ndani wacheke sana.
"Ila hilo jina umenikumbusha mbali sana niliwahi kumpiga mwenzangu tukichunga mbuzi kisa hilo jina, ila toka naingia kwenye ujana hadi utuzima naona kawaida tu" Hamis aliongea huku akicheka.
"Haya jamani ngoja niwaache na soga lenu la kiutuzima" Bi Farida aliongea kisha akatoka humo chumbani akiwaacha Kaka yake, mume wake na shemeji yake.
 Alipofunga mlango wa chumbani mwake mada ikabadilika papo hapo  na ikaongelewa mada inayowahusu hao wanaume watatu waliokuwa na ukaribu tangu utotoni, mambo yao mengi ya siri walikuwa wakiambizana na hata mengine mazito walishirikiana.
" kajua Zayina anashikiliwa na mbaya wetu ambaye bado hatujamtambua" Hamis alimuambia Shafii
"Natambua sana kama anajua hilo kwani wakati anaongea na simu sikuwa nimelala kama anavyofikiri na hata alipolia kwa sauti na kulalamika nikawa namsikia" Shafii aliwaambia.
"Hiii ni balaaa haswa inabidi tumtafute mtaalamu mwenye uwezo wa kudhibiti majini maana anayefanya haya si mwanadamu wa kawaida" Hassani aliongea.
"Hilo ndiyo la kufanya inabidi atafutwe mtaalam ila asiwe mzee Mahmud maana yule mzee atatuvua nguo tuaibike kwanza halafu ndiyo atusaidie maana tiba zake hufanya kazi ukiongea ukweli tu, sasa sisi hatuko tayari kuvuliwa nguo" Shafii aliongea
"Kweli kabisa bwana Shemeji ni bora kufa na matatizo yetu shingoni kuliko kukubali kuvuliwa nguo" Hamis alidakia  baada tu ya Shafii kumaliza kauli yake.
"Jamani hili suala tupiganeni hadi kufa maana wataalamu ni wengi hapa Tanga tena leo hii nimepata taarifa kuna mtaalam mwingine anaitwa Mafindo yupo Pangani nasikia huyo ni kiboko ninahisi ndiyo itakuwa mwisho wa matatizo" Hassani aliongea
"Enhee Hassani umenena haswa naona mkitoka hapa muanze huko au mnasemaje jamani na ningekuwa mzima ningeungana nanyi" Shafii aliafikiana na Hassani.
"Sawa naona tusipoteze muda bali twende huko ili mambo yasiwe mabaya" Hamis alisema kisha akanyanyuka akampa mkono Shafii na Hassani naye akafanya hivyo hivyo.
"Kila la heri jamani" Shafii aliwaambia kuwatakia heri katika mpango huo wanaoenda kuufanya, Hamis na Hassani waliondoka upesi ili wawahi kurudi kwani Pangani kulikuwa mbali na muda ulikuwa umeenda sana.





           SURA YA SITA
  Hali ya hewa ilikuwa ni tulivu sana na mawingu ng'amba yalikuwa yamepamba anga zima na kulifanya jua lisionekane kabisa na kuweka hali ya kivuli na kuwafanya wakazi wa jiji la Tanga kuwa na ahueni ya joto haswa kwa wale wanaotembea kwa miguu pembeni mwa barabara. Hamis na Hassani walikuwa wapo ndani ya gari binafsi wakielekea Pangani na muda huo tayari walikuwa wanaimaliza barabata ya Taifa wakiingia katika mzunguko wa magari unaounganisha barabara nne zikiwemo barabara ya Taifa, barabara ya Pangani, barabara ya jamhuri na barabara iendayo kukutana na barabara ya Chuda. Waliuzunguka mzunguko huo wa unaounganisha barabara hizo na wakafuata barabara ya pangani kwa mwendo wa wastani kutokana  na uwepo wa baiskeli nyingi zikiwa zimebeba wasafiri, walitembea kwa mwendo huo hadi walipofika jirani na duka la dawa la Mang'ombe. Hapo walijikuta wakiingiwa na moyo wa huruma na kusimamisha gari baada ya kijana mwenye asili ya kisomali aliyekuwa amevalia kinadhifu alipowapungia mkono kuwasimamisha, waliegesha gari pembeni na kijana huyo aliwaomba wamsaidie afike Pangani kwani alikuwa ameibiwa pesa yake yote ambayo ingemtosha kuifanya nauli ya kuelekea huko. Kijana huyo alikubaliwa kwa moyo mkunjufu kupanda gari hilo kutokana na moyo wa kusaidia watu alionao Hamis, alipanda kwenye gari akakaa kiti cha nyuma na safari ikaendelea kama kawaida. Njiani maongezi yalitawala kwenye gari hilo kutokana na ucheshi mkubwa aliokuwa nao huyo kijana ambao uliwavutia sana  kwani alitokea kuchangamsha safari yao isionekane imepooza, Hamis ndiye alikuwa dereva wa gari hilo na alionekeana kutendea gia za gari hiyo kwa kubadilisha gia moja na kwenda nyingine na mwendo wa gari aliuzidisha kutokana na uchache wa magari.
 Baada ya mwendo takribani saa moja wakiwa njiani mvua kubwa ilianza kunyesha na ikamlazimu Hamis apunguze mwendo  ili kuepuka ajali kwani mvua hiyo ilifanya kioo cha gari kiweke ukungu kwa ndani na kusababisha iwe tabu kuona mbele, ukungu ulipozidi Hassani aliufuta kwa kitambaa kilichopo ndani ya gari.
"Dah hili eneo kila nikipita huwa nakuta mvua" Yule kijana aliongea
"Labda ulipita kipindi cha mvua tu ila si  kila muda tu linakuwa na mvua, hivi unaelekea Pangani sehemu gani?" Haasani aliongea kisha akamuuliza swali huyo kijana.
"ninaelekea Kuani kumuona babu yangu maana ni muda sijamtembelea" Yule kijana alimjibu.
"Imekuwa kama bahati na sisi tunaelekea hukohuko sasa nafikiri utafika moja kwa moja hadi huko, si tunaenda kumuona mzee Mafindo nafikiri unamfahamu" Hamis naye aliongea huku akibadilisha gia ya gari.
"Said Humud au ukipenda gaza wa mafindofindo, ndiye babu yangu ninayeenda kumtembelea imekuwa kama bahati yaani ila bahati hii imeingia dosari" Kijana huyo alianza kuongea kwa uchangamfu hayo maneno yake lakini mwishowe akamaliza akiwa amekunja sura  na macho yakawa mekundu.
"Kijana unamaanisha nini?" Hassani aliuliuza huku akimtazama yule kijana lakini alijikuta na hofu zaidi baada yakuona sura ya yule kijana imebadilika na kuwa ya hasira"
"Unataka kuelewa siyo? Haya ngoja nikueleweshe" Yule kijana alisema kisha akajibadilisha sura na kuwa ya mtoto yule aliyewatokea watoto wa mzee Buruhan muda mfupi tu kabla hawajafa kwa kuuawa na mikono yake.
"Ushaelewa  au bado unataka uelewe zaidi" Yule mtoto alimuambia Hassan ambaye alipatwa na mshtuko sana baada ya kuiona sura ya yule mtoto.
"Jamadin! Hapana siyo wewe" Hassan alisema na kupelekea Hamis naye ageuke aangalie kwani aliona kama ameangalia vibaya alipotumia kioo cha kati, Hamis alijikuta akikanyaga breki ya gari lakini gari halikusimama bali ndiyo lilizidi mwendo.
"Hamuwezi kunikimbia nyinyi wanaharamu na huu ndiyo mwisho wenu" Yule mtoto wanayemtambbua kwa jina la Jamadin aliongea kwa hasira kisha akamuangalia Hassani akamuambia, "nipe kile ".
"Si....sina"Hassani aliongea kwa uoga huku akiweka mikono ishara ya kuomba msamaha lakini alijikuta akipigwa shingoni na mkono  wa yule mtoto hadi kichwa chake kikakatika na kuruka kwenye mapaja ya Hamis na damu zikawa zinatoka kwa wingi, Hamis alijikuta anatoa yowe la woga baada ya kichwa cha Hassani kutua kwenye mapaja yake hadi akajikojolea papo hapo.
"Mjomba leo ndiyo unakuwa na uoga siyo  wakati mlipokuwa mkifanya yenu wala hakuwa unaogopa, nadhani umetambua kuwa ubaya huzikwi nao bali  unalipwa hapahapa na leo ndiyo hukumu yako" Yule mtoto aliongea kisha akampiga Hamisi ngumi ya kichwa iliyotoboa kichwa chake hadi ubongo na mabonde ya damu yakaruka kwenye kioo cha mbele.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa Hamis na Hassan katika dunia hii baada ya kupatiwa malipo kwa kila walichokitenda kwani ndiyo mwisho wa yoyote afanyaye balaa kana walilolifanya wao, hakika mshahara wadhambi ni mauti kama wahenga walivyonena tangu zamani na ndiyo kilichowapata Hassani na Hamis.
Siku zote mchimba kaburi huingia mwenyewe ndiyo atafanikiwa kulichimba haitotokea mchimbaji wa kaburi akachimba kaburi na kulimaliza pasipo kuingia yeye mwenyewe, Hamis na Hassani hivyo hivyo ni wachimba kaburi waliochimba kaburi na wakaingia ndani yake na matokeo yake wakakutwa na kisanga kizito kilichosababishwa na uchimbaji wao wenyewe. Walichimba kaburi pasipo kujua kama kaburi  hilo litakuja kuwazika wenyewe na wamekuja kujua kuwa kaburi hilo ni kaburi lao wenyewe na wamekuja kujua tayari wameshachelewa, laiti wasingefanya hivyo tangu awali wangekuwa ni miongoni mwa waliosalimika hadi muda huo.



 ****


 Baada ya dakika takribani kumi tangu Hassani na Hamisi waiage dunia, hali ilikuwa shwari katika jiji la Tanga  na hakuna aliyekuwa na habari ya kutokea kwa tukio la kinyama katika barabara ya Pangani likiwahusisha watu maarufu waliouawa kinyama kutokana na kisasi kizito cha mabaya waliyoyafanya kipindi cha nyuma. Nyumbani kwa mzee Buruhan muda huo alitembelewa na rafiki yake kipenzi aitwae Mahmud ambaye anafahamika sana huko Mkinga kama mganga maarufu sana na aliyetatua matatizo mengi yaliyowakumba watu na familia zao na hata yenye utata. Mzee huyu alikuja kwa lengo la kumpa pole rafiki yake kipenzi kutokana na vifo hivyo kwani hakuwepo ndani ya Tanga kipindi msiba unatokea na ndiyo amerejea na ameamua kupitiliza nyumbani kwa rafiki yake moja kwa moja baada tu ya kupumzika nyumbani kwake. Mzee Mahmud alikaribishwa kwa utiifu na rafiki yakr kipenzi na akapatiwa kinywaji anachokipendelea kila awapo nyumbani kwake, alikaribishwa kahawa na rafiki yake huyo  kisha wakachukua bao wakaenda kwenye kibaraza cha nyumba ya mzer Buruhan wakakaa na wakaanza kucheza kama ilivyo kawaida yao.
"Mzee mwenzangu unajua kazi zetu  hizi za kuagua zilinitoa huku Tanga nilipozaliwa na kukulia hadi Mombasa nikaenda kumuagua bwana mmoja aliyetupiwa jini zito, basi hiyo shughuli ilinichukua mwezi na nusu na hadi namaliza huku mshazika ndiyo maana hukuniona" Mzee Mahmud aliongea huku  akiwa na kikombe cha kahawa mkononi.
"pole na majukumu mzee mwenzangu ndiyo kama nilivyokueleza yaliyonifika na hata sijui chanzo chake nini?" Mzee Buruhan aliongea kwa unyonge.
"haina haja ya kuhuzunika mzee mwenzangu bali inabidi uwalaumu wanao na janga hili mzee mwenzangu limeanzwa na wao na sasa mwenzao wanalimaliza" Mzee Mahmud aliongea kisha akanywa kahawa funda moja bila hata kumtilia maanani Mzee Burhan aliyeonekana kutoielewa kauli hiyo.
"Mzee mwenzangu mimi ni rafiki yako wa muda mrefu sana na kuhusu hili suala jua mwanao mkubwa analielewa fikra, na kama yupo tayari kuliweka bayana utabaki na nguzo tu lakini kama hataki kuliweka bayana hutabaki na nguzo hata moja" Mzee Mahmud alizidi kuongea maneno yaliyomfanya Mzee Buruhan  abaki akimtazama kwani anamtambua fika ni mganga mwenye uwezo mkubwa wa kujua yaliyojificha.
"Sijakuelewa mzee mwenzangu" Mzee Buruhan alisema huku akimtazama Mzee Mahmud kwa umakini, Mzee Mahmud alipotazamwa alitoa tabasamu tu kisha akasema, " zamu yako kucheza mimi nishalala mzee mwenzangu".
Mzee Buruhan aliacha kumtazama akaliangalia bao kisha akachukua kete akaanza kucheza huku akiwa njia panda kutokana na kauli ya Mzee Mahmud ambaye huwa hafafanui akishaeleza mambo kama hayo halafu akabadili mada ghafla.



ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment