Sunday, November 29, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA KUMI NA MBILI

RIWAYA: DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE


SEHEMU YA KUMI NA MBILI!!
"Asante  kiongozi wetu, mimi hapa
naungana na wazo alilolitoa mkuu wa majeshi la kwenda kuharibu utengenezwaji wa hao wadudu kwani sote tunatambua kwamba Dainun mpya imeibiwa na mpaka ije kupatikana hatujui
itatuchukua muda gani kwani hao viumbe wataingia ndani ya himaya hii mwezi ujao. Kumbukeni mwezi kwetu tunauona kama juma moja analoliona mwanadamu wa kawaida, sasa hamuoni hapo tutakuwa tumechelewa  na maafa yatakuwa yameshatufikia jamani" Mzee Zultash aliongea na viongozi wote wakamuunga mkono  hata yule waziri aliyetoa hoja ya kutafutwa Dainun naye alimuunga mkono.
"Kama ilivyo sheria yetu inavyosema, hoja ikiungwa mkono zaidi imepita. Basi jeshi la makomandoo litumwe kwenda kuharibu utengenezaji wa wadudu hao huku nikiwa naisaka Dainun kwani mwenye kuimiliki kashajulikana" Zalabain aliongea.




****


Kikao kilikwisha muda huo huo na maandalizi ya kikosi cha kuokoa himaya ya Majichungu yalianza mara moja, Kikosi kilichokuwa chini ya Salmin na mkuu wa majeshi ndicho kilichopewa jukumu zima la kuiokoa himaya hiyo. Vizuizi vya himaya hiyo vilifunguliwa na kikosi hicho kilitoka haraka sana na kisha vizuizi vikafungwa tena ili kuzuia himaya hiyo isivamiwe na maadui kwa ghafla, kikosi hicho kilitumia nguvu zao za ajabu za kijini kusafiri pasipo hata  kutumia usafiri wa aina yoyote  kama ilivyozoeleka kwa wanadamu wanapotaka kwenda mahali. Majini haya yalikuwa yakielea katika anga la chini ya bahari kwa kasi sana yakielekea upande wa kusini wa  himaya yao ambapo ni katika eneo lenye giza kubwa sana kiasi ambacho ingemlazimu mwanadamu wa kawaida kutumia mwanga wa aina yoyote kulivuka eneo hilo, lakini kwa hawa majini ilikuwa kawaida kwao kupita eneo kama hili bila kutumia nuru ya aina yoyote ile. Walipita eneo hilo lenye giza kwa mwendo wa kasi sana  hadi walipokaribia eneo lenye miti mirefu ambayo ilienda juu pasipo kuonekana mwisho wake ilibidi wasimame baada ya kupokea amri kutoka kwa Salmin baada ya macho yake kuwaka kwa nguvu halafu yakazima.
"sasa tunaingia pori la giza  linapakana na  mapango ya Zabakut ambayo ndiyo hutumiwa na  majini wataalam wa himaya  ya giza kutengeneza viumbe mbalimbali  kwa ajili ya kuangamiza himaya zingine, sasa basi katika pori hili kuna ulinzi mkali sana wa viumbe maalim waliotengenezwa mithilli ya miti ili kuwahadaa maadui wao wajue ni miti yote hii  halafu wawaue kabla hata hawajalivuka hili pori. Umakini wenu unahitajika kwani hakuna njia nyingine ya kufika kwenye mapango ya Zabakut zaidi ya hii kwani hii miti haina mwisho urefu wake hivyo hatuwezi kupita kwa juu, nadhani tumeelewana sasa tuingie tukiwa pamoja na si kugawanyika makundi" Salmin alihitimisha hapo akatoa ishara na kikosi chote kikaanza kuingia katika msitu huo kwa pamoja, walipoingia ndani ya pori hilo walipokelewa na giza nene zaidi hata ya lile walilolipita mwanzo na ukimya mkubwa sana ambao unatisha sana na laiti angehema mtu basi ungemsikia papo hapo. Walipita kwa umakini sana na kutembea kwao kulikuwa kwa umakini sana ili wasije wakaingia katika mikono ya maadui zao, walipofika katikati ya msitu mmoja wa wanajeshi wa kikosi chao aliyekuwa nyuma alitoa ukelele wa  maumivu uliovuma pori zima na kuwafanya wenzake wageuke kwa haraka


****


Upande wa nyumbani kwa Shafii ilikuwa tayari usiku umeshaingia na  Bi Farida alikuwa  yupo sebuleni akiongea   na Jamal, Shafii alikuwa yupo chumbani kapumzika muda huo kutokana na kunywa dawa kali sana ambazo zilimlazimu kulala usingizi mzito. Muda huo ndiyo ulikuwa muda ambao kidonda kingine kikubwa zaidi ya kile cha awali katika moyo wa Shafii kilijitokeza kwa namna isiyotarajiwa kabisa  kama ingeweza kutokea, muda huo tayari watumishi wa nyumba hiyo walikuwa wamelala kutokana na kuwa ni usiku sana. Mtumishi peke wa nyumba hiyo aliyekuwa macho ni mlinzi tu ambaye alikuwa bado alikuwa na kibarua cha kuilinda nyumba hiyo kwa muda wa usiku. Bi Farida akiwa anaendelea na mazungumzo na mpwa wake sauti ya maji yakimwagika katika  matanki yaliyopo nje ya nyumba hiyo kwa upande wa uani ilisikika, Jamali aliponyanyuka kwenda kufunga maji hayo Bi Farida alimuambia aache akafunge yeye kisha akainuka akaelekea ulipo mlango wa uani. Bi Farida alifungua mlango na akatoka nje  akakutana na mazingira tofauti na ya nyumbani hapo, aliona nje ya nyumba yake kulikuwa kuna giza lakini alipotoka nje katika baraza la uani aliona wingu jekundu limetanda juu angani na kufanya eneo lote liwe jekundu kama vile muda wa machweo ya jua. Alipoangalia katika ngazi za kushuka chini aliona rundo la viumbe waliovalia  mavazi ya maaskari wa zamani katika vita vya mapanga huko katika himaya roma wakiwa wamejipanga mstari na ngazi zilionekana na ndefu mno tofauti na zilivyo ngazi za baraza nyumbani kwake, hali hiyo ilimshtua sana na  na akaamua ageuze ili arejee ndani alipotoka akiwa  anapiga makelele ya uoga akimuita Jamali lakini alijikuta akikaa kimya  baada ya kuona mazingira ya mlango huo ni tofauti na mazingira ya mlango wa nyumbani kwake. Mlango huu ulikuwa wa dhshabu wenye mapambo mbalimbali ya kupendeza na mlangoni kulikuwana walinzi waliovaa makofia ya chuma  wenye kimo kirefu tofauti na Binadamu wa kawaida,  Bi Farida alijikuta anapiga kelele lakini mmoja wa walinzi alimnyooshea kidole na sauti yake ikakatika hapohapo ikawa haisikiki.
"Huyu mwanadamu anataka kutuzibua masikio sasa, yaani hajui kama sauti yake ni kubwa mno akiwa huku ndani ya himaya hii. Mchukueni nyinyi masikio yanatuuma sasa hivi" Mmoja wa walinzi aliongea kwa sauti nzito huku akiwa ameshika masikio kama ambavyo wenzake wote walivyokuwa wameshika masikio kutokana na kuumizwa na makelele ya Bi Farida, kauli ya yule mlinzi aliposema mchukueni hakuelewa anamaanisha nini na alikuja kuelewa  baada ya kujikuta amezungukwa na wasichana watatu wenye urembo wa hali ya juu ambao haikujulikana walifika vipi hapo hadi muda huo.
Akiwa anajiuliza swali hilo wale wasichana walimshika mkono na akajikuta akitokea katika mazingira mengine  akiwa   pamoja nao hao wasichana, alijikuta akiwa yupo ndani ya chumba chenye mapambo ya kila aina ambacho ukubwa wake kilizidi kumshangaza na kumfanya azubae akishangaa hadi pale alipoondolewa mshangao wake kwa kusikia sauti ya isiyokuwa ngeni masikioni mwake.
"Mama" Ndiyo sauti ya kike aliyousikia ikitokea nyuma yake ambayo ilimfanya ageuke atazame alipoitwa.
"Zayinaa!" Bi Farida alitamka akiwa anaonekana kutoamini macho yake kwa kumkuta Zayina eneo hilo akiwa amevaa mavazi ya kifahari na vito vya thamani na alikuwa akipepewa na  wanawake wawili wenye uzuri ambao haukuwahi kuonekana duniani na walikuwa na nywele ndefu na nyeusi kupitiliza.


****


Yule mwanajeshi mmoja aliyetoa ukelele katika kikosi cha kilichotumwa na himaya ya Majichungu alikuwa amezungukwa na mzizi mmoja  wa mti ambao ulikuwa ulikuwa unatambaa kama nyoka na kitendo cha kupiga  kelele ndiyo ikawa amechokoza nyuki waliofiwa na malkia wao na sasa hasira zote za nyuki zimehamia kwake. Mizizi ya ule mti ilianza kubadilika rangi na kuwa ua rangi sawa na uji wa volkano unaotoka baada ya mlima wa volkano kulipuka, mwanajeshi huyo wa kijini alijikuta akiteketea hadi akawa majivu. 
Kelele za yule mwanajeshi kabla hajafa  zilifanya eneo hilo la msitu lenye giza kuonekane macho yanayong'aa kama ya macho ya simba yakimulikwa na tochi gizani, macho hayo yalionekana kuwa mengi kila sehemu kuashiria kuna viumbe wengi ndani ya pori hilo walikuwa wamewaona na macho hayo yalizidi kusogea karibu kuashiria kuwa viumbe hao wanasogea karibu.
"Zaghari bekatu mudyosiye jikiteee, zaghari bekatu mudyosiye jikitee. Halkumisate  fadyozile gaitak( Washeni nuru za macho yenu muda wa mapambano huu, washeni nuru za macho yenu muda wa mapambano huu. Hakikisheni tunawamaliza tutizimize kazi)" Salmin alitumia lugha inayotumiwa na wanajeshi wa Majichungu pekee  ikitokea dharura kama hiyo, lugha hiyo haikuwa inafahamika na kiumbe mwingine yoyote isipokuwa wanajeshi hao.

Wote kwa pamoja waliwasha nuru ya macho yao  na kuwafanya waone pori zima kama mchana ingawa ilikuwa ni giza nene lipo porini hapo, hapo  waliwashuhudia viumbe wenye maumbo kama miti wakiwa na wanawaangalia na wengine tayari wakiwa wamewazunguka wakiwa na macho yaliyojaa hasira. Viumbe hao walianza kuwashambulia kina Salmin na kupelekea utokee mpambano mkali kwani hadi muda huo tayari kikosi cha Salmin kilikuwa kimeshajianda, viumbe waliopo msituni hapo walijikuta wakipigwa vibaya na  kikosi cha kina Salmin kwani nguvu zao ambazo waliamini wanazo wao peke yao walishangaa Salmin akiwa anazitumia baada ya kumgusa jini mojawapo wa himaya ya giza na kuzinyonya nguvu zake. Mpambano ulipowazidia  majini wa himaya ya giza mmojawapo alianza kukimbia ili akatoe taarifa ya uvamizi, jini huyo alikuwa ameshaonekana na Salmin ambaye alisoma mawazo yake akamjua lengo lake
Salmin alijigeuza mti  kama viumbe wengine kisha akatoa mzizi mmoja mtefu ulioenda kumfunga yule jini halafu akamuunguza kama alivyowaunguzwa  yule mwanajeshi aliyekuwa yupo upande wao, alirudi katika hali ya kawaida akaendelea kupambana  hadi walipowamaliza majini wote wa himaya ya giza ambao walilala chini kama miti iliyoangushwa katika ukataji miti.
Salmin alianza kuwapiga miale ya radi majini hao mmoja baada ya mmoja na wakabadilika wakawa na maumbo ya majini wa kawaida ambao walikuwa wamevaa sare moja, alimvua mmojawapo sare akavaa yeye mwenyewe kisha akawaamuru wenzake wafanye hivyo. Baada ya muda mfupi wote walikuwa na sare zinazofanana kisha wakasonga mbele kuuvuka msitu huo.


****


Bi Farida alienda kumkumbatia mtoto wake  kwa nguvu huku machozi ya furaha yakimtoka akiwa haamini kama angemkuta hapo, alijisahau kabisa kama yupo ugenini katika eneo asilolijua   na akajikuta akiwa na furaha ya kumuona aliyesadikika ametekwa.
"Nani kakuleta huku mama?" Zayina alimuuliza mama yake baada ya kuachiana tangu walipokumbatiana.
"mimi ndiyo nimemleta huku" Sauti ya Zalabain ilisikika kisha  akajitokeza akiwa ameongozana na mwanamke wa makamo aliyebeba chupa na beseni lenye rangi  ya fedha, Bi Farida  aliposikia sauti hiyo akageuka nyuma akakutana uso kwa uso na sura ambayo alihisi aliwahi kuiona mahali.
" we ni nani?" Bi Farida aliuliza huku akimkazia macho Zalabain.
"Kaka Jamadin huyo" Zayina alidakia kujibu na kumfanya mama yake ashangae kwani anatambua mwanae huyo alishafariki.
"Fanya kazi yako" Zalabain alimuambia yule mwanamke aliyekuja naye huku akiupuuzia mshtuko wa mama yake, yule mwanamke alimsogelea Bi Farida akampatia chupa aliyokuja bila hata kujali kama itapokelewa au haitapokelewa. Bi Farida aliipokea chupa hiyo akaifungua na akanywa kimiminika kilichokuwa kipo ndani yake hadi akamaliza, alimrudishia kile kichupa yule mwanamke na yule mwanamke akampatia beseni la rangi ya fedha alilokuja nalo.
Bi Farida alipolipokea hilo  beseni tu alijikuta akibanwa na kichefuchefu cha ajabu na akainamisha kichwa  humo ndani ya beseni akaanza kutapika vitu ambavyo vilimshangaza sana Zayina hadi  akageuza shingo pembeni huku akiwa kaziba mdomo, mwisho wa kutapika alitapika kitu cha duara chenye mizizi ambayo ilikuwa inachezacheza kuashiria kina uhai. Baada ya kutapika hicho kitu Bi Farida alizirai papo hapo halafu akazinduka baada ya sekunde kadhaa huku akihema kwa nguvu, alipoinua macho yake akamuona Zalabain na akajikuta akimuita, "Faimu".
"Hapana mama ni Jamadin mwanao" Zalabain alimuambia Bi Farida.
"Mwanangu Jamadin" Bi Farida aliongea huku akiinuka akaenda kumkumbatia Jamadin hadi Zayina akatokwa na machozi.
"Nafurahi mama umetoka katika kifungo kizito ulichokuwa umefungiwa, Zayina njoo na wewe" Zalabain alimuambia mama yake kisha akamgeukia Zayina aliyekuwa akiwatazama, Zayina alisogea akaungana nao katika kukumbatiana.


****


Baada ya kuwamaliza majini wa himaya ya giza waliowekwa kulinda katika eneo la pori hatimaye walilivuka pori hilo na wakatokea katika eneo la mbele la mapango ya Zabakut, walikuta lango la kuingilia katika mapango hayo  likiwa limefungwa na pembeni kukiwa na walinzi waliovalia sare kama walizovalia wao. Walitembea hadi kwenye lango hilo ambapo Salmin alitoa salamu ambayo hutumika na himaya hii na wenzake  pia wakafanya hivyo, walinzi waliitikia salamu hiyo kisha wakafungua mlango bila kujua wamewaingiza maadui zao ndani ya sehemu yao ambayo hutumika haswa kutengenezea silaha zao hatari na za maangamizi.
Salmin akiwa mbele aliwaongoza wenzake kuingia ndani ya mapango ya Zabakut, waliingia mpaka ndani na wakafuata njia iliyochongwa vizuri kama ukumbi mwembamba wa nyumba unaotengenisha ambao hujulikana korido na waswahili wazungu katika nchi ya waswahili.
Pembezoni ya ukumbi huo katika ukuta kulikuwa kuna  mafuvu ya binadamu yaliyokuwa yamepangwa safu  moja na yalikuwa yakitoa moto ambao ndiyo ulitumika kama muangaza wa humo ndani ya pango, walitembea hadi sehemu yenye makelele mengi wakakuta lango kubwa sana lililokuwa na mlinzi mwenye kichwa cha nyoka na mwili wa kawaida. Waliposogelea mlango huo yule mlinzi anyoosha mkono na ardhi ya mbele yao kina Salmin ikapasuka na kuacha bonde kubwa na uji wa volcano ukaonekana ndani ya bonde hilo, Salmin aliliruka bonde hilo hadi upande wa pili akamfikia yule mlinzi na kumgusa begani halafu akasogea pembeni.
"Toa utambulisho wako" Yule kiumbe alimuambia Salmin huku akijiweka tayari kupambana.
"Mikaf kama wewe" Salmin alimuambia yule.
"mikaf huwa tunauwezo wa kugeuza ardhi vyovyote, mbona nimepasua hiyo hukuiunga upite" Yule kiumbe alimuuliza Salmin swali ambalo hakulijibu na alijigeuza akawa na kichwa cha nyoka kama yule kiumbe  halafu akaiunga njia ile na kupelekea kiumbe yule atabasamu, wenzake walipita wakaja hadi pale alipo.
"Wafanyakazi wapya wa hazina hii, ni wataalam wamekuja kumalizia uundwaji wa silaha zetu" Salmin alimuambia yule kiumbe ambaye alifungua mlango akamruhusu aingie na wenzake akijua ni Mikaf kama yeye mwenye kugawa majukumu.
Mikaf ni majini wa himaya ya giza wenye uwezo wa kuongoza ardhi na udongo na kuupinda au kuufanya watakavyo, majini hawa katika himaya hiyo hufanya kazi ya usimamizi na ulinzi wa sehemu muhimu za himaya ya giza na hutambuana kwa kuoneshana nguvu zao tu. Salmin alivyofika jirani na yule Mukaf anayelinda tayari  alikuwa ameshaijua hulka yake kwa kutumia uwezo wa ajabu alionao, pale alipovunja njia aliruka juu na kumgusa begani ambapo alichukua nguvu zake kutokana na uwezo wake alionao na alipoambiwa ajitambulishe ndiyo akaiunga njia akiwa tayari ameuchukua uwezo wa yule Mukaf.

 Baada ya kuingia ndani ya eneo hilo kikosi cha Majichungu kiliona chupa mbalimbali zikiwa zimehifadhiwa wadudu wa ajabu wenye mabawa ambao walikuwa wakipiga kelele na kurukaruka, kila chupa ilikuwa imeungamishwa na fito za shaba maalum ambazo ziliingia kwenye mtungi mkubwa wenye kimiminika cha njano.
"wapo kwenye hatua ya mwisho ya ukuaji hawa, walikuwa wakitunzwa kwenye hizi chupa tangu watengenezwe sasa inabidi tumalize kazi yetu tuiokoe himaya yetu. Fanyeni kama nitakavyofanya" Salmin aliwambia wenzake kisha akaenda hadi kwenye mtungi mkubwa akaushika na wenzake nao wakamfuata wakafanya hivyo hivyo, alitoa miale ya radi mikononi iliyoingia humo na wengine nao wakatoa  miale hiyo.  Mitungi yote iliyowekwa wadudu hao ilipigwa na miale ya radi hadi wadudu hao wakafa wote na makelele ya wadudu hao yakaisha papo hapo kukawa kimya,  baada ya kumaliza kazi hiyo Salmin alitumia nguvu za mukaf akakanyaga ardhi ikafunguka akaingia na wenzake wakaingia na kutoroka eneo hilo baada ya kazi yao kukamilika.




      

              SURA YA SABA
         Mlio  wa maji kumwagika katika nyumba ya Shadii uliisha kuashiria kuwa koki  ya maji ishafungwa na maji hayaingii kwenye matanki yaliyojaa,  Jamali aliendelea kumsubiri shangazi yake atarudi kwa muda wa saa zima hakurejea na hapo ikamlazimu aende uani kuangalia huenda amekumbwa na tatizo kwani alikuwa hajamaliza kuzungumza naye na hakurejea ndani. Alifika hadi sehemu iliyokuwa na matanki ya  maji ambapo kama maji yakijaa na kumwagika basi hujulikana wa eneo hilo kulowana  hasa bustani ya maua ambayo imezunguka eneo lenye matanki ya maji, cha ajabu eneo hili lilikuwa kavu kabisa hakuna dalili ya kumwagika maji. Akiwa anashangaa hali hiyo alisikia sauti ya mjomba wake akipiga yowe la maumivu huko ndani na ikamlazimu kukimbia kuelekea chumbani kwa mjomba wake (muda huo Shafii anapiga yowe la maumivu ndiyo muda ambao Bi Farida alizirai kule kwemye himaya ya majini baada ya kutapika vitu visivyoeleweka).
Jamali alipofika chumbani kwa mjomba wake alimkuta akiwa ameanguka chini akiwa amekaukiwa na sauti, alimuinua na kumuweka kitandani  ambapo Shafii alionesha ishara ya kutaka maji kwenye bilauri yaliyppo humo chumbani mwake mezani na ikamlazimu Jamali amletee maji upesi. Shafii alikunywa maji yote kwenye bilauri ndiyo akaweka kuongea na neno la kwanza  kulitamka ni jina la mkewe, alipoona hamuoni mkewe alimuuliza Jamali mahali alipo shangazi yake. Jamali alimueleza kila kitu juu ya  kutoonekana kwa shangazi na maajabu aliyoyaona, hali  hiyo ilimshtua sana Shafii akabaki amechanganyikiwa.
"mpigie baba yako muambie aje hapa sasa hivi"  Shafii alimuambia Jamali huku akimuonesha simu ilipo, Jamali alienda kupiga namba ya baba yake lakini haikuwa inapatikana na alijaribu zaidi ya mara nne lakini jibu ni lilelile.
"Haipatikani"Alimuambia mjomba wake
"He...hebu mpigie na Hassan usipompata piga  nyumbani kwenu umuulizie baba yako" Shafii aliongea akionekana amepagawa  kabisa, Jamali alupiga namba ya Hassani ila matokeo yalikuwa yaleyale na ikamlazimu apige nyumbani kwao amuulizie baba yake.
"Anko nyumbani wanasema hajarudi tangu alipoondoka na anko Hassani"Jamali alimuambia Shafii huku akionekana kuchanganywa  na haliya mjomba wake.
"Etii?!" Shafii aliuliza kwa  nguvu halafu akazirai papo hapo kutokana na taarifa anazoambiwa, hali hiyo ilimchanganya Jamali na ikambidi awaamshe wafanyakazi wote wa nyumba hiyo na jitihada za kumuwahisha hospitali zikafanywa mara moja.


****


Shafii alikuja kuzinduka siku iliyofuata akajikuta akiwa yupo hospitalini amelazwa akiwa ametundikiwa dripu ambayo ilikuwa inakaribia kuisha, alipoangaza pembeni aliwakuta Mzee Buruhan, Mzee Mahmud na Mama Jamali mke wa Hamis wakiwa  wamezunguka kitanda chake.
"Faridaaa!" Shafii aliita jina la mke wake  kwa nguvu huku akijaribu kuinuka kitandani
"Shafii hebu tulia kwanza utasababisha  matatizo mengine tu" Mzee Buruhan alimuambia huku akimzuia asifanye fujo.
"Mama Zayina, Zayina mpo wapi?" Shafii alipiga kelele zaidi na ikabidi daktari aitwe mara moja ili kumtuliza, Mzee Buruhan na Mzee Mahmuf walimshikilia  Shafii hadi daktari alipokuja akamchoma sindano ya usingizi ndiyo ikawa ahueni.
Baada ya Shafii kulala mzee Buruhan na mzee Mahmud  walitoka pamoja na mke wa Hamis wakaenda kuka kwenye madawati ya kusubiria wagonjwa, baada ya muda mke wa Hamis aliondoka kwenda kufuata chakula kwa ajili ya mgonjwa akawaacha wazee hao peke yako.
"Kama nilivyokuambia mzee mwenzangu kuhusu huyu mwanao, awe mkweli ujue tatizo alilonalo ndiyo nitakubali kumsaidia" Mzee Mahmud aliongea.



*MAMBO MABAYA

*BI FARIDA MIKONONI MWA ZALABAIN


No comments:

Post a Comment