Saturday, November 19, 2016

WAKAL WA WAGIZA SEHEMU YA SITA



 RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA



    SEHEMU YA SITA!!
          "Ninja" Yule mzee alisema na Norbert akamtazama kwa tabsamu lisiloonesha furaha, yule mzee aliiruka meza kwa sarakasi akapambane na Norbert ana kwa ana lakini Sarakasi aliyoipiga
alipotua mitaa kadhaa toka Norbert alipo alijikuta akianguka chini moja kwa moja  baada ya kuhisi kitu kikitoboa kifua chake, alipoangalia eneo alilotobolewa alikuta kitu chenye rangi ya dhahabu ambacho kinafanana kwa kila kitu na vifungo vya Norbert.

     "Ulidhani sina silaha siyo,sasa pata dose ya kifungo changu hicho" Norbert aliongea huku akimuonesha yule mzee sehemu ya shati ambacho kifungo hamna,alikuwa ametobolewa na moja ya silaha hatari ambazo hukaa kama kifungo katika mashati ya majasusi kwa ajili ya tahadhari. Yule mzee alikichomoa kile kifungo  ambacho kilikuwa na ncha kali sana, ukungu ulitanda kwenye macho ya mzee huyo na hatimaye kiza kikatanda  kabisa.


****

       "Pongezi sana kwako nafikiri umejileta unieleze kile nilichokuwa sikijui" Norbert alimuambia yule mzee kwa dharau na hakujali kuwa yule mzee tayari alikuwa ameshatokwa na fahamu kutokana na kuchomwa na kile kifungo ambacho ni silaha ya kijasusi, sumu kali iliyokuwa ipo ndani ya kifungo hicho ilitosha kabisa kumpa usingizi mzee huyo ambao ndiyo sasa ameuanza. Norbert alimtazama mzee huyo kwa mara nyingine kisha akamsonya halafu akamsogelea hadi pale alipo akampekua kila mahali katika nguo alizovaa na sehemu mbalimbali za mwili wake, aliitoa simu ya mkononi ya yule mzee na hakuwa na kingine cha ziada zaidi ya hiko.

    Aliamua kuufuata ule mkoba aliokuja nao yule mzee akautazama sehemu ya kufunga kwa namba halafu akajaribu kuingiza namba za  kuufungua ule mkoba lakini ikashindikana, alisonya kwa nguvu kisha  akasogeza meza yake anayotumia ofisini humo na akafungua  sehemu ya marumaru ambayo ilikuwa ina sehemu ya kubonyeza ambayo aliibonyeza mara moja kisha akasubiri. Eneo la marumaru liliachana na kupelekea kuonekana na shimo  lenye ngazi zinazoenda chini ya ardhi, Norbert alimbeba yule mzee akaingia naye humo ndani ya shimo akaenda kumfunga kwenye kiti cha chuma kilichopo humo ndani ya shimo halafu akarudi akafunga ule mfuniko akarudisha meza mahali ilipokuwa awali.

   Alirudi akaketi kwenye kiti kisha akauchukua ule mkoba wa yule mzee kwa mara nyingine ili aufungue kwa njia isiyo rasmi baada ya ile rasmi kutofanya juhudi zozote, alichukua  chuma akaupinda mkoba huo ili aufungue lakini alikutana na kitu tofauti na alivyotarajia baada ya ule mkoba kufunguka kwa uwazi mdogo tu. Gesi nzito ilitoka ndaniya mkoba ule kwa ghafla ambayo ilivamia pua zake papo hapo na kumfanya akohoe autupe ule mkobe pembeni, alikohoa kwa nguvu na kisha nguvu taratibu zikaanza kumuishia na mwisho wake na yeye akaanguka chini.

     Ukungu mzito taratibu ulianza kutanda kwenye macho yake na alipolazimisha kufungua haikuwezekana kwa yeye kuweza kuona kama alivyokuwa anaona hapo awali, alijaribhu kusimama lakini ikashindikana na  akaanguka chini   mwili mzima ukaanza kuishiwa nguvu zaidi na akawa hawezi hata kunyanyua mkono wake. Muda huo aliweza kusikia mlango wa ofisi yake unafunguliwa kisha sauti za viatu vikikanyaga chini zikasikika kwa mbali lakini muda huo hakuweza tena kufanya chochote, giza zito lilianza kutanda kwenye macho yake kwa taratibu na hakusikia kitu kinmgine chochote kilichoendelea baada ya hapo.

     Kulowana kwa uso wake ndiyo kuliweza kumuamsha kwa nyingine na akajikuta kwenye mazingira tofauti na aliyokuwa awali wakati anapambana na mzee,alikuwa amemwagiwa maji na mtu ambaye hakumuona.  Mazingira ya eneo alilokuwepo baada ya kuamka yalizidi kumshangaza sana, yalikuwa ni mazingira yaliyojaa giza nene sana ambayo hakuweza kuyatambua kwa mara moja yalikuwa ni ndani ya eneo gani. Maumivu ya sehemu ya mwanzo wa viganja vyake kwa kila mkono ndiyo aliyoanza kuyasikia yakimletea fujo sana.

   Alifumbua macho akaangaza sehemu ya mkono wake ambayo inatoka maumivu hayo   akabaini alikuwa amefungwa kamba ngumu ambayo ilikuwa imefungwa katika vyuma viwili vilivyopo kila upande ndani ya  eneo alilopo, alipoangalia chini kwenye miguu yake alibaini napo alikuwa amefungwa kamba ngumu ambazo zilikuwa zimefungwa kwenye vyuma upande wa kushoto na kulia kama ilivyo mikono yake. Kwa mara nyingine alimwagiwa maji kisha mjeledi mzito ukatua mgongoni mwake ambao ulimletea maumivu sana baada ya kuichana ngozi yake, hakuweza kumuona aliyekuwa anamfanyia hivyo kutokana na uwepo wa taa moja tu iliyokuwa ikimmulika  zaidi usoni mwake kwa muda huo.

         "Norbert Kaila karibu kwenye himaya ya Panthers" Sauti kutoka kwenye spika iliyopo mahali hapo ilisikika vyema ikapenya vizuri kwenye masikio yake kisha taa yenye mwanga mkali ikawaka papo ikamulika uso wa Norbert, taa hiyo yenye kuumiza macho ilimfanya Norbert afumbe macho papo hapo na akainamisha macho yake chini lakini alijikuta akiinua macho yake juu baada ya mjeledi mwingine kutua kwenye mgongo wake.

          "Huwezi kutoka kutoka nje ya mawindo ya Panthers hata siku moja Kaila, jicho la Panther lilikuwa lipo karibu na wewe katika kila hatua yako. Ha! Ha! Ha! Ha! Finaly upo ndani ya mikono ya Panthers, you know what ulitakiwa ufe mapema kwa sumu ya Quantanise kama alivyokufa Bishop Edson na Muft Abdullatwiif lakini kwakuwa una jambo tunalolihitaji inabidi sasa ulieleze kabla ya kufa kwako. Ha! Ha! Ha! Ha! Welcome in the Cats kingdom feel at home Norbert" Sauti iliyosikika kutoka ndani ya spika ambazo Norbert hakujua ni eneo gani zilipo ilizidi kumkebehi na alipogeuza shingo kutazama kila upande ajue ni wapi inapotokea hakuambulia chochote zaidi ya giza tu  na taa kubwa ilikuwa ikimulika eneo lile alilokuwepo yeye tu.

            "Who are you? kama ni mwanaume kweli jitokeze, wanawake ndiyo wanajificha kutokana n auoga na aibu lakini mwanaume kamili anajitokeza wewe" Norbert aliongea kwa jazba yenye lengo maalum baada ya kusikia sauti ya aliyekuwa anamkera huku akiwa hamuoni mhusika, baada ya kuongea maneno hayo taa zote ziliwaka katika eneo hilo na kulifanya eneo zima lionekane vizuri kwa Norbert.

    Alijiona yupo ndani ya ghala kubwa la kuhifadhia bidhaa ambalo hakujua ni ghala gani, sehemu ya ghala hiyo ilikuwa ipo chini na iliyojichimbiwa ikiwa na ngazi maalum zilizoenda juu ambapo kulikuwa kuna korido ndefu kama ya kibarza cha ghorofa ikiwa imeznguka eneo lote alilokuwepo hapo chini. Juu kwenye hicho kibaraza ndiyo kulikuwa na milango sita ya kuingilia humo ndani ya ghala kabla hujashuka ngazi kwenda chini, vile vyuma viwili vilivyoifungwa kamba ambayo ilienda kufungwa kwenye mikono  na miguu yake alibaini ni greda ndogo mbili ambazo hutumika sana kwenda kubeba mizigo midogo bandarini ambazo mbele huwa na vyuma vidogo vilivyopangana kama chaga.

    Alipogeuza macho upande wa mbele yake aliona kundi la watu sita wakiwa wamevaa mavazi na vinyago usoni kama wanyama, wawili kati yao walikuwa wamevaa vinyago vinavyofanana na vya chui mweusi anayeitwa Panther kwa kingereza na wanne waliosalia walikuwa wamevaa vinyago vinavyofanana na chui  wa kawaida ambavyo viliwakaa vyema katika nyuso zao. Mmoja kati ya wale waliovaa vinyago vya chui wa kawaida alikuwa ni mwanamke ambaye aliweza kumtambua kutokana na umbile la kike alilonalo tena lenye mvuto ambalo lilionekana baada ya kuwa amevaa suruali iliyombana yenye rangi ya madoa kama chui.

           "Tumejitokeza sasa shida yako si kutuona tu haya sasa tupo hapa, we are Cats kingdom na wewe ni windo letu. You know what is next Kaila ukikamatwa na wanyama jamii ya paka kama sisi, ni kugeuzwa chakula chao tu. Au Panther nimekosea" Mmoja kati ya wale waliovaa vinyago vya chui mweusi aliongea kisha akamtazama mwenzake akamuuliza juu ya kauli yake.

           "Uko sahihi Panther mwenzangu lakini kabla ya kumgeuza chakula chetu inabidi atuambie ni wapi alipompeleka Lion tuliyemtuma aje kutembelea ofisi yake" Mwenzake alimjibu kisha wote kwa pamoja wakamsogelea Norbert karibu zaidi wakiwaacha wale waliovaa vinyago vya chui wa kawaida nyuma, walipomfikia walimtazama kwa muda wa sekunde kadhaa kisha wakatazamana wao wenyewe wakapeana ishara. Mmoja aliongea,"Kaila you know what kifo ni haki yako mbele ya Panthers hakuna anayeweza kupona kabisa but you have option, kufa kwa kistarabu au upasuliwe kwa hizo greda ulizofungiwa zikikuvuta mikono na miguu kwa kila upande zikuchane kabisa.  Pia utakufa kisrtarabu tu ikiwa utaweza kutuambia ni wapi ulipomuweka Lion  alipovamia ofisi yako, nina uhakika ulimtia mikononi ukambana kabla hawa Leopards hawajafika ofisini kwako na kukuokota. So tell me where is he?".

     Maneno hayo Norbert aliyasikia vizuri yakipenya katika masikio lakini alikaa kimya makusudi  kutokana na jeuri aliyonayo kisha akasonya huku akiwatazama wale Panthers, jambo hilo lilionekana kuwakera sana wale Panthers ingawa walicheka kwa nguvu sana kisha wakamtazama Norbert halafu wakisikitika.

          "Nafikri hujajua kwamba sisi huwa hatutanii tukiongea jambo, ngoja tukuoneshe demo kidogo I hope utasema mwenyewe" Panther mmoja aliongea kisha akawaonesha ishara wale wengine wanne waliovaa mavazi yanayowafananisha na chui wa kawaida, wawili kati yao waliingia kwenye magreda ambayo Norbert alikuwa amefungiwa kisha wakayawasha. Kuwashwa kwa magreda hayo hakukumtisha Norbertna ndiyo kwanza aliwatukana matusi makubwa kwa jeuri, kitendo hicho kiliwakera sana Panthers na waliwaamuru wale wayarudishe magreda hayo nyuma wammalize Norbert moja kwa moja.

     Magreda yaliaanza kutembea kwa taratibu yakivuta miguu na mikono ya Norbert kwa upande wa kulia na kushoto hadi Norbert akaanza kufumba macho kwa maumivu, maumivu yalipozidi Noebert alipiga kelele kwa maumivu na hapo ndipo hali ya usalama kwa watu waliomshikilia Norbert ikabadilika papo hapo na ikawafanya wote waruke pembeni kujificha kwa kila mtu upande wake.

    Mlipuko mzito ulitokea upande wa juu sehemu yenye milango ya kuingilia humo ndani na milango yote sita ilirushwa kwa ndani ikaaanguka hapo walipo, moshi mzito ulitanda eneo  hilo hilo huku milio ya bunduki ikaanza kusikika ikivuma humo. Si Panthers wala Leopards aliyeweza kusalia eneo hilo wote kwa pamoja walijibana katika sehemu wanazohisi ni salama kwao ili waweze kujilinda, milio ya risasi ilirindima karibia dakika tatu na ilipokoma kurindima ilisikika sauti ya bunduki isiyo na risasi ikilia baada ya kubonyezwa sehemu ya kupiga risasi.

     Taratibu moshi mzito uliokuwa  umetanda eneo hilo ulianza kupungua na hatimaye ukaondoka kabisa, eneo alilofungwa Norbert hakuwepo zaidi ya kuwepo kamba ngumu alizokuwa amefungwa. Wale Leopards wawili waliokuwa wanayaongozwa magreda ili yamuue Norbert wote pamoja walionekana wakiwa wamechomwa visu shingoni mwao, Panthers na Leopards walipotazama juu kwenye milango ya kuingilia ndiyo walichoka zaidi kwani hawakuona dalili yoyote ya uwepo wa watu waliokuwa wanapiga risasi zaidi tu ya kuona milango  ikiwa imevunjwa kwa mlipuko.

      Eneo walilosimama halikuwa na hata ganda moja la risasi kuashiria kwamba kulikuwa kunatupwa risasi, haikuwezekana kwa milio ya bunduki za kivita isikikike halafu kusiwe na dalili ya uwepo wa maganda ya risasi eneo.

         "Damn! Tumezidiwa akili sasa hebu Leopards nendeni juu mkaangalie zaidi" Panther mmoja aliongea kea hasira huku akirusha ngumi hewani kutokana na kuzidiwa ujanja na mtu ambaye hakujulikana alifika eneo hilo saa ngapi, Leopards walipanda juu haraka na walirejea wakiwa wameshika bunduki nne ambazo mbili zilikuwa AK47 na mbili nyingine zilikuwa ni SMG T-56.

         "Boss zilikuwa zimefungwa kamba kwenye trigger zake kwa kila bunduki na hazina dalili ya uwepo wa risasi zaidi ya magazine zake kuwa na dalili ya uwepo wa baruti tu" Leopard mmoja aliongea.

         "Oooh! Shit" Panthers kwa pamoja walisema kwa hasira baada ya kubaini walikuwa wamezidiwa akili na mtu ambaye hawakumjua ni nani.



 ILIVYOKUWA
     Kutokana na mapenzi mazito aliyonayo Norene kwa Norbert na kukaa siku nyingi bila kumuona na hata akafaidi siku moja tu akiwa naye, moyo wake haukuridhia kabisa na akatamani kukaa naye kwa siku ya pili lakini majukumu yalikuwa yamemzonga Norbert hivyo akaondoka asubuhi kwenda kwenye mihangaiko.Hamu ya  Norene ya kukaa naye siku nzima ilipozidi aliona hamna jinsi, aliamua kumfuata kazini kwake ili walau akakae naye kidogo kutokana na kuwa na hamu naye sana.

     Alitoka asubuhi akimpeleka Jerry kwa dada yake halafu akaelekea ofisini kwa Norbert akitumia usafiri wake binafsi.

    Alipofika jirani kabisa na ofisi ya Norbert tayari ilikuwa ni saa nne na aliamua apate kifungua kinywa kwenye mgahawa uliopo jirani na ofisi ya Norbert kwanza halafu akimaliza ndiyo aingie kwenye ofisi ya Norbert, eneo alilokaa kwenye mgahawa huo lilikuwa likitazamana na ofisi ya Norbert kwa upande wa pili wa barabara. Wakati anaingia yule mzee ofisini kwa Norbert tayari alikuwa ameshamuona na  kilipopita kipindi kifupi cha muda  toyota hiace inayotumika kubeba wagonjwa ilikuja kuegeshwa jirani na mlango ya ofisi ya Norbert, Norene  tayari alikuwa ameiona kila kitu.

    Norene hapo alihisi kuna kitu kisicho cha kawaida kinachotaka kutendeka baada ya kuiona hiyo gari, kifungua kinywa chote hakikuwa na maana kwake na alikiacha hapohapo akaanza kutembea kwa umakini huku macho yakiwa makini sana kuangalia pale kwenye lango la ofisi ya Norbert. Wasiwasi ulimzidi zaidi alipishuhudia Norbert akitolewa ndani akiwa amelazwa kwenye kitanda cha Magurudumu akiwa amefungiwa dripu kwenye mkono wake, moyo wake ulipiga kwa nguvu kwa kitendo hicho lakini nafsi yake ikamsihi atulie aangalie kila kitu. Norbert aliingizwa kwenye gari ile na milango  ya gari ile na milango ikafungwa hapohapo, ving'ora vya gari hilo la wagonjwa vilianza kusikika na gari hiyo ikaanza kuingia barabarani kwa kasi.

     Kusikika kwa ving'ora hivyo kulimpa utambuzi mwingine Norene kuhusu gari hilo, alijiuliza kwanini gari hilo la wagonjwa lisije likiwa linapiga king'ora mahali hapo na lije kimyakimya tu  tena kwa mwendo wa kawaida. Kwanini halikuonesha dalili yoyote ya kuwahi kumchukua mgonjwa  wakati linakuja, maswali hayo yaliamsha akili ya Norene kwa ghafla na hisia juu ya uwepo jambo jingine tofauti.

      Hakutaka kupoteza kwa haraka sana alikimbia eneo aliloegesha gari lake akaingia akaliwasha  na akaingia barabarani akawa anaenda kwa mwendo wa kasi aliwahi lile gari la wagonjwa, alikuja kulikuta gari hilo la wagonjwa katika  barabara ya  Bibi titi likijiandaa kuingia kwenye barabara ya Morogoro. Gari hilo lilipoingia kwenye barabara ya Morogoro bado alikuwa nalo yupo kwa nyuma na alikuwa anaenda nalo kwa kasi sambamba akionekana alitumia njia hiyo ili awahi aepuke foleni ya barabarani, gari hilo la wagonjwa lilipofika makutano ya barabara ya Fire lilinyoosha moja kwa moja likiwa na mwendo ule ule.

    Norene alilifuatilia lile gari hadi linapita Magomeni, Manzese, Ubungo, Kimara na hadi linafika Mbezi bila kujulikana kama analifuatilia, gari hilo lilipofika  Mbezi Kibanda cha Mkaa kweye kituo cha daladala lilizima king'ora likakata kona  kuingia kona kushoto likawa linaelekea barabara ipitayo jirani na kanisa la kiluteri la Mbezi Louis. Aliendelea kulifuatilia gari hilo hadi linafika tasisi ya Agape ambapo liliendelea mbele kwa mwendo mfupi kisha likatakata kuingia kulia mahali kwenye geti kubwa liloandikwa Northern brothers warehouse, Norene alipofikia eneo hilo alisimamisha gari kwa mbali kidogo ambapo aliliona hilo gari likiingia ndani ya ghala hiyo baada ya lango kufunguliwa.

    Baada ya kuona mahali ambapo gari hilo lilikuwa limeingia Norene alitoa simu akampigia Moses lakini simu iliita bila kupokelewa, alipiga usukani wa gari kwa hasira kisha akageuza gari akaondoka.

    Alirejea majira ya jioni akiwa amevaa nguo za kimazoezi na mgongoni akiwa na begi kubwa sana, aliegesha gari lake mbali na eneo la ghala hilo kisha akashuka akapita njia za mkato akatokea mahali ulipo uzio wa nyuma wa ghala hilo. Norene alitazama pande zote za uzio wa ghala hiyo  kisha akafungua begi  kubwa alilokuja nalo akatoa vitu viwili mithili ya soksi nzito ambavyo aliviva mikononi akaanza kupanda ukutani akiwa amelivaa begi lake mgongoni, alipofika juu kabisa ya uzio huo aliangalia pande zote alipojihakikishia usalama alishuka taratibu kuingia ndani akatokea sehemu yenye magari makubwa mengi.

    Alitembea kwa  kunyata hadi kilipo chumba cha walinzi wa ghala hiyo ambapo kulijaa kila aina ya kelele kutoka kwa walinzi hao wakionesha walikuwa wakifurahia jambo, Norene hapo aliamua kufungua begi lake akatoa chupa inayofanana na ya manukato ambayo ni sumu inayolaza mtu kwa masaa mengi akaifungua huku akiwa amejiziba mdomo  na pua halafu akaitupa ndani ya chumba hicho kwa kupitia upenyo wa dirishani.

    Ndani ya sekunde kadhaa watu hao walikuwa kimya kabisa, alipomaliza sehemu hiyo ya walinzi ndipo akaingia ndani akashuka hadi chini sehemu aliyofungwa Norbert. Alishuhudia kila kitu akiwa amejibana sehemu yenye dirisha dogo na akaona uwezekano wa kumuokoa Norbert upo ikiwa atatumia akili nyingi kuliko nguvu, alifikiria kwa sekunde kadhaa ndipo akapata mbinu ya kwenda kumkomboa mwanaume anayempenda.

    Alifungua begi lake akachukua mabomu madogo yenye rimoti ambayo aliyatega kwenye kila mlango wa kuingilia eneo alilofungwa Norbert halafu akachukua bunduki nne zenye baruti ndani akazielekeza  kwenye milango hiyo zikiwa kwa umbali wa mitaa kadhaa akiwa amezifunga kamba moja sehemu yenye kifyatulio cha risasi, alichukua visu viwili akavichomeka kiunoni pamoja na mabomu mawili ya machozi akayashika mkononi.

   Panther alipoamuru  magreda yamchane Norbert na ukelele wa mamumivu uliotoka kwa Norbert ambao ulimfanya Norene na yeye aumie kwa jinsi anavyompenda Norbert, hapo ndipo alipominya rimoti mabomu yote aliyoyatega kwenye milango hiyo yakalipuka yakalipuka yakavunja milango. Norene aliyatoa mabomu ya machozi ufunguo wake kisha akayatupa kule chini walipo, Moshi mzito ulitanda ambao uliwafanya Panthers na wenzao waamini kwamba walivamiwa na hivyo wakajibana pembeni kujilinda, Norene alivuta ile kamba aliyoipitisha kwenye vifyatulio vya risasi na kupelekea Panthers na wenzao wazidi kujibana kwani waliamini wamevamiwa na hawakuwa na silaha yoyote ya kujihami kwa muda huo baada ya kusikika milio ya risasi ikirindima.

    Norene  alivaa kinyago cha kuzuia gesi na aliutumia muda huo kuvamia eneo la chini kwa kasi ajabu akaanza kwa kurusha visu kwa utaalamu wa hali ya juu na kila kisu kilitua katika shingo ya Leopards waliokuwa wakiendesha magreda. Alimfungua Norbert sehemu aliyofungwa kisha kwa kasi ya ajabu akapanda juu ilipo milango, aliondoka na Norbert akiacha zile bunduki zikiendelea kulia na hata mlio ulipoisha tayari alikuwa ameshatoweka eneo hilo.


****

    Panthers walipandwa na hasira wakazidi kulaani mioyo yao kwa kutaka kujihami badala ya kushambulia pale walipowekewa shambulizi hewa lililowafanya wahisi kwamba wamevamiwa kikosi kizito kumbe ilikuwa ni mchezo mdogo wa kiakili uliochezeka hapo ambao uliwazidi kiakili zaidi, laiti kama wangelitumia akili bado muda huo Norbert angekuwa yupo katika mikono yao na Norene aliyekuwa akiwachezea akili kiasi cha kumtorosha Norbert basi angekuwa yupo katika mikono yao hadi muda huo.

    Walijiona walikuwa wamefanya uzembe mkubwa sana kwa kuendekeza kujilinda zaidi badala ya kufuata akili zao zilizowafanya wapewe jukumu maalum ambalo linawapa ulaji katika maisha yao, muda huo ndipo fikira za juu ya uhalisia wa Norbert zilikuja ndani ya vichwa vyao hawakuelewa alikuwa ni nani mpaka akombolewe na mtu mwenye ujuzi wa kijasusi zaidi. Walipozidi kufikiria zaidi kuhusu Norbert waliona kama vinyago walivyovivaa usoni vinavyoonesha sura ya chui mweusi vilikuwa vikiwaletea  usumbufu katika fikra zao, walivivua wote kwa pamoja kisha wakatazamana bila ya kuambiana kitu chochote kwa sekunde kadhaa halafu wakawatazama Leopards waliobaki wawili  ambao nao walivua vinyago vyao na sura zikaonekana.

    Hakika mapacha hawa wanaojiita jina la chui mweusi kutokana na kuwa na sifa za huyo chui mweusi wote kwa pamoja waliona kama wametukanwa tusi kubwa sana kwa jinsi walivyochezewa akili, kitendo hicho waliona kama walikuwa wamevuliwa nguo mbele ya hadhara kwa jinsi walivyokuwa na mbinu za hali ya ju hawakufaa kupumbazwa kirahisi namna ile.

        "brother we have to find out huyu Norbert ni nani na kamfanya kitu gani Lion, aaaaaargh!" Panther mmoja aliongea huku akimtazama Pacha wake usoni akionekana kuwa na hasira sana.

        "Brother poa kidogo tusitumie hasira katika hili kwani tutazidi kuvuliwa nguo zaidi ya hivi tulivyovuliwa,sasa hivi najiona tumebaki na underwear pekee kwa jinsi tulivyofanywa wajinga. Sasa unafikiri tukivuliwa zaidi si itakuwa ni aibu sasa,akili zetu zifanye kazi" Panther wa pili alimtuliza mwenzake kwani hasira zilikuwa zimezidi uwezo wake wa kufikiri, maneno hayo hatimaye yaliweza kuishusha hasira yake na akahema kwa nguvu zaidi.

         "Ok brother,plan inayofuata ni ipi?" Panther wa kwanza alimuuliza pacha wake baada ya hasira kumshuka.

         "Brother kumbuka samaki hutegwa kwa chambo wala hawezi kutegwa kwa ulimbo, so we have the trap. Leopard Queen atakuambia vizuri, Panther wa pili aliongea kisha akawatazama Leopards waliobaki ambaye mmoja  alikuwa ni mwanamke mrembo sana akiwa amesimama kikakamavu  akamwambia,"Leopard Queen unaweza ukatuambia ndoano ipo tayari maana samaki yupo karibu sana na chambo asije akala chambo wakati ndoano hamna".

          "Ndoano ipo tayari kilichobaki ni kumnasa tu samaki aliyeifuata chambo akitaka kuila tu akijua ndoano hamna" Leopard Queen aliongea na kuwafanya Panthers watabasamu wakiona hawakuwa na haja ya kutia nguvu zaidi. Hawakuwa na zaidi katika mpango huo na kilichobaki ni kuendelea na kazi ile iliyowafanya  wapate ulaji wa awali, hasira zao za kuchezewa akili ziliisha papo baada ya kuhakikishiwa mpango namba mbili ulikuwa ukifanya kazi.



TUKUTANE JUMAPILI PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA



HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA YA MTUNZI