Saturday, November 21, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA NNE




                             DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGIN



SEHEMU YA NNE!!
"Afande tumefanya juhudi za kuuzima huu moto kwa kutumia  kila njia ila imeshindikana hadi maji yanaisha hatukuweza kuuzima na ikatubidi tutumie gesi lakini bado tumeshindwa kuuzima na inasadikika Mkuu wa idara ya sheria makao makuu ya kampuni hizi yupo ndani ya nyumba ya tatu na hajatoka hadi muda huu na hata tulipofika tulikuwa tukisikia kelele za mtu akiomba msaada lakini sasa hazisikiki" Mmoja wa maaskari wa zimamoto aliongea kwa ufupi juu ya tukio hilo la kuungua kwa nyumba hizo, James aliposikia maelezo hayo alipiga kelele huku akiita, "Babaa!". Aliwapita askari wa kikosi cha zimamoto akakimbia kuelekea ulipo moto katika nyumba ya tatu ya kampuni, maaskari wote walianza kumkimbiza ili wamuwahi asiingie ndani ya moto huo kutokana na ukali wake.

****

Mbio za watu wote waliokuwa wakijaribu kumzuia James asiingie ndani ya nyumba hazikuzaa matunda yoyote katika kumzuia kwani James aliingia ndani ya nyumba hiyo kabla hawajamzuia, wenzake pamoja na maaskari wote walipojaribu kuikaribia mlango wa nyumba aliyoingia James walijikuta wakitupwa nyuma wote baada ya mlipuko mzito kutokea katika nyumba hiyo kisha nyumba nyingine zilizosalia nazo zikapata mlipuko wa aina hiyo hiyo. Asp John, maaskari wa zimamoto pamoja na wenzake James wote walisikitika kwa kitendo cha James kuingia katika nyumba hiyo inayoungua ambayo tayari imeshatoa mlipuko mzito wa moto, bado walikuwa wamelala chini baada ya kutupwa na mlipuko mzito waliposogelea nyumba aliyoingia James ili wamuokoe. Ajabu ya mlipuko huo uliowatupa haukuwaunguza hata kidogo wala hata kunuka harufu ya moshi, walikuwa wameumia tu baadhi ya sehemu za miili yao baada ya kuanguka chini. Wakiwa hawana hata akili ya kunyanyuka pale chini tayari jambo jingine la kustajaabisha lilianza kutokea ambalo liliwafanya wakimbie kuelekea ulipo uwanja wa mpira ili wakae mbali na ardhi ambayo imebeba  nyumba hizo, lilikuwa ni tetemeko la ardhi lililoikumba ardhi iliyobeba nyumba hizo huku eneo la jirani na hapo likiwa limetulia bila kupatwa na tetemeko hilo. Matofali ya nyumba hizo ambazo bado zilikuwa zinawaka yaliporomoka katika mpangilio wake uliounda ukuta  na yakajazana kama tanuli katika kila nyumba iliyokuwa imejengwa, tukio hilo lilishuhudiwa na halaiki ya watu ambayo tayari ilikuwa imeshajikusanya katika uwanja wa mpira kuangalia maajabu hayo. Waandishi wa habari kituo cha televisheni cha Tanga nao walikuwa wakilirusha tukio hewani, hata waandishi wa habari waliopo mkoa wa Tanga kuwakilisha vituo vyao wakikuwa wameshawasili pia walikuwa kazini.
Tetemeko hilo la ardhi la maajabu liliendelea kutikisa ardhi hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Extoplus hadi hata matofali yalijijaza vifusi katika kila eneo lililokuwa limejengwa nyumba yakasagika yakawa mchanga mtupu, baada ya tetemeko kutulia ndipo askari wa zimamoto na uokoaji walipopata ujasiri wa kusogelea katika kifusi cha mchanga uliosagika ambao ulikuwa ni wa matofali wa nyumba ile waliyoingia James na Baba yake kwa nyakati tofauti. Walikifukua kifusi hicho kwa kutumia vifaa vyao na kukagua kila sehemu ili waweze kuitoa miili ya baba na mwana lakini hawakuambulia hata kiungo kimoja cha miili ya James na baba yake, askari walizidi kupigwa na mshangao watu tukio hilo kwani ilikuwa ni jambo la ajabu sana.
"mmh! Sijawahi kukutana na tukio kama hili tangu nianze kufanya kazi katika kikosi cha zimamoto  na uokoaji katika jeshi la polisi" Kiongozi wa askari wa zimamoto na uokoaji alimuambia Asp John.
"hivi jambo kama hili linawezekanaje?" Asp John alijikuta akiuliza swali ambalo halina maana yoyote kwa mkuu wa kikosi cha zimamoto na uokoaji.
"hilo swali hata sijui nikujibu vipi unaona kabisa imezekana  katika namna isiyokuwa rahisi, mtu aingie ndani ya nyumba halafu ilipuke tu kisha tetemeko liloikumba ardhi ya ukubwa wa ekari kumi na tano litokee liangushe matofali yasagike halafu moto uzime tusipate hata baki la mwili wa binadamu katika sehemu waliyoingia" Yule mkuu wa kikosi cha zimamoto aliongea.
"ama kweli hii ni dunia ina mambo ambayo usiyoweza kuyadhania" Asp John aliongea huku akisikitika.
"ndiyo hivyo afande" Mkuu wa kikosi cha zimamoto aliongea.
"hapa hamna la ziada ngoja nirudi nikaendelee na tukio la kule la Bwaga macho, vijana nina shida na nyinyi hebu nifuateni" Asp John aliongea huku akiondoka na wale marafiki zake James wakamfuata.



     
    
           SURA YA TATU

      Hadi jioni inaingia tayari tukio lile la ajabu lilikuwa lishaenea jiji zima la Tanga na kwingineko ndani ya nchi ya Tanzania na hata Afrika ya mashariki, ilitokea kuwa habari iliyoteka  vyombo vyote vya habari katika ukanda huu na  hata katika  kituo BBC idhaa ya Kiswahili ilitangazwa na kupelekea kuwa habari iliyosikika karibia dunia nzima kwa watu wanaongea kiswahili. Taarifa za vibweka vilivyotokea huko Duga zilimfikia mmiliki wa kampuni ya Extoplus Hamid akiwa yupo kitandani  katika wodi ya zahanati ya kampuni yake tangu alipoanguka kwenye chumba cha mkutano, aliipata taarifa hiyo kupitia luninga iliyopo katika wodi aliyolazwa akawa amebaki na masikitiko tu kutokana na hasara aliyoipata kuungua kwa nyumba hizo ambazo zilimgharimu pesa nyingi hadi kukamilika kwake. Hadi saa nne usiku anaruhusiwa alikuwa na majonzi kutokana na jambo hilo, alirudi nyumbani kwake kwa msaada  wa dereva wake.
Asubuhi ya siku iliyofuata alitoka mapema nyumbani akaenda ofisini akiwa na mawazo lukuki kichwani mwake, siku hiyo ilikuwa mbaya kwa Hamid kuliko siku zote za maisha yake kwani alipifika ofisini kwake tu akakumbana na kisanga kingine baada ya mwili wa kaimu mwenyekiti mtendaji wa kampuni yake Hisan kukutwa ukiwa chumba cha mkutano alichokuwemo siku iliyopita akiwa na wafanyakazi wake wakuu wakiongea. Mwili wa Hisan ulikutwa na mfanya usafi wa kampuni hiyo ambaye alichanganyikiwa baada ya kuuona ukiwa hauna uhai upo sakafuni. Tukio hilo lilikuwa ni tukio jingine la aina yake ambalo ilionekana ni kama mkosi umeingia kwenye kampuni hiyo kutokana na kuzaliwa kwa jambo jingine lililozidi kumchanganya Hamid, baada ya polisi kuchukua vipimo vyote pamoja na kuondoka na mwili wa Hisan afisa ajira wa kampuni hiyo aliingia katika ofisi ya Hamid akiwa na faili kubwa aliloweka mezani kisha akaweka barua juu yake.
"Msuya ndiyo nini hii unaniletea" Hamid aliuliza.
"Bosi hiyo ni barua ya kuacha kazi katika kampuni hii ili niwe salama na maisha yangu" Msuya ambaye ni afisa ajira katika kampuni hiyo aliongea.
"unasema nini wewe?!" Hamid aliuliza kwa mshangao.
"ndiyo hivyo bosi kutokana na ndoto niliyoiota usiku wa leo iliyonipa onyo juu ya maisha nikiendelea kufanya kazi hapa sina budi kuacha kazi, uamuzi huu si wangu peke yangu bali ni wa mameneja wote pamoja na wakuu wa idara wote na barua zao zipo kwenye faili nililokuletea" Msuya aliongea maneno yaliyozidi kumchanganya Hamid.
"yaani Msuya pamoja na kuwa ni msomi mwenye elimu kubwa bado unaamini ndoto" Hamid aliongea kwa masikitiko.
"Sina budi kufanya hivyo  kwani kila mtu aliyeandika barua hii ameota ndoto kama hii tena ameonywa kuhusu kifo kilichotokana na ubishi wa staff wa idara ya uhasibu waliokufa jana ikiwa atabisha. Nimeamua kuacha kazi mimi na wenzangu na kila mmoja hahitaji marupurupu yoyote tunaondoka kama tulivyokuja" Msuya aliongea kisha akatoka ndani ya ofisi hiyo akimuacha Hamid akiwa amechanganyika akiwa anakaribia hata kulia, alitulia ofisini kwake kwa muda mfupi kisha akaamua kutoka kupitia idara zote kuangalia kama kile alichoambiwa na Msuya ni kweli au ilikuwa ni utani. Huko ndipo aliposadikisha maneno ya Msuya baada ya kukuta ofisi zote zikiwa zipo tupu hakuna hata mfanyakazi, Hamid alijikuta akianza kulia mwenyewe na akaona hali aliyoikimbia kabla hajawa na familia sasa inaanza kumrudia. Yeye hakutaka hali hiyo imtokee tena na alikuwa yupo tayari kuizuia kwa namna yoyote ile na hapo ndipo alipopata ufumbuzi  wa matatizo yake kwa mtaalamu wake maalum.
"Dokta Bundi atanisaidia niepukane na adha hii ngoja niwahi kwenda kwenda kwake Mwamboni" Hamid alijisemea mwenyewe kisha akaanza kutoka mbio kuelekea nje ya ofisi ambapo alipanda gari yake akaiondoa kwa mwendo wa kasi akiwa na haraka ya kuwahi safari yake. Aliendesha gari kwa mwendo wa kasi akiwa na ari ya kuwahi kufika Mwamboni kwa mganga wake ambaye huwa anamsaidia katika matatizo mbalimbali, akiwa yupo ndani ya gari akiwa anakatiza katika barabara ipitayo  Chumbageni alisikia sauti ikimuambia "aisee nishushe hapohapo chumbageni police station nataka kuongea na jamaa yangu".
Hamid alishtuka sana akatizama nyuma kwa uoga na akijikuta anatamani hata apotee kimiujiza humo ndani ya gari, laiti kama moyo wake ungekuwa na nguvu kama ya vijiko vinavyojenga barabara ya kugusa ukuta tu na kuuangusha basi ungekuwa ushapasua kifua chake kwa jinsi ulivyokuwa unadunda kwa nguvu baada ya kumuona Hisan aliyekutwa akiwa amekufa katika chumba cha mkutano asubuhi ya siku hiyo.
"unashangaa nini Hamid hebu simamisha  gari hapo Chumbageni polics station nikaangalie ripoti ya kifo changu kilichonipata jana kama polisi wamechunguza kiusahihi" Hisan aliongea huku akionekana yupo katika hali ya kawaida tu, Hamid alikuwa tayari ameshaachia mkojo ulimtoka bila hata kujijua.
"Ona sasa dume zima una miaka arobaini na nane unajikojolea kisa kumuona mtu aliyekufa akiwa anatembea, hebu simamisha gari nishuke wewe nishafika tayari nataka nikaangalie ripoti ya kifo changu nasikia anayo Inspekta Ismail Mdoe. Au hii sura inakuchanganya ngoja niibadilishe basi uoga ukupungue" Hisan aliongea kisha akabadilika kuanzia sura hadi mwili ukawa wa mtoto aliyemtokea Hisan kabla hajafa.
"Hapo vipi utaniogopa tena?" Aliuliza huku akimtazama Hamid ambaye alizidi kuogopa na akawa anahangaika kufungua mlango ili ajitupe nje kuikimbia sura aliyoiona sasa hivi ikiwa ina macho mekundu, milango ya gari ilikuwa haifunguki na hata alipotoa kifunga mlango bado haikufunguka hata kidogo. Hamid aliendelea kuhangaika na kukivuta kitasa  cha ndani cha mlango akiwa haamini kama mlango umejifunga, alibaki akihangaika kuchezea kitasa kutokana na kuchanganywa na tukio hilo.
"ukimaliza uniambie" Yule mtoto alimuambia huku akikunja miguu yake ikatengeneza umbo la nne akimtazama akiwa na tabasamu lisiloashria furaha hata kidogo.
Hamid alikuwa ameshasahau kama alikuwa anaendesha gari na alipokuja kukumbuka aliona gari linaenda lenyewe kwa mwendo wa taratibu sana na lilikuwa likipitwa na magari yanayowahi. Alibaki akimtazama yule mtoto huku akitetemeka kiuoga na mikono akiwa ameweka ishara ya kuomba msamaha.
"halafu unataka kuruka nje huku  umejifunga mkanda sasa ndiyo unafanya ujinga gani?" Yule mtoto alimuambia  Hamid ambaye hakuwa anatambua hakuwa amefungua mkanda katika harakati za kutaka kuoko nafsi yake, alipotaka kuufungua mkanda yule Mtoto alinyoosha mkono wake na mkanda wa gari ukamzunguka Hamid shingoni  mwake kama nyoka na ukaanza kumkaba kwa nguvu hadi mishipa ya damu ya kichwani ikawa inaonekana.
"Nipe" Yule mtoto alimuambia Hamid huku akimtazama kwa hasira.
"siii....sinaa" Hamid aliongea kwa tabu kutokana na jinsi mkanda ulivyomkaba.
"kimoja umenipatia, nataka unipe kilichobakia. Sasa nipe!" Yule mtoto aliongea kwa hasira huku akitokwa na cheche za moto mdomoni.
"sinaa!" Hamid aliongea kwa tabu huku macho yake yakibadilika rangi kutokana na kukabwa, mishipa ya kichwani ilikuwa imemtoka hasa.
"Ok haya fungua mlango ukimbie" Yule mtoto aliongea na muda huo mkanda ukaacha kumkaba Hamid na mlango ikawa ipo kawaida, Hamid alifungua  mkanda akafungua mlango akajitupa nje bila hata kuangalia barabarani. Kitendo cha Hamid kujitupa nje ilsikika
 honi ya gari ya  mizigo iliyolia kwa nguvu pamoja na vyuma vya breki kutoa mlio mkali, vishindo viwili vizito vikafuata   kwa kupishana sekunde mbili na hapo kila aliyekuwa yupo karibu na eneo hilo akashika kichwa kwa mshangao.

Gari aina ya Scania ya mizigo ndiyo ilikumbana na kishindo cha kwanza baada ya kumgonga Hamid  na kupelekea kichwa chake kupasuka na kutengeneza taswira isiyofaa barabarani kuangaliwa na binadamu wa kawaida kwani haifai binadamu kuona kichwa cha binadamu mwenzako kikiwa kimepasuliwa kama puto liliingia katika kichaka chenye miiba. Kishindo kingine kilikuwa ni cha gari la Hamid baada ya kugonga mti wa mwembe uliopo katika makutano ya barabara inayotoka Kwa minchi, inayoelekea Amboni na hiyi inayopita Chumbageni. Ndani dakika zisizopungua tatu tayari maaskari walishajaa kutokana na kituo cha polisi kutokuwa mbali na hapo ilipotokea tukio hilo, askari hao walikuwa mchanganyiko kati ya askari wa usalama barabarani na wa kawaida ambao walishiriakiana na kuifanya kazi hiyo kwa haraka. Uchunguzi wa magari yote yalipokaguliwa yalizidi kushangaza watu kwani  katika gari aina ya Scania hakukuwa na dereva ingawa mashuhuda walisema dereva hakushuka na katika gari aina ya range rover sport aliyokuwa anaitumia Hamid hakukuwa na dereva vilevile. Maaskari wakiwa bado hata hawajasahau tukio la siku iliyopita tayari wanakutana na tukio jingine la kushangaza kama hilo.
"sasa haya magari yatajiendeshaje yenyewe hebu nyinyi kachunguze vizuri mazingira ya jirani na ule mwembe ilipogonga ile Range tena someni na stika zake tumjue mmiliki nilitaka kusahau hilo" Askari mwenye nyota tatu mabegani mwake aliongea, maaskari walipiga saluti kisha wakaenda kuchunguza walichoambiwa na mkubwa wao kwa haraka. Baada ya dakika moja tu tangu wale askari waondoka simu ya upepo ya yule Inspekta ambaye ndiye mwenye nyota tatu ikakoroma kisha ikasikika sauti ya yule askari mwingine ikimuita kule kwenye gari aina ya Range rover iliyogonga mti wa Mwembe, Inspekta huyu alienda haraka hadi pale kwenye kwenda kuona alichoitiwa. Alipofika alipigiwa saluti kisha akaongozwa na askari mwingine hadi kwenye kioo cha gari hiyo, yule askari aliyemuongoza alimuonesha yule Inspekta stika za gari ile ambazo ziliandikwa jina la mwenye gari.
"Hamid Buruhan, si mmiliki wa kampuni iliyokumbwa na kadhia isiyoeleweka jana" Inspekta aliongea
"ndiyo afande" Yule askari aliyemuita  aliitikia.
"Sajenti Shehoza hebu licheki hili gari halafu..." Yule Inspekta aliongea lakinj akasitisha maneno yake baada ya kuona alama za kung'oka majani yaliyoonekana yametokana na  kuburuzwa kitu kuelekea katika majani marefu yaliyopo jirani na Mwembe, aliamua kufuatilia alama  hizo kuelekea kwenye majani marefu akiwa anatazama chini kwa umakini sana ambapo aliona vitu mbalimbali vya uganga vikiwa vimeanguka njiani kama vile hirizi na vibuyu pamoja na kitambaa chekundu cha kaniki. Inspekta huyo aliendelea kufuatilia hadi mwisho wake ambapo alikutana na mwili wa mzee wa makamo ukiwa umelazwa kwenye majani yaliyoonekana kupunguzwa kwa kitu chenye kali katika sehemu ulipolazwa mwili huo. Mavazi yaliyokuwa yamevaliwa na maiti hiyo ambayo yalionakana aliyavaa mwenyewe kabla hajakumbwa na umauti yalikuwa ni ya kiganga kabisa, kaniki nyekundu aliyojifunga ilitosha kumtambulisha kama mganga ukiachilia mbali  hirizi iliyopo begani kwake.  Inspekta yule aliwaamrisha maaskari wale wachukua vipimo vyote juu ya mwili kisha wawaite wauguzi maaskari waliofika hapo baada ya kupigiwa simu waje wauchukue mwili ukahifadhiwe, Inspekta huyo aliondoka akarudi alipokuwa awali ambapo barabara ilikuwa inasafishwa baada ya uchukuaji wa vipimo kukamilika alisimamia taratibu zingine. Gari la kuvuta magari mabovu maarufu kama Break down nalo liliitwa likaondoa magari yote yakaenda kuhifadhiwa katika kituo cha polisi cha Chumbageni. Maaskari waliokuwa kule kwenye majani marefu walirejea wakiwa na wauguzi maalum wa jeshi la polisi waliobeba machela yenye mwili wa yule mzee aliyekutwa kwenye majani, wakiwa wanaelekea kwenye gari la wagonjwa la hospitali kuu ya Tanga yaani Bombo. Mwanamke mmoja asiyejulikana ametokea wapi alikimbia hadi pale walipokuwa wale maaskari na wauguzi akaufungua ule mwili kisha akaanza kulia kwa uchungu huku akipiga kelele kwa uchungu.
"Jamani mume wangu mimi!" Aliropoka yule mwanamke huku akiishika machela iliyobeba mwili.
"we mama hebu tulia tufanye kazi yetu" Sajenti Shehoza aliongea huku akimzuia yule mwanamke na wale wauguzi wakaendelea na safari.
"Baba Hadija nilikumbia usisaidie usiowajua umeona sasa, Mayoooo mayooo" Yule mwanamke alizidi kuongea kwa nguvu huku akilia kama mtoto mdogo.

****

Wakati askari wakishughulika katika ajali ya kutatanisha iliyotokea Chumbageni, upende mwingine wa jiji la Tanga katika maeneo ya Raskazone hali ilikuwa shwari kuliko kawaida katika kampuni ya mafuta ya Matro inayosifika kwa kutoa huduma bora za mafuta jijini Tanga na kwingineko. Ndani ya makao makuu ya kampuni hii wafanyakazi walikuwa wakiendelea na kazi kama kawaida ili kuinua kampuni na pia kuendesha maisha yao. Siku hiyo mmiliki wa kampuni hiyo  Hussein Buruhan ambaye ni mmojawapo wa matajiri wakubwa nchini alikuwa yupo ofisini kwake ghorofa ya kumi na mbili ya jengo la kampuni hiyo akiendelea na kazi kama kawaida.
Baada ya nusu saa za uchapaji kazi alianza kuhisi kubanwa na haja ndogo na ikambidi aende msalani kutokana na kushindwa kuvumilia kukaa katika hali hiyo, alifunga ofisi kisha akaingia katika maliwato ambayo ipo jirani na ofisi yako.  Aliingia moja kwa moja msalani akajisaidia kisha akatoka akiwa anapiga uruzi wa nyimbo anayoipenda akiwa na tabasamu pana usoni mwake, kama ilivyo kawaida yake huwa akitoka maliwatoni lazima aende kwenye kioo kipana chenye masinki yenye koki kadhaa za maji kwa chini yake ili anawe mikono. Alienda kwenye sinki hilo akafungua maji akanawa mikono kisha akanawa uso akiwa anapiga uruzi wa wimbo anaupenda unaoitwa this i promise you ulioimbwa na kundi la wanamuziki wa kimarekani liitwalo N-sync, akiendelea kupiga uruzi  huo ghafla taa za huko kwenye maliwato zikazima na kukawa giza kutokana na madirisha madogo yaliyomo humo kutopitisha mwanga vizuri.


ITAENDELEA!!



MUHIMU: PDF YA RIWAYA HII IPO TAYARI KUIPATA WASILIANA NA MTUNZI KWA UJUMBE MFUPI NAMBARI +255713 776843, UKIITAKA YOTE PIA IPO KWA BEI NAFUU

No comments:

Post a Comment