Monday, January 9, 2017

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA THELATINI NA SABA





RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________



SEHEMU YA THELATHINI NA SABA!!

                "Kiwewe cha namna gani kile ukumbuke kuvua viatu uvishike mkononi ukimbie vizuri na si kuvitupa, maigizo ya kibongo haya. Haya tuondokeni" Norbert aliongea huku akicheka na alitoa pia
amri ya kuondoka eneo hilo, yule kijana wa kiume ndiye aliyekuwa upo nyuma ya usukani na aliposikia mari hiyo aliliwasha gari na akaweka gia kisha akaliingiza barabarani na kuondoka katika eneo hilo.



_____________TIRIRIKA NAYO

     Pindi Mufti na Askofu walipotoka tu ndani ya makao makuu ya jeshi, simu ya Norbeert iliita wakati akiwa na vijana wake wakikatiza katikati ya jiji la Dar es salaam baada ya kutoka Msasani kufanya tukio la kuwapunguza nguvu maadui wa taifa hili. Simu hiyo Norbet aliipokea na kusikiliza kwa makini sana kwani aliyekuwa akipiga alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa wapo upande wake katika kuhakikisha nchi inakua salama na kuvamiwa na wapenda pesa kuliko maslahi ya taifa, hadi simu hiyo inakatwa Norbert alikuwa ameshapokea taarifa mpya kabisa kutoka kwa M.j Belinda ambaye ndiye aliyempigia hiyo simu akampa taarifa ya kila kitu ambacho hakuwa amekifahamu kama kilikuwa kikitendeka. Ilikuwa ni majira ya saa nne na nusu inakimbilia kwenda saa tano kasoro dakika ishirini na tano, Norbert alipomaliza kuongea na simu hiyo alishusha pumzi kisha akawatazama vijana wake. Walikuwa tayari wameshaingia barabara ya Samora jirani kabisa na kituo cha reli cha Stesheni.
                      "Paki gari haraka sana" Alitoa mari na kijana wake aliitii na kuliegesha gari kando ya barabara mita kadhaa nyuma ya makutano ya barabara ya Somora na barabara inayopita mtaa wa Algeria, walikuwa wapo mbele kidogo ya ATM ya benki ya Exim ambayo ipo mitaa kadhaa kutoka ulipo mzunguko wa barabara unaojulikana kwa jina la Clock Tower.
                     "Sikia Boy we shuka uende msikiti wa Sunni karibia na duka la dawa la Shamsudin, ukanunue kanzu na kilemba kwa mara ya nyingine leo naenda kuswali Ijumaa" Norbert aliwaambia huku akitoa pesa mfukoni mwake, wote walicheka waliposikia kauli hiyo kwani wanajua kabisa mkuu wao huyo kanisa tu ilikuwa ni kituo cha polisi kwake. Kuwaambia kuwa alikuwa akienda kuswali ilikuwa ni jambo la ajabu sana kwao, hakujua kuwa kulikuwa kuna sababu ilimfanya yeye aamue kuingia  katika msikiti kwa siku hiyo ya leo.
                      "Haaaa!  Teh! Teh! Teh! Teh! Teh! Mkuu hiyo ni kali ya mwaka ila usisahau kosho najua mule  hotelini ulipotoka, nikiwa kama muisalamu sitakuruhusu uende msikitini hivyo ni dhambi kubwa sana" Kijana yule aliongea hukua akizipokea pesa za Norbert na mlango wa dereva tayari alikuwa ameshaufungua ili ashuke.
                        "Come on! Salum mimi mkristo ila sheria za dini yenu nazijua barabara na hata kiarabu hapa ni nyumbani kwake, tukitoka hapa ni kwenda kuoga hilo kosho then naenda kumsikiliza hatibu wa siku ya leo kuna jambo muhimu la kulifanya huko we kalete hiyo kanzu na kilemba" Norbert alimuambia.
                        "Sawa mkuu" Alitii amri na akashuka garini akamuacha Norbert na mwenzake wa kike waliyekuwa wapo naye kwenye mpango wa kumnasa Thomas ambaye kwa muda huo tayari alikuwa ni marehemu.
                         "mkuu leo umesilimishwa nini teh! Teh! Teh! Teh!" Yule wa kike aliuliza kiutani huku akicheka.
                          "sasa kinachokushangaza ni kipi na wewe kwani hii ni mara ya kwanza kuingia msikitini na nikaswali wakati nikiwa kazini"
                           "Lazima nishangae yaani, kanisa kwenyewe kuingia kwa tabu sana kama teja kuingia kituo cha polisi ndiyo leo hii uingie msikitini"
                           "kwani umesikia kanisani siingii?"
                           "Ndiyo mkuu huingii we umewahi kuingia lini kama kweli unaingia kanisani?"
                           "Eva sasa unaleta utani na muumini wa dhati wa dhehebu la katoliki kama mimi, nitake radhi"
                          "Haaaaa! Muumini gani wewe usiyelijua kanisa nusu mwaka sasa unaenda"
                         "Haloooo! Unaongea nini wewe wakati kila siku naenda kumuomba bwana"
                         "Mhhh! Toka zako wewe na ukijogoo umuachie nani yaani hata CE anakutambua"
                        "Weeeee! Ntake radhi jamani sasa simba atalalaje njaa kwenye msitu wenye vitoweo, anyway tuyaache hayo mara moja"
                       "ahaa! umeona inakulenga siyo unaua mada"
                       "(Akiwa na uso wa umakini) Turudi kikazi zaidi Eva utani kwa mkuu wako una mipaka pia ukumbuke"
                       "Sawa mkuu ila mimi sijapenda kumuona yule demu ulivyompa nafasi ya kujikomboa wakati ni mtu hatari na mwenye mbinu za kijasusi huoni ni hatari"
                       "Yule ni sawa na mamba asiye na meno hana hatari yoyote kwenye mpango wetu hadi unatimia"
                       "Hata kama mkuu kumbuka mamba asiye na meno akija kuota meno hatari ni ileile tu"
                        "Sasa mpaka aje kuota meno ni lini Eva si tayari nchi hii wasaliti washaondoka ukumbuke hana hatari yoyote hata wewe unamdhibiti muache tu aishi sidhani kama atakuwa na imani na kundi lake"
                         "Kwanini unasema hivyo?"
                         "Mpenzi wake mwenyewe ambaye ni mmoja wao alitaka kumuua  sasa hao waliokuwa siyo itakuwaje, na hapo ndiyo hataweza kuweka imani nao na mwishowe ni kushindwa kuendelea nao kwa hao watakaobakia baada ya fagio la chuma kupita"
                         "Haya nimekuelewa"

    Muda mfupi baadaye mlango wa gari ulifunguliwa  Salum aliingia akiwa na mfuko wa plastiki, alimkabidhi mfuko huo Norbert ambaye aliufungua kutazama kilichopo dani yake akatikisa kichwa kukubali huku akitoa tabasamu. Aliuweka mfuko huo katikati ya miguu yake na akamuamuru Saluma aondoe gari eneo hilo wawahi, zilikuwa tayari dakika ishirini zimepotea wakiwa eneo hilo wakimsubiri Salum aliyekuwa ameenda kununua kanzu na kilemba katika eneo la jirani na msikiti sunni ambao ulikuwa na wauzaji wa vitu hivyo kwa nje ya msikiti huo. Saa nne na dakika hamsini na tano au saa tano kasoro dakika tano ndiyo muda huo ulikuwa, ili wasizidi kuweka muda na kuweza kuwahi swla ya ijumaa ambayo Norbert alipanga akaswali waliamua kuondoka eneo hilo kwa kasi ya wastani ili waziwahi taa za barabarani za mtaa wa gerezani ambazo huweka sana foleni kutokana na uwepo wa askari wa usalama wa barabarani.


****

    Majira ya  saa sita na dakika arobaini na tano au saa saba kasoro robo, ndani ya msikiti maarufu jijini Dar es salam Mufti mkuu wa Tanzania alionekana akiwa ameketi nyuma ya mimbari(eneo ambalo hujengwa kama chumba jirani na eneo ambalo husimama imamu akiswalisha swala ndani ya msikiti)  hiyo akisubiri muadhini amalize adhana ya pili aweze kusimama kutoa hotuba ya siku hiyo Ijumaa. Mufti alikuwa akitazama juu yake katika eneo ambalo kulikuwa na eneo la hatibu kuweka karatasi zake anapokuwa anatoa hotuba, katika eneo hilo alijionea vipaza sauti vya televisheni na redio kadhaa ambavyo vilimfanya atoe tabasamu la ushindi akiwa anasubiri bilal wa msikiti huo amalize kutoa adhana aweze kusimama aonekane mbele ya waumini waliojitokeza katika msikiti huo kusikiliza hotuba ya swala ya ijumaa ikiwa ni sehemu ya swala hiyo.

    Mufti huyu aliamua kwenda kinyume kabisa na maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa kuitumia nyumba ya ibada tofauti inavyotumika, ni aibu iliyoje ndani ya nafsi yake lakini wala hakulionea aibu suala hilo la kuitumia sehemu ya ibada muhimu iliyofaradhishwa na Muweza wa yote kama daraja la kufikisha kile alichokuwa akitaka kifike kwa jamii ya kiislamu na watanzania kwa ujumla. Kawaida hotuba ya swala ya ijumaa ipo ndani ya swala ya ijumaa ndiyo maana swala hiyo huswaliwa kwa rakaa mbili tu, raka zingine mbili ambazo huzoeleka kuswaliwa muda wa adhuhuri ni hotuba ndiyo hufidia rakaa hizo. Hivyo hotuba ya swala ya ijumaa ni sehemu ya ibada, muda huo adhana ya pili ya ijumaa ikiwa inakaribia kumalizika Mufti alikuwa akijiandaa kutoa hotuba yake hiyo aliyokuwa ameiandaaa kwa lengo la kuhakikisha  waumini wa kiislamu wanaridhia mapinduzi haramu yaliyokuwa yameandaliwa na washirika wake. Bilal alipomaliza kutoa adhana ya pili dua baada ya adhana ilifuata na kisha Mufti huyo alinyanyuka  kwa mara ya pili tangu atoe salamu kabla ya adhan ya pili haijatolewa na kuruhusu kanzu yake safi pamoja na kilemba alichokuwa amekivaa kionekane mbele ya kamera za waandishi wa habari waliokuwa wapo msikitini  humo kuirusha hotuba hiyo moja kwa moja kwa hadhira.

   Alianza kwa kumshukuru Mungu kama hotuba nyingine zote zinavyoanza, kisha akashuhudia hapana Mola apasaye  kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezimungu na Muhammad (s.aw) ni mjumbe wake. Kutokuwa na hata haya ya kuwa huyo aliyekuwa akimshuhudia ili aeneze ujahili wake alikuwa akijua kila adhm ayake, Mufti aliendelea kuwausia waisalamu hao wamche Mwenyezi Mungu huku yeye mwenyewe akiwa hamchi mwenyezi mungu zaidi ya kumuonesha unafiki ulio dhahiri. Alijiusia na yeye katika kumcha Mwenyezi Mungu kama hotuba ya swala inamvyomtaka ajihusiw, huku nafsi yake ikimsuta amche Mwenyezi Mungu kiukweli na si kiuongo kama alivyokuwa akifanya  kwa tamaa ya pesa tu. Hotuba yake hiyo aliianza kwa kuzungumzia nafasi yao katika dini na pia kumuunga mkono mtu mnafiki na aliyechukua imani zao kwake kama silaha za kuwachapia wao wenyewe na pia kufanya kile akitakacho akiamini hawawezi kuamini wakisikia, aliianza hotuba hiyo kwa namna ya kisiasa zaidi ambapo haikujulikana alikuwa akiongelea nini hadi pale alipofika katikati ya hotuba hiyo. Hapo aliweza kuzivuta fikra za waumini waliohudhuria ibada hiyo kumsikiliza zaidi na pia kuwa na imani na kile alichokuwa akikiongelea kwa muda huo.

   Bila ya haya yoyote alitoa vifungu vya kitabu kitukufu Qurani na pia kutolea ushahidi wa hadithi huo ushetani wake aliotaka uridhiwe na wanachi wa kawaida, alikuwa akiongea kwa kihisia zaidi na kutoa vigezo hivyo kama kweli alikuwa akiongea kama kiongozi mkuu wa kiislamu katika kutoa msimamo wake juu ya masuala hayo. Ilikuwa ni hotuba iliyokuwa ni ndefu tofauti na hotuba zingine za swala ya Ijumaa zilizoeleka kutolewa ndani ya msikiti huo ambapo saa saba na robo ndiyo sehemu ya kwanza ya hotuba hiyo ilimalizika na Mufti aliinama sehemu ya mimbari baada ya kumaliza kusoma dua, alikaa sehemu hiyo ya mimbari akiwa haonekani kwa muda wa dakika takribani mbili na alipoinnuka alimshukuru kama alivyokuwa akianza kuhutubia kisha akaendelea na sehemu ya pili ya hotuba hiyo iliyokuwa ni hotuba ya kishetani iliyotumia nguvu na elimu ya Mufti katika kuwaaminisha waumini wasiotambua lolote lililokuwa likiendelea nyuma ya pazia.

   Sehemu ya pili ya hotuba hiyo ilichukua robo saa na saa saba na nusu akamalizia kwa kusoma dua kisha akamuamuru Bilala akimu swala watu waweze kuswali. Bilal alinyanyuka kwa haraka na akakimu swala na kama alivyopokea mari kutoka kwa Mufti, watu ndani ya msikiti huo walisimama kwa haraka na wakapanga safu kwa ajili ya kuswali swala hiyo tukufu inayoongozwa na Shetani aliyekuwa yupo katika umbile la binadamu. Mufti alikuwa tayari ameshatoka kwenye mimbari muda huo na alikuwa ameshikilia kipaza sauti akiwa yupo mbele ya safu ya kwanza, aliwahimiza watu wanyooshe safu zao huku akiangalia pande zote za za safu ya kwanza. Aliporidhika  kuwa safu ilikuwa imenyooka aliwasogeza watu waliokuwa wapo safu ya kwanza na akapata wasaa wa kuangalia safu ya pili huku akihimiza watu wanyooshe safu zao, baada ya kuridhishwa na unyooshwaji wa safu ya pili alirudi hadi mbele kwenye eneo maalum la kuswalisha na akakaa mbele ya mtu aliyekuwa yupo katikati ya safu kwanza kwa hatua moja.
                   "Allah akbar" Alifungua swala kwa takbira ya kurimia swala swala, alitulia kwa sekunde kadhaa kisha akasoma sura ambayo ni nguzo ya swala, swla hiyo ilichukua muda wa dakika takribani kumi ikawa imeisha. Waandishi wa habari walikuwa tayari wameshazima kamera zao na kipindi kilichokuwa kikirushwa moja kwa moja katika vituo mbalimbali vya luninga pamoja na redio ziizopo ndani ya Tanzania kilikatishwa kwa muda.

****

     Muda ambao hotuba inatolewa hadi inaisha  Norbeet alikuwa yupo ndani ya msikiti huo akiwa amevaa kanzu nadhifu sana, kilemba kilichofungwa kwa utaalamu wa hali ya juu. Kidevuni alikuwa amebandika ndevu za bandia zilizomkaa sawasawa na usoni alikuwa na sijida ya kubandika, sijida hiyo ilikuwa ni ngumu sana kujulikana kama ilikuwa ni feki kwa muumini yoyote kwa jinsi ilivyokuwa imebandikwa kwa utaalamu wa hali ya juu. Kimtazamo alikuwa hana tofauti na muumini mzuri wa msikiti kumbe kuingia kwake ilikuwa ni aghalabu sana kwa kazi maaluma kama hizo. Baada ya kutolewa salamu aliinuka kisha akafunga swala ya sunna baada ya swala, aliswali swala hiyo kisawasawa kama alikuwa ni muumini wa dini wa kiisalamu kumbe alikuwa yupo kwa kazi maalum humo msikitni. 
     Ndani ya shirika la EASA ilikuwa ni jambo la kawaida sana kwa mpelelezi kama yeye na wa daraja moja yeye kujua mambo mbalimbali ya kijamii, alikuwa na elimu ya dini zote mbili yaani ukristo na uislamu kwa daraja ambalo walikuwa nalo masheikh na viongozi wakubwa wa kanisa. Ujuzi wa elimu hii ndiyo hata ulimuwezesha kujichomeka katika kundi la viongozi wa kanisa la kiluteri katika siku ya kumpokea Askofu Valdermar uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere. Sasa ametumia elimu hiyohiyo aliyokuwa amefundishwa na akiwa katika mafunzo yake kabla hajaingia kazini katika kujichomeka katika msikiti huo aweze kuswali pamoja na waumini wa dini ya kiislamu.
    Baada ya kumaliza kuswali swala ya sunna  aliwapa mikono waliokuwa wamekaa kushoto na kulia kwake, alipowapa mkono watu hao aliweka kiganja chake cha mkono huo wa kulia kifuani mwake kisha akanyanyuka hapo alipokaa na taratibu alianza kupiga hatua akikwepa baadhi ya watu waliouwa wamekaa chini wakisikiliza maneno machache kutoka kwa Mufti baada ya swala  muhimu ya Ijumaa kuweza kuisha . Norbert alifanikiwa kutoka hadi nje ya msikiti huo na akaenda hadi kwenye eneo lenye magari mengi yakiwa yameegeshwa, aliingiza mkono mfukoni na akatoa funguo kisha akabonyeza  kitufe cha rimoti kilichokuwa kipo kwenye ufunguo huo. Gari aina ya toyota Noah muundo mpya yenye rangi nyeusi ilitoa mlio pamoja na taa za pembeni kuwaka kisha mlango ukafunguka, Norbert alienda hadi ulipo mlango wa dereva wa gari hiyo akafungua kisha akaingia akaketi kwenye kiti  na akafunga mkanda. Alitulia hivyohivyo kwenye kiti hicho kwa muda wa dakika takribani ishirini, mnamo saa saba na dakika hamsini na na tano ikiwa imepita muda wa dakika ishirini na tano toka amalize kuswali swala ya ijumaa na pia  zikiwa zimepita dakika ishirini amalize kuswali swala ya sunna. Mlango wa nyuma wa gari hiyo ulifunguliwa kwa taratibu sana, alipoangalia kwenye kioo cha pembeni upande wa kushoto alimuona mwanamke aliyevaa mavazi ya kistara zaidi akiwa na binti aliyevaa nikabu (vazi ambalo huvaliwa na baadhi ya wanawake wa kiislamu kwa kuficha uso na kuacha macho mtu).
                   "Assalaam alaykum" Mwanamke huyo alisabahi
                   "Walaykum salaam" Norbert aliitikia huku akitia lafudhi ya kiarabu ndani ya maneno yake
                   "Hee! Kijana uko makini sana mwanangu na kazi yako tofauti na yule Faraji akinileta kuswali swala ya Ijumaa kila siku. Ingekuwa yeye Wallahi tungasubiri hapa nje ya gari mpaka mawaidha yote ha watu wote msikitini ndiyo naye afuate" Mwanamke huyo aliongea huu akiingia ndani ya gari na binti huyo alifuata.
                    "Mama mimi nkajua kazi yangu hivyo siwezi kuweka usubiri, lazima nfanye haraka nno nkimaliza baadiya tu basi natoka" Norbert aliongea kwa lafudhi ya kipwani.
                  "Vizuri basi Baba tuwahishe nyumbani, wee Ilham hebu funga mkanda basi usalama kwanza" Mwanamke huyo alimuambia yule binti aliyekuja naye ambaye tayari alikuwa ameshapanda naye ndani ya gari.
                   "Mama  nawee si nipo siti ya nyuma mkanda wa nini" Binti huyo aliyekuwa akiitwa Ilham aliongea akiwa hafungi mkanda kama alivyoambiwa na mama yake.
                   "Mh! Mwana mbishi wewe haya" Mwanamke huyo alimuambia
                   "Kwanza mama mimi ninaona joto ngoja nitoe hii nikabu" Ilham aliongea.
                   "Wee tena ntolee ujinga wako umeona Majid ni harimu yako hapa, ole wako ufungue naenda mwambia baba yako. Majid baba tuwahishe nyumbani" Mwanmke huyo aliongea kumkanya mwanae kisha akamuamuru Norbert awawahishe nyumbani.

    Alikuwa ni mwanamke aliyekuwa akishikilia haswa sheria za dini hadi nyingine akazidisha ndiyo maana alimuhimiza sana binti yake kufunika uso wake ingawa haikuwa ni lazima kuufunika uso kwa binti kama huyo kwa mujibu wa sheria za kiisalmu, Norbert alipopokea amri hiyo aliwasha gari kisha akaweka gia ya  kurudi nyuma aliondoe gari hilo sehemu ya maegesho ya gari ya msikitini hapo. Utaalamu aliokuwa nao katika udereva ulimuwezesha kulitoa gari hilo hadi sehemu ya wazi miongoni mwa magari yaliyokuwa yamebanana, aliliondoa gari hilo kwa mwendo wa wastani akielekea kwenye lango la hapo msikitni.

****

        SAA MOJA BAADAYE
     Ilikuwa ni muda ambao Mufti alikuwa amemaliza kujibu maswali ya waandishi wa habari ambao walikuwa wamemzonga mbele yake pindi alipotoka msikitini tu, muda huo Mufti alikuwa yupo ofisini kwake akiendelea na kazi kama kawaida baada ya kumaliza kazi aliyokuwa amepewa kwaa sharti la kupewa donge nono na washirika wake. Alikuwa ni mwenye furaha haswa baada kutoa hotuba hiyo ambayo iliibua chuki kubwa juu ya Rais Zuber, alikuwa ametoka kutibua kabisa heshima ya Rias Zuber aliyokuwa amejijengea nchini kwa kutekeleza yale yote yaliyokuwa yakihitajika kutekelezwa na wananchi.

   Muda huo hakuwa akijua kama alikuwa amelirusha bomu la machozi kwa mtu aliyekuwa naye karibu bila ya kujiziba asiathiriwe na  bomu hilo, wala hakuwa akijua bomu hilo alilolipua basi wangetokwa na machozi wote pamoja yule mtu aliyekuwa akimlenga kumlipua na bomu hilo. Alikuja kutambua kuwa hakuwa amechukua vifaa vya kujikinga na bomu hilo baadaye, bomu hilo hadi muda huo lilikuwa halijalipuka tangu alirushe na muda huo lilikuwa likielekea kulipuka. Muda wa kulipuka bomu hilo ulipokaribia simu yake ya mkononi iliita kwa fujo hapo ofisini kwake, aliitazama simu hiyo na alipoona jina la mpigaji alitoa tabasamu kisha akaipokea kwa haraka.
            "Sema General......kama kawaida yangu nimeenda vilevile...asante sana General.....sasa kazi kwenu ndiyo imeabaki kuhakikisha huyo mtu anatoka mtawala aingie rasmi.....sawasawa mapinduzi yanawezekana hapo.....hamna shida Generala mchana mwema na wewe" Alipomaliza kuongea na simu hiyo alikata simu kisha akaiweka mezani simu hiyo na akashika faili, alianza kulipitia faili hilo  kwa taratibu na haikuchukua muda simu yake hiyo ikaita tena na muda huu namba binafsi ndiyo ilionekana ikimpigia.

    Mufti aliacha kukagua faili hilo na akaichukua simu yake ya mkononi kwa mara nyingine akaitazama kuangalia mpigaji hakuona namba yoyote zaidi ya kuona neno 'Private' likiwa limejitokeza kwenye kioo hiko, Mufti aliipuuzia simu hiyo na akiiweka iite kimyakimya huku akiendelea kupekua faili. Simu iliiita mpaka ikakatika yeye aliendelea kulipekua hilo faili alilokuwa amelishika ambalo lilikuwa na kurasa nyingi sana, simu kwa mara nyingine iliiita ambapo alichukua kisha akaitazama na alipoona ni namba ileile binafsi iliyokuwa ikimpigia aliamua kubonyeza sehemu ya kuifanya simu hiyo iite kimyakimya lakini si kuiweka simu isiweze kutoa milio kwa simu zingine zitakazoingia.. Aliendelea kupekua faili alilokuwa amelishika na akaingia ukurasa mwingine wa hilo faili, alipofika kwenye ukurasa mpya wa hilo faili aliona kitu ambacho kilimfanya anyanyue mkonga wa simu ya mezani kwa haraka sana na akabonyeza namba kwenye simu hiyo ya mezani huku mkonga akiupeleka sikioni.
                 "Assalaam alaykum Ukti..... naomba uniletee hati za viwanja vile tulivyopanga tuviuzie kwa wawekezaji.....sawa nasubiri na pia mgao wako upo tayari fanya hima uje nazo ofisini kwangu nikupatie" Alipomaliza kuingia na simu hiyo ya mezani, simu yake ya mkononi iliita tena na  safari hii akaona ni usumbufu akaipokea kwani namba ilikuwa ni ileile binafsi. Bomu alilokuwa amemrushia adui yake ili limtoe machozi muda huo ndiyo lilikuwa limelipuka, sasa machozi kutokwa  wote ni jambo la kwaida sana
                "Walaykum salaaam, nani mwenzangu....unasema nani" Aliposikia utambulisho wa mpigaji wa simu hiyo alianza kutetemeka huku mpigo ya yakimuenda mbio na alisema, "N001 nini unataka kwangu?.....Hapana Mama Ilham wangu na Ilham wamekusoea nini jamani.....no usifanye hivyo sikiliza kijana" Alipokuwa akijaribu kumuhimiza N001 ambaye  ndiye aliyempigi simu simu ilikatwa kwa ghafla.
"Halloo haloooo!" Aliongea kwa sauti lakini mpigaji alikuwa ameshakata mawasiliano tayari.



*KIMBEMBE, NINI HATIMA YAKE?
*MCHIMBA KABURI KIINGIA MWENYEWE NI KAWAIDA ILA KUTOKA NI MAJALIWA, JE HUYU KATOKA?
*N001 AITWA MAJIDI JAMANI, KAFANYA NINI TENA?

USICHOSHWE SANA NA  MANENO YA MWISHONI WA SEHEMU YANAYOKUUULIZA MASWALI, SEHEMU YA THELATHINI NA NANE NA KUENDELEA  NDIYO JIBU LAKO USIKOSE.




No comments:

Post a Comment