Monday, January 23, 2017

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA AROBAINI NA NNE


RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________





 
****SEHEMU YA AROBAINI NA NNE****



<<<<SEHEMU YA MWISHO TOLEO LA KWANZA>>>>>    


      Yeye ndiye alikuwa akitoa amri kuu baada ya Rais Zuber muda huo ndani ya ikulu  hakukuwa na mwingine yeyote aliyekuwa akipinga amri zao, muda huo walikuwa wakiangalia mazingira ya hapo ndani ya ikulu kwa umakini sana kuhakikisha hakiharibiki kitu.

                 "Mheshimiwa usiwe na shaka kabisa ndani ya usiku huu, ikiwa kama operesheni fagio la chuma ndiyo ilikuleta wewe Rais mzalendo kabla hata haujafanyika uchaguzi mwingine ambao ulikupatia ushindi vilvile. Basi operesheni hii itahakikisha utaendelea kubaki madarakani kwa miaka mitano yako awali na hadi ukigombea tena ukipata ushindi" Moses aliongea huku akimshika Rais Zuber bega.






__________TIRIRIKA NAYO

   Tabasamu hafifu ndiyo lilimtoka Rais Zuber baada ya kupokea maneno hayo kutoka kwa Moses  aliyekuwa yupo naye bega kwa bega kwa kipindi kirefu sana,imani ya kuwa vijana wake bado wapo pamoja naye ndiyo ilizidi kujengeka kwa muda huo.

   Mawasiliano kati yao na vijana wao waliokuwa nje ndiyo yaliyokuwa yakiendelea kwa muda huo waliokuwa wapo kwenye kila pande ndani ya Ikulu hiyo, kila kitu kilikuwa kinaenda sawa na salama kama kilivyokuwa kimetakiwa kwenda. Jambo hili lilimfanya ndiyo azidi kuwa na imani ndani ya moyo wake wakupata ushindi ndani ya muda wa uuliopangwa ukifika, wasiwasi kidogo wa kushindwa nao haukuacha kabisa kumzonga ndani ya muda huo. Hakuwa mwenye kujiamini kwa asilimia mia moja kuwa alikuwa akielekea kufanikiwa na kurudi katika hali ya kawaida ya kuaminiwa na wananchi wake waliokuwa na mapenzi makubwa naye hapo mwanzoni. Kila alipokuwa akifikiria uwepo wa wanajeshi wa kikosi cha maji alikuwa na wasiwasi mkubwa sana wa kuendelea kusalia madarakani, hofu aliyokuwa nayo juu ya kikosi hicho ilikuwa ni kutokea kwa upinzani mzito sana kati ya kikosi hicho na kile kilichokuwa kinamtetea yeye. Aliona upinzani huo ungeweza kusababisha vita ndani ya eneo hilo kwani kila kikosi kilikuwa kimejiandaa vilivyo katika eneo hilo.

   Alibaki akimuomba Muumba ndani ya moyo wake aweze kupita katika wakati mgumu,muda huo vijana wake walikuwa wapo makini sana katika kupeana traarifa ya kile kinachoendelea nje ya eneo hilo na hata ndani ya eneo hilo kuhakikisha kuwa hakuna kinachoharibika ikiwa wao wapo ndani ya eneo hilo.

   Ulinzi ulikuwa ni wenye kuridhisha ndani  ya eneo hilo la ikulu na hata nje ya eneo kwa maaskari wa JWRZ kikosi cha ardhini, mawasiliano ya siri ndiyo yalikuwa yanaendela baina yao na utumiaji wa vifaa vya mawasiliano vyenye kujilinda visiingiliwe ndiyo ulikuwa ukitumika wakiwa wapo ndani ya eneo hilo kuhakikisha kuwa hakuna kinachoharibika.

   Viongozi wa vikosi katika pande zote mbili walikuwa wakiwasiliana kila muda, Moses na M.J Belinda bado hawakuacha kuwasiliana wakiwa wapo ndani ya maeneo tofauti kuhakikisha kuwa hakuna kitakachoenda  vibaya ndani ya muda huo.


****

   
   SAA TANO KAMILI USIKU

     Taarifa ya kuuawa kwa Mufti ilisambaa kama moto wa kifuu baada ya kuwafikia wanahabari waliokuwa  wapo nje ya wodi hiyo, habari ya kujeruhiwa maaskari waliokuwa wapo katika eneo hilo wakilinda maisha ya Mufti nayo ilisambaa kwa muda mfpi tu kutokana na upanuzi mkubwa wa vyomba vya habari nchini Tanzania. Hadi inatimia muda huo hakuna mtu kutoka ndani ya Tanzania ambaye alikuwa hajajua kile kilichokuwa kimetokea ndani ya hospitali ya Aga kahan kukiwa na ulinzi mkali wa polisi  waliokuwa wanahakikisha hapatwi chochote.


    Lawama zote waliangushiwa maaskari wa jeshi la polisi waliokuwa wapo katika eneo hili wakilinda usalama wake, kila aliyekuwa akitumia mitandao wa kijamii alikuwa akililaumu jeshi la polisi kwa uzembe waliokuwa wameufanya hadi auawe akiwa yupo katika mikono yao. Hakuna aliyekuwa akijua kuwa polisi hao walikuwa wakipambana na mwanamke mwenye uwezo zaidi yao hivyo aliwazidi ujuzi na kuweza kumuangamiza Mufti.

    Wale waliokuwa wakitambua juu ya jambo hilo hawakuweza kabisa kuwalaumu askari hao, wale ambao hawakuwa wakijua kile kilichokuwa kimetokea ndani ya hospitali hiyo na wala hawakuwa wakijua chochote juu ya muuaji huyo walibaki wakitumia mitandao ya kijamii kama sehemu za kumwaga tuhuma zao. Walibaki wakituma vifungu vya maandishi vile walivyokuwa wakivijua wao vichwani mwao kwakuwa mitandao hiyo ilikuwa na sehemu inayowauliza kile kilichopo ndani ya mawazo yao.


   Taarifa hiyo ilikuwa ni sherehe kubwa sana kwa Waziri pamoja na Mzee Ole bada tu ya kuipokea kutoka kwa Josephine aliyekuwa tayari amemaliza wajibu wake ndani ya hospitali hiyo, walishangilia sana walipokuwa wapo ndani ya nyumba ya waziri huyo baada ya taarifa hiyo kuwafikia. Sasa walijiona wapo  huru zaidi baada ya taarifa hiyo kuweza kuwafikia, hofu ya kuumbuka ilikuwa imeshapotea kabisa kwa waziri huyo ambaye alikuwa na shaka sana na heshima yake aliyokuwa amejijengea akiwa yupo ndani ya wizara yake. Hakuwahi kuhisiwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye nia mbaya sana  na nchi hii, hata kwa Rais Zuber alikuwa ni miongoni mwa mwaziri wake aliokuwa akiwaamini tangu ateuliwa kuwa Rais kabisa baada ya kuwa rais wa mpito kwa muda wa miaka kadhaa tangu alipopinduliwa Mzee Ole na jeshi.

                  "Sasa roho nyeupe kabisa" Waziri alisema  huku akiwa na tabasamu usoni

                  "Mambo hayaharibiki ikiwa Josephine yupo, sasa tusubiri ya Wilson" Mzee Ole naye alimuambia.

                  "Wilson baada ya kumpiga risasi naye sijajua aliishia wapi maana taarifa sijaipata"

                   "Nafikiri tumngojee aweze kurejea maana simu yake haipatikani hadi muda huu"

                   "Mdogo wangu namjua mimi itakuwa kazima simu baada ya kufanya tukio akiwa na wenge la tukio alilolifanya"

                   "Hata mimi nahisi hivvyo, sasa kesho tuchukue nchi tupate mpunga wetu"

                   "Hilo ndiyo lilobaki tu Waziri mkuu wangu, wananchi wakilalamika sana ni kuwaletea maendeleo kama ya Afrika ya kusini kwa mwaka mmoja tu watakuwa na imani na sisi"

                     "Kabisa Rais wangu ni muda wa wewe kuwafanya waamini walikuwa wakikuhitaji rais kama wewe,watanzania ni kama kuku tu hawawezi kukumbuka mahali walipopigwa jiwe wakati anakula mchele hivyo hurudi tena"

                      "Sasa hizo akili zao ndiyo iwe mbinu ya kuweza kuwakamata kisawasawa"

                      "Kabisa Mheshimiwa Rais"

                      "(Mzee Ole aliposikia anaitwa Mheshimiwa Rais laicheka) ndiyo ushaanza kunipa cheo mapema yote hata kiapo sijaapa kwa mara nyingine"

                      "Sasa si tayari umepita, bado saa moja tu Ikulu yote isafishwe ile na Zuber atoke"

                      "Na kweli sasa hizi yupo kitimoto huko kama kasikia ni waziri wake anahusika na kumsaliti basi atamuhisi wa fedha maana hawakai meza moja kabisa"

                       "Mimi hawezi kunihisi kamwe maana ananiamini sana kumbe uaminifu wangu kwake ni silaha, Mheshimiwa Rais mkumbatie adui ndiyo utammaliza kirahisi na mimi nafanya hivyohivyo"

                       "Mbinu nzuri sana hiyo, ndiyo atakuja kujua kuwa umdhaniaye ndiye kumbe siye"

                       "Ndiyo atajua si kila kizungusho kilichosimama na namba moja ni sifuri niyngine ni herufi O"

                      "Yeye kaona kimiminika cheupa akajua ni maziwa nyingine ni uji wa chokaa ukiugeuza kinywaji kinakuua"

                      "Kabisa Mheshimiwa Rais ndiyo atajuta kuwa na ukaribu nami akijua ni mzalendo mwenzake wa kukataa pesa,uzalendo wa sasa ni kuikubali pesa kwa namna yoyote ile kwani ndiyo kila kitu"

                      "Upo sahihi kabisa waziri mkuu wangu, hebu mpigie Wilson kwa mara nyingine kama atakuwa hewani mwambie asikawie huko kuna Norbert anaweza kumuingiza kwenye anga zake"

    Waziri alichukua simu yake ya mkononi kwa mara nyingine akampigia Wilson akijua ataweza kuwa hewani aongee naye, muda huo hakuna kati yao aliyekuwa akitambua kuwa Wilson tayari ni marehemu. Wala hakuna aliyekuwa akitambua tayari Norbert waliyekuwa wakidhani bado hajamuweka Wilson kwenye anga zake tayari alikuwa amemuweka kwenye anga zake, tayari alikuwa amemuangamiza.

    Mzee Ole alijua ni hofu tu aliyokuwa nayo mdogo wake ndiyo maana alikuwa amezima simu yake, simu ya Wilson haikuwa hewani kabisa kwa muda huo waliokuwa wakimpigia na kila wakijaribu kwa mara nyingine majibu yalikkuwa yaleyale. Wote walishangazwa na hali ile maana haikuwa kawaida kwa Wilson kuzima simu kwa muda mfefu tangu awepo kwenye kazi kama hizo.

                      "Aisee hapatikani tena kuna nini?" Waziri aliuliza swali lisilo na jibu kwao wote

                       "Hebu mpigie Leopard Queen umuulize huenda akawa na jibu" Mzee Ole alimtoa hofu, Waziri alipiga namba ya Josephine muda huohuo.

    Simu hiyo iliiita  kwa muda mfupi tu na kisha ikapokelewa,hapo aliweza kutuliza hofu aliyokuwa nayo kwao na akaona ni muda huo wa kumuulia juu ya Wilson.

                       "Leopard Queen Wilson yupo wapi?......Unamaamisha nini kuniambia hujui inamaana hukuwa naye huko?......Alitoka baada ya kufanya tukio lake na wewe ukabaki ndani......je wewe umeongea naye hata kwa simu baada ya tukio hilo?....,,Ok fanya haraka urudi Ngomeni Mzee Ole anakuja hukohuko sasa hivi" Waziri aliongea baada ya simu yake kupokelewa na Josephine, alipokata simu hiyo alimuangalia Mzee Ole kisha akatikisa kichwa ishara ya kukataa.

                      "Vipi mbona hivyo?" Mzee Ole aliuliza

                      "Hata Leoprad Queen anasema hajamuona na wala hampati kwenye simu"

                      "Ok inabidi sasa niende Ngomeni nikamtazame huenda amerudi na ameamua azime simu kutuliza kichwa si unajua huyu mdogo wangu akifanya tukio lolote huwa anapenda asiwasiliane na mtu na kisha hunywa pombe sana"

                      "Sawa Mheshimiwa Rais wewe nenda ngomeni sasa hivi kamuangalie, utakutana na Leoprd Queen hukohuko"

                      "Sawa tuonane kesho ikulu"

    Mzee Ole hakutaka kupoteza muda alitoka ndani ya nyumba hiyo na akaingia ndani ya gari lake alilokuwa amekuja nalo katika eneo hilo, lango la nyumba hiyo lilifunguliwa na gari hilo likatoka kwa mwendo wa wastani sana na likaongeza mwendo baada ya kuingia barabara kuu.


****


  SAA  TANO NA NUSU

    Habari ya kugundulika mtu aliyempiga risasi ambaye ni mfanya biashara maarfu na pia mdogo wa aliyekuwa Rasi wa Tanzania Mzee Filbert Ole,  ilivuja kwenye mitandao ya jamii kwa muda mfupi tangu polisi wafanikiwe kujua juu ya uwepo wa mwili wake pamoja na vifaa alivyovitumia kwenye tukio hilo.

     Kupitia kwa waandishi wa habari wa kujitegemea haikueleweka habari hiyo ilikuwa imegunduliwa na nani kwani polisi walikuwa wamefanya kwa usiri sana kuuleta huo mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Aga khan. Maaskari hao wa jeshi la polisi walishtuka kusambaa kwa habari hiyo ambayo ilikuwa imechukuliwa ni usiri mkubwa sana, habari hiyo ilianza kugunduliwa na wauguzi wa hospitali hiyo ambao walikuwa wengi wao hawajui juu ya mtu aliyeuawa ufukweni. Wauguzi hao waliipata habari hiyo kwenye simu zao za mikononi ambapo walishangazwa sana na taarifa hiyo, habari hiyo ilienea sana na hatimaye hata ikawafikia IGP Chulanga na DCP John waliokuwa wapo kwenye chumba maalum cha hospitali hiyo wakifanya mahojiano na Askari polisi aliyekuwa akimlinda Mufti ambaye tayari alikuwa ameshazinduka hadi muda huo.

                 "Hizi taarifa zimevuja vipi jamani?" IGP Chulanga aliuliza muda huo ambao tayari walikuwa wameshaanza kumuhoji Askari huyo.

                 "Mkuu tuendelee na mahojiano huenda ni Norbert Kaila yupo kazini si unajua nchi hii hakuna mwandishi mwenye ujanja katika kusaka habari kama yeye" DCP John alimuambia

                 "Huenda itakuwa ni yeye, mwandishi wa habari ni mjanja sana huyu, ok tuendelee naye" IGP  Chulanga alikubali wazo la DCP John.

                  "Private Fred ukimuona huyo msichana unaweza kumkumbuka?" DCP John aliuliza

                  "Ndiyo ninaweza kumkumbuka mkuu" Private Alfred aliyekuwa na jukumu la kumlinda Muti aliongea

                  "Ok nadhani tuna mtalamu wa kuchora katika hao vijana hebu aitwe mara moja" IGP Chulanga aliposikia hivyo alitoa amri, DCP John kwa haraka alitoa simu yake ya upepo akatoa amri hiyo kisha wote wakawa wameacha kumuhoji wakiwa wanamsubiri Askari huyo aweze kufika.

      Baada ya dakika tano mlango wa chumba walichokuwepo ulifunguliwa, aliingia askari mwenye cheo cha Inspekta ambaye alitoa saluti alipomuona IGP katika eneo hilo.

                    "Karibu Inspeka" IGP Chulanga alimkaribisha

                    "Asante mkuu" Inspekta huyo aliitikia

                   "nahitaji usikiliza maelezo ya Private hapa na kisha uchore sura ya mtuhumiwa atafutwe kuanzia hivi sasa" IGP Chulanga aliongea

      Hakukuwa na muda wa kupoteza Askari huyo alianza wajibu haraka sana, karatssi pamoja na kalamu ya risasi vililetwa, muda huo huo Pirvate Fred alianza kutaja sifa na muonekano wa mtuhumiwa kama alivyoapata kumuona muda mfupi ulipita ambao alimshambulia hadi akapoteza fahamu. Haikumchukua muda mrefu sana kazi hiyo ikawa imekamilika kabisa mchoro huo ulioneshwa kwa Private Fred ambaye alishtuka na akashangaa sana alipouona mchoro huo.

                             "Private ndiye huyo" IGP Chulanga aliuliza baada ya mchoro huo kukamilika.

                              "Kabisa mkuu ndiye yeye huyohuyo" Private Fred alijibu

                              "Una uhakika ndiyo yeye?" IGP Chulanga aliuliza tena

                              "Ndiyo mkuu nina uhakika" Alijibu.

                              "Itazame vizuri tena halafu uniambie je una uhakika ndiyo yeye" IGP Chulanga alisema na Private Fred aliitazama picha kwa umakini sana kisha akatikisa kichwa kukubali.

                               "Ndiyo mkuu ni yeye" Alijibu vilevile

                               "Ok kuanzia hivi sasa wauguzi wa hospitali nzima wakusanywe, milango ya hospitali ifungwe hakuna mtu kungia wala kutoka" IGP Chulanga alitoa amri hiyo akiamini kuwa muuaji hakuwa ametoka ndani ya hospitali hiyo hadi muda huo, hakujua kuwa tayari alikuwa ameshachelewa hadi anatoa uamuzi huo ndani ya muda huo kwani Jospeine huyo aliyekuwa akionekana kwenye mchoro alikuwa ameshatoweka ndani ya eneo hilo.

                                "Mkuu" Wote waliitikia na muda huo huo simu za upepo zilitumika kuwapa taarifa maaskari waliokuwa wapo ndani ya eneo hilo la hospitali, milango ya hospitali hiyo ilifungwa mara moja na ulinzi katika maeneo ya ndani ya  hospitali hiyo uliimarishwa mara dufu.

     Wauguzi wa hospitali hiyo pamoja na madaktari walikusanywa sehemu moja kwa haraka sana, maaskari wa jeshi la polisi waliznguka kila uapnde wa hospitali hiyo kuhakikisha kuwa hakukuwa na muuguzi yeyote aliyekuwa anasalia katika chumba au wodi yeyote.

      Muda huo wodi zote na vyumba vya ofisi za wauguzi na madaktari zilibaki tupu kabisa na hakukuwa na yeyote aliyebakia, wote walikuwa wamekusanywa kwenye chumba maalum cha mkutano ndani ya hospitali hiyo. Wote waliketi kwenye viti chumbani hapo wakiwa hawajui kile kilichokuwa kimefanya hadi wakaitwa katika eneo hilo.

      IGP Chulanga pamoja na DCP John waliingia katika eneo hilo wakiwa wapo pamoja na Daktari mkuu kisha wakawasalimu watu ote waliokuwa wapo katika eneo hilo, madaktari pamoja na wauguzi wote waliitikia salamu hiyo wakiwa na hofu sana juuu ya kukusanywa kwao huko ndani ya muda huo tena kwa ghafla sana wakiwa hawalelewi chanzo cha wao kukusanywa hivyo katika eneo hilo ni nini haswa.

                   "Kuweni na amani ndugu zanguni najua wote mna hofu sana juu ya kukusanywa huku kwa muda huu, ni zoezi dogo sana lililofanya tuwakusanye namna hii na zoezi hili linahitaji sana ushrikiano wenu katika kulikamilisha. Muda mfupi uliopita Mufti mkuu wa Tanzania ameuawa akiwa wodini amelazwa tena aliyemuua alikuwa amevaa mavazi ya kiuguzi na pia akiwa na kitambulisho kabisa. Sasa basi hatujapata uhakika kabisa wa kuweza kusema kuwa muuguzi ni mmoja kati yenu au kajichomeka katika kundi lenu. Hivyo kuna karatasi zina mchoro wa sura ya huyo muuaji  zimepigwa photocopy na zitapita kwenu kila mmoja, hivyo naomba ambaye atakuwa anamtambua mwanamke huyo anyooshe mkono mara moja" IGP Chulanga aliongea, muda huohuo ndani ya chumba hicho waliingia maaskari wenye karatasi ambazo walizisambaza kwa wauguzi na madaktari wote ndani ya  chhumba hucho kwa haraka sana.

      Haikuchukua hata dakika tano toka karatasi hizo zisambazwe, kikundi cha wauguzi wa kike ambacho ndiyo kilikuwa kinaongea na Josephine wakati Mufti akiongea na waandishi wa habari walinyoosha mikono yao kwa pamoja. Baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo nao walinyoosha mimono yao kuonesha kumtambua Josephine.

                     "Ok mliomtambua huyo  itabidi mfanyiwe mahojiano,kaeni upande huu" IGP Chulanga alitoa amri na waguzi pamoja na madaktari hao wakasogea katika upande ambao walikuwa wameambiwa wakae kwa muda huo.


****


  SIASA NAYO NDANI

     Kitendo cha polisi kuzidiwa ujanja na Josephine hadi akafanikiwa kumuua Mufti ilikuwa ni nafasi nyinge kabisa ambayo ilivyokewa ni kama ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu sana na mwanachama wa chama cha upinzani ambacho kilikuja kushika kasi sana baada ya kufutwa kwa chama cha PTP kilichokuwa kikiongozwa na Fibert Ole. Chama hicho cha siasa kilikuwa kipo chini ya mwanasiasa Simon Leonard aliyekuwa akihaha kwa kila namna aweze kupata wafuasi wengi katika kipindi hiko aweze kumtia presha Rais Zuber Ameir, taarifa hiyo ya kuzidiwa ujanja yeye aliiona kama ilikuwa ni njia pekee ya kuweza kuwashutumu polisi ili aweze kujichukulia wafuasi.

    Taarifa hiyo ilipofika kwenye mikono yake kitu cha kwanza alichokifanya ni kufungua katika kurasa zake za mitandao mbalimbali, alishusha lawama kwa polisi  kuuawa kwake Mufti. Simon alijionesha ni namna gani alivyokuwa ameguswa sana na suala hilo, huku akimuita Mufti mtu aliyekuwa amejitolea muhanga kuweza kuwaumbua madhalimu wa taifa hili. Alishutumu sana jeshi la polisi kwa kuacha hadi akauawa kwa kutumia maneno dhanifu ambayo yalikuwa yapo ndani ya ubongo wake, katika shutuma hiyo aliweza kutengeneza tuhuma nyingine kwa kutumia kigezo cha jeshi la polisi kuwa ni chombo cha serikali.

    Aliihusisha serikali nzima huku akitaja serikali iyo ilikuwa imewaajiri   maaskari wasio makini kabisa kwa kazi zao hadi Mtuhumiwa anauawa kwenye mikono yao, katika kurasa zake muda huo alikuwa ameandika makala hiyo ambayo kwa siasa zaidi alimlaumu hata IGP kwa kuwa na maasakri wa aina hiyo. Kulaumu huko kulienda hadi akamlaumu waziri wa mambo ya ndani kwa kuwa na IGP aliyepo chini ya wizara yake ambaye hayupo makini kwa vijana aliokuwa nao, bado hakuishia hapo Simon alipeleka lawama hadi kwa Rais Zuber kwa kuteua Waziri ambaye anafuga wazembe waliopo chini ya wizara yake. Mwansiasa hiyo alipotuma makala hiyo haikuchukua muda watu waliisoma sana, wale waliokuwa na kawaida ya kunakiri walifanya hivyo wakawatumia kila mmoja wao.

    Wapo waliompa sifa kwa kuliona suala hilo na wapo pia waliokuwa wakimsema vibaya wakimuambia kuwa alikuwa akitaka umaarufu kupitika migongo ya watu. Asilimia kubwa ya wanachi bado walikuwa na uchungu kwa kuweza kuwafanyia mabaya watu muhimu ndani ya nchi yao ikiwemo Rais Zuber aliyeleta mafanikio kwa muda aliokuwepo madarakani, hivyo ilikuwa ni kama alikuwa akiwazidisha uchungu wale wasio na ustahimilivu na wale wasio na staha walimtukana kabisa.

     Maoni ya watumiaji mbalimbli wa mitandao ya kijamii Simon alikuwa akiyasoma akiwa yupo na tarakilishi yake pambeni akiway upo mke wake chumbani kwake, matusi hayo hayakumkasirisha ndiyo kwanza yalimfanya atabasamu tu hadi mke wake akashangaa.

                "Haya mwenzangu kipi kinachokufanya utabasamu kwa kashfa na matusi ya hao" Mke wake alimuuliza.

               "Wafuasi wanakuja kwa kutukanwa sana kuliko hata kusifiwa" Simon alimuambia.

                "Kivipi?"

               "Huyu aliyenitukana sasa hivi ataenda kumuambia mwingine juuu ya makala yangu na jinsi ilivyomchefua, unajua ni nini kinafuata hapo? Huyo aliyepewa taarifa atatamani kuisoma na yeye aijue na ndiyo hapo wananiletea wafuasi tu,kwani si kila atakayeisoma atakuwa na hisia sawa wapo wataovutika nayo na kuwa wafuasi wangu wataniona ninajali sana"

             "Mhh! Kweli hiyo siasa sikuwezi we mwanaume"

             "Huu ni mchezo mchafu tuachie tunaouweza usiouweza kaa kando"

              "Haya ngoja mi nilale mwanasiasa endedelea"

              "Ukiamka utakuta magazeti tayari wamechapisha hiyo habari huku wanahabari wamenikosoa kabisa"

              "Ujiandae kwa hilo"

               "Watakuwa hawanibomoi bali ndiyo kwanza wananijenga na watakuwa wanafanya kazi ya kufuatilia makala zangu online waweze kupata habariza kuuza, wanapata hela kwa maneno yangu huku wananuongezea wafuasi tu" Simon alimaliza kuongea maneno hayo na akafunika tarakilishi yake ya mapakato kisha akajitupa kitandani pamoja na mke wake, alikuwa akitumia akili ya kisiasa ambayo aliona kabisa ilkikuwa ikielekea kumpa mafanikio kwa muda huo huo hadi miaka kadhaa mbele kwenye uchaguzi mkuu wa Tanzania.

   Hakujali kutukanwa wala kukosolewa alichojali yeye ilikuwa kujiongezea wafuasi tu kwenye chama chake kichanga ambacho kimevitingisha vyama vingine tangu akianzishe, alikuwa ana lengo moja tu la kukitingisha chama tawala tu na ndiyo juhudi ameanza.


*MWANASIASA KATIKA SIASA

*JOSEPHINE ABAINIKA

*JE MAPINDUZI YA KIDHALIMU YATATIMIA?


MATOLEO MAWILI YA MWISHO NDIYO YALIYOBAKI TU NA YATAKUPA MAJIBU USIKOSE KUWA PAMOJA NA MWANDISHI.










No comments:

Post a Comment