Thursday, November 19, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA PILI









DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



 SEHEMU YA PILI!!
"we mwanaharamu wewe simamisha gari nishuke sio kuongeza mwendo" Yule mwanamke alizidi kufoka baada ya kuona mwendo wa gari unazidi kuwa mkali, dereva hakumjibu yule yeye alitoka kwenye usukani akasimama kisha akawaangalia wafanyakazi wa idara nzima akiwa na hofu.
"si mimi ninayeendesha jamani gari linaenda lenyewe hili hebu oneni" Dereva aliongea huku akiwaonesha wafanyakazi wote jinsi usukani ulivyokuwa unajiongoza wenyewe, wafanyakazi wote walipoona hicho kioja walijikuta wakijaribu kutoka nje lakini walishindwa kwani milango haikufunguka na vioo vyote vilijifunga ghafla hata vile vilivyokuwa wazi vyote vilijifunga. Wafanyakazi wote walijaribu kupiga vioo ili wavunje lakini walishindwa kwani vioo vilikuwa vigumu sana, gari nayo ilizidi kuongezeka mwendo hadi ikawa kama ipo kwenye mashindano.



****

 Makelele ya woga ndiyo yalitawala kwa watu wote kasoro kijana mmoja ambaye ni mmoja kati ya wafanyakazi wa idara hiyo ya kampuni ya Extoplus, yeye alikuwa kauchapa usingizi na wala hakunekana kama anatambua kuna tatizo, mwendo wa gari ulivyozidi kuwa mkali ilibidi wamuamshe huku wakimpigia kelele hadi akaamka. Kijana huyo alipoamka alionekana kukerwa na sauti za watu waliokuwa wanampigia kelele, kisha akalala tena akionekana kazidiwa na usingizi.
"We Saleh hebu amka si tupo kwenye hatari we unalala,.amka tusaidiane kutoka ndani ya gari hili tutakufa wote" Yule mwanamke aliyekuwa aking'ang'ania kushushwa alipaza sauti kumuambia yule kijana aamke aache kulala wapo hatarini, yule kijana aliinua kichwa mara ya pili akiwa anaonekana kama mtu ambaye alikuwa hajalala na hana dalili ya kusinzia. Saleh alikuwa amejawa na tabasamu alipoinua uso wake hadi wenzake wote wakawa wanamshangaa sana, wenzake walipozidi kumtazama kwa hofu yeye aliangua kicheko kabisa akionekana kufurahishwa na hofu ambayo imevamia nyuso za wenzake. Alipoona wamezidi kumshangaa aliamua kuwaambia, "mtakufa nyinyi ila sio nitakufa mimi". Kauli hiyo ilizidi kuwashangaza sana wenzake waliokuwa wana hofu na kifo, wote walimuona kama mtu aliyechanganyikiwa kwani si jambo la kawaida kwa mtu mwenye akili timamu kutamka maneno hayo katika eneo la kuelekea kwenye mlango wa kifo.
"We Saleh ni wewe kweli tunaokujua ni muoga au umechanganyikiwa tayari?" Mwanamke mwingine aliyekaa pembeni yake alimuuliza akionekana kuchanganywa na kauli ya Saleh.
"ushasema Saleh ni muoga sasa, utaulizaje ni Saleh au siyo wakati unaona kabisa mimi  siyo muoga, labda jibu la kukusaidia ni kwamba Saleh yupo nyumbani kwake Mikanjuni amepumzika baada ya kuota ndoto iliyokuwa na onyo juu ya safari hii aliyoizingatia lakini nyinyi mnaojifsnya wapuuzaji wa mambo kisa elimu zenu leo utakuwa mwisho wenu" Yule kijana  aliyesadikika kuwa ni Saleh alianza maneno yaliyozidi kuwashangaza wafanyakazi wote pamoja na dereva wa gari. Mwanamke mmoja aliyekaa pembeni yake yule kijana  akiwa upande wa dirishani aliamua kumtandika makofi mawili mazito ya mashavu huku akisema, " hebu amke Saleh nahisi umelala bado".
"Nishaamka tayari ngoja nikulaze wewe sasa ulale milele" Yule kijana aliongea kisha akampiga yule mwanamke ngumi moja ya kichwani juu kidogo ya sikio, ngumi hiyo ilitoboa kichwa cha huyo Mwanamke na ubongo wake uliochanganyika na damu ukaruka hadi kioo cha dirishani na kuibadilisha taswira ya eneo la karibu na hapo kuwa damu  na madonge ya ubongo yakiwa yameruka  hadi kwa wengine waliopo jirani na endo hilo. Mayowe ya uoga yalizidi ndani ya gari hilo huku watu karibia wote wakitamka majina ya mama zao kutokana na tukio waliloliona, Yule kijana alipoona makelele yamezidi aliamua kunyanyuka akawatazama wafanyakazi huku macho yake yaking'aa kama macho ya paka. Mikono yake ilianza kutoa kucha ndefu kama za Simba na sura yake ikabadilika ikawa ya kutisha, mabegsni alitoa mabawa kama ya popo na kinywaji akawa anatoa cheche za moti pamoja na mngurumo unaoashirua hasira.
"Kwa jina la yesu pepo mchafu usiyehitajika tokaaaaa!" Mwanaume mmoja ambaye alikaa kiti cha nyuma kabisa alipaza sauti  huku akimnyooshea  mkono yule kijana ambaye muda huo alikuwa amegeuka kiumbe wa ajabu, Yule kiumbe aliangua kicheko huku akimtazama yule Mwanaume kwa jinsi anavyobabaika kukemea kama Mlokole.
"Ha! Ha! Ha! Ha! Yaani kila siku unashinda bar ukinywa pombe  na unamuasi Mungu kwa kila unachokifanya na Kanisani kwako ni kama kituo cha polisi kwa teja ndiyo utegemee ukikemea nitaondoka. Mungu hasaidii watu kama nyinyi ambao mmeshindwa hata kumtaja mkiwa  na tatizo . Mnashuhudia huyu mwenzenu nikimuua na mmekimbilia kuwataja mama zenu kama ndiyo mnaowaabudu. Sasa naanza na wewe unaejifanya kimbelembele sana" Yule kiumbe aliongea kisha akamnyooshea mkono yule Mwanaume aliyekuwa anakemea, yule mwanaume alijikuta akivutwa kuufuata ule mkono kwa kasi ya ajabu na alipoukaribia mkono wa yule kiumbe aliachiwa pigo moja takatifu lililomgawanya vipande viwili mithili ya papai linalotayarishwa kwa ajili ya kutolewa mbegu ili liliwe. Tukio hilo lilishuhudiwa na kila mmoja humo ndani na hadi wanashuhudia vipande vya mwili vya yule mwanaume vikianguka chini tayari mwanamke aliyekaa kitu kilicho jirani na yule kiumbe alikuwa ameshapoteza fahamu papo hapo kutokana na mshtuko wa moyo na akaanguka jirani na miguu ya yule kiumbe akiwa hajitambui, yule kiumbe alimtazama yule mwanamke kisha akaachia pigo la kutumia mguu wake lililoshuka kwemye shingo ya yule mwanamke hadi kichwa kikaruka na damu zikaanza kusambaa ndani ya gari ikiweka taswira isiyopendeza.
"huyu peke yake ndiyo kafa kifo cha kistarabu akiwa hana fahamu ila nyinyi mtakiona cha mtema kuni" Yule kiumbe aliongea kisha akanyanyua mikono yake juu, watu wote nao walienda juu wakajipigiza kwenye paa la gari hiyo. Yule kiumbe alipoirudisha mikono yake chini watu nao walirudi chini wakijipigiza kwenye sehemu za juu viti ambazo hutengenezwa kwa chuma kilichovikwa godoro gumu. Sauti za kuvunjika kwa viungo vya ilisikika walipojipigiza kwenye viti huku mayowe ya maumivu yskitawala ndani ya gari  ambayo yalimfanya yule kiumbe apeleke mikono yake juu na chini kwa haraka na watu walizidi kujibamiza kwenye paa na kwenye viti.
Waliendelea kubamizwa hivyo kwa mara nyingi hadi wakawa wamevunjika kila viungo vya miili yao na wakawa hawawezi hata kunyanyuka, baadhi ya wafanyakazi walikuwa kwenye hali mbaya kwani mifupa yao mingine iliyovunjika ilikuwa imetoka nje ya miili iliyowaletea maumivu makali yaliyowafanya walie kama watoto wadogo.
"Sasa nyinyi wa kupuuzia mambo nataka mfe huku mjiona kwa kuungua moto" Yule Kiumbe alisema huku akiwasha moto kwenye kiti cha mbele pembeni ya dereva halafu akatoweka huku gari likizidi mwendo kuliko uwezo wa mwendo wake.
Gari hiyo aina ya toyota coastar ilikuwa imeshafika maeneo ya Bwaga Macho ambapo mbele kulikuwa na gari kubwa la mafuta likitembea kwa mwendo wa tararibu sana kutokana na uzito uliolielemea, gari iliyobeba wafanyakazi ilienda kugonga gari la mafuta kwa nyuma na kupelekea gari tanki la mafuta litoboke na mafuta yavujie ndani ya gari lililobeba wafanyakazi ambalo tayari moto ulikuwa unaunguza kiti cha mbele.
Kilichofuata hapo ulikuwa ni mlipuko mkubwa hadi gari zote mbili zikarushwa juu huku zikiteketea, zilipotua chini ziliteketea zote hadi zikabaki mabati tu kutokana na kikosi cha zima moto kuchelewa kufika eneo hilo vikitokea Chumbageni wilaya ya Tanga.

 Ilikuwa kizaazaa kilichozaa vizaazaa vingine kwani wakati tukio hilo linatokea hilo linakaribia kutokea tayari waganga wa jadi wa eneo lote la Bwaga Macho walishaona kwamba kuna kiumbe wa ajabu aliyekuwa anawatesa wanadamu ndani ya gari, walihitaji kuwakomboa wanadamu waliopo ndani ya gari hiyo kwa kupambana na kiumbe hicho. Wakati yule kiumbe anaweka moto kwenye kiti cha ndani ya basi la wafanyakazi halafu anapotea  ndani ya gari lile ili aondoke, alikutana na makombora kumi ya kwa pamoja kutoka kwa waganga kumi tofauti ambayo yalimrudisha nyuma hatua kadhaa lakini hayakumdhuru. Alipoangaza vizuri aliona kundi la waganga wapatao kumi wakiwa wanaelea hewani wakiwa waejifunga kaniki nyekundu viunoni na vilembe vyeusi, waganga hao tayari walikuwa wamemzunguka tayari wakitaka kummaliza kwa pamoja. Waganga hawa hawakutambua kuja kwao hapo ni kujiingiza katika vita isiyowahusu, wao walichojali ni kupambana na kiumbe aliyesababisha kuteseka kwa wanadamu wasiowajua. Wakiwa wanapanga kuachia makombora mengine yule kiumbe alijizungusha kama pia na kikatokea kimbunga kikali kilichowazoa wote kwa pamoja, uzito wa kimbuka hicho ukisababisha hata viti vilivyokuwa jirani na hapo kupeperushwa huku waganga wakitoa mayowe ya maumivu wakiwa wapo ndani ya kimbunga hicho. Hadi magari yanalipuka kimbunga hicho bado kilikuwa kipo angani na hadi yanateketea yanaisha bado kilikuwa angani kikizunguka huku sauti za watu wakilia kwa maumivu zikisikika, tukio hilo lilishuhudiwa na kila mtu aliyekuwa eneo hilo ingawa hawakujua hizo kelele ni za kina nani. Kimbunga hicho kilipoanza kupungua ndiyo wakashuhudia lita nyingi za damu iliyokuwa ina vipande vya nyama pamoja na mifupa ya binadamu ikidondoka barabarani na kulifanya eneo zima liwe kama machinjioni na kupelekea baadhi ya watu wasio na uatahimilivu wa kushuhudia vitu kama hivyo kukimbia huku wengine wakuzirai hapohapo baada ya kuona mafuvu ya binadamu yakiwa yametapakaa damu katika hali ambayo si rahisi kutazamika.

****

   Jirani na uwanja wa mpira wa miguu uliopo jirani na njia ziendazo katika bwawa maarufu la Duga maforoni linalotumiwa na wananchi wa eneo lote la Maforoni kulikuwa na nyumba za kisasa kama ishirini zilizojengwa na kampuni ya Extoplus ambazo zilikuwa zinazinduliwa katika siku hiyo ambapo sherehe ya uzinduzi ilikuwa inasubiri wafanyakazi kutoka makao makuu wafike ili sherehe hizo zianze. Wageni na waandaaji wa sherehe hiyo walisubiri hadi ilipotimu saa sita adhuhuri lakini hawakuona dalili za kufika wafanyakazi hao, ilipopigwa simu makao makuu ya kampuni ya Extoplus walipewa taarifa ya wafanyakazi hao kuondoka ofisini tangu saa mbili asubuhi. Hali hiyo ilizidi kuwachanganya sana  waandalizi wa sherehe hiyo na ikawabidi watume kikosi cha watu kumi wakiwa ndani ya gari kwenda kufuatilia  kilichowapata wafanyakazi hao, gari ya kampuni ya Extoplus nyingine aina ya landcruiser prado iliondoka Duga maforoni kwenda kufuatilia gari ya kampuni iliyokuwa imebeba wafanyakazi wa kampuni yao. Watu waliotumwa kwenda kufuatilia wenzao nao hawakufika mbali kwani walivaana foleni kubwa ya barabarani walipokuwa wapo katika daraja liliopo katika barabara hiyo ya Mombasa ambalo linajulikana kwa vibweka vyake ambavyo vilitokea mwaka 2003 katika ujenzi wa madaraja na uboreshwaji wa madaraja, moja ya vibweka vyake ambavyo vinasemwa na wakazi wa jiji la Tanga vilivyowahi kutokea ni mashine za kupimia wakati wa ujenzi kutofanya kazi na ikapelekea mwaka huo ujenzi wa madaraja ufanyike  na daraja hilo kushindikanika kujengwa.

  Kikosi cha wafanyakazi kumi kilichotumwa kuangalia  wenzao kiliishia hapo darajani ambako kuna lami baada ujenzi wa mara ya pili kufanikiwa kujenga, magari ya hapo darajani yalikuwa hayaendi kabisa.na ikawalazimu washuke waulize kujua kipi kilichosababisha magari hayo yakwame, walipoambiwa chanzo cha kukwama kwa magari hayo walijikuta wakikodi pikipiki kila mmoja wakienda kushuhudia wenyewe kilichotokea huku gari wakimuachia mmoja aliyekuwa dereva ambaye aligeuza akarudi.

  


     SURA YA PILI
    Utepe mwekundu tayari ulikuwa umezungushwa katika eneo la barabarani lenye damu pamoja na mifupa ya binadamu na barabara yote ilikuwa imefungwa , askari wa jeshi la polisi vikosi  vitatu tofauti walikuwa wamefika hapo wakiwa wanafanya kazi yao katika eneo la tukio. Kulikuwa kuna askari wa usalama barabarani ambao walikuwa wakipima kwani inasadikika kuwa chanzo cha tukio hil ni ajali, kulikuwa kuna askari kanzu kutoka kitengo cha CID (criminal investigation department) ambao walikuja kuchunguza juu ya tukio hilo ambalo pia lilihusisha mauaji kutokana na uwepo wa  mabaki ya miili ya binadamu. Kikosi cha mwisho  cha jeshi la polisi tayari kilikuwa kimechelewa kufanya kazi yao kwani magari yote yalikuwa yameshateketea kwa moto kabisa, kikosi hichi cha jeshi la polisi cha zima moto kilifanya kazi tu ya kutoa miili ya watu waliokutwa  katika magari hayo ambayo haikutambulika na kuipakiza kwenye magari ya wagonjwa ya hospitali kuu ya Bombo ambayo tayari yalikuwa yameshafika eneo la tukio.  Askari wa CID waliochukua maelezo kwa mashuhuda wa tukio hilo walijikuta wakiwa na walakini mkubwa juu ya maelezo hayo kwani yalikuwa yametawaliwa na imani za kishirikina hasa baada ya kusikia juu ya kimbunga kilichodondosha damu nyingi iliyochanganyika na vipande vya nyama pamoja na mifupa, mashuhuda wengi wa tukio hilo walisema watu waliouliwa katika tukio hilo la kimbunga ni waganga kwasababu ya kuonekana kwa mavazi kiganga kuonekana pamoja na vitu kadhaa vya kiganga. Mashuhuda wengine wa tukio hilo walikuwa ni wasaidizi wa waganga ambao walithibitisha waliokuwa kwenye tukio hilo ni waganga waliokuwa wakiwaokoa watu waliokuwa wapo ndani ya gari iliyoungua moto. Maelezo yao yalionekana kuwa hayana maana mbele ya jeshi la polisi kwani polisi na serikali nzima ilikuwa haiamini uwepo wa wachawi au uchawi hivyo waliyapuuzia maelezo yao.

****

Kundi la vijana kumi ambao sasa wamebaki tisa baada ya mmoja wao kugeuza na kurudi na gari lilifika Bwaga Macho  kwa msaada wa pikipiki tisa walizozikodi, kitendo cha kushuka kwenye pikipiki zao mmojawapo aliona kibao cha namba za gari kilichokuwa kipo kwenye majani na ikamlazimu akiokote akiangalie. Alijikuta akishtuka sana baada ya kubaini ni namba ya gari la kubeba wafanyakazi la makao makuu, yule mtu aliwaonesha wenzake akionesha haamini kama ni namba za gari la kampuni au siyo.
"hizi namba za usajili za staff bus namba 5?" Aliwauliza wenzake huku akionekana kutoamini.
"eeh! Ndiyo zenyewe kabisa, hebu chekini hii picha niliyopiga mbele ya staff bus namba 5" Mwingine alikiri kuwa namba ya basi hilo kisha akatoa simu yake akawaonesha picha ya mbele ya aliyoiseti kwenye simu yake ambayo hujulikana kama wallpaper kwa lugha ya kigeni, walipoiona hiyo picha waliamua kukimbia kuelekea enro lilipotokea tukio. Waliyaona magari mawili yaliyoungua yakiwa yapo  jirani na dimbwi kubwa la damu lililokuwa limeanza kukauka  tayari. Dimbwi hilo pamoja na magari yaliyoungua yalikuwa yamezungushiwa utepe ili kuzuia watu wasiingie. Vijana hawa walijikuta wakitaka kuingia katika eneo liloozungushiwa utepe lakini  askari hao waliwazuia na kuwaelewesha wapo kazini lakini vijana hawa hawakutaka  kabisa tena mmoja wao ndiyo alionekana kutaka kufanya fujo na mwisho wake wote wakawekwa chini ya ulinzi.  Walipelekwa hadi upande wenye askari wengi wakawekwa chini ya uangalizi wa askari na mmoja kati ya wale vijana  alikuwa muda wote alikuwa akilia huku akiiangalia gari ya abiria ambayo ilikuwa imebeba wale wafanyakazi kutoka idara moja ya makao makuu ya kampuni ya Extoplus.
"Hebu nyamaza mtoto wa kiume wewe unalialia nini" Mmoja wa maaskari ambao alikuwa akiwangalia hawa vijana wa kampuni ya Extoplus alimwambia yule kijana aliyekuwa analia.
"mama yangu yupo ndani ya gari lililoungua sasa wewe ulitaka nicheke" Kijana alimjia juu yule askari aliyekuwa anamwambia hivyo.
"kijana una uhakika gani kama gari  lile ndiyo mama yako alikuwemo?" Yule askari aliuliza.
"uhakika ninao kibao cha namba za gari hiki hapa tumekiokota kule kwenye majani" Aliongea yule kijana kisha akampatia askari kibao chenye namba za usajili wa gari.
"tena askari gari yenyewe ni hii hapa niliwahi kupiga nayo picha" Kijana yule aliyeiweka picha ya gari la wafanyakazi kwenye simu yake akiwa amepiga nalo picha naye aliongea huku akimuonesha askari picha aliyoipiga na ile gari yenye namba sawa na namba zilizokuwa kibao cha namba za usajili walichokiota.  Yule askari aliziangalia kwa umakini kisha akaangalia muundo wa mabaki ya gari la abiria lililoungua halafu akawaambia, "hebu nifuateni mara moja"
Yule askari aliondoka mara moja akaelekea mahali pengine kwenye kundi kubwa la maaskari waliovaa kiraia na waliovaa sare za polisi, alimfuata askari mmoja aliyevaa kiraia akatoa heshima kisha akamuuma sikio huku akiwaonesha kidole wale vijana. Yule askari aliyevaa kiraia aliwasogelea wale vijana akiwa na yule askari aliyewaleta kisha akawaashiria wamfuate, alielekea kwenye gari ya polisi aina ya toyota land cruiser yenye viti katika sehemu ya kuwekea mizigo kisha akapanda akawamuru nao wapande.
"naitwa ASP John Faustin natokea kito cha polisi Mkwakwani, wenzangu mnaitwa nani majina yenu" Asp John alijitambulisha kwa wale vijana huku akionesha kitambulisho chake cha kazi kisha akawauliza majina yao, wale vijana walitaja majina yao wote.
"ok James naomba naomba uache kulia unieleze kila kitu" Asp John alimuambia yule kijana aliyekuwa analia baada ya kuona gari lile lililoungua.
"afande sisi wote ni wafanyakazi wa kampuni ya Extoplus na tulikuwa tupo Duga kwenye sherehe za uzinduzi wa nyumba mpya za kupangishwa za kampuni yetu, tulikuwa tukitarajia ujio wa staff wa idara ya uhasibu kuiwakilisha ofisi ya makao makuu tangu asubuhi lakini hadi inafika saa sita hawakuwa wamefika. Sisi tulitumwa kuwafuatilia na tulifuatilia ndipo tulipokuta hali hii tena tulianza kuanza kuona kibao cha namba za usajili za gari ya kampuni, na tuliifananisha na picha ya gari la kampuni tukaona linafanana kila kitu" James aliongea huku akiwa na uchungu. Asp John aliyanakili maelezo ya James kisha akajiandaa kuuliza swali jingine lakini king'ora cha gari la zima moto kilimkatisha na akajikuta akiangalia lilipo gari la zima moto. Wale vijana nao waliliona lile gari la zimamoto likipita pembezoni mwa eneo la tukio kwa tabu kisha likaingia barabarani kisha likaingia barabarani likawa linaelekea Duga Maforoni kwa mwendo wa kasi sana huku milio ya ving'ora vyake ikiwa imetawala njia nzima. Asp John alipoona hali hiyo alihisi kuna jambo na akawa anataka kujua kuna nini kilichotokea, alinyanyua simu ya upepo akaongea kwa muda kisha akatulia akasikiliza upande wa pili na akajikuta amegwaya.
"nyumba za kampuni yenu zilizokuwa zinazinduliwa zote zimeungua kwa moto  wa hitilafu ya umeme" Asp John aliwaambia wale vijana.
"eti nini?" James alisema kwa mshangao.


*Mmmh! Majanga yanaendelea










No comments:

Post a Comment