Saturday, November 21, 2015

KOSA SEHEMU YA TATU


   KOSA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA

SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



 ILIPOISHIA

"dah! Halafu kweli, kwani saa ngapi?" Hassan aliuliza.
"saa kumi kasoro hii tuwahi graundi kama vipi?" Hussein aliongea huku akiiweka shajara kwenye meza,  wote kwa pamoja walichukua vifaa vya mazoezi kisha wakaondoka kuelekea uwanjani. Vijana hawa mpira wa miguu ndiyo ilikuwa burudani yao kuu na waliupenda sana, mapenzi  yao kwenye mpira wa miguu yalijulikana hata kwa baba yao na ndiye aliyewapa moyo wa kuendelea kuonesha kipaji chao kandanda. Mpira wa miguu kwao ilikuwa kama ni mchezo uliwapa umaarufu chuoni kwao na hata mtaa wanapoishi..






ENDELEA NA MKADA HUU WA KUSISISIMUA





SEHEMU YA TATU!!

Hawakutumia muda mrefu sana kutoka nyumbani kwao hadi ulipo uwanja wa mpira, ni mwendo wa dakika tano tu ndiyo waliotumia kufika uwanjani hapo kwa ajili ya kucheza mpira. Walipofika walianza mara moja kukimbia kuuzunguka uwanja huo wa mpira kwa mizunguko ishirini ili kujenga pumzi yao ya uwanjani, walipomaliza walianza kufanya mazoezi madogo ya viungo kisha wakaanza mazoezi kwa kucheza 'opening space' wakiwa na wenzao  kama ilivyo kawaida yao. Opening space ni mtindo wa uchezaji ambao hutumika mazoezini kwa kuweka timu mbili uwanjani kucheza bila kuwepo kwa magoli, ni mazoezi yanayohusisha pasi tupu baina ya vikosi vya timu moja mazoezini pasipo kuhusisha magoli wala uwepo wa golikipa. Hassan na Hussein pamoja na wengineo katika mazoezi hayo walicheza mchezo huo kwa muda wa nusu saa kisha wakapanga vikosi viwili tofauti kwa ajili ya kuanza mpira mara moja, siku hii mapacha hawa ambao ni viraka katika mpira walicheza vikosi tofauti na ikawabidi wakabiliane  kutetea vikosi vyao. Kiraka ni mchezaji mpira mwenye uwezo wa kucheza namba yoyote uwanjani, Hassan na Hussein ni wachezaji wenye uwezo.wa kucheza namba yoyote uwanjani ndiyo maana wanaitwa viraka. Saa kumi na mbili jioni mazoezi yaliisha na mapacha hawa wakarudi nyumbani kwao, walipofika walisafisha miili yao kwanza kisha wakaifuata shajara ilipo. Waliichukua kisha wakajilaza kitandani kifudifudi ili waisome kwa pamoja, Hassan aliifungua shajara kwa papara hadi walipoishia kisha wakaanza kuisoma.

****

Karatasi yenyewe iliandikwa , 'ABDULHAFIDH NADHANI MUDA WA KUANZA KUJIFUNZA SOMO JIPYA LITAKALOKUFANYA UACHE JEURI YA PESA LIMEWADIA, SASA KAMA UNAHITAJI MALI ZAKO NA KILA KITU CHAKO UKIKUTE KAMA ULIVYOKIACHA INABIDI UFANYE NITAKAVYOKUAMRISHA VINGINEVYO NITAZICHUKUA MALI ZAKO ZOTE KWA KUGHUSHI SAHIHI YAKO. UBISHI WAKO UTAJUTA MAISHANI MWAKO NA UTIIFU WAKO UTAKUOKOA, NSHITAJI DOLA MILIONI MOJA ZA KIMAREKANI NDANI YA SIKU KUMI NA INABIDI UZIWEKE KWENYE SANDUKU LA POSTA AMBALO FUNGUO ZAKE NIMEZIBANDIKA NYUMA YA KARATASI HII. UTAKAPOZITOA HIZO PESA SIJUI ILA NA UKIWA HUNA MBINU ZA KUZIPATA HIZO BASI FUNGUO ZA SANDUKU HILO LA POSTA ZITAKUSAIDIA MBINU ZA KUZIPATA HIZO PESA IKIWA UTALIFUNGUA LEO HII. KILA LA HERI'.  Hiyo ndiyo karatasi ya pili niliyotumiwa na mtu nisiyemjua ambayo imebeba wajibu ambao  uliokuwa mrahisi kwa kuufikiria kwa kichwa na mgumu kama ukiamua kuufanya, nyuma ya karatasi hiyo kweli kulikuwa kumebandika funguo ndogo zenye namba ya sanduku la posta yenye kibango kidogo maandishi yaliyosomeka 'Sam Nujoma drive, Skeleton coast' mwisho wa maandishi haya kwenye kibango hicho kulikuwa kuna namba ya sanduku la posta. Nilikitoa kibango hicho kisha nikamuonedha Jonas ili nipate msaada wake muda huo huo wa asubuhi, Jonas aliweza kunisaidia kwa kunitajia  eneo kuwa maandishi hayo yalikuwa yanaelekeza eneo la ofisi za posta zinapopatikana.
"ndugu unaweza kunipeleka zilipo ofisi hizo?" Nilimuuliza baada ya yeye kunifafanulia juu ya maandishi yao ambayo yalitaja barabara ya Sam Nujoma ambayo sikuwa naitambua ya nchini humo zaidi ya kuitambua barabara ya Sam Nujoma  iliyopo jijini Dar es salaam katika wilaya ya Kinondoni, kumbe Namibia nayo ilikuwa na barabara yenye jina la baba wa taifa lao ambaye ni rais wa kwanza wa nchi hiyo ambaye anaitwa Samuel Daniel Shafiishuna Nujoma kwa kifupi Sam Nujoma. Hapo ndipo nilipotambua kuwa Tanzania imeamua kuipa jina barabara yake moja kwa kuenzi mchango wa huyu kiongozi hodari katika Afrika kwa kutambua mchango wake katika nchi ya Namibia kama ambavyo Afrika ya Kusini na Kenya zilivyoipa barabara zao jina la rais wetu wa kwanza na baba wa taifa la Tanzania mwalimu Nyerere. Jonas alitoka nje baada ya kumuambia suala la kunipeleka zilipo ofisi za posta nilizoelekezwa kutokana na ugeni wangu ndani ya nchi hii, aliniambia nimsubiri kwa muda wa dakika tano atarejea. Niliitikia nitamsubiri kwa dakika hizo kwakuwa sikuwa na njia nyingine ya mbadala, pia niliitikia tu ingawa sikuwa na saa ambayo ingeniwezesha kuhesabu dakika hizo zaidi ya kuzoea ahadi zetu  za kiswahili tunazowekeana huko Tanzania. Yaani mtanzania mwenzangu anaweza akakuambia nipe dakika mbili narudi sasa hivi wakati anatambua kuwa huna hata hiyo saa hata simu ya kuhesabu dakika hizo mbili alizokuambia, ukweli wa ahadi hizi ni haziendi na muda uliotajwa bali hutumika kumpa mtu moyo wa kuendelea kusubiri na asikate tamaa na jambo analoahidiwa. Ndiyo maana Jonas aliniambia hivyo si kweli kwamba angeweza kurejea baada ya dakika tano, hiyo ni kutokana na kunipa moyo mimi nisichoke kumsubiri. Jonas alirejea baada ya dakika ambazo ungezikadiria basi zingekuwa ni dakika kumi na tano, alirejea akiwa tabasamu lililoashiria kuna jambo la faraja amekuja nalo.
"Abdul tumshukuru Mungu nimepata pikipiki ambayo itatusaidia kwenda eneo ofisi za posta, tuondoke haraka tuwahi kurudi" Jonas aliniambia akiwa amepambwa na tabasamu  usoni mwake.
"Alhamdulillahi rabbil a'alamiiin(shukrani zote anastahiki Mwenyezimungu)" Nilijikuta nikimshukuru Mungu kwa faraja hii ndogo niliyoisikia kutoka kwa Jonas wakati mwanzo nilikuwa mchoyo wa kumpa shukrani kwa mambo makubwa aliyonifanyia na hata anayoendelea kunifanyia hadi leo hii, ewe mwanadamu mwenzangu unayepumua kama mimi usiombe ufikwe na tabu yaani hata kama Mungu ulimsahau katika maisha yako utamkumbuka tu. Hata mimi nilikuwa nimemsahau kwa neema alizonipatia kama vile kurithi mali nyingi na pesa nyingi pia alinijalia pumzi ambayo ninayo mpaka naandika mkasa huu ulionikumba, sikuwahi kumshukuru hata  pale nilipoamka  nilipoiona siku mpya lakini huku kwenye majanga ndiyo nilimkumbuka.
Siku hiyo nilivaa nguo mbili ambazo alinikabidhi Jonas pamoja na viatu vya ngozi vilivyochoka, kwa mtu tajiri kama mimi nilikuwa najiona kituko ila kwa walio katika hali ya chini walikuwa wananiona nimependeza.  Ule usemi wa lulu kwako kwa mwenzio ni changarawe ndiyo nilianza kuuamini, yaani unaweza ukavaa ukaonekana umependeza kwa watu walio chini yako na ukaonekana umevaa kawaida kwa watu  na kwa waliokuzidi ukaonekana hujavaa chochote. Tulitoka hadi nje ya kibanda tunachoishi nikiwa na muonekano ambao hata Jonas alinisifia nimependeza, nje ya kibanda tunachoishi kulikuwa kuna pikipiki ya kichina ambayo sikujua hata imefika muda kwani hata mlio sikuusikia. Nilijikuta nikimuuliza Jonas, "hii ndiyo pikipiki yenyewe tunayoenda nayo?"
"Ndiyo hiyo unaionaje?" Jonas aliniuliza akidhani labda nimeudharau muonekano wa pikipiki hiyo kumbe nilishanganzwa na jinsi ilivyofika pale kwani sikusikia mlio wowote wa pikipiki.
"iko vizuri, hivi Jonas hii pikipiki imefika vipi kwani sijasikia mlio wowote wa pikipiki?" Nilimuuliza Jonas.
"Nimeileta hapa kwa kuikokota" Jonas alinijibu huku akitoa kisimamio cha pikipiki kisha akaiwasha kwa kutumia kiwashio cha pikipiki ambacho wengi wetu tunapenda kukiita 'kick'. Pikipiki ilitii amri ya kuwaka ingawa ilikuwa ina makelele sana, Jonas aliniashiria nipande nami nikatii nikakaa nyuma safari ikaanza kuelekea katika ofisi ya posta. Siku hiyo nilipata bahati ya kulishuhudia jiji la Walvis  upande wa mjini lililoonekana limechangamka kutokana na shughuli mbalimbali za watu wa nchi hiyo katika kujipatia maendeleo, baada ya dakika takribani thelathini tulikuwa tumefika katika ofisi ya posta kutokana na mwendo wa kifo aliokuwa anautumia Jonas tulipokuwa tunatoka kijijini. Mwendo huo niliuita wa kifo kwasababu ni mwendo mkali ambao ulisababisha hadi macho yangu yatoke machozi  kutokana na upepo mkali, tulishuka nje ya ofisi hizo kisha pikipiki ikaegeshwa getini halafu tukaingia ndani hadi sehemu yenye visanduku vingi vyenye namba tofauti. Zoezi la kutafuta sanduku la posta lenye namba niliyoikuta kwenye barua ikaanza, tulitafuta namba hiyo kwa muda mrefu kutokana na wingi wa masanduku hayo. Tulipokuja kuipata namba tunayoutafuta niliingiza funguo katika sehemu ya kufungua kwa pupa kisha nikafungua, nilikuta bahasha mbili za kaki zenye picha yangu. Nilizitoa hizo bahasha kisha nikazifungua papo hapo kwa pupa, bahasha ya kwanza ilikuwa ina noti za dola za kimarekani na ya pili ilikuwa ina barua ambayo ndiyo ilielezea wajibu niliotakiwa kuufanya kwa upana. Barua hiyo ilikuwa imeandikwa hivi, 'UKITAKA KUZIPATA DOLA MILIONI MOJA ILI KUTIMIZA WAJIBU WAKO NI LAZIMA UFANYE KAZI HII AU TAFUTA KAZI ITAKAYOKUINGIZIA HELA HIZO KWA SIKU KUMI. KUNA WANAWAKE KUMI AMBAO WAMECHOSHWA NA KUTODHIRISHWA NA WANAUME WA NA NCHI HII HIVYO WANAHITAJI PENZI LA MWANAUME WA KUTANZANIA ALIYEZALIWA KATIKA JIJI LA MAPENZI(TANGA), WANAWAKE HAWA NI WANAKAA MTAA WA WATU WENYE HELA ZAO KATIKA MJI MKUU WA NCHI HII NA ORODHA YAO IPO NYUMA YA KARATASI HII SASA FANYA UFANYAVYO NDANI YA SIKU KUMI UWE UMETIMIZA WAJIBU HUU NA PESA ULETE KATIKA SANDUKU HILIHILI LA POSTA.  UKAIDI WAKO UTASABABISHA KAMPUNI YAKO KOJA IUNZWE , KILA LA HERI'. Nilipomaliza kuisoma karatasi hiyo tayari nilijua natakiwaa nifanye kazi ya kutembea na wanawake kumi ili niweze kuzipata fedha ninazozihitaji, hii ndiyo kazi ambayo ni rahisi kuifanya kama utaifikiria kwa kichwa na ngumu sana kama utaikabili, hata nilipomwomba ushauri Jonas naye hakuwa na la kunisaidia. Pia hakuna njia nyingine ya kuzipata fedha nyingi namna hiyo ambazo zingebadilishwa kuwa za kitanzania basi utajihesabu ni  milionea, sikuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na hali halisi. Pia kuikabili kazi hiyo katika mji wa Windhoek  sikuwa na jinsi kwani sikuwa na kazi ya kawaida itakayoniwezesha kupata pesa hizo kwa siku kumi, nilipozihesabu zile dola za kimarekani zilizokuwa kwenye bahashe zilikuwa ni doka elfu kumi za kimarekani. Muda huo bado tulikuwa tumesimama kwenye eneo lenye masunduku ambako lilikuwa tupu halina watu kabisa zaidi yetu sisi wawili.
"Dah! Huyu mtu hata sijui nimemkosea nini?" Nilinung'unika nikijiona sina kosa kwa mtu anayenipa kazi nisizozitaka.
"Ndugu inakubidi utekeleze tu maana ukipinga utajipa hasara mwenyewe" Jonas alinishauri.
"Sina jinsi inabidi tu nifanye hivyo" Niliongea kwa kuonesha nimekubali kufanya jambo hilo.
"Inabidi uwahi leo leo ndugu ili uweze kuikamilisha si una majina na anuani zao?" Jonas aliniambia.
"ndiyo ninazo" Nilimjibu Jonas.
"funga sanduku tuondoke zetu" Jonas aliniambia huku akitoka kuelekea nje ya ofisi tulipoiacha pikipiki yetu, nilifunga masunduku hayo kisha nikamfuata kwa haraka. Tulipanda pikipiki tukitoka ofisi hizo za posta kuifuata barabara ambayo  nilikuja kuitambua kama barabara ya Sam Nujoma, tulifika sehemu yenye barabara kubwa ambayo sikuitambua jina lake. Barabara hii inakutana na barabara ya Sam Nujoma eneo hilo, Jonas alikata kona kuingia upande wa kushoto kisha akatembea hadi mahali kwenye kituo kama cha daladala halafu akasimama.
"ndugu inabidi nikuache hapa kituoni upande mabasi madogo yatakayo kupeleka Widhoek likipitia Swakopmund hadi huko, kila la heri" Jonas aliniaga kisha akasema,"wewe ni ndugu yangu na ninahitaji kuwa pamoja nawe lakini kwa hili inabidi uende mwenyewe, tutaonana ukirudi". Jonas alinipatia dola kadhaa za kinamibia kisha akanipa mkono wa kuniaga, muda huo gari ndogo aina ya toyota hiace ilifika na ikasimama kwenye kituo hicho. Jonas akiniashiria niingie kwenye gari hiyo, nilimpungia mkono wa kumuaga huyu mwenyeji wangu katika eneo la ghuba ya Walvis na sasa nilikuwa najiandaa kwenda kwenye mji mwingine nikiwa sina hata mwenyeji ingawa katika mji huo niliwahi kufika nikiwa katika shughuli zangu za kibiashara. Nilipanda hiace hiyo kwa unyonge huku nikimpungia mkono wa kumuaga, nilikaa kwenye kiti cha gari hiyo kwa  utulivu nikiwa mpweke kutokana na kutoweza kuongea kiafrikaas ambacho ndiyo kilikuwa kimetawala ndani ya gari hiyo Salamu za abiria wenzangu niliziitikia kama vile bubu kwani lugha yenyewe nilikuwa naibahatisha kuongea hata kule kijijini nilipofikia. Pembeni yangu upande wa kulia katika kiti kilichopo karibu na dirisha alikaa msichana mmoja ambaye ni shombeshombe na mwenye sura ya mvuto, msichana huyo ndiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kumuona na nikakiri  kuwa hata Huwaida aliyenikataa tangu nipo chuo alikuwa haingii hata sumni. Ukweli binti huyo alinivutia na nilimtamani ingawa nilihofu nitaanza kuongea naye vipi kwani hiyo lugha hata aliyonisabahi nayo siijui zaidi ya kuambulia maneno machache, msichana huyu alionekana ni muongeaji kwani haikupita muda mrefu akaanza kuongea na mimi kwa lugha ya kiafrikaas akiujua mimi ni mwenyeji katika lugha hiyo kumbe ni mgeni tena asiyefikisha hata mwezi mmoja. Kunyamaza nisijibu lolote nikawa nashindwa kwa kuhofia nitaonekana nina dharau na itakuwa ndiyo chanzo cha kumkosa mrembo huyu, yaani kukijua kingereza kulisaidia sana kumudu kuongea naye kwasababu lugha imefanana na kingereza kwa maneno mengi. Uzuri wake na muonekano ulinifanya nisichoke maneno yake mengi anayoongea, uchangamfu wake ulinifanya nizidi kumfikiria sana moyoni mwangu. Nilijaribu kumlinganisha na Huwaida aliyenichanganya kiasi cha kuamua kumfanyia kitu kibaya Faiz ambaye ndiye aliyekuwa anapendwa na Huwaida, ukweli ni kwamba kama Huwaida na huyu binti wangekuwa ni mabehewa ya matreni basi huwaida angekuwa behewa la walalahoi na huyu binti angekuwa behewa la wenye nazo. Yaani uzuri wake kwangu ulikuwa ni kama sumaku  iliyoyavuta macho yangu yasichoke kumtazama, binti huyu hadi muda huo sikuelewa ni mchanganyiko wa wazazi wa asili kwani alikuwa ni chotara kimuoneksno aliyewashinda hata machotara wenzangu wa kisomali. Hapo ndipo nilipobaini kwamba ulevusemi usemao ukikaa pwani peke yake utasema mti mrefu kuliko yote ni mnazi, ukikaa bara utataja miti mingine unayoijua huku mnazi ukikataa sio mti mrefu na ukitembea kote ndiyo utajua kuna miti mirefu zaidi unayoiona huko unapoishi. Yaani namanisha hivi ukawa unakaa mji fulani na ukiulizwa yupi mrembo utasema ni msichana fulani. Ila ukizunguka pote ndiyo utajua kuna warembo zaidi ya unaowatambua, binafsi nilikiri Huwaida ni msichana mrembo jiji zima la Dar es salaam  na kwingineko kutokana sijajionea mrembo zaidi yake. Huku Namibia nimemuona mrembo zaidi yake na nikakiri kamzidi kila kitu. Msichana huyu ndiye aliyenitoa kimawazo ndani ya gari hiyo nikajihisi nikiwa nipo naye katika dunia ya peke yangu, maongezi yake sikuwa nayasikia kutokana na ubongo wangu kuwa mbali kimawazo juu ya kumuwaza. Sikuwahi kumuwazia msichana yoyote namna hii hadi mawazo yangu yakahama kabisa, lakini hapa mawazo yalihama bila hata usafiro wowote. Msichana huyu muongeaji alizidi kuongea akijua nipo naye kutokana na mboni za macho yangu kumtazama yeye, kumbe nipo sehemu nyingine kimawazo.

****

"haya haraka sana fungeni hiyo diary nimewaambia" Ilisikika sauti  ya mwanamke kutoka mlangoni ikiwapa amri Hassan na Hussein.
"mama! Umerudi?!"" Wote kwa pamoja waliacha kusoma diary kisha wakamkimbilia mama yao halafu wakamkumbatia huku wakisema, "shikamoo mama".
"marahaba wanangu, wazima nyinyi?" Mams aliitikia salamu halafu akawajulia hali.
"sisi wazima mama, za safari?" Hassan alimuuliza mama yake.
"salama tu, wanangu mnasahau hadi kula hebu twendeni kwanza mkale, saa mbili hii " Mama yao aliwaambia, Hassan na Hussein walishtuka kusikia kuwa muda wa kula umefika tayari. Usomaji wa shajara uliwafanya hata wasitambue kama umeenda kiasi hicho, wote kwa pamoja walitazamana kwa mshangao.
"hivi hiyo diary kawapa nani? Baba yenu?" Mama yao aliwauliza.
"Ndiyo mama" Hussein alijibu.
"haya fungeni mkale mje kuendelea kusoma wanangu wazuri"  Mama yao aliwaambia kisha akatoka chumbani kwao.


*MAPACHA WANANOGEWA NA MKASA WANAOUSOMA HADI WANASAHAU KULA


*ABDULHAFIDH ANATENGANA NA RAFIKI YAKE KISA KAZI YA LAZIMA KUOKOA KAMPUNI YAKE, JE ATAFANIKIWA KUOKOA

*MAWAZO YAMESAFIRI YAKIMUACHA ABDULHAFIDH KWENYE GARI BAADA YA KUSTAAJABU UZURI ZA MWANAMKE, JE NINI KITAFUATA?

YOTE HAYO UTAYAPATA UKENDELEA KUFUATILIA MKASA HUU WENYE KUFUNDISHA, TUKUTANE TENA JUMATATU PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA.








NDUGU MSOMAJI INABIDI UTAMBUE KUWA LIKE
YAKO NDIYO INIPAYO NGUVU YA KUANDIKA RIWAYA
HII, HIVYO LIKE ILI KAMA UPO PAMOJA NAMI.
COMMENT KAMA UNA USHAURI AU MAONI.

HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI AU UONGOZI WA RIWAYA MARIDHAWA.

No comments:

Post a Comment