Saturday, November 28, 2015

MFAHAMU PROFESSA GABRIEL RUHUMBIKA


PROFESSA GABRIEL RUHUMBIKA

    Nadhani kwa wale ambao hawakusoma fasihi jina hili litakuwa ni jina geni sana kwenu, ila si mgeni sana ndani ya ulimwengu huu wa fasihi ya kitanzania. Ni mmoja wa wanafasihi maarufu sana ndani ya nchi ya Tanzania na pia mmoja wa wasomi wakubwa sana katika somo la fasihi Afrika na hata duniani kwa ujumla, ameandika kazi nyingi za kifasihi katika lugha ya kiswahili na kingereza.



  Anaitwa Professa Gabriel Ruhumbika amezaliwa mwaka 1938 katika kisiwa cha Ukerewe kilichopo ndani ya ziwa Viktoria, Ruhumbuka alimaliza elimu yake ya chuo kikuu ngazi ya shahada katika chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda. Pia alihitimu elimu yake ya ngazi ya PHD katika chuo cha Paris Surbonne katika jiji la Paris nchini Ufaransa mnamo mwaka 1969.


  Alianza kuingia ndani ya ulimwengu wa fasihi kupitia riwaya ya kingereza ambayo ni Village in Uhuru ambayo ilitoka mwaka 1969, kilikuwa ni kitabu kilichokuwa kikizungumzia masuala ya juhudi zilizokuwa zikifanywa na chama cha TANU  katika kupigania uhuru wa nchi ya Tanganyika. Pia kitabu hicho kilikuwa ni kitabu cha pili kuandikwa kwa lugha kwa lugha ya kingereza baada ya kitabu cha Peter Palangyo  ambacho ni Dying in the sun . Baadaye aliamua kuandika vitabu vyote kwa lugha ya kiswahili ili kuendeleza fasihi ya lugha hii kama alivyokuwa akifanya mwandishi Ngũgĩ wa Thiong'o.[ katika kuendeleza lugha mama.  Pia ameandika riwaya nyingi ikiwemo  Miradi bubu ya wazalendo(1991) na Janga sugu kwa wazawa(2002). Mbali na riwaya pia Ruhumbuka ameandika hadithi fupi mbalimbali katika lugha ya kiswahili ikiwemo  Uwike usiwike kutakuche.

    Pia mbali na utunzi wa kazi ya fasihi  pia Professa Ruhumbika ni mfasiri mzuri wa kazi za fasihi na amefasiri kazi tofauti za fasihi hasa kutoka lugha ya kifaransa kwenda lugha ya kiswahili, pia amefasiri kazi ya fasihi kutoka lugha mama yake yaani kikerewe kwenda kingereza. Moja ya kazi ambayo aliifasiri ni  Myombekere na Bugonoka na Ntulanalwo na Bulihwali  ambayo iliandikwa na Marehemu Aniceti Kitereza mwaka 1945, kitabu hicho alikifasiri kwa kingereza kikaitwa Myombeke and his wife Bugonoka, Their son Ntulanalwo and   Daughter Bulihwali.

     Professa Ruhumbika pia  amekuwa ni mwalimu katika vyuo mbalimbali ndani ya nje ya bara la Afrika tangu mwaka 1970, amekuwa akifundisha fasihi katika vyuo tofauti vya vikubwa katika nchi mbalimbali. Mnamo mwaka 1970 hadi mwaka 1985 alikuwa ni  professa katika chuo kikuu cha Dare esalaam, mnano mwaka 1985 hadi mwaka 1992 alikuwa ni professa katika chuo cha Humpton Virginia Marekani. Kuanzia mwaka 1992 amekuwa ni professa katika chuo kikuu cha Georgia. Mbali na hayo pia Professa Ruhumbika amepokea tuzo mbalimbali kutokana na mchango wake katika ulimwengu wa fasihi na hata ulimwengu wa kitaaluma.

    Naam huyo ndiye mwanafasihi wetu wa jumamosi ya leo, mwenye historia kubwa ndani ya ulimwengu wa fasihi ya kitanzania na hata duniani kwa ujumla.


TUKUTANE TENA WIKI IJAYO KUMJUA MWANAFASIHI MWINGINE WA WIKI.

   

No comments:

Post a Comment