Thursday, November 26, 2015

KOSA SEHEMU YA TISA

 KOSA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA

SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



 ILIPOISHIA


Nurulayt alizidi kuniambia maelezo ambayo yaliniacha kinywa wazi, Faiz huyu ninayemjua mimi kusikia ni muuaji na jambazi mkubwa.
"Nuru kwahiyo wewe ulikuwa unaishi Afrika ya kusini?" Nlimuuliza Nurulayt ili nipate maelezo yake kiupana zaidi.
"hapana sikuwa naishi Afrika ya kusini ila nilikuwa naenda kumtembelea kaka tu mara chache na hata hiyo siku aliyouawa nilikuwa nilikuwa nimekuja kumsalimia na ndiyo siku hiyo Faiz  akapiga
hodi nikaambiwa nijifiche" Nurulayt alizidi kunieleza huku akiwa na hasira sana.



ENDELEA NA MKASA HUU WENYE KUELIMISHA NA KUFUNDISHA



SEHEMU YA TISA!!
Kusikia habari za mtu ambaye kwangu ni adui na kwake ni rafiki, nilibaki nikiwa na mshangao sana kutokana na nilivyokuwa namfikiria Faiz jinsi alivyo. Nilikuwa namuona kama mtu mchovu tu mwenye ujanja wa kawaida tu lakini sasa nilibadili fikra zangu na nikaziweka kuwa nashindana na mtu hatari na mwenye nguvu nguvu ya kunifanyia kitu chochote kibaya nilianza kumuogopa kutokana kusikia habari zske. Jambazi na muuaji ndiye ambaye fikra zangu ziliniambia napambana naye na ninahitajika nimshinde kwa namna yoyote, nilitaka kumpata Huwaida ili niwe naye na kuna mti wa mbuyu ambao mwanzo niliouona niliuona mchicha ndiyo unaonizuia  kumpata na nilitakiwa kuuondoa huu mbuyu ambao ndiyo unanizuia kupata waridi la moyo wangu. Muda huo bado nilikuwa nikiyafikiria maneno ya Nurulayt, hakika nilimuona ni mwanamke atakayeweza kunirahisishia kupata kila ninachohitaji na kupata kile moyo kitakachojifariji.
"sasa hapo unataka nikusaidie sio?" Nilimuuliza Nurulayt baada ya kufikiria kwa muda mrefu.
"nisaidie na mimi nikusaidie Abdul, kifupi tusaidiane katika hili. Nataka kulipa kisasi kwa Faiz hivyo nahitaji msaada wako, unahitaji kumpata Huwaida hivyo utahitaji msaada wangu ili umpate" Nurulayt aliongea huku akinitazama usoni.
"ok, hilo linawezekana mbele ya pesa hakuna kinashindikana. Nipo tayari kukusaidia nadhani na wewe uko tayari kunisaidia" Nilimwambia Nurulayt huku nikimtazama usoni, Nurulayt aliachia tabasamu mwanana kwa kukubaliwa jambo lake  na mimi.
"vizuri na hapa tunahitajika tutoe kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kumteka Faiz kwasababu tunatumia kundi la wahalifu hatari kutoka Kongo hivyo tujiandae kiuchumi" Nurulayt aliniambia baada ya kumkubalia kisha akajiachia kitandani.
"Nur kuhusu pesa hata iwe milioni mia  moja we usihofu itapatikana hata leo hii" Nilimwambia Nurulayt huku nikimtazama usoni mwake.
"kiasi chote cha pesa utakipataje leo hii hata kama tunatokea familia zenye uwezo mkubwa wa pesa?" Nurulayt aliniuliza kwa mshangao.
"Hilo niachie mimi, Nadhani ni muda wa kutoka kwenda Lugalo kumuangalia yule punda" Nilimwambia Nurulayt huku nikisimama kwa ajili ya kuondoka. Nurulayt  alinivuta mkono nilipotaka kuondoka kisha akanibusu ghafla kwenye papi zangu za midomo bila hata kutarajia tendo hilo, aliponiachia akanikumbatia kwa nguvu halafu akaniambia "Abdul kaa utambue na mimi ni mwanamke na nina hisia kama mwingine, nakupenda sana lakini kwa suala la kusaidiana mimi na wewe sina budi kukupeleka kwenye himaya ya Huwaida".  Wakati hayo maneno Nurulayt alikuwa anahema huku akitazamana na uso wangu kwa karibu wa takribani sentimita mbili, kifua chake kichanga kilikuwa kikinipa majaribu matupu hadi muda huo. Nilijikuta  nikipandwa na hisia za mapenzi na nikaanza vurugu hapo hapo hadi  kitandani, baada ya saa moja wote tuliingia bafuni tukaoga kisha  tukaelekea hospitali ya Lugalo kwenda kumuona mbaya wangu. Tulitumia muda mfupi na tukafanikiwa kufika  katika hoapitali hiyo ya jeshi ambayo haipo mbali sana na eneo ambalo Faiz aliokotwa, Nurulayt aliniongoza hadi jirani na wodi ambayo Faiz alikuwa kalazwa ambapo tulimkuta Huwaida akiwa pembeni ya mlango kwenye dawati akiwa amejiinamia. Nilijifanya naenda kwa kasi huku nikihema hadi Huwaida akautambua ujio wangu  na akanikimbilia akanikumbatia huku akilia kwa uchungu, ulaini wa mwili wake kwangu ulikuwa ni faraja tosha kwani nilihisi kama nimekumbatiwa na mpenzi wangu.
" Shem sijui Faiz wangu kawakosea nini watu hawa mpaka wamfanyie hivi" Huwaida alilalamika sana huku machozi mfululizo yakimtoka, nilimbembeleza huku nikiwa nina firaha moyoni ya kukumbatiwa naye. Baada ya kuachiana kukumbatiana tulikaa kwenye dawati tukiwa tunasubiri, baada ya muda daktari aliyevalia sare za kijeshi pamoja na koti la kitabibu alitoka ndani ya wodi aliyolazwa Faiz.
"dokta mgonjwa wetu anaendeleaje?" Nilijifanya nina wasiwasi nikamkimbilia daktari huyo nikamuuliza.
"mgonjwa wenu anaendelea vizuri ingawa hajarejewa na fahamu bado" Daktari huyo alitujibu.
"tunaweza kumuona dokta?" Huwaida aliuliza akiwa na wahka mkubwa sana.
"mnaweza mkamuona lakini baada ya saa moja" Daktari alitujibu halafu akaondoka akituacha tukiwa tumesimama vilevile kama tilivyokuwa tunamuuliza maswali, baada ya saa moja ya kusubiri hatimaye tuliruhusiwa kwenda kumuona Faiz. Wote kwa pamoja tuliingia ndani ya wodi hiyo aliyolazwa  Faiz hadi kwenye kitanda chake, tulimkuta akiwa amelala na hajitambui huku dripu ya damu ikiwa inaturirika kuingia kwemye mwili wake. Usoni alikuwa ana plasta kadhaaa ambazo zilimfanya Huwaida alie kama kafiwa hadi Nurulayt akawa anafanya kazi ya kumbembeleza lakini haikufanikiwa na ikabidi atolewe nje na Nurulayt kuhofia kutokea usumbufu kwa wagonjwa wengine waliolazwa humo ndani. Wodini nilibaki mimi pekee nikiwa na namtazama Faiz nikiwa na ghadhabu kubwa nilizozificha nafsini mwangu, hadi natoka wodini humo chuki yangu kwa Faiz ndiyo ilizidi kuongezeka. Niliwakuta Nurulayt na Huwaida wakiwa wamekaa kwwnye dawati lililopo pembeni  ambapo na mimi nikajiunga nao.
Baada ya wiki moja na nusu Faiz aliruhusiwa kutoka hospitali na akarudishwa nyumbani kwao Kigogo kwa ajili ya kujiuguza na huo ndiyo ukawa muda mwingine wa kupanga tukio jingine la kulifanya nikiwa mimi na Nurulayt ambaye kwangu alitokea kuwa mwanamke ninayefanya mpango mzito pamoja na kunitimizia haja za kimwili kutokana na mapenzi mazito aliyonayo kwangu. Katika kipindi hicho ndicho kipindi ambacho Faiz na alitoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa watu wa kawaida ingawa kwetu sisi mimi na Nurulayt tulikuwa tunajua kwa kina juu ya suala hilo. Utekwaji nyara wa Faiz ulikuja kujulikana kwa familia yake ambayo  ilipewa sharti gumu ambayo ilikuwa ngumu kulitimiza katika muda wa miezi minne.Huwaida alilia mpaka na na baada ya miezi minne alikata tamaa hasa alipotumiwa mkanda wa video na vijana hatari kutoka Kongo  ikionesha Faiz akiuawa kikatili, mkanda huo ulikuwa gumzo jijini na hata katika bara la Afrika baada ya kunaswa na vyombo vya habari. Maelfu ya watu kutoka nchi mbalimbali walilaani kitendo kama kile cha kuuliwa mtu kikatili, lilikuwa ni tukio lililodumu kwa muda wa miezi kadhaa vichwani na hatimaye lilisahaulika kabisa. Huwaida naye alilia sana lakini alisahau kabisa tukio lile akijua ameshampoteza mwanaume anayempenda, kipindi chote hicho mimi nilikuwa karibu na Huwaida nikiwa namfariji hadi akaniona mtu muhimu katika maisha yake kwa muda huo na alikuwa akiendelea kuniita shemeji na hata darasani alikuwa ni mtu wa kukaa karibu nami kila muda. Kipindi hicho Nurulayt alikuwa akiutumia muda wake mwingi katika kunimwagia sifa ili kumfanya Huwaida azidi kunipenda, penzi ni kama pembe kwa ng'ombe halifichiki  hata siku moja  na hata ulikate litachipua tena na litaendelea. Penzi langu kwa Huwaida lilikuwa kama namna hiyo na nilijitahidi kulificha na hatimaye nikalidhihirisha kwa kwake tukiwa tumekaa katika mgahawa wa Samaki samaki wa Mlimani city, siku hiyo ndiyo siku ilikuwa ngumu kwa Huwaida kutokana na penzi lake kwa Faiz.
"Mh! Abdul ujue mimi nakuheshimu kama shemeji yangu hilo suala haliwezekani" Siku hiyo Huwaida aliniwekea kikwazo pale nilipomfunulia hisia zangu juu yake.
"natambua hilo suala Huwaida ulikuwa ni mpenzi wa rafiki yangu kipenzi nimetokea kukupenda tangu mara ya kwanza tunakutana pale kwenye foleni ya usajiri lakini nilipobaini ni mpenzi wa rafiki yangu kipenzi ambaye ninamuheshimu na kumpenda kama ndugu yangu wa damu niliamua kumuachia ingawa mipango ya Mungu  imetokea" Nilimuambia Huwaida ambaye alionekana kuwa na aibu muda huo.
"ok, Abdul nipe muda wa kufikiria nitoe uamuzi unaostahiki" Huwaida aliniambi baada ya kujifikiria kwa muda wa dakika kadhaa, hali hiyo ilifufua matumaini katika moyo wangu wa kupata penzi nililokuwa nalipigania kwa muda mrefu. Sikutaka kabisa kumuharakisha Huwaida hivyo niliamua kumpatia muda wa kutosha wa kujifikiria nikiwa nina uhakika wa kumpata, muda huo niliuona moyo wangu umekuwa mwepesi kwa kubeba mzigo mzito kwa muda mrefu ambao hadi hapo nilikuwa nimeutua.
"ok nakupa muda wa kujifikiria nadhani utakuwa umefanya maamuzi yanayostahiki, kesho nina safari ya nje ya mji kidogo na huko nitakaa siku kadhaa. Nadhani nikirudi nitapokea jibu zuri kutoka kwako" Nilimwambia hivyo ili nimpe muda wa kutosha wa kujifikiria nikijua nitapata jibu zuri kutoka kwake, tuliongea mambo mengi tukiwa hapo na hatimaye tukaagana na kila mmojw akaondoka anapoishi.
Asubuhi iliyofuata nilisafiri kwa ndege kwa shirika la ndege la Kongo hadi jijini Brazaville katika mji wa Kongo ambayo ilikuwa ni safari ya masaa kadhaa angani, nilifanikiwa kufika Brazaville salama na nikakuta wenyeji wangu ambao nimewazoea kila siku  wakiwa wananisubiri ambao walikuja na usafiri kwa ajili ya kunipeleka eneo ambalo ninaloelekea. Wenyeji wangu walinipokea kwa furaha na tukaingia katika moja ya magari mawili waliyokuja hapo katika Uwanja wa kimataifa Maya-maya kuja kunipokea, safari ilianza salama kuifuata barabara ambayo sikuwa naitambua jina kwa masaa kadhaa tukawa tumefika kwenye msitu ambao naujua kwa jina la Patte d'ioe. Tuliingia kwenye barabara ya vumbi kisha tukatembea kwa mwendo wa kilomita kama tano tukawa tumefika kwenye uzio wenye geti la  nyavu ambalo linalindwa na watu wenye silaha nzito za moto, geti hilo lilifunguliwa gari ikaingia  hadi ndani halafu tukatembea umbali wa kilomita moja tukawa tupo mbele ya jengo la ghorofa moja. Wenyeji wangu walishuka na mimi nikashuka na  tukongozana hadi ndani ya jengo lililopo mbele yetu katika sehemu ya juu, tuliingia katika ofisi moja ya jengo hilo iliyojaa silaha za kila aina na mbele palikuwa na mtu ambaye nilikuwa nafahamiana naye sana ambaye alinichangamkia aliponiona.
"Ohooo! Somalian welcome(Ohooo! Msomaji karibu)" Mtu huyo ambaye nilimkuta alinilaki.
"Thanks , I don' have time i think you know the aim of being here(asante, sina muda  nafikiri unajua  dhumuni la kuwa hapa) Nilimwambia yule mtu.
"ok, follow me (sawa, nifuate)"Aliniambia huku akitoka nje ya ofisi na mimi nikamfuata, tulienda hadi chini ya ardhi ya jengo hilo kwenye chumba chenye giza ambacho kiliwashwa taa baada ya sisi kuingia ndani. Mbele yetu alionekana mtu aliyedhoofu akiwa amefungwa kwa kamba ngumu akining'inia, nilipoiona sura  yake niliishia kucheka hadi yule mtu akawa ananitazama kwa hasira.
"Tanzania nzima inatambua kama wewe ni marehemu hasa baada ya kuisambaza ile video ya kutengeneza ikionesha unavyouawa kikatili, ila miongoni mwa watu wachache wanatambua kama bado upo hai unakula mateso kwa ukaidi wako Faiz" Niliongea huku nikicheka kimadharau hadi Faiz akatema mate ambayo hayakunifikia.
"Jeuri siyo  kabisa, sasa nilitaka nije  nikuambie kwamba Huwaida ni wangu kwa sasa na nikirejea Tanzania jua ninaenda kukaa na mwanamke aliyepaswa kuchukuliwa na mimi mtoto wa kitajiri na si wewe masikini na jambazi wa kutupwa uliye chini ya mikono ya wabaya wako. Faiz una siku nne tu za kuendelea kuishi duniani kabla hujauawa na sumu ambayo umechomwa kupitia sindano, sasa basi nataka utambue kuwa ukifa utakuwa utakuwa msosi wa fisi na tai wala mizoga huku msituni. Buriani rafiki yangu" Nilimwambia Faiz kwa dharau halafu nikamgeukia mwenyeji wangu nikamwambia " After his death, his body suppose to be food for Hyena and Vulture(baada ya kifo chake, mwili wake  unatakiwa uwe chakula kwa Fisi na Tai). Nilipomaliza kuongea hivyo Faiz alianza kulia mwenyewe huku akisikitika kwa mambo yanayoenda kumkuta, nilitoka humo ndani nikiwa sina hata chembe ya huruma kwa huyu aliyekuwa akiniona kama ndugu yake hapo awali. Muda huo huo niliondoka huko porini kwa kutumia magari niliyoletwa nayo awali hadi katikati ya jiji la Brazaville,  nilichukua chumba katika hoteli mojawapo katika jiji la Braazaville  na nilikaa kwa siku mbili. Asubuhi ya siku  ya siku ya tatu niliondoka nchini Kongo kurudi Dar es salaam na nikafanikiwa kufika salama kwa mapenzi ya anayenipa pumzi, majira ya saa nane mchana nilikuwa njiani kuelekea hosteli nikiwa sina hili wala lile. Nilikuwa nina furaha sana  nikijua ninaenda kuanzisha ukurasa mpya wa mahusiano na Huwaida kwani Faiz angekufa ndani ya siku moja inayokuja, furaha yangu ilitimbukia nyongo baada ya mambo kwenda mrama tofauti na ilivyokuwa. Nilipokuwa nakaribia maeneo ya Tazara ikiwa ndani ya teksi simu yangu iliita kwa fujo na nilipoitoa kuangalia jina mpigaji nilikuta ni Nurulayt ndiye ananipigia, niliipokea na kuiweka sikioni halafu nikatulia kimya bila ya kuongea neno lolote.Taarifa aliyonipa Nurulayt ilinifanya nisems, "unasema mambo hovyo?.......kivipi?....upo wapi?...ok nakuja". Nilikata simu kisha nikamwambia dereva wa teksi, " kaka samahani  kwa usumbufu, naomba unipeleke Kawe sasa hivi nitakulipa hela yote ya usumbufu huu". Yule dereva wa teksi alitii nilichomuelezaa safari ikaanza kuelekea Kawe, baada ya dakika thelathini niliwasili Kawe na nikamlipa yule hela yake kisha nikaanza kutembea kuelekea  katikati ya tarafa ya kawe, nilipofika katikati ya mitaa nilienda moja kwa moja hadi kwenye geti la kiwanda ambacho kimefungwa siku  zingi. Niligonga geti kwa nguvu na baada ya sekunde kadhaa Nurulayt alikuja kufungua akiwa ameonekana kuchanganyikiwa.
"vipi kuna nini?" Nilimuuliza hapohapo.
"nifuate" Nurulayt aliniambia huku akielekea ndani, nami niliingia nikafunga geti kisha nikamfuata kule alipoelekea. Nurulayt aliniongoza hadi kwenye mashine za kiwanda hicho kidogo ambacho hakitumiki, tulipofika eneo hilo Nurulayt alinionesha kwa ishara upande ambao kulikuwa na mateka mmoja aliyekuwa amefungwa kwa kamba ngumu sana.
"sikuwa na jinsi Abdul imenibidi nifanye hivi maana siri ilishavuja kwake kupitia kwa mtu asiyejulikana" Nurulayt aliniambia huku akinitazama usoni kwa huruma, taarifa hiyo ilinifanya nijihisi naelekea kupagawa kwani haikutarajiwa kutokea.
"hebu mtoe kitambaa cha mdomoni kwanza maana naona anababaika" Nilimwambia Nurulayt huku nikimtazama kwa huruma yule mtu akiyefungwa pale. Nurulayt alimtoa kitamba kile mdomoni na hapo ndipo nikaanza kulaumiwa na mateka yule.
"Abdul yaani umeamua kuniulia kipenzi changu ili niwe nawe sasa kwa taarifa yako sikuhitaji shetani mkubwa wee" Alikuwa ni Huwaida akiropoka maneno hayo huku akilia kutokana na kitendo nilichomfanyia Faiz ingawa hakuonekana kujua kama Faiz yupo hai hadi muda, maneno hayo yalinishtua sana  kuyasikia.
"Nuru imekuaje hebu nieleze vizuri" Nilimuuliza Nurulayt ambaye aliishia kunipatia simu ya mkononi ya Huwaida bila kuongea chochote.  Niliipokea simu hiyo ambayo nilipoigusa kitufe cha kuionesha  mwanga katika kioo nilikutana na barua pepe  pamoja na picha mbalimbali za Faiz akiwa amelala akionekana ni mfu tayari, nilipomuangalia Nurulayt ambaye muda huo alikuwa ameshika kisu kikali kisha nikamuambia, "mfungulie" baada ya kuona Huwaida anatukana matusi mfululizo. Nurulayt alimfungulia kwa kuzikata halafu akasimama pembeni ya Huwaida huku anamtazama, macho ya dharau. Huwaida baada ya kufunguliwa alinifuata kwa kasi huku akiniita mwanaharamu, aliponikaribia alinipiga kibao kikali  halafu akaokota chuma kizito akiwa anahema. Alikinyanyua kila chuma akawa ananielekezea usoni ili anipigae nacho, alikinyanyua kisha akakishusha kwa nguvu. Nilibaki nikifumba macho huku nikisubiri hukumu yangu kwa Huwaida kwa kitendo nilichomfanyia, nilijiona sina thamani tena ya kuendelea kuishi ikiwa yeye anaonesha dhahiri ananichukia na hataki hata kuiona sura yangu kuanzia muda huo. Nikiwa nasubiri hukumu yangu nilihisi  kama kitu kikitoboa mfuko wa gunia kisha kimiminika kizito kikinirukia usoni, nilipofumbua macho nilijikuta nikiwa sina hata nguvu ya kusimama.


*Mambo magumu


No comments:

Post a Comment