DHAHAMA
MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA
SIMU:+255713776843
+255762219759
WHATSAPP:+255713776843
SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGIN
SEHEMU YA SITA!!
Alikiweka kile chombo mbele ya Shafii kisha akamwaga dawa zake kwenye moto uliomo kwenye chombo hicho, moshi mzito ulitanda humo ndani na mzee Sauti ya radi akawa anaimba nyimbo zisizoeleweka huku akimzunguka Shafii akicheza kama anacheza ngoma ya kikabila. Moshi huo ulipokuja kupungua Mganga akiendelea kucheza alihisi anashikwa kiuno wakati akicheza, moshi ulipoisha alihisi anashikwa makalio kwa kutomaswa. Alipogeula nyuma kumuangalia anayemshika alikutana uso kwa uso na Zalabain akiwa anatabasamu.
"Yaani ungekuwa mwanamke ungefaa kucheza Baikoko kwa jinsi inavyojua kukata kiuno" Zalabain aliongea akiwa bado hajatoa mikono kwenye makalio ya Mganga Sauti ya radi.
****
Zalabain alizidi kuonesha uso wa dharau kwa kuyaminya makalio ya mganga Sauti ya Radi na kusanabisha mganga huyo apandwe na hasira sana, Mzee Sauti ya Radi alinguruma kwa nguvu kama simba dume aliyejeruhiwa akiashiria mashetani yamempanda tayari kwa ajili ya kukabiliana na kiumbe aliyejitokeza muda huo ambaye hakuonekana na nia nzuri kwake wala kwa Shafii. Alipogeuka nyuma akabiliane na Zalabain aliambulia patupu kwani hakuonekana kabisa, Mganga alipoona anachezewa akili alizidi kupandwa na hasira mara dufu. Aligeuka kila pande za eneo alilopo lakini hakumuona Zalabain na alimuona Shafii akiwa amekaa pale alipokuwepo akionekana hajui chochote kinachoendelea, Mganga hapo alishusha pumzi kisha akasema "ana bahati sana yule".
"Nina bahati sana kwa kuweza kushika makalio yako sio, sasa nimeyashika tena ili nikujulishe kwamba bahati hiyo ni yangu tu" Sauti ya Zalabain ilisikika kwa mara ya pili na Mganga akahisi kushikwa makalio kwa mara nyingine tena safari hii alijiona kaingia katika mikono ya basha kwa jinsi alivyokuwa anatomaswa, mara hii hata Shafii alimshuhudia Zalabain akiwa yupo nyuma ya Mganga Sauti ya Radi akifanya udhalilishaji wake. Mganga alipogeuka nyuma akabiliane na Zalabain alipigwa kofi moja lenye uzito wa aina yake hadi shavu lake likachanika kabisa, Zalabain alipotea kwa mara ya pili na moshi mzito ukatanda kama ukungu ikifuatiwa na sauti ya Mganga akilia kama mtoto mdogo. Sauti ya mtu akipigwa vibao ndiyo iliyokuwa imetawala ndani ya nyumba hiyo ya Mganga kwa muda wa dakika kadhaa, ilipokuja kuisha moshi uliotanda ghafla uliondoka papo hapo na Zalabain akaonekana amesimama akiwa ameukanyaga mwili ya Mganga ambao haukuwa hata na dalili ya kuwa na uhai. Alama za mikono zilionekana katika mwili wa Mganga zilizoweka kama mhuri karibu kila sehemu katika mwili wa Mganga huyo, Zalabain alikuwa kasimama akiwa na hasira tena akiwa anamtazama Shafii huku akihema kwa nguvu sana.
Shafii naye alijikuta akitokwa na upepo bila hata kutarajia na jasho lilikuwa likimvuja kama alikuwa amekaa jirani na moto mkali kwa muda mrefu, kila akitazama macho ya Zalabain yalivyo na hasira ndiyo alizidi kusota kwa kurudi nyuma hadi akafika ukutani kabisa akawa pa kwenda hana akabaki akimtazama Zalabain kwa uoga sana.
"Unafikiri unaweza kunizuia mimi kwa kutumia nguvu za huyu mzee?" Zalabain alimwambia Shafii huku akiukanyaga mwili wa Mganga Sauti ya Radi kwa nguvu hadi viungo vikawa vinavunjika na kuzidi kumtia uoga Shafii.
"Ujue kila mwizi na arobaini yake na siku ya arobaini yake ndiyo hukamatwa au kuuliwa, sasa wewe utabaki unapumua kwakuwa arobaini yako bado ila ikifika utakufa kifo cha huzuni kuliko hata hiki cha huyu" Zalabain aliongea huku akimtazama Shafii na akamaliza kauli kwa kuikanyaga shingo ya mganga hadi kichwa chake kikaruka upande aliopo Shafii na kupelekea yowe la uoga limtoke kwa uoga kutokana na kuogopa kichwa hicho kikiwa hakina uhai. Zalabain alipotea papo hapo baada ya kichwa kuruka upande aliopo Shafii na hapo ndipo akili ya kukimbia ilipomjia Shafii na akasimama na kuanza kukimbia bila hata kuangalia wala kuangalia mlango upo wapi, alijikuta akipigiza uso ukutani katika ukuta wa nyumba ya mganga baada ya kukimbilia ukutani akijua ni mlango ulipo kutokana na kuchanganyikiwa na balaa aliloliona.
"Oooow!" Aliachia ukelele wa maumivu kutokana na kuumia pua yake alipojibamiza ukutani hapo, Shafii alinyanyuka akawa anaona mawenge tu na asijue wapi mlango ulipo. Alipoamua kutimua tena mbio alikutana tena na ukuta ulimbamiza puani kisawasawa hadi zikaanza kumchuruzika damu puani, aliumia sana lakini alinyanyuka na kuanza kukimbia tena mbio akiwa amefumba macho kwa maumivu ya puani aliyonayo. Alifanikiwa kutoka nje na akatimua mbio moja kwa moja bila hata kuangalia mbele tena akiwa na mbio kuliko kawaida, laiti angeshindanishwa na mwanariadha Usain Bolt mwenye uwezo wa kukimbia mita 100 kwa sekunde tisa angekuwa mshindi yeye kwa jinsi alivyokuwa ana kasi ya ajabu kukimbia eneo ambalo alishuhudia mauzauza ya kifo cha Mganga wake wa toka siku nyingi.
Mbio za Shafii zote hakuwa ameangalia mbele na alikuja kufumbua macho na kurudiwa na akili zake za kawaida baada ya kuhisi amekumbwa kikumbo kikubwa na mtu mwenye mwili wenye ubavu kuliko yeye, alianguka chini moja kwa moja lakini alijiinua akiwa na wasiwasi sana moyoni mwake baada ya kumshuhudia mtu aliyechafuka kwa mchanga mweupe akiwa ameshika gunia.
"hivi we mzed una akili timamu kweli? Huoni kama ulikuwa unakimbilia mtoni tena kwenye Korongo ambalo chini kuna mamba wengi sana?" Yule mtu alimuuliza Shafii huku akimshangaa sana.
"hapa ni wapi?" Shafii naye alijikuta anamuuliza yule mtu.
"We mzee umechanganyikiwa nini hebu angalia kushoto kwako" Yule mtu alimuambia Shafii huku akimuonesha upande wa kushoto, Shafii alipogeuza macho upande wa kushoto aliona yupo mita takribani mbili kutoka mwisho wa Korongo refu ambalo chini yake mto Zigi unapita tena sehemu hiyo ya mto huo mkubwa Tanga nzima ulikuwa umejitanua sana na chini mamba walikuwa wanaonekana bila hata kificho wakiwa wapo pembeni.
"Hiii!" Shafii alisema kwa uoga akaanza kukimbia upande mwingine ili akae mbali na eneo hilo la korongo.
"Mzee wangu una matatizo sana, yaani isingekuwa mimi kukuona wakati naenda kuchimba mchanga mtoni basi ungekuwa kitoweo cha Mamba sasa hivi" Yule mtu alimuambia Shafii ambaye alikuwa ametulia tayari na akawa anamsikiliza.
"asante kijana, sasa utaendaje kuchimba mchanga mtoni wakati kuna mamba?" Shafii alimuuliza yule mtu kutokana na kushangazwa na mtu kwenda kuchimba kwenye mto huo wenye mamba wengi sana, yule mtu aliposikia swali la Shafii alimuonesha kamba nyeusi iliyofungwa begani mwake yenye hirizi pamoja na simbi kadhaa.
"hii ndiyo kinga yangu Mamba hanishiki ila kwa mgeni ukisogea hata pembeni umeisha, mzee umekumbwa na nini mbona una damu puani na usoni umechanika?" Yule mtu alimueleza Shafii kisha akamtazama kwa udadisi na akagundua ameumia, alimuuliza juu ya kilichomuumiza kwani alikuwa anavuja damu nyingi sana.
"Kijana ni habari nyingine kabisa usijali sana....asante sana hii ni zawadi yako ya kukomboa maisha yangu" Shafii aliongea kisha akatoa pochi yake mfukoni akamkabidhi noti kadhaa yule mtu halafu akamuaga akaondoka. Ilikuwa bahati kwa yule mtu kupata kitita kikubwa cha pesa kama hicho kwa kumuokoa mtu asiyemjua asiingie katika maskani ya mamba wengi wa mto Zigi ingawa kwa Shafii ilikuwa ni jambo dogo sana kutoa kitita kama hicho cha fedha kwani alikuwa ni tajiri sana. Shafii alirudi hadi alipoacha gari lake akaingia akamuamuru dereva aondoe gari kuelekea hospitali.
****
Muda ambao Shafii alikuwa anaona vibweka vya kuuliwa mganga wake aliyeanza kumtumia miaka mingi iliyopita, ndiyo muda huohuo mdogo wake aliwasili nyumbani kwa shemeji yake Shafii yaani kaka wa Bi Farida mke wa Shafii anayeitwa Hamis. Ally aliingia nyumbani kwa Hamis akiwa na huzuni kwa kuwapoteza kaka zake tena machozi yalikuwa yakitaka kumtoka kila akiwakumbuka kaka zake hao, alipokelewa na mfanyakazi wa ndani wa nyumba ya Hamis na akapelekwa hadi ukumbini ambapo alimkuta Hamis akiwa amekaa kwenye jamvi akinywa shurubati ya maembe.
"Ally vipi kwema?" Hamis alimuuliza Ally kutokana na hali ya huzuni aliyomuona nayo.
"si kwema shemeji" Ally alijibu na machozi yalianza kumtoka hapo hapo.
"heeh! Kunani hebu nieleze?" Hamis alimuuliza Ally.
"Kaka Hamid na Hussein hatunao" Ally akiongea na hapo machozi yakaanza kumtoka kama chemchem.
"Eti nini?" Hamis aliuliza kwa hasira na hapo akaanza kunguruma na mwili wake ukaanza kutetemeka kama kamwagiwa maji ya baridi, Ally alipoona hali hiyo aliacha kulia hapohapo akatoka mbio kufuata ukumbi mwembamba uliopo katika nyumba hiyo na alirejea akiwa ameshika udi unaowaka akamuwekea Hamis mbele yake jirani na pua zake.
"Kuna dhahama, kuna dhahama! Linataka kuikumba familia zetu nasema sikubali lazima nililizuie......nasema sikubali! Nasema sikubali! Nasema sikub...Aaaasrgh!" Hamis aliongea akionekana tayari ameshapandisha mashetani kichwani lakini alijikuta akikabwa shingoni hadi akashindwa kuongea akabaki akitoa ukelele wa maumivu huku akishika shingo yake hadi Ally akaanza kuogopa. Hamis alianza kukoroma huku macho yakiwa yamemtoka kwa namna ya kutisha, Ally alipoona hivyo alinyanyuka akataka kukimbia lakini mtama mzito ulimkuta na yeye akaanguka chini huku mpigaji akiwa hamuoni. Alipoanguka alipigwa kofi la nguvu la kwenye shavu akatulia chini kama maji mtungini, baada ya Ally kuanguka ndipo Hamis alipohisi kuachiwa tangu aanze kukabwa. Alikohoa mfululizo akamkimbilia Ally akamtikisa Ally lakini hakuonesha dalili ya kuamka, Hamis alipagawa kabisa hasa alimpotazama Ally aliyetulia tu.
"Sijatumwa kuua bali nimetumwa kuzuia, Hamis umerithi majini kutoka kwa babu yako lakini ukataka kuyatumia kupambana na usichokiweza sasa nimeyakaba nikayaua na wewe utakiona. Huyo mwenzako pia kapata aliyostahiki kwa kiherehere chake" Sauti ilisikika ikitokea juu ya dari ikawa inavuma kama mwangwi ikapotea.
"Hamidaa!" Hamis aliita kwa nguvu huku akimnyanyua Ally.
"Abee Baba!" Sauti ya kike iliitika ikitokea chumbani.
"leta funguo za gari upesi" Hamis aliongea akielekea mlangoni, binti wa miaka takribani kumi na nane alimfuata kwa nyuma akiwa na ufunguo wa gari. Hamis alienda kwenye gari lake na yule binti akafungua mlango wa gari Ally akawekwa, geti kubwa lilifumguliwa na Hamis akaingia ndani akawasha akaliondoa kwa kasi.
SURA YA NNE
Hali ya jiji la Dar es salaam ilikuwa tulivu na muda huo sehemu mbalimbali za jiji kulikuwa kuna watu wakiendelea na pilikapilika zao za kila siku, upande wa chuo kikuu cha Dates salaam wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo yao kama kawaida yao. Ilikuwa ni vipindi vya pili vya masomo baada ya vile vya asubuhi na wanafunzi wote wenye vipindi muda huo walikuwa wapo madarasani wakifundishwa.
Darasa la wanafunzi wanaosoma shahada ya sheria masomo yaliendelea kama kawaida na muda huo Professa wa chuo hicho alikuwa akifundisha darasani na wanafunzi walikuwa wapo makini sana kumsikiliza, katikati ya kipindi aliingia kaimu mkuu wa chuo darasani akiwa na mgeni ambaye hakufahamika ni nani hadi muda huo. Kaimu mkuu alimfuata Professa aliyekuwa anafundisha akamuuma sikio kwa sekunde kadhaa, Professa alimsikiliza kaimu mkuu wa chuo kisha akaafiki kwa kutikisa kichwa.
"Zaina Buruhan you are needed (Zaina Buruhan unahitajika)" Professa aliongea na wanafunzi wote wa humo darasani wakamtazama binti aliyenyanyuka katika viti vya katikati ya darasa.
"Take your things you are not return today, there is an emergence(Chukua vitu vyako hutarudi leo, kuna dharura)" Kaimu mkuu wa chuo aliongea na Zaina akachukua vitabu vyake akamfuata Kaimu mkuu wa chuo akiwa na yule mgeni kisha wakatoka nje.
Walipofika nje kaimu mkuu wa chuo alimtambulisha yule mgeni kwa Zaina na mgeni akaonesha kitambulisho chake akajieleza kwa Zaina dhumuni lake la kuja hapo chuoni.
"kuna dharura gani huko nyumbani?" Zaina alimuuliza yule mgeni
"nimetumwa tu kuja kukufuata mengine utayajulia huko huko nyumbani, Baba yako na mama yako wameniambia nisikueleze chochote" Yule mgeni alijibu, kwakuwa alikuwa ameshakamilisha taratibu zote za hapo chuoni Zaina na yule mgeni waliondoka kwa pamoja hadi kwenye gari la kifahari alilofika nalo yule mgeni wakaingia kwa pamoja na safari ikaaza, baada ya dakika thelathini walifika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakashuka wakaingia ndani ya majengo ya ndani ya uwanja sehemu ya ndege binafsi. Walipanda kwenye ndege ndogo ya kisasa ambayo ilikuwa ikiwasubiri wao na wakafunga mikanda, milango ya ndege ilipofungwa ndege ilianza kutembea taratibu ikielekea kwenye njia za kurukia na hatimaye ikaiacha ardhi ya jiji la Dar es salaam.
Baada ya dakika ishirini ndege hiyo ilianza kuinama kwa mbele kisha ikashuka chini taratibu, baada ya muda ndege hiyo iligusa ardhi kisha ikasimama papo bila kutembea ardhini kama ilivyozoeleka ndege ikigusa ardhi lazima itembee mitaa kadhaa ndiyo isimame.
"mbona ikitua hii ndege haitembei kama ndege zingine" Zaina alimuuliza yule mfanyakazi wa baba yake aliyemfuata chuoni.
"hii ni tofauti na ndege unazozijua, unaweza ukashuka sasa" Yule mgeni aliongea, Zaina alisogea mlangoni akafunguliwa na akakutana na ngazi ya kushuka kwenye ndege zenye rangi ya dhahabu tofauti na zile alizotumia kupanda. Aliposhuka chini kabisa alikutana na mandhari tofauti na ya uwanja wa ndege wa Majani mapana wa jijini Tanga, anga la eneo hilo lilikuwa jekundu kupitiliza na lisilo na wingu hata. Mbele yake kulikuwa kuna kasri kubwa la kifahari lililotandazwa zulia jekundu kuanzia mlangoni hadi pale aliposimama, alipogeuka nyuma kuangalia ndege aliyoitumia ndipo aliposhtuka zaidi baada ya kubaini hakuwa amepanda ndege bali alikuwa yupo kwenye joka kubwa lenye miguu na masharubu kwenye mdomo na mgongoni alikuwa na kitu kama behewa la treni lilipambwa kwa vito mbalimbali na lilikuwa na ngazi ya dhahabu ambayo ndiyo ile aliyoshuka wakati anatoka. Hadi kufika eneo hilo kumbe alikuwa amempanda mnyama anayejulikana kama dragon bila kutambua akijua ni ndege, alipoona yupo katika mazingira asiyoyaelewa aliachia ukelele wa uoga na kupelekea eneo zima pembeni ya zulia kuanzia kwenye ngazi alizoshukia hadi kwenye mlango wa kaari kuonekane kuna viumbe wenye sura za binadamu wakiwa wamekaa mstari mmoja.
"We mwanadamu hebu wacha kelele" Sauti ya yule mtu aliyemchukua chuoni ndiyo ilisikika ikitokea kisha yule aliyemdhania ametumwa na baba yake akatoka ndani ya behewa lililopo mgongoni mwa dragon akiwa ana mavazi sawa na viumbe waliojipakaza mstari.
"hapa ni wapi na wewe ni nani?" Zaina aliuliza kwa uoga.
"sina mamlaka ya kujibu maswali yako msubiri mwenye mamlaka akujibu maswali yako" Aliongea kisha akashuka akapiga hatua kumsogelea Zaina halafu akamwambia "angalia kule mlangoni kama ukijijua wewe ni mgeni, mkuu wa eneo hili mjukuu wa mfalme anaingia".
Alipomuambia hivyo alipiga goti la kiheshima na viumbe wote nao walipiga goti na mlio kama wa tarumbeta ulisikika na milango ya kwenye kasri ikafunguka, Zalabain alionekana akija hadi pale alipo Zaina huku akitabasamu akiwa na umbile lake la kibinadamu.
"Karibu sana Zaina nadhani majibu ya maswali yako yote utayapata" Zalabain aliongea akitabasamu.
"Wewe ni nani na hapa ni wapi?" Zaina aliuliza akiwa na hofu.
"Naitwa Zalabain mjukuu wa mfalme na hapa ni ndani ya makao ya himaya ya Majichungu" Zalabain alieleza
"Majichungu?! Ni wapi?" Zaina aliuliza kwa wasiwasi ingawa tabasamu la Zalabain lilimuonesha kwamba hakuna hofu yoyote.
"chini ya bahari" Zalabain alijibu.
"unasema?" Zain aliuliza akiwa na mshtuko kisha akaanza kurudi nyima kwa uoga. "Haina haja ya kurudia mara mbili Zaina utanijua zaidi ila inabidi ukae huku kwa ajili ya usalama wako tu na pia kwa ajili ya tahadhari, hutakiwi kuingizwa kwenye mtego wa panya bila kujijua wakati huna hatia, Hallain!" Zalabain alimueleza Zaina kisha akaita kwa sauti na kupelekea viumbe wengine wenye sura za wanawake warembo wenye asili ya bara la Asia wajitokeze mbele ya Zalabain.
"Kiongozi wetu tumeitika wito wako" Viumbe hao waliongea kwa utiifu wakiwa wamepiga goti moja kiheshima.
"Mchukueni huyu mmoja wa wanadamu wenye heshima huku kwetu.......Zayina utakaa hapa na usijaribu kuleta ubishi upate matatizo huku binadamu wanachukiwa kwani wao ndiyo chanzo cha kuwa na wingu jekundu kila muda humu kwenye himaya na mwanga wenye nuru haufiki kutokana na kuibiwa kito Dainun cha baba yangu Zaif" Zalabain aliongea na wale viumbe wakamchukua Zaina wakatoweka naye. Baada ya Zaina kuchukuliwa Zalabain aliingia ndani ya kasri akiwa ameongozana na yule kiumbe aliyemleta Zaina hadi katika chumba cha siri cha ndani ya Kasri hilo, huko ndani ya chumba hicho walikutana na Salmin akiwa amekaa kwenye kiti kimojawapo kilichonakshiwa na mapambo ya lulu. Zalabain na yule kiumbe waliketi kwenye viti vya aina hiyohiyo wakawa wanamtazama Salmin.
"je mmefanikiwa kuipata Dainun?" Salmin alimuuliza Zalabain
"hapana bado sijafanikiwa kuipata kwani kila anayetakiwa aende na maji nikimuuliza anasema hana" Zalabain alimueleza.
"Inabidi uipate hiyo ndiyo taji la kifalme litakaa kichwani mwako hata kama ukilipa visasi hadi ukamaliza bila ile hutakuwa mfalme na hata ukiipata hujalipa kisasi bado taji litakukataa vilevile" Salmin alimuambia Zalabain.
*mambo yanazidi kupamba
No comments:
Post a Comment