Saturday, November 21, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA TATU

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



SEHEMU YA TATU!!
Asp John aliyanakili maelezo ya James kisha akajiandaa kuuliza swali jingine lakini king'ora cha gari la zima moto kilimkatisha na akajikuta akiangalia lilipo gari la zima moto. Wale vijana nao waliliona lile gari la zimamoto likipita pembezoni mwa eneo la tukio kwa tabu kisha likaingia barabarani kisha likaingia barabarani likawa linaelekea Duga Maforoni kwa mwendo wa kasi sana huku milio ya ving'ora vyake ikiwa imetawala njia nzima. Asp John alipoona hali hiyo alihisi kuna jambo na akawa anataka kujua kuna nini kilichotokea, alinyanyua simu ya upepo akaongea kwa muda kisha akatulia akasikiliza upande wa pili na akajikuta amegwaya.
"nyumba za kampuni yenu zilizokuwa zinazinduliwa zote zimeungua kwa moto  wa hitilafu ya umeme" Asp John aliwaambia wale vijana.
"eti nini?" James alisema kwa mshangao.

****

"Ndiyo maana yake hizo nyumba mlizotakiwa kuzizindua leo zote zinateketea kwa moto" Asp John alimuambia   James ambaye alionekana kutoamini  kwa alichomuambia, vijana wote wa kampuni ya Extoplus walichoka kuliko walivyochoka baada ya kusikia mali ya kampuni ikiwa inaungua. Taarifa hizo zilikuwa ni kama kupigilia msumari wa moto kwenye kidonda ambacho hakijapona kwa James, kilio chake kilichoanza kunyauka usoni mwake mithili ya mche usiopata  matunzo kilianza kuchipua tena kwa taratibu mithili ya mti wa muhogo unavyoota  majani baada ya kuwa umechimbiwa chini kwa muda wa siku kadhaa. Kilio hicho kilikolea baada muda wa dakika   mbili tu mithili ya garimoshi la makaa ya mawe lililosaza mabeleshi kadhaa ya makaa ya mawe, Asp John ilimbidi asitishe kufanya mahojiana na akawa ana kazi ya kumbembeleza James akishirikiana na wenzake ili waendelee na mahojiano. Ilikuwa ni kazi ngumu sana kumtuliza James ambaye alionekana kuna jambo jingine linamuuma ambalo halikujulikana kwa wenzake wala kwa Asp John.
"nina mkosi gani mimi?" James aliongea akiwa yupo katikati ya kilio chake.
"ya nini useme hivyo wakati  huna dalili ya kuonekana na mkosi katika maisha yako" Asp John alimfariji.
"we afande hujui hulisemalo na mimi ninajua nilisemalo" James aliongea huku akipangusa michirizi ya machozi iliyokuwa inatiririka mashavuni mwake.
"James unaongea nini mbona hatukuelewi?" Kijana mmojawapo aliyefika na James aliyefika eneo hilo alimuuliza akionekana kutatizwa sana na kauli zake.
"Gasper yaani ungejua nilichokutana nacho juzi" James alisema huku akimtazama yule kijana aliyesema hawamwelewi.
"hebu wengine nyamazeni kwanza, James  hebu eleza vizuri nikuelewe" Asp John aliongea akiwa amemahika bega James.
"Afande juzi nikiwa natoka  kazini niliamua kuelekea Makorora jirani na kituo kikubwa cha mabasi yaendayo mikoani, niliamua kwenda kwa mguu kutokana na eneo lenyewe kutokuwa mbali na ofisi yetu. Wakati navuka reli zilizopo njiani kuelekea kwenye kituo cha basi nilikutana na mwanamke wa kiarabu ambaye alinichangamkia kwa kunisalimia ingawa hatufahamiani. Yule msichana aliniambia kuwa anafikiri kuwa mimi nimepotea njia na alitaka anielekeze njia iliyosahihi kuifuata, nilimwambia mbona sikuelewi na yeye akaniambia hivi punde utanielewa wala usijali. Aliniambia nyenzo yangu kuu ya maisha imegharamiwa kwa kitu kilicholetwa baada ya kuondoka maisha ya mwingine, mzazi wako wa kiume anatambua hili ingawa  analificha ndiyo maana ana maslahi mazuri kutokana na kusitiri  kisichostahiki kusitiriwa. Sasa basi tambua na wewe unafuata njia ambayo baba yako ndiyo maana nikakuambia umepotea njia sasa basi unatakiwa ubadili muelekeo  uende njia nyingine la si hivyo utakuja kuzama shimo moja   ukiteketea  ambalo wazazi wako watazama  wakitekea siku ya sherehe ya nje ya mji. Kusema kweli nilimuona yule msichana ni kachangayikiwa na nilibaki nikiwa nashindwa hata kumuuliza swali, msichana yule nilimuona akivuka barabara kisha akawa anafuata uelekeo wa reli zinazopita pembeni ya shule ya sekondari ya Usagara . Nilibaki namtazama hadi pale lilipopita basi kubwa la abiria ambalo llinikinga nisimuone na basi hilo lilipopita sikumuona tena yule msichana na sikuelewa ameondoka vipi. Nilibaki nilishangaa kwa muda wa dakika kadhaa hadi pale nilipohisi kushikwa bega na nilipogeuka nilimuona mwanamke ambaye kiumri anafaa kunizaa akiniuliza nina tatizo gani, nilipomjibu sina akaniuliza kwanini nilikuwa naongea mwenyewe kwa muda mrefu. Nikamwambia nilikuwa naongea na mtu ambaye  tayari ameshavuka barabara ameelekea njia iliyopo relini inayoelekea katika shule ya Usagara, nilpomuambia maneno hayo aliniambia nina matatizo maana yeye alikuwa akinitazama kwa muda mrefu na ameniona nikiongea peke yangu. Niliona huyo mwanamke ananichanganya tu kama alivyonichanganya yule msichana kwa kauli zake" James alieleza akiwa amepunguza kulia kwa muda na alipomaliza aliendelea kulia, maelezo yake yaliwashangaza sana wwnzake hadi ingawa hayakuwa wazi kwao kuelewa kinamchomliza James. Imaniza kishirikina pamoja na uchawi ndiyo uliyotawala maelezo ya James, wenzake wote walimshangaa sana.
"James unajua maelezo yako hayana tija yoyote katika ushahidi wa kiserikali kwani hakuna kipengele  chochote  cha  sheria za serikali inayosema uchawi unahusika katika ushahidi pia katika maelezo yako hayajaonsha kiini cha wewe kulia uliposikia kuhusu kuungua kwa hizo nyumba" Asp John aliongea kwa upole huku akimtazama James usoni.
"Afande nimeambiwa wazazi wataketea katika shimo moja siku ya sherehe ya nje ya mji, huoni kama siku ya sherehe yenyewe ndiyo leo  na mzazi wangu mmoja ameshateketea  kwenye huu mlipuko wa basi la kampuni. Unafikiri  moto wa pili atakuwa salama huko  hebu jaribu kufikiri, tena ngoja niende hukohuko" James aliongea akionekana amechanganyikiwa kabisa kwa matukio yaliyomtokea hadi muda huo, aliamua kunyanyuka ili aondoke lakini Asp John akamzuia na kupelekea aanze kizazaa kutokana na fujo alizozianzisha James. Wenzake nao walijaribu kumtuliza lakini ilishindikana kabisa na  hata walipomzuia alipiga makelele kama kichaa akiwasihi wamuachie.
"James hebu tulia kwanza huna uhakika wa kifo cha baba yako sasa fujo za nini?" Asp John alimuambia
"unasemaje wewe? Hivi ingekuwa ndiyo wewe unakutana  na mtu anakupa habari za namna hii na siku himi uliyoambiwa unakutana na mabalaa kama hili utakuwa katika hali gani? Hebu fikiri ingekuwa ndiyo mzazi wako na si kufikiri imemtokea mwenzako" James aliendelea kulalamika huku akizidi kuleta utata kwa Asp John na wenzake waliombana ili asiondoke.
"subiri basi nimalize kukuhoji ndiyo uende James" Asp John alimsihi.
"hapa hahojiwi mtu ikiwa sijaenda Duga kumuona kama baba yangu yupo hai au la, ukitaka mahojiano nami basi uniache niende na nikitoka huko ndiyo unihoji" James alizidi kuwela utata.
"ok haina shida ngoja twende wote huko kwa gari....Kostebo ondoa gari usawa wa Duga Maforoni" Asp John alimuambia James kisha akapaza sauti kumuambia  askari aliyekuwa amekaa kwenye usukani.
"afande" Aliitikia yule askari kidha akawasha gari na akaweka gia akaanza kulipitisha gari pembeni ya barabara kuvuka eneo lenye utepe halafu akaongeza mwendo kuelekea Duga maforoni.

****

  Muda ambao ajali ya pili ya moto inatokea kwa upande mwingine mkoa wa Tanga katika sehemu ya jiji kulikuwa kuna kikao kizito cha viongozi waiuu wa kampuni ya Extoplus wakiongozwa na mwenyekiti mtendaji na mmiliki wa kampuni hiyo bwana Hamid Buruhan, kikao hicho kilikuwa kinajadili mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza kampuni hiyo. Mambo mbalimbali ya kimaendeleo yalikuwa yakijadiliwa kuhusu kukuza kampuni ikiwemo suala la kuongeza nyumba za kupangisha katika sehemu zote zenye maendeleo duni ambazo watumishi wa umma hupelekwa ili wapate makazi bora kama waliyoyaacha mjini. Mojawapo ya kutekezwa mpango huo ulikuwa umeshaanza katika kijiji cha Duga na ulitegemea kuendelezwa katika sehemu zingine za Tanga nzima, mameneja hawa wakuu walikuwa, mkurugenzi, pamoja na mwenyekiti mtendaji wa kampuni hiyo walionekana wana ari ya kuwa na kampuni kubwa yenye maendeleo katika kila kona ya nchi na hata nchi nyingine.
"Hadi kufikia mwaka 2020 mpango wetu huu utatufikisha mahala tulipojiwekea kufika katika nyanja za kimaendeleo. Extoplus kwa maendeleo" Hamid alihitisha kisha  kikao hicho na hapo kikao kikawa kimefikia mwisho kwa siku hiyo, alipeana mikono na wafanyakazi wake wakuu huku akibadilishana nao mawazo kwani walikuwa pia ni marafiki zake.  Walionekana na furaha sana wala hawakutambua kama kuna kuzungumkuti kimetokea kinachohusu kampuni yao, walikuwa na furaha sana kutokana na kiasi kikubwa cha fedha wanachokiingiza kutokana miradi yao na hata uzuri wa maisha wanayoishi.
"GRIIIIII! GRIIIIIIII!" Mlio wa simu ya mezani isiyo na waya ulisikika ukilia ambayo ilikatisha maongezi na Hamid akaipokea  kisha akasema, "halloo!".
"kuna tatizo gani wewe Gasper hebu eleza vizuri nikuelewe" Hamid aliongea
"etii! Unase.."Hamid alisema kwa mshangao sana akionekana ameshtushwa sana na taarifa aliyopewa na hata maneno aliyoyataka kuyasema hakuyasema kabisa kwani nguvu zote zilimuishia kutokana na taarifa hiyo na akaanguka kama gunia la chumvi akiwa tayari ameiachia simu. Wenzake walipomfikia na kumtazama mapigo yake ya moyo walikuta yanapiga kwa mbali na ikawalazimu wote kwa pamoja wambebe kumuwahisha katika zahanati ya kampuni hiyo iliyopo ghorofa ya pili ya kampuni hiyo, walifanikiwa kufika salama na wakamuingiza kwenye wodi akaanza kuhudumiwa kwa haraka sana. Mameneja wakuu wote walikaa kwenye dawati la kusubiria wagonjwa ili wasubiri majibu ya daktari pamoja na wauguzi ambao walikuwa wanashughulika katika kumtibu mkuu wao wa Kampuni, baada ya kupita dakika kumi na tano tangu waanze kusubiri kaimu mwenyekiti mtendaji wa kampuni na hiyo na rafiki wa karibu wa Hamid  anayeitwa Hisan Shelukindo alinyanyuka kwenye dawati la kusubiria wagonjwa akasema, "jamani mimi nimesahau simu katika chumba cha mkutano floor ya nane wacha niifuate nitarejea maana  ni muhimu kuwa nayo kwa ajili ya kupokea taarifa muhimu".  Hisan aliposema hivyo wenzake waliitikia kwa kutikisa vichwa kisha akaondoka hadi nje ya mlango wa kuingilia katika zahanati, akitokea kwenye korido kisha akatembea hadi zilipo lifti za jengo la kampuni yao. Alibonyeza kitufe kilichokuwa kipo jirani na lifti kisha akasubiri kwa muda mfupi ambapo lifti ilifunguka akaingia akabonyeza kitufe namba nane, milango ya lifti ilijifunga na lifti ikaanza kupanda kuelekea juu hadi ghorofa ya nane, lifti ilifunguka kisha Hisan akashuka akatembea hadi kwenye mlango wa chumba cha mkutano akaufungua. Alikutana na giza kutokana na taa ya humo kuzimwa na chumba chenyewe huwa hakipitishi  mwanga hata mchana kutokana kuwa na vioo visivyoruhusu mwanga kupita.
"Mmh! Hizi taa za humu kazizima nani tena" Hisan ajisemea huku akiwasha taa na ilipowaka alirudishia mlango wa chumba hicho cha mkutano kisha akatembea kuelekea mezani alipoiacha simu yake, akiwa yupo katikati ya umbali uliopo kati ya meza na mlango taa za humo ndani zilizima tena na giza likarudi kama ilivyokuwa awali kabla hajawasha taa.
"Shit! Hawa vijana wa chumba cha kuongozea umeme wanafanya upuuzi gani, inamaana wameachia umeme wa Tanesko ndiyo ufanye kazi" Hisan alijisemea kisha akageuka ili aende kufungua mlango ili hata mwangaza wa madirisha yaliyopo kwenye ngazi yamuongoze kuifuata simu yake, alipopiga hatua moja taa zikawaka ten akaghairi kwenda kufungua mlango  akarudi kuchukua simu yake. Alianza kutembea kuelekea kwenye meza na alipofika akaichukua simu yake halafu akaanza kuelekea mlango ili atoke nje, alitembea kwa hatua kubwa hadi mlangoni akanyonga kitasa kuufungua lakini haukufunguka na ilionekana ulikuwa umefungwa kwa nje. Hisan alijikuta  akiachia tusi zito sana kutokana na kitendo hicho, aligeuka nyuma  akaangalia chini akaiona simu iliyoangangushwa na Hamid alipopoteza fahamu.
Wazo la kuiokota ndiyo lilimjia kichwani mwake na akalitaka kulitekeleza tu kwani hakukuwa na njia nyingine itakayomuwezesha yeye kupata msaada kutoka nje, alipoanza kupiga hatua ili aifuate taa zilizimika tena kisha kofi zito lilitua shavuni mwake lililompeleka hadi chini. Taa zilipowaka hakuona mtu yoyote ndani ya chumba hicho ingawa maumivu ya kofi alilopigwa alikuwa anayasikia, aliposimama miguu yake yote ilizolewa yote kama anapigwa mtama na akajikuta ameenda kusalimiana na sakafu yenye marumaru katika chumba hicho. Taa za chumba hicho zilizima tena safari kipigo kizito kikawa kinamshukia Hisan bila hata kumuona huyo anayempiga, taa zilipowaka tena Hisan hakuwa anaweza hata kuinuka na alikuwa akitokwa na damu usoni sehemu nyingine za mwili wake na mbele yake kulikuwa kuna mtoto wa miaka takribani saba akiwa amekasirika san ambaye sura yake haikuwa ngeni sana kwa Hisan.
"Jamadin" Hisan aliita kwa uoga na macho  yake yakawa yakimtazama yule mtoto.
"nipe" Yule mtoto alisema kwa sauti nzito iliyojaa kitetemeshi.
"nikupe nini?!" Hisan aliuliza kwa uoga.
"narudia kwa mara ya mwisho nimesema nipe" Yule mtoto aliongea kwa hasira akaanza kumfuata Hisan
"nikupe nini?!" Hisan aliongea akiwa anatetemeka akijiburuta kusogea nyuma kwa makalio yake, Yule mtoto alizidi kumsogelea na alipomkaribia alipotea kimaajabu akamuacha Hisan akiwa anashangaa lakini mshangao wake haukudumu kwani alijikuta akishikwa kichwa chake kwa nguvu kutokea upande wa nyuma. Kichwa chake kiliminywa kwa nguvu hadi kikapasuka na akawa ameingia katika orodha ya wasio na uhai waliowahi kuwa hai.

****

Gari ya waliyopanda James na wenzake pamoja na Asp John ilikuwa ilienda kilomita kadhaa kutoka pale bwaga macho kwenye ajali wakaikuta ile gari aina ya Landcruiser prado iliyotumiwa na wakina James kuja nayo ikiwa ipo pembeni na mwenzao akiwa yupo pembeni akiwa ameegemea. Gari ya polisi waliyopanda kina James ilienda kuegeshwa mbele ya gari hiyo na kisha wote kwa pamoja wakashuka wakamfuata mwenzao wakiwa na Asp John.
"Vipi Tom gari mbovu nini?" Gasper alimuuliza yule mwenzao waliyemuachia gari arudi nalo kule Duga kwenye sherehe ya kampuni.
"aisee hii gari kuiendesha ni kujitakia kifo bora mlivyokuja tuondoke wote mimi siigusi  tena na kazi kwenye hii kampuni naacha" Tom aliongea  huku akiwafuata.
"kuna nini kijana?" Asp John alimuuliza.
" jamani baada ya kuniachia hii gari nimeendesha vizuri ila nilipo fika hapo nyuma nikiwa kwenye mwendo mkali naanza kusikia sauti ya bosi mkuu ikivuma kama mwangwi masikioni mwangu ikisema nataka damu ya vijana wangu kumi. Nikiwa najifikiria juu ya eneo inapotoka sauti hiyo si ndiyo nikashudia kioo cha mbele chote kikiwa kimejaa damu hadi nikawa sioni kabisa ingawa nilijitahidi kusimamisha gari nikafanikiwa na hapo damu hizo zikawa zimetoweka mara moja na kioo kikawa kawaida kama ilivyokuwa awali. Nimeshuka ndani ya gari  na sina hamu nalo tena" Tom aliongea akiwa anahema sana kwa uoga, wenzake wote waliposikia kilichomkuta ndiyo walizidi kuingiwa na hofu kasoro tu Asp John alionekana yupo kawaida tu.
"nyie hebu wacheni uoga wenu, wewe hebu nipe hizo funguo za gari hiyo niendeshe mimi na nyinyi pandeni hiyo ya polisi tuondoke" Asp John aliwaambia akionekana hana hofu kabisa.
"Afande utakufa usipande" James aliongea.
"kwani wewe ndiyo utakuwa hufi, kama leo ndiyo  nitatakiwa nife nitakufa tu hata nisipoendesha hili gari, hebu nipe ufunguo sasa"Asp John aliongea na Tom akampatia ufunguo wa gari.
"mambo si hayo bwana sio kuleta uoga wa kike wakati nyinyi ni wanaume" Asp John aliongea akiwa anaelekea kwenye gari ya kampuni ya Extoplus baada ya kukabidhiwa ufunguo na Tom, aliufikia mlango wa gari hiyo akaufungua akawa anaingia ndani ya gari.
"leo sihitaji damu ya askari jasusi nataka ya hawa hapo mbele sasa ukijipendekeza tu katika jambo lisilo kuhusu utasalimiana na kaburi" Sauti ya mwangwi ilivuma kwenye masikio ya Asp John lakini akaipuuzia na kuamua kuingia ndani ya gari kisha akaiwasha gari hiyo, alinyonga ufunguo na gari ikawaka kisha ikazima. Alinyonga tena ufunguo safari hii gari ikatikisika sehemu ya injini kisha  moto mkubwa ukawaka ukawa unakuja kwa kasi mithili ya moto wa nyikani kwenye katika upande aliopo Asp John.
"Ha!  Ha! Ha! Ha! Si mbishi wewe ngoja nikuchome kama kuni" Sauti yenye kuvuma iliendelea kusikika masikioni mwa Asp John na hapo  akaona hatar ipo mbele yake na akaamua kujirusha nje akaangukia upande  wa pili barabara sehemu yenye majani, moto uliokuwa unawaka ndani ya gari haukuonekana na wala gari halikuonesha kama linalipuka. Asp John alijinyanyua kutoka pale alipojirusha akaenda hadi pale alipowaacha vijana wa kampuni ya Extoplus akawaambia, "pandeni kwenye gari tuondoke".
"Afande kulikoni mbona umejirusha nje baada ya gari kuwaka si ulisema unaliendesha" Tom alimuambia Asp John kwa kejeli kutokana na tabia yake ya kudharau mambo anayoambiwa.
"kaa kimya na upande kwenye gari na mwenzako tuondoke" Asp John aliongea huku akipanda kwenye gari la polisi aliyokuja nayo, vijana wa Extoplus nao wakapanda na safari ikaendelea na muda huo ndiyo Gasper alimpigia simu msichana wa mapokezi makao makuu aliyemuunganisha simu na  mkuu wao Hamid akamueleza tukio zima. Baada ya dakika kumi na tano walikuwa tayari wameshafika  Duga maforoni na wakielekea moja kwa moja hadi kwenye soko kuu la Duga maforoni wakashukia upande huo kutokana na upande wa pili kwenye eneo la tukio kutokuwa na nafasi, walivuka barabara wote kwa pamoja wakaupita uwanja wa mpira wakakuta umati wa watu ukiwa umezunguka nyumba hizo bado zilikuwa zinateketea na moto huo ulishindikana kuzimwa na kikosi cha zima moto kilichofika hapo kwani magari yao yalitumia maji hadi yakaisha lakini moto haukuzimika hata kidogo. Asp John pamoja na wale vijana waliwafuata wale askari wa jeshi la polisi kikosi cha zimamoto ambao walionekana kukata tamaa kabisa katika uzimaji moto, maaskari hao walitoa saluti kwake huku wakisema, "jambo afande".
"jamboo, nipeni taarifa mmefikia wapi katika kazi yenu kwani naona bado moto unawaka" Asp John aliwaambia.
"Afande tumefanya juhudi za kuuzima huu moto kwa kutumia  kila njia ila imeshindikana hadi maji yanaisha hatukuweza kuuzima na ikatubidi tutumie gesi lakini bado tumeshindwa kuuzima na inasadikika Mkuu wa idara ya sheria makao makuu ya kampuni hizi yupo ndani ya nyumba ya tatu na hajatoka hadi muda huu na hata tulipofika tulikuwa tukisikia kelele za mtu akiomba msaada lakini sasa hazisikiki" Mmoja wa maaskari wa zimamoto aliongea kwa ufupi juu ya tukio hilo la kuungua kwa nyumba hizo, James aliposikia maelezo hayo alipiga kelele huku akiita, "Babaa!". Aliwapita askari wa kikosi cha zimamoto akakimbia kuelekea ulipo moto katika nyumba ya tatu ya kampuni, maaskari wote walianza kumkimbiza ili wamuwahi asiingie ndani ya moto huo kutokana na ukali wake.


*Balaa linazidi

*Mtoto mdogo anataka apewe, apewe nini tena




No comments:

Post a Comment