Thursday, November 19, 2015

KOSA SEHEMU YA PILI








    KOSA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA

SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



 ILIPOISHIA
 Walijumuika naye mezani hapo huku wakimtazama sana usoni.
"hivi baba yale ni matukio ya kweli?!" Hussein aliuliza.
"kwa sasa siwezi kuwajibu  mpaka mmalize  kusoma yote" Baba yao aliwajibu.
"ni kisa chenye kuvutia sana" Hassan aliongea akiwa na tabasamu usoni hata kile kilio chake kilichokuwa kinamsumbua sana alikisahau kutokana na kuvutiwa na ukurasa  wa kwanza wa maelezo yaliyomo ndani ya Shajara ya baba yake.
"malizeni kula kwanza ndiyo mengine yatafuata, kama kuongea basi ongeeni mkimaliza kula" Baba yao aliwaambia.





ENDELEA NA MKASA HUU WENYE KUFUNDISHA


SEHEMU YA PILI!!
Hassan na Hussein walikula kwa haraka ili wawahi kuisoma ile shajara ya baba yao ambayo imetokea kuwa kivutio kwao, kisa walichokisoma kwa ukurasa mmoja tu kiliwavuta wakasome zaidi. Walipomaliza kula wakirudi hadi chumbani kwao walipoiacha shajara hiyo, jambo la kuisoma shajata kwa muda huo ndiyo lilikuwa katika akili zao. Vijana hawa ambao wapo likizo kubwa ya chuoni kwao, waliamua kuutumia muda wao huo wa mapumziko kwa ajili ya kuisoma shajara hiyo.  Wote kwa pamoja walipanda kitandani kwao huku kila  mmoja akitaka awahi kuishika shajara hiyo na kupelekea waanze kugombania kuishika shahara hiyo, walikuwa kama watoto wa shule ya msingi  ya kata wakigombea kitabu darasani ili wasome darasani. Vijana hawa walianza kuivuta shajara hiyo kila mtu upande wake na hawakutaka waisome kama walivyosoma awali, yote haya ilikuwa ni papara za kutaka kuisoma shajara hiyo kutokana na kuvutiwa nayo.
"Hussein utaichana" Hassan alimwambia mwenzake kwa kulalamika.
"tulia basi na mimi nisome" Hussein aliongea akizidi kuivuta shajara hiyo.
"kwani mimi ndio sitaki kusoma" Hassan aliongea.
"basi tusome wote" Hussein aliongea huku akiiweka shajara katikati yao.
"mambo si hayo sasa, tuendelee kusoma" Hassan aliongea baada ya kuridhishwa na uamuzi wa Hussein.

****

Uji uliokuwa upo mezani niliunywa kwa pupa ingawa ulikuwa na ladha nyingine yenye kuvutia ambayo sikuwahi kuionja, ulikuwa ni uji ambao hata nyumbani Tanzania huwa hatuunywi kabisa na sikuweza kuutambua umetengenezwaje hadi kuwa hivyo ingawa ulikuwa ni wenye ladha nzuri sana. Nguvu za mwilini mwangu zilianza kunirudia kwa taratibu na nikajihisi mwepesi kutokana na uji huo ulionipa nguvu kidogo, jambo la kwanza kulifanya baada ya kumaliza kunywa uji huo ni kujinyoosha viungo vyangu ambavyo vilikuwa vikiniuma sana. Baadaye niliikumbuka bahasha niliyokabidhiwa na Jonas ambayo ina picha yangu ndogo, nilipoiona bahasha hiyo tu maswali mfululizo yasiyo na majibu yalianza kupita kwenye halmashauri ya ubongo wangu. Bahasha hiyo nilipoifungua nilokutana na karatasi yenye maneno machache sana ambayo niliyasoma kwa pupa, nilipomaliza kusoma karatasi hiyo nilizidi kushangaa sasa nikatambua kuna mchezo ambao siujui nachezewa na mtu anayenijua lakini mimi simjui. Karatasi hiyo iliandikwa hivi, 'ABDULHAFIDH KARIBU SANA NAMIBIA ILI UPATE SOMO JINGINE LA KUYAONGOZA MAISHA YAKO YALIYOPOFULIWA NA PESA ULIZONAZO, SASA UNACHEZA NA MTU MWENYE PESA KAMA WEWE NA MWENYE UWEZO WA KUFANYA LOLOTE KATIKA DUNIA HII NA HATA KUKUFILISI WEWE UKABAKI MASIKINI KATIKA MAISHA YAKO YOTE INGAWA SITAKI KUFANYA HIVYO. HUU NI MCHEZO KATI YANGU MIMI NA WEWE SASA JIANDAE KUCHEZA MCHEZO HUO NA MTU MWENYE PESA KAMA WEWE ASIYE NA MZIZI NDANI YA DUNIA HII, NAJUA UTAJIULIZA MIMI NI NANI NA NINAFANYA HAYA KWA LENGO GANI. UKITAKA MAJIBU YA HAYA MASWALI NA UKITAKA URUDI KWAKO SALAMA BASI USIJIFANYE MJUAJI KWANI NAKUONA ULIPO NA NAITAMBUA KILA HATUA YAKO, KILA LA HERI'.  Karatasi hiyo ilizidi kunichanganya na nikajikuta sina la kufanya zaidi ya kuduwaa tu nikiwaza na kuwazua lakini sikupata jibu kabisa, mtu mwenye pesa kama mimi asiye na mzizi ndani ya dunia hii sikuweza kumtambua hata nilipoushughulisha ubongo wangu kwa kwa namna yoyote. Kichwa changu nilihisi kikishindwa kuhimilo haya matatizo ambayo yananikuta katika kipindi hichi cha maisha yangu kwa muda huu, nilizidi kuchoka bila hata kufanya kazi hasa kila nikiyafikiria mambo yanayonikuta katika maisha yangu. Tayari nilikata tamaa ingawa dini yangu ya kiislamu inaniambia anayekata tamaa ni yule asiye na imani na asiye miongoni mwa waumini, ndugu msomaji usiombe matatizo kama haya yakufike halafu dini una imani hafifu au umeiweka kando kama mimi. Utaomba dua zote unazozijua kwa Mwenyezimungu na utakumbuka uwepo wake katika matatizo kama haya kama ulikuwa dini umeiweka kando, pia unaweza kukanusha Mungu hayupo pamoja nawe ikiwa una imani ndogo katika dini yako. Haya mambo yanamkuta mtu yoyote na muda mwingine matatizo katika maisha ni sehemu ya kipimo cha imani yako , kwangu mimi mtoto wa tajiri aliyekuwa mwenye imani sana nilijikuta nikimkumbuka  Mungu baada ya kuiweka dini kando kwa muda mrefu. Hakika matatizo yaliyoniweka njia panda yalinizidi uwezo na hata kuyamudu niliona sitoweza ingawa sikukubali ninyooshe mikono juu kuonesha nimeshindwa.
"Eeeeh! Mungu wee nimekosa nini mja wako mimi" Nililalamika peke yangu nikiwa namtamguliza Mwenyezimungu baada ya kumuasi kwa muda mrefu kwa mambo niliyokuwa nayafanya ambayo kwake yalikuwa hayampendezi hata kidogo, nafsi yangu iliniambia mimi ni mpotevu na sina kimbilio zaidi ya ninayemuabudu huku nikisahau  kuwa nilikuwa nimefanya mambo yasiyompendeza kwa muda mrefu sana. Kumbukumbuza maneno ya marehemu baba yangu katika kuniusia kuhusu kuswali na kufanya mema ndiyo zilikuwa zinatafuna sehemu kubwa ya ubongo wangu, laiti kama nisingejiingiza kwenye mchezo wa kununua makahaba yote haya yasingenikuta na nisingekuwa hapa nilipo kwa muda huu. Usemi wa waswahili usemae 'majuto ni mjukuu' ndiyo sasa ulianza kuonekana katika haya mambo yaliyonitokea na nilitamani hata siku zirudi nyuma ili niweze kusahihisha mambo niliyoyafanya na hata kufuata ushauri wa marehemu baba, jambo hilo halikuwezekana kwani siku haziwezi kurudi nyuma haijawahi kutokea suala kama hilo. Msemo wa mwanafalsafa wa mwandishi wa kitabu kiitwacho STUDENT'S COMPANION chenye kusheheni misemo,nahau na methali mbalimbali za lugha kingereza, ndiyo niliweza kuuona ukiwa na ukweli ndani yake. Msemo huo 'what done can not be undone' uliotafsiriwa kwa kiswahili 'kilichofanyika hakiwezi kuwa hakijafanyika', ndiyo hasa ukweli wake umedhirika kwa kutoweza kuyafanya yaliyofanyika yawe hayajafanyika. Hakika mwandishi WILFRED D BEST wa hicho kitabu nilichopenda kukisoma kipindi nikiwa shuleni alikuwa na maana pana katika maneno  yake ambayo nimekuja kuitambua nikiwa ugenini tena mbali na nyumbani.

       Baada ya saa moja kupita tangu nilipoisoma ile karatasi yenye bahasha ya rangi ya kaki, Jonas aliingia ndani ya chumba nilicholala ambacho kwangu kilikuwa kama kaburi kutokana na kuzoea maisha ya raha na kusahau kama kuna shida na dhiki katika dunia hii. Alikuwa amevaa mavazi mengine tofauti na nilyomuona nayo wakati anaingia kwa mara ya kwanza humu ndani na hata wakati ananiokoa kule ufukweni.
"Abdi nadhani upo sawa na unaweza kunieleza juu ya masaibu yaliyokupata" Jonas aliongea kwa upole huku akinitazama usoni, maneno yake yalinifanya nishushe pumzi kisha nikaanza kwa kumsahihisha kwa kulitamka jina langu tofauti na nilivyomwambia. Niliongea, "ni Abdul sio Abdi" kisha nikampatia karatasi niliyoikuta ndani ya bahasha halafu nikamwambia, "hebu soma hii kwanza halafu ulinganishe na maelezo yangu niliyokuambia hapo awali". Jonas aliipokea ile karatasi kisha akaanza kuisoma kwa umakini na aliirudia mara mbili ili ahakikishe kuwa kama alichokisoma ndicho au alisoma vibaya maelezo hayo, alipomaliza aliikunja ile karatasi halafu akanipatia.
"hiyo karatasi imetoka kwenye hiyo bahasha  uliyonipatia" Nilimuambia huku nikiipokea hiyo karatasi niliyompatia.
"Abdul unajua mwanzo nilijua umechanganyikiwa kutokana na maelezo uliyoyatoa lakini sasa nimeanza kukuamini. Kwanza mra ya mwisho ni lini ulikuwa kwako?" Jonas aliongea.
"mara ya mwisho nakumbuka ni jana jumapili ndiyo nilikuwa kwangu na usiku niliingia na mwanamke na asubuhi nilikuja kuamka nikajikuta nipo kwenye kisiwa chenye nyoka mkubwa" Nilimwambia nikiwa nimeweka mikono kichwani kwangu kwa kukata tamaa na matatizo haya.
"unajua leo sio jumatatu mpaka useme jana ilikuwa ni jumapili, leo ijumaa  ndugu na inawezekana umewekewa madawa ya kukulevya yaliyokulaza siku tano hadi leo" Jonas aliongea kunisahihisha kuwa nilikuwa nimekosea siku, hapo ndipo nilizidi kuchanyikiwa na nikawa naona watu walionifanyia hivi sio watu wa kawaida kabisa bali watakuwa ni wenye kujua kitu gani wanachokifanya.
"inamaana nimekuwa sijitambui kwa muda wa siku tano?!" Nilijikuta nikimuuliza Jonas kwa mshangao mkubwa sana.
"ndio maana yake, pole sana ndugu yangu kutoka katika nchi yangu" Jonas aliongea.
"Jonas umesema wewe ni mtanzania umefikaje huku" Nilimuuliza Jonas nikiwa nimeweka kando matatizo yanayonihusu na nikiwa nina shauku kubwa ya kutaka kujua zaidi kuhusu yeye.
"ni maisha tu ndugu yangu ndiyo yamenifikisha hapa nilipo, mimi nimezaliwa katika familia ya hadhi ya chini na nimekulia kimasikini. Nimesoma hadi kidato cha nne nikawa nimefanya vibaya na nikaamua kuzamia nikiwa na Afrika ya kusini kwa kutumia lori nikiwa na kaka yangu  lori hilo lililotupeleka hadi Congo kisha tukaingia kwenye meli sehemu ya injini iliyokuwa inaelekea Afrila ya kusini kwa kupitia bahari hii ya Antlantiki, ilikuwa ni safari yenye misukosuko na hadi tunakaribia bandari ya Cape town Afrika ya kusini tuliamua kujitosa kwenye maji kisha tukaogelea hadi nchi kavu. Maskani yetu katika jiji hilo yalikuwa ya kuhamahama na kipato kilikuwa si cha kuridhisha kutokana kazi ndogo tunazozifanya, mwisho wake tukaamua kujiingiza katika ujambazi na uuzaji wa madawa ili tupate pesa kwa haraka tuwe na mafanikio tuliyokuja kuyatafuta. Kazi hii haramu hatukudumu nayo kwani kaka yangu  aliuawa na wenzetu kwenye biashara hii na kigogo mmoja wa nchini humo  ambaye ndiye mkuu wetu akanipa kesi hiyo mimi ili aweze kuniharibia maisha yangu. Hapo ndipo nikakimbila huku na nikaanza kutumia jina langu halisi na nikaacha jina bandia la Mike nililokuwa nalitumia" Jonas alielezea kwa kifupi  historia ya maisha yako hadi akafikia hapo alipo katika nchi hii.
"pole sana ndugu" Nilimuambia kutokana na kusikitishwa na historia yake na magumu aliyopitia mpaka kuingia Afrika ya kusini kwa njia za panya, Jonas nilimuona ni mtu jasiri kwa matatizo hayo aliyoyapitia. Nathubutu kusema ingekuwa mimi mtoto niliyelelewa kwenye raha nisingeweza kufanya hivyo ila kwa huyu kijana shupavu na mjasiri imewezekana.
"Abdul unajua watanzania katika sehemu za ugenini kama huku huwa ndugu, hivyo ukae utambue kuwa sisi ni kitu kimoja na usiongee kiswahili tena maeneo haya ya Walvia" Jonas alinisisitiza.
"sawa nimekuelewa ingawa mimi hiyo lugha mnayotumia siijui nitatumia kingereza" Nilikubali maneno yake kwasababu yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu katika nchi hii ambayo ni ngeni kwangu na sikuwa naweza kumpinga mtu kama yeye aliyeniokoa na kunipa hifadhi.
"Kiafrikaas nitakufundisha ili uongee kama wengine katika kijiji hiki, sasa ngoja mimi jioni hii nielekee baharini maana uvuvi ndiyo kila kitu" Jonas aliniambia huku akielekea mlango.
"Jonas twende wote hapa kumeshanichosha kukaa ndani peke yangu muda wote huo najihisi mpweke" Nilimuambia Jonas huku nikisimama.
"kama upo sawa twende ili ujifunze na wewe kuvua" Jonas aliniambia huku akifungua mlango kwa ajil ya kutoka nje, nami nilimfuata nyuma kwani yeye kiongozi wa njia kwangu. Nilitoka nje ya kibanda hicho kwa mara ya kwanza tangu nilipoletwa nikiwa sijitambui, niliweza kuona mandhari ya eneo hilo vizuri ingawa tayari giza lilishaanza kuingia na taa mbalimbali zenye kutumia moto zikiwa zimesheheni katika vijumba vidogo vilivyojengwa kwa mabati katika kijiji hiki. Kilikuwa ni kijiji kilichochangamka sana  kutokana uwepo wa watoto wenye uchangamfu  kwa watu wazima na waliojaa adabu pia waliokuwa wakicheza michezo mbalimbali ya kitoto. Hakika walikuwa ni watoto wenye adabu na heshima tofauti na hawa wa nchini kwetu, kwani kila nilipopita walinisalimia kwa lugha ya kwao ingawa sikuwa naielewa.
" goeienaand(habari ya jioni)" nilipokea salamu hiyo ambayo sikuwa naielewa na niliishia kutabasamu tu huku nikiwapungia mkono. Jonas alikuwa akiwajibu,"goeienaand" kama walivyomsalimia. Watu wa kijiji hichi kidogo walionekana ni watu wastarabu sana kwani kila tulipopita tulikuwa tukipokea salamu mbalimbali za lugha ya Kiafrikaas ambazo nyingine niliishia kuzibahatisha kwa sababu zimeingiliana na lugha ya kingereza kimatamshi. kijiji hichi cha watu wa hali ya chini kilionekana kunivutia sana  hasa muundo wa nyumba zao ndogo. Hadi tunafika baharini nilikuwa nimeburudika vya kutosha kwa kuangalia mazingira ya ugenini nilipo kwa muda huo kwa muda huo. Mtumbwi wenye shuka kubwa ndiyo uliokuwa upo kwenye maji ukiwa una vifaa vyote kwa kuvulia, naweza kusema hiyo ilikuwa ni siku nyingine katika maisha yangu kwani nilipata ujuzi mpya wa kimaisha wa kuweza kuvua samaki katika bahari. Tulifanya shughuli za kuvua wote kwa pamoja baada ya kuelekezwa vitu vidogovidogo katika uvuaji wa samaki, hadi inaingia usiku wa manane tayari mtumbwi wetu ulikuwa umejaa samaki na safari ya kurudi ufukweni ilianza. Tulifanikiwa kufika ufukweni salama na tukashusha samaki wote  kwa ajili ya kwenda kuuza. Muda wote huo nilikuwa bado sijasahau matatizo yaliyonikumba ingawa nilionekana kuwa na furaha iliyotokana na kupendezwa na mazingira mapya ninayoyakabili, kutabasamu au kufurahi katika kipindi cha matatizo kutokana na jambo lolote la kumfanya mtu atabasamu ni kawaida kwa binadamu yoyote hata awe na matatizo kiasi gani. Hata mimi nilifurahi sana kutokana na kuona ni jambo lenye kufurahisha moyo wangu uliojaa matatizo nisiyoyajua ni nini chanzo chake kwa muda huo. Hayo ndiyo maisha yangu mapya niliyoyaanza katika kijiji hicho kilichopo karibu na ghuba ya Walvis, nilikaa wiki moja katika ghuba hiyo pasipo kugunduliwa kama ni mzungumzaji wa kiswahili. Wiki ya pili ya kukaa katika ghuba hiyo ndiyo ilikuwa janga jingine kwangu, wiki hiyo nilipokea bahasha nyingine yenye rangi ya kaki ikiwa na ujumbe mzito uliobeba wajibu ambao nilitakiwa kuufanya kwa kuhofia kupoteza ninavyohusudu ndani ya dunia hii. Ujumbe huu ulizidi kunichanganya kwani kazi niliyotakiwa kuifanya ni kazi inayohitaji moyo la si hivyo huwezi kuifanya, matatizo ambayo yangetokea ndiyo yalipelekea niifanye kazi hii rahisi kwa kuitazama ilavni ngumu sana. Karatasi iliyokuwa ndani ya bahasha hii ambayo sikuitambua inatumwa na nani na anayenijua nipo ndani ya nchi hii, mtu anayenitumia karatasi hii alikuwa ananifahamu fika ingawa mimi sikuwa namfahamu. Kuchanganyikiwa ndiyo kulichukua nafasi yake katika kichwa changu, hata nilipomweleza rafiki yangu kipenzi Jonas  naye hakuwa na njia ya kunisaidia. Karatasi yenyewe iliandikwa....

****


Walipofika mwisho wa ukurasa wa pili ili waendelee na ukurasa wa tatu, Hussein aliutoa uzi wa kuzuia kupotea kwa ukurasa ikiwa itaifunga shajara kisha akauweka katika ukurasa huo. Aliifunga shajara kwa nguvu huku akimtazama Hassan.
"Huasein mbona unaifunga diary wakati tumeishia katikati?" Hassan alimuuliza pacha akionesha kutofurahishwa na kitendo hicho.
"muda wa mazoezi huu wewe hujui kama tuna ligi ya chuo tukifungua tu" Hussein alimwambia Hassam huku akichukua shajara.
"dah! Halafu kweli, kwani saa ngapi?" Hassan aliuliza.
"saa kumi kasoro hii tuwahi graundi kama vipi?" Hussein aliongea huku akiiweka shajara kwenye meza,  wote kwa pamoja walichukua vifaa vya mazoezi kisha wakaondoka kuelekea uwanjani. Vijana hawa mpira wa miguu ndiyo ilikuwa burudani yao kuu na waliupenda sana, mapenzi  yao kwenye mpira wa miguu yalijulikana hata kwa baba yao na ndiye aliyewapa moyo wa kuendelea kuonesha kipaji chao kandanda. Mpira wa miguu kwao ilikuwa kama ni mchezo uliwapa umaarufu chuoni kwao na hata mtaa wanapoishi..



*MAPACHA WANAZIDI KUISOMA SHAJARA WALIYOPEWA NA BABA YAO AMBAYO INAZIDI KUWAVUTIA

*UJUMBE WA PILI UNAMFIKIA  ABDULHAFIDH, JE UJUMBE ULIMUAMRISHA AFANYE WAJIBU GANI HUO


ITAENDELEA!!

No comments:

Post a Comment