Saturday, November 28, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA KUMI NA MOJA


 DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE



SEHEMU YA KUMI NA MOJA!!
"haina haja ya kuhuzunika mzee mwenzangu bali inabidi uwalaumu wanao na janga hili mzee mwenzangu limeanzwa na wao na sasa mwenzao wanalimaliza" Mzee Mahmud aliongea kisha akanywa kahawa funda moja bila hata kumtilia maanani Mzee Burhan aliyeonekana kutoielewa kauli hiyo.

"Mzee mwenzangu mimi ni rafiki yako wa muda mrefu sana na kuhusu hili suala jua mwanao mkubwa analielewa fikra, na kama yupo tayari kuliweka bayana utabaki na nguzo tu lakini kama hataki kuliweka bayana hutabaki na nguzo hata moja" Mzee Mahmud alizidi kuongea maneno yaliyomfanya Mzee Buruhan  abaki akimtazama kwani anamtambua fika ni mganga mwenye uwezo mkubwa wa kujua yaliyojificha.
"Sijakuelewa mzee mwenzangu" Mzee Buruhan alisema huku akimtazama Mzee Mahmud kwa umakini, Mzee Mahmud alipotazamwa alitoa tabasamu tu kisha akasema, " zamu yako kucheza mimi nishalala mzee mwenzangu".
Mzee Buruhan aliacha kumtazama akaliangalia bao kisha akachukua kete akaanza kucheza huku akiwa njia panda kutokana na kauli ya Mzee Mahmud ambaye huwa hafafanui akishaeleza mambo kama hayo halafu akabadili mada ghafla.



****


Maneno ya mzee Mahmud bado yalibaki ndani ya kichwa chake ingawa yalikosa ufafanuzi wa kutoka kwa mzee huyo aliyebobea katika uganga, Mzee Buruhan aliendelea kucheza bao huku akiwa na mawazo sana juu ya  maswali ya maneno ya utata aliyoambiwa  na mzee Mahmud. Hadi alipolala katika mchezo huo wa bao bado mawazo lilikuwa juu ya maneno hayo, mzee Mahmud alipoanza tena kucheza bao huku ameinamisha kichwa chake  akitazama kwenye bao kwa umakini hakujua kama mzee mwenzie alikuwa akimtazama sana kichwani mwake na alitamani hata akione ndani hicho kichwa chake ili atambue ni nini anachowaza lakini suala hilo lilishindikana kabisa kwani yaliyomo katika ubongo wa mtu huwezi kuyaona hata ukipasua kichwa chake na kuangalia ndani.
"Kuna kisa cha zamani sana mzee mwenzangu nakikumbuka hadi leo hii katika kichwa changu, hakika wahenga hawakukosea kukitunga kwani ni kisa kinachohusu vijana wawili waliompenda msichana mmoja kigori huko mashariki ya mbali" Mzee Mahmud alianzisha mada nyingine huku akiendelea kucheza bao na safari hii alikuwa anamtazama mzee Buruhan usoni mwake akiwa na tabasamu hafifu.
"Mzee mwenzangu kama kawaida hukaukiwi visa vyenye mafunzo na kuburudisha, hebu nipe habari bwana" Mzee Buruhan alimuambia mzee mwenzie ili apate kusikiliza kisa kutoka kwake kwani mzee Mahmud alikuwa akijulikana kwa jinsi alivyokuwa hodari kwa kusimulia visa na hadithi zenye kufundisha, hakika taaluma ya fasihi simulizi ya wakati wa zamani bado ilikuwa ipo ndani ya halmashauri ya ubongo wake ingawa alionekana kuzeeka sana.
"Katika kijiji kimoja cha jamii ya wastarabu alizaliwa binti mmoja mrembo sana aliyeitwa Giguna katika familia yenye hadhi duni sana katika Jamii ya Watarabu, binti huyo alianza kuwa gumzo kijijini happ tangu akiwa mdogo kutokana na uzuri aliokuwa nao uliokuwa wa ajabu sana. Hadi anavunja ungo  ilikuwa ni habari nyingine katika kijiji hicho kwani vijana wa rika lake walikuwa wakimtamani kila kukicha kutokana na umbo maridadi alilokuwa nalo, haikuwahi kutokea binti mwenye umbo kama lake ambalo lilijaa utata mtupu tena alijaliwa kuwa na kiuno kilichojitenga kama mdudu Mavu. Usoni alikuwa na sura  yenye mvuto wa ajabu sana na jicho lenye umbo la nusu mwezi,  Giguna alikuwa ni binti mrembo haswa na kila alipokuwa akiwatazama wavulana wa rika lake walidhani kuwa wanaitwa lakini haikuwa hivyo bali asili ya jicho lake ndiyo lilimchengua sana kila mvulana. Ilipotimia majira manne ya mwaka katika kijiji hicho walihamia familia ya wasafiri kutoka mbali ambao walipenda sana kuweka makazi katika kijiji hicho na walipewa ukaribisho mkubwa kutoka kwa kiongozi wa kijiji hicho, familia hiyo nayo ilikuwa gumzo kijiji hapo kutokana na kuwa na kijana aliyekuwa na mvuto wa ajabu na usafi uliopitiliza kuliko hata vijana wengine wa kijiji hicho.  Kijana huyo alijulikana kama Mufedi ambaye alikuwa na asili mchanganyiko iliyomfanya awe na nywele za kipekee sana ambazo hata angeishi bila chanuo basi zingeonekana ni nzuri sana na zipo  kama zimechanwa. Mufedi alikuwa ni mtu wa kukaa na vijana wenzie wa rika lake hadi wakamzoea kutokana na ucheshi wake alionao ambao uliwafanya vijana wenzake wafurahi kila kukicha, ndani ya muda mfupu tu katika kijiji hicho tayari Mufedi alikuwa yupo midomoni mwa mabinti wa kijiji hicho kama ilivyo kwa Giguna alivyokuwa yupo katika midomo ya wavulana wa kijiji hicho. Ilifika kipindi hata wasichana wa kijiji hicho wakawa wanakuja nyumbani kwao Mufedi na kumsaidia mama yake Mufedi kazi mbalimbali wakiwa na lengo tu la kuiona sura ya Mufedi jinsi ilivyokuwa ni nzuri na yenye kuvutia, baadhi ya wasichana waliokuja hapo nyumbani kwao Mufedi na kumuona akiwa sehemu kubwa ya kifuani mwake haijastiriwa walikiri kwamba alikuwa ni mvulana mwenye uzuri wa ajabu. Maneno ya chini kwa chini juu ya uzuri wa ajabu alionao kijana huyo yalienea hapo kijijini kama ilivyokuwa akisemwa Giguna na wavulana wa kijiji hicho, muda wote huo si Giguna wala Mufedi aliyewahi kumuona mwenzake kwa macho na kila mmoja alisikia sifa za mwenzake kupitia marafiki zake. Siku moja ambayo ndiyo ilikuwa chanzo cha kuanzishwa kitu ambacho hakikutarajiwa kuanzishwa ndiyo siku ambayo wawili hawa kwa mara ya kwanza walionana, siku hiyo Mufedi alikuwa akiongea na marafiki zake vipenzi walioitwa Nikeze na Nunele. Giguna siku hiyo aliagizwa kupeleka mzigo nyumbani kwao Mufedi baada ya wazazi wake na mufedi kufanya biashara ya kubadilisha mali kwa mali kwani kipindi hicho bado fedha zilikuwa hazijaanza kutumika. Ilikuwa ni muda mrefu Giguna alikuwa hajaonekana kutokana na kuwasaidia sana wazazi wake na bibi yake kazi za hapo nyumbani kwao, eneo alilopita ndiyo walikuwa wamekaa Mufedi, Nikeze na Nunele wakipiga soga na kuchia vicheko. Giguna alipokaribia Nikeze alimuita lakini hakuitikiwa ndipo Nunele alipomuita akasimama kutokana na heshima aliyokuwa nayo, Nunele na Giguna walikuwa ni ndugu wa damu na Nunele ndiyo mkubwa kwa Giguna. Hivyo Giguna alijongea hadi walipo akiwa amejitwisha furushi kichwani  lililokuwa na mzigo aliotumwa kuupeleka, hapo ndipo kwa mara ya kwanza Giguna alimuona Mufedi na Mufedi alimuona Giguna na wakaongea kwa lugha ya macho na nyoyo pasipo wengine kutambua wanachozungumza.
"Giguna u waitwa wanyamaza si vizuri hivyo" Nunele alimuambia Giguna baada ya kunyamazia salamu ya Nikeze.
"Kaka nataka wahi nilipotumwa niweze wahi rejea" Giguna aliongea kwa sauti nyororo huku akimtazama Mufedi kwa jicho la kuibia.
"hapana dada sifanye hivyo muache wslau akusindikize kidogo tu hutachelewa kurudi" Nunele alimuambia kisha akampa ishara Nukeze amfuate Giguna, Nukeze hakufanya ajizi alimfuata Giguna na taratibu akaanza kwenda huku akiongea kwa maneno ambayo hayakusikiwa na yoyote zaidi yao wenyewe. Huo ndiyo mwanzo uliozua safari nyingine kabisa isiyosafiriwa kwa umbali mrefu, ilikuwa kama ukurasa ila haukuwa na karatasi. Siku na siku zilisogea na hatimaye dalili za dhahiri kabisa zikachipuka na kuonesha kila mmoja alikuwa akimuhitaji mwenzake, katika msogezo huo wa  siku ndipo ikafika siku ambayo haitasahaulika kwenye ukurasa mpya wa upendo ulioanza kuchipuka katika mioyo yao"   Mzee Mahmud aliweka kituo hapo katika kusimulia na kumuangalia Mzee Buruhan  ambaye alionekana kuwa na hamu ya kuendelea kuisikiliza hicho kisa anachosimuliwa.
"Aaaah! Mzee mwenzangu wakatisha pasipo stahiki kukatishwa" Mzee Buruhan alimlaumu mzee Mahmud kwa kukatishiwa uhondo mwanana uliokuwa unapita kwenye masikio yake na kujenga taswira kwenye ubongo wake kama vile alikuwa anaangalia sinema ya kile anachosimuliwa na kusikiliza simulizi tu.
"Weka mafuta kwanza tuendelee na safari huoni kikombe kitupu hicho na birika lina mafuta tele ya kunifanya niendelee kutoa burudani" Mzee Mahmud alimuambia mzee Buruhan huku akimpa kikombe chake cha kahawa ili aongezewe kahawa aweze kuendelea kusimulia.
"simulia walau kidogo basi mzee mwenzangu huku nakuongezea kahawa"  Mzee Buruhan alimuambia Mzee Mahmud akiwa amenyanyua birika la kahawa ili amuongezee kahawa.
"Basi bwana siku hiyo si wakaombana namba za simu ili waweze kuongea vizuri maana ya vijana unayajua" Mzee Mahmud aliamua kusimulia kitu kingine kabisa tofauti kabisa na kufanya Mzee Buruhan amtazame kwa mshangao.
"Ushaanza visa vyako tayari mzee mwenzangu, sasa umesema zamani na hizo namba za simu zimeingia vipi" Mzee Buruhan alimuambia Mzee Mahmud huku akianza kucheka.
"Sasa si wewe  unalazimisha gari kwenda wakati mafuta yamekwisha, umeona wapi likatembea  huku likisubiri mafuta" Mzee Mahmud aliongea huku akicheka kidogo na kusababisha Mzee Buruhan acheke kwa nguvu kutokana na vituko vya mzee mwenzake.
"Yaani mzee mwenzangu hubadiliki kabisa tangu upo kijana tabia ni zile zile tu" Mzee Buruhan aliongea huku akimtilia kahawa mwenzake.
"ewaaa! Mambo si hayo sasa twende kazi" Mzee Mahmud aliongea huku kisha akinywa kahawa kidogo.
"sasa endelea mzee mwenzangu usikatishe habari" Mzee Buruhan alimuambia.
"Siku hiyo ilikuwa ni majira ya jioni baads ya jua kuzama, Giguna alicheleewa kuchota maji mtoni na ikambidi akimbie mara moja mtoni ili walau apate maji ya kuoga kwa usiku wa siku hiyo kwani ilikuwa ni kawaida kulala akiwa nadhifu usiku. Alipofika mtoni ndipo akakutana na Mufedi akiwa na kabeba  vazi lake la juu lilionekana kuloa na alibakiwa na shuka kubwa aliyojifunga kiunoni iliyofika juu ya kitovu, kitendo cha wao kuonana tu walibaki wakitazamana tu kwa muda mrefu bila hata kusema chochote. Walikuwa wapo kwenye njia nyembamba iliyochongwa baada ya miguu ya watu kukanyaga nyasi hizo kwa muda mrefu hatimaye baadhi zikakauka na kufanya njia, ilikuwa lazima mmoja ampishe mwenzake kwenye  hiyo njia ili apite kwani haikuwa inatosha kupishana. Kwa ufinyu wa njia hiyo hakuna aliyefanya hivyo wote walisimama tu wakizamana tu hatimaye Mufedi akajikaza akamshika Giguna bega, walisogeleana karibu zaidi  na muda huo hakuna yoyote aliyetambua nini wanafanya kwani walijikuta wamefikwa na hisia za ajabu kila mmoja kutokana upendo walionao kwa mwenzake. Ule usemi aliousema nabii wa Mungu kwamba kwenye watu wawili wa jinsia tofauti basi watatu wao atakuwa ni ibilisi ndiyo ulijidhihirisha hapo na wakajikuta wameingia sehemu isiyotakiwa kuingilika, tangu siku hiyo ndiyo ukurasa haswa wa mapenzi ya dhati baina yao ukafunguliwa  na mapenzi ya siri  baina yao yakawa yanaendelea. Katika kipindi hicho ndipo Mufedi alipokuja kubaini kwamba Nukeze alikuwa akimtaka Giguna kwa muda mrefu lakini hakukubaliwa kabisa ndiyo maana hata siku ile alipomuita hakuitika kutokana na kuchoka  usumbufu wake, mapenzi baina yao yaliendeshwa kwa usiri mkubwa na hawakumueleza yoyote hadi pale siku moja mmoja wa watu hapo kijijini alipokuja kubaini uhusiano huo. Ginota rafiki kipenzi wa Giguna ndiye mtu aliyekuja kufahamu uhusiano huo baada ya kuwakuta wakitoka kuvuja ile amri sijui ya ngapi  ya imani ya wenzetu hao, siku hiyo ilibidi Giguna amuambie ukweli juu ya uhusiano wao na akamuapiza kumtunzia hiyo siri pasipo kujua anamuaminisha nyoka. Giguna jambo ambalo hakuwa analijua ni kwamba Ginota ni mmoja kati ya wasichana  waliokuwa wamezama kabisa katika kumpenda Mufesi lakini hakuwahi kumuambia Giguna kwasababu ana mahusiano na Nunele na laiti angemwambia ungekuwa ugomvi kati yao kwani Giguna asingekuwa tayari kuona kaka yake Nunele anasalitiwa. Pia katika jambo ambalo Giguna hakulitambua ni kwamba Nukeze alikuwa akimtumia sana Ginota katika kumshawishi  Giguna amkubali lakini jitihada hizo ziligonga mwamba kwani macho ya Giguna hayukutamani hivyo moyo wake haukuhitaji, kumbuka macho yasipotamani moyo hauwezi kuhitaji. Ginota hakuweza kustahimili kuona rafiki yake kampata mwanaume aliyekuwa anagombewa hapo kijijini na wasichana wote kama vile ni lulu yenye thamani, Ginota aliifikisha habari hiyo kwa mpenzi wake Nunele na kupelekea taarifa hiyo ifike kwa Nukeze. Hapo ndipo vita mpya ya mapenzi ilipoanza chini kwa chini, Nunele na Nukele walikuwa wanacheka na Mufedi kwa jino pembe tu lakini walikuwa wakipanga kumuua Mufedi kila muda lakini ilishindikana na kila walipoenda kwa waganga  ili wamuue kazi yao ilikataliwa na mwisho wake wakafanya kitu ambacho kilimuumiza sana Mufedi na ikawa ndiyo mwisho wa mapenzi ya Giguna na Mufedi. Waliamua kwenda kwa mganga wakafanya dawa ili ambayo walimtilia Giguna kwenye maji ambayo alikuwa anakunywa na alipoyanywa ndiyo ikawa mwanzo wa Giguna kumpenda Nukeze na Mufedi kukosa penzi lake baada ya kukataliwa wazi na kutolewa maneno yasiyofaa na Giguna. Mufedi alidhani utani lakini alikuja kujua ni kweli baada ya kutaka penzi mtoni wakati Giguna alipoenda kuchota maji, Giguna alipiga kelele ya kuwa anavakwa na kusababisha watu wajae na Mufedi aliambulia kipigo nusura afe. Tangu siku hiyo Mufedi hakumgusa tena  Giguna na alipopona tu aliondoka kijijini hapo akiiacha familia yake baada ya wanakijiji kutomuhitaji, huo ndiyo mwisho wa kwanza wa simulizi hii na muendelezo utaujua mzee mwenzangu tuombeane uzima tu" Mzee Maud aliishia hapo kuelezea simulizi hiyo.
"Mzee mwenzangu unajua ninamuonea huruma sana huyo kijana yaani naona kama nimefanyiwa mimi hivyo" Mzee Buruhan aliongea baada ya kuisikiliza hiyo simulizi kwa umakini.
"Fahari yetu waswahili kujaliwa sanaa inayokuteka akili zako ukaona kama tukio ni la kweli" Mzee Mahmud aliongea huku akimalizia kikombe cha kahawa.
"Yaani hata bao nimesahau kulicheza" Mzee Buruhan aliongea huku akitabasamu.
"Mzee mwenzangu huku leo silali naondoka maana narudi Mkinga leo leo nimekuja kukupa pole tu ujue sijakutupa rafiki yako wa toka utotoni" Mzee Mahmud alisema huku akinyanyuka kivivu.
"Haya mzee mwenzangu ngoja nikuitie kijana akutoe na usafiri hadi Makorora ukapate gari ya  kurudi nyumbani" Mzee Buruhan alimuambia mzee  Mahmud.
"Hasbuk mzee mwenzangu shukran sana muache kijana apumzike mimi nitatumia sehewa  hapo tu niende chapuchapu haina haja ya gari" Mzee Mahmud aliongea huku akitembea na Mzee Buruhan akawa anamsindikiza, walitoka hadi nje ya nyumba  eneo linaloegeshwa baiskeli nyingi za kukodisha. Mzee Mahmud alikodi moja na dereva wake akamuaga Mzee Buruhan akaondoka.


****



Majira ya jioni kwa huku duniani upande mwingine wa himaya isiyokuwepo juu ya ardhi ya wanadami tayari kikao kilikuwa kimeshawekwa ndani ya chumba maalum cha mkutano, ilikuwa ni ndani ya himaya ya Majichungu katika ya bahari ambapo ndiyo makazi ya majini wasiyohusika na utumikishwaji katika nguvu za giza. Ndani ya chumba hiki cha mkutano walikutana viongozi mbalimbali wa himaya hiyo baada ya mkutano wa dharura kufanywa ghafla kutokana na hali inayokuja mwezi  mmoja baadaye iliyoonwa na jicho la Salmin ambaye naye alikuwa ni mmoja kati ya waliohudhuria mkutano huo akiwa pamoja na baba yake mzazi. Hali iliyokuwa inatarajia kuingia hapo mwezi mmoja baadaye ilikuwa ni hali ya kutishia usalama wa viumbe wote waliokuwa majini kwa asili zote kasoro wale wa mchanganyiko ndiyo pekee wangeweza kusalimika na mkasa huo na si vinginevyo, ilikuwa ni lazima hali hiyo idhibitiwe haraka iwezekanavyo lasi hivyo himaya hiyo itakumbwa na  na balaa kubwa sana.
"Jamani hali ni tete katika himaya yetu na tusipofanyia ufumbuzi suala hili basi tujue himaya yetu itakubwa na balaa kubwa, hebu tumsikilize Salmin atuambie ni nini alichokiona katika maono yake ya kuona mambo yajayo" Zalabain alifungua mkutano huo kwa maelezo hayo.
"Asante sana kiongozi wetu na mfalme mtarajiwa wa himaya  hii kwa kunipa nafasi hii, hali halisi inayokaribia kutufikia ni ujio wa wadudu kutoka himaya ya giza baada ya wao kubaini  kuna ukosefu wa giza kwa muda mrefu katika himaya hii baada ya kufariki  kwa mtukufu mfalme. Viongozi wa himaya ile ambao ni maadui wakubwa wa himaya hii wameona ndiyo njia pekee ya kuidunisha himaya yetu kwa kutuma wadudu watakaoachia vimelea ambavyo vikimpata jini yoyote ambaye hana damu ya binadamu yaani ambaye hajachanganyika au hajatokana na uzao wa binadamu na jini itakuwa ndiyo mwisho wa maisha baada ya vimelea hivyo kumtesa kwa muda mfupi tena kwa maumivu. Balaa hili  namaanisha tutakaopona ni mimi na mfalme mtarajiwa tu ikiwa halitozuiwa ila kama likizuiwa ni himaya nzima itasalimika, hivyo mchango wenu ndiyo unahitajika katika kusaidia kulitatua hili janga" Salmin alitoa maelezo yake.
"wote tumemsikia Salmin mwenye nguvu kuliko sisi sote akitueleza juu ya kinachokuja kutokea ikiwa tu hatutalichukulia hatua hili suala. Sasa basi nimewaita hapa ili tujadiliane kwa pamoja kama ilivyo kawaida yakitokea matatizo kama haya huwa lazima viongozi wa himaya hii wahusishwe, nitasikiliza maoni yenu kila mmoja kuhusu hili suala" Zalabain aliongea, halafu akawatazama wote waliomo humo ndani mmoja baada ya mmoja na macho yake yalitua kwa mkuu wa majeshi wa himaya ambaye macho yake yaliwaka kama taa kuashiria ana jambo anataka kulisema.
"Ndiyo Jenerali" Zalabain alimuambia mkuu huyo wa majeshi wa himaya hiyo huku akimuashiria asimame, mkuu wa majeshi alisimama kisha akatoa heshima kwa Zalabain na wengine  waliopo hapo ndani kisha akasema, "Kiongozi wetu mkuu na viongozi wengine napendekeza  tuwawahi hao wanamajini wa himaya ya giza kabla hata hawajawaachia hao wadudu kuja huku, najua wadudu wote wanaotaka kuwaachia bado watakuwa wanawaunda kwani wangekuwa tayari wangeachiwa muda wowote. Hivyo mimi napendekeza tutume jeshi liende kwa siri likaharibu huo utengenezaji wa hao wadudu itakuwa tumeiokoa himaya nzima kuliko njia nyingine yoyote".
Mkuu wa majeshi alipomaliza kutoa kauli hiyo alikaa chini na  viongozi kadhaa wakanyoosha mkono kuashiria wamekubaliana na hilo wazo la mkuu wa majeshi, upande wa mawaziri wa himaya hiyo mmojawapo macho yake yaliwaka kuashiria anataka kuongea.
"Ndiyo  waziri tunakusikiliza" Zalabain alimuambia waziri huyo ambaye alisimama akatoa heshima zote halafu akasema, "Kiongozi wetu mtukufu nimekaa katika himaya hii  kwa muda wa  miaka 4000  hadi inatimu siku hii ya leo ninapopokea taarifa hii, katika miaka hiyo yote  nimeshuhudia balaa kama hili liliwahi kutaka kutokea kwa kutengenezwa viumbe wenye sumu na himaya hiyo hiyo ya nguvu za giza lakini kwa masaada wa Dainun ya kale ambayo muda wake uliishia siku ile alipotawafu babu yako. Hivyo basi kinga mpya ya balaa hili ni kupatikana kwa dainun mpya ambayo ilikuwa ipo mikononi mwa hayati baba yako ndiyo itasaidia kuzuia haya mabalaa milele mpaka utakapoiacha dunia hii"
"Asante kwa maoni yako waziri, mzee Zultash ongea" Zalabain aliongea kisha akamruhusu baba yake Salmin aongee baada ya macho yake kuwaka. Mzee Zultash alisimama akatoa salamu kwa wote waliomo humo ndani pamoja na kuonesha heshima kwa viongozi wakubwa.
"Asante  kiongozi wetu, mimi hapa
naungana na wazo alilolitoa mkuu wa majeshi la kwenda kuharibu utengenezwaji wa hao wadudu kwani sote tunatambua kwamba Dainun mpya imeibiwa na mpaka ije kupatikana hatujui itatuchukua muda gani kwani hao viumbe wataingia ndani ya himaya hii mwezi ujao. Kumbukeni mwezi kwetu tunauona kama juma moja analoliona mwanadamu wa kawaida, sasa hamuoni hapo tutakuwa tumechelewa  na maafa yatakuwa yameshatufikia jamani" Mzee Zultash aliongea na viongozi wote wakamuunga mkono  hata yule waziri aliyetoa hoja ya kutafutwa Dainun naye alimuunga mkono.
"Kama ilivyo sheria yetu inavyosema, hoja ikiungwa mkono zaidi imepita. Basi jeshi la makomandoo litumwe kwenda kuharibu utengenezaji wa wadudu hao huku nikiwa naisaka Dainun kwani mwenye kuimiliki kashajulikana" Zalabain aliongea.


*Kumekucha ujinini


No comments:

Post a Comment