Wednesday, November 25, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA NANE







"We! We! We! Tena komaeh! Usiniite mkeo mimi, nafikiri nilioana na wewe kwasababu uliniloga lakini sikuridhia hivyo mimi siyo mkeo" Bi Farida aliongea kisha akamsindikiza na singi  Shafii hadi akadondoka.
"Tena umuombe msamaha huyo hapo na siyo sisi" Mzee Buruhan aliongea huku akioneaha kidole kwenye mlango mkubwa wa kuingia ndani ya nyumba hiyo mbovu ya kizamani, Mtu mwenye joho jeusi alionekana akiingia akjwa ameahika sururu lenye mpini mweupe. Mtu huyo alipomkaribia Shafii, Mzee Buruhan, Bi Farida na Zaina walitoka nje wakimuacha Shafii na huyo mti aliyeingia.
"We shetani unakufa" Yule mtu alimuambia Shafii halaf akampiga sururu la kichwa kwa nguvu.
"Aaaaaaaaaaaargh!" Shafii aliachia ukelele wa maumivu lakini alipoangaza macho yake alijikuta yupo sehemu yenye kitanda cheupe na shuka jeupe, alipoona mazingira hayo alizidi kupiga kelele kwa nguvu akidhani labda yupo kuzimu.
"jamani atajitoa dripu yule, muwahini na sindano ya usingizi kabla hajajitonesha  na ile shingo yake iliyovunjika" Ilisikika sauti ya kike ikitokea kushoto kwake.

****

Ilikuwa ni sauti ya muuguzi wa kike baada ya kuona dalili za purukushani anayotaka kuileta Shafii baada ya kuzinduka kutokana na ndoto mbaya aliyokuwa anaiota, mandhari ya eneo alilokuwepo ndiyo ilizidi kumchanganya kabisa akajiona ndiyo kama anaandaliwa kwa ajili ya kupigwa sururu na yule mtu aliyemuota ndotoni. Wauguzi waliokuwa wapo ndani ya wodi aliyolazwa walimuwahi kwa sindano ya usingizi ili asije kusababisha madhara mengine zaidi kwa mwili wake. Hadi muda huo tayari mwili wake ulishapata madhara mengi kutokana na ajali ya gari na laiti kama angecheleweshwa basi ingekuwa ni mengine, Shafii tayari alikuwa kashavunjika shingo.na kiuno katika ajali ya gari aliyoipata kutokana na kuchanganyikiwa baada ya sauti kusikika akilini mwake ikimwambia mwanae kipenzi tayari yupo ndani ya mikono ya mtu asiyemjua tena mwenye nia mbaya na yeye.

****

     RASKAZONE
          TANGA

   Siku iliyofuata katika jiji la Tanga ilikuwa ni siku nyingine iliyobeba tukio la ajabu jingine ambalo lilistahiki kuingia katika matukio ya ajabu yaliyowahi kutokea nchini Tanzania, ilikuwa ni siku ya pili imepita baada ya  kutokea tukio la kuungua zile nyumba za kampuni Hamid kule Duga maforoni. Majira ya saa nne asubuhi wafanyakazi wa kampuni ya mafuta ya Matro ambao hawakumalizia kazi zao kutokana na tukio lililotokea hapo ofisini kwao la kuuawa kwa mmiliki wa kampuni hiyo walihitajika kufika mapema kumalizia viporo vya kazi yao ili waweze kwenda mapumzikoni kutokana na kifo cha mmiliki wa kampuni hiyo, ilipotimu saa tano asubuhi wafanyakazi wote walikuwa kwenye ukumbi wa mkutano wakimsikiliza msemaji wa kampuni hiyo baada ya kumaliza viporo vya kazi vilivyosalia siku iliyopita.
"Natumai wote ni wazima wa afya na mpo hapa kusikiliza jambo nililowaitia, kikubwa kilichonifanya niwaite hapa ni juu ya kutokea kwa msiba wa bosi wetu kipenzi na wote mnalitambua hili. Sasa basi kwa taarifa zilizonifikia ni kwamba kumetokea vifo viwili ndani ya siku moja ambacho kimoja ni cha bosi wetu kipenzi na kingine ni cha kaka yake mmiliki wa kampuni ya Extoplus nadhani wote mnamfahamu. Hivyo misiba hii yote miwili itafanyika nyumbani kwa baba yao mzazi mzee Buruhan maeneo ya Sahare jijini hapahapa, ikiwa sisi ni miongoni mwa wafanyakazi wake tuliyempenda inabidi wote twende tukamfariji mjane wa marehemu pamoja na familia nzima ya mzee Buruhan. Hakika sisi ni wa....." Msemaji mkuu wa kampuni ya Matro alitoa maelezo kwa wafanyakazi wa kampuni aliyoyapata ambayo hayakuwa yamefika kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo, alipokuwa anataka kuhitisha maelezo hayo alisikia mlango mmojawapo wa chumba cha mkutano ambao hautumiki ukifunguliwa kwa nguvu na ikaonekana aliyefungua ni mtu mwenye ubavu mkubwa kwa jinsi ulivyotoa kishindo hadi kitasa chake kikaanguka papo hapo. Macho ya kila mmoja aliyepo eneo hilo yalielekea kwenye mlango huo na hapo ndipo wakapigwa na butwa baada ya kumuona mtoto mdogo wa kike mwenye takribani miaka sita akiingia huku kabeba mdoli mdogo mwenye umbo la dubu mweupe, macho ya baadhi ya wafanyakazi yalionesha kumtambua huyo mtoto ila baadhi hawakumtambua hata kidogo. Mtoto huyo wa kike mzuri alizidi kumfanya Msemaji mkuu wa kampuni hiyo apagawe zaidi, mtoto huyo alipiga hatua hadi alipo Msemaji mkuu wa kampuni hiyo kisha akamuangalia usoni huku akitabasamu.
"Annet mwanangu umekuja na nani?" Msemaji mkuu alijikuta akiuliza huku akiwa ameduwaa na hata wengine waliduwa kwa jinsi mlango aliopitia huyo mtoto ulipotoa kishindo kizito sana hadi kitasa chake kikaanguka.
"nimekuja mwenyewe baba" Mtoto huyo anayeitwa Annet alijibu kwa lafudhi ya kitoto ambayo ilisikika na kila mmoja humo katika chumba cha mkutano.
Msemaji wa kampuni aliposikia hilo jibu la mtoto wake alichuchumaa chini akamshika mashavu huku akitabasamu kwa ishara ya upendo wote anaotakiwa kuuonesha baba kwa mtoto wake kisha akamuuliza, "ni nani aliyeufungua mlango kwa nguvu hadi kitasa kikaharibika?"
"Mimi hapa nimeugusa tu kwa mkono mmoja nikausukuma ukafunguka" Annet alijibu na akazidi kuwashangaza watu waliomo humo ndani hadi Msemaji mkuu wa kampuni naye akazidi kushangaa majibu anayoyatoa binti yake huyo mdogo.
"Samahani kwa kuwavamia mkutano wenu na kuwakatisha, nimetumwa tu kuwaeleza ujumbe niliopewa ambao unawahusu nyinyi na ujumbe hamtakaa kuusambaza wala kusimulia kwa wengine kwani mlipewa nafasi  mkaichezea. Ni hivi siku iliyopita baada ya kufa kwa bosi wenu nyinyi mlipoondoka hapa kwenye kampuni hii ilikuwa ndiyo salama yenu ila kwakuwa mmerudi, nimeambiwa niwaambie kuwa hili ndiyo kaburi lenu" Annet aliongea kwa sauti nzito tofauti na ile ya kitoto aliyokuwa anaongea tena akatoa maneno yaliyozidi kuwachanganya.
"We Annet unasemaj..?" Msemaji wa kampuni hiyo alishindwa kumalizia kauli yake baada ya Annet kupotea katika mazingira yasiyo ya kawaida, jengo zima lilianza kutingishika kama limekumbwa na tetemeko la ardhi vioo vya madirisha vikaanza kuvunjika na kuzidi kuwatia wafanyakazi wote hofu. Wafanyakazi walipojaribu kukimbilia mlangoni ili watoke  walikuta milango ikiwa imejifunga, mtetemeko wa jengo hili ulizidi kuwatia hofu  na wakajikuta wakitaja jina la muumba kwa mara ya kwanza baada ya kutaja majina ya mama zao kwa  muda mrefu.

****
  

    LAS VEGAS
    MAREKANI

 Wakati wafanyakazi wa kampuni ya Matro wakikumbana na janga lililotokea hapo kwenye makao makuu ya kampuni hiyo, upande mwingine wa  bara la Amerika ya kaskazini katika mji wa Las Vegas nchini Marekani majira ya saa nne usiku kwa masaa ya huko ambapo yapo masaa kumi nyuma ya Tanzania. Kijana mwenye mavazi ya anasa zaidi alionekana akiingia ndani ya klabu maarufu ya usiku ya jijini humo, Falzal ndiyo jina lake huyu kijana mwenye kila aina ya majigambo na mwenye jeuri ya kuchezea pesa katika starehe. Ingawa bado ni kijana msomi na aliyekuja nchini humo kwa ajili ya masomo, aliishi mithili ya mtu maarufu wa jijini humo.
Alipoingia ndani ya klabu hiyo ilikuwa kama kawaida yake lazima aende kwenye meza ya wacheza kamari kama kawaida, hiyo ndiyo ilikuwa starehe yake nyingine ambayo ilimuingizia pesa nyingi na kumfanya aishi maisha ya kifahari sana jijini humo. Aliwasalimu watu anaocheza naoo kamari kila siku akiwemo Miliver mcheza kamari maarufu hapo La vegas kisha akaketi, alimuangalia Miliver akatabasamu kisha akasema, " naona leo umekuja kunikuzia mtaji kama kawaida yako"
"Ha! Ha! Ha!  Leo unaliwa wewe ngoja utaona tu"Miliver aliongea huku akicheka.
    Faiz alipotaka kuchukua kete alishtushwa na mlio wa simu kutoka kwenye suruali yake na ikamlazimu awaombe radhi wachezaji kamari wenzake halafu akasogea pembeni sehemu isiyo na sauti nyingi na akaipokea simu.
"Baba vipi mbona usiku hivi?" Falzal aliongea baada tu ya kumsalima aliyekuwa anaongea naye kwenye simu.
"kuna tatizo gani baba mpaka nirudi nyumbani si uniambie tu nielewe hapahapa"Falzal alizidi kulalamika akiona anaharibiwa starehe zake.
"Sawa baba nakuja kesho asubuhi" Falzal alikata simu kisha akionekana ni mwenye uso wa masononeko kisha akaondoka humo kwenye klabu ya usiku pasipo kumsemesha yeyote na uso wake ulikuwa unalengwa machozi, aliingia ndani ya gari na akaondoka hapo akionekana ni mwenye kuchanganyikiwa sana baada ya kupokea simu kutoka kwa baba yake.

****

   RASKAZONE
        TANGA


Wakati Faizal akiondoka kwenye klabu ya usiku majira ya saa nne usiku kwa saa za Marekani, huku Tanzania majira kama hayo ya saa nne ila asubuhi kuna kitu kingine kabisa kigeni ndani ya nchi hii kilikuwa kinaanza kutokea. Tukio la aina yake ndiyo lilianza kuonekana kwa watu waliopo karibu na jengo lenye ofisi za makao makuu ya kampuni ya mafuta ya Matro, jengo hilo lilianza kutetemeka na taratibu likaanza kuporomoka kuelekea chini likivunjika vioo  pamoja na kuta zake zikiporomoka. Lilikuwa ni tukio la kustajaabisha sana kwani eneo la chini ya ardhi lenye msingi wa jengo hilo lilipasuka kisha likafunguka na jengo zima likaingia chini ya ardhi huku eneo zima linalomilikiwa na kampuni ya Matro likiwa lunatetemeka kama kuna tetemeko la ardhi, tetemeko hilo lilipokuja kutulia eneo lenye msingi wa jengo la Matro lilibaki kama urefu wa kaburi lililojengewa. Jambo la namna hiyo halikuwahi kutokea nchini Tanzania ingawa huwa inakumbwa na matukio makubwa, tetemeko la ardhi lililoikumba eneo lenye ukubwa wa ekari moja ambalo ndani yake ndiyo zilipo ofisi kuu za kampuni ya Matro halijawahi kutokea hata katika nchi nyingine ndani ya dunia hii.
Baada ya muda mfupi kikosi cha uokoaji kilikuwa kimeshafika katika eneo hilo ambapo walibaki wakishangaa tu kwani hawakuwa na kifaa chenye uwezo wa kuchimba chini lilipodidimia ghorofa hilo wakati linavunjika, kikosi hicho kilichokuja kwa ajili ya uokoaji na chenye ari ya kufanya uokoaji kilijikuta kikishindwa kufanya uokoaji kutokana na ugumu walioukuta eneo hilo lililohitajika kufanyiwa uokoaji.
Wakiwa wamesimama hapo mlio wa mkoromo wa simu ys upepo ya kiongozi wao ilisikika na ikamlazimu kiongozi huyo atoe simu hiyo ya upepo na kuiweka mdomoni kisha akazungumza  kwa kutaja eneo alipo halafu akajitambulisha, sauti yenye kukoroma ilisikika ikiongea ambapo ilisikika vyema kwa kiongozi ambaye alibaki  akiwa amepigwa  na butwa halafu akawaangalia wenzake huku akihema kwa kasi.
"Jamani sheli zote za Matro zinaungua sasa inahitajika timu kubwa ya msaada ya kusaidia uokoaji, sasa hatuwezi kukaa hapa mpaka mashine ya uokoaji kutoka Dar es salaam iletwe. Team twendeni tukasaidiane na wenzetu  kwenye uwezekano wa kutoa msaada na sio kubaki" Kiongozi huyo aliongea kisha akaanza kukimbia yalipo magari yao na wenzake wakawa wanafuata nyuma, magari ya kikosi cha uokoaji yaliondoka eneo hilo la Raskazone kwa kasi yakiacha mamia ya raia kutojua sababu ya wao kuondoka eneo hilo

****


            SURA YA TANO


         Siku iliyofuata nyumbani kwa Mzee Buruhan tayari turubai kubwa lilikuwa limeshafungwa katika eneo la wazi la nyumba hiyo pamoja na maeneo jirani na eneo hilo, hadi muda huo tayari watu walishajaa nyumbani hapo kutokana na umaarufu wa watoto wa mzee Buruhan waliofariki katika vifo vya kutatanisha. Upande wa kinamama kulisikika vilio  kutoka kwa watu wa karibu ambao walikuwa na uchungu wq kuondokewa watu hao, ilikuwa ni siku ya kuhuzunisha kwa familia nzima ya Mzee Buruhan kutokana simanzi iliyowakumba.
Watoto wa mzee Buruhan waliosalia ambao ni ,Ally,Hassan na Falzal tayari walikuwa wapo msibani wakiwa na huzuni sana huku kaka yao mkubwa Shafii akiwa yupo hospitali kutokana na ajali aliyopata. Taratibu zote za mazishi ziliendelea kama zilivyopangwa na baada ya adhuhuri  ndugu wawili wa damu walizikwa kwa wakati mmoja, baada ya mazishi watu walitawanyika na kuwaacha watu wa karibu wa marehemu wakiwa hapo msibani kuendelea na taratibu zingine zilizokuwa zimewekwa hapo awali katika ratiba ya msiba huo uliowagusa wengi kutokana na vifo vilivyowapata ndugu hao wawili wa damu.

****


HIMAYA YA MAJINI YA MAJI CHUNGU


   Wakati mazishi ya Hamid na Hussein yakiwa yanaendelea yalikuwa yakishuhudiwa kwenye kioo kikubwa mithili ya sinema kilichopo katika chumba maalum ndani ya kasri la himaya ya Majichungu, Zalabain na Salmin walikuwa wakishuhudia kila kitu hadi maziko yanakamilika, baada ya kumaliza kuangalia tukio hilo waliangalia pia tukio la kuanguka kwa ghorofa la kampuni ya Matro na kuungua kwa sheli zote za kampuni hiyo.
"kazi nzuri ewe mjukuu wa mfalme  nadhani bado magugu makuu manne ili kazi yetu ikamilike na hakikisha kila mmoja anaondolewa kwenye ardhi waliyokufanyia ubaya yaani Tanga na ukimmaliza yeyote nje ya Tanga utakuwa umefanya kazi bure tu" Salmin aliongea
"Nashukuru kwa kunifahamisha ewe jini mwenye nguvu uliyezaliwa milenia moja na robo tatu iliyopita, naishukuru sana nafsi yangu iliyonizuia kumuua yule mmoja wao anayesoma Marekani. Usiku kwa masaa ya Marekani tayari nilikuwa nimeshafika kwenye eneo maarufu analochezea kamari yule binadamu kwa lengo moja tu la kummaliza. Nilitumia njia ya kujigeuza Miliver ambaye ni mchezaji kamari maarufu jijini Las Vegas ambaye nilimlaza usingizi ili asije kucheza kamari siku hiyo. Nilikuwa na kila njia ya kumuangamiza lakini nafsi ilinizuia kufanya hivyo na mimi nikaacha, nafikiri nisingeisikiliza nafsi ningekuwa nimejipa hasara" Zalabain aliongea
"ungejipa hasara haswa kwani ufalme ungeupata kwa njia ya kafara ya ndugu yako wa damu kama ungefanya uzembe huo" Salmin alisisitiza kisha akaendelea kusema, "hakikisha yule binadamu harudi tena Marekani yaani kwa lugha rahisi ni kwamba anahitajika awafuate ndugu zake"
"Hilo ondoa shaka nitalifanyia kazi haraka iwezekanavyo na inabi......." Zalabain alimuambia Salmin na alipotaka kuendelea kuongea Salmin alimzuia huku macho yake yakibadilika rangi na kuwa mekundu yaliyokuwa yanawaka kisha yakarudi  katika hali ya kawaida.
"vizuizi vya kuingia vya kuingia kwenye himaya hii vinavyozuia tusivamiwe vipo wazi" Salmin aliongea huku akisimama kwa haraka.
"Ndiyo ni kweli vimefunguliwa maana kuna mfalme wa himaya ya jirani ana ziara hapa kwenye himaya yetu" Zalabain aliongea
"Ni mtego huo hao ni watu wa jamii ya kishetani ya KAKIN  wametuma majini yao kulipa kisasi, wale wabaya wako mmoja wao ni mwanachama wa jamii hiyo na hao majini wameshaingia inabidi tuwazuia kabla hawajaleta madhara sasa hivi" Salmin aliongea kisha akapotea hapohapo na Zalabain naye akapotea akatokea nje ya Kasri akamkuta Salmin akiangalia juu ya anga la himaya yao ambalo limebadilika rangi kutoka ile rangi nyekundu hadi nyeusi isiyopendeza kiasi cha kuleta giza.
"tangu Dainun iibiwe hatujawahi kupata giza sasa jiulize giza hili linatokana na nini kama sio kuvamiwa huku, agiza askari wa baragumu apulize baragumu la hatari ili raia wote waingie majumbani mwao na hii vita ni yetu wasihusike" Salmin aliongea huku akimtazama Zalabain  ambaye alipiga kofi moja akatokea kiumbe wa ajabu mbele yake.
"Ndiyo mtukufu mfalme mtarajiwa" Yule kiumbe aliongea kwa utiifu.
"puliza baragumu la hatari haraka iwezekanavyo raia wote waingie majumbani mwao" Zalabain alitoaamri kwa kiumbe huyo, kiumbe huyo aliitikia kwa ishara kisha akapotea papo hapo na baragumu la hatari muda huo huo likaanza kulia.
Salmin na Zalabain walipaa juu huku macho yao yakiwaka kama nuru ya nyota angani, walipofika juu walitanua midomo yao wakapuliza na ukatoka upepo mzito sana ambao uliliondoa giza lote kama unavyoondoka ukungu na mwanga ukarudi. Mbele yao walikuwa wakitazamana na viumbe wenye sura za ajabu tena wenye rangi nyeusi, miili ya viumbe hao haikuwa ikieleweka ilivyo ilikuwa na umbile kama tambara bovu jeusi. Viumbe hao walikuwa wamebeba silaha za aina mbalimbali za kijini wakiwa na hasira za dhahiri, viumbe hao wakihema walikuwa wanatoa moto mdomoni kwa jinsi hasira zilivyokuwa zimewazidi.
"Jisalimisheni kwa usalama wa jamii yenu yote hii" Mmoja wa wale viumbe aliongea.
"Ondokeni kwa amani kwa usalama wenu na si mpaka tutumie nguvu" Salmin aliongea kwa upole sana
"Naona jeuri sasa ngoja tuanze na wewe" Yule kiumbe alisema kisha akamnyooshea silaha yake Salmin iliamuangamize lakini alijikuta anaangamia yeye baada ya shoti kali zilizotoka kwenye macho ya Salmin kutua mwili mwake.
 Wenzake waliosalia walijiandaa kuwashambulia Salmin na Zalabain lakini walichelewa kwani walijikuta wakizungushwa na upepo wa ghafla uliotengenezwa na Zalabain ambao uliwafunga kama wamefungwa na kamba ngumu kisha waliangamizwa wote kwa pamoja kwa kuunguzwa na moto uliotoka mdomoni kwa Salmin uliowaunguza wote wakawa majivu.
"Habari yao imekwisha funga kizuizi" Salmin aliongea kisha akashuka chini taratibu na Zalabain akaenda juu zaidi akanyoosha mkono mmoja uliotoa mwanga wa ajabu ulioelekea juu halafu akashuka chini taratibu baada ya kumaliza kazi yake.            
"hakuna atakayeweza kuivamia himaya ya majichungu nikiwa mimi nipo na himaya hii itadumu mpaka mwisho" Salmin aliongea kumuambia Zalabain kisha akainama chini kiutiifu  akapotea mbele ya macho ya Zalabain.
Baragumu la kuashiria hakuna hatari tena katika himaya hiyo lilipulizwa na raia wa himaya hiyo wakatoka majumbani mwao kuendelea na shughuli nyingine za kawaida na Zalabain akarudi ndani ya Kasri la ufalme.

****

 Wakati majini waliotumwa kuleta maafa wanauawa upande mwingine kwenye chumba chenye watu waliovalia majoho meusi ambacho kilionekana kwa muonekano kilikuwa kipi chini ya ardhi. Kilikuwa kimetawaliwa na jazba miongoni mwa watu waliomo humo ndani, kiongozi wa watu ndiyo alionekana kuwa na jazba za wazi hadi akavua kofia ya joho lake akasema kwa hasira, "Haiwezekani! Haiwezekani! Hussein wamuue na majini yetu wayaue, lazima! Lazima! Tulipe kisasi kwa ajili ya Hussein mwanachama wetu".
Sauti ya kiongozi huyo ilisikika kwa nguvu na kusababisha tetemeko zito litokee kwa sekunde kadhaa na lilipotulia ilisikika sauti ikisema, "Dalipso Londo usiingie kwenye vita isiyokuhusu hata kidogo, Hussein alikuwa ana janga lake tofauti alilolichuma kabla hajaungana nanyi,nimetumwa na mkuu wa wakuu nikuonye ukae mbali na tukio hilo na uhakikishe unamtia nguvuni Qwanta Alfred Lumaki aliyetutia hasara".
Wote walikuwa wameinama kiutiufu na waliinua vichwa vyao baada ya sauti hiyo kuacha kuzungumza.
"ndiyo mkuu" Dalipsol Londo alitii.


*mambo yamezua jambo



No comments:

Post a Comment