Thursday, November 26, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA TISA

 DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE


SEHEMU YA TISA!!
Kilikuwa kimetawaliwa na jazba miongoni mwa watu waliomo humo ndani, kiongozi wa watu
ndiyo alionekana kuwa na jazba za wazi hadi akavua kofia ya joho lake akasema kwa hasira, "Haiwezekani! Haiwezekani! Hussein wamuue na majini yetu wayaue, lazima! Lazima! Tulipe kisasi kwa ajili ya Hussein mwanachama wetu".
Sauti ya kiongozi huyo ilisikika kwa nguvu na kusababisha tetemeko zito litokee kwa sekunde kadhaa na lilipotulia ilisikika sauti ikisema, "Dalipso Londo usiingie kwenye vita isiyokuhusu hata kidogo, Hussein alikuwa ana janga lake tofauti alilolichuma kabla hajaungana nanyi,nimetumwa na mkuu wa wakuu nikuonye ukae mbali na tukio hilo na uhakikishe unamtia nguvuni Qwanta Alfred Lumaki aliyetutia hasara".
Wote walikuwa wameinama kiutiufu na waliinua vichwa vyao baada ya sauti hiyo kuacha kuzungumza.
"ndiyo mkuu" Dalipsol Londo alitii.


****

"kazi ianze sasa hivi ili dunia iwe chini yetu tukiipata damu ya Alfred Lumaki na Qwanta wenzake,ndiyo furaha ya mkuu wa wakuu ni ushindi kuwa upande wetu na si vinginevyo" Sauti ile iliendelea kusikika kama mwangwi kisha ikapotea haraka sana, Dalipsol Londo aliwageukia wenzake akawaambia, "vita ya mamba kiboko haimtii wahka kwani amani hutawala hata bila kuingilia hiyo vita hivyo haina haja ya yeye kuingilia, ndiyo hivyohivyo vita ya Hussein na familia yake haitufai sisi kuingilia ile inawahusu yeye na familia yake na wala haivurugi hata kipengele cha kazi yetu".
Baada ya Dalipsol Londo kusema maneno hayo alipiga kofi mara moja na mlango wa eneo walilopo ukafunguliwa, aliingia mtu aliyevaa joho jeusi akiwa anavuta kitoroli kidogo kilichofungiwa kondoo mweusi na pembeni kulikuwa kuna kifaa chenye ncha kali. Toroli hilo lilivutwa hadi mbele ya Dalipsol Londo kisha yule mtu akamkabidhi kifaa chenye ncha kali huku akiwa ameinamisha kichwa kwa heshima, Dalipsol Londi alikipokea kifaa hicho kisha akasema, "ni muda kuanza ibada kuu zaidi ya zote kwa mkuu ambaye ndiye mungu yetu mkuu, hatuna Mungu mkuu zaidi yake mkuu wa wakuu".
Alipomaliza kutamka maneno hayo alimtoboa yule kondoo shingoni kisha chombo kikubwa kikakingwa chini, damu ya yule Kondoo iliingia ndani ya chombo hicho hadi kikajaa na Kondoo aliondolewa na yule mtu aliyemleta akiwa bado anatapatapa kutokana na jeraha lililotobolewa na Dalipsol Londo. Damu ile ya Kondoo ilitiwa kwenye kwenye bilauri zilizotengenezwa na madini ya fedha na zikasambazwa kwa watu waliokuwa wapo humo ndani, kila mmoja alikamata bilauri yake na wakazinyanyua juu kwa pamoja huku vichwa wakiviinamisha.
"Kwa jina la mkuu wa wakuu mwenye mamlaka kuu ya kutupa nguvu pamoja na pumzi kuu" Dalipsol alitamka maneno hayo huku bilauri akiwa ameinua juu kama wengine, alipomaliza kutamka maneno hayo aliinywa damu ile huku wenzake wakifanya hivyo hivyo.

   Kakin ni jamii ya watu wanaoabudu nguvu za giza ambayo ilianzishwa miaka mingi iliyopita huko mashariki ya mbali na iliingia Afrika miaka mingi iliyopita kupitia waziri mkuu wa utawala wa Roma aliyetoroka katika himaya ya Roma kuepuka kuuawa na mtawala wa himaya hiyo aliyekuwa anaitwa Miltonus baada ya kubainika ni mwanajamii wa Kakin. Bwana huyu aliitwa Hilainus aliingia barani Afrika na akapokelewa kwa ukarimu sana kama ilivyo kawaida ya Waafrika kupokea wageni kwa ukarimu, aliingiza falsafa za jamii ya Kakin kwa siri sana hadi akajipatia wafuasi kutoka pande mbalimbali za Afrika. Hadi anafariki  tayari alikuwa na familia yake na jamii hiyo ya siri ilikuwa imeshasambaa mhalimbali na ilikuwa inaendeshwa kwa siri mno kwani habari za uovu wa jamii zilikuwa zishasambaa barani kote ingawa haikujulikana ni nani aliyeileta Afrika.
Usiri wa ibada za jamii hii ulizidi sana pale mtawala wa himaya ya Soghai Sunni Ali alipowaua kwa kuwakata vichwa watu waliobainika ni watumishi wa jamii hiyo, asilimia kubwa ya himaya za kiafrika tayari zilikuwa zimeufuata uislamu baada ya kufanya biashara na waarabu kwa muda mrefu kipindi ambacho himaya ya roma bado inanyanyasa watumwa. Hadi imani za Kakin zinaingizwa barani hapa tayari Uislamu ulikuwa umeshasambaa sana, juhudi za upambanaji dhidi ya jamii haramu  ziliwahusisha wanajamii wote wa Afrika bila kujali tofauti ya kiimani iliyokuwa ipo kati ya waislamu na ambao walikuwa wana imani za kizamani za kuabudu miti na mapango ambao walitofautiana sana kiimani na Kakin ingawa walitegemea majini walioiita mizimu. Wote kwa pamoja walipambana sana na udhalimu na Kakin na baadaye hatimaye waislamu walijitoa baada ya kuzaliwa mtoto aliye na mchanganyiko wa mashariki ya mbali na Habaishi waliokuwa  wafuasi wa  Waothodoksi, mtoto huyu alipewa jina cheo cha Qwanta ambaye katika uzao wake walishirikishwa majini weupe wanaojulikana kwa jina la majini wa nuru. Majini hao walikuwa wametengana na wale wa giza waliokuwa wako pamoja na Kakin, majini hawa walikuwa wapo tayari kuona jamii nzima ya Kakin inaangamia ili dunia iwe huru na walimpatia nguvu za ajabu mtoto huyo  ili alete mapinduzi katika, kisa hicho kilichoelezewa na mwandishi wa mkasa huo aitwae Hassan Omar Mambosasa alichokipa jina la KUANGUKA KWA KAKIN kuanzia kitabu cha kwanza na hadi cha mwisho  ndiyo kinaelezea kinagaubaga juu ya jamii hii na kuanguka kwake.

****

    
   Baada ya siku kadhaa tangu mazishi ya Hamid na Hussein yafanyike Falzal alipanga arudi Marekani na alienda kukata tiketi katika ofisi za shirika la ndege la Ermirates za jijini Tanga lakini alijikuta akishindwa kuondoka baada ya kuambia kuwa hakuna ndege hata moja iliyokuwa ikiingia Marekani kutokana na hali ya ukungu iliyokuwa imetanda katika bahari ya Antalantiki, habari hiyo ilimnyong'onyesha sana na akajikuta akibakia kwenye jiji la Tanga na hata alipojaribu kwenda jiji la Dar es salaam ili akaendelee na starehe napo alijikuta akishindwa kutokana na kukosa gari linaloenda huko. Alipouliza juu ya chanzo cha kuvunjika kwa safari hiyo  alijibiwa kuwa daraja la mto Wami lilikuwa  limevunjika na hata alipojaribu kwenda uwanja wa ndege wa Majani mapana wa jijini Tanga kukata tikeri ya ndege  alikosa vilevile  akaambiwa ndege za mashirika mbalimbali zilizokuwa zinarusha ndege zake kuja Tanga zimevunja safari zao. Hali hiyo ilimfanya Falzal ajihisi ana mkosi baada tu ya kurejea nyumbani akiwa ili ahudhurie msiba wa kaka zake, maisha ya anasa aliyoyazoea kuishi kule marekani ndiyo yalimfanya ashindwe kukaa jijini Tanga kwani akiishi maisha hayo alikuwa anamtia aibu baba yake mzazi.
Heshima ya mzee Buruhan ndani ya jiji la Tanga kutokana na busara alizonazo kwa kuwaongoza wanae zilimfanya aheshimike kwani wanae ni watu maarufu sana ndani ya jiji hilo, hivyo laiti Falzal angeishi hivyo hapo Tanga angetia doa heshima ya baba yake. Falzal alijiona ni kama yu kifungpni kwa kukosa  maisha anayoyapenda na aliyoyazoea, alivumilia kukaa hivyo kwa muda wa takribani siku mbili na hatimaye siku ya tatu akachukua mizigo yake akaiweka kwenye gari na akaazimia kuondoka mbali na jiji la Tanga ili akaishi atakavyo hadi pale atakapoondoka tena Marekani. Eneo alilofikiria kwenda ni Arusha tu kwani ndiyo ambapo hapakuwa na kikwazo chochote, aliamua kutumia usafiri binafsi ili awe huru zaidi.
Hakika hakutambua kama alikuwa anajaribu kukwepa jambo lisilokwepeka labda akukwepeshe muumba ndiyo linaweza kukwepeka lakini si kwa nguvu za kawaida kuweza kulikwepa, hakujua na alikuwa ameshasahau juu ya janga walilolifukia ambalo limejifukua bila ya wao kujijua. Hakutambua kama vikwazo vya safari vinatokana na jambo ambalo lisilokuwa na la kawaida.
Falzal aliwaaga ndugu zake pamoja na mzazi wake kisha akaingia kwenye gari binafsi anayoitumia aina ya toyota landcruiser, alianza safari vizuri huku akiwa na shauku kuu ya kuliacha jiji la Tanga ili aende kuendelea na maisha yake ya anasa aliyoyaacha hapo awali.
Aliendesha gari kwa mwendo wa wastani hadi alipoanza kukaribia Majani mapana ndipo alipozidi kuongeza mwendo wa gari  ili aendane na mwendo unaotakiwa katika barabara aliyopo, alipokaribia eneo ambalo kuna njia iendayo kwenye mzani wa magari makubwa wa Majani mapana aliona  mzee mwenye mizigo akumpungia mkono njiani ili amsimamishe lakini alimpita kwa mwendo mkali sana huku akisonya.
"Vizee vingine bhana vinadhani kila gari ni ya kubeba watu masikini kama wao, akapande basi huko asinisumbue mimi" Falzal aliongea kwa dharau kisha akaongeza mwendo zaidi.
"vijana wengine bhana wanadhani kila mali inaweza ikadumu bila  kujali imepatikana kwa njia gani, wakatafute kupitia jasho lao wenyewe" Ilisikika sautu ikitoka kwenye kiti cha nyuma cha gari hilo  na ikamfanya Falzal ageuke nyuma huku akiwa ameachia usukani, loh! Sallaleh alimuona yule mzee aliyempita pale barabarani akiwa amekaa kwenye kiti cha nyuma akiwa amekunja nne akiwa na mavazi yake machakavu aliyomuona nayo pale njiani wakati anampita. Falzal alizidi kupatwa na uoga sana kwani haiwezekani mtu akiyempita njiani tena kwa mwendo wa kasi amkute ndani ya gari yake, alibaki akimtazama huku akitetemeka kwa uoga hasa alipoona tabasamu la yule mzee.
"Kijana kamata usukani utagonga huoni kama tupo kwa Minchi  tunaelekea kwenye ule mzunguko tena kuna tuta mbele, dereva gani usiyekuwa na umakini uwapo barabaranu wewe tena punguza mwendo maana tunaingia katikati ya jiji magari ni  mengi" Yule mzee alimwambia Falzal huku akutabasamu  na mahali alipomtajia Falzal palikuwa ni mahali ambapo ni mwanzo kabisa alipapita hata kabla hajafika Majani mapana, Falzal alipoangalia mbele kweli aliona  anakaribia kwenye tura na alipunguza mwendo haraka sana na akalipita tuta kisha akashika usukani vizuri akawa anaingia kwenye mzunguko wa kwa Minchi. Falzal alilizungusha gari kwenye mzunguko huo ili arudi alipotokea katika barabara kuu iendayo Segera, alipotaka kunyoosha tairi kisha akate kidogo aingie barabara ya hiyo ambayo alitokea kuingia mzunguko huo wa kwa Minchi alijikuta akishindwa baada ya usukani kugoma na hivyo akazunguka tena ule mzunguko na gari ikaingia katika barabara kuu iendayo Mombasa.
" Huwezi ukatoka nje ya Tanga hata kwa namna gani , ulidhani ukimaliza hiyo roundabout ya Kwa Minchi utaweza kurudi kule ulipokuwa unaelekea. Sasa umeula wa chuya kijana" Yule mzee aliongea huku akitabasamu.
"we...we.....wewe ni nani?" Falzal aliuliza huku akitetemeka na alikuwa akimuangalia huyo mzee pamoja na kuangalia mbele ili asipate ajali, uoga uliokuwa umeibugika nafsi yake ulimfanya ashindwe kutambua kama gari hiyo ilikuwa inaenda yenyewe kwa mazingira ya ajabu pasipo yeye kuiendesha.
"Achia usukani kijana maana unajisumbua gari hiyo inaenda yenye na si wewe unaiendesha na si unataka kunijua mimi ni nani sio?" Yule mzee aliongea kisha akaongea akajibadilisha akawa na sura ile ya mtoto ambayo iiliwatokea kaka zake muda mfupi kabla hawapoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.
"Jamadin! Ha..pana siyo we..we" Falzal aliongea huku akitetemeka kwa uoga kwani hakutarajia kumuona aliyemuona hapo.
"Unashangaa kuniona mimi? Ha! Ha! Ha! Kwanini usijishangae kwa kuhusika kufanya maisha ya mwenzako aliyeumbwa kama wewe kuwa duni" Yule mtoto aliongea kwa sauti yenye kukwaruza tena alicheka kicheko kisichokuwa kinaashiria furaha kwani machoni alishaanza kutoa damu.
"Kutumia nguvu za wenzenu kujitajirisha mliona raha sana sasa leo ni zamu yako Falzal ambaye hupaswi kuitwa baba mdogo kwa mabaya uliyonifanyia" Yule mtoto aliongea huku akilia kwa machozi ya damu
"Si.....siyo mimi Jamadin ni kaka ndiyo aliyekukosea na ndiyo aliyepanga kila kitu" Falzal aliongea kwa uoga.
"Huna cha kujitetea kwa sasa kitachoweza kufanya nikusamehe wewe mwanaharamu, kwanza nipe ukitaka ufe kistarabu la si hivyo nakurarua kama Simba anavyorarua  nyama ya swala"  Yule mtoto aliongea kwa hasira hadi miale ya moto ikawa inamtoka mdomoni mwake.
"Ni...nikupe nini Jamadin?" Falzal aliuluza huku akiwa anazungusha macho yake kuangalia kama anaweza kupata upenyo wa kukimbia lakini hakukuwa na upenyo wa kutokea   kwani milango ilikuwa imefungwa na vioo vimebanwa hadi mwisho.
"Mmmhu! Yaani hilo suala la kunitoroka usifikirie kabisa, nimesema nipe kile kinachowafanya muwe matajiri kila kukicha na kile kinakufanya uwe na bahati kila ukicheza kamari" Yule mtoto aliongea kwa hasira sana.
"sinacho mimi Jamadin anacho..." Falzak alijitetea na alipotaka kumtaka mwenye kitu kinachotafutwa na huyo mtoto lakini alijikuta akikabwa kooni baada ya huyo mtoto huyo kumnyooshea kidole.
"sijakuambia umtaje huyo aliyenacho, sasa nilikuambia nakurarua ukiwa huna na sitengui kauli yangu" Yule mtoto aliongea kisha akatoa makucha mikononi akaanza kumrarua  hadi mwili wa Falzal ukawa ni damu tupu tu na vidonda kila sehemu  ingawa roho yake haikuachana na mwili na maumivu ndiyo yalitawala mwili wake wote, alipiga makelele akilia kama mtoto mdogo lakini hakukuwa na mtu aliyesikia kulio chake kwa muda huo.
"Sasa wasalimie ndugu zako waliokuwa wametangulia kaburini nadhani watakuwa wanakungoja huko walipo" Yule mtoto aliongea kisha akatoa moto mkubwa wenye mlipuko mithili wa bomu ambao ulisambaa gari zima
Hadi muda huo tayari gari la Falzal  lilikuwa limeshafika maeneo  ya Kisosora kwenye matanki ya mafuta ya kampuni ya BP iliyopo jirani na bahari ya hindi, yule mtoto alipopuliza ule moto  gari  lote lilipuka na likarushwa juu hadi ndani ya maji na hu ndiyp ukawa mwisho wa maisha ya Falzal ndani ya dunia na ukawa mwanzo wa maisha mengine nje ya dunia hii katika ulimwengu usionekana kwa macho ya kawaida.

****
 Hali ya Shafii kiafya iliendelea kuwa nzuri na hadi muda huo alikuwa tayari amesharuhusiwa na yupo nyumbani akiuguzwa na mke wake, huzuni kubwa ilkuwa ni sehemu iliyoutawala moyo wake hasa akikumbuka vifo vya wadogo zake. Hakuwa na la kufanya kwa muda huo kwani yeye alikuwa ni mtu wa kutembea na baiskeli ya walemavu kwani kiuno kilikuwa ni sehemu iliyopatwa na kadhia katika ajali ile iliyomkuta na ingemchukua muda mrefu mpaka kutengemaa na kuwa na hali ya kawaida kama ilivyokuwa hapo awali. Hadi muda huo si yeye wala familia yake waliokuwa na habari na jambo lililomkuta Falzal tangu alipowaaga anasafiri kuelekea Arusha akitumia gari binafsi, hawakujua akama falzal ni mmoja wa marehemu kwa muda huo.
Kusononeka, kuhuzunika na kuumia moyo ndiyo jambo ambalo lilikuwa likimsumbua Shafii kila siku hasa alipowakumbuka ndugu zake na jambo lile aliloambiwa na sauti asiyoitambua kuhusu mwanae wa pekee Zayina kuwa ametekwa na yupo chini ya adui yake ambaye hamtambui hadi muda huo aliwahi kumfanyia ubaya upi kwani hakuna dui yake mwenye ubavu wa kumfanyia mambo hayo kwa mujibu wa mganga wake marehemu Sauti ya radi kama alivyomuambia. Alikuwa akimiliki cheni yenye kidani chenye kito kisichofahamika hapa duniani ambayo ndiyo ilifanya awe na nguvu miongoni mwa maadui zake na pia kidani hicho kilikuwa na uwezo wa kuwalainisha mioyo wanadamu wenzake ambao walitaka kufanya jambo baya kwake au kwa jamaa zake. Fikra zilizokuwa zipo kichwani ni kuwa adui aliyekuwa anamfanyia ubaya alikuwa ni mwanadamu wa kawaida na hakuwahi kuwaza kama kuna jini anayeweza kumfanyia hivyo kwani fikra zake zilimpa asilimia mia moja kuwa hajawahi kumfanyia ubaya jini katika maisha yake zaidi ya kuwafanyia ubaya wanadamu wenzake tu.
"ni nani huyu na ana shida gani na mimi kwani hata cheni niliyokuwa nayo inashindwa kumtambua hata kidogo.Jamadin,gasper,Hilson na wengine wengi niliowahi kuwafanyi ubaya tayari wametangulia mbele za haki"  Shafii alijiuliza katika nafsi juu ya utata wa tatizo linalomsumbua la kuondokewa na watu anaowapenda.
"Eeeh! Mungu nimekosa nini mja wako nipo njia panda mja wako" Kwa mara ya kwanza Shafii alijikuta alijikuta akimtaja muumba baada ya kukaa kwa kipindi kirefu akimuasi mwenyezimungu kwa kumtegemea mwingine tofauti na yeye, maneno yake yalisikiwa nyema na mke wake ambaye alikuwa yupo nyuma yake akimtazama mumewe wake kwa masikitiko makuu jinsi anavyolalalmika kwa Mwenyezi mungu. Bi Farida muda wote huo akimtazama mumewe kwa jinsi anavyolalamika alijua  ni kutokana na vifo walivyokufa wadogo zake, wala  hakutambua kama mumewe alikuwa akiteswa na sauti ya mbaya wake ambaye alikuwa hamtambui. Machozi yalipoanza kutiririka katika macho ya Shafii. Hali ya Shafii ilimfanya Bi Farida amkumbtie kwa nyuma kisha akambusu shavuni kwa upendo halafu akamwambia,"Baba Zayina kazi ya Mungu  haina makosa yapasa kumshukuru katika kila hali kwani amekujalia uzima katika ajali mbaya uliyoipata, haipaswi kumlaumu kwakuwa ndugu zako wamepoteza maisha mpenzi wangu"
"Mke wangu inauma sana nahisi dunia yote nimeangushiwa mimi  inauma.....inauma sana" Shafii aliongea huku machozi yakimtiririka machoni mwake.
"Ha! Ha! Ha! Ha! Nadhani unatambua ule msemo wa waswahili waliosema kwamba jeraha la kujitakia halihitaji pole, sasa usitegee pole kwa mtu ambye baadaye akija kukujua upande wa pili wa maisha atakuacha na janga lako mwenyewe. Ha! Ha! Ha! Ha! Ha! Mwanao Zayina najiandaa kuwapikia supu mbwa wangu wamle nikishamchinja" Sauti ileile iliyompa taarifa ya kuwa kuna jambo baya lnalotaka kutokea kwa mtoto wake ndiyo ilimpa taarifa iliyomfanya ashtuke
"He! Baba Zayina kuna nini mbona unashtuka hivyo hadi unanitisha mume wangu" Bi Farida aliuliza
"Nimejitonesha sehemu ya mgonogni mke wangu kutokana na kusononeka huku" Shafii aliamua kudanganya huku akiuma meno kwa maumivu kana kwamba alijitonesha kweli kumbe alishtushwa na sauti ya adui yake mkuu ambaye aliyewahi kumlea mwenyewe kwa mikono yake bila kujua ambye alimwambia jambo baya ambayo ameazimia kwenda kulifanya kwa binti yake kipenzi aliyempenda. Laiti kama wanadamu tungalipewa uwezo wa kuona yaliyojificha katika mioyo ya wenzetu basi Bi Farida angeliomba talaka mapema sana lakini Mungu muumba hakutupa uwezo huo wa kuona yaliyo katika mioyo ya wenzetu ndiyo maana Bi Farida hakutambua jambo linalimtatiza. Ama kweli moyo wa mtu ni kiza nene zaidi hata ya giza nene lililotanda kwenye pori nene  katika usiku mnene, mungu muumba alikuwa na maana yake sana kutuumba wanadamu kwa kuficha yaliyopo mioyoni kwani hadi muda huo tayari wanadamu tungekuwa tushafarakana kama tungebaini yaliyopo kwenye mioyo ya wenzetu.

*kizungumkuti

No comments:

Post a Comment