Tuesday, November 24, 2015

DHAHAMA SEHEMU YA SABA

DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGIN




SEHEMU YA SABA!!
Baada ya Zaina kuchukuliwa Zalabain aliingia ndani ya kasri akiwa ameongozana na yule kiumbe aliyemleta Zaina hadi katika chumba cha siri cha ndani ya Kasri hilo, huko ndani ya chumba hicho walikutana na  Salmin akiwa amekaa kwenye kiti kimojawapo kilichonakshiwa na mapambo ya lulu. Zalabain na yule kiumbe waliketi kwenye viti vya aina hiyohiyo wakawa wanamtazama Salmin.
"je mmefanikiwa kuipata Dainun?" Salmin alimuuliza Zalabain
"hapana bado sijafanikiwa kuipata kwani kila anayetakiwa aende na maji nikimuuliza anasema hana" Zalabain alimueleza.
"Inabidi uipate hiyo ndiyo taji la kifalme litakaa kichwani mwako hata kama ukilipa visasi hadi ukamaliza bila ile hutakuwa mfalme na hata ukiipata hujalipa kisasi bado taji litakukataa vilevile" Salmin alimuambia Zalabain.

****

"Sawa nimekuelewa, enhe wewe Kainun niambie kazi niliyokuagiza imeendaje" Zalabain alimuuliza yule kiumbe aliyemchukua Zaina.
"Mtukufu mjukuu wa mfalme na  mfalme wetu mtarajiwa kazi imeenda kama ulivyoniagiza kwa kumzuia yule mwanadamu anayeitwa Hamisi  aliyepandisha vijini vyake akataka kuingilia kazi yako ya kurudisha nuru iliyopetea katika himaya yetu" Kainun alitoa maelezo kwa Zalabain.
"Vizuri kama umemzuia, je niambie ulimzuia vipi?" Zalabain alimpongeza kisha akahitaji kujua aliyoitumia kumzuia Hamisi asiingilie kazi yake.
"Baada ya yeye kuwapandisha majini wake kwenye kichwa chake niliamua kumkaba shingo yake hadi yakafa yote kisha nikampiga kofi moja yule mwenzake aliyetaka kuchochea kuharibika kwa kazi yako kwa kuleta udi unaowaka" Kainun alieleza  kila kitu alichokifanya hadi Zalabain akatabasamu huku akitikisa kichwa kuashiria amependezwa na kazi yake.
"Vizuri sana kwa kumtandika kibao huyo Ally Buruhan maana anafuata mkumbo tu" Zalabain aliongea.
"Kainun napenda asipewe kazi nyingine  hadi hali itulie maana majini aliowanyonga ni watoto wa mganga Sharkar aliyeuawa na kaka yangu Saliim miaka mia moja  na ushee kupita baada ya kristo kuondoka, kwa mujibu wa maono yangu hao vifo hivyo tayari vishagundulika kwa ukoo wa Sharkar sasa huyu kumuachia kazi nyingine itakayomlazimu kutoka nje ya himaya hii ni sawa na kumkaribisha na vita na kifo chake" Salmin aliongea baada ya kukaa kimya kwa muda  mrefu tena macho yake yakibadilika rangi yakawa yanawaka kama ya paka, Zalabain aliposikia maelezo hayo akatulia akajifikiria kwani hakuwa na mwingine mwenye kuaminika na kutumwa katika kazi zake miongoni mwa majini wote wa himaya hiyo isipokuwa Kainun na ndiyo huyu ameambiwa asimtumie na jini mwenye nguvu zaidi na mwenye kuona yajayo. Himaya hiyo kuna baadhi ya watumishi walikuwa sio wa kuaminika kutokana na kuwa miongoni mwa wafuasi wa waziri kkuu aliyetaka kupata ufalme kwa hila sana, alipoambiwa asimtumie Kainun kwake lilikuwa ni jambo jingine gumu kwake.
"Hapo unanipa wakati mgumu sasa, watumishi hawa sio wa kuaminika huenda kuna wengine ni wafuasi wa aliyekuwa waziri mkuu aliyefungwa katika gereza la giza. Sina wa kuaminika atakayekuwa akisaidia kuzuia kazi yangu isiharibike zaidi ya huyu tu" Zalabain aliongea.
"Usisononeke Zalabain nadhani yupo jini mwingine mwenye msaada mkubwa kwako kama Kainun na naamini atakufaa kuzuia watu na viumbe wasiohusika wasiharibu kazi yako" Salmin alimuambia Zalabain kwa utulivu.
"unafikiri nani atakayeweza kuwa mbadala wa Kainun?" Zalabain aliuliza.
"Baada ya mimi na pacha wangu Saluim kuzaliwa katika kasri la mfalme Mukhatar wa bara Arabu kuna jini mmoja alinieleza kuhusu asili na chanzo cha kufanya mambo yasiyofanywa na binadamu wa kawaida. Jini huyu alinieleza kuhusu asili yangu mimi ni jini na niliyezaliwa na mwanamke wa kibinadamu ila baba yangu ni  jini huyu Ibin Zultash na sio mfalme  Mukhtar kama nilivyoelezwa wakati nikiwa mdogo na mama yangu ambaye alikuwa Malkia wa himaya baada kifo cha mfalme Mukhtar. Jini huyu ndiye aliyemuelekeza kaka yangu akaenda kwa mganga wa kijini Sharkar akaongezewe nguvu, baada ya kaka yangu kuongezewa nguvu alikosea sharti akanywa damu aliyoambiwa asinywe na hapo akawa muangamizi  akaangamiza himaya ya mama yetu na akataka kumuangamiza huyu jini ambaye aliamua kujisalimisha nyumbani kwao ambapo ndiyo hapa Majichungu. Nilipopambana na kaka yangu kwa msaada ya mganga Zaid wa bara Arabu nilifanikiwa kumshinda kaka yangu na nikamfungia kwenye sanduku nikaja kulifukia h Afrika kipindi hicho ni pori tu kwani ilikuwa imepita miaka 100 tu tangu Kristo aondoke duniani, baada ya kazi hiyo niliwachukua Zaid na mama yangu tukaja kuishi huku na tukapokelewa na babu yako kipindi hicho bado ni kjana mdogo wa miaka arobaini hivi. Jini huyo alipokuja huku akifungiwa katika gereza la giza na hakuwahi kutoka hadi leo hii ninavyokusimulia habari hii, huyo ndiyo jini pekee kwa mujibu wa maono yangu anaweza akakaimu nafasi ya Kainun" Salmin alisimulia kisa cha MUANGAMIZI  kisha akamtajia jini mwingine mwenye kuaminika.

NDUGU  MSOMAJI NAJUA KISA HICHO KILICHOELEZEWA NA SALMIN WENGI WENU HAMJAKISOMA, HIYO NI RIWAYA YA KWANZA YA 'MUANGAMIZI' AMBAYO INAELEZEA  UZAO WA SALIIM NA SALMIN  KAMA MAJINI WENYE NGUVU. SALIIIM ALIFUKIWA NA MDOGO WAKE SALMIN BAADA YA KUWA MUANGAMIZI LAKINI ALIFUKULIWA NA WATU WA KAKIN WENYE KUMTUMIKIA SHETANI ILI WAITWALE DUNIA.  KWA WASOMAJI WA MWANZO NADHANI WANAKUMBUKA HIYO RIWAYA AMBAYO NI SEHEMU YA MFULULIZO WA KITABU CHA THE FALL OF KAKIN( KUANGUKA KWA KAKIN).

"je naweza kulijua jina lake huyo kiumbe?" Zalabain aliuliza.
"usiseme unaweza bali ni wajibu wako kumjua anaitwa Maalun nadhani ukimpa uhuru atakaimu nafasi ya Kainun... Kainun utaendelea kuwa mkuu wa majeshi ya angani kama ilivyokuwa awali" Salmin aliongea kisha akamtazama Zalabain usoni, Zalabain alipotazamwa hivyo alipiga kofi mara na viumbe wa ajabu wakatokea mbele yake wakiwa na mavazi yanayofanana.
"Ndiyo mtukufu tumeitikia wito wako" Wale viumbe waliongea kwa utiifu wakipiga goti moja mbele ya Zalabain.
"nahitaji nimuone Maalun hapa akiwa ametolewa gereza la giza ndani ya sekunde tatu tu" Zalabain aliongea na  wale viumbe walipotea kisha wakarejea wakiwa wamemkamata Maalun aliyeonekana kuwa mnyonge sana.
"muwekeni kwenye kiti na nyinyi muondoke haraka sana" Zalabain na wake viumbe wakakuweka Maalun kwenye kiti wakapotea.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Maalun kuwa huru baada ya kufungea gerezani kwa muda wa miaka takribani 2000 kutokana kuisaliti himaya hiyo na kwenda kuishi kwenye ardhi ya wanadamu, alipoona wale majini waliomleta wamepotea alianza kuwatazama wote waliobaki ambapo hakumtambua Zalabain wala Kainun. Yeye alimtambua Salmin tu na hapo akamuangukia miguuni akaanza kuonesha kuomba msamaha.
"Maalun yaliyopita na pia kuongelewa kwake kumepita, kosa ulilotenda milenia mbili zilizopita nishakusamehe cha msingi inabidi tuangalie liliopo hapa" Salmin aliongea na wote wakaafiki kwa kichwa, kauli hiyo ilimfanya Maalun atabasamu na apotee ghafla alipokuwa ameamuangukia na akatokea kwenye kiti kimojawapo kilichopo hapo  walipo wenzake.
"Oooh! Namshukuru mungu kumbe nguvu bado zipo, haya nawasikiliza" Maalun aliongea huku akiwatazama wenzake kwa zamu kisha macho yake yakaweka kituo kwa Zalabain halafu akamwambia " nakusikiliza ewe mtukufu"
Zalabain alianza kumueleza Maalun kila kitu hadi majukumu aliyotakiwa kuyafanya, maelezo yalipofikia mwisho wote walimtazama Maalun wakisubiri kusikia uamuzi wake.
"Kwa ajili ya kuokoa himaya hii isiteketee kwa kukosa  mfalme anayestahiki nipo tayari kwa kazi  yako ewe mtukufu na hata ungeniambia nikusaidie kuwaangamiza nipo tayari" Maalun alikubali na wote wakatabasamu.
"vizuri Maalun na anza kazi yako kuanzia sasa, yeyote atakayeingilia kazi ya mfalme mtarajiwa wewe mzuie ashindwe kuendelea kabisa na si kuua maana utamuharibia kazi Mfalme wetu mtarajiwa" Salmin aliongezea kisha akasimama akapotea na wote waliosalia wakatoka ndani ya chumba cha siri.

****

Upande wa ardhi ya binadamu kwa muda huo ndiyo muda ambao Shafii alifanikiwa kufika katika hospitali yake akapewa tiba ya majeraha yaliyompata na kushonwa usoni alipopasuka kutokana na kujigonga alipoona tukio la Mganga Sauti ya Radi akiuawa na Zalabain, alipomaliza kutibiwa ndipo alipopokea taarifa ya kulazwa kwa mdogo wake katika hospitali hiyohiyo upande wa wagonjwa mahututi. Taarifa hiyo ilimfanya atoke sehemu aliyokuwa anatibiwa baada ya kumaliza tu kushonwa vidonda vyake akaelekea mahali zilipo wodi za wagonjwa mahututi wa hospitali hiyo iliyopo chini ya kampuni yake, alipokaribia katika mlango wa chumba cha wagonjwa mahututi alimuona Hamisi akiwa amekaa kwenye dawati la kusubiria wagonjwa akiwa amejiinamia. Shafii alimfuata upesi kisha akamuuliza. "Shemeji kuna nini kimemkuta Ally" Shafuu aliuliza huku akimtazama Hamisi ambaye naye aliishia kumshangaa kutokana na plasta alizonazo usoni pamoja na michubuko kadhaa.
"Aisee! Shemeji we acha tu. Hii ni vita kali na Ally amekumbwa na kadhia ya kupigwa na kiumbe kisichoonekana na mimi majini yangu yote yameuawa " Hamisi aliongea kwa masononeko.
"Vipi hali yake ipoje huko wodini?% Shafii aliuliza.
"bado madakatari wanafanya kazi yao, na wewe vipi mbona maplasta mengi usoni? Umepata ajali? Hamisi alimuekeza Shafii kisha akamuuliza kilichomsibu hadi akawa na plasta nyingi usoni.
"Yaani shemeji ni bora ingekuwa ajali ingekuwa afadhali kuhusu kisanga kilichonikuta huko kwa Sauti ya Radi, yeye mwenyewe ni mfu hadi muda huu" Shafii aliongea akioneksna anakaribia kukata tamaa kabisa
"hivi huyu anayeiangamiza familia yangu nimemfanya nini? Au uadui wa kibiashara,  yaani Ally mdogo wangu hata kuoa hajaoa ndiyo kwanza anajijenga kimaisha yeye aje kumfanyia hivi kweli. Sikubali hata kidogo nitapambana kulipa kisasi cha hawa wadogo zangu" Shafii aliongea huku machozi yakimtoka kwa uchungu alionao.
"Shemeji nafikiri hii vita tutakuwa wote katika kukomboa familia zetu, waite Hassan, Yusuf na Halid waje watuongezee nguvu" Hamisi alimuambia Shafii, muda huohuo mlango wa wodi ulifunguliwa na daktari akatoka akiwa anaelekea ofisini kwake. Wote walipomuona walimkimbilia wakawa wanamuuliza ju ya hali ya Ally lakini dakari aliwasihi waende naye ofisi, wote walitii wakaelekea hadi katika ofisi ya Daktari huyo na walipofika wakaribishwa katika viti. Shafii na Hamis walikaa wakawa wanaamuangalia Daktari ili wapewe raarifa za Ally kimatibabu.
"Mgonjwa anaendelea vizuri kwa sasa ingawa bado hajarejewa na fahamu, tatizo kubwa alilolipata mgonjwa wenu ni kuvunjika kwa taya yake kwani inanekana alipigwa na kitu kizito shavuni na kupelekea damu zivuje sikioni pia ikionekana hata sikio lake limepatwa ingawa bado haijathibishwa na E.N.T surgery wa hapa hospitali. Kwa sasa tumempatia matibabu kwa ajili ya taya lake na baadaye mtaalam wa E.N.T atakuja kucheki sikio lake. Ni hayo tu bosi" Daktari aliongea kwa kirefu juu ya tatizo lililomkuta Ally, maelezo hayo yalimsikitisha sana Shafii na akajikuta anapandwa na hasira zaidi hadi machozi yakawa na yanamtoka.
"Ha! Ha! Ha! Ha! Ha! Na bado tu huo ni mwanzo tu ila kwa sasa naomba utambue binti yako wa pekee yupo katika himaya yangu" Mwangwi wa sauti ya Zalabain ulivuma katika masikio ya Shafii na kumfanya ashtuke sana hadi Hamisi na Daktari wakamshangaa.
"shemeji  kuna nini?" Hamisi alimuuliza Shafii baada ya kumuona alivyoshtuka na sasa alikuwa anaangalia dari la ofisi hiyo ya Daktari kama ndiyo kwanza analiona kutokana na sauti hiyo iliyomjia masikioni mwake ikitokea huko darini.
 "Ohoo! Zaina, Zaina  mwanangu" Shafii aliropoka kisha akatoka mbio huko ofisini kwa daktari hadi Hamisi naye ustahimilivu ukamshinda ikabidi amkimbize shemeji yake, Daktari naye alijitahidi kukimbia kwa uwezo wake wote ili amuwahi Shafii. Wote kwa pamoja mbio zao hazikuzaa matunda katika kumkamata Shafii aliyeonekana amechanganyikiwa kwani aliingia kwenye gari yake aina ya Cadillac akaiwasha bila hata kumuambia dereva wake aliyekuwa yupo pembeni katika mti akiwa amepumzika, Shafii aliwaachia vumbi tu kwa mwendo bao aliondoka nao kama jambazi anayefukuzwa na polisi baada ya kupora benki.
"Beka daka ufunguo huo tumuwahi huyo asipatwe na matatizo" Hamisi alimwambia dereva wa Shafii kisha akamrushia funguo za gari halafu akakimbia kuelekea lilipo gari lake, Beka naye alimfuata akaingia upande wa dereva akawasha gari, Hamisi naye alishaingia kiti cha pembeni ya derwva akafunga mkanda.
Gari ya Hamisi nayo iliondoka kwa mwendo uleule alioondoka nao Shafii kuingia barabarani, baada ya kukimbiza gari sana waliona moshi mwingi ukiwa umetanda  katika reli zilizopo katika njia iendayo Makorora  tena kichwa cha treni kikiwa kimesimama mita kadhaa kutoka eneo la lenye moshi mzito. Barabara nzima ilikuwa imefungwa na kundi hilo na ikawalizimu Hamisi na Beka wasimamishe gari lao wafunge milango vizuri waende kuangalja kuna nini kimetokea, waliposogea karibu zaidi ndipo walipoliona Cadillac la Shafii likiwa lipo matairi na wananchi walikuwa wakimtoa Shafii ndani ya gari hiyo baada ya kufanikiwa kuvunja kioo. Hawakutaka kupoteza muda nao walijichanganya katika kundi hilo la watu wakafanikiwa kufika mbele wakamtoa Shafii ndani ya gari hilo ambaye alikuwa hajitambui, walimpakiza kwenye gari wakishirikiana na wasamaria wema wakampeleka wakamkimbiza hospitali kwani alionekana bado anapumua.

****

  Zaina alipelekwa kwenye chumba ambacho kilikuwa kina hadhi kubwa kuliko hata chumba alichokuwa akikitumia kule nyumbani kwao, alikuwa akipewa kila huduma aliyokuwa ya muhimu kwa wanadamu kutoka kwa vijakazi wa kasri la kifalme hadi akajihisi yupo ndani ya sehemu salama. Zilipita siku mbili akiwa ni mtu wa kukaa ndani na hana popote pa kwenda zaidi ya kukaa humo, hali hio ilianza kumchosha tu ndani ya siku hizo mbili tu kutokana na mazoea kutokaa ndani aliyokuwa nayo. Siku ya tatu ilipoingia alianza kulalamika kwa kufanywa mateka kwa watumishi hao waliomletea chakula, onyo alilopewa na Zalabain alilipuuzia na akawa anawatolea maneno mabovu vijakazi hao.
"Kelele wewe mwanadamu la sihivyo nitakiponda kichwa  chako  kwa ngumi moja tu ukasalimiane mababu zako waliotangulia"  Sauti ya ukali ilisikika na kisha Kainun akatokea akiwa na hasira baada ya kusikia maneno ya Zaina.
"nirudisheni kwetu hamtaki!" Zain alizidi kuongea kwa ukali kama anaongea na binadamu wa kawaida.
"unasemaje wewe sasa nakutoa utumbo huku unajiona maana nyinyi wanadamu ndiyo chanzo cha matatizo kwenye himaya hii yote yaani nuru hatuijui tangu Mfalme wetu alipokufa kwa ajili ya ubaya wenu mlioufanya" Kainun aliongea kwa hasira akawa anamfuara Zaina kama Mbogo aliyejeruhiwa na sasa hivi akageuka na kuwa umbo la kutisha. Kuonekana kwa Kainun akiwa na umbile lake la kijini kulimfanya Zaina apatwe na mshtuko na azirai hapohapo, Zalabain naye alitokea hapohapo akiwa na hasira kupitiliza hadi macho yakawa mekundu. Alimpiga pigo la nguvu Kainun hadi akaenda chini kama gunia la udongo ulaya, alimuinua Kainun akamkunja akamuinua akamtazama usoni kwa hasira sana.
"unataka kufanya nini wewe?!" Zalabain alimuuliza halafu akampiga kichwa kizito.
"Ewe mtukufu hakika unatambua sisi tunavyowachukia binadamu kwa kutusababisha tusiwe na nuru, binti huyu wa kibinadamu ameanza kutoa maneno machafu katika kasri hili takatifu" Kainun aliongea kwa ghadhabu zaidi.
"hata kama afanye hivi unamjua ni nani huyu na kwanini nimempa hadhi sawa  na familia ya kifalme?" Zalabain aliongea kwa hasira hadi mdomo wake ukawa unatoa cheche akamsukuma Kainun akaanguka chini.
"Mtukufu huyu si binti wa yule mmoja wa wabaya wako tu" Kainun aliongea akiwa amekaa kitako chini.
"Hata kama ni mtoto mtoto wa mbaya wangu lakini elewa mama yake ni mama yangu ila baba yake si baba yangu, huyu ni dada yangu mdogo Kainun. Unafikiri ukimuua nitakuacha wewe ukiwa hai" Zalabain aliongea kwa hasira zaidi hadi akawa anatetemeka, Kainun  aliposikia hivyo alibaini kama ametenda kosa akaomba radhi hapohapo akiwa amepiga magoti.
"Inuka uende na usitie mguu chumba hichi ushamtisha Zaina" Zalabain alimuambia Kainun ambaye aliinuka na kuondoka.

y****

  SIKU ILIYOFUATA

Ndani ya nyumba mbovu yenye vumbi pamoja na samani za kizamani katikati ya jiji la Tanga, ndani ya nyumba hiyo Shafii alionekana akiwa amezungukwa na mke wake, mtoto wake na baba yake mzazi wakiwa wanamtazama kwa chuki huku yeye akionesha uso wa majuto akiwa amesimamia magongo mafupi kutokana na kushindwa kutembea.
"naomba kuanzia leo usiniite baba yako  na mimi nasema sikuwahi na mtoto kama wewe!" Mzee Buruhan aliongea kwa hasira huku akimtazama Shafii ambaye alikuwa analia kama mtoto akiomba msamaha.
"Mke wangu, mwanangu nisameheni ili baba naye anisamehe" Shafii alipiga hadi magoti ingawa alikuwa anasikia maumivu kutokana na kutopona vizuri mguu.
"Baba yangu aliyepelekea uzao wangu hawezi akafanya hivi, nina wasiwasi nilikuwa nakuita baba kimakosa tu. Sina baba mshirikina na katili kama wewe" Zaina naye alitia msumari wa moto kwenye kidonda cha Shafii kwa maneno aliyoyaongea.
"We! We! We! Tena komaeh! Usiniite mkeo mimi, nafikiri nilioana na wewe kwasababu uliniloga lakini sikuridhia hivyo mimi siyo mkeo" Bi Farida aliongea kisha akamsindikiza na singi  Shafii hadi akadondoka.
"Tena umuombe msamaha huyo hapo na siyo sisi" Mzee Buruhan aliongea huku akioneaha kidole kwenye mlango mkubwa wa kuingia ndani ya nyumba hiyo mbovu ya kizamani, Mtu mwenye joho jeusi alionekana akiingia akjwa ameahika sururu lenye mpini mweupe. Mtu huyo alipomkaribia Shafii, Mzee Buruhan, Bi Farida na Zaina walitoka nje wakimuacha Shafii na huyo mti aliyeingia.
"We shetani unakufa" Yule mtu alimuambia Shafii halaf akampiga sururu la kichwa kwa nguvu.
"Aaaaaaaaaaaargh!" Shafii aliachia ukelele wa maumivu lakini alipoangaza macho yake alijikuta yupo sehemu yenye kitanda cheupe na shuka jeupe, alipoona mazingira hayo alizidi kupiga kelele kwa nguvu akidhani labda yupo kuzimu.
"jamani atajitoa dripu yule, muwahini na sindano ya usingizi kabla hajajitonesha  na ile shingo yake iliyovunjika" Ilisikika sauti ya kike ikitokea kushoto kwake.

ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment