Friday, August 18, 2017

TENDAGURU SEHEMU YA TANO






RIWAYA: TENDAGURU
NA: HASSAN O MAMBOSASA
MAHALI: TANZANIA NA MAREKANI





<><><>SEHEMU YA TANO<><><>

Hilo lilikuwa ni zao la kupigana mabusu mbele ya kumbe huyu mwenye miguu mwili asiyejua kuachia nyama yeyote, hapo ndipo wakajiweka huria zaidi hata alipokuja kuketi Mtu mwingine aliye na mwili mkubwa wala hawakujali lolote wao walitulia tu. Hakuna aliyempelekea jicho mtu huyo mwenye asili ya barani ulaya aliyevaa fulana iliyobana pamoja na suruali aina ya jeans


_

_________________TIRIRIKA NAYO
Walipokuja kuachiana huku wakiwa wameegemeana bado hawakuwa na shaka na yule mtu, hii ndiyo ilikuwa desturi za watu wa mji huu kila mmoja alikuwa na mambo yake na hakuna wenye kufuatilia watu . Si mji huu hata nchi nzima watu wapo hivyohivyo, hawawezi kumtilia maanani yeyote anayefanya mambo yake hadharani. Hata itokee watu maarufu wanafanya filamu kwenye mitaa ndani ya nchi hii hakuna mwenye habari nao, wengi wanaweza wakapita tu kwenye mitaa hata wakichukuliwa na kamera kwa bahati maya ila wao hawajali.

      Mambo ya kukodoleana macho yalibaki nchini  Tanzania tu lakini si huku, pamoja na hayo bado ilihitaji kumuwekea umakini huyu mtu kwani inaonekana wazi ni mwenye kitu cha ziada. Kumtilia maanani kulikuja baada ya huyo mwenye mwili mnene  wenye kujengeka kimazoezi alipomshika Mwanamke aliyejiachia kwa Nobeert. Hilo lilifanya atazamwe kwa jicho kali na wote wawili lakini yeye hakujali zaidi ya kucheka na kuonesha ishara  ya busu kwa binti. Mara pili aliepeleaka mkono na kugusa sehemu ya upande kwenye eneo la kukalia la binti, hapo alipokea kibao kizito kwani alionesha udhalilishaji wa dhahiri kwa Mwanamke.

     Kupigawa kibao na mwanamke aliona ni dharau kubwa na alijikuta akisogea akiwa na ghadhabu kali, kabla hajafika Norbert alimnyanyua Bibie kwa namna ya kimaajabu vile mithilia ya ameshika kitu chepesi. Alimuweka upande wa pili na yeye akawa amekaa sambamba na yule mwenye kuleta udhalilishaji, Mtu huyo  hakutarajia jambo hilo na akawa anataka kumvuta mkono mwanamke lakini Norbert aliuwahi mkono wake na kumrudisha nyuma kwa kasi kubwa.

"Its better to leave us alone(ni bora kutuacha )" Norbeert alisema kufanya atazamwe kwa jicho kali na huyo Mbabe.

"Norbert please(Norbert tafadhali)" Binti alihimiza.

"No Alice" Norbert alipotoa kauli hiyo tayari yule Mbabe alishakunja nguo yake kudhiirisha yeye ni mwenye mabavu kiasi.

"Hey! How dare you(Umetuhubutu vipi)?" Alisema huku hakijaribu kumvuta Norbert baada ya kumkunja.


    Hilo halikufanikiwa kabisa kwani Norbert alifytua miguu yake na kuipeleka shingoni mwa yule Muonevu. Alimrudisha tena kitini na akaudaka mkono wake huku miguu ikiwa shingoni, alimpiga kabali moja matata ambayo huyo hakufikiri kama angepigwa. Alibakia hapohapo kwenye kochi  akihangaika kuitoa lakini haikuwezekana kwa jinsi Norbert alivyotumia nguvu, alitapatapa hata akapiga kelele lakini hakuna aliyemjali na sauti kubwa ya muziki ilimeza mtetemo wa midomo yake. Mwishowe alipiga mkono mwenye kochi kuashiria ameshindwa, alipoachia alibaki ni mwenye kuhema hata ule ubabe wote ulimuingia mfukoni.

"Out of my face, now!" Norbert alitoa karipio na yeye mwenyewe aliamka kwa uoga na akaondoka mara moja, baada ya hapo alimtazama Alice aliyekuwa ameingiwa na kihoro kwa kumuona amechokoza balaa jingine.


    Binti mwenyewe alijikuta akimkumbatia kwa nguvu kwa kuweza kumuondosha yule ambaye alidhalilisha utu wake, alimganda mwilini kwa sekunde kadhaa na hata alipokuja kumuachia mwenyewe alijikuta akivamia papi za midomo ya mtoto  wa kiume. Huo ulizaa mengine kabisa ambayo hayakuhitajika kumalizika hapo kitini, bali waliinuka kwa pmoja na kuitoka humo  ndani ya ukumbi na kisha wakaelekea chumbani kwa Norbeert ndani ya hoteli hiyohiyo.



****


                   SAAA TATU ASUBUHI.
HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI, DAR ES SALAAM

     Ndani ya chumba maalum  ambacho hutumiwa na Matabibu wa jeshi la polisi katika kufanya tafiti miili mbalimbali yenye utata, Inspekta Mtela pamoja na yule Tabibu wa jeshi la polisi Maganga walikuwepo wamesimama jirani na meza pana ambayo miili yote ililazwa hapo kufanyiwa uchunguzi. Hii ndiyo nia ambayo mkaguzi huyu wa polisi aliiweka usiku uliyopita kukikucha tu aweze kuifanya, tayari miili hiyo alishaipitia kwa muda mrefu hadi kufikia hapo alibaki kuamini kile ambacho alikiona.

"Afande  una uhakika kweli hii si michoro ya kujichora wao wenyewe hawa?" Tabibu Asakri aliuliza.

"Hakika Sub Inspekta nina uhakika na hichi ninachoongea , hii si michoro ya kutambulisha kundi fulani au genge. Bali hii ni alama waliyokewa hawa watu shingoni mwake, huwezi  kuita tatoo hii bali ni Mhuri wa Muuaji kabisa, inabidi nijue hii alama inamaanisha nini haiwezi kuwa bure hii lazima kuna kitu chochote kile nyuma yake ambacho kimebeba maana"


"Afande hapo siwezi kukupinga moja kwa moja  au kukubali moja kwa moja, najua hujawa  na uhakika juu ya hili ila unahitaji kuthibitisha hizo hisia zako"

"Hiyo ndiyo kazi yangu, kwanza ninahitaji kujua huu mchoro unaamanisha nini. Nitaanza kuutafuta hadi niupate, dunia hivi sasa ni kama kijiji na nchi imekuwa kama mtaa sidhani kama nitashindwa kuwadaka"

"Ok All the best Sir, nikipata jipya huku kwangu likihusiana kila kitu na kazi yako  basi sitosita kujulisha"

"Shukrani sana na kazi njema"


     Inspekta Mtela alitoka nje ya  chumba hicho akiwa amepata kile cha kuanzia kwenye kesi hiyo, aliingia ndani ya gari na aliondoka. Tayari alishapiga hatua kubwa mno yenye kumpa mwangaza kwa mujibu wa mtazamo wake, hali ya kujiamini ilikaa ndani ya mtima wake pasipo hata kujali huko alipokuwa akielekea kulikuwa na hali gani ya kiusalama. Ilikuwa inafaa au ni mbaya zaidi kuliko ile ya awali.


****

        Huku napo  uchachuko wa  nafisi ya Missinzo ulifikia kiwango cha juu na hakutaka kabisa kulaza damu, akiwa na anuani zote alianza kazi mara moja akiwasaka wale wote waliyohusika na kutaka kuyatoa maisha yake kwa bomu. Bado alibaki na lawama  katika upande mmoja wa nafsi yake kwa kushindwa walau kuitilia maanani ile gari ambayo imetoka eneo ambalo aliegesha kipandio chake kwa nyuma yake. Alihisi ni uzembe mkubwa kati ya yote aliyowahi kufanya tangu ajiunge kwenye kazi hizi, alijibebesha lawama mwenyewe  kwa kosa hilo kwani ingekuwa ni hatua nzuri ya kuweza kukumbuka kila kitu kilichotokea.

      Hakika Muumba alimpenda ndiyo maana bado anavuta pumzi kwa kukoswa na bomu ambalo limeharibu gari yake binafsi anayotumia kuitembelea akijulikana kama Mtumishi wa umma. Mtaalamu huyu wa tarakilishi kutoka wizara ya maliasili aliwasili  Kurasini kwenye nyumba ya kifahari ambayo imejengwa jirani kabisa na reli ya Tazara iliyokuwa ikielekea bandarini.  Akiwa ndani ya gari nyingine kabisa aliyoletewa aweze kufanya kazi kiufasaha  alifika eneo ambalo kuna uwanja wa mpira uliyozungushiwa  magurudumu ya gari, hapo aliegesha gari jirani kabisa na mipira hiyo iliyoweka uzio kisha akateremka na kuanza kutembea kwa kujiamini akielekea ilipo nyumba ambayo alihitajika na mtima wake kufika.


       Mwendo wa dakika tano aliweza kufika kwenye nyumba hiyo ya kisasa ambayo imejaa utulivu ndani yake ingawa haipo kwenye mtaa wenye utulivu, alifikia lango la nyumba hiyo na kisha akaliwekea kituo kwa kulitazama kwa sekunde kadhaa. Alipojiridhisha na kulitalii kwa maono alibonyeza kengele iliyopo mlangoni hapo, sehemu ndogo ya lango  ambayo hutumiwa na mtu aliyepo ndani kumchungulia wa nje. Ilifunuliwa na kisha ikaonekana sura ya kijana mwenye sare maalum, huyo alitazama kwa kitambo kifupi kisha akaulizwa shida yake. Kwakuwa ni mwenye taarifa zote  aliweza kujieleza kwa ufasaha kabisa kuwa ni mwenye shida na mwenye nyumba hiyo, kitu ambacho kilifuata baada ya maelezo hayo ilikuwa ni kuhitaji kujua jina lake ili atoe taarifa kwa mwenye nyumba.

"Mwambie Israel Missinzo" Alinena.

"Sawa subiri tafadhali hapahapa"

  Mlinzi alitoka hapo  kwa mwendo wa  mchakamchaka hadi kibandani mwake na kisha akatulia humo kwa dakika takribani mbili kisha akarejea tena.

"Mzee yupo Kaka ila anauliza kama una shida naye kiofisi au kinyumbani"

"Mwambie kiofisi kwani siku ya leo hayupo ofisini nimeamua nije huku mwenyewe"


           Kijana aliondoka tena kwa  mara nyingine na kisha alikaa huko kwa muda mfupi, aliporejea alifungua na lango, Missinzo aliingia kwa kujiamini huku akimtolea mchanuo mwanana. Alimpa shukrani zake kwa kuweza kufungua kizingiti hicho hadi kufikia yeye kuweza kuingia ndani. Aliongozwa moja kwa moja kuelekea alipo huyo anayemtafuata  na aliongoza njia kuelekea huko, alifuata muelekeo wa kwenye nyumba yenye muonekano mwanana iliyozungukwa na bustani nzuri za maua. Hapo alipelekwa  hadi mlango mkubwa na kisha akafunguliwa na mlinzi, alikaribishwa tena kwa mara nyingine, alijongea zaidi na akatokea kwenye sebule pana iliyosheheni samani za kisasa ikiwa na usafi wa kupitiliza. Hapo alimkuta Mtu mzima wa makamo akiwa amevaa kaptula na fulana ya timu ya mpira juu, huyu alimpa tabasamu pana alipomuona kutokana na utanashati wake.

"Israel Missinzo si jina geni sana masikioni mwangu,  karibu sana kijana"  Mtu huyo alisema.

"Nashukuru sana, shikamoo Mzee" Alisema kwa bashasha kubwa mno.

"Karibia uketi hapa, jina lako tu lilivyo nimejikuta nikikukaribisha mwenye ingawa si utaraitbu wangu   kufika watu huku  kwa shughuli za kiofisi"

"Shukrani sana"

"Nakusikiliza, utanisamehe kidogo wametoka humu ndani wa kuweza kukuhudumia vinywaji"

"Hakuna shaka juu ya hilo. Nashukuru sana kwa kunipatia wasaa huo Mzee wangu, kikubwa mimi nilihitaji sana kusafirisha wageni ambao wangeingia Tanzani kutokea Urusi. Hawa ni waafrika kama sisi lakini walihitajika kufikia hapa na kufika mahali stahiki, hivyo  kutokana na shughuli zangu hizi nimeweza kubaini kuwa wewe ndiyo mwenye kuweza kunisaidia kuhusu hili" Kauli hiyo ilimfanya ajiweke kwenye kiti vizuri na kisha akamtazama Missinzo kwa umakini mkubwa. alikutana na sura iliyojaa msisitizo kuliko yake hata akashusha pumzi kutokana na hilo.

"Haya amekwambia nani kuwa ninashughulika na haya?"

"Mzee wangu dunia hii hakuna litakalofichikana juu ya haya, mimi ni kibaraka wa kutupwa kutoka kwenye Genge hatari nchini Urusi. Ninajua kila njia hatari iliyokuwa ikitumika nchini Tanzania kuweza kufikisha wageni wasiyohitajika, zote nimeziona kuwa hazifai kwa kazi hii. Kuna White Gorillas transport wale  ni careless kabisa  sikuona umuhimu wao, hawa Mboni transport nao ni kabisa hamna kitu ndiyo maana nikaja kwako niongee  nawe private si suala la kulipeleka kule ofisini hili"

"Kijana hadi kuwajua hao wapinzani wetu kwenye shughuli hizi ni wazi wewe ni mwenye kuwa ndani ya mtandao mweusi, lakini bado ngumu kukuamini wewe. Sikujui kiundani zaidi kwanza eleza kazi yenyewe na kisha nikutajie advance"

"Ngoja nisifiche kitu nikuweke wazi kabisa uelewe  hilo, hawa wanaoletwa ni makomandoo na wanahitajika kufika nchini Kongo. Lengo likiwa moja tu la kusababisha mauaji kwa familia ya rais wa kule ili Makamu wa rais aichukue nchi, mpango huo haukutakiwa kushriikishwa  wazawa walipaswa wafanyaji tukio na kuondoka. Ndiyo hawa wanaotakiwa kwenda huko kwa usafiri wa gari, hivyo nimeteua kampuni yako kutokana na kuwa na madereva makini na wenye kujua kazi yao"

"Kijana kidogo nimeanza kukuelewa lakini  je unatuhakikishiaje ulinzi wetu juu ya biashara hii  ili na sisi tujue jinsi ya kuhakikisha ulinzi wako. Mambo yakivuja nitakatwa kichwa siku yeyote Bosi wangu ni  mwarabu na katili sana"

"Usalama upo  daima kikubwa ni sise kuaminiana juu ya kazi  hii,imani  ndiyo ya kwanza na sisi wenyewe tutalindana  baada ya kuwa nayo kwa kila mmoja"

"Ok hamna tatizo sasa nahitaji mchoro mzima pamoja na advance ya pesa"

"Kuhusu Mchoro usijali kabisa leo muda wa jioni nikitoka hapa nitakuletea nikiwa nina advance yote. Nafikiri tukubaliane mahali pa kukutana."


"Ok hamna shida, nadhani niachie mawasiliano yako hapa. Nitakuambia kila kitu"

"Hamna shida chukua business card yangu hii, nipo hewani karibia muda wote. Tutawasiliana mahali pa kukutana jioni ya leo ili niweze kukupatia mchoro mzima pamoja na advance.

"Hakuna shida"

"Asante sana Mzee nikuage tu nikimbilie kuweka mipango mingine sawa"

"Karibu tena  Mr Israel"

"Asante"


      Missinzo alipeana mkono naye kisha akapelekwa hadi ulipo mlango wa kutokea nje, baada ya hapo aliagana naye kwa mara nyingine na kisha akatoka. Alipiga hatua kulifuata lango la kutokea ndani humo akiwa ameshaweza kumuingia mtu aliyekuwa akimfuata kwa namna ya kirahisi sana ambayo hakuitarajia kabisa. Alifunguliwa lango na akaanza kupiga hatua hadi alipoliacha gari, hakuwa na cha kumuweka hapo zaidi ya kuingia usafirini na akatokomea Kurasini hiyo aliyoenda kujaribu karata yake ya kutafuta ukweli.

     Ukihitaji kukaa na mtu mbaya basi na hata kuzuga naye kwa ajili ya biashara, wewe muingie ukiwa unajifanya unajua kiundani kila kitu chake alichokuwa akikifanya. Hichi ndicho alichokifanya Missinzo. Kitendo cha kuonesha kumjua mtu na pia kuhitaji kufanya naye kazi,  kunamfanya hata  ashindwe kukutilia mkazo juu yako haswa ukionesha ni mwenye kujua kila harakati zake. Hila hii ilimfanya MKijan  shupavu aweze kumchimba haswa Kibosile wa kampuni maarufu ya usafiri jijini Dar es salaama ambayo ina makao yake makuu  nje ya jiji.


****

      Upande wa Afisa wa jeshi la polisi aliyepo kazini alifanikiwa  kufika hadi kwenye kilabu kimoja ya kukesha iliyopo jirani na ufukwe wa bahari. Hapo ndipo alipoamua kuanzia baada ya kuperuzi kwa muda mrefu akitafuta kuhusu mchoro ule uliyokutwa kwenye miili ile ya wafanyakazi wa wizara ya maliasili, kutokana na mtandao kuwa mpana aliweza kutambua kuwa hiyo ni alama ya taasisi kubwa mno duniani. Nchini Tanzania kituo cha taasisi hiyo ilikuwa ni ndani ya ukumbi huo aliyokuwa akienda, ukumbi uliyojaa kila aina ya laana na haukuwa na usiku wala mchana. Mambo yote yaliyokuwa yakitendeka humo yalikuwa ni sawa muda wote, kumbi ambayo kuingia kwake ndani tu ni gharama kubwa tena unafanyiwa upekuzi wa kila aina. Ndiyo alithubutu Inspekta Mtela kupiga hatua kusogelea hapo, aliamua liwalo na liwe lakini lazima asimamie wajibu wake kwa raia. Dhima ya polisi ilikuwa ni kuhakikisha usalama wa raia, ndiyo maana yupo hapo. Ikiwa tayari wazawa watano wa nchi hii  washapoteza maisha yao, ni haki yake yeye kuwanasa wabaya ili azuie mauaji ya wengine na kuweka usalama ule uliyokuwa ukihitajika. 

     Aliwasili langoni ambapo kuna walinzi waliyokuwa na kifaa maalum cha kukagua, hapo walimkagua  kuhakikisha hakuwa na hatari yeyote ile. Afisa kutokana na ukaguzi wa hapa aliamua kuacha silaha yake garini, hivyo anajitosa mikono mitupu.


ITAENDELEA!!









WAKATI  TUNAANZA KWA PAMOJA RIWAYA HII, PIA TUNAPENDA TUWAJULISHE YA KWAMBA, RIWAYA NYINGINE  YA NORBERT KAILA TOLEO JIPYA INAPATIKANA  NDANI YA PROGRM YETU PENDWA YA SIMU YA ANDROID IITWAYO HADITHIAPP. INAITWA RALOND NA DESMOND KWA BEI NAFUU TU, PIA RIWAYA YA  SHUJAA AMBAYO ILIWAHI KUKATISHA KWENYE  BLOGU YETU  IPO HUKO UTAUPATA MWENDELEZO WAKE KWA BEI NAFUU. KAMA NI MDAU  WA BLOGU MARIDHAWA, HAKIKISHA UNA  PROGRAMU HII UWEZE KUJISOMEA. KUJIPAKUA FUATA LINK HII>>>>> https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi

No comments:

Post a Comment