Thursday, August 17, 2017

TENDAGURU SEHEMU YA NNE





RIWAYA: TENDAGURU
NA: HASSAN O MAMBOSASA
MAHALI: TANZANIA NA MAREKANI




<><><>SEHEMU YA  NNE<><><>


"Huu ni mwanzo tu nyinyi, tena ninaanza na wewe jioni ya leo" Alisema huku  akiweka alama kwenye jina mojawapo ambalo lipo juu kabisa ya karatasi yake, alipomaliza kuiweka tu hilo jina barua pepe iliiingia kwenye tarakilishi yake na kutoa mlio kutokana na kuiweka proramu maalum ya baruapepe.

"Enheee!" Alijisemea


___________________TIRIRIKA NAYO

      Ilikuwa ni ujumbe murua kutoka kwa mmoja wa wenzake aliyepo mbali na eneo alilopo, huyu aliweza kumsaidia mapema siku hiyo kabla  mapambazuko. Muda huo anampa tena mkono kuweza kufanikisha ile kazi yake, jambo ambalo alilihitaji kulijua ndiyo ambalo ameweza kulipata wakati huo aliyokuwa akipanga mkakati mwingine. Missinzo alijikuta hana cha kupoteza ndani ya  muda  wenye giza majira  hayo ya saa tatu usiku, aliingia garini na kuliondoa kwa mwendo wa wastani akifuata uelekeo wa Mwenge kutoka hapo Ilala.

      Hakufika   kabisa  kwenye kituo kamili cha uelekeo huo bali aliishia Magomeni ambapo aliingia kwenye barabara ya Morogoro upande wa kuelekea Ubungo. Napo hakukawia  baada ya mwendo wa mita kadhaa aliingia barabara ya  lami ndogo iliyokuwa ikiingia kwenye mitaa ya Magomeni. Huko alizunguka mitaa huku  akihesabu kuendana na maelezo aliyopewa. Baada ya muda  mfupi alikuja kufika kwenye nyumba yenye udogo wa wastani,  aliitazama kwa kitambo na kisha akaipita hadi nyumba ya tatu kutoka hapo ndipo alisimamisha gari na kulizima.

       Alifunga kila kitu na kisha akaanza kutembea kurudi kule alipotoka,akiwa ni mwenye kujihami kwa kila hatua yake hatimaye alifika kwenye nyumba ile aliyoipita. Hapo alitazama pande zote na kisha akagonga mlango mara mbili kisha akatulia, ukimya ulimpokea    si kutikiwa kule ugongaji wake kwenye mlango wa mbele wa nyumba. Mlio wa luninga ulisikika dhahiri kutoka hapo alipo ambao huwa na sauti ya kipekee ukiambatana na sauti ya kitu kinachooneshwa, hilo lilimfanya aamini kuwa mwenye nyumba alikuwepo au  ametoka kidogo hapo sebuleni kwa dharura ndogo na angerejea muda mfupi. Ndiyo maana mlio wa luninga ulisikika kwani angeenda mbali  basi angezima, imani hiyo haikumpa tabu aligonga tena kwa mara nyingine mlangoni hapo na kisha akasubiri tena kuweza kuitikiwa.

       Ukete ulitawala tena hata ukamzidisha shaka ndani ya mtima wake, alitamani hata apaze sauti huenda mwenyewe angemsikia lakini hiyo hakuona umuhimu wake. Ingekuwa ni kuwapa faida wengine na kama huyo aliyekuwa akimfuata ni mmoja mwenye kuhusika na mnyororo mrefu wa Mtandao. Angempa nafasi nzuri  ya kujiandaa, mwishowe alikata shauri akaona liwalo na liwe tu lakini lazima atie mguu ndani ya nyumba hiyo. Aligeuza shingo kushoto na kulia na kisha akaipeleka nyuma, alipoona hakuna hadhira iliyokuwa ikimtazama mithili ya Mchezaji filamu. Alijaribu kunyonga kitasa cha nyumba hiyo akiwa ni mwenye kucheza kamari tu na  uamuzi wake, hakuna na uhakika kama kingetii amri kwa uonevu wake aliyokuwa akikifanyia.

       Kitasa kilikubali amri na bawaba za mlango zilizokaa muda mrefu zilifanya kizingito hicho kiitikie labeka alipoamrisha kibanio chake, hakika hakukufungwa k muda huo jambo ambalo si  la kawaida  kwa nyumba za mtaa huu. Mita ya jiji la Dar es salaam inafahamika sana kwa wizi lakini pamoja na hayo bado  hakukuwa na ujihami wowote wa nyumba hii, hii lilimpa alama ya kuuliza kichwani. Hakuwa na jibu la kiini cha kuwa vile kwenye nyumba ile ambayo ndani yake  inaonekana wazi kuna vitu vya thmani, mlango ulipokuwa wazi aliingia ndani kwa ghafla kwa namna ya kubiringita na alipokaa sawa alishatoa bastola yake na kunyoosha pale kwenye eneo la sebuleni.

     Yote ni kutokana na kutaka kujihami na pia kuingia ndani ya milki ya mtu pasipo ruhusa yake, ndiyo maana kaingia kwa namna ya kushtukiza hivyo. Hali halisi ya humo ndani kutokana na mandhari ilivyo alihisi kabisa humo ndani  kuna mtego usiyo wa kawaida au kuna  tukio la kuweka mdomo wazi, ndiyo maana akaingia kwa namna ya kiukakamavu zaidi.

"My God!" Alijisemea kwa sauti ya chini akitazamana na mwili wa binadamu uliyokaa kwenye kochi ukielekea luninga ile, shingo ulionekana kuchimbwa na kitu chenye makali.

      Huyu alikuwa ni yule dereva aliyemuona   kwenye kila rekodi ya mkanda wa kamera za kila siku kule uwanja wa ndege akifuata wazungu, huyu ndiye alipewa anuani zake pamoja na mahali alipokuwa akiishi. Aliambiwa ni mtu ambaye alikuwa na maisha ya kawaida tu ya kupanga chumba kimoja tu, lakini hivi karibuni ni ameongezeka hali ya kimaisha kwa ghafla kiasi cha kuweza kumiliki nyumba yake ikiwa na samani za kutosha. Haikujlikana alizipata wapi pesa za kufanya yote hayo, ndiyo maana alimuwekea shaka kwa kumuanza yeye akiamini angeweza kumuwahi lakini tayari mwenye akili zaidi yake amemuwahi na kumtoa kauli.

      Akiwa hata hajakaa sawa tangu akutane na ajabu hilo, king'ora cha gari la polisi kilisikika nje ya nyumba hiyo huku vishindo vya kutua watu vikifuatia. Missinzo alitambua alishachelewa na hakutaka hata tabu na polisi, hata wangemtia nguvuni angeweza kutoka kwani ni mwanausalama. Pamoja na hayo hakutaka wamjue mapema hivyo, yeye aliona ni wakati wa kupotea hapo kabla hawajaufikia mlango wa nyumbani hapo, kitendo cha haraka aliufuata ukumbi mwembamba unaotengeanisha vyumba humo ndani hadi akakutana na mlango mwingine.  Alifungua mlango huo kwa upesi na kisha akatoka nje na kukutana na ua wa nymba uliyosheheni vyumba vingine pamoja na choo cha nje, pembeni jirani na mwanzo wa vyumba vya huko nyuma kulikuwa na mlango mdogo wa kutokea nje.

     Hapo ndipo alipoona pa kutokea na si sehemu nyingine, ilimbidi atoke bila ya kuufungua mlango kiusalama zaidi. Hapo alipanda juu upesi na kuruka nje, alitokea upande wenye njia nyembamba iliyokuwa ikipita kuelekea ndani ya mitaa hiyo. Kufika hapo alihisi usalama upo na aliweka silaha yake vizuri na kisha akaanza kujongea kuelekea mbele ya nyumba ile akiwa ni kama mpita njia aliyetoka ndani ya mitaa hiyo, hakufika mbali alipishana na watu waliyokuwa wakikimbia  kuelekea kule alipokuwa ametoka. Hao walimfanya akae pembeni ya njia na kuivaa hofu ya maigizo, walimpita kwa haraka na kueleka  huko alipotia miguu yeye naye akaendele na safari. Alitembea kwa mwendo mfupi hatimaye akafika barabarani alipotokea, hapo alikutana na gari mbili za polisi pamoja na Maaskari waliyokuwa wamejazana eneo la mbele la hapo.

        Kuwaona hao alitambua wazi hata wale waliyompita muda mfupi uliyopita ni masskari pia waliyopo kazini, wao wapo hima kumuwahi Mtuhumiwa asiweze kukimbia hapo. Hakika ni mtego aliyowekewa bila ya mwenyewe kujijua na ilionekana wazi kuna kiumbe mwenye kufuatilia nyendo zake zote, ndiyo maana alipoingia ndani Pilisi walifika mara moja ilihali tukio limetokea na hakukuwa mwenye habari  mtaa huo kiasi cha kupewa taarifa hao. Haikuingia akilini hatari itokee majirani wasijue na polisi wajue kwa haraka, hapa kuna mchezo mbovu ulichezwa na mwenyewe hakuwa anaujua ulisukwa na nani.

     Bila ya kuweka giza zaidi kwenye harakati zake, alinyoosha njia moja kwa moja hadi lilipo gari lake.  Alipofika nyuma ya gari lake kulikuwa na Motokaa nyingine ambayo ilikuwa imeegeshwa, hiyo hakuitilia maanani na aliipita lakini alipolifikia gari lake lile  liliwashwa na hapo kumfanya asite na akalitupia macho. Lilirudi nyuma kidogo kuweza kupata nafasi ya kukata kona, lilipoipata liingia barabarani na kuondoka kwa mwendo wa wastani na kisha likakoleza mwendo lilipofikamita kadhaa.  Missinzo alilipuuzia na kutaka kupanda gari lake  lakini alisita baada ya kupigiwa mbinja upande wa pili wa barabara, alipotazama kule alikutana na nyumba ambayo mbele ilikuwa na baraza kubwa.


         Sehemu ya mbele ya nyumba hiyo alikaa Mzee wa makamo aliyejifunga msuli, huyu alivaa shati jekundu pamoja na kofia  maarufu kwa jina la baraghashia, mwangaza wa barazani hapo ulitosha wazi kuonesha kila kitu alichokiweka mwili mwake kuifanya stara itimie. Missinzo hakutaka kuonesha kiburi kwa Mzee huyu aliyekuwa amemzidi kumri, alivuka barabara na kumsogelea hadi hapo barazani alipo.

"Shikamoo Mzee" Alimsanahi alipomfikia.

"Marhaba kijana, ubukheri wa afya?"

"Hakika Mzee, sijui wewe?"

"Alhamdulillah nipo  mzima wa afya, kijana wangu wewe ndiyo mwenye gari lile?"

"Ndiyo Mzee"

"Sasa basi ukiwa na umri wako huo na umeonesha ni mwenye heshima na adabu. Sitaki yakukute mabaya kwani pale ulipopaki ni mbele ya nyumba ya Mwanajeshi na ana tabu sana, watu wanaosimama hapo mara nyingi hugombana naye kiasi cha kuwapa adhabu. Ukija tena huku usiweke gari pale"

"Nashukuru Mzee wangu kwa kunipa taarifa, mimi si mwenyeji wa mtaa huu hilo sikulijua"

"Hakuna shida katoe tu pale kabla hajarudi maana mida yake ya kurudi inakaribia tena muda huu anakuwa kanywa"

"Sawa Mzee, nikutakie usiku mwema tu"

"Nawe pia"

 
       Kuachana namna hiyo Missinzo hakutaka kuuweka muda yeye alianza kujongea lilipo gari lake, dhamira yake ya kuifikia motokaa yake haikutimia hata. Hatua tano tu  toka atoke pale barazani ulitokea mlipuko mzito kutoka lilipo gari lake, hilo lilimfanya ajirushe nyuma kwa nguvu kisha akalala chini.  Akiwa chini alitazama kule ambapo yupo Mzee alimuona akiwa yupo chini  akiwa hajitambui ilihali hakuguswa na athari za mlipuko ule,hakika ni mshtuko mzito ndiyo ulimkumba kwa balaa hilo lililojitokeza mbele yake.


****


       Majira hayohayo nyumbani kwa Inspekta Mtela hakukulalika baada ya ripoti ya uchunguzi wa miili ya awali kuweza kufika kwenye mikono, muda huo alikaa  kwenye meza ya kujisomea hapo ndani akiwa amejaza picha mezani huku Ripoti ikiwa ipo mkononi. Tarakilishi yake  pembeni ikimsaidia katika kufunua kichwa chake kujua mahali pa kuanzia kwenye kazi yake nzito, ripoti haikuenda nje ya hisi zake juu ya kifo cha watu wale. Kweli kabisa walikufa kabla ya kutupwa kwenye maji ili waonekane wamezama maji,  vipimo vya miili vile iliweza kugundua mengi kabisa juu ya vifo vile, hakika ilihitaji kukuna kichwa kuweza kung'amua waliyopo nyuma ya yote ni kina nani hadi kufikia kukatisha uhai wa wanausalama wale ambao yeye hakuwafahamu wasifu wao.

"Wamekufa masaa sita kabla ya kukutwa pale asubuhi muda wa saa mbili, hii inamaanisha wamekufa saa nane usiku wa kuamkia leo. Kwanini wauliwe? Kuna  nini walichokuwa wamekiingia watu hawa hadi wakafanyiwa hivi?  Ni wafanyakazi kutoka wizara ya maliasili ya utalii wameuawa kwa sumu, kwanini wafanyiwe hivyo?"  Alijikuta akiongea mwenyewe ndani ya nyumba yake ambayo imejaa upweke kupitiliza hadi kufikia mwia huo, maswali yake hayakupata jibu kabisa juu ya kile kilichotokea.


     Alijikuta akiweka ripoti ile kando na kisha akaisogeza tarakilishi mbali kidogo, baada ya hapo aliziweka picha vizuri jirani na uso wake, alizipa macho moja baada ya nyingine huku akitazama sehemu mbalimbali za miili hiyo pamoja na mikao yao ilivyo. Baada ya kupitia kwa muda mrefu hatimaye alikutana na michoro ya kufanana ikiwa ipo pembezoni mwa shingo za wale watu, hili  ilionesha ni wazi ni wanachama wa kikundi fulani hadi wakafikia kuchora michoro  ya aina hiyo ambayo inafanana kwa kila kitu. Alijikuta nimwenye hamasa zaidi ya kutaka kujua kuhusu mchoro huo kwani hakuamini ni sehemu ya pambo tu ambalo vijan wengi hupenda haswa kutumia kupendezesha miili yao.

          Inspekta Mtela alinyakua karatasi moja mezani hapo kisha akachukua kalamu  nyeusi ya wino ambayo hupenda sana kuitumia, alianza kuichora michoro hiyo kama ilvyo hadi alipoumaliza. Baada ya hapo aliinua karatasi ile na kuanza kutazama jinsi ulivyotokea, alijitikiza kichwa kuridhia kabisa jinsi mkono wake ulivyopitisha kalamu juu ya karatasi kuendana na lengo lake  alilotaka litimie. Hakika aliupatia vilivyo hadi akajikuta akaichia tabasamu mwenyewe mithili ya  ameshanda shindano la kuchora kwa  mpitisho ule wa kalamu kwenye  zao hilo la mti.

         Aliiweka kando ile karatasi na kisha akaendelea kutazama jinsi tswora ile ilivyopita kwenye ngozi zao, macho aliyakaza haswa kama vile alikuwa akiona ngozi hiyo dhahiri hadi akaweza kung'amua kingine tofauti juu ya mchoro ule. Hapo aliweka shaka kabisa na alihitaji kuhakikisha kuwa mawazo yake ni sahihi kabisa, aliweka nadhiri kabisa hilo ni suala ambalo angeanza nalo iwapo mwanga ungeibuka kwa siku inayofuata kufukuza giza lenye kuficha mengi.

****

    SAA TATU USIKU.
WASHINGTON DC,MAREKANI

         Masaa kadhaa mbele kwa saa nchini Marekani ilikuwani saa tatu usiku lakini kwa saa nchini Tanzania, Ilikuwa ni saa kumi Alfajiri. Ndani ya mgahawa wa hoteli ya Hay Adams  majira hayo Norbert ni ameketi kwenye kiti akiwa na chakula pamoja na kinywaji mbele yake, mkabala naye alikuwepo yule binti ambaye alisimamishwa saa sita ya siku kwa kuzibwa njia pindi alipotaka kuingia Mgahawani. binti huyu alipendeza haswa kwa kuvaa gauni jekundu ambalo halikukadirika urefu kabisa kutokana na kuketi, uso wake ni mwingi wa tabasamu mbele ya kijana huyu mzawa wa Tanzania mwenye ugonjwa haswa kwa mabinti. Haikujulikana hata ilifika vipi hadi kuweza  kukaa pmoja nae huyu asiyeweza kupita kimyakimya akiona tunda zuri lipo mtini.

       Binti alijiweka huru kabisa mbele ya Mamba asiyejali njaa wala shibe yeye huweka chochote kinywani akijisikia, ucheshi wake pamoja na mitindo  ya kisasa aliyonayo Norbert. Vyote vilimfanya  hata asijihisi kuhitai kuondoka hapo, hawa walifurahi kwa pamoja wakipata chakula huku wakisogeza saa kwa kuongea. Ilifika wakati wakamaliza maakuli yao na hapo wote wawili walinyanyuka na kuondoka hapo Mgahawani, walihamia upande wa pili kwenye hoteli hiyohiyo kulipokuwa na ukumbi wa usiku ambao hautoi sauti nje  ya mlango wake.  Huko kulichangamka haswa kutokana na kuwepo muziki uliyoruhusu watu kucheza pamoja na unywaji vileo kwa watu mbalimbali.

          Norbert akiwa ametanua kiwiko chake cha mkono na kufanya binti yule apitishe kinganja chake na kumshika, alimuongoza hadi ilipo meza ambayo ilijitenga mbali na fujo. Kutembea hivyo kulivuta macho ya wengi mno kutokana na gauni fupi alilolivaa binti baada ya kuonekana dhahiri aliponyanyuka kule Mgahawani hadi kujongea huku. Hapo walikaa karibu na kuongea mengi mno huku wakionekana ni wenye furaha mno, binti alijiweka huru zaidi na hata akawa anamuegemea zaidi Simba mwenye kunoa meno yake. Hilo lilikuwa ni zao la kupigana mabusu mbele ya kumbe huyu mwenye miguu mwili asiyejua kuachia nyama yeyote, hapo ndipo wakajiweka huria zaidi hata alipokuja kuketi Mtu mwingine aliye na mwili mkubwa wala hawakujali lolote wao walitulia tu. Hakuna aliyempelekea jicho mtu huyo mwenye asili ya barani ulaya aliyevaa fulana iliyobana pamoja na suruali aina ya jeans.


ITAENDELEA!!






WAKATI  TUNAANZA KWA PAMOJA RIWAYA HII, PIA TUNAPENDA TUWAJULISHE YA KWAMBA, RIWAYA NYINGINE  YA NORBERT KAILA TOLEO JIPYA INAPATIKANA  NDANI YA PROGRM YETU PENDWA YA SIMU YA ANDROID IITWAYO HADITHIAPP. INAITWA RALOND NA DESMOND KWA BEI NAFUU TU, PIA RIWAYA YA  SHUJAA AMBAYO ILIWAHI KUKATISHA KWENYE  BLOGU YETU  IPO HUKO UTAUPATA MWENDELEZO WAKE KWA BEI NAFUU. KAMA NI MDAU  WA BLOGU MARIDHAWA, HAKIKISHA UNA  PROGRAMU HII UWEZE KUJISOMEA. KUJIPAKUA FUATA LINK HII>>>>> https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi

No comments:

Post a Comment