Wednesday, June 22, 2016

SHUJAA SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO

RIWAYA: SHUJAA
MTUNZI: Hassan O Mambosasa
SIMU:+255713776843
+255762219759
WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII KWA MARA NYINGINE





SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO!!
 Annie alipoona kile alichoekewa na Moses alijikutaanakaa chini kwenye zulia la sebuleni hapo bilakujitambua, alibaki akiwa anakodolea luninga hukuakiwa haamini kwa kile alichokiona.


"vipi hizi sofa za hapa sebuleni ni invisible kwamacho yako nini mpaka ukae kwenye zulia?"Moses alimuuliza Annie kwa dharau, Annie alijikuta akitembea kwa magoti kumfuata Moses alipo huku uso wake ukiwa na hofu.

"dada siku hizi miguu yako haifanyi kazi mpaka utumie magoti" Moses alizidi kumuandama Annie kwa maneno ya kumchanganya.

  Annie kwa magoti alitembea hadi akamfikia Moses huku machozi yakiwa tayari yanamtoka, alishika mapaja ya Moses kwa viganja vyake vya mikono huku akimtazama Moses kwa huruma lakini Moses hakuwa na muda hata wa kumtazama yeye ndiyo kwanza alichukua simu yake akaanza kuperuzi kama vile hamuoni. Annie alizidi kulia baada ya kubaini Moses kampuuzia na hataki hata kumsikiliza, alimminya Moses mapaja yake huku akilia akiwa anamtazama usoni.

"Moses! Moses! Moses please" Annie aliongea kwa sauti huku akiweka mikono kwa ishara ya kuomba, hali hiyo ilisababisha Moses aache kuchezea simu yake ya kiganjani amtazame Annie huku akiwa anatabasamu.

"Dadaeh! Umefiwa? Halafu hayo magoti na kuweka mikono hivyo ungekuwa unaweka ukiwa kanisani huku ukitubu kwa madhambi yako si ungekuwa umo miongoni mwa wanakondoo wa bwana" Moses aliongea huku akitabasamu.

"Moses nisamehe usifanye hivyo" Annie aliomba msamaha huku akitokwa na machozi.

"wewe si unajifanya unajua kuwafanya boyfriend wa wenzako watumwa wa ngono sasa wewe sepa hapa kabla sijamuita Anko wangu aje akufanye kitu kibaya" Moses aliongea akiwa anaonesha wazi kuwa ana hasira na Annie.

"No! Moses sitoki hapa mpaka unisamehe, hata anko wako akija sitaondoka" Annie aliongea.

"ohoo! Hutaki sio ngoja nikuoneshe picha yake, Iam hope ukiiona utaondoka mwenyewe" Moses aliongea kisha akafungua akamuonesha Annie picha yake aliyopiga na Kennedy ambaye sio mgeni kwa Annie, Annie alipoiona hiyo picha alijikuta akishtuka hata kulia aliacha hapohapo na hofu.


"Unaogopa nini sasa au kisa umemuona anko wangu na kwa taarifa yako anaishi hapahapa, sasa wewe leta ubishi nimpigie simu aje akupe kichapo kama alivyomfanya yule mtu mliyemtuma wewe na mdogo" Moses aliongea huku akimtazama Annie machoni ambaye uoga tayari ulishamuingia baada ya kuona sura ya mwanaume ambaye alikuwa mpenzi miaka kadhaa iliyopita, hakuamini kabisa kama mwanaume anayemfahamu kwa jina la Tassu ambaye ndiye aliyeoneshwa picha yake ni mjomba wa Moses.

"Heeh! Bado upo kumbe? Ngoja nimpigie nimuite maana unajifanya wewe kichwa ngumu" Moses aliongea kisha akaanza kubonyeza namba kadhaa kwenye simu yake akaiweka sikioni mwake huku akimtazama Annie kwa hasira, hofu ya ghafla iliuvamia moyo wa Annie na akajikuta akinyanyuka akaenda hadi kwenye luninga akaichomoa flash kwa hasira kisha akaitia kwenye mkoba wake.

"sasa hii huipati tuone sasa" Annie aliongea kwa kiburi kisha akatoka sebuleni hapo.


"Ha! Ha! Ha! Ha! Haya hiyo flash ichukue kama unataka ila ujiandae maana kuna blog tumeitengeneza tunaiachia soon na hiyo video tumeupload tayari, jua sipo peke yangu mwenye hiyo video" Moses aliongea huku akicheka na kupelekea Annie arudi hadi karibu kisha akafungua mkoba na kuitoa flash hiyo lakini alipelekea Moses aone kitu kingine tofauti na flash hiyo, Moses alishtuka baada ya kuona kitu ambacho anatembea nacho Annie kwenye mkoba wake lakini aliamua kujikaza kisabuni. Annie hakumuambia neno lolote zaidi ya kuondoka alipompa flash Moses kwa haraka hadi nje kisha mlio wa gari ukafuatia, Moses alipohakikisha Annie ameondoka alitoa simu yake akampigia Hilary akamuita pale nyumbani kwao. Baada ya dakika tano Hilary alifika nyumbani kwao Moses kama alivyoitwa, alimkuta rafiki yake akiwa yupo kwenye kochi sebuleni akiwa ana hofu kidogo.

"vipi mbaba mbona hivyo au kuna jingine jipya?" Hilary aliuliza.

"Dah! Hilary Mwana huyu demu ni wa ngwasuma tuwe makini sana" Moses aliongea kwa wasiwasi, Hilary muda huo alikuwa amesimama mkabala wa Moses na alikuwa anatazama karibu na uvungu wa kochi alilokaa Moses kisha akainama akimuacha Moses akumshangaa anatafuta nini. Alipoinuka aliinuka akiwa ameshika kifaa kidogo chenye umbo la mcheduara akamuonesha, Moses alibaki akikiangalia kile kifaa kwa mshangao.

"hiki kinasa sauti kimetoka wapi?" Hilary alimuuliza Moses ambaye alibaki ameduwaa tu kutokana na kutojua hicho kilipotokea.

"mmh! Hata sijui kilipotokea nahisi ni huyu malaya maana nilipomuoneaha hiyo video alikuwa  amepiga magoti kwenye miguu" Moses aliongea

"inanekana anajifanya yeye mjanja sana" Hilary kisha akakikanyaga kinasa sauti na mguu akakivunja.

"tena anatembea na mguu wa kuku kwenye handbag yake, nadhani huyu si mtu wa mchezo Hil" Moses alimuambia Hilary.

"ooh! Shit hebu twende control room kuna kitu tukakicheki nahisi huyu demu anajifanya mjanja sana" Hilary aliongea kisha akaanza kuelekea kwenye chumba cha kuongozea kamera cha hapo nyumbani kwao Moses huku Moses akimfuata nyuma.

****


   Baada ya kutoka nyumbani kwao Moses aliamua kwenda nyumbani kwa mzee Bernard ingawa hakuingia ndani aliishia getini tu akiwa yupo ndani ya gari, akiwa hapo getini Annie aliamua kumpigia simu Victoria ambaye baada ya dakika kadhaa alitoka nje akiwa amejiandaa akaingia kwenye gari la Annie.

"niambie Shosti" Victoria alimchangamkia Annie.

"safi tu za kwako Shostito" Annie alionesha uchangamfu kwa Victoria.

"Safi tu, enhe! Niambie kuna suprise gani hiyo unataka kunionesha" Victoria aliongea akionekana ana shauku sana kutaka kujua.

"aaaaah! Shosti papara ya nini? Kama upo tayari twende hutochelewa" Annie aliongea.

"Poa nichukue V8 maana kuna sehemu napitia shosti hivyo lazima niwe na usafiri nikirudi" Victoria aliongea kisha akashuka ndano ya gari ya Annie akaingia ndani kwa haraka, baada ya muda geti la nyumba ya Mzee Bernard lilifunguliwa na gari aina ya Toyota landcruiser V8 ikatoka nje na muda huo huo gari la Annie likaanza kuondoka na landcruiser V8 ikawa inalifuata kwa nyuma.

  Safari ya magari hayo mawili ilienda kuishia Kitunda katika eneo ambalo Victoria hakuwa analitambua, gari ya Annie ilipiga honi katika geti kubwa kama la kiwanda katika eneo lenye uzio mrefu hapo Kitunda. Geti hilo lilifunguliwa na magari yote yakaingizwa ndani kisha likafungwa, waliingia katika mandhari ya nyumba kubwa ya kifahari iliyopo jirani na nyumba ya kizamani ambayo inaonekana haijamaliziwa. Annie na Victoria wote walishuka ingawa Victpria hakuwa anaelewa kipi kinaendelea hadi muda na hicho kitu alichoambiwa ni kipi, Annia alimfuata Victoria alipokuwepo akiwa ameficha mikono nyuma ambayo ilionekana kuficha kitu. Usoni alikuwa amepambwa na tabasamu pana ambalo hata Victoria lilikuwa linamfanya ahisi uwepo wa amani ndani ya eneo hilo, Annie alipomkaribia Victoria alifanya kitu ambacho hakikutarajiwa kabisa kama angefanya hivyo kwa rafiki yake. Mikono aliyokuwa ameificha aliitoa mbele ikiwa imeshika bastola ndogo aina ya revolver ambazo hutumiwa sana na polisi, alimnyooshea Victoria katika paji lake la uso akiwa ameliondoa lile tabasamu feki alilokuwa ameliweka usoni mwake.

"Annie what are doing? Stop joking ( Annie unafanya nini? Acha utani)" Viktoria aliongea kutokana na kushangazwa na kitendo cha Annie kumnyooshea bastola.

"Iam not joking Vik, you are in my empire and you are my prison ( Sitanii Vik, upo katika himaya yangu na wewe ni mfungwa wangu" Annie aliongea akiwa anatabasamu kifedhuli halafu akapiga makofi mara mbili, kundi la vijana wenye silaha za kivita walijitokeza wakawazunguka wote.

"Annie kwanini lakini?" Viktoria aliongea kwa kulalamika huku upga ukiwa umeitawala nafsi yake.

"Ni mapenzi tu Vik ndiyo yamenipelekea nikuteke siwezi nikakaa nikashuhudia mtu anayeninyima usingizi nisimpate mwanaume wangu wa maisha ni mdogo wako Beatrice. Nampenda Moses ndiyomaana nimemlevya nikalala naye nikiwa katika siku za hatari, pamoja na hayo bado mdogo wako ni kikwazo katika hili" Annie aliongea kwa jazba huku akimzunguka Viktoria akiwa yupo katikati ya vijana wake.

"Annie huwezi ukatembea na Tassu mjomba wake Moses halafu uwe na Moses ambaye hakupendi anampenda Beatrice" Annie aliongea kwa uoga.

"Nani kakuambia Moses hanipendi? Unafikiri kuna mwanaume timilifu anaweza asinipende mimi? Sema huyo mdogo wako ndiye anayesababisha asinipende na ndiye anayesababisha wewe pia uwepo hapa na kuanzia leo wewe ni mateka wanguhutatoka mpaka huyo mdogo wako amuache Moses. Boys mchukueni mkamfungie kule safe room kwakuwa sio teka rasmi" Annie aliongea huku machozi na Viktoria ndiyo akazidi kutetemeka, alipotoa amri vijana walimkamata Viktoria kwa nguvu wakawa wanamvuta kuelekea kwenye nyumba ya kifahari.

"Annie hapana kumbuka mimu ni rafiki yako" Viktoria aligoma kwenda akajikuta akisema kwa uchungu huku akiburuzwa kuelekea ndani.

"urafiki wetu ulikuwa ni moto lakini sasa umezimwa matone ya mvua, mapenzi ya Beatrice ndiyo matone ya mvua yaliyouzima urafiki wetu. Tambua sisi siyo marafiki tena Vik ingawa tulikuwa wote tangu O level hadi Univertsity" Annie aliongea kwa sauti kutokana na Viktoria kuwa tayari ameshafikishwa mbali na wale vijana waliomkamata. Viktoria aliendelea kulia kwa uchungu na akiwa anafanya majaribio ya kuwaponyoka wale vijana lakini alishindwa kutokana na nguvu waliyokuwa nayo wale vijana, aliingizwa ndani huku akiendelea kutoa vilio ambavyo havikuwa na manufaa yoyote kwake na wala hazikuweza kumfanya ajikomboe katika eneo alilopo.

Viktoria alipoingizwa ndani Annie aliwageukia vijana wake wengine wakiosalia akawauliza, "ratiba ya biashara leo ipo vipi na mteja wa leo ni nani?"

"Ratiba ya leo inasema kilo ishirini za Heroine zitatoka na kwenda kuuzwa kwenye warehouse kule Bunju, mteja wa leo ni Komredi pamoja na Gotta" Kijana mmoja alimueleza Annie.

"Nini? Komredi ni adui yetu na Gotta ni adui yangu ingawa ni ndugu yangu wa damu, Boys vijanamlipoenda kupambana nao kule Mbezi Afrikana juamnaenda kupambana nao leo. Kikosi cha ziada nakihitaji kwani siwezi kukataa biashara na sipo tayari kupoteza mzigo, bebeni kikosi chenye shotgun tu ili kujihami. Hasara yoyote nawakata vichwa mmoja mmoja nadhani mmenielewa" Annie aliongea kwa hasira.

"Madam" Vijana hao waliitikia.

"mnaweza mkaendelea na kazi" Annie alisema kisha akapiga hatua kwa maringo kuingia ndani ya nyumba katika mlango alioingizwa Viktoria ndani.


    Vijana hao walimtambua kama Annie alikuwa ni katili wa kutupwa na alikuwa akisema kitu hapindishi, hata hapo alipowaambia kuwa atawakata vichwa wakimpa hasara alikuwa hatanii hata kidogo na ikitokea kazi ikaharibika basi itakuwa hasara yao kweli. Annie ni msichana katili na mwenye roho ngumu tofauti na muonekano wake, pamoja na ukatili huo bado alikuwa ni mwenye udhaifu mdogo ambao unamfanya awe mpole kama akifanyiwa na mtu mwingine kama ilivyo kwa viumbe wote hakuna asiye na udhaifu. Udhaifu wa binti huyu ulikuwa ni Moses pekee na hawezi kufanya chochote kibaya hata akiudhiwa vipi na Moses, ndiyo maana hata alipooneshwa video yake alishindwa hata kumfanya chochote Moses ingawa alikuwa amebeba bastola iliyosheheni risasi. Aliishia kupachika kinasa sauti tu kijanja tu ili aone kama kuna lolote atakalolipata litakaloweza kumsaidia aondokane na aibu aliyoipata, hivyo ukatili wake wote na hata ubebaji vitu hatari bado haikuwa chochote mbele ya Moses Baada ya kuingia ndani Annie alipitiliza moja kwa moja hadi katika chumba kimojawapo chenye mitambo mingi, kilikuwa ni chumba chenye mitambo ya kuongezea ulinzi pamoja na mashine mbalimbali za kurekodi sauti. Annie aliwasha  mashine mojawapo akaweka masikioni spika ndogo za kusikilizia sauti ili kuondoa kelele kwa mtu aliyepo jirani na eneo hilo, alisikiliza sauti iliyokuwa inasikika katika mashine ambayo haikudumu kwa muda mrefu sana na wala hakuwa amepata chochote cha maana zaidi ya kusikia maongezi Hilary na Moses. Sauti ilikatika pale Hilary alipokikanyaga kinasa sauti baada ya kubaini uwepo wa kinasa sauti sebuleni hapo, Annie aliishia kutukana matusi yasiyoweza kuandikika au kuelezeka kwa mtu aliyestarabika.

"Hilary unajifanya mjanja sio sasa ngoja nikutie mkononi nitakugeuza vipisi maana wewe ndiyo unayempa Moses jeuri, pumbavu!" Annie aliongea kwa hasira baada ya mpango wake kufeli kisha akatoka katika chumba cha kuongezea mitambo mbalimbali ya jengo akaelekea katika chumba ambacho Viktoria alipelekwa akiwa na hasira sana.



****

               GUHO WAREHOUSE
                     BUNJU
                  DAR ES SALAAM
Wakati Annie akiingia katika chumba alichomficha Viktoria akiwa na hasira kutokana na mipango yake kufeli, upende wa pili mdogo wake Andrew (Gotta) alikuwa yupo ndani ya jengo ambalo lilikuwa linatumika kama Ghala ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali. Eneo hilo la ghala ambalo kwa muda huo lilikuwa ni tupu kutokana na kutotumuka kwa siku nyingi ndiyo ambalo vijana wa Annie pamoja na vijana wa Komredi walipanga kufanyia biashara, upande wa Annie alitambua wazi anafanya biashara na maadui ila upande wa Komredi na Andrew hawakutambua hilo suala ingawa walikuwa wamejipanga kuwaua wanaofanya nao biashara ili wachukue madawa bila ya kutoa pesa. Andrew aliwahi mapema katika eneo la biashara kisha akawapanga vijana wake vizuri ndani ya jengo hilo ili wawe tayari kwa kufanya mchezo mchafu kama nafasi ikipatikana. Baada la kuwapanga vijana wake hodari aliowaficha sehemu mbali ambazo sio rahisi kuonekana na mtu labda awe kwa juu kabisa kutoka jirani na hapo walipo.

" najua nyinyi ni simba na hamuwezi kuvamiwa na mtu aliyepo ndani ya jengo hili labda awe sniper katika jengo lile pale ambalo haliwezi kuingilia kutokana na ulinzi uliopo" Andrew aliongea huku akionesha ghorofa lililopo jirani na jengo la ghala ambayo wanataka kufanya biashara na watu ambao walikuwa hawawajui, baada ya hapo aliondoka akiwa ameshapanga watu wake vizuri ili aje muda maalum wa miadi.

****


  Annie alipoingia katika chumba cha kisasa alichofungwa Viktoria alimkuta bado akiwa analia ingawa aliwekwa kwenye chumba chenye hadhi sawa na chumba anacholala nyumbani, Annie alimfikia Viktoria akatoa bastola kwenye mkoba wake akamnyooshea akiwa hana hata chembe mzaha usoni mwake.

"Annie nimekukosea nini mimi?" Viktoria aliuliza huku akilia.

"Hujanikosea ila kiburi cha mdogo ndiyo kimekufanya uwe humu, sipo tayari kushindwa ninapopenda. Leta handbag yako nikaitelekeze hiyo simu yako yenye GPS isiniletee matatizo" Annie aliongea akiwa amemuelekezea bastola Viktoria, Viktoria alimpatia mkoba wake huku akitetemeka sana kutokana na sura ya hasira aliyokuwa nayo Annie. Annie aliufungua mkoba huo akatoa simu ya Viktoria akaikagua hadi akamaliza, aliirudisha simu ya Viktoria kwenye mkoba na uso wake ndiyo ulikuwa na hasira zaidi na alipoifunga zipu ya pochi alimvamia Viktoria akamtandika makofi yasiyo na idadi kwa hasira.


"Pumbavu wewe yaani kukuacha na simu yako ndiyo ujaribu kupiga simu ukifikiria mtandao wowote humu ndani unakamata, tena ukijifanya mjanja tena namwaga ubongo wako wewe" Annie aliongea kwa hasira akampiga teke la mbavu Viktoria kisha akamwambia "upo ndani ya himaya yangu ujanja hautakiwi la si hivyo utarudi jina. Aliondoka humo ndani akimuacha Viktoria akiwa yupo katika maumivu makali, alifunga mlango kwa nje.

****

               MIKOCHENI
             DAR ES SALAAM


  Nyumbani kwa mzee Bernard hadi inaingia Saa mbili ya usiku mtoto mkubwa wa mzes Bernard hakuwa ameonekana tangu alipotoka akiutumia usafiri wake mwenyewe, simu yake ulipopigwa mwanzo ilikuwa haipatikani lakini baadaye iliita bila kupokelewa na kuzidi kuongeza hofu kwa Mzee Bernard. Taarifa ya kutoonekana kwa binti yake aliitoa upesi katika kituo cha polisi na suala hilo likaanza kufanyiwa kazi upesi, hadi saa tano usiku inaingia Mzee Bernard hakuwa amelala na wala hakuwa amekula kutokana na suala hilo. Alikuwa yupo nyumbani kwake na kundi kubwa la maaskari walikuwa wakifanya mahojiano na familia yake, mitambo ya kipolisi iliunganishwa na tarakilishi baada ya juhudi zote kugonga mwamba na zoezi la kutafuta mahali simu ilipo kwa kutumia GPS (Global positioning system) ndiyo likafuata baada ya askari wa jeshi la polisi kubainishiwa simu ya Viktoria ilikuwa imeunganishwa na GPS.

"Hii hapa tumeipata kubwa" Askari aliyekuwa anashughulikia kutafuta simu kwa tarakilishi alisema kwa sauti kubwa, kila aliyesikia suala hilo alikimbia kwenye kioo cha tarakilishi ya jeshi la polisi.




TUKUTANE TENA  PANAPO UHAI NA AFYA.







MWENYE KUIHITAJI RIWAYA HII HADI MWISHO ANAWEZA KUWASILIANA NA MTUNZI KUPITIA NAMBA ZAKE HAPO JUU KWA NJIA YA UJUMBE MFUPI TU WA MANENO NA SI KUPIGA. HUKO UTAIPATA YOTE.



KWA RIWAYA ZAIDI LIKE UKURASA WETU WA FACEBOOK AMBAO NI:




      Riwaya Maridhawa
       Riwaya Maridhawa
      Riwaya Maridhawa
       Riwaya Maridhawa
        Riwaya Maridhawa

No comments:

Post a Comment