Wednesday, November 23, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA KUMI




 RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA


    SEHEMU YA KUMI!!
   Safari yake ya kasi iliishia kwenye hotel ya Kangaroo akaingiza gari ndani kwa kasi,
alienda hadi kwenye maegesho ya ndani ya hotel  akasimamisha gari halafu akalizima.

         "Nawatakia ufutiliaji mwema, si wanajua kufuatilia magari ya watu" Moses alisema huku akinyoosha kiti cha dereva akajilaza

         "na inaonekana wanajua tunaelekea Muhimbiliwalipolazwa wanajedhi waliokuwa wanalinda kwa Jeneral waliokutwa hawajitambui" Norbert aliongea.

            "ndiyo maana yake" Moses alidakia.

     Moses na Norbert walikaa hapo kwenye maegesho ya hoteli kwa dakika kadhaa kisha wakashuka kwenye gari yao wakiwa na wazo jipya litakalozidi kumchanganya aliyekuwa akiwafuatilia, waliamua kuingia ndani ya hotel hiyo iliyo chini ya Gawaza& Son company ambayo ipo chini ya Moses baada ya kuachiwa urithi na baba yake.

****

     Baada ya muda wa dakika takribani kumi na tano tayari Norbert na Moses walikuwa wameshabadili mavazi waliyokuwa wameyavaa hapo awali, ubadilisho wa kiutambuzi tayari ulikuwa katika miili yao ambapo ingekuwa ngumu kwa mtu wa kawaida kuwatambua. Kofia maarufu kama kapelo ndiyo zilikuwa zimefunika vichwa vyao vikawafanya wasijulikane kwa urahisi kabisa, walitumia gari nyingine tofauri na ile waliyoingia nayo hapo hotelini ambayo iliwafikisha hospitali ya taifa ya Muhimbili.

     Walienda hadi kwa Dokta Hilary wakiwa na wahka wa kutaka kuwahoji wale wanajeshi kwani waliamini wakifanya hivyo watakuwa wameweza kusaidia kwa kiasi fulani katika kufanikisha jambo, walipofika ofisini kwa Dokta Hilary walipokewa na simanzi nzito iliyokuwa imetanda katika uso wa daktari huyo. Dokta Hilary alikuwa ameweka mikono shavuni tangu kina Moses wanaingia ofisini na hakuwa ameitoa mikono hiyo shavuni hadi wanaketi kwenye viti, alionekana kuzama ndani ya majuto zaidi.

     Moses na Norbert walipoketi kwenye viti vyao hakuwa amenyanyua kauli kuwakaribisha kama ilivyozoeleka, utofauti wa hali hiyo uliwapa mshangao nao wakataka kujua kipi kilichomsibu rafiki na pia mtu wao wa karibu kwa baadhi ya vitu. Ukimya wa Dokta Hilary ulipozidi Norbert aliamua kupiga meza na kumshtua kisha akamuuliza, "whats the problem(nini tatizo)?".

             "Hii sasa ni uzembe wa hali ya juu najuta hata kwanini nilikuja humu nisibaki kule" Dokta Hilary aliongea huku akijipiga kichwa chake kwa nguvu mithili ya mtu anayeelekea kupatwa na wazimu, alikiona kichwa chake hicho ndiyo kilisababisha afanye huo aliuona uzembe ndani ya nafsi yake ambao hakutakiwa kuufanya kabisa.

               "aaaaargh! My head!(Kichwa changu) My brain(ubongo wangu), ndiyo chanzo cha yote haya natamani hata ningefuata ile sauti iliyonisihi nisiende ofisini kuliko kulusikuliza. Huenda haya yote yasingetokea huenda huyu mdondosha kadhia asingeweza, ila hili bichwa na bongo iliyomo ndani yake ndiyo chanzo" Dokta Hilary alizidi kulalamika kwa hasira sana zilizosababishwa na majuto ndani  ya nafsi yake, alipiga ngumi kwa nguvu kwenye meza yake ya kitabibu kwa mara tatu mfululizo kisha akapiga ukelele wa jazba.

       Alipotaka kuongeza ngumi nyingine  kwenye meza hiyo isiyokuwa na hatia juu ya hilo linalomfanya ajute ndani ya kichwa Norber aliudaka mkono ili asizidi kuiadhibu meza hiyo isiyokuwa na hatia wala kuhusika na hicho alichokuwa akilalamikia.

              "Hey hebu punguza hasira na utuambie nini tatizo basi" Norbert aliongea huku akimkamata mkono kwa nguvu Hilary ili asizidi kuiadhibu hiyo meza ambayo haina hatia yoyote wala haikustahiki adhabu hiyo aliyokuwa akiipa, pia alimzuia ili  apate kumtuliza ili ajue kile kilichomsibu Hilary ndani ya kichwa chake hadi akawa na jazba hiyo.

               "Aaaargh! Hichi kichwa hiki ndiyo chanzo kimenishawishi niondoke, ngoja nikitie adabu kwanza. Haiwezekani kabisa" Dokta Hilary aliongea kisha akachukua mashine ya kutobolea karatasi ili zibanwe katika mafaili iliyopo mezani, aliinyanyua mashine hiyo kwa mkono mwingine tofauti na ule wa awali aliokuwa anautumia kuiadhibu meza ambao sasa hivi ulikwa umekamatwa barabara na Norbert.

     Aliiituliza mashine hiyo katikati ya utosi wake hadi sehemu ya nyuma ya mashine hiyo yenye plastiki maalum kwa kuhifadhi vipande vinavyotobolewa ikavunjika, hakuridhika kabisa na wala hakuhisi kama kichwa chake kitakuwa kimepata adhabu kwa kujipiga na plastiki hilo hivyo hamu ya kuendelea kukiadhibu kichwa chake ikamjia. Aliinyanyua mashine hiyo ambayo kwa sasa imebaki chuma kitupu akiazimia kuituliza katika utosi kwa mara nyingine ikiwa imebaki chuma kitupu tu, hakujali kujeruhiwa na mashine hiyo zaidi ya kutaka kukipa adhabu kichwa chake alichokiona kina hatia sana.

      Alinyanyua mashine hiyo kwa mara nyingine tena kwa kutumia nguvu kuliko awali akilenga kuituliza kwenye kichwa chake ili akipe adhabu tena, mashine hiyo ya chuma  nayo ilikuwa imetulia kimya sana na ilikuwa ikitii amri wa mikono ya Hilary na jinsi alivyokuwa akiiiamrisha. Mashine hiyo ilipotaka kutua kwenye kichwa cha Dokta Hilary kwa mara nyingine Norbert aliipangua kwa karate moja matata kabisa ikaenda chini moja kwa moja ikakutana na sakafu, mlio wa chuma cha mashine ndiyo ulifuata ambao ulimrudisha Hilary sawasawa akawa na hali ya kawaida.

       Alibaki akihema kwa nguvu huku akishikilia kifua chake kisha akaketi kwenye kiti chake akawa ameinamisha uso wake chini, muda wote huo Moses  alikuwa akimtazama rafiki yake akiwa amezama ndani ya tafakuri nzito juu ya kile anachokifanya.

            "Hilary tuambie kuna nini" Moses alimuambia Dokta Hilary kwa sauti ya upole huku akimtazama usoni.

            "wanajeshi walioletwa hapa baada ya kuwa hawajitambui tayari ni marehemu kwa sasa na mmoja hajulikani halipo, chanzo cha kifo ni kimoja na kile cha Bishop Edson, Mufti na General" Dokta Hilary alimuambia Moses akiwa ameingiwa na unyonge baada ya hasira yake kumshuka.

              "Nesi mmoja amemuona mwanamke aliyevaa mavazi ya wauguzi akitoka katika wodi hiyo" Dokta Hilary aliwaambia, Moses na Norbert kwa pamoja walibaki wamegwaya kwa taarifa hiyo. Akili zao tayari zilikuwa zimezidiwa na mtu aliyekuwa akijua kwa kina juu ya mipango yao, tegemezi la mwangaza mwingine wa jinsi ya kuanza kazi zao tayari lilikuwa limemalizwa na adui yao wasiomtambua.

              "Hili ni tatizo Moses try to think chanzo cha kifo cha General, wanajeshi hawa ikifika makao makuu jeshini nini kitafuata unafikiri? Moses kumbuka hii sumu uliitengeneza wewe itumiwe kwa ajili ya kuua wadudu waharibifu wa mazao lakini sasa inatumuea kuua watu, Luteni Jenerali Ibrahim Salim ndiyo mwenye cheo kikubwa aliyebakia katika majeshi ya hapa. Jaribu kufikiria akiipata taarifa hiyo atakuchukulia hatua gani? Hapa utakamatwa wewe tu na heshima yako kwa taifa itaingia doa Moses, wewe ni professa na ni mtoto wa professa hebu fikiria hilo" Dokta Hilary aliongea kwa hisia sana kisha akanyanyuka kwenye kiti chake kwa mara nyingine akapiga hatua akaelekea dirishani, alisimama dirishani akawa anaangalia nje kwa dakika kadhaa kisha akageuka akawatazama Moses.

             "You know what(unajua nini)? Mimi ni daktari  wa kuaminika na hawa wanajeshi hawa nimeletewa mimi niwape huduma kwa kuaminika kwangu kwani kutoka Oysterbay hadi Lugalo hospital ni mbali sana na Muhinbili ni karibu. Wameamua wawalete hapa kwani wakicheleweshwa wangekuwa na hali mbaya sana na hata kupoteza maisha kabisa, wameniletea hapa nimewahudumia wakawa na hali nzuri kabisa hadi mmoja amerudiwa na fahamu kabisa. Lakini hichi kichwa kilichobeba uso wangu kimesababisha nichukue uamuzi wa kwenda ofisi ya manesi kumuita nesi aje kuwahudumia na hatimaye nikaja ofisi kuendelea na kazi zingine, matokeo yake ni nesi huyo kupishana na mwanamke aliyemuona mlangoni akiwa ana sare za manesi akitoka humo ndani. Yaani wagonjwa niliokabidhiwa niwatibu kwa kuaminiwa na L.J Ibrahim tayari wameuawa, ni aibu kwangu pia ni balaa kwetu hebu fikiria  aliyenipa jukumu hili atanionaje mimi na atakufikiria vipi Moses ikiwa anatagundua sumu iliyowaua watu wake na mkuu wake inatoka kwako" Dokta Hilary aliongea kwa kulalamika sana,  aliwatazama Moses na Norbert akaona ukimya ulikuwa umetanda kwao. Ilichukua muda wa dakika nzima ndipo Moses akanyanyua kinywa chake akasema, "Hilary wasiwasi juu ya hili suala haupo kwako bali upo kwangu kwani hawa wamefariki na kuna baadhi ya watu wamejua nimekuja hapa Muhimbili ndiyo watu hao wakafariki, nimeshaanza kuharibikiwa ila nitaomba msaada wako kwa mara nyingine ili unisaidie".

                  "No Moses siwezi kukusaidia tena utaniweka matatizoni zaidi kumbuka urafiki wetu unajulikana" Dokta Hilary alikataa kumsaidia rafiki yake kutokana na tatizo alilonalo, kauli hiyo ya rafiki yake kipenzi ilimfanya Moses aheme kwa nguvu kisha akamtazama Norbert ambaye alimpa ishara ya kificho sana. Aliporudisha uso wake kwa Hilary tayari ulikuwa umebadilika usio na hata na chembe ya mzaha, alikaa kimya kwa sekunde kadhaa kisha akazamisha mkono wake mfukoni akatoa kitu cha rangi ya kahawia mfano wa kitabu cha kutunza namba za simu chenye nembo ya rauda pembeni akamkabidhi Dokta Hilary.

                 "Sipo kiurafiki tena na inabidi ufanye ninachokuambia Hilary nipo kwa ajili ya kutetea taifa" Moses aliongea huku akimpatia Moses kitu hicho akichokitia katika mfuko wake, Dokta Hilary  alikipokea kisha akakifungua aone kilichomo ndani yake.

          Macho ya Dokta  Hilary yalitua juu ya kitambulisho adimu kuviona vya usalama wa taifa ambacho kulikuwa kikimtambulisha vizuri Moses kuwa ni mmoja wa wanausalama hao, mshtuko wa ghafla ndiyo ulimpata Hilary baada ya kubaini kuwa alikuwa na urafiki na mwanausalama wa siri kwa muda mrefu sana.

                "Inabidi utusaidie katika kazi yetu Hilary na huu utambulisho wangu ubaki siri yako umeelewa?!" Moses aliongra kwa msisitizo huku akipuuzia mshangao uliomkumba Dokta Hilary halafu akachukua kitambulisho chake.

              "namuhitaji huyo nesi aliyemuona huyo mwanamke na pia nahitaji nijue ni dawa gani iliyowalaza hao wanajeshi hadi wakawa na hali mbaya hivyo" Moses aliendelea kuongea
.
            "OK, wagonjwa hawa wamevuta dawa ya gesi ambayo hutumika katika upasuaji tu na hairuhusiwi kuuzwa kwa maduka mengine ya dawa isipokuwa hupatikana bohari kuu ya dawa tu tena kwa kibali maalum tu" Dk Hillary aliongea.

             "unaweza ukanionesha ripoti kamili?" Moses aliuliza

            "Bila shaka" Dk Hilary alijibu kisha akafungua mtoto wa meza akatoa makaratasi ambayo alimkabidhi Moses, Moses aliyapitia makaratasi hayo kisha akamkabidhi Norbert ambaye naye aliyapitia hadi mwisho.

            "Lexone hutoka kwa madaktari maalum tu kule bohari kuu ya dawa kwa ajili ya kuzuia damu isitoke nyingi katika upasuaji mkubwa tu na mara nyingi hutolewa kwa taasisi ya moyo katika kufanya upasuaji tu" Moses aliongea huku akimtazama Norbert halafu akamgeukia Dk Hilary akamuambia, "muite huyo nesi ninuhitaji nataka atusaidie katika jambo hili pia".

      Dk Hilary aliafiki maneno hayo ya Moses na akanyanyua mkonga wa simu  ya mezani abonyeza kitufe cha tarakimu moja akaweka sikioni, alisubiri kwa muda wa sekunde kadhaa simu ilipopokelewa akaongea, "namuhitaji Phina ofisini kwangu haraka sana".

     Aliweka mkonga wa simu mahala pake kisha akawaashiria kina Moses wasubiri baada ya simu hiyo kutoa ujumbe kwa mhusika, muda huo wakisubiri mlango wa ofisi ya Dk Hilary ulifunguliwa kwa taratibu akaingia muuguzi wa kiume ambaye alishtuka baada ya kuona ugeni uliopo humo ndani.

              "We Japhet ndiyo adabu gani kuingia bila hodi ofisini kwangu?" Dk Hillary aliongea kwa  ukali.
 
              "samahani Dokta" Muuguzi huyo wa kiume aliomba radhi kisha akatoka nje mara moja akiwa na wasiwasi sana, Dokta Hilary alimpuuzia huyo muuguzi sambamba na Moses na Norbert.

     Baada ya dakika mbili mlango wa ofisi ya Dk Hilary uligongwa mara mbili, Dk Hilary alimuamrisha anayegonga hodi aingie na hapo akaingia muuguzi wa kike aliyevaa gauni la rangi ya kijani iliyopauka ambalo lilimuishia juu kidogo ya magoti na kuifanya miguu iliyojaa vyema ionekane kwa wote. Alikuwa amesuka nywele kwa mtindo uliompendeza, alikuwa ni mwenye mwili wa wastani wa wastani sura pana mwenye pua iliyo na umbo dogo pamoja midomo mipana iliyopakwa rangi ya mdomo iliyoendana na rangi ya ngozi yake.

             "Abee Dokta" Muuguzi huyo aliitikia.

            "Phina kuna wageni hawa walihitaji msaada wako kidogo" Dk Hilary aliongea huku  akimuonesha Phina  wageni hao ambao  hawakuwa wageni katika  macho yake, kisha akaendelea kusema, "Nafikiri wewe ndiyo uliyemuona yule mwanamke ambaye umesema hujawahi kumuona nesi kama huyo hapa hospitali".

     Phina aliitikia kwa kutikisa kichwa akiafukiana na kauli ya Dk Hilary.

              "Sasa basi unaweza ukawasaidia shida yao Phina" Dk Hilary aliongea kisha akawatazama Norbert na Moses akiwaashiria waongee.

               "Phina una uhakika kabisa umemuona huyo mwanamke vizuri?" Norbert aliuliza.

               "ndiyo" Phina alijibu.

              "ukiweza kumuona kwa mara nyingine utamkumbuka?" Norbert aliuliza tena.

              "Ndiyo nitamkumbuka" Phina alijibu huku akiinama chini kutokana na kutazanwa na macho ya Norbert yasiyokuwa na hata chembe ya mzaha.

           "vizuri, Dokta naomba penseli na katarasi nyeupe" Norbert alimuambia Dk Hilary ambaye alifungua faili lililopo mezani akampatia karatasi kisha akafungua mtoto wa meza akatoa penseli akampatia.

           "taja sifa zake jinsi alivyo" Norbert alimuambia Phina huku akiwa ameshika kalamu ya risasi na karatasi ikiwa mezani, Phina alianza kutaja sifa za huyo mwanamke hadi akamaliza na Norbert alitumia muda huo kumchora huyo mhusika kuendana na sifa anazotajiwa. Baada ya dakika takribani tano mchoro wa sura ya mwanamke ilikuwa ipo kwenye karatasi aliyokuwa anaichora Norbert, Norbert alimuonesha Phina ile karatasi huku akimuuliza, " anafanana na huyu?"

      Mshtuko wa ghafla ulimpata Phina baada ya kuona mchoro huo uliochorwa na Norbert, aliishia kutikiza kichwa kukubali bila hata kuulizwa suala linalimpasa akubali kwa ishara. Aliitazama tena ile karatasi iliyobeba mchoro wenye kufanana kwa kila kitu na huyo mhusika aliyemtaja, alikubali tena kwa kutikisa kichwa bila hata kuulizwa kitu kitakachomfanya akubali.

             "Ndiye huyu?" Norbert aliuliza.

            "Ndi...ndiyo yeye" Phina alikubali huku akibabaika kutokana na taaluma ya juu ya uchoraji aliyonayo Norbert kiasi cha kuchora sura ya mtu alipotajiwa sifa zake, ilikuwa ni jambo la kawaida kwa wapelelezi wa daraja la kwanza wa shirika la upelelezi la Afrika mashariki kuwa na taaluma hiyo kwani wamefundishwa kila taaluma ya wanausalama wa kawaida na wana ujuzi wa vitengo vyote  vya usalama.

      Norbert alichukua ile karatasi akamuonesha Moses ambaye naye alibaki na bumbuwazi akionekana kutoamini kile alichokiona, ilikuwa ni sura ambayo hakutarajia kuiona muda huo kwenye tukio kama hilo na sasa ameiona sura ya mwanamke yule mrembo na mwenye sura ya upole.

             "Damn!" Moses alisema kwa hasira kisha akamtazama Phina akasema, "usiondoke hapa utaondoka na sisi ikiwa umemuona huyo mtu kama ni muuaji kweli jua maisha yako yapo hatarini".

       Phina alibaki akiwa ameduwaa kabisa asijue la kufanya kwani hakuelewa walikuwa wana wadhifa gani, aliitikia kwa kichwa tu kwani aliona hawakuwa wa binadamu wa kawaida kiasi cha kumchora mtu ambaye hajabahatika kumuona akifanya tukio kwa kutumia ushahidi wa sifa na muonekano wake.

            "Dokta huyu hakikisha anapewa likizo ya muda mrefu na uongozi wa hospitali nitaongea na mganga mkuu" Moses aliongea kisha akasimama akapeana mkono na Dk Hilary halafu akaongea, " dada tufuate".

     Kwa pamoja waliondoka hospitalini hapo ili kulinda usalama wa Phina huku wakijua wapo peke yao walioona wakati wanaondoka nae, kumbe kulikuwa kuna kibaraka mmoja aliyeshuhudia ujio wao na hadi wakiwa ofisini kwa Dk Hilary. Laiti wangelijua wangelimuweka kiti moto kibaraka huyo wangepatsma mengi huyo lakini hawakujua juu ya hilo, waliondoka naye na muda huohuo kibaraka akafanya kazi yake iliyomleta.



****



    Muda ambao Moses na Norbert wanaingia katika hospitali ya Taifa ndiyo muda ambao Leopard Queen na Panther asiyejua kuongea kiswahili vizuri walikuwa wakiingia barabara ya Umoja wa mataifa baada ya kumaliza kutekeleza kazi waliyokuwa wameazimia kuitekeleza katika hospitali hiyo. Walikuwa wamo ndani ya gari aina ya toyota Altezza nyeusi ambayo ndiyo ilikuwa ikiwafuatilia kina Norbert kabla hawajaingia chaka baada ya kupigwa chenga na Moses, furaha ilikuwa imewatawala na kupelekea kusahau kuwa walikuwa na ushahidi waliouacha huko nyuma ambao ingekuwa ni hatari sana kwao.

            "Baby nimekumbuka kitu, inabidi tumpigie Japhet aibe ripoti yote isije ikatutia matatani" Leopard Queen alimuambia Panther huku akimchezea shingoni kwa mikono yake laini, Panther alikuwa yupo makini katika kushika usukani wa gari na mwili ulianza kumsisimka baada ya kufanyiwa hivyo.

             "Oooh its true Mrembo call him" Panther aliongea na muda huo akakata kona kuingia kushoto baada ya kuimaliza barabara ya Umoja wa mataifa akaingia barabara ya Ally Hassan Mwinyi, Leopard Queen alipiga simu akatoa maelezo kwa Japhet ambaye ndiye yule muuguzi wa kiume aliyeingia ofisini kwa Dk Hilary  bila hodi pia akamkuta Norbert na Moses ofisini humo. Taarifa za uwepo wa Norbert na Moses ofisini kwa Dk Hilary pia kuitwa muuguzi aliyemuona Leopard Queen nazo ilifika kwa Leopard Queen kupitia huyo kibaraka, ilikuwa ni taarifa aliyoiona ya kawaida sana kwani hakuona uhatari wowote katika taarifa hiyo.

               "baby Norbert na Moses wapo ofisini kwa daktari aliyekuwa anawatibu wale soldiers, nesi aliyeniona kaitwa" Leopard Queen alimuambia Panther baada ya kukata simu, taarifa hiyo ilimfanya Panther acheke sana kwa kuwaona kina Norbert wajinga sana.

                "They are insane, I think they are after Doctor's report on soldiers' bodies before they died. Ha! Ha! Ha! Ha! Ha! They are lost( Wao ni wendawazimu, niafikiri wanafuatilia ripoti ya Daktari katika miili ya wanajeshi kabla hawajafa. Ha! Ha! Ha! Ha! Ha! Wamepotea)" Panther aliongea huku akicheka na kusababisha Leopard Queen naye acheke kwa nguvu kutokana na jambo ambalo aliona ni ujinga kulifanya.

                 "Ngoja Japhet aibe ripoti watajua pengine pa kuanzia, wajinga" Leopard Queen aliongea  huku akicheka.

                "Ha! Ha! Ha! Ha! Fools( Ha! Ha! Ha! Ha! Wajinga) watajuta" Panther aliongea kisha akasimamisha gari akaegesha kwenye kituo cha daladala kilichopo na mwanzo wa barabara ya Kenyetta, Leopard Queen alimbusu mdomoni Panther kisha  akashuka akaelekea kwenye kutio cha daladala cha upande wa pili wa barabara. Panther aliondoa eneo hilo kwa kasi sana baada ya kuhakikisha Leopard Queen amepanda daladala tayari.



****



    Majira ya saa tisa na nusu tayari Norbert alikuwa ameegesha gari eneo la pembeni ya barabara ya Sokoine lilpo jirani na bandari ndogo ya boti, alisubiri hapo kwa muda wa mfupi na hatimaye Josephine akaonekana akitoka nje akiwa anatembea kwa madaha sana kutokana na viatu alivyovivaa miguuni . Josephine hakuwa amemuona Norbet na alianza kutembea kuelekea kwenye kituo kikuu cha daladala Posta akapande daladala ili aondoke, aliipita gari ya Norbert hadi pale Norbert alipopiga honi ndiyo aliiona gari yake akaifuata hadi ilipo akasimama jirani na mlango wa dereva

              "ni siku nyingine tena" Norbert alimuambia Josephine ambaye aliishia kutabasamu baada ya kumuona Norbert kwa mara nyingine.

               "Norbert niambie" Josephine aliongea huku akitabasamu.

               "safi, naona promise umeisahau tayari" Norbert aliongea huku akiachia tabasamu.

               " Yaani acha tu  mambo mengi mine yaani hadi kichwa nahisi kinaelekea kupasuka kwa kuzidiwa na haya majukumu" Josephine aliongea akikwepesha macho yasitazamane na Norbert.

                "Kawaida hayo ni majukumu pigana mtoto wa kike" Norbert aliongea.

                "akhaa! Yamezidi bora niolewe tu nipumzike" Josephine aliongea huku akiegemea gari ya Norbert.

                "Kakuambia nani kuolewa kuna kupumzika si ndiyo kuna kwata za saresare kabisa" Norbert aliongea huku akimkonyeza Josephine na kusababisha kicheko cha nguvu kimtoke Josephine.

                 "Afuu wewe una maneno kama nini" Josephine  huku akiwa bado anacheka.

                 "tuondoke basi" Norbert alimuambia Josphine ambaye alizunguka upande wa pili kwenye kiti cha pembeni ya dereva akafungua mlango akaingia, Norbert aliweka gia akaliingiza gari barabarani kisha akaelekea barabara ya Sokoine.

         Foleni kubwa ya magari waliikuta kwenye mzunguko maarufu wa magari unaoitwa Clock tower ambao mara nyingi huwa na foleni sana majira ya jioni kutokana na askari wa barabarani anayezuia magari katika makutano ya barabara ya Kariakoo gerezani, hiyo ilikuwa ni nafasi nyingine kwa Norbert kutimiza kile ambacho hakukitimiza zaidi tu ya kupewa ahadi na Josphine. Walikuwa wapo kwenye maongezi ya kawaida lakini urefu wa foleni hiyo ulimfanya Norbert abadili maongozi, ulikuwa ni muda  muafaka sana kwake ambao alikuwa akiungoja kwa hamu sana.

         Nafasi nyingine kwake ambayo hakupaswa kuitumia vibaya na ilimbidi aitumie vizuri ili aweze kupata kile alichokuwa anakihitaji, kwa macho yaie mawili alimtazama Josephine aliyekuwa akitazama nje kisha akanyanyua mkono na kiganja chake kikatua juu ya paja la Josephine.

        Mguso wa kiganja chake kwenye paja ulisababisha  Josephine ageuke kukitazama kiganja cha Norbert kisha akainua macho juu kumtazama Norbert, macho ya Josephinee yalikutana na macho ya Norbert ambayo yalikuwa ysmeshazungumza kitu ingawa kwake ilikuwa ngumu sana kukiri kuwa ameelewa lugha ya macho ya Norbert kutokana na kutotaka kuonekana mrahisi.

     Lugha ya macho ya Norbert ilipozidi kumsihi atoe maana Josephine aligeuka pembeni kutokana na aibu, alirudisha macho chini aliutazama mkono wa Norbert uliokuwa pajani kisha akashusha pumzi akamuangalia Norbert usoni akajiandaa kutamka neno.


*macho yameongea tayari

*mengine yanaleta ubishi kuelewa


TUKUTANE TENA ALHAMISI PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA





HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA  YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI