Sunday, November 27, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA KUMI NA NNE



RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________





    SEHEMU YA KUMI NA NNE!!

     Mfumo huo huwezi kuweka P ambayo ni parking bila kuivuka  R ambayo ni  reverse yaani gia ya kurudi nyuma, Norbert alipoona geti lililofunguluwa lipo usawa wake alirudisha gia kama anaipeleka parking na alivyofika R alifanya kitu ambacho Leopard Queen hakutarajia kama anaweka kukifanya kwa muda huo.

    Kwa kasi ya ajabu alikanyaga mafuta akaachia breki akarudisha gari nyuma kwa nguvu sana akamuacha Leopard Queen akipiga risasi zilizoishia kwenye kioo chake cha gari kisichoingia risasi, alienda kuigonga ile pikipiki matairi matatu akaitoa hadi nje kutoka pale getini ikarushwa umbali wa mita kadhaa kutoka geti liliopo na hapo akaweza kutoka nje ya geti hilo.


*****

      Alirudi nyuma kwa kasi sana  kisha akageuza gari kwa namna ya ajabu, aliweka gia ya kwenda mbele akatimua vumbi akimuacha Leopard akiwa ametoka nje ya geti akibaki haamini alichokifanya na hata kupiga risasi alishindwa kutokana na sauti ya bastola hiyo kuleta kizazaa katika eneo hilo. Hakuweza kuamini kama Norbert angeweza kumponyoka namna ile akiwa yupo usawa wa mdomo wa bastola yake, hasira zilimpanda zaidi Leopard Queen na alisonya kwa nguvu akaachia tusi zito sana.

     Aligeuka upande ilipo ile Toyo iliyoleta tanki hakumuona dereva wake na wala hakujua ni wapi alipo, pande zote zilizo katika usawa wa macho yake hakuweza kubaini unekano wowote wa dereva huyo aliyetumwa tenki la maji. Leopard Queen alichekecha akili yake kwa haraka sana kisha akapaza sauti, "Gasper!"

         "Madam" Gasper aliitikia kwa upesi sana.

         "ulikuwa wapi hadi huyu anatutoroka?" Leopard Queen aliuliza.

         "Madam niliweka silaha mbali halafu niliruka  pembeni,  angenigonga na mimi" Gasper alijieleza.

          "Ok! Ingiza hiyo Toyo ndani na umfuatilie huyu dereva upesi sana asije akaleta polisi hapa, tumeelewana?!" Leopard Queen aliongea kwa nguvu.

            "Madam" Gasper aliongea na kwa haraka sana akaiendea ile pikipiki, Leopard Queen aliingia mule ndani ya ghala akaketi jirani na  kibanda cha ulinzi bado akiwa haamini jinsi alivyotorokwa na Norbert.

    Alibaki akijiuliza Norbert ni nani kwani hakuwa amemtambua hadi muda huo kabisa, uwezo wa Norbert wa kufikiri kwa haraka ulimfanya ahisi hakuwa mwanadamu wa kawaida hata kidogo hasa kwa jinsi walivyomkosa kwa mara mbili tofauti akiwa yupo chini ya mikono yao. Alizidi kuwaza juu ya uhalisia wa Norbert lakini hakupata jibu hata kidogo, haikuwa kawaida kwa mwandishi wa habari wa kawaida akombolewe na mtu aliye na mbinu za kijasusi siku ile walivyomteka.

    Haikuwa kawaida kwa mwandishi asiye na ujuzi wowote wa kijeshi au wa kijasusi aonekane katika  katika hali ya kawaida wakati amewekewa bastola ubavu mwake, hamu ya kutaka kumjua Norbert ilipanda zaidi baada ya kukumbuka kitu kingine kilichomtia wasiwasi zaidi. Hapo wasiwasi wake dhidi ya Norbert ukamzidi na akajikuta anataka kufanya kitu ili wasiwasi huo umpungue, hakutaka kupoteza muda aliingia ndani ya chumba kidogo kilichopo ndani ya ghala hiyo akakaa kwa muda wa sekunde kadhaa na alipotoka alikuwa yupo katika muonekano mwingine kabisa wa kisura na hadi umbo.

    Alikuwa amebadili sura kuvaa nyingine ya bandia, aliporudi aliikuta ile pikipiki ikiwa tayari imeingizwa ndani na Gasper tayari alikuwa ameshatoka kwa mara nyingine. Alitabasamu kwa kufurahishwa na wepesi  wa Gasper kisha akaiendea ile pikipiki, alibaki akiitazama kila mahala hasa katika eneo la mbele lililokuwa limeharibika vibaya  baada ys kugongwa na gari ya Norbert.

     Hasira za kutorokwa kwa Norbert zilimpanda zaidi na alajikuta anaipiga teke pikipiki hiyo isiyo na hatia kabisa katika suala hilo, hakika alikuwa amechezewa akili kwa namna asiyopenda yeye kuchezewa akili na mtu ambaye hakumdhania kama angeweza kumfanyia hivyo. Alijiona kafanywa mjinga sana na Norbert kwa namna alivyomtoroka na hata akimueleza Panther yoyote kati yao atalaumiwa, alizidi kujilaumu  kwa kumuarisha Norbert asimamishe gari katika eneo ambalo lipo usawa wa geti la kuingia humo ndani ambalo limemfanya atoroke kwa urahisi sana.

      Lawama za nafsi yake zilizidi kumtafuna lakini zilishindwa kummeza baada ya kusikika mlio wa gari ya toyota landcruiser ikisimama mlangoni  hapo, vishindo vya watu wakishuka ndani ya gari hilo vilifuata  ambavyo vilfanya atazame kila upande kwenye eneo hilo la uzio wa ghala kisha akaenda kujibana baada ya kusikia vishindo vya watu vikikaribia  getini.


****


    Baada  ya kuwakimbia  wabaya wake Norbert alienda moja kwa moja Temeke nyumbani kwake ambapo aliingia ndani akabadili nguo, alijipamba kwa silaha za kijasusi zisizoonekana katika sehemu mbalimbali za mwili wake. Alikuwa yupo tayari kuingia kazini lakini utayari wake ulimezwa sauti ya simu yake ya mkononi ambayo iliita aliipokea baada ya kumbaini mpigaji, ilikuwa ni simu ambayo haipigwi pasipo kuwepo na dharura hata siku moja.

    Norbert aliipokea simu hiyo kutoka tawi la EASA ambapo ilimpa habari za kuhitajika ofisini hapo mara moja, Norbert hakutaka kupoteza muda aliamua kuingia ndani ya gari nyingine akaondoka kuelekea  huko alipohitajika.


     Nusu baadaye gari aina ya Toyota Noah ilionekana ikiegeshwa kwenye maegesho ya magari katika hoteli maarufu iliyopo Ilala mtaa wa Lindi, mlango wa dereva  wa gari hilo ulionekana ukifunguliwa na Norbert alionekana akishuka. Alikuwa amefika kwenye jengo la hoteli ambalo ni makao ya siri ya shirika la kijasusi la Afrika ya mashariki(EASA), aliingia ndani ya eneo la mapokezi la hoteli hiyo akiwa kama mtumiaji hoteli hiyo. Kituo cha kwanza kukifikia ilikuwa ni mapokezi ambapo alikuta wasichana watatu warembo wakiwa wamekaa katika dawati la mapokezi,  Norbert aliwafuata wasichana hao wakiwa na tabasamu kubwa ambapo nao walipomuona walitabasamu pia.

           "Kijogoo naona leo umetukumbuka" Msichana aliyepo katikati ya wenzake wote alimuambia

            "Siyo nimewakumbuka Hidaya sema ninawakumbuka nitaendelea kuwakumbuka wake zangu" Norbert aliongea huku akitabasamu.

               "Loh! Huna haya nani mke wako wewe" Msichana aliyekuwa yupo pembeni ya Hidaya kwa upande wa kushoto alidakia na kusababisha Hidaya acheke kwa nguvu, wote kwa pamoja walicheka kicheko cha kike wakagonganisha mikono yao.

              "Basi poa kama sina wake ngoja nikaonane na meneja   kuhusu mkataba mpya wa matangazo ya hoteli, haya warembo nikitoka nitatafuta mke mwingine" Norbert alipngea huku akianza kuondoka na kusababisha Hidaya amzuie.

              "Nor bwana na wewe hutaniwi" Hidaya aliongea kwa kudeka lakini Norbert alimtoa mkono baada  ya simu yake kuanza kutetemeka mfukoni mwake.

             "Tutaongea nikirudi wacha kwanza nikaongee kuhusu mkatsba" Norbert alimuambia kisha akapiga hatua kuifuata lifti ya ghorofa hiyo ambayo ilikuwa imejitenga peke yake, aliingia ndani ya lifti akiwaacha wasichana hao ambao walijua alikuwa anaenda kuonana na Meneja wa hoteli.

    Haikuwa hivyo bali alikuwa  anaenda ofisini  ambapo alihitajika na mkuu wa kazi, wafanyakazi wote wa hoteli hiyo hawakuwa wakifahamu juu  ya uwepo wa  makao madogo ya EASA  ndani ya jengo hilo zaidi ya meneja wa hoteli hiyo ambaye ndiye mkuu wa kazi wa Norbert. Kuonekana kwa Norbert eneo hilo ilikuwa kunatambulika kama yupo kwa kuonana na Meneja wa hoteli  hiyo kwani alikuwa akionekana kwa mara chache sana, siri ya ofisi hiyo ilikuwa ipo miongoni mwa watu wachache sana wenye kuaminika ambao waliweza kuitunza siri hiyo.

     Norbert alipoingia ndani ya lifti hiyo alibonyeza sehemu ambayo haijulikani kama kulikuwa kuna kitufe cha kubonyeza, lifti hiyo ilianza kushuka chini taratibu kwa kiasi cha urefu wa ghorofa mbili kisha ikafunguka baada ya kufika eneo husika. Norbert alitoka ndani ya lifti hiyo akatokea sehemu yenye korido ndefu ambayo ilimpeleka hadi kwenye mlango  ambao unafunguliwa kwa kuweka alama za kiganja, aliweka kiganja chske sehemu hiyo na taa ya rangi ya kijani iliyopo juu ya mlango ikawaka mara moja kisha ikazima.

              "Karibu N001" Sauti maalum ya kutengenezwa  kwa mitambo ilisikika kisha mlango huo ukajifungua, Norbett aliingia ndani na mlango ukajifunga tena.


    Alitokea katika eneo lenye vyumba vingi vya ofisi kukiwa na watu tofauti wakifanya kazi humo, Norbert alizipita ofisi hizo akaenda kwenye mlango ulioandikwa CE ambao ulikuwa wa kitasa cha kawaida. Aliufungua mlango huo akaingia akapita moja hadi katika ofisi ya Katibu Mukhtasi, hapo alimkuta Norene akiwa yupo makini na kioo cha tarakilishi.

          "Mama watoto nimekuja" Norbert alimuambia Norene ambaye hakujibu chochote zaidi ya kumuonesha upande ilipo kamera ya ulinzi iliyounganishws na ofisi ya CE ambaye anaona kila kitu kinachofanyika hapo.

           "Vipi mbona nimeitwa ghafla tu?" Norbert alimuuliza.

           "Hilo la kukueleza sina mamlaka nalo nenda kwa mkuu mwenyewe, anakusubiria kwa hamu sana" Norene alimuambia Norbert ambaye aliishia kujishika kiuno chake kisha akahema kwa nguvu  sana, hakutaka kupoteza muda aliamua kuingia ofisini kwa CE kwani alikuwa ameshajulikana uwepo wake ofisini hapo.

     Ndani ya ofisi ya CE alimkuta akiwa amekati kwenye kiti chake akiwa na faili kubwa mezani, alitoa salamu kisha akaketi kwenye kiti baada ya kuamriwa afanye hivyo na CE ambaye alionekana na jambo lililomfanya amuite hapo.

          "N001" CE aliita kisha akampatia picha Norbert kisha akaendelea, "Jack Shaw ndiyo jina lake huyo kiongozi wa genge hatari la ualifu kutoka Ujerumani.  Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika ofisi hii huyu mtu  anaingia Tanzania saa tisa alasiri leo hii katika ndege  ya shirika la Qatar ambayo atakuja nayo Askofu Achim Valdermar kutoka kanisa kuu la kiluteri akija kuhudhuria maziko ya Askofu Edson yatakayofanyika mapema kesho. Ujio wa mtu hatari kama yule kutoka taifa la mbali huenda upo kwa namna au anataka kufanya jambo baya, mtu huyu ameonekana uwanja wa ndege wa Cairo lakini amepotea katika mazingira ya kutatanisha. Kwa mujibu wa taarifa za wazi ni kwamba mtu huyo anataka kuazimia jambo baya kwa Askofu Valdermar akiwa huku ndani ya Tanzania kuja kuhudhuria mazishi ya rafiki yake kipenzi, N001 nataka uwaoneshe Tanzania siyo uwanja wa kufanya uhalifu. Hakikisha Askofu Valdermar anaingia salama na anaondoka salama bila mtu yoyote kutambua kama wewe upo kwa ajili ya kazi hiyo, huyu mhalifu akikamatwa nafikiri wengine wenye akili kama zake watakuwa wamepata ujumbe kwamba EASA wapo makini kuilinda Afrika ya mashariki. Tumeelewana".

          "Mkuu, ila samahani nina ombi moja" Norbert aliongea kwa utaratibu kisha akaendelea baada ya CE kumruhusu aongee, "Ndani ya wiki hii kumetokea vifo  viwili vya viongozi wa dini pamoja na General Kulika wote  wakifa kwa namna moja kwa sumu ya Quantanise ambayo hadi sasa imemtia doa Gawaza ambaye ni mmoja wetu, uchunguzi binafsi wa jambo hilo nimefikia hatua nzuri katika kuzifikia nyayo za muhusika. Ujio wa kazi mpya utazorotesha ya zamani, hivyo ninaomba nizifanye zote kwa pamoja".

          "Kwanza nikupongeze kwa kuamua kujitosa kwenye uchunguzi bila ridhaa ya ofisi  ingawa taarifa tayari zipo kwa ajili ya kufanikisha usalama wa nchi, upo huru kuendelea ila sitaki viza na kama unajua moja itaviza acha moja tumteue N002 ambaye yupo ana kazi ndogo tu" CE aliongea.

          "Tarajia mazuri kutoka kwangu" Norbert aliongea.

           "Ok unaweza ukaenda   hakikisha Askofu Valdermar aje na aondoke salama na pia wahalifu wakamatwe, sitaki ubaki kwa mkeo asiye rasmi Norene sasa hivi uwahi uwanja wa ndege tena umwambie Gawaza asionekane katika public areas hadi kazi ikamilike" CE alitoa amri, Norbert alinyanyuka kwenye kiti akatoa heshima akaondoka.





   SAA TISA ALASIRI

UWANJA WA NDEGE WA NDEGE WA MWALIMU JULIUS NYERERE


     Ndege kubwa ya shirika la ndege la Qatar aina ya Airbus 330-300  ilionekana ikishuka kwa mwendo wa kasi katika ardhi ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, matairi yake yalipogusa ardhi ilianza kukimbia na hatimaye ikasimama kwenye  eneo maalum la kusimama kwa ndege. Ulinzi katika uwanja huo wa ndege ulikuwa umeongezwa mara dufu kutokana  na ujio wa Askofu Valdermar,  mapokezi yake yaliongozwa na wakuu mbalimbali wa kanisa la Kiluteri Tanzania pamoja na  makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

     Mtu mwenye asili ya kizungu aliyevalia nguo ndefu nyeupe yenye ukosi mnene na kikoti kirefu cha kahawia alionekana akitoka ndani ya ndege hiyo huku akipunga mkono, wapokezi wake kutoka srrikalini pamoja na kanisa la kiluteri walipiga makofi kumkaribisha. Askofu Valdermar  ndiyo alionekana mbele ya wageni wake waliokuwa wakimsubiri awasili hapo, alishuka taratibu kwenye ngazi za  ndege hiyo na alipofika chini akaanza kusalimiana na viongozi mbalimbali wa kidini na wa kitaifa waliojitokeza katika mapokezi hayo ya kiongozi huyo mkubwa wa dini kutoka Hamburg Ujerumani.

     Ulinzi katika uwanja huo uliimarishwa zaidi  kwa kutumia ulinzi wa kudhihirika na macho ya watu na usiodhihirika na macho ya watu wa kawaida isipokuwa wenye ujuzi wa hali ya juu, ulinzi usiodhihirika na macho ya kawaida ulikuwa ukiwakilishwa na Norbert akiwa yupo katika muonekano tofauti kuanzia sura hadi mavazi.

     Hakuwa tofauti kimavazi na wawakilishi wa kanisa la KKKT ambao walikuja kumpokea Askofu Valdermar, msafara wa Askofu Valdermar hadi unaondoka uwanjani hapo Norbert alikuwa tayari amekuwa karibu na askofu huyo hadi kufikia kuwa katika msafara huo. Hakuna aliyekuwa amejua kwamba ndani ya msafara huo kulikuwepo majasusi wawili hatari wenye itikadi tofauti  kutoka ardhi tofauti, mmoja tayari alikuwa ameshatambulika na kalamu ya mwandishi kuwa ni Norbert aliyevaa sura ya bandia pasipokutambulika na waliomo ndani ya msafara huo.

     Jasusi mwingine ambaye tayari alikuwa ameingia kwenye msafara huo hakuwa ametambulika, msafara huo uliishia katika hoteli ya Kilimanjaro iliyopo kata ya Magogoni ambapo askofu huyo ilihitajika apumzike kabla hajajianda kuongoza ibada ya kuuaga mwili wa Askofu Edson siku inayofuata. Ulinzi katika hoteli hiyo nao uliimarika maradufu na bahati nyingine ikamuangukia Norbert ambaye aliteuliwa kuwa mtu wa karibu atakeyekuwa na Askofu Valdermar katika kipindi chote hadi anaondoka nchini, Askofu Valdermar alivutiwa sana na Norbert hadi akapenda kuwa naye karibu, hakika hakutambua kabisa kwamba alikuwa anatimiza malengo ya Norbert zaidi ya kujali yeye kutimiza malengo yake aliyoyajua mwenyewe tangu anamuona Norbert kwa mara ya kwanza pale uwanja wa ndege akiwa yupo katika kundi la watumushi wa Mungu waliokuja kumpokea.

     Majira ya saa kumi hadi  saa kumi na mbili hoteli hiyo ilikuwa ikiingia viongozi mbalimbali wa kikanisa na wa kitaifa waliokuwa wamekuja kumsalimia kiongozi huyo, Norbert alikuwa ameteuliwa kukaa pembeni ya Askofu  Valdermar akiwa yupo sambamba na watu wawili waliovaa mavazi ya watumishi ambao walifika pamoja na Askofu Valdermar. Majira ya jioni kwenye machweo ya jua Askofu Valdermar aliaga kwenda kupumzika chumbani kwake hotelini humo, Norbert hakuwa mbali  alikuwa akilala chumba cha pembeni yake huku akiwa makini katika kulinda usalama wa Askofu huyo. Alikuwa akikaa makini kila muda katika kuhakikusha kuwa Askofu huyo havamiwi, muda mwingine ilimbidi atembee kwenye korido inayotenganisha vyumba ili kuhakikisha usalama wa kiongozi huyo mkubwa wa kiroho unakuwepo.

     Majira ya saa mbili usiku baada ya kiongozi huyo wa kiroho kupata  chakula, alirudi chumbani kwake kupumzika kusubiria siku mpya ianze. Mapumziko hayo yalimfanya Norbert abaini uwepo wa kitu kingine kilichokuwa kimejificha nyuma ya pazi, ni muda ambao aligongewa mlango wa chumba chake na alipofungua akakutana na mmoja wa watumishi aliyekuja nao Askofu

              "You are needed(Unahitajika)" Alimuambia kisha akaondoka, Norbert naye alitoka akaingia katika chumba cha Askofu Valdermar akamkuta akiwa amekaa kwenye kochi akiwa amevua mavazi aliyokuja nayo.

              "Sit down(sit down)" Askofu Valdermar alimuambia huku akitabasamu akimuonedha Norbert mahali pa kuketi karibu na yeye, Norbert aliketi kwa heshima huku akiwa amekaa kwa umakini kusikiliza wito alioitiwa.

               "My son I need your help in this foreign country (Mwanangu nahitaji msaada katika nchi hii ngeni)" Askofu Valdermar aliongea huku akimtazama Norbert usoni.

               "Yes father(ndiyo baba)" Norbert alimuitikia kwa heshima akiwa yupo tayari kuusikiliza wito ws Askofu Valdermar.

              "There is another son like you in the car parking, I received his email(Kuna mwana mwingine kama wewe katika maegesho ya magari, nimepokea baruapepe yake)  Askofu Valdermar aliongea kisha akamtazama Norbert kwa umakini sana, alishusha pumzi kisha akaendelea "Go and take him  secretly, I need to see him. You will find him  in black BMW (nenda ukamchukue kwa siri, nahitaji kumuona. Utampata kwenye BMW nyeusi )".

             "Ok father(sawa baba)" Norbert aliitikia kisha akanyanyuka kiheshima akatoka humo ndani, alienda hadi nje ya hoteli hiyo kwenye maegesho ya magari.

     Haikumuwia vigumu kulipata gari alilokuwa analitafuta ambalo lilikuwa lipi katikati ya gari mbili za kifahari, Norbert aliifuata ile gari ambayo ilikuwa na vioo vya giza na alipofika aligonga katika upande wa dereva. Kioo cha gari hiyo kilishushwa taratibu na mtu aliyekuwa anahitajika amfuate alimuona na hapo moyo wote ukapiga sarakasi ya kificho kwa kumuona mtu huyo ambaye hakutarajia kama ndiye huyo aliyekuja kumfuata, alikuwa ni mtu ambaye hakuwa mgeni ambaye alimuona mara chache tu ndani  ya siku moja. Hakuwa amemsahau mtu huyo ambaye alikuwa amemuona ndani ya siku moja tu ambayo ilitosha ubongo wake kumkariri, mtu huyo alishuka ndani ya gari huku akiwa na tabasamu tele akasalimiana naye.

    Alikuwa yupo katika vazi la suruali ya kitambaa  kigumu cha rangi ya kahawia na fulana ya mikono mifupi iliyofanya mkono wake kulia uonekane na kovu la mshono ambao ulizidi kuiamsha akili ya Norbert. Mtu huyo hakumtambua Norbert kutokana na sura ya plastiki aliyokuwa amevaa wala hakutambua kwamba alikuwa ametambulika vizuri na Norbert, alionekana kuwa na uchangamfu kwa Norbert ambaye alimuongoza moja kwa moja hadi ndani kwenye chumba cha Askofu Valdermar akatoka akarudi chumbani kwake baada ya kukamilisha kazi yake sasa akabaki akimfikuria yule mtu ambaye alianza kumuhisi ni mhusika nambari moja wa kifo cha Jenerali Kulika kwani alama aliyokuwa nayo  mkononi ndiyo alama ambaye mtoto mkubwa wa kike wa Jenerali Kulika aliiona kwa muuaji aliyezima taa chumbani kwake akamfungia kwa nje.

     Uhakika zaidi juu ya mtu huyo ulianza kujengeka taratibu katika fikra  zake baada ya kumkumbuka mhusika huyo alikuwa amevaa shati la mikono mirefu kwemye msiba wa Jenerali Kulika  ambalo lilificha alama hiyo, hakika aliona  mhusika mkuu wa tukio hilo tayari alikuwa amempata ilikuwa bado kumtafuta mhusika wa pili mwenye mchoro wa Kipepeo mkononi ambaye hakumjua hadi muda huo.

    Alianza kumfikiria juu ya mhusika huyo na akajikuta akikataa kwa nafsi kwamba uwepo wa wauaji wawili siyo, alifikiria namna ya kutoa funguo kwa mkono ambao mgongo wa kiganja utaonekana katika chumba cha Jenerali Kulika na pia katika chumba cha watoto. Jawabu alilolipata  ni kwamba mkono uliotumika kutoa funguo na kumfungia mke wa Jenerali Kulika ulikuwa wa kushoto, mkono uliotoka funguo chumbani kwa watoto wa Jenerali Kulika ulikuwa wa kulia hivyo alijua kabisa muuaji alikuwa mmoja aliyetumia mikono yake yote katika muda tofauti kufanya hayo.

           "Vyumba vilivyopo mkabala haiwezekani kutoa funguo kwa ndani kwa sawasawa kwa kila chumba mgongo wa kiganja kuonekana, natakiwa niangalie mkono wake wa kushoto kama una mchoro nilioambiwa" Norbert aliwaza akiwa amejilaza chali kitandani na mavazi ya kiroho aliyokuwa nayo, ushindi wa kile alichokuwa akikitafuta tangu awali alianza kuuona ukimjia waziwazi.

           "Benson you are the Killer(Benson wewe ni muuaji)" Alijisemea moyoni mwake kisha akakumbuka kutafuta simu yake ilipo kutokana na uhitaji aliokuwa nao katika hiyo simu.


****


    Wakati Norbert akiwa yupo anawaza juu ya upelelezi wake, upande mwingine nyumbani kwa Mfanyabiashara mkubwa nchini Wilson Ole mkutano ulikuwa umeitishwa mara moja baada ya taarifa ya kutoroka kwa Norbert kuwafikia kutoka kwa Leopard Queen aliyekuwa amemtia nguvuni. Panther aliyekuwa hajui kingereza ambaye alikuwa yupo eneo hilo akimuwakilisha mwenzake alikuwa amekasirika sana, Wilson Ole alibaki akifarijika kwa ujanja aliofikia Leopard Queen wa kuweza kumuwekea silaha Norbert.

    Wilson Ole mdogo wa aliyekuwa rais wa Tanzania Filbert Ole tayari alikuwa ameshaibaini kazi halisi ya Norbert baada ya kupata uhalisia kutoka kwa  Jackline mwanausalama aliyetiwa mikononi na Allison secret service wa EASA kutoka Burundi baada ya kutaka kumuua Koplo Daniel Uyomo katika kisa cha JINAMIZI, asubuhi ya siku hiyo Wilson Ole alimtembelea mwanausalama huyo ambaye kwa sasa ni mfungwa katika gereza la Segerea na hapo ndipo alipobaini ukweli.

    Lawama za kushindwa  kumtia nguvuni Norbert ziliangushwa kwa Leopard Queen na muda wote huo Wilson alikuwa amenyamaza, walipomaliza kumlaumu ndipo na yeye alianza kueleza.
"Jamani hatuna haja ya kumlaumu Leopard Queen kajitahidi sana awezavyo kumkamata mtu kama Norbert" Wilson aliongea huku akiwatazama kila mmoja.

            "Hapana ni uzembe aliyoufanya" Kamishna aliongea.

           "Hapana nafikiri nyinyi hamuijui rangi halisi  ya Kaila mimi nimepata kuijua nilupomtembelea Jackline yule akiyekuwa TISS kipindi marehemu Kitoza akiwa ni mkurugenzi, huyu amenieleza rangi halisi ya Kaila" Wilson aliongea kisha akawatazama wenzake ambao walijaa shauku ya kutaka kumjua Norbert kiundani, aliendelea kusema, "Kaila ni mpelelezi hatari tena mwenye uwezo wa hali ya juu wa EASA si mwandishi wa habari mjanja kama mnavyofikiria na mkae mkijua tunapambana na EASA".

           "Shit! Leopard Queen you have to be careful(Shit! Leopard Queen unatakiwa uwe mwangalifu)" Panther aliongea.

            "Hivyo basi huyo ndiyo Kaila na tukienda vibaya kwake tumeumia  hata mabosi hawatatuelewa si umesikia wote wapo ndani ya nchi hii Don kaingia jana na mke wake kaingia leo" Wilson aliongea.

            "Nauona ugumu wa kazi ila sitakubali mpaka nilipe kisasi kwa Kaila ndiyo furaha yangu" Kamishna aliongea kwa uchungu.

            "Kamishna cool down najua kama Kaila ndiyo kamuua Kitoza aliyekuwa  binamu yako, ila usiweke hasira mbele kumbuka tumepewa kazi hii kutoka kwa Don  na ikiharibika hii kazi pia Sir Shaw hatatuelewa" Wilson aliongea kisha akamtazama Panther akamuambia, "Kaila atauliwa na Leopard Queen kwa kumtegea ugonjwa wake tu, yeye si mpenda  mabinti sasa binti ndiye atakayemuua".


TUKUTANE JUMATATU PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA


HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI










No comments:

Post a Comment