Sunday, November 20, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA SABA


                                          


 RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA



SEHEMU YA SABA!!
      "Brother kumbuka samaki hutegwa kwa chambo wala hawezi kutegwa kwa ulimbo, so we have the trap. Leopard Queen atakuambia vizuri, Panther wa pili aliongea kisha akawatazama Leopards waliobaki ambaye mmoja  alikuwa ni mwanamke mrembo sana akiwa amesimama kikakamavu 
akamuambia,"Leopard Queen unaweza ukatuambia ndoano ipo tayari maana samaki yupo karibu sana na chambo asije akala chambo wakati ndoano hamna".

     "Ndoano ipo tayari kilichobaki ni kumnasa tu samaki aliyeifuata chambo akitaka kuila tu akijua ndoano hamna" Leopard Queen aliongea na kuwafanya Panthers watabasamu wakiona hawakuwa na haja ya kutia nguvu zaidi. Hawakuwa na zaidi katika mpango huo na kilichobaki ni kuendelea na kazi ile iliyowafanya  wapate ulaji wa awali, hasira zao za kuchezewa akili ziliisha papo baada ya kuhakikishiwa mpango namba mbili ulikuwa ukifanya kazi.


****

       Norene baada ya kumkomboa Norbert alitumia usafiri wake kutoweka eneo hilo kwa kasi sana, alienda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Norbert akiwa hana amani ndani ya moyo wake kutokana na hali ya Norbert ilivyokuwa mbaya sana. Alifika nyumbani akiwa salama pasipo kufuatiliwa   na mtu yoyote akamuingiza Norbert ndani ya nyumba akaanza kumpa huduma ya kwanza kutokana na maumivu aliyoyapata baada ya kunusurika kupasuliwa na magreda ya kubebea mizigo.

      Baada ya kumuhudumia hadi akamaliza ndipo Norene alipokumbuka kwa  mara nyingine kumpigia simu Moses kwa mara nyingine baada ya  simu yake kutopokelewa kwa mara ya kwanza alipompigia, mara ya pili simu ilipokelewa na Moses mwenyewe na Norene akampa taarifa juu ya hali ya Norbert na kilichompata. Taarifa hiyo ilizimwa na taarifa nyingine kutoka kwa Moses ambayo ilikuwa ni zaidi ya hiyo taarifa aliyoipata, taarifa hiyo ilimfanya Norene aropoke kwa fadhaa sana kutokana na uzito wa taarifa yenyewe ambayo haikuwa ya kawaida kwa Moses.

              "sasa sikia wewe upo wapi sasa hizi?......ok njoo Temeke kwa Nor  kama umefanikiwa kuwapumbaza kabisa" Norene alimuambia Mosea akionekana kuwa na wahka sana kwani mambo yalikuwa  yameanza kuwa mabaya kwa upande wao, alipoikata  simu yake ya mkononi aligeuza shingo kumtazama Norbert ambaye alikuwa amezama kwa usingizi mzito muda huo. Norene alimshukuru Mungu sana kwakuweza kufanikisha kumkomboa Norbert, alinyanyua mikono yake pamoja na uso wake juu kama  anaomba dua kisha akafanya alama msalaba.

     Aliachia tabasamu hafifu akamsogelea Norbert pale alipolala akambusu kwnye paji la uso kwa upendo mkubwa sana halafu akatoka akaelekea sebuleni ili akamsubiri Moses

     Baada ya nusu saa Moses alifika nyumbani hapo akiwa anatumia pikipiki, aliiingia ndani akamkuta Norene akiwa amekaa sebuleni akiwa ameshika tamaa la kuvuta fikra akionekana anawaza kitu kingine cha kufanya. Aliketi kwenye kochi kisha akamtazama Norene kwa muda mfupi akaachia tabasamu hafifu sana lililotoka sambamba na kushusha pumzi mithili ya mtu aliyepata faraja hafifu.

           "Mchana au usiku upande wenu?" Moses aliuliza

           "naona ni alasiri sijui kwako" Norene alijibu kwa kimafumbo kama swali lilivyoulizwa na Moses, mchana uliokuwa unamaanishwa ni mambo yapo vizuri na usiku uliokuwa unamanishwa ni mambo yameharibika. Alipojibu alasiri alimaanisha yanaelekea kuwa mabaya kabisa.

           "kwangu yalikuwa jioni ikielekea usiku ila nimepata nusu ya ghafla imekuwa alasiri, vipi jamaa huko wamemkaliaje?" Moses aliongea huku akitabasamu.

            "we acha tu yaani tena ni watu wanaojua kazi zao waliomfanyia hivyo, vipi wewe imekuaje" Norene aliongea kisha akamuuliza Moses.

            "Dah! Nafikiri mizimu ya babu zangu iliniotesha niwe makini nyumbani kwangu maana special force imeingia na sijui aliiagiza nani maana hata IGP Chulanga amekana hakuagiza kikosi" Moses aliongea  halafu akasikitika akaendelea, "yaani nimetumia ujanja wa panya kuwakwepa wale".

           "Ila ujanja wa Panya mbaya ikiwa utakutakana na mwenye ujanja wa paka" Norene alisema huku akitabasamu halafu akanyanyuka kwenye kochi akaenda kwenye jokofu akachukua chupa moja ya mvinyo usio na kilevi, akauweka kwenye meza ya inayotumika kula chakula ambayo ipo jirani na jokofu, alienda kwenye kabati la vyombo akarudi na bilauri mbili ambazo alizimimininia mvinyo halafu akarudi sebuleni akiwa amebeba bilauri hizo.

            "Kidume mwenzio kapewa kifinyo kidogo na hao Cats kalala" Norene aliongea huku akimpa Mosea bilauri ya mvinyo, Moses aliipokea bilauri hiyo na hakuinywa na badala yake alimnyooshea  Norene ambaye alisogeza mdomo wake akapiga funda  moja akaachia tabasamu.

            "uaminifu hakuna kwa yoyote" Moses alisema huku akitabasamu baada ya Norene kuonja mvinyo aliomletea.

            "ni sehemu ya kazi yetu" Norene alisema kisha akaketi kwenye kochi kisha akaendelea kunena, "special forces huwa wanapewa mamlaka na  IGP na makamishna na huwa hawaonekani kwa sababu ndogondogo isipokuwa kwa sababu maalum sasa tambua hao kuna kamishna mmojawapo ndiyo katoa mamlaka".

            "Hiyo fact kabisa, sasa suala kujiuliza ni wamepewa mamlaka kwa lengo gani?" Moses aliongea

            "huenda ile sumu imekuwa matatani" Norene alikisia.

            "hiyo sababu nafikiri hawa watu walitaka kuniangamiza mimi wakanikosa au walitaka kumtia nguvuni mke wangu vilevile. Kosa nimempa sumu mwenye kushawishi umuamini kumbe hafai kumuamini, bishop Edson ndiyo chanzo"  Moses aliongea.

           "ni vyema kwa kulitambua hilo" Sauti ya Norbert ilisikika ikitokea kwenye korido ndefu inayotenganisha vyumba, Norene na Moses walipotazama upande huo walimuona Norbert akija kwa kujikongoja huku akiwa ameachia tabasamu usoni mwake.

      Norene aliweka bilauri ya mvinyo haraka akamkimbilia Norbert ili amsaidie katika kutembea lakini Norbert alimzuia na akajikongoja hadi sebuleni akakaa kwenye kochi lililopo mkabala na kochi alilokaa Moses.

           "Naona dogo umeanza wizi yaani unakaa unaongea na mali za watu wakati wenyewe tupo vyumbani" Norbert alitumbukiza utani huku akitabasamu na kusababisha wote wacheke.

            "akaa babu wee hujanimiliki mpaka uniite mali yako" Norene alibatilisha maneno ya Norbert.

            "Alaaa sasa naenda kumiliki nyingine kama ndiyo hivyo" Norbert aliongea akionesha kususa baada ya kusikia hayo maneno ya Norene, maneno hayo yalimfanya Norene anyanyuke sehemu aliyokaa aje kukaa pembeni ya Norbert akionesha hajafurahishwa na maneno hayo na alianza kudeka.

            "Loh! Kumbe unakashifu zimamoto na nyumba inaungua muone vile" Moses alimuumbua Norene baada ya kubatilisha maneno ya Norbert ilihali hajiwezi katika penzi.

           "Haya tuachaneni na hayo, Mose kule ofisini kwangu kwenye basement yenye emergence exit nimemuhifadhi kunguru mmoja aliyetumwa kuja kuniua mimi kipanga!" Norbert alimuambia  Moses kisha akameza mate kidogo akaendelea, "inabidi ukamchukue upitie mlango wa nyuma na umlete hapa yeye ndiyo atakayetuambia kuhusu wenzake nafikiri umenipata".

     Moses alitikisa kichwa kuashiria amekubali kisha akanyanyuka kwa haraka ili akatekeleze kazi aliyopewa, alionekana ni mwenye papara na Norbert alimzuia kwa papara hizo ili asije akaingia kichwakichwa.

           "Hey siyo ngumi zako na marehemu Andrew Kabaita unazoenda kuzifuata, jiandae wewe" Norbert alimuambia Moses ambaye alisitisha kuondoka  kisha akauliza, "mapambo yapo ya kujiandaa?"

            "Kila kitu wewe nenda ukajipambe kwanza" Norbert alimjibu, Moses alipojibiwa hivyo aliifuata korido ndefu iliyompeleka hadi  kwenye mlango wa chumba ambacho kilikuwa hakitumiki kabisa.

    Alifungua mlango wa chumba hicho akaingia akaenda hadi lilipo kabati la nguo nalo akalifunga ajakutana na mlango mwingine, aliufungua mlango huo akakutana na ngazi ambazo alizifuata akashuka hadi chini akatokea sehemu yenye silaha za kila aina za kijasusi na za wanausalama wa kawaida.

    Hakika alikuwa ameingia kwenye chumba chenye mapambo ambayo ndiyo hayo yalikuwa yanazungumziwa na Norbert, alikuwa akimaanisha silaha za kijasusi na hakutaka kuongea kwa uwazi kwani hakuwa na imani na eneo lolote alilopo hata iwe ndani ya nyumba yake. Lugha hiyo ilikuwa ikieleweka kwa wapelelezi wenzake lakini si kwa mtu wa kawaida na ilikuwa ikitumiwa kuficha mtu memwingine yeyote atakayekuwa anasikiliza asijue wanamaanisha nini, ilikuwa ni bora mpango ujulikane kuliko kujulika eneo la siri la silaha ndiyo maana hawakuwa tayari kutoa taarifa za wazi ili wamchanganye mtu.

    Moses alipomaliza kujiandaa alitoka humo ndani akiwa amevaa mavazi ya aina nyingine na viatu vya  aina nyingine pamoja na kofia aina ya hat nyeusi, urembo wote unaozungumziwa na Norbert tayari  ulikuwa ndani ya mwili wake kwa ajili ya usalama.


****


     SINZA

    Majira ya saa tano za usiku ndiyo muda aliokuwa anatoka Moses nyumbani kwa Norbert ambao kwa upande wa pili ulikuwa ni muda wa kulala kwa walio na uchovu wa kutwa nzima, ilikuwa ni ndani ya mtaa wa Megasiti maeneo ya Sinza katika nyumba ambayo ilikuwa kubwa na ya kifahari ambayo ilitambulika kama nyumba ya mkuu wa majeshi ya anga na nchi kavu nchini Tanzania. Utulivu ndani ya nyumba hiyo ulikuwa upo kama ulivyozoeleka kutokana na kuheshimika sana mwenye nyumba hiyo ambaye anaogopeka sana kutokana na cheo alichonacho halafu yupo katika umri mdogo sana, hakuna mkazi wa Sinza asiyemjua Meja jenerali huyu ambaye amesaidia katika kuufanya mtaa unaoishi uwe na utulivu kupitiliza.

     Nyumba hiyo yenye utulivu iliingiwa na dosari ambayo iliufanya utulivu wake uwe katika hali tata baada ya ugeni usio rasmi kuingia katika nyumba hiyo namna isiyo rasmi, ugeni huu wa usiku wenye mambo yanayofanana na rangi ya usiku uliingia katika namna isiyokuwa ya kawaida.
Lilikuwa ni kundi la watu sita wenye mavazi meusi yaliyoandikwa SPECISL FORCE ndiyo lilikuwa limeizuru nyumba ya Meja Jenerali wakiwa na bunduki aina ya UZI zenye kiwambo cha kuzuia pamoja na silaha mbalimbali za hatari, ujio wao ulitanguliwa na umwagaji wa hewa ya sumu iliyowalaza walinzi kisha wote kwa pamoja wakauruka uzio wa nyumba hiyo kwa utaalamu wa juu.

     Waliingia kwa kupitia mlango wa nyuma wa nyumba hiyo huku wakinekana kuitambua vilivyo nyumba hiyo kwani wote walielekea kwenye mlango wa chumba kimoja, walifungua mlango wa chumba hicho wakaingia ndani wakakuta kitanda ambacho kilikuwa kimebeba umbile la mtu aliyeonekana amelala kwenye kitanda chake akiwa hana hili wala lile. Watu hao walielekeza silaha  zao alipolala huyo mtu, kisha wakamsogelea aliyelala kitandani hapo wakamzunguka kwa ukaribu.
Mmojawao alishusha silaha yake kisha akatoa sindano yenye kimiminika chekundu, aliitoa sindano hiyo kifuniko chake akachoma sehemu ya begani kwa nguvu. Alipotaka kuingiza dawa iliyokuwa kwenye bomba la sindano umeme wa nyumba nzima ulizimika kwa ghafla na kukawa na giza, taa za nje zilizowapa mwangaza watu hao wa kuona ndani sasa ziliwanyima uhuru wote wa kuona vizuri.

    Umeme wa humo ndani uliwaka na hadi taa ya humo chumbani iliyokuwa imezimwa iliwaka na hapo kile kikosi kilishangaa kuona walikuwa wameizunguka mito iliwekwa kama mtu kitandani, walibaki wakiwa wameduwaa na hata kabla hawajazinduka kwenye mshangao wao umeme ukazimika tena kisha sauti ya kila mmoja akitoa maumivu ikasikika. Ulipokuja kuwaka kwa mara nyingine kila mmoja alikuwa akishikilia kiganja chake kinachovuja damu  kwa maumivu huku silaha zao zikiwa chini, walipotaka kuinama waziokote walishindwa papo hapo kwani walikuwa wameshawahiwa tayari.

          "inamisha mgongo tu nimwage ubongo wako" Ilisikika sauti ya kike ikitoka ndani ya kabati  huku mkono wenye bastola yenye kiwambo cha kuzuia ikitoka ndani ya kabati, walipoangalia upande inapotoka sauti walimuona Meja Jenerali Belinda aliwa na mavazi ya kulalia yaliyo katika mfumo wa suruali na shati refu mithili ya nusu kanzu akiwa kawanyooshea bunduki.

           "nani kawatuma? , sirudii swali mara mbili" Meja Jenerali Belinda aliuliza, swali hilo liliwafanya wote wanyamaze wakawa wanababaika. M.J Belinda hakuuliza  lile swali tena na badala yake alimtandika mmoja risasi ya goti akatoa ukelele wa maumivu akawa anataka kukaa chini.

           "Weee! Kimya mbona hukupiga kelele wakati unaingia, tena hakuna kukaa simama hivyo hivyo na goti lako" M.J Belinda aliongea kwa sauti ya chini ya ukali baada ya mpinzani wake, mwingine alipuuza agizo la M.J Belinda akainama kwa upesi akijua ataiwahi silaha yake. Alitumia wepesi wake wa kimazoezi katika kuinama akajua ataiwahi bila hata kufikiria kwamba alikuwa akishindana kasi na komandoo ambaye mkononi ana chombo cha moto, kuinama kwake mkono wake ukiwa haujafika hata kwa sentimita kumi kutoka ilipo silaha tayari bastola ya M.J Belinda ilikuwa imeshakohoa tena ikafumua kichwa chake.

           "mwingine nani anataka kuiokota silaha yake amfuate mwenzake kuzimu?" M.J Belinda aliuliza kisha akasema, "nimesema sirudii  swali nataka jibu sasa hivi, kimya chenu navunja goti la mwingine. Kwanza pigeni mateke silaha zenu mbele".

    Hawakuwa na ujanja wote kwa pamoja walizipiga teke silaha zao mbele wakawa wanamtazama M.J Belinda kwa wasiwasi.

    Swali hilo walikaa kimya kwa mara ya pili ili wasitoe siri ingawa walikuwa mbele ya mdomo wa bastola, kimya chao kilisababisha  bastola ya M.J Belinda ikohoe mara mbili mfululizo akiwa ameielekeza kwenye magoti ya wawili wengine ambao walishindwa kustahimili wakaenda chini moja kwa moja wakabaki wawili waliokuwa hawajajeruhiwa.

    Kikosi hicho kilidhamiria kutotoa chochote juu ya mpango huo uliowaleta nyumbani kwa M.J Belinda, kubaki wawili nao walikuwa wajeuri hawakutaka kitu chochote ambacho kingezidi kuwaweka pabaya waliowatuma. Wawili waliobaki nao walionja risasi za goti moja kila mmoja kama ilivyo wenzao lakini hakuna yoyote aliyejaribu kuufungua mdomo, walikuwa wameweka kiburi chao cha kukaa kimya kuliko kuongea kile walichoulizwa. Jeuri ya kufunzwa katika sehemu za hatari ndiyo iliwafanya wasinyanyue midomo yao katika kuongea, M.J Belinda aliwataza tu jinsi wanavyougulia maumivu ya magoti akiwa na tabasamu lisilotangaza furaha yoyote katika uso wake.

            "Kwangu mtasema tu si viburi nyinyi mmejileta wenyewe wavamizi" M.J Belinda aliongea kwa hasira sana huku tukio lililomkuta miaka kadhaa iliyopita likirudi ndani ya kichwa na kuzidi kumchanganya kabisa, alipowaona kikosi hicho kinachofanya uvamizi alikumbuka mengi ya miaka iliyopita hasa mauaji ya Simion aliyekuwa mpenzi wake na pia rafiki mkubwa wa Norbert. Tangu afariki huyo mpenzi wake Belinda hakuhitaji kuwa na mwanaume yoyote na alijiapiza hadi anakufa hatakuwa kimahusiano na mwanaume yeyote, macho yake yalipowatazama kwa makini wale vijana ndipo akakumbuka kile kisa cha Unyayo wa simba ambacho Simion alipoteza uhai kwa kumkingia kifua jasusi mwenzake Norbert asipigwe risasi na gaidi Elius katika mpambano wa kumtia nguvuni gaidi huyo.

     Hasira za kuuawa kwa mpenzi wake zilimjia kichwani kwa kasi ya ajabu na akajikuta akinyanyua risasi kwa mara nyingine ili awamalize wavamizi waliomkumbusha kifo cha mpenzi wake, alianza kumuelekezea mmoja risasi akaminya sehemu ya kufyatulia risasi lakini bastola ilitoa mlio wa vyuma vyake vinavyosukuma risasi tu kuashiria ilikuwa imeisha risasi. Hasira zake zikazidi zaidi baada  ya bastola kuisha risasi ikasaliti adhama yake ya kuwamaliza hao wavamizi, aliitazama bastola yake akiona imemfanyia usaliti mkubwa sana kwa  mgomo joto iliyomuwekea. Suala la kuisha risasi halikuwepo ndani ya kichwa zaidi ya kuona amesalitiwa na bastola, hasira za kuwamaliza zilimfanya hata asahau kabisa kama alikuwa ameweka risasi sita tu katika bastola yake baada ya wavamizi kuwa sita ambao aliwaona kipindi wanaingia nyumbani kwake.

    Hasira zake zilikuwa zimeonwa kama ni njia pekee kwa wale wavamizi wake waweze kupambana naye, wavamizi wawili kwa kasi ya ajabu walisimama kwa mguu  mmoja wakiwa na wazo tu la kujirusha mahali zilipo silaha zao baada ya kuzipiga mateke kutokana na kuamriwa na M.J Belinda wafanye hivyo.

   Fikra zao zilizotoka katika halmashauri ya ubongo ziliona ni jambo la zuri kufanya hivyo ili wapambane, lilikuwa ni jambo ambalo lilikuwa ni kosa kubwa kulifanya kwani lilirudisha mahala pake kile kilichokuwa kimetoka.

   Kitendo cha wao kusimama kwa ghafla tayari walikuwa wameshaurudisha umakini wa M.J Belinda uliokuwa umetoweka hapo awali kutokana na kutawaliwa na hasira kupitiliza, walipojirusha kufuata silaha zao  M.J Belinda tayari alishajua lengo lao naye alijirusha kwa mateke mawili ambayo yaliwapata wavamizi wake kutoka Special force kwenye vifua vyao wakarudi walipotoka.

   M.J Belinda hakuishia hapo aliendelea kuwapa kipigo kizito wale wavamizi mmoja baada ya mmoja hadi wakapoteza fahamu wote wakiwa na majeraha mbalimbali katika miili yao.

       "mkiamka mtasema wenyewe" M.J Belinda aliongea huku akihema kwa nguvu baada ya kumaliza kugawa kipigo.


****

    Muda ambao vijana wavamizi wa special force wanaingia matatani nyumbani kwa M.J Belinda ndiyo muda ambao Moses aliwasili ofisini kwa Norbert akiwa na mapambo yake aliyojipamba katika nguo alizovaa, alitumia mlango wa nyuma ambao ulimpeleka moja kwa moja hadi kwenye chumba kilichokuwa kikifungwa kwa namba maalum. Moses aliingiza namba hizo za kufungua huo mlango ambao ulifunguka na akaingia ndani ya chumba chenye giza nene ambapo aliwasha taa kisha akabonyeza kitufe kilichopo ukutani mlango alioingia nao ukajifunga.

     Chumba chenye ukubwa wa wastani ndiyo kilionekana mbele ya macho yake kikiwa kina kabati moja pamoja na kiti ambacho hutumika katika kutesa watu. Kiti hicho kilikuwa kimefungwa yule mzee maarufu kama Lion aliyekuwa akipigana na Norbert ambaye muda huo tayari alikuwa amerudiwa na fahamu akiwa hana nguvu kutokana na sumu hatari iliyomuingia mwilini baada ya kuchomwa na kifungo chaa Norbert, Moses alisimama kwa muda akawa anamtazama Lion halafu akamsogelea karibu zaidi jirani kabisa na kiti alichofungwa.

     Muda huo Lion alikuwa ameinamisha kichwa chini kutokana na sumu ya Norbert kumlevya na kumfanya hata ashindwe kuwa na nguvu ya kuinua kichwa chake, Moses alimtazama kisha akampiga kibao cha shavu kilichomfanya ajaribu kuinua kichwa lakini akashindwa kutokana na kuzidiwa sana.  Lion alibaki akihena kwa nguvu sana kisha akatukana tusi zito lililosikika kwa sauti ya chini sana ambayo ilieleweka kwa Moses, kibao kingine kilitoka kwenye  mikono ya Moses ndiyo kilifuata ambacho kiliacha alama katika shavu la Lion.

            "Uzee huo bado unaleta jeuri tu, basi utakuwa mpole tu kwanza pokea hii zawadi yako" Moses aliongea huku akitabasamu akatoa kitambaa cheupe ambacho alimbandika Lion kwenye pua na mdomo wake, alimshikilia kwa nguvu na kitambaa hicho na hatimaye Lion nguvu zikamuishia kabisa akaondokwa na fahamu kwa mara nyingine.

     Moses alimfungua kwenye  kiti kisha akamshusha chini akajiandaa kumbeba atoke naye humo ndani akijua ilikuwa ni kazi rahisi tofauti alivyodhani kumbe ilikuwa ni kazi ngumu sana. Ugumu uliopo kwenye kazi hiyo hakuwa ameuona na  hadi muda huo na alikuja kuuona baada ya kuhisi vumbi likimuangukia kwenye suti aliyovaa. Moses alitazama juu usawa mahali lilipotoka vumbi hilo akahisi kulikuwa kuna kitu kikiendelea huko juu ambapo ndiyo kuna ofisi ya Norbert, kishindo kikubwa kilifuata kikazidi kumfanya Moses akae kwa tahadhari humo ndani kwani hali ya usalama ilishaanza kuwa mbaya.

     Aliamua kujibana kwenye pembe ya chumba hicho kisha akazima taa kukawa na giza zito, kwa mara nyingine aliona mfuniko wa chuma unaotokea ofisini kwa Notbert ukiwa mwekundu kisha moto ukaonekana ukiwa unatoboa mfuniko kuuzunguka. Tobo kubwa lilitokea baada ya moto huo wa gesi ya kutoboa vyuma kutoboa mfuniko huo ambao ulimfanya Moses azidi kukaa kwa tahadhari, kurunzi yenye mwanga mkali ikamulika katika eneo alilokuwa amelazwa Lion baada ya Moses kumuacha akabana pembeni kwa tahadhari.

            "Yupo humo ndani, mmoja ashuke amfuate aje naye juu wengine tulinde usalama" Ilisikika sauti ya chini ikiongea baada ya Kurunzi kumulika kuonesha kuwa kuna mtu waliyekuwa wanamfuata, sauti hiyo ilikuwa imesikika sawia kwenye masikio ya Moses na hapo akabaini tayari kuna ugeni umekuja kumfuata yule aliyemfuata. Ambao wangeweza hata kumuharibia kazi iliyomleta humo ndani, hakuwa tayari kuona jambo hilo linatokea kwani wangekuwa wamerudi nyuma hatua mbili nyuma badala ya kupiga  hatua moja mbele  katika kazi yao. Wale watu waliokuwa juu nao walikuwa wameshaanza kumtanguliza mwenzao ili akamchukue Lion, muda huo huo Moses alikuwa akiyakagua mapambo yake aliyojipamba kama yapo sawa ili aweze kuyatumia.
 
     Mtu mwenye mavazi meusi alionekana akishuka kwenye ngazi zilizopo kwenye mfuniko huo na hatimaye akafika hadi chini, alianza kuangaza kwa kutumia kurunzi yake aone mandhari ya humo ndani na hatimaye miale ya kurunzi hiyo ikamulika katika sura ya Moses. Lilikuwa ni jambo asilolitarajia kama humo ndani kutakuwa na mtu mwingine tofauti na yeye, pia lilikuwa ni jambo ambalo hakulitarajia kama humo ndani kutakuwa na mtu mwingine ambaye ni kikwazo katika kazi yao waliyotumwa hapo.

     Mshtuko wa ghafla ndiyo ulimkumba papo hapo kutokana na jambo lenyewe kuwa la ghafla, nywele na  vinyweleo vyake zilimsisimka baada ya kumuona Moses akiwa eneo hilo tena muda ambao ameiweka silaha yake kwenye kipochi maalum cha kuweka silaha kilichokuwa kipo begani na silaha yake ikiwa inaning'inia kwapani ambapo ni gumu kuitoa bila Moses kumuwahi. Mshutuko aliyoupata ulikuwa siyo wa kawaida kutokana na mavazi nadhifu meusi aliyovaa Moses na utulivu aliokuwa nao Moses baada ya kumuona adui yake ambaye akipatwa na mshtuko mkubwa sana ambao ulimfanya huyo mvamizi aone kuwa alikuwa akitazamana na kiumbe asiyekuwa wa kawaida ambaye muda huo alikuwa anatabasamu tu baada ya miale ya kurunzi kutua katika uso wake.

          "hey" Alijikuta akiropoka basda ya kumuona Moses.


*Aaaaargh nini tena?!



JUMATATU NAYO SIKU TUKUTANE PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA




HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA YA MTUNZI