Friday, November 18, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA TANO


 RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTEKWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA



SEHEMU YA TANO!!
  Alikata simu kisha akaihifadhi namba hiyo kwenye simu ya Josephine akamrudishia  huku akiwa anatabasamu.

      "sijui nimefanya vibaya?" Alimuuiza Josephine huku akimpatia simu yake.

      "No hujafanya vibaya jamani" Josephine alijibu.

     "Ok nadhani tomorrow tutaonana" Norbert aliongea huku akimpatia Josephine ili waagane, Josephine alipompatia mkono aliuvuta karibu akaubusu halafu akamtazama usoni.

  Ilikuwa ni tendo ambalo halikutarajiwa na Josephine na alibaki akimtazama Norbert kwa mshangao kisha akatabasamu akaangalia pembeni kwa aibu.


****

  Josephine alishuka ndani ya gari ya Norbert kisha akampungia mkono akaingia mtaani huku akitembea kwa madaha sana, miondoko yake na jinsi mapambo aliyojaaliwa yalikuwa yakileta ugomvi kwa kila hatua aliyokuwa anaipiga wakati akiingia mitaani. Norbert alibaki akimtazama kwa muda wa dakika takribani moja kisha akatingisha kichwa kuashiria anasikitika, Josephine alipoingia kwenye mitaa ya ndani sehemu za Keko ndiyo ukawa mwisho wa Norbert kumuona na pia kufaidi uhondo aliouona  sehemu ya burudani kila akiuona na macho yake.

    "Aisee kama kashushwa vile" Norbert aliongea huku akiweka gia ya gari lake akaachia breki gari likaingia barabarani, alikuwa akiwaza  sana juu ya uzuri wa Josephine na jinsi itakavyokuwa siku  akiwa naye mahali palipo na uhuru zaidi. 

    "bahati naishi Temeke hivyo sijapoteza mafuta sana, ningekuwa naishi mahali kama Tegeta mama angu ningekuja hadi huku nirudi tena Tegeta. Mtoto mkali balaa" Norbert aliongea mwenyewe akiwa anakata kona kushoto alipofika Tameko jirani kabisa na maghorofa ya shirika la nyumba la taifa NHC, aliingia kwenye barabara ya Chang'ombe akawa anaongeza mwendo wa gari kutokana na uchache wa magari katika barabara hiyo.

   Alienda hadi kwenye  mataa ya Chang'ombe akasubiri baada ya taa kuwaka nyekundu katika upande wake, kwa mara nyingine mataa hayo yalimfanya arudi kwenye mawazo juu ya mwanamke yule kutokana na kuweka subira yaweze kuruhusu apite. Uzuri wa Josephine kwa mara nyingine ulijirudia ndani ya kichwa chake na kumfanya atikise kichwa kila akikumbuka umbo lake aliloliona kwa mara ya kwanza, hamasa ya kuwa naye tayari ilishaamka katika mwili wake lakini hakuwa katika moyo wake kabisa.

  Alikuwa hana tofauti na muonjaji karanga  bila ya kununua ili ajue karanga hizo zina ladha gani tu, pia alikuwa na muuza karanga maalum ambaye karanga zake hakuchoka kuzila kwa muda wowote ule autakao ule na ndiyo huyo aliyekuwa yupo moyoni mwake siku zote. Kwa huyo ambaye yupo moyoni mwake laiti Norbert angekuwa ni treni basi  huyo angekuwa ni mwisho wa reli haendi popote pale, hakika alikuwa hasikii wala haoni kwa huyo aliyekuwa moyoni mwake ingawa hakuacha tabia yake ya kuonja kila kinachopita mbele yake.

  Nusura za Mungu muweza katika uonjaji wake ndiyo zilimfanya aweze kuwa mzima mpaka muda huo kwani katika uonjaji wake huo hakuwahi kuonja sumu hata siku moja, hakika muweza bado alikuwa akimpenda sana mja wake huyu na bado alikuwa anahitaji kumuona akipumua katika mgongo wa ardhi ndiyo maana yupo salama mpaka muda huo.

  Mataa yaliporuhusu Norbert alinyoosha moja kwa moja barabara ambayo ilimpeleka hadi jirani kwenye kituo cha polisi cha Chang'ombe maarufu kama Usalama, alikata kona upande wa kushoto akaingia katika barabara ya Temeke ambapo alitembea kwa umbali mdogo tu halafu akakata kona akaingia upande wa kulia kwenye barabara ya vumbi inayopita jirani na mtaa wa Maneno kitongoji cha Temeke.  Alienda na barabara hiyo hadi alipoipita shule ya msingi ya Muungano akakata kona akaingia upande wa kushoto, alienda kwa mwendo mfupi kisha akasimama kwenye geti la nyumba yenye uzio mkubwa sana.

  Hapo alipiga  honi mara moja geti likafunguliwa akaingiza gari ndani akalipeleka hadi sehemu maalum ya kulaza gari akalizima akashuka, alitembea kuelekea ndani ya nyumba yake  akiwa hana habari juu ya mabadiliko yaliyopo ndani nyumba hiyo. Hakuwa na habari kama palikuwa na ongezeko la watu ndani ya nyumba hiyo na  alikuja kujua baada ya kumuona mmojawapo ambaye alikuwa  akimpenda sana, huyo ndiyo alimfanya abaini kwamba kulikuwa na mwingine ndani ya nyumba  hiyo kwani hawezi kuja peke yake hata siku moja.

  Jerry ndiye  alikuwepo mbele ya macho yake kwa muda huo akamfanya abaini kwamba hakuwa amekuja peke yake kabisa kwani hakuwa na uwezo wa kuja peke yake, mtoto huyo hakuwa na uwezo wa kuja peke yake bila uwepo wa mama yake na hapo ndipo akabaini kwamba Jerry alikuwa amekuja na mama yake hapo nyumbani. Jerry alikuwa ni mtoto aliyefanana na Norbert kwa sura hadi mwendo wake anaotembea na bila shaka haikuwa na haja ya kuhitaji vipimo vya vinasaba katika kujua kama ni mtoto wake kwani alikuwa na kila ushahidi wa kumuonesha ni damu yake.

  Jerry alipomuona Norbert alimkimbilia kwa haraka sana akamkumbatia huku akionesha furaha aliyonayo kwa kumuona baba yake kwa muda huo, Norbert alimnyanyua kwa furaha mtoto wake huku akifarijika sana na kumuona eneo hilo.

     "Oooh! Son, mummy yupo wapi?" Norbert alimuuliza Jerry akiwa amembeba kwa furaha.

     "Inside, I miss you daddy" Jerry aliongea huku akimkumbatia baba yake kwa upendo na alionesha alikuwa akitaka kumuona baba yake kwamuda mrefu sana.

     "me more my son, masomo vipi?" Norbert alimuuliza Jerry huku akifanya matani naye ambayo yalizidi kumfurahisha sana Jerry, aliingia ndani akiwa amembeba Jerry na alienda sebuleni ambapo alipokelewa na mama yake Jerry kwa mapokezi tofauti na yale aliyompokea Jerry.

  Alimkuta Norene akiwa amekaa kwenye kochi akiwa amenuna sana na alipomuona aligeuza sura pembeni kabisa, Norbert hapo alibaini kwamba Norene hakuwa amependezwa na kitu ambacho hakukifahamu na hata alipomfuata akamshika mkono Norebe aliupiga kibao mkono wake.

    "Nor ulikuwa wapi muda wote huo?" Norene aliuliza akiwa amenuna.

    "Norene nilikuwa nina kazi ya kiofisi kidogo" Norbert alijitetea.

    "Muongo wewe haukuwa ofisini kwako nimepiga simu yako ya mezani hukupokea, hivi unajua nimekuja muda mrefu sana nakusubiri wewe" Norene aliongea akuoneshwa kutopendezwa kabisa na kutopokelewa kwa simu yake.

    "Siyo ofisi ya mazugio bali ni ofisi halisi, nilikuwa na Gawaza tukipiga kazi muhimu" Norbert alijitetea.

    "una uhakika ulikuwa na Moses? Nimpigie simu nimuulize?" Norene aliuliza akiwa amekaza macho yake

    "unaweza ukampigia simu hiyo hapo mezani" Norbert  alimuambia Norene huku akijiamini na hakuonesha chembe yoyote ya wasiwasi kwani alijua yupo anajibu maswali ya jasusi mwenzake, kauli hiyo ilimfanya Norene asimame wima amkumbatie Norbert.

     "Nakupenda sana Norbert tambua ukiwa mbali nami na usipopokea simu unanipa wasiwasi mpenzi" Norene aliongea kwa hisia akiwa amemkumbatia Norbert.

     "Nakupenda pia mama yake, kuwa na amani tu" Norbert aliongea.

     "amani nitakuwa nayo wapi mpenzi wakati wewe kazi yako ni ya hatari na muda mwingine inakuhitaji uwe karibu na wanawake" Norene aliongea kwa kulalamika akiwa bado amemkumbatia Norbert.

     "wewe ndiyo mwisho wa vituo vyote sina pa kwenda zaidi mpenzi wangu" Norbert aliongea huku akimtoa Norene mwilini mwake akamshika kiuno akawa anaelekea naye chumbani huku wakiwa na Jerry.


****


   Wakati Norbert akiwa yupo na Norene wanaelekea chumbani muda huo ndiyo muda ambao Moses alikuwa akirejea nyumbani kwake kutoka kwenye mihangaiko yake, aliingiza gari yake sehemu maalum ya kulaza magari na akaingia ndani ya nyumba. Sura isiyo na furaha ya mke wake ndiyo ilimpokea kuashiria hakukuwa na taarifa nzuri usoni mwa mke wake ingawa yeye aliijua taarifa hiyo tangu hata mke wake hajapatiwa, alimkuta Beatrice akiwa amekaa kwenye kochi akiwa ni mwingi wa mawazo huku mkono wake akiwa ameweka shavuni kuonesha alikuwa na huzuni sana.

   Moses alipoona yupo katika hali hiyo alimsogelea akapiga magoti mbele halafu akaweka mikono kwenye mapaja yake  akambusu mdomoni akionesha mwingi wa furaha kama ilivyo kawaida yake lakini Beatrice alionesha kutokuwa na hali ya furaha hata kidogo. Chozi lilianza kumdondoka taratibu kwenye macho yake akabaki akimtazama Moses kisha mvua isiyosababishwa na mawingu kwenye macho ya Beatrice ilianza kwa manyunyu taratibu na hatimaye ikawa mvua kubwa sana iliyoanza hata kumtia simanzi hata Moses mwenyewe, Beatrice alikuwa akilia kilio cha uchungu na alimkumbatia Moses kwa nguvu wakati akilia na machozi yake yakachukua nafasi nyingine ya kulowanisha kifua cha Moses.

     "Mume wangu nakupenda sana na sipendi kuwa mbali nawe ila.." Beatrice aliongea huku akilia kwa uchungu sna kwa taarifa aliyopewa mchana ambayo kwake ilikuwa ni zaidi ya simanzi kabisa.

     "No no usilie mke wangu tell me tatizo nini?" Moses aliuliza huku akianza kuumika moyoni kwa kusikia kilio cha mke wake,alimtoa Beatrice kifunai mwake na akamfuta machozi yaliyokuwa yakimtoka na akambembeleza hadi alipotulia kisha akamuambia "nieleze my queen tatizo nini hujui sipendi kukuona ukihuzunika".

  Beatrice alichukua nafasi hiyo kumueleza Moses kila kitu juu ya taarifa aliyopewa mchana wa siku hiyo alipokuwa kazini kisha akabaki akimtazama Moses aone taarifa hiyo ataipokea vipi,haikuwa taarifa ngeni katika masikio ya Moses kwani yeye ndiye aliyetuma hicho kitu kifanyike kwa ajili ya usalama wa mke wake.

  Taarifa hiyo ilipopenya kwa mara ya pili kwenye masikio yake alisimama pale alipokuwa amepiga magoti mbele ya mke halafu akageuka nyuma akampa mgongo akawa anapiga mkono kichwani kwake akionesha taarifa ile ilikuwa ni taarifa ambayo hakutarajia kuisikia hata kidogo, alipogeuka kwa mara ya pili kumtazama mke wake tayari uso wake ulikuwa umebadilika na kuwa usio na furaha hata kidogo hadi akaanza kumpa Beatrice hofu.

  Alishusha pumzi kwa nguvu kisha uso wake ukarudi katika hali ya kawaida kama awali akataka kufungua mdomo kutamka kitu ila akasita akahema kwa nguvu halafu akainamisha uso wake chini. Alipoinua uso wake  alionesha kuwa na hali siyo na furaha kabisa na alibaki akimtazama Beatrice kusema chochote, alifumbata mikono yake kifuani mwake halafu akawa anatafuta neno la kuongea.

     "Mke wangu" Hatimaye alitamka akamfanya Beatrice amtazame asikie kauli itakayotoka kwenye kinywa chake kwani alihisi asipomtazama usoni atakuwa haisikii vizuri kauli ya mumewe.

  Moses aliendelea,"wewe ni mke wa professa tena tajiri mwenye utajiri binafsi na pia amerithi kutoka kwa mzazi professa aliyekuwa tajiri, wanawake wenzao wanataka uwaoneshe mfano ulivyo ingawa mume wako ni tajiri. Ukaamua kuchapa kazi kama wewe ukionesha mwanamke hutakiwi kubweteka ukitosheka na utajiri wa mumeo, ukiwa mke wa mtu maarufu umeweza kuwahamasisha wenzako pongezi kwa hilo na najivunia kuwa na mke kama wewe nakupenda sana. Sasa basi hiyo ni sehemu ya kazi mke wangu unatakiwa uwaoneshe upo mchapakazi kiasi gani,naumia sana kwa wewe kwenda mbali na mimi lakini yote ni maisha mke wangu hicho kitu ni cha muda mfupi".

     "No Moses" Beatrice alisema huku akisimama akamkikmbilia Moses akamkumbatia halafu akatamka kwa uchungu, "sitaki kuwa mbali na wewe". Kilio cha uchungu kutoka kwa Beatrice ndiyo kilifuata akabaki akimkumbatia Moses Moses kwa nguvu, Moses alimpokea mke wake na akawa ana kazi ya kumbembeleza tu.

     "Najua nina mwanamke shupavu na mchapakazi sasa show how strong you are,upo mbali nami ila umebeba kiumbe changu mke wangu huo ni wajibu usilie baby" Moses alimuambia Beatrice huku akichezea nywele zake, Beatrice alitingisha kichwa kukubaliana na Moses halafu akasogeza mdomo wake jirani na mdomo wa Moses kuashiria alikuwa na hitaji jingine alilokuwa analihitaji tofauti na hiyo taarifa aliyompa mume wake.

  Moses alitambua hitaji la mke na alimtimizia papo hapo kisha akamuinua kwa ghafla na kusababisha Beatrice arudiwe na furaha kisha akacheka kwa nguvu sana kuonesha alikuwa na furaha sana kila anapokuwa karibu na Moses. Aliingia naye ndani na siku hiyo wakaimaliza wakiwa na furaha akama ilivyo kawaida yao kuwa na furaha kila siku,walipopanda kitandani kupumzika napurukushani za aina zote za siku nzima bado walikuwa na furaha vilevile.

  Asubuhi ya siku iliyofuata Beatrice alijiandaa na Moses pia akajiaandaa kwa kama ilivyo kawaida yake, wote kwa pamoja walitoka na gari moja na safari ya kuelekea Uwanja wa ndege ilianza kwani ndani ya saa moja na nusu lijalo ndege ya shirika la ndege la Uswisi ilikuwa ikisafiri kuelekea Uingereza ikipitia nchi tofauti. Ilikuwa ni siku inayowatenganisha wapendanao ambao hawakuhitaji kutenganishwa lakini kutokana na sababu isiyoepukika ilibidi watengane tu.

  Baada ya saa moja tayari walikuwa wameshafika katika maeneo ya maegesho ya uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, wote kwa pamoja walishuka na Moses akamsaidia mke wake kukokota sanduku la vitu vyake muhimu ambavyo angevitumia akiwa safarini. Waliingia ndani  kwani muda wa abiria kuingia kwenye ndege ulikuwa umeshawadia,kwa pamoja waliachana eneo maalum ambalo msindikizaji hutakiwa kuishia hapo ndipo ikachukua huzuni ikazidi mahala pake.

  Waliagana kwa kukumbatiana kisha Beatrice akaelekea sehemu maalum ya ukaguzi na hatimaye akaingia ndani ya ndege, Moses aliendelea kusubiri eneo hilo hadi ndege ilipoacha ardhi ya Tanzania ndiyo na yeye akaondoka eneo hilo akiwa yupo huru ndani ya nafsi yake na hana wasiwasi wowote ule kwani udhaifu wake tayari ulikuwa umeshaondoka ndani ya eneo hilo sasa ilikuwa ni muda mzuri kwa yeye kuanza kufanya kazi kwa ufasaha kabisa.


****

       IKULU
      MAGOGONI
     DAR ES SALAAM

  Taarifa za kuuawa kwa viongozi mbalimbali wa kidini tayari zilikuwa zishafika kwenye ofisi ya rais Zuber Ameir na kutokana na upeo wake mkubwa kufikiria aliamua awaite viongozi wakubwa wa polisi wakiongozwa na IGP Rashid Chulanga, katika chumba cha mkutano  ndani ya ikulu hiyo rais alionekana kutokuwa na mzaha kabisa na suala la linalotaka kuchangia kuvurugika kwa amani nchini. Baada ya kuhakikisha viongozi wote aliowaita wametimia wakiwemo makamishna mbalimbali wakiongozwa na IGP mkutano ulianza rasmi.

    "Hali ya amani kwa sasa naona itaelekea  mahali pasipohitajika nchi iwe, mauaji haya viongozi wakubwa wa kidini siyo suala la kulifumbia macho hata kidogo kwani naona litaelekea mahali ambapo si pazuri. Nimeamua kuwaita hapa ili niwaambie kuhusu hili suala ambalo litaweza kuchukua sura nyingine ndani ya nchi yetu iliyo na amani, yametokea mauaji ya kwanza ya askofu wa KKKT dayosisi ya Mashariki tukajua ni moja ya njama ya wahalifu hivyo uchnguzi ufanyike ili watiwe mbaroni wahukumiwe lakini yalipotokea haya mauaji ya Mufti wa jiji jili nimeona kama kuna kitu kinataka kupandikizwa katika vichwa vya waumini sasa inabidi nyinyi kama viongozi wa jeshi la polisi mhakikishe suala hili halitokei. Amani ndani ya nchi yote ni suala la muhimu kudumishwa sasa nataka suala la kuvurugika kwa amani lisiwepo ndani ya nchi hii, nimemaliza ningehitaji kusikiliza maoni yenu juu ya suala hili" Rais Zuber aliongea, baada ya kumaliza kuongea Kamishna wa kanda maalum alinyoosha mkono akiashiria  ana wazo.

    "Ndiyo kamishna Wilfred" Rais Zuber alimruhusu aongee, Kamishna Wilfred alisimama akatoa saluti kwa Rais Zuber kuonesha heshima kisha akajikohoza ili kuweka sawa njia yake ipitayo shingo apate kuongea kwa ufasaha.

    "Mheshimiwa rais pamoja na wakuu mbalimbali mliopo humu napenda nitoe maelezo ytafuatayo, undani wa matukio haya ni malipizo ya kisasi baada ya kutokea matatizo mbalimbali ya kidini ndani ya jiji hili ambayo yalianzia Yombo kwa kusababisha mauaji ya watu kadhaa. Kimtazamo wangu naona baadhi ya watu walikuwa hawajiridhika na sabau hiyo ndiyo maana wakaanza kumuua askofu wa kanisa la KKKT kwani chanzo cha ugomvi kule Yombo ilikuwa ni mzee wa kanisa la KKKT, hivyo basi kutokana na kuuawa  kwa askofu huyo waumini wachache waliokuwa na hasira naona ndiyo wakafanya mauaji kwa mufti wa jiji hili. Mheshimiwa rais suala hili litafikia tamati na amani itarudi ikiwa tu tutawaita viongozi wa dini zote na kukaa nao meza moja kisha tusuluhishe suala hili na si vinginevyo, wao ndiyo wana uwezo wa kuwatuliza waumini wao tu. Ni hayo tu mheshimiwa" Kamishna Wilfred aliongea.

    "Asante kamishna, naam DCP John ongea" Rais Zuber alishukuru mchango wa Kamishna Wilfred kisha akamruhusu kamishna msaidizi wa polisi ACP John Faustin aongee, DCP John alisimama akapiga saluti kwa Rais Zuber kisha akawatazama kila mmoja aliyekuwemo humo ndani halafu akarudisha macho yake kwa rais Zuber Ameir.

    "Mheshimiwa rais mimi sikubaliani kabisa na mawazo ya kamishna Wilfred kwa kwasababu" DCP John aliongea kisha akaweka kituo halafu akaendelea, "hii ni mbinu ambayo inatumiwa na kikundi fulani cha watu katika kuhakikisha amani inatoweka ndani ya Tanzania na wao waweze kufanya kazi yao wanayoijua wao, hivyo basi tusihadaike na mpango wa watu wachache tu inabidi tutumie mbinu za ziada katika kuhakikisha hawa watu wanatiwa nguvuni halafu ndiyo hao viongozi hao wa dini waitwe waeleweshwe na pia wawaeleweshe watu wao tutakuwa tumefanikiwa vinginevyo nchi itavurugika".

  Makamishana wote pamoja na IGP waliposikia kauli hiyo waliiunga mkono kwa pamoja ingawa mmoja alikuwa akiiunga mkono kwa shingo upande, walipoulizwa wengine kama walikuwa na  la zida bgaada ya kauli hiyo wote kwa pamoja walikataa kuwa hakuyna mwenye la ziada.

    "Nafikiri DCP John amemaliza kila kitu sasa kilichobaki ni utekelezaji tu, naomba timu nzima ya CID iiingie kazini kuanzi muda huu tuokoe janga amblo litaikumba nchi yetu,  kazi ianze mara moja na kabla mwezi huu haujaisha watuhumiwa wote wawe mikononi mwa vyombo vya dola,uzembe wowote mtawajibishwa. Sina la ziada" Rais Zuber alitoa amri kisha akaondoka eneo hilo bila hata kuongeza neno jingine la ziada.

  Alitoka katika chumba cha mkutano ndani ya ikulu akaingia katika ofisi yake ya ambapo akakutana na ugeni wa ghafla sana ndani ya ofisi hiyo, katika kiti cha upande wa pili wanachokaa waqeni alimkuta Moses akiwa amekaa akimsubiri na hakuelewa alikuwa kaingia muda gani humo ofisini.

    "Moses vipi mbona ghafla?" Rais Zuber aliuliza

    "kwasababu nimekumbwa na ughafla" Moses alijibu.

    "ongea nikuelewe basi" Rais Zuber alimuambia

    "Mkuu tambua kuna mbwa mwitu kati ya kondoo wote uliokuwa nao sasa jambo hili usimuamini mtu" Moses aliongea.

    "unasema?!" Rais Zuber aliuliza kwa mshangao sana.

    "Ni mapema sana kujua ya jioni wakati ndiyo kwanza jua linachomoza, subiri hiyo jioni ifike ndiyo ya jioni utayajua. Suala lipo mkononi mwangu utalielewa zaidi" Moses aliopngea kisha akatoka ndani ya ofisi hiyo ya rais, rais Zuber hakutaka kumuuliza neno kwani alimtambua fika katika hatua kama hiyo Moses huwa hafafanui jambo hadi likamilike ndiyo hatoi ufanunuzi wote.

****

  Majira ya saa nne asubuhi ofisi ya Norbert anayoitumia kama muandishi wa habari ilipata ugeni ambao ulikuwa wa ghafla sana ambao hakuutarajia kabisa,majira hayo ilikuwa ni muda ambao katibu mkhtasi wake alikuwa ameenda kupata kifungua kinywa akamuacha Norbert akiwa ofisini akimalizia kazi ambazo hakuwa amezimalizia siku iliyopita.

  Mlango wa ofisi yake uligongwa mara mbili kisha mgongaji akatulia, Norbert alimruhusu mgongaji huyo huku macho yake yakiwa yapo makini kwenye tarakilishi yake akiwa hajamjua  aliyekuwa anangonga mlango huo alikuwa nani. Alipoinua macho yake alikutana uso kwa uso na mzee wa takribani miaka hamsini akiwa amevaa suti nadhifu sana na akiwa amebeba mkongoja mrefu ambao hupendwa sana kubebwa na matajiri, mkono mwingine mzee huyo alikuwa na mkoba wa kufungwa kwa namba.

     "Karibu mzee wangu" Norbert alimkaribisha mzee huyo huku akimsanifu mwili wake na muonekano wake jinsi ulivyo na hapo akabaini alikuwa na alama atofauti na watu wengine wa kawaida ambayo wanayo.

     "Asante kijana mimi si mkaaji ila nimekuja kukupa ujumbe tu ambao utapata bahati tu ya kuuona" Mzee huyo aliongea kisha akawa anaunyanyua mkongoja wake juu kidogo, Norbert alikuwa akimtazama huku akijizungusha kwenye kiti chake cha matairi alichokuwa amekikalia.

     "ndiyo mzee wangu nakusikiliza" Norbert aliongea huku akili ikiwa imeweka utulivu wa hali ya juu na macho yake yote yakiwa yapo katika mkono wa mzee huyo.

  Kwa wepesi wa hali ya juu yule mzee alipigiza sehemu ya chini ya mkongojo wake katika marumaru zilizopo ofisini  hapo, fito za fimbo hiyo ziligawanyika zikaanguka na ndani yake kikaonekana kisu kikali sana. Mzee huyo alifanya wepesi mwingine katika kukipeleka kile kisu usawa wa eneo alilokaa Norbert lakini aliambulia patupu baada ya Norbert kujisukuma na kiti cha matairi akaeleka pembeni kisha akapiga sakarakasi akatua upande aliokuwa amesimama yule mzee.

  Yule mzee naye hakubaki nyuma aliendela kumletea mashambhulizi ya panga Norbert kila upande anaoenda na ikawa ni kazi ya ziada kwa Norbert kuanza kukwepa mapanga hayo kwa umakini wa hali ya juu na alipoona mzee huyo kazidi kushambulia aliruka sarakasi nyingine akarudi kule alipokuwa  kisha akalegeza vigungo vya shati lake akasimama kimakabiliano.

      "Ninja" Yule mzee alisema na Norbert akamtazama kwa tabsamu lisiloonesha furaha, yule mzee aliiruka meza kwa sarakasi akapambane na Norbert ana kwa ana lakini Sarakasi aliyoipiga alipotua mitaa kadhaa toka Norbert alipo alijikuta akianguka chini moja kwa moja  baada ya kuhisi kitu kikitoboa kifua chake, alipoangalia eneo alilotobolewa alikuta kitu chenye rangi ya dhahabu ambacho kinafanana kwa kila kitu na vifungo vya Norbert.

     "Ulidhani sina silaha siyo,sasa pata dose ya kifungo changu hicho" Norbert aliongea huku akimuonesha yule mzee sehemu ya shati ambacho kifungo hamna,alikuwa ametobolewa na moja ya silaha hatari ambazo hukaa kama kifungo katika mashati ya majasusi kwa ajili ya tahadhari. Yule mzee alikichomoa kile kifungo  ambacho kilikuwa na ncha kali sana, ukungu ulitanda kwenye macho ya mzee huyo na hatimaye kiza kikatanda  kabisa.


TUKUATANE SIKU YA JUMAMOSI PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA






HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA YA MTUNZI