Wednesday, November 30, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA KUMI NA SABA





RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________




SEHEMU YA KUMI NA SABA

               "Albert mwana wa Mungu wasalimie huko mbinguni maana ndani ya dakika tatu bomu hili ninaloliweka mbele yako litasambaratisha viungo vyako vyote" Jack Shaw aliongea huku akimuita kwa jina la bandia alilojiita Norbert, wote kwa pamoja walicheka kisha wakaingia kwenye gari wakaondoka  kwa umbali wa mitaa takribani mia tatu halafu wakasimama.



   Walisubiri kwa muda wa dakika tatu hadi waliposikia mlipuko mzito wa bomu ukitokea walipomfunga Norbert, hapo walijua kazi yao imeshaisha na waliondoa gari kwa mwendo wa kasi.


____________________


     Kawaida ya mpelelezi siku zote ni kubeba vitu vitakavypmsaidia kwenye  jambo la dharura, Norbert naye ilikiwa ni kawaida yake kufanya hivyo akiwa yupo mahali popote hata kama akijihisi yupo eneo la lenye amani. Mwilini mwake siku zote alikuwa na silaha alizoziita mapambo ambazo humsaidia maeneo ya hatari, siku hiyo kabla hajaenda chumbani kwa Jack Shaw aliweka silaha mbalinbali pamoja na vitu vya ushahidi kama vile kamera ndogo aliyokuwa ameifunga kwenye kifungo cha shati lake. Mguuni alikuwa amepachika bastola  ndogo yenye kiwambo kidogo cha kuzuia sauti ambayo alitaka kuitoa hata alipokurupushwa usingizini na kugongwa kwa mlango, alipoambiwa abadilishe nguo yeye alifanya kazi ya kuiweka bastola hiyo isionekane katika nguo alizovaa.

    Jack Shaw, Spider na Scorpio wakati walipomfunga kwa pingu katika mti bila ya kumpekua, walikuwa wamefanya kosa kubwa bila wao kutambua kama walikuwa wamefanya kosa. Walipoondoka wakiwa wametega bomu mbele yake tayari walikuwa wameamsha akili ya Norbert katika kujikomboa na hatari, pingu walizomfunga zilimfanya Norbert mgongo wake uwe kwenye gogo jembamba la mti huo mgumu.

   Mikono na miguu yake vilikuwa vimefungwa kwa nyuma, bomu lilikuwa mbele yake tena mshale wa saa unaohesabu sekunde ulikuwa ukienda kwa mwendo wake wa kawaida huku ukizidi kuzipunguza dakika tatu zilizotegwa kwenye bomu hilo. Mlio wa mshale wa dakika katika bomu hilo vilimfanya Norbert ahangaike kujivuta mbele lakini ugumu wa pingu ulimrudisha palepale alipokuwa, alijaribu kujitikisa kulia na kushoto lakini ugumu wa pingu aliyofungwa ulimfanya asogee kidogo tu kwenda upande wa kushoto na kulia.

    Hapo ndipo Norbert akakumbuka kwamba alikuwa ana bastola yake ya dharura aliyokuwa ameifunga mguuni, alizitazama sekunde katika bomu hilo zinavyomaliza dakika kisha akajilazimisha kupiga magoti kwa haraka huku mapigo yake ya moyo yakimuenda mbio kila akiitazama saa ya bomu ambayo ilkuwa tayari imeshamaliza dakika moja kati ya dakika tatu na sasa ipo dakika ya pili.

   Alipopiga magoti chini alijitahidi kuupindisha mgongo wake pamoja na kuipindisha mikono yake aliyofungwa pingu hadi akafanikiwa, gogo alilofungiwa lilipita katikati ya miguu yake kwenye eneo la baina ya goti ma kifundo cha miguu. Hiyo ilimuwia rahisi kuweza kuulazimisha mkono wake kufika katika mguu wake kulia juu ya kifundo cha mguu, macho yake yalikuwa yakiitazama  ile saa ya bomu ambayo ilikuwa ikitoa mwanga kwenye mishale yake eneo hilo la gizani ambayo ilimfanya Norbert ang'amue dakika zilizobaki ili bomu hilo lilipuke.

   Mwendo wa sekunde katika saa hiyo kulimfanya azidi kuwa na kasi ya kutaka kujinasua katika kifo hicho kibaya cha kutawanywa viungo vyake na bomu, alifanikiwa kuufikisha mkono wake pale alipokuwa akihitaji ufike na aliuingiza mkono huo ndani ya soksi yake baada ya kuisogeza juu suruali. Alipekua katika soksi yake  aliyoivaa mguu wa kushoto kwa haraka akitafuta akiitafuta bastola yake lakini hakuipata, hakukata tamaa  aliamua kuipekua na soksi yake aliyovaa mguu wa kulia akafanikiwa kuipata bastola hiyo akaitoa haraka.

   Moyo wake ulizidi kupiga kwa nguvu alipiangalia saa ya bomu hiyo ambayo ilionesha imebaki dakika moja na nusu kabla bomu halijalipuka, hakuwa na njia nyingine ya kujiokoa zaidi ya hiyo bastola ambayo tayari alikuwa ameshafanikiwa kuitia mikononi mwake. Aliishika bastola hiyo kwa tabu akaelekeza bomba la kiwambo cha kuzuia sauti kwa juu katika pingu za mkononi, alibinya kidude cha kuachia risasi katika bastola hiyo na hapo risasi ikakata  pingu ya mikononi lakini bastola ikamponyoka ikamdondoka kwa bahati mbaya  kutokana na jinsi alivyoishika.

   Norbert aliachia mguno wa fadhaa ingawa hakutaka kukata tamaa hata kidogo, aliamua kupeleka mikono yake nyuma na kupapasa katika giza hilo kubwa kwa muda wa sekunde kadhaa hadi akaipata bastola hiyo. Kitendo  kingine cha haraka ndiyo alikifanya cha kuikata pingu ya miguuni kwa risasi halafu akasimama haraka sana, aliangalia kwenye bomu akakuta imebaki nusu dakika tu yaani Sekunde 30.

    Aliamua kukimbia kwa uwezo wake wote aliojifunza wakati yupo mafunzoni katika nchi tofauti, alifika umbali wa mita takribani mia moja na hapo ndiyo akasikia mlipuko wa bomu hilo ukitokea nyuma yake. Alishusha pumzi hapo kwa kufanikiwa kujikomboa na bomu hilo kisha akaketi chini ili kutuliza akili yake katika kivuli cha mti mkubwa, mkononi alikuwa ameishikilia bsstola ambayo ndiyo aliiona imekuwa msaada yake katika kumkomboa.

   Alipumzika kwa muda wa dakika kadhaa kisha akasimama akaangalia pande zote akaona kupo shwari, alianza kukimbia kwa kasi sana akiwa hana uelekeo maalum kwani hakujua ni wapi pa kuelekea kwa usiku huo. Alikimbia sana na hatimaye akachoka akapumzika chini ya mti ya mti mwingine ambao aliuona salama kumbe haukuwa na usalama, hapo chini ya mti Norbert alijishika kidevuni mwake mithili ya mtu anayetaka kujichomoa kichwa chake. Alivuta kwa nguvu akavua sura ya bandia iliyomfanya atambulike kama Albert mbele ya Jack Shaw akabaki na sura yake halisi, hapo aliamua kutazama kamera yake ndogo aliyoifunga kwenye kifungo cha shati lake akaona ipo salama.

    Norbert aliendelea kupumzika katika eneo hilo lililokuwa halina usalama ingawa yeye aliliona lipo salama, hakujua kama eneo la chini ya mti juu kulikuwa kuna mwindaji aliyeona windo lake muda huo wa usiku. Alikuja kujua hilo baada ya kuhisi majani yakijitikisa huko juu kuashiria kulikuwa kuna kitu kinaanguka chini  usawa wa eneo alilopo, Norbert hakutaka kujiuliza mara mbili juu ya kitu hicho kikichojiachia zaidi ya kubiringita pembeni halafu akajiinua kwa namna ya kiufundi kabisa. Alipoangalia katika eneo alikuwa amekaa hapo awali kwa msaada wa mbalamwezo ya usiku huo alimuona chui akiwa anamtazama kwa hasira, Norbert hapo alijua alikuwa ameingia katika anga za muwindaji wa pori hilo ambaye ilimpasa kuwa makini sana.  

    Chui yule alitoa mngurumo wa hasira na aliruka upande ule aliokuwa yupo Norbert akiwa ametanguliza kucha zake mbele, Norbert alikuwa ameshaliona hilo na alihama eneo alilopo kwa kasi ya ajabu kisha akaishika bastola yake vizuri. Chui alipogeuka amshambulie tena alionja risasi ambayo ilitua kwenye paji lake la uso ndiyo ukawa mwisho wa upinzani wake  kwa Norbert, chuo huyo hakufanya purukushani wakati roho yake inaachana na mwili zaidi ya kutulia papo hapo.

   Eneo la mbugani hapo hakuona usalama wake kama utakuwa mzuri  ikiwa ataendelea kukaa, Norbert alinyanyuka na kuanza kukimbia kuelekea upande wa kaskazini.


****



  ASUBUHI ILIYOFUATA,
        KARATU,
        ARUSHA

    Gari kubwa la kubeba mizigo aina ya Scania liliokuwa limesheheni mizigo mingi lililokuwa likitoka nchini Kenya likupunguza mwendo ili liingie kwenye kituo cha kujaza mafuta, kupunguza huko mwendo kuliambatana na kufunguka sehemu ya juu ya gari hiyo kisha mwanaume mrefu aliyevaa shati ya rangi bluu bahari lenye mikono mirefu pamoja na suruali ya nyeusi kushuka kwa haraka akatua chini pasipo kuonwa na dereva wa hilo. Mwanaume huyo hakuwa mwingine isipokuwa Norbert aliyedandia gari hilo lilipopita katika barabara inayopita mbuga ya Serengeti usiku uliopita, gari hilo lilipunguza mwendo katika tuta usiku uliopita na hapo ndipo Norbert akapata nafasi ya kulidandia pasipo kujulikana.

    Hadi saa nne asubuhi tangu alipolidandia gari hilo ndiyo alikuwa amefika wilayani Karatu mkoani Arusha ambapo alishuka , alitembea kwa haraka hadi pembezoni mwa barabara  huku akiwa na tabasamu pana kama ilivyo kawaida yake akitaka kufika katika eneo lolote analotaka kufika. Mifukoni mwake bado alikuwa ana vitu muhimu ambavyo vingemsaidia  kwenye shida ikimtokea, pochi yake yenye vitu muhimu yote ilikuwa ipo mfukoni mwake.

   Norbert alishukuru Mungu kwa kutopekuliwa na Jack Shaw pamoja na vijana wake kwani laiti angepekuliwa basi hata hapo asingefika, muda wa saa nne asubuhi Norbert alikuwa tayari ameshachoka hivyo alihitaji muda wa kupumzika kama ilivyo wanadamu wengine wakiwa hawakupata usingizi. Aliamua kutafuta nyumba ya wageni ya bei ya kawaida ambayo alilipa akapata chumba, Norbert alipoingia ndani ya chumba alicholipia aliamua kujitupa kitandani kutokana na usingizi kuizidi hamu ya kula aliyokuwa nayo na ndani ya dakika chache tayari alikuwa amelala usingizi mzito.

****

    Wakati Norbert akiwa anauchapa usingizi upande wa jiji la Dar es salaam tayari mambo yalishaanza kuwa mabaya zaidi kwa Moses, muda huo tayari ilikuwa imatimia siku ya tatu tangu Rais Zuber alipopewa agizo na L.J Ibrahim la kutoa maelezo ya kutohusika kwake na kifo cha Jenerali Kulika ikiwa  Moses mtu wake wa kuaminika alikuwa anahusika. Siku hiyo ndiyo siku ambayo L.J Ibrahim aliahidi kumtangaza Moses kama muuaji aliyehusika na mauaji ya Jenerali Kulika, Askofu Edson pamoja na Mufti.

   Siku hiyo ndiyo alifanya hicho hicho alichoahidi ambapo alihitisha mkutano wa dharura wa waandishi wa habari, katika mkutano huo aliamua kueleza kwa kifupi juu ya nini chanzo cha mauaji hayo. Aliitaja  sumu iligunduliwa na Moses ndiyo chanzo cha kifo hicho, L.J Ibrahim alieleza juu ya umiliki wa sumu hiyo ulivyokuwa wa kimakini mno ambapo isingewezekana kwa mtu yoyote kuupata pssipo kibali maalum.

    Alizidi kwenda mbali zaidi akaeleza juu ya kutonunuliwa sumu hiyo ndani ya Tanzania zaidi ya kusafirishwa nje ya nchi tena mbali na bara la Afrika, katika maelezo yake hayo alibainisha sumu hizo kwa Tanzania mtu ambaye alikuwa akizimiliki ni mwenyewe aliyezitengeneza  hivyo alihitimisha kwa kumtaja yeye ndiye muuaji mkuu kutokana na ushahidi uliokusanywa. Alieleza Professa Moses Gawaza tangu yalipotokea mauaji hayo hakuwa ameonekana kazini kwake na sumu hizo bado zipo chini ya umiliki wake, mwisho wa maelezo ya L.J Ibrahim  ilikuwa ndiyo mwanzo wa hasira za  wananchi mbalimbali hasa waumini wa dini ya kiislamu na wakristo wa dhehebu la Kiluteri.

   Maandamano makubwa yalifanyika na barabara zote zikafungwa na wananchi ambao walienda kuivamia Maabara ya Umoja wa mataifa wakaharibu vifaa vyote pamoja na kupiga wafanyakazi wake, vurugu hizo zilipozidi  amri kutoka kwa Rais Zuber ilipelekwa kwa IGP Chulanga ambaye aliamriwa aagize vijana wake waweze kudhibiti hilo. IGP Chulanga naye alitoa amri kwa makamishna hatimaye kikosi cha jeshi la polisi cha kutuliza ghasia nacho kikapewa amri kikaingia kazini.

    Askari hao waliingia maeno ya katikati ya jiji yaliyokuwa yakiongoza kwa fujo wakajitahidi kuzuia fujo lakini walishindwa kabisa kuzuia vurugu hizo na wao wakajikuta wakizidiwa na wananchi wenye hasira kali, hata walipochukua uamuzi wa kunyoosha bendera nyekundu juu kisha wakawaua watu wachache ndiyo kwanza hasira za wananchi zilizidi wakajikuta hata nao wakirudi nyuma kwani tayari walishaanza kushambuliwa.

    Vurugu hizo ziliwazidi askari wa kutuliza ghasia na hawakuwa na la ziada ya kukimbia kuokoa maisha yao kutoka kwa wananchi hao, amani ndani ya katikati ya jiji la Dar es salaam wakati Norbert akiwa amelala usingizi mwanana huko Karatu ilikuwa imevurugika. Matukio mbalimbali ya fujo hizo yalikuwa yalirushwa moja kwa moja na vyombo vya habari kupitia kwa kamera zilizokwa zimefungwa kwenye ndege, ilikuwa ni tukio liliogusa hisia za raia wengi wa nchi jirani waliobahatika kuliona kupitia vyombo vya habari.


  MIKOCHENI
 Eneo hili pia hali ilikuwa hiyohiyo ambapo wakazi wengi wa eneo hilo  walikuwa wamejifungia majumbani mwao, nyumba ambayo inatambulika na umma kuwa ni makazi ya Moses tayari ilikuwa imevamiwa na wananchi wenye hasira kali wakiharibu vioo vya nyumba hiyo ya kisasa huku baadhi ya vibaka wakiitumia nafasi hiyo kuiba samani na vitu mbalimbali vilivyomo humo ndani. Uharibifu wa nyumba hiyo ya Moses uliendelea na kuifanya ikawa haina dirisha wala mlango, wananchi hawakuridhika hsta kidogo na uharibifu huo kutokana na kumkosa mhusika waliyekuwa wanamtafuta. Kitendo cha kumkosa Moses waliamua kuichoma moto nyumba hiyo pamoja na magari yake yote ambayo alitumia jasho lake katika kuyanunua, waliiacha nyumba hiyo ikiqa imeteketea moti hadi ikabaki gofu ndiyo wakaondoka eneo hilo.


****

    Matukio yote yaliyokuwa yakitendeka ndani ya jiji la Dae es salaam yalikuwa yakishuhudiwa na mtuhumiwa mkuu Moses kupitia luninga iliyopo ndani  ya sebule ya nyumba ya EASA Kurasini, alikuwa akiangalia tukio hilo pamoja na Dokta Hilaty na Irene ambao walimsikitikia sana  kwa kile kilichompata. Moses aliishuhudia kwa macho yake nyumba aliyoijenga kwa fedha nyingi, alikuwa akiyashuhudia magari yote aliyotumia pesa nyingi katika kuyanunua yakiungua kwa moto. Alibaki akisikitika kupoteza mali zake lakini moyoni mwake alikuwa akihisi afadhali kwa kumuokoa mke wake kipenzi juu ya mabalaa yaliyokuwa yakikaribia kumkumba.

             "Aisee Mose pole sana" Dokta Hilary alimuambia huku akimshika bega lake.

             "Ni jambo la kawaida Hilary  kupoteza mali ndogo mojawapo ya mali  nyingi, poa ni jambo la kawaida kupotezewa heshima mbele waliyokuwa wanakuheshimu. Jambo baya kabisa ni kupoteza moyo na ndiyo nimeliepuka kwa kumsafirisha Beatrice pia na wewe nikakuepusha kwa  kumkomboa Shem Irene" Moses aliongea akiwa ameshika tamaa kwa simanzi kubwa, mawazo yalikuwa yamemzonga kichwani mwake ingawa yeye alichukulia ni jambo la kawaida. Muda huo akiwa kwenye mawazo simu yake ya  mkononi iliita na akaitoa  akaangalia jina kisha akawatazama Dokta Hilary na mke wake.

              "Beatrice huyu nafikiri taarifa kaipata" Aliwaambia kisha akasimama  akapokea simu akaiweka sikioni , "hellow honey.......nipo okay usijali mke wangu kuwa na amani........no! No! Usije mpenzi baki tu everything will be alright.... kuwa muelewa mke wangu ukija utapata matatizo....okay kuwa na amani na umalize ziara yako nitakuja kulufuata mwenyewe, subiri niongee na mama huyu anapiga"

       Moses aliikata simu hiyo kisha akapokea simu yake nyingine ya mkononi akaongea, "Naam mama....nimechezewa mchezo mama yangu sihusiki chochote.....asante sana mama.....Mke wangu yupo salama nafikiri baba atakuambia kila kitu juu yake......asante mama"

    Moses alikata simu kisha akawaangalia Dokta Hilary na mke wake halafu akashusha pumzi, aliamua kujitupa kwenye kochi huku akionekana na mawazo mengi.

            "Shem vipi mbona hivyo?" Irene aliuliza.

            "Beatrice anajua kila kitu kilichotokea huku na alikuwa anataka kurudi lakini nimemkataza" Moses aliongea.

           "Sasa wasiwasi wako ni nini?"  Dokta Hilary aliuliza akamfanya Moses akae vyema kwenye kochi huku akitoa simu yake ya mkononi.

            "Beatrice nimemkataza lakini kwa jinsi minavyomtambua atakuja yule kwakuwa bado haamini, cha kufanya ni kumzuia tu" Moses aliongea huku akibonyeza namba kadhaa kisha akaweka simu sikioni mwake, "hakikisha mke wangu hapati njia ya kurudi Tanzania weka vikwazo kote"
 
    Alipokata simu aliondoka  eneo la sebuleni akiwaacha Dokta Hilary na mke wake wakiwa hawamuelewi kabisa.


****


    GEREZA LA UKONGA
           PUGU

   Hali ya afya ya Ole ilibadilika na kuwa mbaya kwa ghafla tu akiwa yupo ndani ya chumba chake cha gereza, hali hiyo ilisababisha mkuu wa gereza hilo atoe amri ya kukimbizwa  hospitalini kwani hakutaka afe mpaka yeye amuue kwa mikono yake ili ajipize kifo cha mdogo wake aliyeuawa kwa njama zake  Filbert Ole kipindi alipokuwa madarakani.

   Gari aina ya landrover mali ya jeshi la magereza ambayo hutumika kubeba wagonjwa ilitoka ndani ya gereza hilo ikiwa imeongozana na toyota land cruiser mbili zilizojaa maaskari ambazo zilikuwa zimekaa mbele na nyuma ya gari hilo. Msafara huo uliingia barabara ya mwalimu nyerere kwa kasi mno ukawa unaelekea katikati ya jiji, magari mbalimbali yaliyopo barabarani ilibidi yapishe  msafara huo upite kutokana na kasi yake pamoja ma makelele ya ving'ora yaliyokuwa yakisikika. Msafara huo ulipita kwa kasi sana hadi kwenye kituo cha daladala cha njia panda ya Segerea ukakata kona kuingia kushoto.

    Msafara huo kwa kasi ya ajabu ulipita hoteli maarufu ya kulaza magari na watu Ukonga maarufu kama Transit Motel, ulizidi kwenda mbele ukavuka mgahawa maarufu wa Salum machips ns ukawa unaekekea katika eneo ambalo barabara hiyo inakutana na reli ya kampuni ya TRC. Mwendo mkali uliokuwa unaitumia ulisababisha msafara huo ufike mapema kwenye makutano na ulipunguza mwendo ukavuka reli hizo kisha ukaendelea mbele, haukufika mbali msafara huo ulisimama kwenye njia panda baada ya gari kubwa la mizigo kuziba njia kutokana na kuharibika. Askari wenye silaha walishuka wakawa wanalinda  gari lililombeba mgonjwa huku askari wengine wakiwa wamesogea mbele kuangalia tatizo lililokuwa limetokea ndani ya gari hilo la mizigo hadi lisimame.

    Askari hao wakiwa wanalinda eneo hilo hawakutambua kama walikuea wamefanya makosa sana kupita barabara hiyo kutokana na msongamano wa magari  kule Tazara ambapo iliwawia vigumu kupishwa, gari la wagonjwa walilokuwa wanalitumia hawakutambua kwamba lilikuwa lipo wazi sehemu ya chini ambapo kulikuwa kuna mfuniko ukisogezwa tundu linabaki wazi.

    Mfuniko  huo ulikuwa umekaa sambamba na mfuniko wa mtaro mkubwa wa maji upitao ardhini ambapo ndani ya mtaro huo kulikuwa kuna watu chini waliokuwa wakisubiri kwa hamu nafasi hiyo waweze kuitumia. Watu hao walifungua mfuniko huo kisha wakafungua  mfumiko wa chini wa gari wakapuliza dawa iliyowalaza wauguzi wote kasoro dereva wa gari hiyo aliyekuwa amefunga kioo kulichopo nyuma yake ambacho hutumiwa kuwasiliana na wauguzi waliopo nyuma, walimshusha Ole ndani ya gari hilo kisha wakatega bomu wakafunga vilevile wakarudi ndani ya mtaro wa maji machafu wakatokomea bila kujulikana.

    Maaskari wa Magereza waliona ni jambo gumu sana kupita kuendelea kwa muda huo hadi gari hilo la  mizigo liondolewe, hali hiyo iliwafanya warudi kule walipotokea ili wapitie barabara ya Mwalimu Nyerere. Iliwabidi pia wawasiliane na Askari wa usalama barabarani waliopo makutano ya barabara ya Tazara ili waruhusu magari yote ya upande waliopo waweze kupita njia ikiwa tupu.

    Walizidi kuongeza mwendo wa magari yao wakijua wana mgonjaa kumbe walikuwa wamebeba hatari kubwa katika hilo gari la wagonjwa, walipofika makutano ya barabara ya Mwalimu Nyerere kwenye kituo cha daladsla cha Njia panda ya Segerea ndiyo balaa hilo lililokuwa limelala liliamka kwa ghafla.

    Mlipuko mzito ndiyo uliamka ukachukua nafasi yake kweli gari lilikokuwa limebeba wauguzi askari, gari la wagonjwa lilirushwa juu zaidi nap mlipuko huo. Magari ya mengine yaliyosalia yalipoteza muelekeo ambapo la mbele lilipitiliza hadi kando ya barabara na la nyuma lilienda kugonga kituo cha daladala cha njia panda  ya Segerea.

     Raia wa kawaida waliopo eneo hilo hawakuweza kustahimili kubaki na kuangalia tukio hilo, kika mmoja alikimbia  akifuata njia anayoijua yeye au anayoona yeye inaweza kumuokoa. Baadhi yao walikimbia pasipo uelekeo maalum kutokana na kuchanganyikiwa, ilikuwa ni patadhika juu ya tukio hilo ambalo halikuwa na tofauti yoyote na tukio la ugaidi.


****


   Muda ambao kunatokea mlipuko mzito wa bomu kule Ukonga ndiyo muda ambao Norbert anaamka usingizini katika chumba cha nyumba ya wageni alichokodi. Uchovu wa mwili wake tayari ulikuwa umemuisha na sasa alijisikia yupo imara kuliko kawida, njaa pekee ndiyo ilibaki kuwa bughudha kubwa sana kwa mwili wake na ikambidi aende kupata chakula aondokane na bughudha hiyo iliyokuwa ikishambulia tumbo lake.

   Alitumia muda wa robo saa tayari akawa ameshaiondoa bughudha iliyokuwa ikiushambulia tumbo lake na sasa akabaki na bughudha moja ya taka mwili zilizopo mwilini kutokana na kutooga toka usiku uliopita alipojinasua kwenye mdomo wa kifo. Alitumia muda huo  wa mchana kwenda kununua nguo mpya katika duka la nguo hapo Karatu, alioga kisha akabadili  nguo zile pamoja na kuhamisha mapambo yake ya kujihami.

   Majira saa kumi alasiri aliwasha simu yake ambayo aliizima kutokana na kazi zake, muda huo huo alianza safari ya kuiacha wilaya ya Karatu ili aende uwanja wa ndege wa Arusha aweze kurudi jijini Dar es salaam.

    Alikuwa yupo katikati pikipiki ya kukodisha ambayo ndiyo aliona ni njia pekee ya kumfikisha uwanja wa Ndege wa Arusha haraka sana, kutokana na mwendo mkali uliokuwa unatumiwa na dereva wa pikipiki hiyo alitumia saa moja na akawa tayari yupo katika uwanja wa ndege wa Arusha.



TUKUTANE TENA KESHO PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA

HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI



No comments:

Post a Comment