RIWAYA: WAKALA WA GIZA
MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA
SIMU: +255713776843
+255762219759
WHATSAPP: +255713776843
SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA
SEHEMU YA NNE!!
Wakati Moses akiwa anaongea na msaidizi ilikuwa tayari ni mida ya saa tisa na nusu ambao ni muda kutoka kazini kwa baadhi ya wafanyakzi wa mashirika mbalimbali, Norbert muda huo alikuwa yupo ndani ya gari yake aina ya suzuki Escudo akiwa ameegesha kando ya barabara akionekana alikuwa navuta subira ya jambo ambalo lilimfanya awepo hapo.
Alikuwa yupo jirani na bandari inayotumiwa na na boti ndogo zinazosafiri kwenda zanzibar, baada ya dakika takribani kumi yule binti aliyeleta kitabu cha rekodi walipokuja hapo kuulizia kuhusu boti zilizoondoka jana alionekana akitoka ndani ya geti, alikuwa akielekea barabarani akitembea kwa mwendo wa uchovu sana ingawa mapambo yake aliyojaliwa yalikuwa yakitikisiika na kuzidi kumchanganya Norbhert.
"Moyo wee! Usikome mjini hamna mwenye chake" Moyo aliongea kwa sauti ya chini huku akiachia breki ya gari akimfuata binti huyo.
****
Yule binti alikuwa akitembea kivivu sana pembezoni mwa barabara ya Sokoine bila ya kujua kama alikuwa akifuatiliwa na Nobert kwa nyuma yake akiwa na anamtazama kwa uchu sana, alikuja kumuona Norbert baada ya gari ya Norbert kumfikia ikiwa inaenda kwa mwendo wa wastani huku Norbert akimuangalia akiwa anatabasamu usoni. Tabasamu lake ambalo ndiyo sumu kubwa sana kwa mabinti lilionekana kwa binti huyu mrembo ambaye alimtambua Norbert kutokana na umaarufu alionao kama mwandishi wa habri wakujitegemea nchini. Alimtazma Norbert kwa tabasamu aliloliachia na akajikuta akiona aibu sana akatazama pembeni.
"uchovu ni kitu cha kawaida kinachomkuta mtu yoyote akiwa anatoka kwenye mihangaiko mrembo" Norbert aliongea huku akiwa analiachia gari katika mwendo wa taratibu huku akiwa anaenda sambamba na yule binti akionekana kuwa ni msindikizaji wake, maneno yake yalinyamaziwa kimya na binti huyo ambaye alizidi kuongeza mwendo ndipo Norbert akaegesha gari pembeni akamfuata akamshika mkono ili kumzuia asiende.
"We kaka nini jamani?" yule binti alilalamika baada ya Norbert kumvuta mkono na kumzuia asiende mbali zaidi.
"ukiona nakuzuia hivi ujue nakuzuia na mengi binti kukubali kuzuiwa na mimi utakuwa umeepuka mjengi bibie" Norbert aliongea huku akimtazama yule binti usoni.
"mbona sikuelewi unaongea nini?" Yule binti aliuliza baada ya kuona haelewi Norbert anachoongea.
"utaelewa tu ikiwa ukinipa wasaa wa kukuelewesha haya ninayoyaongea" Norbert aliongea huku akimtazam yule binti usoni akionesha anamaanisha kile anachokiongea, binti yule alimtazma Norbert kwa sekunde kadhaa kisha akashusha pumzi halafu akaangalia chini kukwepesha macho yake yasikutane na macho ya Norbert.
"kiufupi we nione kama mwokozi niliyetumwa kuja kukukomboa na kadhua iliyopo mbele yako bibie ikiwa tu utanipa wasaa wa kuyasikiliza maneno yangu ya uokovu" Norbert aliongea huku akiachia tabsamu hafifu usoni akiwa anamtazama sana yule binti.
"kaka yangu ongea nakusikiliza nataka niwahi daladala" Yule binti alimuambia.
"kwanza wokovu wa kwanza wa kuokoka na kadhia ya daladala ushaupata bibie nafikiri uokovu kamili unafuata hivyo vuta subira hutachelewa kufika kwako" Norbert aliongea
"Ayiii! Jamani si useme tu nitachelewa mwenzako daladala za Tandika zinazopita Keko ni chache sana kaka yangu, hebu ongea basi niwahi kabla usafiri haujawa wa tabu zaidi" Yule binti aliongea
"Ndiyo maana nikakuambia hata uokovu wa kupanda daladala umeupata kwani usafiri wangu unapita hapo unapoelekea hivyo ondoa wasi kabisa leo hutapata tabu ya kutumia nguvu katika kupata usafiri" Norbert aliongea huku akimtazma yule binti ambaye aliona ni bahati kutopanda daladala kwa siku hiyo kutokana na kubainishiwa juu ya usafiri Bwana mkubwa ulikuwa ukipita maeneo hayo. Alishukuru kimoyomoyo kwa kupata bahati ya kubana bajeti yake asipande daladala .
"Nafikri leo ni siku nzuri ya kuwahi kupumzika mapema nyumbani kwako kwa uokovu huu wa awali naweza nikakusogeza hapo unapoelekea bibie" Norbert aliongea huku akiachia tabasamu lake ambalo ni ugonjwa tosha kwa mabinti, tabasamu hilo lilimfanya yule binri ashindwe kumtazama machoni kwani alihisi hali ya tofauti alipomtazama Norbert usoni.
"Nitashukuru" Hatimaye yule binti alikubali kupanda katika usafiri wa Norbert.
"Ni vyema, Norbert naitwa wewe je?" norbert alijitambulisha huku akimpa mkono akihitaji kuju jina ya yule binti.
"nakujua vema,Josephine" Yule binti alimpa mkono huku akitaja jina lake.
"ok unaweza kuingia kwenye uokovu wako wa awali" Norbert alimuambia Josephine huku akimuonesha mahala gari lilipo, Josephine hukujibu kitu zaidi ya kumtazama Norbert kwa jicho linaloashiria yupo tayri kuingia kwenye gari lake. Jicho hilo lilimfanya Kidume atembee hadi ulipo mlango wa pili wa abiria kwenye gari lake akamfungulia Josephine ambaye alimfuata Norbert kwa nyuma na akaingia ndani ya gari baada ya mlango huo kufunguliwa, ilikuwa ni hatua ya awali ya mafanikio aliyoipata mzee wa mabinti baada ya kuweza kumshawishi yule binti aingie ndani ya gari yake.
Furaha iliyojificha ndani ya moyo iliendelea kuwepo na aliona ameanza kupata ushindi katika hatua yake ya awali kumfuata Josephine, alizunguka upande wa dereva akaingia akaliongoza gari kuingia barabarani akafuata barabara ya Sokoine hadi stesheni akaingia upande wa kushoto kuifuata barabara iendayo katika mzunguko wa clock tower. Njiani Norbert aliendelea kuongea maongezi ya kawaida yenye kufurahisha ambayo yalimfanya yule binti atabasamu muda wote, alikuwa akiongea huku akiwa hajsahau dhumuni lake liliolomfanya amfuate bunti huyo kule kazini kwake.
Walipofika eneo la karibu na kwenye mataa ya Kariakoo mtaa wa Gerezani walikuta foleni kubwa ambapo ndiyo Norbert alitumia muda huo kuanza kutimiza kile kilichomfanya apoteze muda wake kumsubiri binti tangu alipomuona alipokuja kiupelelzi zaidi.
"Josephine umeona sasa umepata uokovu mdogo hadi sasa nafikiri bado uokovu mkubwa haujaupata" Norbert aliongea wakati wakisubirio magari yaweze kuruhusiwa.
"upi huo Norbert?" Josephine aliuliza.
"Huo uokovu mkubwa zaidi kupita yote unatakiwa uwe nayo katika maisha yako na mimi ndiyo nimetumwa kuja kukupati uokovu huo" Norbert aliongea huku akitabasmau na kusababisha Josephine aone aibu na kuishia kucheka akaangalia pembeni.
"Mh1 Nawe nawe unataka kuanza vituko vyako nicheke tu maana hapa mbavu zinaniuma kwa jinsi ulivyokuwa ukinichekesha" Josephine aliongea huku akicheka kutokana na kufurahishwa na vituko vya Norbert alivyokuwa akivionesha ndani ya gari hilo kabla hajafika hapo kwenye mataa.
"Huu wakovu nafikri utakuwa ni tulizo kwa hizo mabvu zinazouma kwa ajili ya kucheka bibie, utegee sikio wala hutapata maumivu ya kuumia mbavu kama mwanzo" Norbert aliongea huku akimtazama Josephine kwa umakini sana.
"Mh! Haya" Josephine aliguna akionekana yupo tayri kuusikiliza wokovu huo anaoambiwa na Norbert ingawa hakutambua ni wokovu wa aina gani, alimtazama Norbert akionesha nataka kusikiliza kile anchotka kuambiwa na tabasamu la Norbert ndiyo lilizidi kumpa ari ya kutaka kusikiliza kile anachotaka kuambiwa na Norbert.
Hakujua kama yupo anaongea na bwana wa mitego ambaye ni nadra sana mtego wake kukosa malengo akiutega, hakujua kama naongea na bingwa kudungua ambaye ni nadra sana kukosa shabaha na anapodungua mioyo ya kina dada warembo. Hakujua anaongea na simba dume mwenye njaa ambaye hana jike wa kuweza kumletea chakula hivyo huwinda mwenyewe kutafuta chakula, utanashati wa Norbert alionao na mavazi anayovaa ambayo yanaonekana kumkaa sana ndiyo vilizidi kumpa hamasa zaidi Josephine ya kumsikiliza kile anachokisema. Uzuri wa sura alionao Norbert nao ulizidi kumpa hamsa huyo binti ya kumsikiliza na uchangamfu pamoja na sifa nyingine alizonazo zilizidi kumvutia.
"kwa muda wa siku nne nimeagizwa nije kukuletea uokovu katika moyo wako ambao ulikuwa ni muhimu sana kuwa nao, siku zote hizo nilikuwa nikija eneo la jirani na kazini kwenu nikiwa ninavuta subira zaidi ili nikupatie wokovu huo lakini aliyenituma alizidi kunihimiza nifanye hima nikukomboe kutokana na balaa ambalo lingekufika ndiyo maana leo nikakusubiri hadi unatoka nikaweza kukupa uokovu wa awali kabla ya kukupa uokovu kamili" Norbert aliongea huku akimtazama kwa umakini yule binti tena aliongea kwa hisia aonekane kile anachoongea ndiyo anahokimaanisha.
"Norbert wait umesema umetumwa uwahi ili balaa lisije likanifika. Nani aliyekutuma na balaa gani linataka kunifika" Josephine aliuliza akiwa hajaelewa kauli alizozitumia Norbert.
"Aliyenituma hayupo mbali na hapa bali yumo amejificha ndani ya ya sehemu ya kifua changu na si mwingine bali ni moyo wangu tangu kwa mara ya kwanza nilipokuona alinihimiza nikuokoe na balaa la kutekwa na wale wasio na upendo kwako na nikupe sehemu ya hifadhi katika chumba cha upendo wangu upate uokovu wa kudumu Josephine,ndiyo umenifanya nifunge safari hadi hapa nikakupa wokovu wa kukuokoa usipate na kadhia ya kugombania daladala ambayo huleta maafa mengi kwa watumiaji ikiwemo kuibiwa vitu muhimu" Norbert alitiririka maana ya maneno aliyokuwa anampa Josephine ambayo yalimfanya Josephine aangalie pemebni kwa iabu.
Norbert alitaka kuongeza neno jingine baada ya kuona aibu iliyomuingia Josephine lakii sauti ya honi ya gari iliyopo nyuma ilimshtua na ikamfanya aangalie mbele kwa haraka baada ya kushtuliwa na honi hiyo, alipotazma mbele aliona magari yameanza kuondoka ndipo akabaini kuwa Askari wa usalama barabarani alikuwa ameruhusu magari tayari na hapo akaachia breki ya gari akaliondoa kwa kasi ili asizidi kukera watu waliopo nyuma yake kwenye foleni hiyo.
Ndani ya nafsi yake aliachia tusi zito kwa yule Askari wa usalama barabarani kwa kuruhusu magari kwani ulikuwa ndiyo muda muafaka wa kuweza kumchombeza Josephine, aliweka umakini mbele akiwa anawahi foleni nyingine iliyopo katika makutano ya barabara yaliyopo Keko. Muda huo akiweka yupo makini kwa kucheza na usukani hakuwa akitambua kuwa Josephine alikuwa akimtazama na alipokaribia kwenye makutano ya barabara yaliyopo keko kwenye foleni ndipo alipobaini kuwa alikuwa akitazamwa.
Alipogeuza jicho kumtazama Josephine baada ya kumbaini alikuwa akimtazama alimfanya Josephine aingiwe na aibu ambapo alitazma kando kutokana na kutostahimili kuweza kutazmana na macho ya Norbert.
"Bibie nadhani umenisikia juu ya wokovu niliyokuwa nahitajika kukupatia na ndiyo huo, sasa nafikiri upo tayari kuupokea' Norbert alimuambia Josephine huku akimtazama kwa jicho lenye ujumbe mzito sana.
"Norbert" Josephine aliita akiwa ameangalia pembeni baada ya kusikia maneno ya Norbert.
"Naam nakusikiliza" Norbert aliitikia
"Aaah! Hamna" Josephine alijikuta akibabaika baada ya kuita jina la Norbert.
****
HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI
UPANGA
DAR ES SALAAM
Wakati Norbert akiwa yupo na harakati za kufuata mrembo Josephine upande mwingine katika hospitali ya taifa Muhimbili katika wodi mojawapo ya wagonjwa kulikuwa kuna watu wawili tu walikuwa wamelazwa huku wakiwa na pingu mguuni kila mmoja, muonekano wa watu hao walikuwa ni watuhumiwa kabisa kwani watuhumiwa ndiyo hulazwa wakiwa na pingu ili kuwazuia wasitoroke.
Walikuwa ni watu wenye miili mikubwa ya kimazoezi ambao mmoja alikuwa amefungwa bendeji ngumu mguuni na mwingine alikuwa amelazwa huku ubavu mmoja ukiwa juu akiwa amefunikwwa shuka,pembeni yao kulikuwa kuna askari mwenye silaha akiwa anaonekana yupo makini kulinda kuhakikisha watuhumiwa hao hawatoroki. Ulinzi wao waliekewa ulikuwa ni ulinzi dhabiti sana kimuonekano kutokana na aina ya ya tuhuma waliokutwa nayo, askari polisi wengine wanaolinda eneo hilo walionekana kuwa ni makini sana kiasi kwamba eneo la wodi hiyo likawa linawatisha hata wauguzi waliokuwa wakiwahudumia watuhumiwa hao
Upeo wa macho na akili za maaskari hao katika kuimarisha ulinzi katika eneo hilo ulikuwa umezidiwa na upeo na akili za mtu mwingine tofauti ambaye ana ujuzi kuliko wao, waliendelea kufanya ulinzi wao uliozidiwa daraja na umakini wa mtu mwingine tofauti ambaye alikuwa anawatazama umakini wao ulivyo. Hakika akili kila mtu anazo sawa na mwingine ila hutofautiana katika kuzitumia hizo akili ndiyo maana tunaonekana hatupo sawa kiakili kabisa, hata hawa maaskari walikuwa na akili sawa na mtu anayewatazama umakini wao ila walizidiwa jinsi ya kuzitumia hizo akili.
Nusu saa baadaye muuguzi wa kiume alifika katika eneo la wodi hiyo akiwa amebeba kisahani chenye dawa pamoja na mipira ya mikononi, maaskari walipomuona muuguzi huyo waliangalia saa zao wakampekua ili kuhakikisha hana chochote cha hatari wakamruhusu aingie ndani ya wodi hiyo. Muuguzi huyo aliingia ndani ya wodi hiyo akakutana na askari mwingine aliyepo hapo ndani ambaye alimpekua kisha akakaa kwenye kiti akimuacha ahudumie wagonjwa, askari huyo alimuangalia Muuguzi huyo kwa umakini akiwa anaanza kuhudumia wagonjwa huku mikono yake ikiwa inachezea bunduki uake aina ya SMG. Kutazamwa huko na askari kulimfanya yule mhudumu asite kufanya kazi yake akabaki anamtazama Askari huyo kwa macho yaliyojaa uoga.
"Aisee we vipi hebu fanya kazi yako uende" Askari huyo aliongea kwa ukali.
"samahani Afande sauti ya juu hairuhusiwi eneo kama hili pia mimi ni raia wa kawaida tu ninayeuguza wagonjwa tu sasa kitendo cha kunisimamia na bunduki eneo hili jua unanifanya nisiweze kufanya kazi yangu kwa ufanisi unaotakiwa. Kwa uoga niliokuwa nao nikiona hiyo silaha na magwanda yako na jinsi unavyonitazama jua utanifanya hata nizidishe kiwango cha dawa kwa mgonjwa akapoteza maisha wakati ni muhimu kwenu kuwa hai, afande kama hutojali naomba unisubiri nje ya mlango niwahudumie hawa wagonjwa kwa ufanisi" Yule Muuguzi aliongea akionesha wazi kuwa ana hofu sana, maneno yake yalimuingia yule askari aliyekuwa ana jukumu la kulinda wagonjwa hao ndani ya wodi hadi akanyanyuka akaelekea nje akimuacha Mhudumu afanye kazi yake. Maneno yaliyomlainisha askari yule yalikuwa ni wasaa mkubwa kwa Mhudumu yule kufanya kazi iliyomleta hapo ndani ya wodi hiyo, aliwaamsha wagonjwa hao ambao walishtuka sana baada ya kumuona aliwa eneo hilo.
"Panther" kwa pamoja walitamka kwa sauti ya tabu sana.
"Shiiiii! Mbona wajinga sana nyinyi niliwaambiaje?" Yule mhudumu aliuliza kisha akaendelea kuongea, "yaani mnaenda kutumia Klorofomu katika kuwanasa wale watu kwanini msitumie sumu kabisa muwaue, klorofomu si nusu kaputi ya kufanyia upasuaji kama wana maji si mnatambua haifanyi kazi sehemu yenye maji"
"Mkuu sisi tulitaka tuwatie nguvuni kwanza halafu ndiyo tuwamalize, sumu ya gesi tuliyokuwa nayo ni hatsri sana ingesambaa eneo zima na hatukuwa na vifaa vya kujizuia" Mmojawapo aliyevunjika mguu aliongea mbele ya Panther.
"Ok my boys siyo neno tena nafikiri nitafute njia ya kuwakomboa eneo hili" Panther aliongea huku akitabsamu na kusababisha vijana wake nao watabsamu pia, alikuwa tayari ameshavaa mipira ya mikononi.
"sawa bosi tunakutegemea kwa hilo sana maana tukiingia rumande hatutatoka, gari yetu imekutwa na MP5 mbili" Yule mwingine aliyevunjika mbavu alioongea kwa tabu sana huku akisikia maumivu kwa kila anavyoongea.
"Worry out my boys, give me your hands tupo pamoja" Panther aliongea huku akimyooshea mkono kila kijana wake akitaka wampe mikono yao kuashiria kuwa wapo pamoja katika hili. Vijana wale walimpa mikono yao wote kwa pamoja ambapo mmoja alishikana naye kwa mkono wa kushoto na mwingine kwa mkono wa kulia wakiwa na tabasamu pana ambalo halikudumu hata ndani ya nusu dakika kwani wote waliohisi kutobolewa na vitu kwenye viganja vyao. Walikuwa wamekamatwa kwa nguvu sana na mikono ya Panther iliyojaa nguvu nyingi sana, Panther alipoachia mikono yao kila mmoja alikuwa na damu kwenye kiganja chake huku akiugulia maumivu kwani walihisi maumivu makali sana baada ya kutobolewa.
"Stupid! Mnadhani mtapona mbele ya uzembe wenu kwenye kazi ya Panthers. Yaani mnabeba MP5 silaha ya kivita katika mission ndogo hivyo, sasa onjeni uchungu wa sumu ya Quantanise ikitembea kwenye miili yenu kuwamaliza, mna dakika moja tu ya kupumua" Panther aliongea kwa sauti ya chini ambyo ilikuwa imejaa ukali sana.
Miili ya wale vijana wake taratibu ilianza kubadilika rangi na kuwa ya rangi nyekundu kuanzia walipotobolewa na sindano za mipira ya mkononi aliyovaa Panther, rangi nyekundu hiyo kwenye ngozi yao ilikuwa ikisambaa kwa kasi sana mithili ya moto wa nyikani unavyosambaa kwenye nyasi na ndani ya sekunde kadhaa ilikuwa imeshasambaa mwili mzima na huo ndiyo ukawa mwisho wa maisha yao na Panther alitoweka eneo hilo kwa nja nyingine tofauti na mlangoni.
***
Askari aliyekuwa anawalinda wale vijana alikuwa amekaa nje ya wodi hiyo pamoja na maaskari wenzake na hapo ndipo akakumbuka alisahau simu yake katika meza ndogo iliyopo humo ndani na ikamlazimu aingie ndani kwenda kuifuata kwa haraka ili ampishe mhudumu aendele kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi, alifungua mlango na akaingia ndani akakutana na hali ambayo hakutarajia kama atakutana nayo kwa muda huo. Muguzi aliyekuwa akifanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa hao hakumkuta na badala yake alikuta kisahani tu cha dawa alichokuwa amekibeba kikiwa kipo juu ya meza ndogo inayotenganisha vitanda vya wagonjwa hao, miili ya wagonjwa aliiona ikiwa ina dalili ya kutokuwa na uhai kabisa na ilikuwa imebadilika rangi na kuwa ya rangi nyekundu ambayo inaonesha kabisa kuwa damu imeviria juu ya ngozi mwili mzima.
Askari huyo kwa haraka alichukiua silaha yake akaitoa usalama akawa anasogea upande waliokuwa wagonjwa akiangaliwa kila pande na hapo ndipo akashududia sehemu ya mfuniko wa dari ikiwa haijafungwa vizuri, hali hiyo ilimpa uhakika kwamba aliyeingia ndani ya wodi hiyo hakuwa Muuguzi bali ni mhalifu mwingine aliyekuja kupoteza ushahidi wa uwepo wa watu hao. Askari huyo kwa haraka zaidi aliwataarifu wenzake juu ya kile alichokiona mule ndani kupitia simu ya upepo.
Msako mkali ulianza mara moja ndani ya wodi za jirani ambazo dari hilo lilikuwa na mifuniko wa kutokea ambayo ingeweza kumpa nafasi mtuhumiwa kutoka ndani ya dari na kushuka chini, waliingia ndani ya wodi zote lakini waliambulia patupu kwani hapakuwa na dalili za uwepo wa mtuhumiwa waliyekuwa wanamtafuta. Mwisho kabisa walieleka katika Maliwato ambayo ipo mbali kidogo kutoka kwenye wodi waliyokuwa wamelazwa watuhumiwa waliokuwa wanawalinda ili waweze kukagua napo, kwa kasi walifika kwenye Maliwato hiyo ambapo walimkuba kikumbo mzee mmoja aliyezeeka aliyekuwa anatoka huko chooni alimanusura aanguke chini.
"Samahani mzee wangu" Askari mmoja aliomba radhi kwa haraka kisha akaingia pamoja na wenzake humo ndani ya Maliwato na wakaanza kukagua chumba kimoja baada ya kingine vya vyoo ili wahakikishe wanamtia mtuhumiwa nguvuni, ukaguzi wao uliendela kwa kasi ya ajabu hadi walipofikia kwenye mabafu ambapo ndipo walipopigwa na butwaa baada ya kuona zile nguo alizovaa yule mhudumu pamoja na viatu vyake vikiwa vipo katika chuma la kuwekea nguo bafuni na sehemu ya dari ikiwa ipo wazi.
"Wait" Alisema askari mmoja kisha akafikiria na hatimaye akasema,"jamani ni yule mzee tuliyempush mlangoni maana hakuna mtu mwingine humu mwingine humu na yeye ndiye aliyetoka humu".
Kauli hiyo iliwazindua wote kwa pamoja wakatoka nje wote wakakimbilia nje kumtafuta yule mzee huku wakiuliza baadhi ya watu juu ya yule mzee alipoeleka na walitaja muonekano wa huyo pamoja na jinsi alivyovaa. Majibu ya kila waliyemuuliza yalikuwa ni kutomuona mzee huyo na hapo maaskari hao wakazidi kupagawa na jinsi ambavyo mtuhumiwa wanyemtafuta alivyowapiga chenga ya kuwatoroka katika mazingira ambayo hawakuyaeleweka.
Hawakutambua kwamba Mtu waliyekuwa wanamtafuta alitumia akili zaidi yao ndiyo maana akawaacha kwenye mataa wakiwa wanashangaa zaidi, hakika walizidiwa ujanja wa kila namna na mtuhumiwa wao aliyekuwa amefanya tukio ndani ya wodi waliyokuwa wanailinda kutokana na uwepo wa watuhumiwa waliokuwa na shaka nao.
****
Muda ambao askari wakiwa wanachezeshwa kandanda la kutumia ubongo na mtuhumiwa aliyekuwa amewaachia maafa ya kuwaua watu waliopewa jukumu la kuwalinda, Norbert tayari alikuwa ameshafika Keko na alikuwa ameegesha gari pembeni akiwa yupo anaongea na Josephine ambaye alikuwa ameshafika mwisho wa safari yake. Alikuwa tayari ameshafanya kazi nzito ya kumvua pweza mkorofi katika kina kirefu cha bahari na alikuwa na anapima kama pweza yule alikuwa na dalili ya uzima ili asije akamletea athari yoyote ile, alikuwa tayari ameshalainisha ugumu wa moyo wa Josephine kwa mbinu zote za hali ya juu alizonazo katika kulainisha mioyo ya kinadada.
"Norbert bwana mbona mapema sana kuhusu hili suala?" Josephine aliongea huku mikono yake ikiwa inachezea kucha zake nadhifu zilizo na matunzo ya hali ya juu sana.
"Hayana wakati wala ratiba useme yamewahi sana cha msingi ni kufungua mlango wa moyo wako uruhusu yaingie ndani yako" Norbert aliongea huku akipeleka mkono wake kushika viganja vya Josephine,alipogusa alikutana na ulaini wa ngozi ya Josephine ambao ulikuwa usio wa kawaida ambao ulizidi kumfanya aone hakukosea kuja kuleta maombi kwa binti huyo ili aweze kuijaribu ladha iliyokuwepo kwa binti huyo.
"Basi tufanye kesho Norbert leo muda tayri umeenda jamani" Josephine aliongea.
'Ok, no problem nakupa muda wa kulifikiria zaidi suala hili ila nilikuwa nina obmi jingine" Norbert aliongea aliongea kisha akaendelea,"nikiwa kama muokozi naomba unipatie simu yakko mara moja kama hutojali".
Ombi hilo lilimfanya Josephine amuangalie Norbert kwa sekunde kadhaa kisha akamptia simu yake ya kiganjani,Norbert aliichukua simu hiyo akaandika namba zake za simu kisha akapiga ambapo simu yake ilianza kuita. Alikata simu kisha akaihifadhi namba hiyo kwenye simu ya Josephine akamrudishia huku akiwa anatabasamu.
"sijui nimefanya vibaya?" Alimuuiza Josephine huku akimpatia simu yake.
"No hujafanya vibaya jamani" Josephine alijibu.
"Ok nadhani tomorrow tutaonana" Norbert aliongea huku akimpatia Josephine ili waagane, Josephine alipompatia mkono aliuvuta karibu akaubusu halafu akamtazama usoni.
Ilikuwa ni tendo ambalo halikutarajiwa na Josephine na alibaki akimtazama Norbert kwa mshangao kisha akatabasamu akaangalia pembeni kwa aibu.
ITAENDELEA!!
HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI