Tuesday, November 22, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA TISA




RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA



SEHEMU YA TISA!!

             "Mama" Moses aliita kisha akaendelea kuonges, "pole sana mama yangu".

    Maneno hayo yalimfanya mke wa Jenerali Kulika aanze kulia kwa uchungu huku akitamka maneno yenye kumlaumu muumba kwa kumchukua mume wake kipenzi, wote kwa pamoja walimuacha alie mpaka akanyamaza akawa kainamisha uso wake kwa majonzi.

               "Mama naamini Jenerali hakufa  hivihivi tu bali kuna mtu ndiyo chanzo naamini hivyo, imani yangu inaweza ikapata uhalisia kuwa ni kweli ikiwa tu nitasikia kidogo kutoka kwako na nikakusanya na kile nilichokipata kwingine kibaini ukweli" Norbert aliongea kisha akatoa simu yake ya mkononi akabonyeza kitufe cha kurekodi.





_______________TIRIRIKA NAYO

    Mke wa Jenerali Kulika alipoambiwa kuhusu hilo alianza kulia upya tena zaidi ya mwanzo Mke wa Jenerali Kulika alianza kuvuta picha tukio aliloliona usiku uliopita na akajikuta hata akishindwa jinsi ya kulielezea na akazidi kulia. Iliwabidi wambembeleze kwa muda mrefu na wakisitisha kumhoji mwanamke ambaye weupe wake tayari ulikuwa ushajenga rangi nyekundu juu ya ngozi kwa kulia, alipobembelezwa na kunyamaza Mke wa Jenerali Kulika ndipo alipopata wasaa wa kuweza kuongea kile ambacho Norbert na Moses walihitaji kukijua kwa muda huo.

               “Mume wangu nakumbuka vizuri ni jana tu ametoka safari ya nje ya nchi na alikuwa ameenda kiofisi zadi, nilikuwa na hamu sana na mume wangu kutokana siku zote hizo kutomuona akiwa nje ya nchi kwa ajili ya safari hiyo ya kikazi. Usiku wa jana tulilala pamoja vizuri hadi muda ambao simu yake ilipoita ndiyo alipotoka kwenda kuzungumza nayo, muda mfupi baadaye baada ya kutoka kwenda kuzngumza nayo nilishuhudia mlango wa chumbani ukifunguliwa na kisha mkono wa mtu ambaye niliamini ni mume wangu ulichomoa funguo kwenye kitasa kwa ndani. Kutokana na usingizi niliokuwa nao niliamini kabisa alikuwa ni  mume wangu anachukua funguo hiyo kwani ilikuwa si mara ya kwanza kwa yeye kuchukua ufunguo akiwa ameamka usiku ili aende kufungua chumba chake cha vitabu na nyaraka zingine muhimu sana” Mke  wa Jenerali Kuiika aliongea.

                  "Kwanini unasema mwanzoni uliamini je hivi sasa huamini kama alikuwa ni mume wako?" Moses aliuliza.

                   "Ndiyo  hakuwa na sikuweza kumtilia maanani kutokana na usingizi nilionao na pia  mume wangu hana mchoro wa kipepeo mkononi" Alijibu.

                 "Je baada ya kuchukua ufunguo wa mlnago alifanyaeje?"Moses aliuliza tena

                   "Baada ya kuchukua ufnguo wa mlangoni nilisikia mlio wa ufunguo ukichomekwa kwenye kitasa cha nje kisha ukafungwa kabisa, sikuwa na wasiwasi nilijua kwa muda huo huenda ni yeye lakini asubuhi hii ndipo nilikumbuka kuhusu ule mchoro nikajua kabisa hakuwa mume wangu yule aliyefungua mlango ule" Alijibu

                   "Baada ya kukumbuka mama ulichukua hatua gani?" Norbert aliuliza.

                      "Niliamka kitandani baada ya kukumbuka suala hilo mume wangu hakuwepo na sikuwa na imani nalo kabisa niliamini ulikuwa ni wasiwasi wangu tu. Nilipoenda mlangoni kwenda kuufungua nilibaini ulikuwa umefungwa kwa nje" Alieleza

                    "Enhe ikawaje baada ya hapo?" Norbert aliuliza

                       "Nilimuita kwa nguvu Baba Dorry nikimuambia anifungulie mlango nikiamini alikuwa amefunga kwa kujisahahu lakini sikuitikiwa, muda huo nikasiikia sauti ya Dorry na wadogo zake wakimuambia baba yao pia awafungulie mlango hapo ndipo nikahisi kulikuwa na hali tofauti ndani ya nyumba" Alieleza.

                      "ulikuja kujua vipi kama kumetokea tukio ndani ya nyumba yako?" Norbert aliuliza.

                      "Nilikuja kujua kama kumtokea tukio ndani ya nyumba yangu baada ya kutoitikia na mume wangu kwa mara zote nilizokuwa nikigonga mlango na kumuita jina lake na kumuhimiza afungue mlango,nilienda dirishani na kuchungulia eneo la getini labda vijana wake watanisikia hapo niliwaona wote wakiwa wamelala chini kila mmoja wakiwa hawajitambui kuashiria kulikuwa najmbo lisilo la kawaida. Sikuweza kuvumilia nilipoona hali hiyo niliamua kupiga kelele kwa nguvu  sana hadi majirani wakanisikia nidyo waliyokuja kutoka msaada wa kunifungulia mimi na wanangu" Alieleza

                      "Je watumishi wa ndani wa nyumba hii nao hawakuwepo siku iliyopita?" Moses aliuliza

                     "Wote walikuwepo baba yangu ila walikuwa wamefungiwa kama nilivyofungiwa mimi na wanangu isipokuwa hawakuwa na fahamu hadi muda huo ambao tunafunguliwa na majirani" Alijibu, baada ya kujibu swali hilo Moses na Norbert walitazamana kwa muda wa sekunde kadhaa katika nyuso zao kisha wakaafikiana jambo kwa ishara.

                       "Ok mama yetu asante kwa maelezo yako tukikuhitaji tutakuja kwa mara nyingine ilimradi tu mhalifu afikishwe katika chombo cha sheria,sote tuna uchungu hapa kwa kumpoteza  kamanda mwenye msimamo ndani ya nchi hii. Tupo pamoja na wewe hadi tunampata huyo mhusika aliyesababisha haya" Norbert aliongea huku akimpatia mkono mke wa Jenerali na Moses naye akampatia hivyo, wote kwa pamoja walitoka humo chumbani wakiwa pamoja na M.J Belinda.

      Walipofungua mlango wa kutoka nje walimuona Benson ambaye awali walikuwa wamemuacha nje akiwa anaongea na Koplo usu ambaye alikuwa yupo mlangoni mwa chumba hicho, alipowaona alitoa tabasamu huku akimuangalia kila mmoja wao na akawa amesitisha kuongea na Koplo Usu huyo wa kike aliyekuwa akiongea naye kwa muda huo. Koplo Usu huyo naye alishtuka alipomuona mkuu wake akiwa amemkuta anaongea na Benson katika eneo hilo, wote wAlibaki wakiwatazama kina Norbet baada ya kutoka humo ndani ya chumba cha mke wa Jenerali Kulika.

                     "Lance koplo" M.J Belinda alimuita yule Koplo usu

                    "Afande" Koplo usu aliitika huku akitoa heshima.

                       "Kaendelee na kazi yako ndani" M.J Belinda alitoa amri huku akimtazama Benson kwa umakini, Benson alirudishha tabasamu kwa kutazamwa huko na macho ya kirembo ya M.J Belinda ambaye hakutabsamu badala yake alikwepesha macho kisha akawatazama Norbert na Moses.

                      "Tunaweza tukaenda" Aliwaambia huku akitembea kuufuata ukumbi huo mwemba hadi mwisho kabisa ambapo kulikuwa na chumba kingine, walipofika kwenye chumba hiko M.J Belinda alifungua mlango akaingia ndani akiwaacha Moses na Norbert nje wakiwa wanamsubiria yeye kama alivyowasihi wamsubiri. Alitumia muda mfupi humo ndani ya chumba ambapo alirejea akiwa ameongozana na askari mwingine wa kike  aliyekuwa amevaa sare za JWTZ za ofisini akiwa na cheo cha sajini(V tatu).

                        "Kutana na Norbert Kaila mwandishi wa habari maarufu wa makala za kufichua maovu" M.J Belinda alimwambia Sajini huyo wa kike ambaye alitoa tabasamu kisha akampatia mkono Norbert ambaye aliupokea mkono huo akamtekenya kwenye kiganja cha mkono kisha akambania jicho wakati anasalimiana naye.a

                         "Pia kutana na Professa Moses Lawrence Gawaza kutoka UN laboratory, wote kwa pamoja wanataka kufanya mahojiano na Dorry hivyo naomba usubiri hapa mlangoni na uhakikishe mtu haingii ndani wala kusogelea huu lango hadi sisi tutoke. Tunaelewana!" M.J Belinda aliongea kumtambulisha Moses ambaye pia alipeana mkono na Sajini huyo wa kike ila hakufanya kituko kama alichofanya Norbert baada ya kupewa mkono na Sajini huyo, M.J Belinda pia alimpa maelekezo mapya Sajini huyo pindi atapokuwa yupo ndani kutokana na kutokuwa na imani na watu wote waliokuwa wapo humo ndani ya nyumba hiyo hadi huo ambao wanaingia.

      Wasiwasi wa kuwepo msaliti ndani ya eneo hilo ndiyo ulikuwa umemtawala ndani ya moyo wake muda huo baada tu ya kungia ndani ya eneo hilo kutokana na kushuhudia kitu ambacho hakuwa anakielewa kabisa tangu aingie ndani ya ukumbi huo ambao ulikuwa na vyumba vya wanafamilia wa Kamanda wake mkuu, hivyo maelekezo juu ya kutoruhusu mtu kusogea katika eneo hilo yalikuwa ni muhimu sana kwa Sajini aliyekuwa na jukumu la kulinda chumba cha watoto wa Jenerali Kulika katika kipindi hiko ambacho walikuwa na wasiwasi muuaji hakuwa mbali na maeneo na huenda hata kwenye msiba huo alikuwa amekuja kutokana umaarufu alionao Jenerali Kulika.

       M.J Belinda pamoja na kina Norbert waliingia ndani ya chumba hicho ambapo ndani kulikuwa na binti wa takribani miaka ishirini na ushee kidogo aliyekuwa amekumbatiwa na wadogo zake ambao wote walikuwa wakilia tu muda wote. Binti huyo ndiye aliyekuwa mtoto mkubwa wa Jenerali Kulika,macho ya binti huyo tayari yalikuwa yamebadilika rangi kwa kulia muda mrefu kutoka na uchungu alionao kwa kufiwa na baba yake

                         "Dorry antii" M.J Belinda alimuita biti huyo huku akiketi kitandani jirani naye, Dorrry aliposikia kuitwa huko na M.J Belinda alimkumbatia kwa haraka sana huku akilia kwa uchungu sana akimtaja baba yake akilalamika kwanini alikuwa amemuacha mwenyewe. Ilimchukua muda wa ziada kuanza kumbembeleza hadi aliponyamaza ndipo alipoambiwa lengo la uwepo wa Norbert na Moses ndani ya eneo hilo kwa muda huo ambao alikuwa na majonzi ju ya kifo cha baba yake, Dorry kwa kuwa alikiuwa na uchungu na mapenzi makubwa sana kwa baba yake alikubali kutoa ushirikiano huo kwa watu hao ambao walikuwa wamekuja katika eneo hilo kumhoji kama walivyomuhoji watu wengine waliokuwa wametangulia kabla yao.

                         "Binti unaweza ukatuambia jana usiku mlipolala hadi inafika muda wa asubuhi ilikuwaje"" Moses aliuliza.

                        "jana usiku baba yatu alikuwa amerudi kutoka safari na tulikuwa tumemkumbuka sana hivyo tulikaa naye kwa muda mrefu hadi ulipofika muda wa kulala ndiyo akaenda kulala chumbani kwake pamoja na mama" Dorry alieleza

                      "Enhe ikawaje?" Moses aliuliza tena.

                         "Nasi tulikuja kulala chumbani kwetu hadi kama kawaida, sisi tulikuwa na kawaida ya kusahau kuzima taa ambapo Baba yetu huwa anakuja kuizimma tukiwa tumelala. Usiku muda ambao nilishtuka kutoka usingizini nilisikia mlango wa chumbani kwa baba ukifunguliwa nikajua kabisa ni yeye maana huwa ana kawaida kutoka usiku na kuelekea sebuleni au makataba yake akiwa anaongea na simu muhimu au ana kazi ambayo imemjia kwa ghfla usiku huo. Nilisikia mtu akiwa anashuka ngazi za kuelekea sebuleni na kisha baada ya muda mfupi nilisikia sauti ya kufunguliwa mlango wa chumbani kwa baba nikajua ni mama alikuwa natoka hivyo sikuwa na wasiwasi kabisa,mlango huo ulifungwa tena  na hapo  baada ya muda mfupi nikashuhudia mlango wa chumbani kwetu ukifunguliwa. Muda huo mama alikuwa hapendi sana kutuona watoto wake tukiwa macho hivyo ili asijue niko macho niliamua kujifunika shuka hadi usoni nikiamini alikuwa ni yeye anafungua mlango  huo" Dorry alisita kueleza na akapandisha takamwili za ndani ya pua huku akivuta pumzi kwa kasi sana.

                       "Haikuwa kama mawazo yangu yalivyokuwa yanadhania kuwa huwa huyo alikuwa ni mama, kwani mama hakuwa na kawaida ya kupapasa kujua taa ilipo ili aizime kutokana kuijuan nyumba hii na mfumo wa swichi ulivyo. Nilisikia huyu aliyefungua mlango akiwa anapapasa ukutani kwa sekunde kadhaa hapo ilinibidi nifungue shuka niweze kumuona alikuwa ni nani. Nilivyofungua shuka tu mkono huo tayari ulikuwa umeshaifikia swichi na ulikuwa umezima taa na kuiichukua funguo mlangoni lakini niliweza kuuona ule mkono" Aliendelea kueleza.

                      "Je huo mkono ulikuwa ni wa nani hasa?" Norbert aliuliza.

                        "ulikuwa ni mkono wa mwanaume ambao ulikuwa na kovu la mshono" Dorry alijibu.

                     "Je ulipouona huo mkono hukuweza kupiga kelele?" Norbert aliuliza

                        "Sikuweza kwakweli kutokana na uoga na pia nilijua nilikuwa nimeona vibaya labda kwani kufunguliwa kwa mlango wa chumbani kwa mama kulinipa uhakika huo" Alijibu.

                    "Ok Baada ya hapo ilikuwa vipi?" Moses aliuliza kwa mara nyingine.

                     "Baada ya hapo nilipitiwa na usingizi hadi nilipokuja kusikia makelele ya wadogo zangu wakimuita baba afungue mlango, mlango ulikuwa kufunguliwa na ndiyo hapo nilikuja kujua baba hatupo naye" Dorry aliongea na alipofikia hapo alianza kulia tena, M.J Belind alichukua wasaa mwingine wa kumbembeleza hadi pale alipotulia.

     Moses na Norbert walipomaliza kuuliza maswali hayo walitazamana na wakapeana ishara kama walivyokuwa wamemaliza kumuhoji mke wa Jenerali Kulika, walimtazama na M.J Belinda kisha wakampa ishara ileile waliyokuwa wamepeana ambapo M.J Belinda naye alitikisa kichwa kukubaliana nayo.

                     "Dorry asante sana kwa ushirikiano wako nakuahidi kukusaidieni katika hali hii,tukikuhitaji tutarejea tena" Moses aliongea hukua akimpa mkono na Norbert akafanya hivyohivyo, wote kwa pamoja walitoka humo ndani baada ya kuridhishwa na maelezo ya Dorry ambayo yalikuwa yapo kwenye kifaa chao cha kunasia sauti.

     Sajini aliyekuwa yupo mlangoni alirudi ndani muda huohuo baada ya wao kutoka nje ambapo bado walimshuhudia Benson akiwa yupo kwenye eneo la hapo kwenye ukumbi ambao unatenganisha vyumba hivyo, muda huo alikuwa yupo kwenye eneo la mwanzo ambapo ngazi  za kupanda huko juu kutoka sebuleni zilikuwepo. Wote walipomuona walitazamana kisha wakawa wamemetilia shaka juu ya uwepo wake mahala hapo lakini hawakutaka kuzionesha shaka zao juu yake, walikuwa bado wamesimama kwenye ukumbi huo mbele ya mlango wa chumbani kwa Dorry wakiwa wanamtazama Benson ambaye alikuwa amewapa mgongo.

                  "Huyu jamaa sina imani naye kabisa" Moses aliongea kwa sauti ya chini sana.

                    "Hata mimi sikuwa na imani naye kabisa nilipomuona yupo mlangoni mwa chumba cha mjane nilijiuliza kafuata nini maana huku maofisa wa jeshi wenye kazi maalum na ndugu tu ndiyo wapo" M.J Belinda alisema

                    "Ok hebu muweke jicho la umakini naye kabisa, halafu  Belinda kuna jambo nilisahau kukuuliza" Norbert aliongea

                  "Yap  lipi hilo umesahau?" Belinda alimuuliza naye.

                    "Hivi hawa majirani waliokuja kuwafungulia walikuta kuna athari yoyote zaidi ya kuukuta mwili wa marehamu?" Norbert aliuliza.
 
                    "Hakukuwa na athari yoyote zadi ya kuukuta  huo mwili wa marehemu ukiwa upo sebuleni na walinzi wake wa jeshi wakiwa wapo jirani na geti ambao sasa hivi wapo Muhimbili walipowahishwa kwa ajili ya matibabu" M.J Belinda alijibu.

                    "Nahitaji kuwahoji na hao walinzi pia nahisi watakuwa na jingine, Moses safari moja Muhimbili" Norbert alimuambia Moses na wote kwa pamoja wakatoka kwenye eneo hilo hadi kwenye ngazi na kumpita Benson akiwa amesimama kwenye eneo hilo.

      Walishuka ngazi  hadi sebuleni ambapo walitoka nje moja kwa moja hadi barazani mwa nyumba hiyo. M.J Belinda alibaki katika eneo hilo Moses na Norbert walitoka hadi nje kwenye eneo la maegesho ya dharura kwa ajili ya msiba huo. Waliingia ndani ya gari walilokuwa wamekuja nalo eneo hilo na wakatoweka kuelekea Muhimbili, walikuwa wakitaka kwenda kumalizia sehemu ya kujua kile ambacho walikuwa nacho wanajeshi waliokuwa wakilinda nyumba ya Jenerali Kulika kwa siku hiyo iliyopita.

     Moses ndiye alikuwa dereva wa gari hilo katika safari hiyo ya kuelekea Muhimbili, alikuwa yupo makini sana gari na kuangalia usalama wao katika muda huo ambao walikuwa wakielekea katika hospitali ya Muhimbili. Hadi wanaingia barabara ya Ally Hassan Mwinyi bado hali ilikuwa ipo shwari isipokuwa waliona baadhi ya magari yakiwa yapo nyuma yao na hawakuwa na wasiwasi nao kabisa,Moses aliendelea kuendelea kuendesha hadi walipovuka kwenye kituo cha polisi cha Daraja la Salenda ambapo gari aina ya Toyota altezza nyeusi ndiyo pekee ilikuwa ipo nyuma yao.

     Walipoyafikia makutano ya barabara ya umoja wa mataifa gari hiyo ilikata kona kuingia upande wa kulia kwenye barabara ya Umoja wa mataifa. Moses alipoiona gari hiyo imeingia upande huo alishusha pumzi kisha akaongeza mwendo kuendelea na barabara ya Ally Hassan Mwinyi hadi kwenye kituo cha daladala cha Palm Beach, hapo alikata kona kuingia kwenye barabara ya lami iliyokuwa ikielekea ulipo ubalozi wa Burundi. Walienda nayo nayo barabara hiyo na wapofika kwenye ubalozi wa Burundi walipita moja kwa moja hadi kwenye makutano ya barabara hiyo na barabara ipitayo mtaa wa Lugalo.

     Hapo kwa mara nyingine waliishuhudia ile gari aina ya Toyota altezza nyeusi ikiwa ipo upande wa barabara hiyo wanayotaka kuingia katika upande ambao ilikuwa ikielekea kukutana na barabara ya Umoja wa mataifa, gari hiyo ilipowaona walikuwa wanataka kuingia katika barabara hiyo ilisimama na ikawawashia taa za mbele mara moja na kuwaaashiria waingie kwenye barabra hiyo. Moses hakutaka kusita yeye alikata kona kuingia upande wa kushoto na akaingia rasmi kwenye barabara hiyo inayopita mtaa wa Lugalo, aliongeza mwendo huku ile gari ikiwa ipo nyuma yake.

     Walienda na barabara hiyo huku ile gari ikiwa bado ipo nyuma yao hadi walipofika makutano ya Mtaa wa Kitonga na mtaa wa Lugalo, hapo Moses aliingia kwenye barabara  iliyokuwa ikipita mtaa wa Kitonga akiiacha ile gari ikinyoosha barabara ya Mtaa wa Lugalo. Moses alienda na barabara hiyo hadi alipofika kwenye makutano ya barabara hiyo na barabara ya Malik iliyokuwa ikielekea kwenye makutano ya barabara ya Mtaa wa Magore na kuendelea hadi Muhimbili, alipofika kwenye makutano ya barabaara hiyo na barabara ya Malik alikata kona kuingia kulia mwa barabara ya Malik kisha akaaangalia nyuma kupitia vioo vya pembeni hakuweza kuliona tena gari hilo.

      Alinyoosha na barabara hiyo na alipokuwa akikaribia kwenye makutano ya barabara ya Magore aliiona ile gari ikiwa inakuja kwa mwendo wa wastani sana jambo ambalo lilimfanya aingie kwenye barabara inayopita mtaa wa Magore jirani kabisa na shule ya sekondari ya Shaaban Robert akiacha ile inayopita kati ya makao mkuu ya jeshi na ukumbi wa Aga Khan Diamond jubilee na kwenda moja kwa moja Muhimbili. Aliongeza mwendo akiwa kwenye njia hiyo hadi alipoivuka njia shule hiyo na akaingia upande wa kushoto kwenye barabara ya mtaa Undali kwa kasi. Safari yake ya kasi iliishia kwenye hoteli ya Kangaroo akaingiza gari ndani kwa kasi,alienda hadi kwenye maegesho ya ndani ya hotel akasimamisha gari halafu akalizima.

                   "Nawatakia ufutiliaji mwema, si wanajua kufuatilia magari ya  watu" Moses alisema huku akinyoosha kiti cha dereva akajilaza

                    "na inaonekana wanajua tunaelekea Muhimbili walipolazwa wanajedhi waliokuwa wanalinda kwa Jenerali waliyokutwa hawajitambui" Norbert aliongea.

                  "ndiyo maana yake" Moses alidakia.

     Moses na Norbert walikaa hapo kwenye maegesho ya hoteli kwa dakika kadhaa kisha wakashuka kwenye gari yao wakiwa na wazo jipya litakalozidi kumchanganya aliyekuwa akiwafuatilia, waliamua kuingia ndani ya hotel hiyo iliyo chini ya Gawaza&Son company ambayo ipo chini ya Moses baada ya kuachiwa urithi na baba yake.



ITAENDELEA!!