Monday, November 21, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA NANE





 RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759
           +255788602793

WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




  SEHEMU YA NANE!!

   Mshutuko alioupata ulikuwa siyo wa kawaida kutokana na mavazi nadhifu meusi aliyovaa Moses na utulivu aliokuwa nao Moses baada ya kumuona adui yake ambaye akipatwa na mshtuko mkubwa sana ambao ulimfanya huyo mvamizi aone kuwa alikuwa akitazamana na kiumbe asiyekuwa wa kawaida ambaye muda huo alikuwa anatabasamu tu baada ya miale ya kurunzi kutua katika uso wake.


          "hey" Alijikuta akiropoka basda ya kumuona Moses.


****


    Mzubao alioupata ulimfanya hata asahau mbinu nyingine zitakazomuwezesha kutoa silaha kwenye mkoba uliopo kwapani, sauti yake ya kuropoka nayo ilizidi kuufanya moyo wake upige kwa nguvu na kumfanya abaki anaduwaa zaidi.

    Hiyo ilikuwa ni hatua pekee kwa Moses katika kumtangulia mpinzani wake huyo kimbinu, hakutaka kuitumia nafsi hiyo vibaya kwani hakuwa na uhakika kama angelipata nafasi nyingine adimu kama hiyo. Kwa wepesi wa ajabu alitoka mahali alipokuwa amejibana akaruka juu akiwa ametanguliza mguu mmoja mbele, mguu huo ulitua sawia kwenye kifua cha mpinzani ambaye alienda chini moja na kurunzi yake ikaruka huku ikiwa inazunguka inapiga miale hovyo ambayo ilimulika juu sehemu yenye mfuniko kulipokuwa na wavamizi wengine.

    Muale wa tochi uliomulika juu ulikuwa ni alama tosha kwa wavamizi wengine kujua  kwamba mwenzao amekumbwa na kitu cha hatari, tochi ilivyomulika moja kwa moja fikra zao zikajua dhahiri kwamba wenzao amekimbwa na balaa hivyo alihitaji kusaidiwa. Kwa upesi nao wakajiachia ndani ya mfuniko huo kwa umakini sana lakini walikuwa wamefanya kosa moja kubwa sana, hawakutambua kwamba walikuwa wanaingia kwenda kukabiliana na kiumbe asiyekuwa wa kawaida ambaye alikuwa anatumia udhaifu mdogo katika kuwamaliza wapinzani wake.

    Pia hawakutambua kuwa udhaifu mdogo ambao adui  wao wanayemfuata anaweza kutumia kuwamaliza tayari walikuwa wameuonesha dhahiri walipoingia humo ndani, mbinu kali ya kuingia kwa ghafla katika eneo hilo tayari ilikuwa imemezwa na udhaifu waliokuwa wameingia nao humo ndani ambao haukufaa kuwepo kabisa wakati wanaingia kupambana na adui yao.

   Kurunzi walizoingia nazo ndiyo ilikuwa ni udhaifu tosha ambao haikutakiwa kuwepo muda wanaenda kupambana na adui mwepesi sana katika mapigano ambaye yupo humo ndani ya shimo, walipotua tu  humo ndani mmoja wao alitoa ukelele wa maumivu kisha akaanguka chini na wote wakaelekeza bsstola zao upande ambao mwenzao alishambuliwa wakapiga  risasi lakini waliambulia patupu hawakuona mtu yoyote hsta walipomulika na kurunzi zao.

             "Aaaaargh!" Mwenzao mwingine alitoa ukelele wa maumivu akaanguka chini akawa anatupatupa miguu mwisho akatulia, walimulika upande mwingine ambao wanahisi mwenzao alishambuliwa kisha wakapiga risasi lakini napo waliambulia patupu.

    Kuchanganyikiwa ndiyo kulivamia vichwa vyao hadi fikra zao zikaenda mbali sana zikawaza mawazo yaliyokuwa potofu kabisa juu ya mtu waliyekuwa wanaapambana naye, hakika waliona walikuwa wakipambana na mzimu ambaye alikuwa haonekani ni wapi alipo. Walikuwa wamebaki wawili tu humo ndani na muda huo walikuwa wanatembea kwa uoga sana, wakijua wamepatikana na wameingia katika himaya ya mzimu.

    Mvurugano wa fikra juu ya tukio hilo ulivamia vichwa vyao wakachanganyikiwa hadi wakaharibu kazi iliyowaleta humo ndani bila hata kutarajia kama wangeweza kuiharibu, mmojawapo katika harakati za kutembea alijikuta akimkanyaga Lion akashtuka akamimina risasi katika mwili wa Lion  kisha akamulika na kutunzi aone kama kama mpinzani eake tayari risasi zimempata.

            "Ooooh! Damn" Alisema kwa fadhaa baada ya  kubaini alikuwa amempiga risasi mtu waliyetumwa waje kumkomboa, alishusha hata silaha yake chini akionekana amekata tamaa kabisa kwa jambo hilo alilolitenda.

    Mfadhao uliyompata ulikuwa ni uzembe ambao ulimuweka kwenye hatua nyingine kabisa ambayo hakutakiwa kuwemo kirahisi namna hiyo, kitu chenye ncha kali kilipenya kwenye mkono wake ulioshika silaha na silaha ikaenda chini kisha muda huo huo taa zikawaka kwa ghafla sana. Walichanganyikuwa zaidi baada kuona mwangaza kwa mara ya pili kisha kicheko cha kejeli kikafuata, walipotazama upande ulipo mlango wa kutokea humo ndani walimuona Moses akiwa amesimama amewanyooshea bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti.

        "Weka bastola chini na uisukume mbele nilipo" Moses alimuambia yule aliyekuwa bado ana silaha ambaye alikuwa ameishusha baada ya kuchanganywa na jinsi taa zilivyowaka humo ndani, hakuwa na ujanja zaidi ya kutii amri aliyopewa na Moses akaitupa silaha  chini kisha akapiga teke.

         "nafikiri mmekuja muda muafaka kabisa niliokuwa nawahitaji muje sasa ngoja niwape uturi kidogo muendane na hadhi ya ukaribisho wenu" Moses aliongea kisha akaingiza mkono mfukoni akatoa chupa inayofanana na ya uturi akawarushia kisha akaipiga risasi na hewa ya gesi ikatoka ndani ya chupa hiyo ambayo waliivuta bila kupenda na wakaanza kuishiwa nguvu wakaanguka chini.

    Alibaki akitazama kwa dharau jinsi walivyopitiwa na usingizi mzito baada ya kuivuta hewa iliyotoka ndani ya uturi  yenye sumu ya kulaza, hewa hiyo kwake haikuwa imemdhuru chochote kutokana na kuwa amepaka dawa inayozuia hewa hiyp isiingie ndani ya mwili wake kupitia puani.


****

     Mawasiliano baina ya vikosi vya specilal force na watu waliowatuma yalikuwa yamekatika kwa ghafla, katika chumba cha mawasiliano ndani ya eneo lililotangaza usiri wake kutokana na mandhari yake jinsi ilivyo. Panthers na Leopard pamoja na kijana mwingine wa makamo anayelekea utuzima ndiyo walikuwa wapo kwenye mitambo hiyo wakiwasiliana na vikosi vya special force vilivyopo chini ya amri yao, baada ya kuita kwa muda mrefu wakiwa wameshikilia vifaa vya mawasiliano hatimaye walikata tamaa wakabaki wanatazamana.

            "Something is wrong, si kawaida hii" Panther mmoja aliongea.

              "ni kweli brother but hatuwezi kuacha kazi yetu iharibike hivihivi tena zaidi ya mara moja kwa siku moja" Panther mwingine aliongea kisha akamtazama yule kijana anayeelekea utuzima akamuuliza,"Kamishna tutumie njia nyingine au tuache?".

               "Tumieni tu ila hawa walioshiriki operesheni fagio la chuma iliyomuua binamu yangu na mkuu wetu wasibaki hai, Gawaza,Kaila,Belinda, Kulika hawatakiwi kubaki hai ni sehemu ya hatua ya awali kabla mkubwa zaidi hajingia nchini" Kamishna aliongea kutoa amri ya kutumia njia nyingine kabisa  ili wakamilishe mpango wao

               "Ok we must kill General Kulika, yeye ndiye kiongozi wa operesheni fagio la chuma kama file lililotupa kazi linavyosema" Panther aliongea kisha akamtazama Kamishna ambaye alitikisa kichwa kukubali, alimgeukia  pacha wake kisha akamuambia "Brother no time to waste lets go" Kauli ilimtoka Panther mmoja ambaye kiswahili kilikuwa tabu na huwa anapenda kuchanganya kiswahili na lugha ya wenye ngozi nyeupe waliopata kuitumia ardhi ya bara la mtu mweusi waitakavyo, Panthers hawa walikuwa wanafanana kila kitu ila walitofautiana huo mtindo wa kuomgea ambapo mmoja alikuwa ni mwenye ujuzi katika kiswahili na mwingine alikuwa anakielewa kiswahili lakini si mjuzi katika kukiongea.

                  "Kamishna nafikiri leo ndiyo siku ya mwisho ya kupumua kwa general Kulika, ufagio wa tindikali sasa unampitia kufagia ufagio wake wa chuma" Panther mwenye uelewa wa kiswahili aliongea.

                   "nawaamini sana nafikiri kazi yenu itakuwa na mafanikio" Kamishna aliwaambia huku akitabasamu kutokana na uwezo walionao Panthers katika kazi yao, matunda mazuri ya kazi ya Panthers alianza kuisikia harufu yake kwani dalili za kuiva kwa matunda hayo tayari zilianza kuonekana.

      Adhma iliyowekwa na wakubwa zake katika umoja wao iliyoonekana kuanza kwenda kombo sasa ilianza kurejea baada ya kuwagiza watu hao wenye uwezo wa hali ya juu ulioendana na sifa ya mnyama waliyejipatia jina lake. Chui mweusi ambaye ni hatari kwa mawindo ya usiku kutokana na rangi yake kumfanya asionekana hata kwenye mwanga hafifu ndiyo sifa kuu hawa mapacha waliojiita jina hilo, Panthers walikuwa ni wapiganaji hatari wakiwa katika maeneo yenye giza ndiyo maana wakapewa jina hilo.

       Walijua kulitumia giza vyema katika mapambano tofauti na wapambanaji wa kawaida, tumaini la mafanikio katika kazi yao tayari alikuwa ameshalinusa katika pua yake kutokana na sifa hiyo waliyonayo Panthers. Hadi anabaki na Leopard katika chumba chenye mitambo ya kuongezea mawasiliano, bado tumaini hilo liliendelea kuwa ndani ya kichwa chake baada ya kuona Panthers tayari walikuwa wameondoka.


****


               "griiii! Griiii! Griiii!" Mlio wa simu ya mkononi ya kisasa ulisikika ukileta bugudha kwa mpumzikaji aliyekuwa na mwenza wake wakiwa wamejifunika shuka mwili mzima, karaha za mlio wa simu hiyo zilipozidi mkono wa mwanaume ulionekana ukitoka ndani ya shuka hiyo iliyofunika mwili ukaishika simu hiyo simu kisha mkono wa pili ukaonekana ukiifunua shuka hiyo kwa sehemu ya usoni.

     Mwanaume huyo aliitazama kioo hicho cha simu kisha akawasha taa ndogo za umeme zilizo katika mfumo wa kandili ambazo huwekwa pembezoni mwa vitanda  katika nyumba zilizojengwa kisasa, mwangaza wa taa hiyo uliifanya sura ya mwanaume huyo ionekane dhahiri  akiwa yupo kifua wazi.

    Mkuu wa majeshi Jenerali Augustin Kulika ndiyo alionekana sura yake kwa dhahiri baada ya mwangaza wa taa hiyo ndogo kufukuza giza lililokuwa likificha sura yake, pembezoni mwake alionekana mke wake ambaye tayari alikuwa ameshaamka baada ya mume wake kuwasha taa.

     Jenerali Kulika aliipokea simu hiyo iliyomkatishia starehe zake na akaongea, "Jambooo!...Unasemaa! Ok subiri". Alinyanyuka kitandani hivyo hivyo simu yake ikiwa katika sikio lake la kushoto akawa anauendea mlango, alikuwa akitoka kimya kimya bila hata kumsemesha mke wake jambo lilimfanya mke wake ahisi kulikuwa kuna jambo lisilo la kawaida ambalo lilikuwa limekatisha kupumzika kwake kwa raha na starehe akiwa amelala juu ya kifua cha mume wake.

      Aliona ameondolewa raha ya kupumzika na mume wake ambaye ndiyo amerejea kutoka  safari ya kikazi nje ya nchi, kitu alichokuwa akikihitaji kwa mume wake alikuwa tayari amekipata lakini muda wa kujilaza na mume wake ndiyo nao aliokuwa anauhitaji ambao umevurugwa na mlio wa simu hiyo iliyoita usiku wa manane akiwa yupo katika usingizi wa raha uliongezwa raha kwa kulala na mume wake kitandani.

             "Baba Dorry kuna nini mbona.." Alimuuliza mume wake kwani haikuwa jambo la kawaida kabisa kuongea na simu mbali na yeye katika kipindi cha usiku kama hicho, kuuliza kwake juu ya hali  hiyo kulikatishwa na Jenerali Kulika akichelea sauti ya mke isikike kwa mtu aliyekuwa akiongea.

     Jenerali Kulika alimuashiria mke wake amsubiri kisha akatoka ndani ya chumba cheke cha kulala mkono wake bado ukiwa umeshikilia simu sikioni mwake, alitembea kwa haraka akifuata korido ndefu hadi zilipo ngazi kisha akawasha taa akateremka ngazi hizo hadi sebuleni kwake akaketi kwenye kochi linalotazamana na mlango wa kuingia sebuleni kutokea nje.

              "ndiyo Belinda umesema special forces kutoka police force wamekuvamia nyumbani kwako wakiwa na lengo la kukumaliza...aisee kuna mtu nyuma ya tukio hilo aliyewaagiza hao.....ok ok asubuhi waletwe kambini kwa mahojiano maalum watutajie wahusika wa mchezo kabla hatujawauliza viongozi wa juu wa  polisi. Halafu nita" Jenerali Kulika kaa sauti ya chini wakati akimpa maelekezo mwanajeshi wake wa kuaminika aliyepo chini yake kwa vyeo viwili, alipotaka kutoa maelekezo zaidi umeme ulizimika humo ndani.na ukamfanya aseme, "nina wageni tayari nitakupigia simu nikimaliza kikao na wageni wangu wasio na taarifa".

     Ukweli wa msemo huo wa mwisho haukumaanisha wageni hata kidogo bali ulimaanisha kuvamiwa, umeme kuzimika ndani ya nyumba haikuwa jambo la kawaida kwani alikuwa akitumia umeme wa mionzi ya jua kwa muda wa usiku na si kutumia umeme wa shirika la umeme ambao muda mwingine hukumbwa na hitilafu na vitu kama hivyo hutokea.

      Dalili ya kuvamiwa ndiyo ilikuwa ipo ndani ya kichwa chake, wavamizi wenye uwezo wa hali ya juu ndiyo aliwawaza katika fikra zake kutokana na uwepo wanajeshi wa private wenye jukumu la kulinda nje ya nyumba yake. Kengele ya hatari ndani ya kichwa chake tayari ilikuwa imelia na akajionya nafsini mwake awe makini zaidi kwani hali ya hatari ilielekea kuikumba familia yake, Jenerali Kulika hakutambua kabisa kama kufika kwenye sebule ya nyumba yake tayari alikuwa amefanya kosa kubwa pindi alipokuwa alijiandaa kushusha ngazi za kuja hapo.

      Utambuzi wa kosa alilolifanya haukuwepo ndani ya kamati kuu ya fikra katika mwili wake kutokana kuwa na sifa ya wanadamu wa kawaida kutojua lijalo mbele, akili yake ilimtuma apande juu ghorofani kwa tahadhari aende chumbani kwake akachukuae silaha yake aihami familia yake ambayo ilikuwepo huko ghorofani.

      Alijiinua kwenye kochi kwa umakini wa hali ya juu akiyalazimisha macho yake kuzoea hilo giza ghafla kisha akawa anaelekea upande ilipo ngazi ya kuelekea ghorofani kwa tahadhari iliyokuwa ikitazamwa na wenye hadhari zaidi, hakuwahi kuzikifikia ngazi za kuelekea ghorofani tayari ngumi nzito ya  ilitua kwenye taya lake ikamyumbisha na kumuachia maumivu ambayo aliyapuuzia ili asipoteze umakini katika kupambana Teke zito la kuzunguka lilifuata ambalo halikumpata baada ya kuinama aliposikia mlio wa suruali ya mpigaji teke hilo, teke jingine la mgongo kilifuata alipokuwa yupo kwenye hali ya kuinama ambalo lilitokea upande wa nyuma yake ambalo lilimpeleka chini moja kwa moja.

     Jenerali Kulika alibiringita pale chini alipo akasogea kwa umbali wa mitaa takribani mbili kisha akajiinua kwa kufyatuka akakaa sawa akaangalia upande yalipotokea mapigo hayo ambayo tayari yalimpa tangazo kwenye ubongo wake juu ya uwepo wa wapinzani wawili wanaomshambulia, ngumi nyingine ilifuata ambayo aliikwepa aliposikia mlio wa nguo aliyovaa mpigaji na teke jingine likatua juu ya kifua chake likamsukuma nyuma akaanguka kwenye kochi la kukaa watu watatu sebuleni hapo.

     Pigo jingine la kutumia goti lilikuwa lilifuata ambalo lililengwa kumpata kifuani kwake lakini Jenerali Kulika alijibiringisha kwa upesi akasogea pembeni, mpigaji wa pigo hilo alitua na pigo lake kwenye mito ya kochi na Jenerali Kulika akaachia teke liitwalo ushiro geri kekomi (teke linalopigwa kwa kutumia kisigino) ambalo lililompata kwenye mbavu hadi mguno wa kubana pumzi ukasikika na hapo Jenerali Kulika akabaini mpinzani wake huyo alibana pumzi kwa nguvu ili kuzuia teke hilo lisimvunje mbavu.

      Jenerali Kulika alisimama wima kwa mara nyingine akatuliza masikio yake ambayo ndiyo kiungo peke kitakachomsaidia katika kujihami na mapigo ya wapinzani wake, kwa mara nyingine alisikia mapigo ya mateke mawili yakija upande wa kushoto  akayumba kimapigano zaidi yakamkosa. Alijirudisha sawa baada ya kuyumba kuyakwepa mateke ya mpinzani wake wa pili na hapo ndipo ikawa nafasi kwa mpinzani aliyempiga teke kwenye kochi kutimiza azma iliyowafanya wawepo humo ndani, kofi zito lilitua kwenye shingo ya Jenerali Kulika ambalo liliambatana kutobolewa kitu ambacho hakukitambua.

      Maumivu makali ndiyo yalifuata baada ya kutobolewa huko kisha misuli ya shingo ikaanza kumkamaa na nguvu zikaanza kumuishia muda huo, nguvu yote ya kupigana ilimuishia papo hapo  kisha alajikuta akipiga magoti baada ya kuanza kuishiwa nguvu.

            "You are dead General" Sauti ya mpinzani wake mmoja ilisikika ilimuambia kisha teke zito la kifuani ndiyo lilifuata hadi likaenda kumtupa kwenye kochi, taratibu Jenerali Kulika alikunja miguu yake kisha akainyoosha kwa nguvu akatulia hapohapo.


****

    ASUBUHI ILIYOFUATA

     Taarifa ya kifo cha mkuu wa majeshi nchini ndiyo habari iliyoteka vyombo vya habari, ilikuwa ni taarifa yenye kuhuzunisha kwa watu waliomtaka awepo kwenye orodha ya viumbe hai na pia yenye kufurahisha kwa watu wasiomtaka awepo kwenye orodha ya viumbe hai. Hali ya huzuni ilikuwa imetawala miongoni mwa wanajeshi pamoja na raia waliokuwa wakimpenda sana Jenerali Kulika kutokana na mchango wake kwa taifa, majira ya saa nne asubuhi mkuu wa majeshi ya majini Luteni Jenerali Ibrahim Salim alithibitisha juu kifo hicho.

     Taarifa hiyo ya kifo cha mkuu wa majeshi kilitolewa mbele ya vyombo vya  habari, mzizimo wa nchi juu ya kifo cha komandoo  hatari na kiongozi wa makomandoo ndiyo ulifuata huku uchunguzi wa kifo chake ukiwa unaendelea. Nyumbani kwa Jenerali Kulika tayari kulishaanza kujaa watu asubuhi hiyo na ilipofika saa tano asubuhi viongozi mbambali wa kijeshi na wa kitaifa walianza kumiminika nyumbani hapo kwa utaratibu maalum, waandishi wa habari nao hawakuwepo nyuma katika suala hilo tayari walikuwa wameshaweka kambi nyumbani kwa Komandoo wa kutegemewa wakiwa wanarusha habari za matukio yanayoendelea humo kwa wasioweza kushuhudia kile kinachoendelea.

     Ulinzi dhabiti ulikuwa umeimarishwa ndani ya eneo hilo kutokana na uwepo wa viongozi wazito ndani ya serikali, askari wenye nguo rasmi , wasio nguo pamoja na wsnajeshi walikuwa wapo ndani  ya mazingira ya nyumba ya Jenerali Kulika maeneo ya Oysterbay.

      Moses akiwa kama kiongozi wa usalama wa taifa  naye alikuwepo ndani ya eneo hilo, upande wa kulia kwake alikuwa amekaa M.J Belinda na upande wa kushoto kwake aliuwa amekaa Norbert Kaila ambaye tayari alikuwa amepata ahueni baada ya kuokoka siku iliyopita kwa msaada wa Norene. Walikuwa wametulia katika viti vyao wakiwa wamezama kwenye fikra nzito juu ya tukio hilo, mkombozi mwenzao aliyeikomboa nchi pamoja nao kabla rais mzalendo hajapata wasaa wa kuiongoza nchi.

      Ilikuwa ni simanzi kwao pamoja na hasira za kuuawa kwa kiongozi wa operesheni fagio la chuma lililoacha historia kwa watanzania, kadri muda ulivyozidi kwenda ndiyo walivyozidi kuzama kwenye fikra zao katika kuliangalia hilo suala hilo kwa upana zaidi. Akili zao za kijasusi tayari ziliamka na zikaanza kulichekecha hilo suala, Moses na Norbert kwa pamoja baada ya kuwaza kwa muda mrefu walijikuta wakiangukia kwenye wazo la aina moja ambalo lilisababisha wamuite M.J Belinda kwa pamoja kwa sauti ya chini kisha kila mmoja akawa na wahka wa kuongea kumuambia lile wazo lilipo ndani ya kichwa chake.

            "aongee mmoja basi" M.J Belinda aliwaambia baada ya kuona wote waliingiwa na wahka wa ghafla wa kutaka  kuongea juu ya suala hilo.

            "Unaweza ukaanza" Norbert alimuambia Moses kisha akatega masikio asikilize kile kitakachotoka kwenye kinywa cha Moses.

            "ninahitaji kuonana na Mke wa General nafikiri ataweza kutupa mwangaza wa kutegua hichi kitendawili kinachonikabili ndani ya kichwa changu" Moses aliongea kisha akakaa kimya akamtazama Norbert akimuashiria aseme naye.

            "wazo ndiyo hilohilo nililolifikiri" Norbert aliongea halafu akatazama kulia na kushoto kisha akasema, "tunahitaji msaada wako juu ya hili".

    M.J Belinda aliwatazama wote kwa pamoja baada ya kusikia maneno hayo kisha akawa anajiandaa kutamka kitu lakini alisita baada ya kuona mkubwa wake kicheo akija eneo hilo akiwa ameongozana na mwanaume wa makamo aliyevalia kinadhifu. Alisimama kwa haraka akatoa saluti kisha akaganda kumsikiliza kutokana na kutambua ujio wa huo ulimlenga yeye, Luteni Jenerali Ibrahim Salim ndiyo alikuwa mbele yake akiwa na huyo mtu aliyeonekana ni mgeni kwake.

              "Benson, kutana na Major general Belinda. Major General Belinda kutana na Benson afisa aliyepo hapa kwa kazi maalum" Luteni Jenerali Ibeshim aliongea kutoa utambulisho, M.J Belinda na Benson walishikana mikono huku wakitoleana tabasamu hafifu la kuridhika na utambulisho huo.

              "Major General Belinda nafikiri utakuwa msaada kwake katika kazi iliyomleta, ni hayo tu" Luteni Jenerali Ibrahim aliongea kisha akaondoka akiwa na Benson.

     Belinda aliwageukia Norbert na Moses kisha akawapa ishara wamfuate, alitembea kutoka katika eneo hilo la kupumzika wageni akiwa pamoja na Norbert na Moses. Walipanda ngazi ndogo za kibsrazani wakiekea katika mlango wa mbele wa kuingia humo ndani ambapo walimkuta mwanajeshi mwenye cheo cha koplo aliyetoa saluti  akafungua mlango wakaingia ndani, walipita sebuleni hapo ambapo kulikuwa na kundi kubwa la kinamama wakapanda ngazi kuelekea juu. Walifika juu kwenye ghorofa wakatembea kwenye korido ndefu iliyowapeleka hadi kwenye mlango wa chumba ambao waliufungua wakaingia, walikutana na mwanajeshi wa kike ambaye alitoa saluti baada ya kumuona M.J Belinda.

             "Huyu ni Moses Gawaza kutoka UN laboratory na huyu ni Norbert Kaila mwandishi wa habari wa kujitegemea, wana maongezi maalum na mfiwa hivyo unahitajika usubiri nje ya mlango wa chumba Koplo usu" M.J Belinda alimuambia mwanajeshi wa kike aliyekuwemo humo ndani na alimuita kuendana na cheo cha V moja iliyopo begani ambayo huitwa Koplo Usu.

           "Afande" Aliitikia kwa ukakamavu akatoka nje mara moja.

     Koplo usu wa kike alipofunga mlango baada ya kutoka nje, Moses na Norbert walibaki wakimtazama mke wa Jenerali Kulika kwa huruma sana kisha wakamtazama M.J Belinda kwa sekunde kadhaa. Waliyarudisha macho yao kwa mke wa Jenerali Kulika wakamtazama sana mama yule ambaye kiumri alikuwa sawa mama yao akiwa amekuwa mwekundu baada ya kulia sana, nywele zilizovurugika zilionekana kichwani mwake na macho yalikuwa yameuka rangi na kuwa yanafanana nyanya mbivu.

               "Mama" Moses aliita kisha akaendelea kuonges, "pole sana mama yangu".

       Maneno hayo yalimfanya mke wa Jenerali Kulika aanze kulia kwa uchungu huku akitamka maneno yenye kumlaumu muumba kwa kumchukua mume wake kipenzi, wote kwa pamoja walimuacha alie mpaka akanyamaza akawa kainamisha uso wake kwa majonzi.

                 "Mama naamini Jenerali hakufa  hivihivi tu bali kuna mtu ndiyo chanzo naamini hivyo, imani yangu inaweza ikapata uhalisia kuwa ni kweli ikiwa tu nitasikia kidogo kutoka kwako na nikakusanya na kile nilichokipata kwingine kibaini ukweli" Norbert aliongea kisha akatoa simu yake ya mkononi akabonyeza kitufe cha kurekodi.


JUMANNE  NAYO NI SIKU TUKUTANE PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA





HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA YA MTUNZI