Monday, November 28, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA KUMI NA TANO



RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________



SEHEMU YA KUMI NA TANO!!

           "Shit! Leopard Queen you have to be careful(Shit! Leopard Queen unatakiwa uwe mwangalifu)" Panther aliongea.

       
    "Hivyo basi huyo ndiyo Kaila na tukienda vibaya kwake tumeumia  hata mabosi hawatatuelewa si umesikia wote wapo ndani ya nchi hii Don kaingia jana na mke wake kaingia leo" Wilson aliongea.

             "Nauona ugumu wa kazi ila sitakubali mpaka nilipe kisasi kwa Kaila ndiyo furaha yangu" Kamishna aliongea kwa uchungu.

             "Kamishna cool down najua kama Kaila ndiyo kamuua Kitoza aliyekuwa  binamu yako, ila usiweke hasira mbele kumbuka tumepewa kazi hii kutoka kwa Don  na ikiharibika hii kazi pia Sir Shaw hatatuelewa" Wilson aliongea kisha akamtazama Panther akamuambia, "Kaila atauliwa na Leopard Queen kwa kumtegea ugonjwa wake tu, yeye si mpenda  mabinti sasa binti ndiye atakayemuua".



****


                "Nafikiri hiyo kazi niendelee nayo mtego mmoja bado upo" Leopard Queen aliongea.

                "No! No! Stay away from him(Hapana! Hapana! Kaa mbali naye" Panther aliongea kwa uchungu sana aliposikia Leopard Queen anataka kujitosa kuendelea na kazi, uhatari wa Norbert ulimfanya awe na hofu sana ya kuendelea kumuacha mpenzi wake aingie kupambana naye.

                "Panther come on! Muache afanye hiyo kazi ikishindikana mnaingia nyinyi najua kabisa hamuwezi kushindwa kuhusu hilo" Wilson alimuambia

                 "I can't(Siwezi)" Panther aliongea kwa uchungu.

                  "Usiwe na hofu nami B boy nitamaliza hiyo kazi then tutakuwa na ushindi" Leopard Queen aliongea.

                  "Na pia usiruhusu hisia za mapenzi zikutawale katika kazi kama hii Panther" Kamishna aliongea,


         Muda huo huo mlango ulifunguliwa na aliingia mtu aliyewafanya wote wasimame juu, walisimama kwa pamoja baada ya kuingia mgeni huyo ambaye wanamuheshimu sana mchango wake katika mpango wao.

                 "Karibu jenerali mtarajiwa wa dola tarajiwa"Wilson aliongea akimkaribisha mgeni huyo ambaye hakuwa mwingine, L.J Ibrahim ndiye mgeni mwenyewe ambaye alikuwa ahudhurii sana vikao vyao lakini ni  sehemu ya mpango wao.

                "Asanteni wana mapinduzi wenzangu niambieni mpango unaendelea vipi?" L.J Ibrahim aliuliza huku akiketi kwemye kiti na wote wakaketi kwenye viti.

                "Mpango kidogo umechukua sura mpya, na kuna mapya yamezuka" Kamishna alijibu.

               "enhee nipeni ripoti kamili" L.J Ibrahim aliongea.

              "Kwanza baya zaidi ni kwamba ni kwamba EASA ipo kazini na zuri zaidi ni kwamba Don na mkewe wapo nchini hapa katika mikoa tofauti" Wilson aliongea.

       Kauli ya kwanza ilimfanya L.J Ibrahim ashtuke huku kauli ya pili ilimfanya aingiwe na tumaini kidogo, kusikia kuingia kwa mabosi wao nchini ilikuwa ni jambo la kufarijika kwake kwani aliona dalili za mpango wao zilikuwa zikielekea kutimia.

               "Napenda ufahamu kuwa Norbert Kaila ni mpelelezi hatari wa EASA na ndiye yupo kazini na tayari amemponyoka Leopard Queen kwa namna ya kutatanisha sana" Kamishna aliongezea.

              "Maelezo yenu yananipa wasaa wa kuharibu zaidi heshima ya Moses ili tuzidi kumuweka pabaya Zuber atoke pale ikulu" L.J Ibrahim aliongea akaweka kituo kisha  akaendelea kuongea, "napiga simu pale ikulu nampa siku saba atoe maelezo ya kwanini Mkuu wa idara ya usalama wa taifa aliyemteua anayemuamini kwa siri anahusika na mauaji ya General na  nitamuambia ana ushahidi gani wa kujitetea kuwa na yeye ahusiki katika mpango huo ikiwa huyo ni mtu wake wa kuaminika. Akishindwa kutoa majibu ndani ya siku tatu namtangaza Professa Gawaza ni muuaji wa General, siku ya saba tunaipindua nchi mradi wetu unaanza kwa watanzania wote tuone suala alilokuwa analipinga na amekataa kulisaini atakuwa  kalizuia vipi".

                  "Good plan General but what about Kaila(Mpango mzuri Jenerali lakini vipi kuhusu Kaila)?" Panther aliuliza.

                  "Kaila ni jukumu lenu na ikishindikana Don na mke wake wataingia kumtuliza, sidhani kama atatoka. Kwa sasa mimi ndiyo mkuu kati ya wanajeshi wote hivyo majeshi yapo chini ya amri yangu, mapinduzi lazima" L.J Ibrahim aliongea akiwa na tabasamu pana zaidi.

                 "Njia ya kupandikiza machafuko ya kidini naona haifai kwa sasa na wale viongozi wa dini walioteuliwa kwa ajili ya mpango huo hawana kazi tena ila inabidi wabaki na siri milele, Panther  unajua nini cha kufanya kwa askofu na mufti mkuu" Wilson aliongea.


                  "I know(najua)" Panther aliongea.


    Mradi wa kupandikizwa Tanzania ulikuwa tayari umeanza kuonesha matumaini kwa hawa wahusika, ambapo suala la mapinduzi kwa namna ya kijeshi ndiyo ilitaliwa kufanyika kwa kutengeneza serikali mpya na kuiondosha serikali ya rais Zuber Ameir. Mbinu ya kumpandikizia hila ya kuhusika na kifo cha Jenerali Kulika ndiyo iliongelewa ili kuwaondoa imani  wananchi  kwa rais wao, kikundi hiki tayari kilikuwa kimeweka makubaliano na kundi la hatari la kihalifu la nchini Ujerumani lililopo chini ya  Jack Shaw ambaye tayari ameingia nchini  kwa kutumia mbinu ya kinyonga awapo kwenye maeneo ya hatari ili kudumisha mpango huo.

     Siri ya kuundwa kwa mpango huo ilikuwa ni mkataba feki amba uliletwa kwa kivuli cha Jumuiya ya madola, ulikuwa na hila ya kuitumbukiza Tanzania mahali pasipo stahiki lakini Rais shupavu  Zuber Ameir aligoma kusaini pasipo kujua kimetumika kivuli cha Jumuiya ya madola katika kumshawishi asaini. Haukuwa mkataba uliotoka jumuiya ya madola bali ilikuwa ni hila ya kuingiza Tanzania mahali pasipostahiki kwa kisingizio cha kuleta maendeleo nchini, Rais Zuber alipowagomea ndipo ikaundwa hila ya kupandikiza machafuko ya kidini ili kuidhoofisha serikali na hatimaye kupinduliwa na jeshi na mradi huo kupandikizwa kwa ulaini sana.

    Mapinduzi yaliyokuwa yakizungumziwa yalikuwa yafanyike kwa sharti la kuondoshwa kwa Jenerali Kulika katika uso wa dunia na bila hivyo mapinduzi hayo yasingeweza kutelekelezeka hata kidogo ndani ya nchi ya Tanzania. Tayari Jenerali Kulika mwenye amri katika majeshi ameuawa hivyo hatua iliyokuwa inafuata ni kuipindua serikali ya Rais Zuber baada ya kumpandikizia chuki kwa wanachi wake kupitia mauaji hayo, hakika walikuwa ni maadui wakubwa wa Tanzania ingawa asilimia kubwa walikuwa wamezaliwa ndani ya Tanzania.

    Watu wasiotaka kuiona Tanzania ikiwa ni nchi iliyokuwa ikiendeshwa kizalendo kama ilivyo hivi  sasa zaidi ya kuona ni nchi wanayoistahiki kuwa sehemu  yao kutekelezea mpango wao ambayo ingewaingizia kiasi kikubwa sana cha pesa, uzalendo alioonesha Rais Zuber kwa kukataa dola milioni 500 za kimarekani ikiwa tu ataweka saini katika mkataba alioletewa wao waliuona ni ujinga kupitiliza. Hivyo fedha hizo walikuwa wakizitaka wao kwa kupandikiza mpango wao kwa kilazima kama mabosi wao walivyowaahidi, uchu wa pesa kuliko kitu chochote  ndiyo ulisababisha wakodi  kikundi cha Cats kingdom ambacho ni sehemu ya kundi la hatari la Jack Shaw lililopo  ndani ya Afrika ya mashariki.

     Uchu wa pesa kutoka kwa mabosi wao ndiyo ulisababisha hata watanzania wenye nyadhifa kubwa  katika masuala ya ulinzi waweze kuisaliti nchi yao, pia waliweka kuwasaliti wananchi ambao walikuwa wakiwategemea sana. Hawakuona hasara ya kupoteza roho zaidi ya kuona hasara ya kupoteza pesa, hawakuona hasara ya kupoteza utu wa wananchi wao zaidi ya kujali kuingiza fedha.

****

KILIMANJARO HOTELI

     Baada ya Benson kuingia ndani ya chumba cha Askofu Valdermar wapambe wote walitoka nje  kutokana na amri ya Askofu huyo iliyowataka wafanye hivyo, usiri wa jambo lililowafanya watoke nje tayari walikuwa wakilitambua na ilikuwa ni kawaida  kwao kutolewa nje akiingia Benson katika eneo kama hilo. Ajenda kubwa ambayo ni zaidi hata ya kikao cha siri  iliwafanya watoke nje, ilikuwa ni siri kubwa iliyobaki miongoni mwa watumishi hao wawili waliokuja na Askofu huyo.

     Benson alipoingia ndani milango ilifungwa na Askofu huyo akabaki akimtazama kwa macho yaliyoashiria kitu, ukakamavu wa kiume alionao Askofu huyo ulipotea mara moja kuanzia sura na hata mwili. Kwa namna isiyotarajiwa Askofu huyo alilegeza macho mithili ya mtu anayesikia usingizi huku akmsogelea Benson, alipofika mbele kabisa ya Benson aliweka mikono juu ya mabega ya Benson kisha akafanya kitu ambacho hakikutarajiwa kufanywa  na mtumishi wa Mungu mkubwa kama huyu.

     Askofu Valdermar na Benson walianza kubadilishana mate  vinywani mwao mithili ya wapenzi wa jinsia tofauti, mmoja alikuwa amechukua wasaa  wa kujifanya mwanamke na mmoja alikuwa akibaki katika uanaume wake kamili. Hali ya kusikitisha na hata kuhuzunisha kwa mtu anayeonekana kwa hadhira ni mtumishi wa Mungu kama huyo kutoka barani Ulaya  akitomaswa na mwanaume mwenzake tena akitoa mihemo mithili ya binti, hali nyingine ya kusikitisha kwa mwanaume mwenye kujitambua akimtomasa mwanaume mwenzie mithili ya mwanamke. Haikustahiki kabisa kumuita Askofu Valdetmar mtumishi wa Mungu kwa kufanya kitendo ambacho Mungu  aliwaangamiza wanadamu wallikuwa wakiishi Sodoma kwa kukifanya, aibu sana kwa jinsia ya kiume kufanya kitendo kama hicho ambacho ni haramu kwa dini zote.

    Benson pasipo kuwa na haya  ya kwamba aliyempa pumzi anamuona yeys alimvua vazi maalum la kulalia Askofu Valdermar akabaki kama alivyozaliwa, pasipo hata kuwa na chembe ya haya katika uso wake aliamua kumuandaa kwa ajili ya kufanya tendo hilo haramu, Alifanya kama vile anavyomuandaa mwanamke katika tendo ambalo Mungu kalibariki kufanywa na waliomo kwenye ndoa, alitumia muda  huo kumundaa huku Askofu Valdermar akitoa miguno mithili ya mtoto wa kike kwa sauti ya puani. Aibu iliyoje ilizidi kwa mtu anayeonekana ni wakala wa nuru kwa kutoa maneno mema kwa jumuiya, kumbe ni wakala wa giza anayefanya mambo yanayofanywa na watu wa giza.

     Askofu Valdermar kwa mara nyingine baada ya kumaliza kuandaliwa na yeye alizidi kufanya jambo la aibu kwa kuzitoa nguo za Benson zote kisha akaanza kumuandaa mithili ya mwanamke anayemuandaa mume kwa ajili ya jimai. Mambo mengine waliyofanya hayakustahiki kabisa kuandikwa kwa kalamu ya mwandishi, mambo hayo yaliwachukua masaa mawili wakawa wamemaliza kabisa na hapo wakajisafisha wakarudi wakavaa mavazi yao.

             "Asante sana Benson, unanipa burudani zaidi hata ya mume wangu" Askofu Valdermar yule aliyekuwa akiongea kingereza kumuambia Norbert akamuite Benson sasa hivi aliongea kiswahili fasaha kabisa tena bila kuonekana kama ni mgeni katika lugha hiyo, laiti kama ingesikika sauti yake tu pasipo kumuona yeye mwenyewe basi ingedhaniwa anayeongea ni mtu mweusi kabisa.

               "Anytime(muda wowote), nafikiri taarifa yote unayo. Don ameingia tayari yupo hoteli ya Singita Grumeti Serengeti kwa ajili ya mradi wetu" Benson aliongea.

                "Ndiyo ninayo, ninamaliza mazishi ya Edson ndiyo nitaenda kuungana naye" Askofu Valdermar aliongea.

               "Ok, Sir kuna jambo naona uliache" Benson aliongea.

                "Benson tukiwa wawili niite madam usiniite sir, ok jambo lipi?" Askofu Valdermar aliongea.

                 "Naomba huyu kijana aliyekuja kunipokea asiwepo karibu nawe" Benson aliongea huku akionekana ameshikwa na wivu.

                   "Hiyo siyo kazo yako Benson ana kazi yake huyo ndiyo maana nimemteua, nafikiri nikienda kwa mume wangu Serengeti ndiyo utakuwa mwisho wa kazi yake. Unaweza ukaenda" Askofu Valdermar aliongea, Benson hakuwa na ubishi zaidi ya kuondoka humo ndani kutokana na amri aliyopokea kutoka kwa bosi wake.

     Wivu wa kumuona Norbert eneo hilo ndiyo ulimtafuna na akajikuta hana la kumfanya, hakika alimuonea wivu mwanaume  mwenzake kwa mwanaume mwingine.


****

     Benson alipotoka  watumishi wale walirudi ndani ya chumba hicho wakimuacha Norbert akiwa anatoka na kuingia ndani ya chumba chake ili aweze kupata kile alichokuwa akikihitaji kutoka kwa hao watu. Wasiwasi juu ya Askofu Valdermar tayari  ulikuwa umeshamuingia ingawa hakutaka kupuuza agizo la ofisi pasipo kuzifanyia utafiti fikra zake zilizompa wasiwasi sana baada ya kumuona Benson akiwa na alama aliyonayo mtu aliyeonekana nyumbani kwa Jenerali Kulika siku ambayo aliuawa, nafsi yake ilimuambia anahitaji umakini sana katika kumlinda Askofu Valderamar hasa baada ya kutambulishwa kuwa  Benson yupo nchini akichunguza kifo cha Askofu Edson. Upande mwingine wa nafsi yake ulimuambia aendelee kumlinda Askofu Valdermar kama ofisi inavyomuhitaji ili asije akadhuriwa na Benson, alifikiri sana juu ya hayo.

    Mwisho wake akaamua aendelee kumlinda Askofu Valdermar huku akizidi kumpeleleza Benson. Hakika mwanadamu hakuwa anayajua ya  mbeleni mwake na laiti angekuwa na utambuzi wake, Norbert angezidi kuongeza umakini wake kwani alikuwa akicheza na watu wanne tofauti wenye hatari kubwa ingawa yeye aliona anacheza na watu wawili.





 SIKU ILIYOFUATA
    JUMAPILI

     Kanisa la kiluteri la Azania front siku hiyo lilifurika mamia ya waumini kwani ilikuwa ni siku ya ibada, pia ndiyo ilikuwa siku ya kuagwa mwili wa Askofu Edson. Viongozi mbalimbali wa kiserikali walikuwepo ndani ya kanisa hilo wakiongozwa na Rais Zuber  katika kuhudhuria ibada ya mazishi ambayo ingeanza baada ya kumalizika kwa misa ya pili, ndani ya kanisa hilo pia Norbert alikuwepo pembeni ya Askofu Valdermar kwa kipindi chote kama agizo la ofisi yake lilivyomtaka.

    Siku hiyo misa ya kanisa hilo iliongozwa na Askofu Valdermar akiwa na mkalimani wake Norbert hadi inaisha, kisha ikaingia ya pili hadi inaisha na hapo ndipo ibada ya mazishi ikaanza. Jeneza la lenye.mwili wa Askofu huyo lilikuwa lipo mbele na ibada hiyo ilikuwa ikiendelea, muda wa kuuaga mwili wa askofu Edson ulifuatia. Ulikuwa ni muda ulioibua majonzi na simanzi kwa wafiwa na hata waliokuwa wakimpenda sana Askofu huyo, muda wa kuaga ulipoisha safari ya kupeleka jeneza uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere ili usafirishwe kuelekea Musoma kwa maziko ndiyo ilifuatia. Viongozi mbalimbali wa kiserikali walitawanyika baada ya kutoa salamu za pole kwa  wafiwa wakiongozwa na Rais Zuber, baada ya hapo shughuli zingine za kawaida zilifuata huku Norbert akiwa yupo kwenye msafara wa Askofu Valdermar kwa mara nyingine ambao ulikuwa unaelekea uwanja wa  ndege kusafiri kuelekea Musoma kwenye mazishi.

****

    Muda ambao msafara unaondoka kuelekea Uwanja wa ndege ndiyo muda ambao msafara wa rais Zuber ulikuwa unarejea ikulu baada ya kumaliza kumuaga Askofu Edson, ilikuwa ni lazima arejee ikulu kabla hajaondoka baadaye kuelekea Musoma kwa ajili ya kuhudhuria  mazishi. Msafara wake ulitumia dakika tano tu kutoka kanisa la Azania front hadi ikulu, kuwasili kwa msafara wake ikulu hapo ndiyo kulikuwa mwanzo wa kuzuka jambo jingine ambalo hakutarajia kama litazuka. jambo hilo lilimfanya asitishe  safari yake yote ya kwenda kwenye mazishi kutokana na uzito wake, simu yake ya mkononi iliita na hapo ndipo jambo lenyewe lilipoanza.

    Aliipokea simu hiyo akaiweka sikioni mwake pasipo kujua dhumuni la kupigiwa simu hiyo, ilikwa ni simu kutoka kwa L.J Ibrahim ambayo haikuwa na ishara ya kuwepo kwa jambo zuri hata kidogo. Simu hii ndiyo ilimpa taarifa ya kupinduliwa kwa nchi siku saba zijazo ikiwa tu hatatoa maelezo ya kina juu ya kuhusika kwa Moses katika mauaji ya Jenerali Kulika, kitendo cha kumuamini Moses na kumfanya kuwa msiri wake ndiyo jambo ambalo lilimfanya ahisiwe anahusika na mauaji hayo moja kwa moja. Taarifa ya kupinduliwa kwa nchi ndani ya siku saba zijazo ilizidi kumchanganya sana kwani hakuhusika lolote katika mauaji hayo, alikuwa amebebeshwa gunia la misumari ambalo hakutakiwa alibebe yeye.

    Rais Zuber alizidi kupagawa sana  akawa hajui nini cha kufanya kwani mtu aliyempa amri hiyo majeshi yote yalikuwa yapo chini yake, alishindwa kumpigia simu Moses kutokana na uzito wa jambo lenyewe kwani alihofia huenda Moses angeweza hata kummaliza yeye mwenyewe kwa kuficha siri hiyo ya kuhusika. Hakuwa na imani tena na Moses na aliona kama ndiyo mhusika namba moja wa jambo hilo basi akimuita anaweza kumfanyia kitu kibaya. Uamuzi wa kufanya kwa jambo hilo aliona ni kuomba msaada katika shirika la kipelelezi la Afrika ya mashariki(EASA) ili walau apate nusra ya jambo ambalo hahusiki nalo analotaka kuhusishwa nalo, hapo Rais Zuber alipiga simu  kwa CE na kumueleza juu ya tatizo hilo ambapo  kidogo alipata ahueni.


****


SIKU ILIYOFUATA
  MUSOMA
      Baada ya  Askofu Eddson kuzikwa safari nyingine kabisa ilianza iliyomuhusisha Askofu Valdermar, Norbert na vijana wake aliokuja  nao, safari hiyo iliwachukua masaa kadhaa wakawa wamefika katika mbuga ya taifa ya Serengeti. Walifika kwenye hoteli ya kitalii namba moja duniani iiitwayo Singita iliyopo ndani ya ardhi ya Tanzania, walipokelewa kwa uchangamfu mkubwa na wahudumu wa hoteli hiyo wenye uchangamfu wa kuweza hata  kumsahaulisha mteja uchungu wa gharama za juu za hoteli hiyo inayoongoza kwa kuwa na gharama za juu  nchi nzima. Walipokelewa wakapakiwa kwenye gari maalum lililokuja kuwapokea kuwapeleka kwenye lodge ambayo walitakiwa, kutokana na ukubwa wa hoteli hii iliwalazimu watu kutumia usafiri kutoka lodge moja hadi nyingine.

     Usafiri uliwafikisha lodge walipokuwa wameichagua salama ambapo walikutana na mtuambaye alimfanya Norbert azidi kushangaa, alikuwa ni mtu ambaye yeye aliishia kumuona tu kwenye luninga. Mtu huyo ndiye aliyekuwa anawasubiri hapo jambo ambalo haliwezekani, haikutokea kwa mtu kama huyo mwenye msimamo mkali amsubiri Askofu Valdermar tena akionekana ni mchangamfu sana.

      Norbert alibaki kutoamini kwa mtu huyo kusalimiana na Askofu Edson kisha akawapungia mkono yeye na vijana wa askofu, kitendawili  kizito kilitanda ndani ya ubongo wake juu ya hali hiyo.

              "Sheikh Ahmed" Alibaki akijisemea moyoni huku akimtazama  mtu huyo ambaye alikuwa amevaa mavazi ya kiislamu, alikuwa akitazamana na mtu huyo mwenye asili ya kiarabu ambaye amefuga ndevu nyingi sana kidevuni mwake. Akiwa ndani ya kanzu safi nyekundu pamoja na kiremba cheupe chenye kizibao chekundu,  sehemu ya uso ilitangaza kwamba mtu huyo anaingia sana nyumba ya ibada  lakini mambo aliyoyaonesha yalimtia shaka Norbert.

*Wakala wa giza



TUKUTANE TENA JUMANNE  PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA.



HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI






No comments:

Post a Comment