Friday, January 20, 2017

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA AROBAINI NA MBILI



RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________




SEHEMU YA AROBAINI NA MBILI!!
    Wilson alikuwa akitumia nguvu zaidi katika kukimbia huku akiwa amebana mdomo kwa nguvu sana  asiweze kuvuta pumzi kwa kutumia mdomo, akiwa bado yupo kwenye mbio na kasi yake hiyo Norbert aliupiga teke dhaifu mguu wake mmoja na kupelekea ugongane na mguu mwingine kisha aanguke vibaya na kubiringita kwenye mchanga.

               "Aaaah!" Alitoa sauti ya kukata tamaa kwa kuangushwa na Norbert huku akiwa anasalimiana na mchanga huo wa ufukweni.






_____________TIRIRIKA NAYO

    Norbert baada ya kumpiga teke hilo lililomfanya abiringite aliamua kumfuata kwa kasi kipindi alipokuwa akibiringita, kabla hata hajasimama kwa kubiringita huko Norbert alimuongeza teke la dochi ambalo lilikuja kumpata sawia kwenye mbavu hadi Wilson alitoa mguno wa maumivu. Aliendelea kumsogelea Wilson ambaye bado alikuwa anabiringirita hadi aliposimama kabisa akawa anaugulia maumivu ya dochi hilo la mbavu, Wilson alikuwa akihisi sehemu hiyo ya mbavu kama alikuwa amepigwa na chuma kutokana na nguvu za miguu alizonazo Norbert ambazo ndiyo alizitumia kumpiga dochi hilo la mbavu.

     Norbert alisimama karibu kabisa na Wilson akawa anamuamgalia Wilson jinsi alivyokuwa akiugulia maumivu ya pigo alilokuwa amempatia, tayari Wilson alikuwa ameshaweka ugumu katika moyo wake katika kupambana na Norbert jambo ambalo lilikuwa ni kosa kubwa sana kwake. Alikuwa hajajiweka sawa kiakili ndiyo aweze kupambana na Norbert, ndiyo maana hata alipomuona alikimbia ili asikutane naye kwani hakuwa amejiweka katika hatua ya kupambana naye. Laiti kama tangu mwanzo angekuwa ameiweka akili vizuri katika kupambana na si kumkimbia mtu kuwa hamuwezi, ingemsaidia sana aweze kupambana na mtu huyo ambaye kwa sasa alikuwa amemuweza akiwa hana ujanja kabisa wa kukimbia kwani ukaribu aliokuwa yupo naye haukumfaa kabisa katika kumtoroka mtu huyo. Kukimbia kwake ilikuwa ni sawa kumkimbia mamaba kwenye mto wakati ng'ambo ya mto ni mbali sana, jambo ambalo haliwezekani kabisa kutokea kwani mamba  kaumbwa na kasi kwenye maji.

     Kitendo cha Wilson kumkimbia Norbeet ni ishara kubwa ya kutomuweza kimapigano, tayari mwili wake hadi moyo wake ulikuwa umeshakiri hivyo  ndiyo maana akamkmbia katika eneno ambalo walikuwa wapo wawili tu hapakuwa na mtu mwingine na hata kama wangepigana basi wangepigana wawili tu si kupigana na mtu mwingine. Wilson akiwa hapo chini alikuwa akijaribu kufikiria jinsi ya kumtoroka tu Norbert na si kingine katika eneo hilo, tayari alikuwa ameshapunguzwa nguvu kwa pigo alilokuwa amepewa na sasa alikuwa na nguvu dhaifu zaidi kuliko hata nguvu alizokuwa nazo hapo awali alipokuwa akijaribu kumkimbia katika eneo hilo. Ili asionekane kuwa  alikuwa amekubali kushindwa kikondoo tu aliamua kujiinua akasimama na akawa anatazamana na Norbert. Alijitahidi asioneshe kuwa amejeruhiwa lakini mwili uliokuwa umepata hitilafu hiyo ulikuwa unamsaliti kabisa na kupelekea atoe ishara zote kwa  Norbert kuwa amejeruhiwa, kila alipokuwa akihema kwa huko kujeruhiwa kwake alikuwa akipatwa na maumivu kwenye mbavu jambo ambalo lilimfanya azidi kumpa ishara ya kufumba macho kwa maumivu adui yake.

    Akili ya kukiri kuwa alikuwa hawezi kabisa kusimama na mwanaume mwenzzake huyo kimapigano ndiyo zilikuwa zipo kichwani mwake, muda huo aliokuwa akimtazama Norbeet aligeuza jicho pembeni kutazama katika upande wa nyuma kwa namna ya kijanja zaidi ili  akimbie akiwa amepata nafasi tu ya kukimbia katika eneo hilo. Alikuwa akitafuta nafasi za dhahabu ambazo zote zilikuwa zimebanwa kisawasawa, hata nafasi ya makaa ya mawe katika kutoroka katika eneo hilo hakuipata mbele ya mjanja wa wajanja ambaye alikuwa yu mwenye uwezo wa kujua ujanja wa kila namna kutokana na akili nyepesi aliyokuwa nayo kichwani.

                "Mwanamama usijaribu kukimbia nitategua mbavu yako nyingine" Norbeet kwa kujua adui yake hayuko tayari kimapigano alizidi kumchanganya kabisa, maneno hayo yalikuwa ni tusi zito sana kwa mwanaume mwenye kukamilika kila kitu kwenye mwili wake kama Wilson Ole.

               "Hii sasa ni too much" Wilson alijisemea moyoni baada ya kuona kuwa alikuwa amedhalilishwa vya kutosha na adui yake huyo, alijua kabisa alikuwa amegundulika hawezi kupambana naye ndiyo maana akamdharau namna hiyo.

   Wilson hasira zilimzidi kichwani akiona dharau hizo zilikuwa zimezidi kabisa hadi kufikia hatua hiyo, hata kama hakuwa akiweza kupambana na mtu kama Norbert aliona hakufaa kuitwa mwanamama. Tusi hilo alilokuwa ameitwa na Norbert lilimfanya hata uoga aliokkuwa nao kwa Norbert umuondoke papo hapo, moyo wa liwalo iwe ndiyo ulikuwa umeingia ndani ya muda huo. Hakung'amua kabisa hilo ndiyo Norbert ndiyo alikuwa analitaka na si kumpiga tu kama anapiga punda aliyegoma kwenda, hasira tayari zilikuwa zimeishaivamia akili ndani ya muda huo. Mawazo ya kupambana kisa amedhalilishwa kwa kuitwa jina baya, ndiyo yalikuwa yamechukua taji la ufalme katika mishipa yake ya fahamu ndani ya mwili wake kwa muda huo.

    Aling'ata kabisa papi za midomo yake za chini kwa jinsi hasira zilivyokuwa zikimuongoza ndani ya mwili wake, viganja vya mikono yake alivikunja kwa nguvu sana na kutengeneza ngumi iliyokuwa ikitetemeka kama miguu ya mcheza sarakasi akiwa anatembea juu ya kamba.

    Bila ya kusita alinyanyua mguu wake mmoja akapiga hatua moja mbele kwa kasi, na alipoongeza hatua ya pili tayari alikuwa ametoka na ngumi mbili za usawa wa usoni kama vile alikuwa ni mcheza masumbwi mzuri sana akiwa ulingoni akipambana na mpinzania wake. Alikuwa akiulenga uso wa Norbet kwa ngumi hizo ambazo zote zilikuwa zimelenga upande mmoja,alirusha ngumi hizo huku akiwa amesahau kabisa kuwa mchezo huo aliokuwa akiutumia kurusha ngumi ulikuwa na lengo lake. Mchezo haukuwa umeundwa kwa ajili ya kumuumiza adui bali ulikuwa umeundwa kwa ajili ya kujizuia usiumizwe na adui yako, ngumi alizokuwa amerusha Wilson zote zilikosa lengo baada ya Norbeet kuanza kuyumba kulia alipotupa ngumi ya kushoto na kisha akayumba kushoto alipotupa ngumi ya kulia. Baada ya kuyumba namna hiyo Norbert alimrudisha Wilson nyuma kwa teke la kusukuma la kifua  ambalo lilimfanya ayumbe nusura adondoke, Wilson alipojiweka baada ya kuyumbishwa na teke hilo alikunja ngumi zake akiziweka usawa mbele ya uso wake kisha akamfuata Norbert kwa kasi sana na alipomkaribia  aliamua kurusha ngumi ya walioshindwa mapambano maarufu kama kota(kwa watu wauswahilini ngumi hii siyo ngeni kwao hurushwa kwa kuzunguka kama feni).

   Ngumi hiyo Norbert aliinama ikapita, Wilson alileta nyingine ya mkono wa kulia kama ile baada ya mkono wakushoto kukosa lengo. Ngumi hiyo ya pili aina ya kota nayo ilikosa lengo kabisa na Norbert aliinama tena akampa akili Wilson ya kujaribu ngumi nyingine kutokana na kuinama huko.

   Wilson bila ya kuchelewa alijaribu ngumi kuchimbua maarufu kama upper cut wale uswahilini hupenda kuiita ambakati kutokana na kushindwa kulitamka jina lake kwa ufasaha, ngumi hiyo Norbert nayo aliiona kwakuwa Wilson alikuwa akitumia nguvu nyingi katika kuzirusha ngumi na kupelekea ishara muhimu za mwili wake zinazoashiria kutoka kwa ngumi ya aina hiyo Norbert kuziona. Kitendo cha haraka alichokifanya Norbert ilikuwa ni kutegesha kiwiko chake usawa wa chini ya kidevu ambapo ngumi hiyo ilikuwa ikija, ngumi ya Wilson yote iliishia kwenye mfupa wa kiwiko kilichokomaa cha Norbert hadi vidole vyake vikateguka na kutoa sauti ya kugoka.

                "Aaargh!" Alitoa ukelele wa maumivu kwa kuumia mkono wake na hakujua kabisa alikuwa amefanya kosa jingine.

    Ukelele wake huo uliambatana na kusindikzwa na ngumi nzito ya uso iliyotoka kwa Norbet pamoja na teke zito la pembeni la kutumia kisigino ambalo lilitua kwenye kifua cha Wilson hadi akaenda chini kabisa, alikuwa amevunjwa mifupa ya kifuani kwa mara nyingine na Norbert kwa  teke hilo la nguvu sana. Wilson alianguka chini akajua kabisa mwisho wake ndiyo ulikuwa huo kwa muda huo, Norbert alipoona mpinzani wake alikuwa ameanguka chini aliitazma saa yake mkononi kisha akasonya.

                "Napoteza muda tu hapa" Aliongea kwa dharau na kisha akamsogelea Wilson ambapo alimuachia mapigo ya karate katika sehemu mbalimbali za mwili wake,pigo la mwisho alilimalizia katika mfupa wa koo wa Wilson na huo ndiyo ukawa mwisho wa Wilson  kujaribu kupambana naye. Baada ya kumaliza kwa pigo hilo hakutaka kupoteza katika eneo hilo yeye aliamua kuvaa kofia yake kisha akaondoka taratibu hadi barabarani, alipofika  barabarani alitembea kwa mwendo wa taratibu akiwa anarudi kwenye makutano ya barabara ya Sea view,Ufukoni na Obama ambako ni upande kulipokuwa na hospitali ya Aga khan kwa karibu.


****


   Baada ya kuingia ndani ya chumba cha kuongozea kamera alipokuwa  Godwin,  DCP John alimuamru auweke mkanda wa kamera ziliyopo pale kwenye wodi ya Mufti. Godwin aliuweka ule mkanda ambao ulikuwa ukionesha katika eneo ambalo waandishi wa habari walikuwa wamekaa wakiwa wanasikiliza maneno ya Mufti,pia katika upande ambao Mufti alikuwepo kwa kioo kingine. DC John alitumia muda huo kuangalia mwandishi wa habari mmoja baada ya mmoja na akajikuta akiwa amevutika kumuangalia mwandishi wa habari aliyekuwa na kamera ya kizamani akiwa amejibana pembeni katika eneo ambalo alikuwa akichukua mkanda wa video katika nyuzi arobaini na tano wakati kamera zingine zilikuwa zikichukua mkanda wa video kwa nyuzi tisini kamili. Alitazama kwa umakini mwandishi wa habari huyo akiwa yupo ametegesha kamera yake tu  akiwa hatii jicho katika sehemu ya kuchukulia mkanda huo, alikuwa amevaa spika za masikioni na waya mmojawapo ulikuwa umetoka kwenye kamera yake na kwenda hadi kwenye moja ya vipaza sauti ambavyo vilikuwa vimewekwa mbele ya Mufti.

     DCP John alikuwa akimtazama mwandishi wa habari huyo kwa umakini sana hadi pale Mufti alipopigwa risasi na akamuona mwandishi wa habari akiwa kama mwenye kushtuka baada ya risasi kupenya kwenye kifuo cha Mufti, ajabu aliposhtuka alitazama kushoto na kulia na alipooona waandishi wa habari wengine wakiwa wanchanganyika kutoka nje kuokoa maisha yeye alichomoa waya wa kipaza sauti chake kisha akainyanyua kamera yake kwa wepesi wa hali ya juu na akaivaa shingoni kisha akatoka kwa kasi sana. Mkanda huo wa video ulipofikia hapo DCP John alimwambia Godwin ausimamishe haraka naye akatii, ilikuwa imeganda katika sehemu ambayo mwandishi wa habari huyo alikuwa akiuvuka mlango huo.

                   "Mh! Waandishi wa habari wenye kamera ndogo na za kisasa waliposhuhudia risasi ikitua kifuani kwa Mufti walikimbia, kwanini huyu mwenye kamera kubwa tena la analojia akumbuke kuibeba kamera hiyo kama kweli likuwa amechanganywa na tukio hilo. Apate hata  muda wa kuuchomoa waya wa mike ya kamera yake na kukimbia kwa haraka. Inawezekana vipi?" DCP John alijiuliza maswali kichwani mwake, mikono alikuwa ameiweka kidevuni huku viwiko vya mikono vikiwa vipo juu ya meza kubwa ambayo mbele yake kulikuwa na vioo vingi vya tarakilishi  ambapo viwili kati ya hivyo ndiyo vilikuwa vikionesha kile alichokuwa akikiangalia.


                   "Hebu urudie tena huo mkanda" Alimpa amri Godwin ambaye aliurudisha nyuma tena mkanda huo wa video na ukaanza kuonesha upaya kile alichokuwa akikiangalia hapo awali, safari hii
aliutazama mkanda huo kwa umakini wa hali ya juu sana.

    DCP John alikuwa akiyatazama matendo yote aliyokuwa akiyafanya mwandishi huyo wa habari aliyekuwa amevalia kama mtu mzima asiyeenda na wakati, alimtazama kwa umakini sana wakati akizungumza maneno yaliyomfanya awaite waaandishi wa habari yeye hakuwa na umakini kabisa wa kamera yake alikuwa yupo akimtazama Mufti tu. Alimuona akitoa simu yake mkononi akiandika ujumbe wa maneno kisha akairudisha mfukoni, baada ya hapo aliendelea kutulia tu eneo hilo akiwa anamtazama tu Mufti na baada ya muda alishtuka kisha akarudisha jicho kwenye kamera yake halafu akasimama tena wima akawa anamtazma tu Mufti.

    Ilipita kipindi cha muda wakati Mufti akiendelea kuzungumza ambapo alimshuhudia akiwa ametulia tu, baada ya Mufti kuanza kutaja majina ya wasaliti yeye alikuwa akimtazama kwa umakini sana. Haikupita hata muda mrefu alitumbukiza mkono kwenye mfuko wa suruali yake akatoa simu yake kisha akagusa kwenye kioo hicho cha kugusa cha simu hiyo na akaiweka sikioni. Alisikiliza simu hiyo ikiwa sikioni kwa sekunde kadhaa kisha akairudisha tena mfukoni, baada ya hapo aliweka jicho kwenye kamera yake kwa umakini sana huku akiwa anaipeleka pembeni kidgo  na akasita kuipeleka na kushika kitu kama plstiki kilichokuwa kipo chini ya kamera hiyo akakirudisha nyuma kwa haraka. Muda huohuo kioo kingine cha tarakilishi kilichokuwa kipo pembeni ya kioo kile alichokuwa akiangalia DCP John kilioensha jinsi kifua cha Mufti kilivyotifuka damu kwa risasi.

                "Hapohapo rudisha tena nyuma kidogo" Alimuamuru Godwin ambaye alitiii amri hiyo na kuurudisha mkanda huo wa video nyuma, aliangalia tena kisha akamuamuru asimamishe pale  mwandishi yule alipokuwa akichukuliwa na kamera ya ulinzi kwa mbele ambapo kamera yake ilionekana vizuri sana.

                 "Kuza hiyo kamera niione vizuri" DCP John aliamuru naye akatii  amri, Dcp John aliona tundu juu ya kamera ya mwandishi huyo wa habari ambalo lilimfanya asikitike sana baada ya kujua kuwa huyo ndiye alikuwa ni mwandishi wa habari aliyekuwa amempiga risasi Mufti. Bila ya kuchelewa DCP John aliingiza mkono kwenye mfuko wa suruali yake akatoa simu ya ake ya kisas kabisa ya kuguza kioo.

                "Una USB cable hapo" Alimuuliza Godwin

                  "Ndiyo upo" Godwin alijibu kisha akafungua mtoto wa meza akatoa waya maarufu wa kuunganisha tarakilishi na simu ya mkononi kwa ajili ya uhamishaji mafaili, alimpa waya huo DCP John ambaye aliuchomeka kwenye simu yake na kisha akauchomeka kwenye mashine ya tarakilishi.

                   "Ingiza hizo viedo zote mbili kwenye memory card ya simu yangu"DCO John alitoa amri baada ya kuruhusu mtindo wakuhamisha mafaili katika simu yake, Godwin bila ya kuchelewa aliingiza video hizo mbili zote.

                  "Asante kwa ushirikiano wako kijana" DCP John alimuambia huku akimpatia mkono.

                 "Karibu muda wowote" Godwin  aliikubali shukrani hiyo.
DCP John baada ya kuchukua ushahidi huo kwenye  simu yake hakuwa na cha kupoteza humo ndani ya chumba cha kuongozea kamera, alitoka nje kwa haraka sana akimuacha Godwin akiwa anaendelea na kazi nyingine zilizokuwa zikimuhusu.


****

    Majira ya saa tatu usiku Mufti aliondolewa kwenye chumba cha upasuaji baada  madaktari kufanikiwa kuitoa risasi kuitoa risasi iliyokuwa ipo ndani ya kifua chake, alikuwa yupo katika hali mbaya sana na alipotolewa ndani ya chumba hicho alikimbizwa haraka katika eneo la wagonjwa mahututi akiwa yupo chini ya ulinzi mkalina pingu moja ikiwa mguuni mwake katika chumba cha pekee yake kati ya vyumba vingi vya wagonjwa mahututi. Ulinzi ndani ya wodi hiyo ulikuwa ni imara zaidi na nje na ndani ya wodi hiyo kulikuwa kumewekwa askari mwenye silaha  ambaye alikuwa na jukumu la kuhakikisha maisha ya Mufti yanakuwa yapo salama kwa muda huo  ambao alikuwa akihitsjika kuwa hai kuliko kitu chochote na jeshi la polisi.

    Muda huo tayari IGP Chulanga alikuwa ameshawasili katika hospitali akakuta kazi kubwa ikiwa tayari imeshafanywa na vijana wake waliokuwa wana utiifu wa hali ya juu wakiwa katika eneo lao la majukumu, kila alichokuwa akikitazma ndani ya hospitali hiyo tayari kilikuwa kimeshatekelezwa vile alivyokuwa akitaka yeye na kumfanya awe kimya na awe hana cha ziada cha kuongea kwa muda huo ambao kazi zote zilikuwa zimetimia tayari. Alikuwa akipewa maelezo yote na DCP John ambaye tayari alikuwa yupo eneo hilo akiwa amesimamia kila kitu kwa uadilifu wa hali ya juu, baada ya  kukagua  kila kitu na kuhakikisha kuwa kitu kilikuwa vile alivyokuwa akitaka yeye alirudi katika eneo la mapokezi akiwa na DCP John.

    Yule msichana wa mapokezi aliyekuwa akimletea jeuri DCP John alikuwa haishi kumtazama afande huyo kijana aliyekuwa na cheo kikubwa sana, roho yake ya huruma ilikuwa imemvutia sana na hakutegemea kama atakuwa na moyo wa namna hiyo akiwa kama askari aliyekuwa ameudhiwa.

    Muda ambao IGP Chulanga akiwa amekaa kwenye makochi ya mapokezi pamoja na DCP John yeye hakuisha kabisa kumtazama kama alikuwa akisikiliza kile ambacho maafisa hao wa ngazi za juu wa jeshi la polisi walichokuwa wakikijadili kwa muda huo. Hakuwa akitilia maanani kabisa maongezi ya wanausalama hao zaidi ya kuwa yupo makini kuutazama tu uso wa DCP John ambaye wala hakuwa na habari naye kabisa yeye alikuwa akisikiliza maongezi ya mkuu wake wa kazi.

               "John nimependezwa na kazi yako, hongera sana" IGP Chulanga alimpongeza

               "asante mkuu" DCP John alishukuru

                "sasa wewe endelea kuhakikisha vijana hawaleti uzembe hawa maana itakuwa aibu sana kwetu"

              "Sawa mkuu usihofu kuhusu hilo"

                 "Narudia tena hakikisha hawaleti uzembe hawa vijana na kuepelekea mtu aliyekuwa yupo chini ya ulinzi wetu tena kafungwa pingu mguuni aweze kupata madhara zaidi"

                "Sawa mkuu usihofu kabisa kuhusu hilo kazi hii imefika kwangu tegemea mazuri"

                 "Nakutegemea ndiyo maana nategemea mazuri kwako wewe ni kijana shupavu sana"

                "Kikubwa ni yupo hai  katika mikono yetu na jukumu la kuhakikisha anakuwa salama hadi anapata siha njema ni la kwetu sisi vijana wako"

                "Haswa kabisaa nafikiri....." IGP Chulanga alikatishwa na mlio wa simu yake mkononi ambayo alikuwa kaishika mkononi kwa muda huo, aliitazama simu hiyo akaona jina la N001 likiwa halina namba kama ilivyokuwa kawaida yake akiwapigia akiwa kazini. IGP Chulnga alipoona jina hilo alitambua wazi alikuwa akipigiwa simu na Mwanausalama mkubwa sana ambaye alikuwa akiogopeka na maadui  kutokana na ufanisi wake anapokuwa kazini, hakutaka hata kupoteza hata sekunde zingine kuiacha simu hiyo iite yeye aliipokea kisha akaiweka sikioni.

                 "Ndiyo N001........unasema mtuhumiwa yupo wapi?........ ok ok tunaenda kumuangalia sasa hivi" Simu hiyo ilikatwa na IGP Chulanga alishusha pumzi halafu akamtazama DCP John ambaye alikuwa tayari akisubiria jambo jipya pale alipoisikia namba ya utambulisho ya Norbert ikitajwa na IGP Chulanga.

                 "John huyu N001 sijui ni mshirikina maana simuelewi, hebu twende ukaone mwenyewe mtuhumiwa kashammaliza na kamuacha ufukweni kwenye barabara ya Sea view"

               "Etiii?!" DCP John alijifanya kushangaa lakini alikuwa akitambua wazi kuwa ilikuwa ni jambo la kawaida sana kwa Norbert kufanya kazi namna hii.

               "Kibaya zaidi kamkata kauli tayari ili asiendelee kuishi kwa ubaya alioufanya, hebu tukimbie mara moja hapo ufukweni na vijana"


    Baada ya kuongea maneno hayo IGP alinyanyuka kwenye kochi akifuatiwa na DCP John, kundi la maaskari wenye silaha walifuatana nao kwa pamoja kutoka nje ya hospitali hiyo. Walikimbia kwa pamoja mchakamchaka kwenda huko ufukweni kwenda kuangalia kile walichokuwa wameambiwa na Norbert kwa njia ya simu, ndani ya dakika kadhaa tayari walikuwa wameshafika katika eneo hilo la ufukweni na wakawa wanakimbia kuufuata uelekeo wa mbele ambapo kulikuwa na kuna alama za viatu kuashiria kuwa  kuna watu walikuwa wanakimbizana. Walienda kwa umbali mfupi hatimaye wakauona mwili wa Wilson ukiwa umelala mchangani ukiwa hauna uhai, wote kwa pamoja walipouona mwili huo waliusogelea karibu zadi ili waweze kumtambua alikuwa ni nani huyo mhalifu aliyekuwa ametumwa kuja kumuua Mufti lakini alishindwa kutokana na risasi yake kutofanikiwa kuutoa uhai wa mlengwa.

    Wote kwa pamoja walijikuta wakiwa hawaamini baada ya kusogea karibu kwa kumuona mtu ambaye hawakuwa wakidhania kabisa kama angeweza kujihusisha na shughuli za kihalifu ndani ya nchi hii, alikuwa ni mtu aliyekuwa akiheshimika kutokana na utajiri alionao na pia alikuwa ni mtu aliyekuwa akionekana ni mtaratibu mno. Chuki za wananchi juu ya kaka yake hazikuwa zikimpata yeye kutokana na moyo aliokuwa akisadia watu, watu masikini ndani ya nchi hii walikuwa wakimtambua vyema mtu huyo ambaye alikuwa akiwasaidia sana hata kuwapa ajira katika miradi yake.

     Si IGP Chulanga wala Askari wengine waliokuwa wameambatana naye walikuwa wakitarajia kuwa aliyekuwa amefanya tukio alikuwa ni mtu huyo, DCP John ndiyo pekee katika moyo wake hakuwa akishangaa ingawa katika uso wake alikuwa ameweka mshangao mkubwa sana. Alikuwa tayari ameshatambua alikuwa ni mmoja wa watu wabaya lakini hakuwa amejua kuwa ndiyo alikuwa amefanya tukio hilo, nguo zake ambazo alimuona nazo kupitia ule mkanda wa video ambao tayari alikuwa amemuonesha IGP ndiyo ulimfanya aamini kabisa alikuwa ni Wilson kwani umbile la mwili wake bado lilikuwa ni lile na halikuwa na ishara yeyote ya kupungua wala kuongezeka.

                    "ama kweli umdhaniaye siye kumbe ndiye, sikutegemea kabisa kama mtu kama huyu ndiye atakuwa adui wa taifa hili hadi atumike kuja kujaribu kufanya mauaji" IGP Chulanga aliongea.

                     "Mkuu unajua bado siamini lakini ule mkanda unaeleza kila kitu" DCP  John aliongea akijifanya kutoamini.

                     "John ndiyo hivyo imeshatokea, na hapa hamna uchunguzi wa zaidi hata mchoro hauna haja kwa mtu kama huyu aliyeuawa na mwanausalama anayeijua kazi yake" IGP Chulanga aliongea kisha akawageukia Askari aliokuja nao akawaambia, "hakikisheni mnaangalia huko nyuma hadi muipate kamera yake aliyotumia kufanyia tukio"

                   "Mkuu" Maaskari hao walitii amri wakapiga saluti na kugeuka nyuma kisha wakawasha kurunzi zao na kuanza kufanya msako.


*N001 KAMA MZIMU

*WILSON KAFAGIWA TAYARI

*USHAHIDI JUU YAKE BADO UNAKUSANYWA ENEO LA TUKIO, JE NINI HATMA YA MUFTI?



SEHEMU YA AROBAINI NA TATU SI MBALI TUWE PAMOJA KUONA UFAGIO UTAMALIZA KILA KITU AU UTABAKISHA TAKA NGUMU ZISIZOONEKANA.


No comments:

Post a Comment