Friday, January 6, 2017

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA THELATHINI NA TANO





RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________


SEHEMU YA THELATHINI NA TANO!!
            "Son of a bitch (mtoto wa mbwa)! Nani shoga?!" Thomas aliongea kwa kwa kali na ajitutumua akasimama ingawa maumivu bado alikuwa nayo na hata nguvu kwenye mwili wake ilikuwa imepungua kabisa, hasira zilezile alizokuwa akimuonya Benson na Santos wasiziendekeze sasa  zilimjia yeye na akawa nazo muda huo kutokana na maumivu aliyokuwa nayo. Alisimama kwa kuj
ikaza ingawa bado alikuwa anayumba kwa kukosa nguvu kutokana na teke zito la shingo alilopigwa na Norbert, akiwa kasimama hivyohivyo alikunja ngumi zake kwa nguvu sana hadi mikono ikawa inamtetemeka


______________TIRIRIKA NAYO

ILIVYOKUWA
    Muda mfupi kabla ya Thomas  kutoka ndani ya ngome yao, Josephine alitoka wa kwanza akiwa ameaga alikuwa anaenda kununua dawa kwa ajili ya maumivu ya kichwa chake katika eneo ambalo alikuwa amepigwa na kitako cha bunduki  katika siku chache zilizopita. Haukuwa udhuru uliokuwa na uongo ndani yake bali ulikuwa ni udhuru uliokuwa na kweli tupu ndani yake, bado Josephine alikuwa akitumia dawa maalum kwa ajili ya kupunguza maumivu katika sehemu yenye uvimbe ambao ulikuwa umeazna kupungua tangu alipopigwa na kitako cha bastola na Norbert. Alitoka kwa haraka ndani ya muda huo ili aepuke pia kukutana na mwanaume aliyetokea kumchukia ndani ya siku moja iliyopita, hakutaka hata kuonana  naye kwa siku hiyo na muda huo wa asubuhi kwa jinsi alivyokuwa akimchukia mwanaume huyo. Udhalilishaji uliokuwa ukifanywa  na Thomas katika siku iliyopita bado ulikuwa ukizunguka ndani ya kichwa chake, kila akiufikiria udhalilishaji huo alikuwa akizidi kumchukia mwanaume huyo ambaye alimuheshimu kama shemeji yake kwa Marehemu Benjamin.

    Chuki aliyokuwa nayo kwa Thomas ilikuwa ni mara mbili ya chuki aliyokuwa  nayo kwa Norbert kwa kumuulia mwanaume aliyekuwa akimpenda katika maisha yake, kitendo cha kushikwa kinguvu mithili ya kahaba kilikuwa ni tusi kubwa na hakutaka hata kumuona mwanaume huyo ndani ya asubuhi hiyo akiwa na hasira iliyochanganyika na kisirani cha kike. Hasira hizo alizokuwa nazo ndiyo ilikuwa chanzo cha yeye kuumwa kichwa kwa asubuhi hiyo kwani zilikuwa zikimtesa zaidi ya hata alivyoteseka moyoni baada ya Benjamin kufa tena ikiwa sababu kubwa ikiwa ni yeye kwa kusababisha hadi akapoteza umakini wake kwa Norbert aliyesababisha kifo chake. Sehemu ya nyuma iiyokuwa imeathiriwa kwa kupigwa na kitako cha bunduki ilianza kumuuma kwa taratibu kudunda mithili ya kuna moyo wake ndani yake, kukaa mbali na eneo hilo kwa masaa kadhaa ndiyo aliona ilikuwa ni suluhisho sahihi.
     Alifanikiwa kutoka ndani ya nyumba hiyo pasipo kuonekana na Thomas aliyemuona ni adui aliyekuwa yupo ndani yao, siku hiyo hakutumia usafiri kabisa kwani maumivu hayo ya kichwa yalimfanya hata asiwe na hamu ya kuendesha gari. Alitoka hadi  nje ya geti la nyumba ihyo akitembea kwa miguu pasipokutambua kuwa lilikuwa ni kosa kubwa sana kwa yeye kutembea kwa miguu  asubuhi hiyo. Josephine alikuwa akikaza mwendo aziwahi teksi aondoke huko kwenda kununua dawa  akiwa hatambui kabisa kuwa alikuwa tayari ameshafanya kosa kubwa kwa kutoka bila usafiri wa aina yeyote ile. Alipofika mbali na ngome hiyo alihisi  kushikwa begani na mtu kama alikuwa ana urafiki mkubwa sana naye, mtu huyo alimuwekea mkono begani kisha akauzungusha karibu na shingo na akamkaba kwa namna ambayo ni vigumu sana kuonekana na wapita njia. Ilikuwa ni kabali ya utaalamu wa juu iliyoibana shingo ya Josephine kwa kutumia eneo la nyuma ya kiwiko cha mkono.

     Kabali hiyo ilimfanya Josephine aumie kwani bado alikuwa ana maumivu kichwani mwake hasa sehemu ya nyuma ya kichwa na shingo, pamoja na maumivu bado hakuonesha kuwa alikuwa ameumia mbele ya mtu huyo alitulia vilevile ingawa ishara za mwili za kwake zilikuwa zimeshaonekana na mtu huyo kuwa alikuwa amepata maumivu kwa kabali  ile aliyokuwa amemkaba. Josephine aligeuza shingo kwa haraka ingawa haikugeuka vizuri kutokana na kukabwa na mtu huyo, alimtazama yule aliyekuwa akimkaba shingoni mwake kwa muda huo na akapokewa na tabasamu pana haswa kutoka kwa Norbert. Moyo wa Josephine ulimpuka haswa kwa kukutana na mtu huyo akiwa hata hajajiandaa kinamna yoyote kukabiliana naye, uhatari wa Norbert alikuwa akiufahamu vyema  na kuukabili alikuwa akitambua kabisa kuwa maandalizi muhimu sana.

    Alikuwa ameshachelewa kabisa katika kufanya maandalizi  hayo amkabili mtu hatari kama huyo ambaye alikuwa ana akili za zaidi ya binadamu wa kawaida, Josephine akiwa bado hata hajaongeza hatua ya pili alihisi kitu kikimgusa katika mbavu zake kwa kukandamiza. Alipotazama hakuambulia chochote zaidi ya kuona koti zito likiwa limeziba sehemu ambayo mkono wa pili wa Norbert  ambao haukuwa umemkaba shingoni mwake, ugumu wa kitu hicho kilichokuwa kikimkandamiza alitambua kabisa kilikuwa na asili ya chuma au bati gumu. Josephine alisimama ghafla huku  mapigo yake ya moyo yakimuenda mbio sana, fikra zake zilikuwa zimemuambia kuwa huo ndiyo ulikuwa ni  mwisho wake wa kuishi ndani ya dunia hiyo kama wenzake waliokuwa wametangulia. Hofu ya kifo ndiyo ilimchachafya haswa kwa muda huo hadi akashindwa kutembea, alikuwa akihema kwa nguvu sana huku akitazama wapita njia waliokuwa wapo pembeni yake.
     Wapita njia nao walikuwa wapo makini sana katika kuendelea na mambo yao kwani walikuwa wapo katika kuelekea katika mchakato wa kutafuta chakula cha siku, alipoangalia mita kadhaa kutoka pale alipo aliweza kuwaona madereva wa pikipiki wakiwa wanashuhudia kile ambacho kilikuwa kimemkumba ingawa haawakuwa wameelewa uhalisia wa kitu hicho hadi muda huo. Madereva hao waliona kama Norbert alikuwa amemshtukiza mpenzi wake kumbe alikuwa amemtia nguvuni adui yake kwa namna ya kijanja kabisa, Josephine akili yake ilifanya kazi mara mbili ya kawaida na akaona atumie njia ya kike zaidi katika kujikomboa na tukio hilo. Njia pekee ya kujikomboa na  mkono wa Norbert aliona ni kupiga kelele na hakuwa na namna nyingine, hakutambua kuwa wazo lake hilo alilokuwa akilifikiri ndani ya kichwa chake tayari lilikuwa limeshajulikana na Norbert kwenye uwezo wa hali ya ju katika kufikiri.
               "Usifikirie hilo wazo lako kelele hazitokusaidia kabisa kutoka hapa ni bora uwe mpole tu" Norbert alimuambia Josephine kisha akampiga mabusu mawili akiwa bado ameweka mkono wake  shingoni mwa Josephine, busu moja alimpiga la shavuni na jingine alimpiga la mdomoni.
                "Tabasamu basi" Alimuambia kisha akamuongeza busu jingine pasipo kujali waendesha pikipiki waliokuwa wapo katika kituo chao wakisubiria abiria walikuwa wakishuhudia suala hilo, Josephine alijikuta akiwa hana ujanja na alitabasamu tu na kupelekea madereva hao wa pikipiki wafurahie kitendo hicho, hawakujua kabisa kama Josephine alikuwa yumo ndani ya hatari wao waliona walikuwa ni wapenzi wa kawaida tu.
                  "Piga hatua na twende ninapoenda, usijidanganye kama unaweza kunitoroka my love. Hii iliyogusa mbavuni mwake ni bastola ileile iliyokujeruhi bega nadhani unaikumbuka. Pia ndiyo aina moja na bastola uliyojaribu kuniteka nayo kule Mwembeyanga, tasabasamu basi jamani usinune hata hupendezi" Norbert alimuamuru na Josephine hakuwa na ujanja alifanya vile alivyokuwa ameamrihwa, maneno yote hayo Norbert alikuwa akuyaongea kwa sauti ya chini sana kama alikuwa akimchombeza mpenzi wake.

      Josephine naye aliachia tabsamu kila alipoambiwa na Norbert afanye ivyo na akazidi kuwapoteza kabisa kimawazo wale madereva wa pikipiki maarufu kama 'Bodaboda' , madereva hao waliona kuwa walikuwa wakipewa faida kabisa katika kuona kile ambacho hawakupaswa kukiona kwa jamii ya kitanzania. Wao waliamini utandawazi ndiyo ulikuwa ni chanzo cha watu hao kuonesha mapenzi hadharani, waliona ni sehemu moja ya burudani katika kushuhudia watu waliokuwa na mapenzi ya dhati hadi wakwa hawaoni hofu kuonesha mapenzi yao hadharani.  Norbert pamoja na Josephine walikaza mwendo hadi wakawapita madereva wa bodaboda ambapo Norbert aliwaonesha dole gumba na wote wakashangilia, alipowapita huko nyuma aliacha wakiwa bado wanawaza kile walichokiona  kwao wakiamini ilikuwa ni mapenzi makubwa kumbe ni mtu katiwa nguvuni na adui yake ambaye ni moja ya watu waliokuwa wapo katika orodha ya watu aliokuwa akiwachukia ndani ya dunia hii.
     Baada ya kuwavuka kwa hatua kadhaa Norbert alitoa Mkufu wenye kidani ambacho kinapendeza machoni kwa mtazamaji yeyote akamvisha Josephine kwa mkono ambao alikuwa ameuweka shingoni, baada ya hapo alimuachia atembee naye akiwa yupo huru kabisa huku silaha yake akairudisha kiunoni kiusiri zaidi.
               "Ukae utambue nilichokuvalisha shingoni mwako si kidani bali ni bomu, kidani hicho ni bomu dogo  lina hatari kubwa hivyo usijione upo huru kabisa. Tuondoke bibie nimekuhamu sana" Norbert aliongea kwa tabasamu kama alikuwa akimuambia Josephine kitu cha furaha kumbe alikuwa akimuambia kitu kisichohitajika kufurahiwa kabisa labda kifurahiwe na asiye na akili timamu, Josephine aliona sana alikuwa amekamatika kwani ule mkufu aliyokuwa amevalishwa ilikuwa imekamata shingoni mithili ya mikufu ya asili maarufu kama 'culture'.
       Josephine na Norbert walitembea hadi ilipo hoteli ya Enot ambapo walichukua chumba kisha wakaenda hadi chumbani humo kinamna ileile. Muda ambao walikuwa wakiingia ndani ya chumba hicho ndiyo muda ambao Thomas alikuwa akitoka ndani ya ngome kwenda mazoezini ajiweke sawa kwa ajili ya kumaliza kazi iliyokuwa imemleta Tanzania, hakujua kabisa hiyo kazi aliyokuwa akijiandaa wala asingefanikiwa hata kufika muda huo wa kazi hiyo ili aweze kuitimiza.
       Walipoingia ndani ya chumba hicho Norbert aliweka vifaa vingine nyuma ya mlango baina ya chini ya kitasa na chini mahali ambapo komeo la kitasa lilikuwa likiingia pindi mtu anapofunga na ufunguo, kati ya vifaa hivyo viwili aliweka waya mgumu sana ambao ungeweza kuzuia mlango usifunguliwe na yeyote. Baada ya kumaliza kuviweka vifaa hivyo aliweka kidole gumba kwenye moja ya vifaa hivyo na taa nyekundu ikaonekana ikiwaka, alipomaliza kufanya hvyo alimgeukia Josephine ambaye muda alikuwa amekaa kitandani tu akiwa hana ujanja wowote zaidi ya kusali  ndani ya nafsi yake atoke salama ndani ya eneo hilo. Norbert alimtazama sana usoni jinsi alivyokuwa na hofu kisha akambania jicho moja huku akitabsamu, alimsogolea hadi pale alipkuwa ameketi akamshika viganja vya mikono yake kisha akamvuta juu akasimama bila kuleta pingamizi lolote lile.  Alipomsimamisha alimvuta upande wake kisha akaachia viganja vyake na kukikamata kiuno chake kilaini kabisa ambacho kilikuwa kimefunikwa na gauni laini, alimvuta karibu hadi kifua kilichobeba vifuu visivyokuniwa nazi kikawa kimegusa kifua chake. Norbert pasipo kujali hofu aliyokuwa nayo Josephine yeye alimbusu mdomoni huku akimpapasa sehemu mbalimbali za mwili wake, alipomuachia alimtazama huku akitabasamu lakini yeye hakulipata tabasamu kutoka kwa Josephine.
                "Bibie huna ujanja na ukweli ndani yako tu ndiyo utakaokuokoa na si kingine, mmebaki watano katika mpango wenu kwani Kamishana tayari yupo mikononi mwetu. Sasa chagua ufe wewe au nimpate mwenzako kwa kukutumia wewe" Norbert alimuambia huku akimtazama usoni, Josephine alionekana ni mwenye kufikiria sana  alipoulizwa jambo hilo na alitumia dakika takribani dakika mbili bado hakuwa ametoa uamuzi juu ya suala aliloambiwa.
                "Aaaah! Bibie huwezi kutoka humu kumbuka nimekufunga bomu shingoni mwako na hata pale mlangoni kuna bomu sasa jiulize utatokaje kinamna hiyo kweli,nimekupa njia ya kutoka humu sasa chaguo ni lako" Norbert alizidi kumshawishi Josephine aweze kumoata yeyote kati ya wanne waliokuwa wapo huru kwa muda huo, alimtazama Josephine usoni huku akiwa anasubiri jibu kutokana na ushawishi wake aliokuwa ameufanya.
   Ndani ya dunia hii hakuna kitu kibaya kama kuwekewa chuki na mwanamke kwani huwa moyo uliojaa kisirani na visasi sana, mwanamke ni mgumu sana kusamehe ikiwa alikuwa amefanyiwa jambo ambalo lilimuumiza ndani ya moyo wake ikiwa hakuombwa radhi. Haa akiombwa radhi pia ni vigumu sana kusamehe ndani ya muda mfupi au hata upite muda mrefu tangu akosewe, ndugu msomaji kama ulikuwa umemfanyia jambo lenye kuchukiza mwanamke kwa maslahi yako binafsi na unatambua kabisa mwanamke huyo anayajua mambo mengi yanayokuhusu  ni bora ukamuombe radhi na ukubali kujishusha. Bila ya kufanya hivyo ni jambo hatari sana kama ulikuwa na adui ambaye anafahamika wazi na mwanamke huyo, Thomas alikuwa amefanya udhalilishaji mkubwa sana kwa mwanmke asiyependa kudhalilishwa namna hiyo na hakuwa ameomba msamaha kwa udhalilishaji huo aliokuwa ameufanya usiku uliopita. Alikuwa akitambua kabisa kuwa Josehine anafahamu kila kitu kuhusu wao na alilichukulia jambo hilo ni kawaida, Thomas aliamini kabisa Josephine asingeweza kufungua mdomo wake katika kulitamka suala hilo kwa yeyote.

   Alikuwa akiamini kabisa kuwa anayeweza kushtaki suiala hilo ni yule mwanamke ambaye hajakua  kimwili na hata mwanaume hamjui, kosa kubwa hilo alilokuwa amelifanya zaidi ya makosa yote aliyoyawahi kuyatenda katika maisha yake ambayo yalimgharimu ndani ya dunia hii. Kisirani ndani ya mwanamke ni jambo la kawaida sana kama bahari kuwa na maji chumvi, hata awe na mafunzo kiasi gani ya kijasusi kama aliyokuwa anayo Josephine bado kiirani kitakuwa kipo ndani yake na ataweza kujizuia kwa mambo ya kawaida ila si kwa kudhalilishwa ikiwa ni mwenye kujiheshimu. Josephine akiwa yupo mikononi mwa Norbert aliwafikiria watu wote waliokuwa  wapo daniya kundi lao na hatimaye akaweka fikra zake kwa Thomas, alifikiria jinsi alivyokuwa akimtomasa usiku uliopita kinguvu kama alikuwa akimtomasa mcheza utupu ndani ya ukumbi wa usiku. Hasira zilimzdi sana na akaona huo ndiyo ulikuwa wakati muafaka wa kumkomesha mwanaume huyo asiyejua thamani na heshima ya mwanamke, bila kusita jambo lolote aliamua kufunguka yote kwa Norbert juu ya Thomas  ambapo alimpa mbinu nzuri adui yake ya kumnasa mwenzake ambaye ana chuki naye. 

   Ama kweli chuki ni ndugu wa damu wa usaliti kuwa na mwenye chuki juu yako anaweza kukufanyia jambo baya sana, mpango wa kumnasa Thomas ulipikwa ndani ya muda huo ukapikika na ulisukwa ukasukika. Josephine alipewa karatasi ndani ya muda akaandika ule ujumbe wa maandishi ambao ulikuwa umemfikia Thomas na kumfanya aende mtegoni mwenyewe. Ndani ya eneo hilo Norbert hakuwa peke yake bali alikuwa yupo na vijana wawili wa EASA  ambao aliwaita  kisha akatoa ule waya nyuma ya mlango na kuwapa mpango huo, mmoja wa vijana hao alikuwa ni mwanamke na mwingine alikuwa ni mwanaume. Norbert alipowakaribisha vijana hao alipokea begi la wastani kutoka kwa vijana hao, begi hilo aliliweka kando humo chumbani kisha akawa anasubiri kwa hamu mpango huo ufanyike baada ya vijana hao kuondoka. Vijana walipangiwa kila kitu na Norbert ambapo mmoja alikuwa ndiye yule muuza magazeti aliyempatia ujumbe Thomas na mwingine alikuwa ni msichana aliyejifanya anampa ujumbe kisha akatoweka kabla Thomas hajamuona.
   Baada ya vijana hao kuondoka humo ndani Norbet alirudisha mitego yake kama kawaida kisha akamrudia Josephine ambaye alikuwa yupo kitandani, alimshika vile awezavyo ambapo Josephine hakutoa upinzani wowote hadi miemko ikampanda akiwa  katika hali hiyo baada ya kushikwa maeneo mabaya ya mwili wake. Mihemko mbele ya chuki ina nguvu sana na hapo Josephine akajikuta naye akienda sambamba na Norbert katika zoezi hilo, ndani ya muda mfupi tayari  Josephine alikuwa ameondolewa mavazi yote yaliyokuwa yapo mwilini mwake na Norbert akiwa amepunguza baadhi ya mavazi. Walirudi mchezo ambao walikuwa wameufanya katika chumba cha hoteli kabla hawajaaanza kuisgi kama maadui dhahiri ambao uliwachukua saa moja wakawa wameshamaliza, Norbert baaada ya kumaliza alivaa nguo zake alizokuwa amezipunguza na akaketi kwenye kochi akiwa anasubiri majibu ya mtego aliokuwa amemuwekea Thomas.
   Mtego aliowekewa Thomas ulipozaa matunda wale vijana walimpa taarifa Norbeert ambaye alimuamuru  Josephine apige simu mapokezi na kuwaambia wamruhusu aingie moja kwa moja, Thomas alipokuwa akikaribia ndani ya jengo la hoteli hiyo yule mwanamke ambaye yupo chini ya Norbert alimpa taarifa mkuu wake.   Wakati Thomas akiwa anakaribia kufika mapokezi Norbert alipata taarifa na kwa aharaka zaidi alimfunga Josephine pingu miguuni, pingu hiyo aliifunga na kamba ambayo iliingia chini ya kitanda ikaenda kufungwa kwenye chuma maalum lilipo  usawa wa dirisha. Thomas alipokuwa akikimbia kupanda ngazi yeye aliutoa ule waya wa bomu uliokuwa upo mlangoni na aliuacha mlango ukiwa umerudishiwa tu, Thomas alipofungua ue mlango akamuona nJosephine akiwa yupo ndani ya taulo baada ya kutoka kucheza kwata na Norbert na kuingia kichwakichwa. Norbert alimpa pigo zito la shingoni kisha akaufunga ule mlango pamoja na kuuweka ule waya wa bomu. Hivyo  ndivyo Norbert alivyopanga mawindo yake kwa kutumia akili na hatimaye adui yake akawa ameingia ndani ya mtego wake.

****

    Kuitwa shoga na Norbert ni jambo ambalo lilizidi kumvuruga kabisa Thomas, akili yake yote ya kijasusi ilimtoka  ndani ya muda huo akawa anaendeshwa na hasira tu. Hasira zake zilizidi maradufu kutokana na maumivu makubwa aliyoyapata baada ya kupigwa teke zito na Norbert lililoenda  kutua kwenye shingo yake, hasira hizo zilimfanya atumie nguvu tofauti na nguvu alizokuwa nazo muda huo ambazo hata kusimama vizuri ilikuwa tabu. Nguvu hizo za ziada zilimuwezesha kusimama hata kumfuata Norbert akabiliane, hakuwa akijali kabisa kuwa utumiaji wa nguvu namna hiyo ni jambo la hatari sana kwani kuchoka upesi hakukuwa mbali kwa mtu mwenye hali kama hiyo. Thomas akiwa hana hata muhimili wakurusha teke zaidi ya kuwa na muhimili wa kusimama alimfuata Norbert akirusha ngumi kwa nguvu sana tena zisizo na idadi, alikuwa akirusha ngumi ambazo hazikuwa zikifikia lengo na asilimia kubwa zilikuwa zikienda nje ya lengo kutokana na kuongozwa na hasira kuliko akili aliyokuwa nayo ya kimapigano.

  Norbert naye baada ya kuona lengo lake la kumpoteza kiakili adui yake limefanikiwa, alikuwa akikwepa tu ngumi hizo ambazo zilimmaliza nguvu Thomas hadi akawa anamfuata Norbert huku akiyumba kama mlevi. Nguvu zilizidi kumuishia kuliko hata zilivyokuwa zimemuishia mwanzo lakini hakujali yeye alirusha ngumi tu hovyo huku akimfuata Norbert katika kila upande aliokuwa amehama akimkwepa, ndani ya robo saa tangu aanza kupigana alikuwa akihema kwa nguvu sana huku akipepesuka na hata macho alikuwa akitazama kwa kufumba kutokana na kutokuona vizuri baada ya uchovu kumzidi kiwango. Bado hakukubali kushinwa ingawa viungo vyake vilikuwa tayari vimeshakubali, aliamua kumfuata Norbert hivyohivyo hadi nguvu zikamuishia akaanguka alipomkosa Norbert kwa ngumi yake aliyotumia mwili mzima katika kuirusha. Aliangukia kidevu chini hadi akajing'ata ulimi na maumivu aliyoyapata ndiyo yalizidi kumtia hasira hadi akawa anaona kizunguzungu, pamoja na kuchoka bado hakuwa tayari kukubali kushindwa. Alijikakamua na akajaribu kujiinua sakafuni huku mikono yake ikiwa inamsaidia katika kuinuka huko ikiwa inatetemeka, alijitahidi aweze kufika hatua ya kusimama lakini mikono ilimsaliti na hatimaye akateleza mahali pasipokuwa na utelezi na akaangukia kidevu kwa mara nyingine.
         "Aaaaaaaaargh!" Alitoa ukelele dhaifu kwa viungo yake vya mwili kumsaliti katika kumkabili Norbert ambaye alikuwa amesimama mita kadhaa  kutoka hapo alipodondoka akimtazama kwa dharau.

*THOMAS HALI MBAYA, JE ATAPONA?
*CHUKI YAZAA USALITI KWA JOSEPHINE, JE ANYE ATASALIMIKA?
*NORBERT KATIKA UBORA WAKE, JE KAZI HIYO ATAIKAMJLISHA?


SEHEMU ZIJAZO ZA RIWAYA HII NDIYO ZINA MAJIBU YA MASWALI HAYO, USIKOSE KUWA PAMOJA NAMI KATIKA KUJUA MWISHO WA YOTE






MTUWIE RAHI, UMEME ULIKUWA NI TATIZO KWA SIKU ILIYOPITA

No comments:

Post a Comment