Thursday, January 12, 2017

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA AROBAINI

RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________





    SEHEMU YA AROBAINI!!
           "Niacheni mie nikamfuate huyu mshenzi!" Alifoka  kwa nguvu akiwa hafurukuti kwa jinsi alivyoshikiliwa kwa nguvu, Daktari na muuguzi huyo waliendelea kumshikilia Mufti kwa nguvu sana hadi alipotulia mwenyewe na kuacha kufanya fujo. Hapo walimuachia na wakabaki wakimtazama kwani machozi tayari yalikuwa yameshachukua nafasi yake machoni mwake, Mufti alianza kulia kwa muda mrefu kimyakimya na alipoacha kulia alimtazama Daktari aliyekuwa amekuja.

             "Nahitaji kuongea na waandishi wa habari muda huu huu" Alimuambia Daktari huyo ambaye alikuwa akifahamiana naye sana na alikuwa ni Daktari ambaye ni rafiki yake mkubwa sana, Daktari huyo aliposikia kauli yake hiyo alimkubalia kwa kutikisa kichwa huku akimtazama Mufti kwa tabasamu hafifu.



__________TIRIRIKA NAYO

                                     YALIYOJIFICHA HADHARANI
    Mnano saa moja jioni ndani  ya wodi aliyokuwa amelazwa Mufti tayari ilikuwa na halaiki ndogo ya watu waliokuwa wameshika kamera na wengune wakiwa na vifaa vya kunasia sauti,wengine walikuwa na kalamu na karatasi wakinukuu kile kilichokuwa kikiongelewa hapo. Ilikuwa ni muda ambao Mufti aliamua mwenyewe kukiri kile alichokuwa kakisema kuwa ni uzushi na pia ni muda ambao alikuwa akikiri kuwa Rais Zuber hakuwa na hatia hata kidogo, aliamua mwenyewe kukubaliana na masharti ya Norbert ya kuamua kukiri makosa yake ili ainusuru familia yake ambayo ilikuwa ipo mikononi mwa Norbert aliyekuwa yupo kwa maslahi ya taifa zima na si kwa Maslahi ya mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu waliokuwa wapo kinyume na matakwa ya taifa.
    Udhaifu wake ndiyo uliokuwa umeshikiliwa na Norbert na hakuwa na ujanja mwingine wa kuuokoa udhaifu huo mikononi mwake zaidi tu ya kueleza kile kilichokuwa kinahitajika kujulikana na umma wa watanzania, uamuzi aliokuwa amefikia ni kukifikisha kitu hicho kwa umma wa watanzania ili ainusuru familia ambayo aliamini kabisa ilikuwa kwa mtu hatari ambaye alikuwa hana mzaha na kile alichokuwa akikifanya. Sifa za N001 ambazo amewahi kuzisikia kutoka kwa viongozi mbalimbali katika nchi za Afrika ya mashariki ndiyo zilimfanya azidi kuwa na hofu na familia yake, uwezo alionao N001 wa kumuondoa mtu ndani ya dakika kadhaa ndiyo ulimfanya awe na hofu zaidi na familia yake.
    Hakuna mtu aliyekuwa hamjui mpelelezi huyo kila akitajiwa  namba yake ya kipelelezi, wote walikuwa wakimjua vyema alikuwa ni mtu mwenye zaidi ya hatari akiwa kazini. Hata nje ya bara la Afrika mtu huyu  walikuwa wakimjua ni nani ndiyo sembuse ndani ya bara hili asijulikane, kufikia mwaka huo tayari alikuwa ameingia katika wapalelezi bora wa dunia hii. Kile aliyekuwa akifungua katika tovuti ya umoja wa mataifa iliwaorodhesha wapelelezi hawa tayari alikuwa ameshamtambua huyu mpelelezi ingawa hakuwahi kuiona picha yake.

  Ndani ya tovuti hiyo ilikuwa ikionekana kivuli sehemu ya picha na chini  ya kivuli hicho ilionekana namba yake ya kipelelezi ndani ya EASA, haikuwa inajulikana yupo nchini gani kwa muda huo wala haikuwa inajulikana ni raia wa nchi gani. Sehemu ya kuonesha nchi anayotoka ndani ya tovuti hiyo kulikuwa kukionekana ukanda anaopatikana tu, hivyo haikuwa ikijulikana yupo nchi gani kati ya nchi tano za ukanda wa Afrika ya mashariki. Rekodi ya kazi yake bora ilikuwa imebaki kwenye vichwa vya watu ndani ya dunia hii waliopata kumsikia, tangu afanikishe kukamatwa kwa gaidi Brown Stockman  ambaye alizishinda nchi nyingi za Ulaya na kutoroka aliweza kubaki kuwa katika rekodi hiyo ya wapelelezi bora wa dunia.
   Sifa hizo alizokuwa nazo mtu aliyekuwa akimtambua kama N001 bila ya kumtambua jina lake kutokana na washirika wake kutomuweka wazi juu ya hilo kuwa wamemjua huyo mtu, zilimfanya akubali mwenyewe kukiri ubaya wake aliokuwa ameufanya kwa Rais Zuber. Washirika wake walikuwa wamemficha juu ya utambulisho wa huyo mtu kwakuwa hakuwa anajishughulisha zaidi kwenye mpango huo baada ya kazi ya kumchafua Rias Zuber tu itapokamilika, hivyo hakuwa amemjua Norbert Kaila ndiye huyohuyo aliyekuwa akimsumbua muda huo  yupo kitandani katika wodi ya hospitali ya Aga khan. Tangu kuuawa kwa Akosfu Edson baada ya kufanya kosa kubwa yeye bila ya kutambua,viongozi wote wa dini waliokuwa kwenye mpango huo hawakuaminiwa tena. Ndiyo maana hata kwenye mipango mizito dhidi ya Norbert kwenye ngome ya Wilson wao hawakuwepo, walikuwa wakipewa mpango baadaye na L.J Ibrahim baada ya wote kuukubali mpango huo. Mufti katika mpango wa kina L.J Ibrahim alikuwa ni kama muwa tu na muda huo kazi yake ilikuwa imeisha baada ya kutiwa mdomoni na kutemwa, si yeye tu hata Askofu naye alikuwa hivyohivyo ni wa kutumika ingawa wote walikuwa wakijiona thamani yao katika mpango huo ilikuwa ni ya milele tu hata baada ya kupata mgao.
   Akiwa mbele ya waandishi wa habari Mufti alijikohoza kusafisha koo lake kisha akatoa salamu kuwasalimia wanahabari hao pamoja na umma wa watanzania waliokuwa wakishuhudia moja kwa moja kile alichokuwa akikiongea muda huo, baada ya hapo alimshukuru Mungu kwa kuweza kumjalia ameweza kuzinduka kwa muda huo tangu alipopoteza fahamu. Aliongea mengi sana ya utangulizi asieleweke alikuwa anaongea nini lakini waandishi wa habari waliweka ustahimilivu wa kumsikiliza na pia kurusha kile alichokuwa akikiongea moja kwa moja, alitumia takribani dakika ishirini nzima katika kuongea ya utangulizi kisha akaamua kuingia kwenye dhamira ya kile kilichomfanya aamue kuongea na waandishi wa habari baada tu ya kupata na fahamu.

   Wengi wa waandishi waliona ilikuwa ni wasaa mzuri wa kuongea na kiongozi  huyo wa dini ambaye kupatwa kwake kwa mshtuko kuliitikisa jamii nzima ya kitanzania wakihofia alikuwa amekumbwa na kadhia nyingine kwa maneno aliyokuwa ameyatoa kwenye hotuba yake ya siku hiyo. Jamii ya watanzania walikuwa na hamu ya kusikia kile alichokuwa akitaka kukizungumza baada ya kuzinduka kwake kwa siku hiyo kwani tayari alikuwa ametokea kuwa kipenzi cha watanzania wa dini karibia zote ndani ya muda mfupi tu tangu kutolewa kwa hotuba yake, ilikuwa ni habari ambayo ilikuwa na soko kwa magazeti na hata kutazamwa na televisheni mbalimbali. Hivyo waandishi wa habari waojali habari zenye kuuza zaidi gazeti na kuongeza mamia ya watazamaji waliipa kipaumbele ndiyo maana walikuwepo hapo kwa muda huo.
             "Allah (s.w) najua ndiye aliyenipa fahamu hizi ili niweze kutimiza kile nilichokuwa natakiwa nikitimize kwa umma huu wa watanzania, Sina budi nimshukuru zaidi na zaidi hata kama akinichukua kwa mara nyingine nitakuwa nimekamilisha kile nilichokuwa nahitajika kukikalimilisha ili watanzania waondokane na upofu huu niliowaweka na pia wawe wenye kuona nuru ilipo walikimbie giza na mawakala wake.  Ndugu waislam na wale wasio waislamu nimekuwa wakala wa giza kwa kipindi kirefu sana na nikifanya yale yaliyokuwa yakienda kinyume na maamrisho ya Allah (s.w), leo hii nimeamua kuwa muwazi kwenu ili iwe funzo kwa viongozi wakubwa wa dini na pia waumini kuwa kila baya lina mwisho wake. Nimeshiriki katika njama nyingi katika kiongozi wa dini ikiwemo kuuza viwanja vya waislam kwa wawekezaji, kuwa upande mmoja na wale waliomuua viongozi wenzangu wa dini, mkuu wa majaeshi na pia. Nikiwa kama mwanadamu napasa kuwaomba radhi kwani nimekosea kama wanadamu wengine walivyokuwa wakikosea, nimechukua uongozi wa taasisi ya kiislamu na nimeikuta taasisi hiyo ikiwa na vitega uchumi vingi sana na hata maeneo yenye rasilimali chungu nzima ila niliviuza kwa maslahi binafsi na watu wachache ambao wapo serikalini na wengine watu maarufu Tanzania. Nilikuwa mtekelezaji mzuri sana wa yale niliyokuwa nikiwausia waumini wa dini ya kiislamu kutoyafanya, nikishirikiana na viongozi wengine wa dini hata kwa upande wa pili katika kuyafanya mambo kama hayo. Leo hii mabaya yangu yote hayo niliyokuwa nikiyafanya mwisho wake ni familia yangu kuingia hatiani, mke wangu na binti yangu" Mufti alisitisha kuongea baada machozi kumzidi kiwango na akayafuta, waandishi wa habari walikuwa wakisikitika sana kwa yale aliyokuwa akiyafanya, milango ya wodi yote ilikuwa wazi alipokuwa akitoa hotuba hiyo kutokana na uwepo waandishi wa habari wengi pamoja na wauguzi waliokuwa wapo sehemu ya mlangoni wakisikiliza maneno hayo ya Mufti.

             "Kikubwa zaidi na kibaya nilichokifanya ni kusimama kwenye mimbari takatifu kutoa hotuba yenye uzushi  katika eneo takatifu, kutumia imani za waumini juu yangu katika kuwaenezea uongo ambao waliuamini moja kwa moja ili tu serikali ya Rais aliyeleta maendeleo ndani ya nchi hii kuweza kupinduliwa na jeshi la wananchi wakiwa wameridhia kupitia kwetu sisi viongozi wa dini. Watanzania kwa ujumla napenda mtambue kuwa ndani ya siku mbili zijazo maneno niliyoyaongea yanapaswa yarudiwe tena yaleyale na Askofu mmoja maarufu hapa nchini ikiwa na yeye ni sehemu ya mpango wetu, pia tukaona haitoshi tukamsambazia uzushi Professa Moses Gawaza aliyeliletea taifa hili heshima kubwa kuwa  ndiye muuaji wa Jeneral Augustin Kulika, wanajeshi wa JWTZ waliokuwa nyumbani kwake na Askofu Edson ambaye alikuwa mwenzetu. Kutokana na uzushi huu tuliokuwa tumemuwekea Professa tumemfanya aweze kuishi kama digidigi akikwepa mkono wa dola yote ni kutokana na ukaribu wake na Mheshimiwa Rias, tulijali tu pesa wala si kujali kile kilichokuwa kikiwaumiza wao kwa tuhuma hizi za kizushi. Najua nimepatiwa pumzi hii kwa muda mchache  tu niweze kuwatoa tongotongo macho watanzania wote ili waweze kuona kiufasaha kile kilichokuwa kinahitajika kukiona, uzito wa mambo haya ninayoyaongea sidhani kama nitaweza kuiona siku ya kesho labda muweza wa yote aaamue hivyo na si vinginevyo". Mufti aliongea na alipofikia hapo alisita kwa mara ya pili na akachukua bilauri ya maji na akanywa mafunda kadhaa huku akihema kwa kasi.

****

MASAKI
    Saa moja jioni ikiwa inakaribia Mwanaume mmoja mtu mzima alikuwa amekaa kwenye kochi sebuleni akiangalia taarifa ya habari katika kituo cha televisheni cha BBC cha nchini Uingereza kujua kile kilichojiri  huko nje ya bara la Afrika, mwanaume huyu tayari alikuwa na habari ya kile kilichotokea mchana wa siku hiyo na hadi taarifa ya kulazwa kwa Mufti. Hakuwa na habari kabisa ya kuitishwa mkutano wa waandishi wa habari na Mufti huyo baada ya kuzinduka kwake ambayo ilikuwa imebaki muda mfupi iweze kuanza, akiwa yupo na bilauri ya Shurubati mkononi alikuwa akifuatilia kwa umakini sana juu ya kile kilichokuwa kikiendelea kwenye kituo cha BBC. Macho yake alikuwa ameyaelekeza kwenye televisheni wala hakutilia maanani hata mke wake alipokuja kukaa pembeni yake akiwa anamtazama yeye usoni, Mwanaume huyu aliendelea kuangalia televisheni kutokana na kuvutiwa sana. Mwanamke huyo alipoona mume wake hamuangalii aliamua kumuwekea mkono begani mwake na kupelekea mume wake huyo ageuke na kumtazama.
                   "Mume wangu jamani huoni kama saa moja ndiyo hiyo inakaribia" Mwanamke huyo alimuambia mume wake.
                    "Saa  moja hii kuna nini mama Salma"
                     "Jamani hujui kama Mufti ameitisha waandshi wa habari habari  baada ya kuzinduka na anaongea live"
                     "Ohhh! Kuna la muhimu labda hebu weka tuangalie" Mwanume huyo aliongea huku akimpatia mke wake rimoti ya luninga, Mwanamke huyo kwa haraka zaidi aliibadilisha chaneli aliyokuwa akiitazama mume wake hadi wakafikia chaneli ya kitanzania ambayo ilikuwa ikikua kwa kasi sana ambayo ndiyo iliku inaonesha tukio hilo muhimu. Tayari neno live lilikuwa limeshaonekana kwenye kioo cha luninga yao  na vipaza sauti mbalimbali vilikuwa vipo mbele ya kitanda cha hospitali mbele ya Mufti ambaye alikuwa amevaa mavazi maalum ya hospitali. Wote kwa pamoja waliweka macho yao kwenye televisheni kuangalia kile kilichokuwa kikiendelea kwa muda huo, mnamo saa moja kamili Mufti alianza kuongea na wao wakawa wanafuatilia kwa umakini sana muda wote aliokuwa akiongea utangulizi wa maongezi yake kabla hajaingia moja kwa moja kwenye kiini cha jamo alilokuwa akilitaka kuliongea.
                   "Mufti naye anatia siasa si aongee kama ana jipya nahisi huyu alitaka tu watanzania wamjue kama yupo hai hamna jingine lolote" Mwanaume huyo aliongea akionekana kutopendezwa na utangulizi wa Mufti.
                    "Jamani mume wangu si utulie kidogo tu aongee hadi amalize ndiyo useme hivyo" Mwanamke huyo alimtuliza mume wake.
                    "Hapa hakuna la maana naona kuna...." Mwanaume aliendelea kukosoa kile kilichomfanya Mufti aitishe waandishi wa habari lakini mke wake alimzuia baada ya Mufti kuanza kuomba radhi kabla hajaanza kupasua jipu ili watanzania waondokane na damu chafu iliyokuwa imejificha ndani ya jipu hilo, alipoanza kueleza juu ya uovu wake alioufanya mwaaume huyo alitulia kimya mwenyewe na akasikiliza kwa umakini sana. Alipofika katika eneo ambalo Mufti alikuwa amefichua mengi sana aliyokuwa hayafahamu uvumilivu wa kuendelea kusikiliza ulimshinda, alijikuta akisimama kwa haraka kisha akatoa simu yake mkononi na akatafuta sehemu ya majina kwenye simu yake hadi alipolipata jina ambalo alikuwa akilitafuta akapiga. Alisubiri simu hiyo ikiita na wala hakuwa ameweka macho yake kwenye televisheni tena, simu aliyokuwa anapiga iliita kwa muda mrefu sana jambo ambalo lilimfanya atembee hapo sebuleni kwake kama vile amewehuka akisubiria simu yake iweze kupokelewa na mtu aliyekuwa anampigia kwa muda huo. Mtetemo wa simu yake ya mkononi baada ya kupokelewa ulilitetemesha kidogo shavu lake, hapo mtu huyo alibaini kuwa simu hiyo ilikuwa imepokelewa na mtu aliyekuwa akimpigia.
                   "John upo wapi sasa hivi......sasa ondoka nyumbani kwako sasa hivi ukiwa na pingu.....nahitaji sasa hivi uende Aga khan hakikisha Mufti unamtia nguvuni na anakuwa yupo chini ya ulinzi  akimaliza tu maongezi hayo.....wahi haraka sana nahisi maisha yake yako hatarini na tukimkosa yey basi tutakuwa tumekosa shahidi mzuri wa juu ya mabaya walizofanya" Mwanaume huyo aliongea kisha akakata simu kwa haraka na akarudi kuketi kwenye kochi jirani na mkewe akiangalia luninga. Aliendelea kusikiliza mazito yaliyokuwa yamefichika ambayo Mufti alikuwa akiyafichua wa muda huo, akiwa anaendelea kuangalia kile kilichokuwa kikiendelea kwenye luninga jambo la ghafla ambalo lilimuacha mdomo wazi alilishuhudia likitokea hapo kwenye luninga. Jmabo hilo hakutarajia kabisa kama lingetokea katika eneo kama hilo, Mwanaume huyo alinyanyuka kwenye kochi kwa ghafla na mikono akaweka kichwani baada ya kulishuhudia jambo hilo. Si pekee aliyeshangazwa na jambo lile lililotokea bali hata mke wake naye lilimshangaza sana kutokea kwenye mazingira kama hayo, mke wake alibaki akiwa ameweka viganja vya mikono yake mdomoni baada ya kushuhudia kile kilichokuwa kimetokea muda huo.
                    "Kostebooo!" Mzee huyo aliita kwa nguvu baada ya kushuhudia kile ambacho kilikuwa kimetokea hapo kwenye luninga, haikupita dakika moja askari wa jeshi la polisi mwenye V moja begani aliingia kwa haraka hadi sebuleni hapo akapiga saluti.
                    "Afande" Aliitikia Askari huyo mwenye cheo cha kostebo
                    "Tayarisha gari  haraka sana tunaenda Aga khan sasa hivi" Alitoa amri
                    "Afande" Askari huyo aliitika kwa haraka sana kisha akatoka nje, mwanaume huyo naye hakuchelewa aliondoka sebuleni hapo aliingia ndani ambapo alikaa kwa daika kadhaa na alipotoka alikuwa amevaa nguo nyingine tofauti na alizokuwa nazo hapo awali.
                    "Mke wangu natoka mara moja naenda huko mwenyewe" Alimuambia mke wake
                     "si ungeagiza vijana wako mume wangu haina haja ya kwenda"
                      "No inabidi niende mwenyewe hii ishu si ndogo, kuwa IGP haimaanishi ndiyo kila kitu nitume tu"
                        "mmh!  Sawa baadaye basi, kuwa mwangalifu"
                      "Usihofu kuhusu hilo" Alimtoa hofu kisha akatoka sebuleni hapo kwa kasi sana kuelekea ulipo mlango wa kutokea nje, hakuwa mwingine ila ni mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Rashid Chulanga kwa mara nyingine anaamua kwenda kushuhudia kile alichokuwa amekiona kwenye luninga ambacho hakutarajia kama kitatokea muda huo.

****

                  "Ninaomba radhi kwa hili niilolifanya kwa watanzania wote, nimewafanya wasiwe na imani na kiongzi wao kisa tu mapinduzi ya jeshi yaweze kutokea kama ambavyo nilivyokuwa nimepewa kazi hiyo na mshirika wangu ambaye kwa sasa ndiye kiongozi wa jeshi ndani ya nchi hii.  Chanzo cha yote hayo hadi kutaka kuondolewa madarakani kwa Rias wetu mpendwa ni ndoa ya jinsia moja, ndugu watanzania wote napenda mfahamu kuwa rais wetu aligomea kusaini mkataba huu ambao alikuwa alipwe pesa nyingi sana ambazo zimezidi hata utajiri wote wa baadhi ya matajiri hapa nchini Tanzania. Mapenzi yake na uzalendo wake ndiyo vimechangia asiweze kukubali kuleta jambo hili nchini, kukataa kwake huku kumesababisha watu hawa ambao walikuwa wakitaka lihalalishwe wale njama na sisi  pamoja na waziri mmojawapo wa serikali anayeitwa...."  Mufti hakumalizia kulitaja jina la hiyo kwani mshtuko mkubwa sana ulikumba kifua chake na mdomo wake ukabaki kuwa wazi kama alikuwa amebanwa na pumu kali, eneo la kifuani mwake kulionekana damu ikitifuka kwa nguvu. Aliangukia mto uliokuwa nyuma yake kwa taraitibu na akawa ana hema kwa tabu sana, tukio hilo lilishuhudiwa na  waandishi wa habari ambao walikuwa wapo hapo kwenye wodi hiyo wakisikiliza maneno yake.

    Haikuhitaji elimu ya ziada kutambua kuwa alikuwa amepigwa risasi ya kifua na silaha iliyotumika ilikuwa imewekwa kiwambo cha kuzuia sauti ndiyo maana haikusikika sauti pindi mfyatuaji wake alipoipa ruhusa ya kutoka nje ya bomba lake. Kilichofuata baada ya hapo ilikuwa ni mvurugano wa watu waliokuwa eneo hilo kukimbia baada ya kushudia tukio hilo, waandishi wa habari hasa wa kike pamoja na wauguzi waliokuwa wapo karibu na eneo hilo walitoa mayowe ya uoga na wote walikimbia ndani ya chumba hicho huku waandishi wa habari wa kiume wenye mioyo ya ujasiri pekee wakawa wamebaki humo ndani wakipiga picha tukio zima lilitokea.

    Muda huo ndiyo IGP Chulanga alishuhudia katika luninga nyumbani kwake  kupigwa risasi huko kwa Mufti hadi akanyanyuka kwenye kochi, tukio hilo ndiyo lilimfanya afunge safari kwenda kwenye hospitali hiyo mwenyewe ingawa alikuwa amemtuma afisa wa chini yake aende. Karibu watanzani nchi nzima waliokuwa wakitumia luninga walikuwa wakishuhudia jambo hilo lilivyotokea huku wachache wasiotumia luninga walikuwa wakisikiliza kupitia redio ambapo walilisikia suala lote lililotokea huko wodini alipokuwa amelazwa Mufti. Chuki dhidi ya L.J Ibrahim akiwa ni mtu pekee aliyetajwa kwenye mpango ndiyo zilijengeka katika mioyo yao, wengi wao walisikitika sana walipogundua kuwa walikuwa wakimuhukumu asiye na hatia na hata kumtilia uharibifu yule ambaye hakuwa na hatia.
    Mufti kupigwa risasi katika muda mbao alikuwa akimtaja mmoja wa mawaziri waliopo chini ya baraza la mawaziri ambalo linaongozwa na Rais Zuber alikuwa yupo katika usaliti huo, suala hilo lilichukua sura yake nyingine kabisa katika vyombo vya habari vya kawaida na hata mitandao ya kijamii baada ya kusemwa na Mufti ambaye hakulimalizia kwani risasi ilipenya kwenye kifua chake ambayo ilitosha kabisa kumfanya asiendelee kuongelea suala hilo na pia kuwatawanyisha wanahabari waliokuwa wapo eneo hilo. Kupigwa risasi kwa Mufti akizungumza suala hilo ilikuwa ni kuaminisha kabisa umma wa watanzania kuwa alikuwa akiongea ukweli, wananchi moja kwa moja waliamini kuwa Mufti alikuwa ameongea ukweli ambao ulikuwa unaelekea mahala pabaya kama Mufti angeendelea kuongea na kuzuia kuendelea kuwaweka pabaya wahusika ndiyo risasi ikatumika kumnyamazisha.
     Hadi DCP John anawasili ndani ya eneo hilo la hospitali tayari baadhi ya askari wajeshi la polisi walikuwa wameshawasili hapo, Mufti alikuwa tayari amekimbizwa chumba cha upasuaji ili waweze kuyaokoa maisha yake baada ya kubainika bado alikuwa akipumua kwa shida. Alikuta maaskari wakiwa wameweka utepe maalum katika eneo ambalo Mufti alikuwa amepigwa risasi kuzuia watu wasiingie na ulinzi wa hospitali hiyo ulikuwa umeimarishwa  na maaskari hao huku msako wa mtuhumiwa ukiendelea. DCP John alipokea saliuti kutoka kwa maaskari tofauti ambapo aliingia moja kwa moja hadi kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Mufti, alitazama mazingira yote yaliyokuwa yapo hapo ndani kwa umakini mkubwa sana akabaini uwepo wa kamera ya ulinzi. Alipoiona kamera hiyo alitoka moja kwa moja ndani ya wodi hiyo kwa haraka sana akaeleka mapokezi katika hospitali hiyo, alitumia dakika mbili kutoka wodi aliyokuwa amelazwa Mufti hadi mapokezi akawa amefika kutokana na umbali uliopo.
                       Alipofika hapo mapokezi DCP John akiwa yupo ndani ya mavazi ya kiraia alitoa kitambulisho cha kazi na akajitambulisha halafu akasema, "nahitaji kuonana na mhusika wa chumba cha kuongozea CCTV kamera sasa hivi"


*MHALIFU KAFANYA TUKIO, JE NANI HUYO JAMANI?
*MUFTI MUHUTUTI ZAIDI YA AWALI, JE ATASALIMIKA?
*IGP CHULANGA NDANI YA NYUMBA KWA MARA NYINGINE

BADO TUNA SAFARI YA KUJUA MWISHO WA HAYA TUWE PAMOJA NDANI YA WAKALA WA GIZA


No comments:

Post a Comment