Tuesday, January 10, 2017

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA THELATHINI NA NANE





RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________



SEHEMU YA THELATHINI NA NANE!!

             "Walaykum salaaam, nani mwenzangu....unasema nani" Aliposikia utambulisho wa mpigaji wa simu hiyo alianza kutetemeka huku mpigo ya yakimuenda mbio na alisema, "N001 nini unataka kwangu?.....Hapana Mama Ilham wangu na Ilham wamekusoea nini jamani.....no usifanye hivyo sikiliza kijana" Alipokuwa akijaribu kumuhimiza N001 ambaye  ndiye aliyempigi simu simu ilikatwa kwa ghafla.

              "Halloo haloooo!" Aliongea kwa sauti lakini mpigaji alikuwa ameshakata mawasiliano tayari.



_____________TIRIRIKA NAYO

   Ubaya wa simu binafsi ni kutoweza kumpigia mpigaji aliyepiga simu hiyo ikiwa atakata,  simu hizi huweza kukupigia tu na si kumpigia mpigaji ikiwa atakata. Jambo hili lilimfanya Mufti ashindwe kuipiga namba ya N001 ilikuwa imempigia muda huo, kila alipojaribu kuipiga simu hiyo hakuiona namba  zaidi ya kuona neno 'Private'.  Alikuwa haamini kama namba ya mpigaji ilikuwa haionekani kwa  jinsi alivyochanganyikiwa na akajikuta akipiga tena simu hiyo, matokeo ni yaleyale kila alipopiga simu hiyo kuwa hakuna namba katika rekodi za kuingia katika simu hiyo. Mufti alianza kuhema kwa shida sana alipoona namba ambayo ilikuwa ikimpa taarifa ya kushikiliwa kwa mke wake na binti wake ilikuwa haipo, taratibu wahka aliokuwa nao ulianza kumsababishia hata kofia aliyokuwa ameivaa kichwani  mwake aone ilikuwa ikimletea joto.

    Kofia yake ya bei ghali iliyonakshiwa kwa uzi uliotengeneza pambo zuri aliivua akaiweka mezani, bado joto alikuwa akiliskia mwilini mwake na ikambidi avue na koti la suti alilokuwa amevaa juu ya kanzu. Upendo aliokuwa nao kwa mke wake taratibu ulianza kumtia hofu nzito ambayo ilifanya hata mapigo yake ya moyo yaende mbio, kiti alichokuwa amekikalia alikiona kilikuwa kikimuumiza na ikambidi asimae wima ofisini hapo mikono akiwa ameweka viganja vya mikono usoni mwake kutokana na kugwaya kwa taarifa aliyokuwa amepewa na N001  katika simu aliyokuwa amempigia. Aliweka mikono hivyo usoni huku akihema kwa kasi na alipoitoa mikono usoni jambo la kwanza alilolikumbuka ilikuwa ni kuichukua simu yake ya mkononi na  kutafuta jina la dereva wake mpya aliyemtuma kwenda kumchukua mke wake na kumpeleka msikitni kwa siku hiyo ya Ijumaa.

   Alipiga simu namba ya dereva wake huyo na kuiweka simu sikioni, alisikiliza mngurumo wa kuita kwa simu hiyo hadi pale  ulipokoma baada ya simu kutopekelewa. Bado hakuchoka aliipiga tena namba ya dereva huyo na simu iliita vilevile kisha ikakatika, Mufti alizidi kupagwa akajikuta akizunguka humo ofisini kwake akiwa hana uelekeo maalum.  Taratibu kichwa kilianza kugonga kwa maumivu ya taarifa hiyo na akajikuta akikaa chini kwenye zulia ofisni kwake kama kulikuwa hamna kiti, alijifikiria kwa muda alipokaa chini kwenye zulia hapo ofisini kwake na alichukua simu yake kwa mara nyingine kisha akapiga namba za nyumbani na akaisubiria simu ilipokuwa ikiiita hadi inapokelewa.
             "Enheee Subira!....vipi mama yako karudi hapo nyumbani......inamaana toka atoke hapo kwenda msikitini hajarejea...ok sawa mwanangu"  Alipomaliza alikata simu kisha akajikuta akimtukania tusi zito N001  tofauti na wadhifa wake unavyomtaka kuishi, alirusha mikono huku na huko huku akijifikiria cha kufanya na hatimaye akaitafuta namba ya dereva wake kwa mara nyingine na kisha akaipiga. Safari hii simu ya dereva wake huyo mpya aliyetoka kumuajiri siku chache zilizopita, ilipokelewa, Mufti ilipopokelewa hiyo simu alianza kuongea kwa wahka mkubwa hata bila ya salamu.
               "Eheeee! Majid......walaykum salaam....ah! Ukti si kwema sana vipi  Majid  yupo wapi?.... Unasema? Kalazwa tangu saa tano kwa kubanwa na pumu.......heeee! Mbona nimesikia kenda mchukua mke wangu kumpeleka msikitini na mpaka sasa mke wangu hajarejea nyumbani.......unasemaa! Kaja dereva dereva mwingine kamuachia gari baada ya kunipigia simu nikawaahidi kuwa nitamtuma mwingine aje kuchukua gari hapo nyumbani kwake.......ooooh! Mungu wangu" Mufti alipomalizia kauli hiyo alikuwa amekaa kitako na kiwiliwili chake kililegea kisha kikamalizia kwa kuanguka kurudi nyuma fahamu zilimpotea pao hapo.

****

     Moja ya kitu kilichokuwa kimewahi kuleta athari kubwa tangu kuwahi kupata uhuru kwa Tanzania, basi hotuba ya Mufti ilikuwa ni miongoni mwa vitu hivyo. Baada ya kumalizika kwa hotuba hiyo tayari waumini walikuwa wameshajikusanya na ilipotimia muda huu ambao Mufti alikuwa akipokea simu ya N001 maandamano makubwa ya kiislamu ambayo hayakuwahi kutokea nchini Tanzania yalianza kuchukua nafasi yake kwenye msikiti huo ambao ulikuwa umetolewa hotuba hiyo na Mufti katika swala ya Ijumaa. Maandamano hayo yalikuwa ni maandamano yasiyokuwa na kibali na hata polisi walishindwa kuyazuia, jeshi la polisi lilikaa kando kuhusu suala hilo na hawakuthubutu kuingilia maandano.

    Kuhofia jeshi la wananchi lililokuwa likitaka kumpindua Rais kwa sababu hizohizo hawakuingilia maandamano hayo. Maandamano hayo yalipita katikati ya jiji na kisha yakapita kwenye mitaa mbalimbali, maandamano hayo yalikuja kuweka kituo jirani kabisa na ikulu kwenye upande wa barabara ya Obama mita kadhaa kutoka ikulu ilipo kwa upande wa barabara inayopita karibu na viwanja vya gofu vya Gymkhana. Hapo waumini hao wa dini ya kiislamu wasiojua chochote kinachoendela waliweka kituo tena barabarani kwakuwa barabra iyo ilikuwa haitumiki kwa muda huo, waumini hao wakiwa hawajui chochote walikuwa wakipaza sauti juu kwa nguvu wakishinikiza Rais Zuber atolewe madarakni wakidai hakufaa kuwa rais hata kidogo. Waislam hao hawakuridhika kabisa kukaa hapo katika kushinikiza Rais Zuber atolewe madarakani, walisogea mbele zaidi hadi wakafika karibu na hospitali ya Ocean road ambapo waliweka kituo nacho wakendelea kushinikiza vilevile Rais Zuber hakufaa kuwepo madarakani alitakiwa atolewe mapema.

   Kiongozi wa maandamano hayo alikuwa ni Sheikh maarufu sana ambaye yupo chini ya taasisi ambayo Mufti alikuwa akiiongoza, mtu huyo ndiyo aliwashawishi waislamu waweze kuandamana naye hadi huko baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa. Ajabu kabisa aliyetoa hotuba iliyokuwa imeleta uchochezi hakuwepo kabisa kwenye maandamano hayo, waislamu hawa waliokuwa hawajui walitendalo wala hawakujiuliza kuhusu kutokuwepo kwake Mufti katika maandamano hayo. Hawakujiuliza kabisa kuwa imekuwaje huyo aliyekuwa ametoa tamko hilo ambaye alikuwa na taarifa na maandamano hayo hakuwa amejiunga nao, walikuwa hawana tofauti na wafuasi wa vyama vya siasa ambao walikuwa wakihimizwaa waandamane na viongozi wa vyama vyao huku viongozi hao wakiwa hawakushiriki maandamano hayo yenye kupinga jambo hilo kuonesha msimamo wao kivitendo na si kimaneno. Waumini hao walipoona kamera za waandishi wa habari zikiwaosogelea ndiyo walifanya sifa kabisa kwa kuzidi kupaisha sauti zao wakishinikiza hilo suala, walikuwa wapo huru zaidi kwani hakuna chombo cha dola chochote kilichokuwa kimewaingilia katika maandamano hayo yasiyo na kibali kama ilivyozoeleka kuingiliwa kwa maandamano mengine yasiyo na kibali katia nchi hii.

   Walivimbishwa vichwa zaidi walipoona kamera za waandishi wa habari zilikuwa zikichukua tukio zima, walijua kabisa kuchukuliwa huko na kamera za waandishi wa habari Rais Zuber alikuwa akiona kila kitu moja kwa moja. Kupata uhakika wakuwa ujumbe wao ulikuwa unafika moja kwa Rais Zuber wao ndiyo walizidi kupaza sauti wakimwaga shutuma mbalimbali juu yake, walikuwa ni watu wasiojua walitendalo wakitumia misimamo ya dini kwa jambo la uzushi walilokuwa wamepewa na kiongozi wao  ambaye hakuinua mguu wake katika kufuatana nao ili athibitishe kuhusu uzushi huo.

   Waumini bila ya kutambua walikuwa wakifanya makosa waliamua kumbadili jina Rais Zuber na kumbandika jina ambalo hakuwahi kuitwa katika maisha yake yote, walisahau kabisa  alikuwa ni muumini mzuri sana na swala za ijumaa alikuwa hakosi katika misikiti labda awe ametingwa na kazi za kiofisi. Siku hiyo bila ya kujali walikuwa naye kwenye swala  na hata katika kutoa shahada wakiwa wote kwenye 'tahiyatu' (huu ni kao amnao ni nguzo moja kati ya nguzo kumi na nne za swala zilizoorodheshwa na kitabu cha fiqhi, kwa wale wasiokuwa waislamu basi nafikiri inabidi mtambue kuhusu hilo ikitajwa neno hilo ambalo maana yake kiarabu ni   maamkizi).
   Waliamua kumuita kafiri waziwazi wakisema si pamoja nao na hakufaa kuwa muislamu kwa mambo aliyokuwa ameyafanya, walimuita pia ni kinyonga ambaye alikuwa akijibadili rangi rangi kutokana na mazingira yalivyo. Walisema mbele ya vyombo kuwa rangi yake kamili walikuwa wameshaijua hivyo hawakuwa wakihitaji wao kama waislamu kuwa na kiongozi kama huyo, yalikuwa ni  maandamano yenye fujo za midomo tu tofauti na fujo zingine zilizoeleka na kufanya vitendo. Uwepo wa wanajeshi jirani na eneo hilo pamoja na uwepo wa nyumba takatifu ya ikulu kuliwafanya wasifanye fujo ya vitendo ya aina yoyote kwa kuhofia kuzua tafrani kati yao na wanajeshi, uongo  ni sumu na muda huo walikuwa wamemezeshwa na sasa ilikuwa ikifanya kazi katika miili yao.

****

NDANI YA IKULU
    Hali ilikuwa tete haswa kwa Rais Zuber kila alipotazama kila kilichokuwa kikiendela nje ya ikulu, hakuamini kabisa Mufti aliyetokea kuwa na urafiki naye mkubwa na pia kuwa nae bega kwa bega kama viongozi wengine wa dini nchini ndiyo angetoa tuhuma ya uzushi kama ile hadi waumini wakaandamana hadi meneo ya jirani na Ikulu. Alikuwa akuyatazama matukio hayo kupitia kwenye luninga akiwa yupo ndani ya ofisi yake pamoja Moses, alipoiangalia hiyo taarifa aliweka viganja vya mikono yake usoni mwake mwenyewe huku akiinamisha kichwa chake chini. Aliona kabisa mwisho wake na familia yake ulikuwa umekaribia hadi muda huo, tamaa alikuwa amejikatia kabisa katika kujikomboa na suala kama hilo, Moses alikuwa akimtazama Rais Zuber tu pasipo kusema lolote na hakutaka amuoneshe ishara yoyote ya kumkatisha tamaa alipoiona hali hiyo. Moses alipoona Rais Zuber anazidi kukta tamaa katika suala hilo, aliamua kumpa moyo kwa kumbainishia nguvu zzilizopo upande wake.
                "Mheshimiwa hakuna baya litakalotokea ikiwa sisi tupo" Moses alimuambia
                "Ooooh! Moses come on unafikiri uongozi wangu utaendelea hapa, wananchi hawana imani na mimi tena wanashinikiza nitolewe. Jeshi lipo upande wao unafikiri nani atakuwa mwokozi wangu" Rais Zuber alilalamika
                "Mheshimiwa cool down, everything is undercontrol hakuna kitakchoharibika hata muda huu nafikiri tuhesabu masaa machache tu heshima yako itarudi na wabaya wako watakuwa weak" Moses alimuambia
                "But how, Belinda aanze kupinga amri za Ibrahim wakati anajua ni kinyume na amri za kijeshi huoni ni hatari maana majeshi yake  yashanizunguka"
                "Kuzungukwa si ishara wako upande wao wale wako upande wetu daima na ikitoka hiyo amri ya kuanza kukutoa humu ndani wao ndiyo watakuwa wanakulinda wewe amini fagio la chuma lipo  upande wa rais daima na si upande wa wasaliti. Mtoaji mkuu wa amri ni wewe katika jeshi hivyo Belinda ahwezi kukusaliti"
     Muda huohuo wakiendelea kuongea mlango wa ofisi hiyo maalum iliyopo humo ikulu ulifunguliwa kwa ghafla, wote kwa pamoja walielekeza macho yao mlangoni ulipofunguliwa mlango  huo kutoka na ughafla uliotummika katika kuufungua mlango huo. Hawakuwa wametarajia kama mlango huo ungefunguliwa kwa muda huo kwani walikuwa hawana kijana wa hapo mwenye shida au dharura kubwa ambayo Mheshimiwa anapaswa kuijua kiasi cha kumfuata bila hata kuwasiliana naye kwa mawasiliano ya simu. Macho yao yote yalikuwa yapo mlangoni kwa mshangao mkuu, walipomuona huyo aliyekuwa amefungua mlnago hakuwa ni adui yao wala  kijana wao yoyote walishusha pumzi za ahueni.
                "Mke wangu ni ufunguaji gani wa mlango huo hadi unatutisha si unajua hali ilivyo kwanini usifungue taratibu" Rais Zuber alimwambia mke wake ambaye ndiye alikuwa amefungua mlango muda huo
                 "Samahani mume wangu kama nimekukera lakini imebidi tu nije,mume wangu kumbuka Ummy ana mitihani shuleni kwao na inapasa ahudhurie katika mitihani hiyo. Watoto wote masomo wanatakiwa wahudhurie kila siku sasa kukaa ndani na kutotoka itakuwa mpaka lini jamani, huoni watoto wanapitwa na wenzao" Mke wake huyo ambaye uvumilivu wa kukaa ndani kwa watoto wake ulikuwa umeshamchosha aliongea.
                  "Khaaah! Sasa  mama Ummy kwahiyo unataka mimi nijisalimishe tu wakati sina kosa lolote" Raiz Zuber aliongea akoneshwa amekereka na maneno ya mke wake ambayo si mara ya kwanza kumuambia
                   "Sasa mume wangu unafikiri tutafanyaje kwa ajili ya maisha ya wanetu ya baadaye ikiwa tutaendelea kugoma hivi" Mke wa rais aliendelea kumuhimiza mwanmke baada ya uvumilivu kuwa umemshinda, Moses hakuwa ametia neno lolote katika maongezi hayo alikuwa  wakiwatzama tu jinsi tu na mke wake walivyokuwa wakibishana.
                    "Khaaa! Hivi we mwanamke una akili timamu kweli yaani nijisalimishe nifungwe halafu hapa Ikulu arudi Filbert Ole  kisa tu niliongea na Moses ambaye ni mtu wangu wa karibu ambaye kasingiziwa kama mimi. Haya nikishafungwa jiulize hao watoto wapate malezi ya upande mmoja na wakae na watoto wenzao wanaoamini  Baba yao alifanya baya jiulize wataishije? Akiingia Ole madarakani na  mawaziri wake watakuwa upande wake sasa jiulize kama watasoma shule moja na watoto wa hao mawaziri watakuwa na hali gani kama si kunyooshewa vidole kisa baba yao yupo ndani" Rais Zuber aliongea kwa hasira sana huku akimtazama mke wake ambaye aliingiwa na kimya cha ghafla tu bada ya kuambiwa maneno hayo.
                       "Yaani kukaa ndani hata siku tano hazijafika tayari uvumilivu ni zero je ungekaa mwezi si ungekuwa ushanigeuka wewe kama napingana maamuzi  yako hayo yasiyo na tija, kama ulikuwa na mimi katika kipindi chote nagombea na naungwa mkono na wewe ukifurahia na hata kwenye kampeni uliongozana na mmi ukiwa na furaha. Hukutambua kuwa shida inaweza kuja siku yoyote hii ni sehemu ya maisha vikwazo lazima viwepo, hivi kama kikwazo kidogo kama hiki umekosa uvumilivu na unanishauri mabovu inaonekana vikizidi utanigeuka wewe" Ris Zuber aliendelea kulalama, lawama hizo zilipofikia hapo Moses aliamua atoke humo ofisini.
                       "Samahani" Aliongea kwa kuomba radhi kwa malalamishi hayo ya mke na mume aliyokuwa ameyasikia ambayo hayakuhitajika yaingie kwenye masikio yake kwa muda huo, alikuwa akikwepa kusikia yale yasiyomuhusu na wala yasiyompasa yeye kusikia. Baada ya Moses kutoka nje matuta kwenye paji la uso wa Rais Zuber ndiyo yaliinuka kabisa na akamtazama mke wake akionesha kachukia kabisa, mke wake huyo alikuwa amekosa la kuongea baada ya kuangushiwa maneno hayo ambayo yalikuwa ni zaidi ya mzigo.
                      "Hata haya huna unakuja kuniambia mbele ya Moses mambo kama hayo unaonesha ni kiasi gani huna uvumilivu wala ustahimilivu kwenye shida wewe mwanamke, unafikiri katika kipindi hiki kigumu nani wa kunifariji mimi niweze kuwa na moyo wa uvumilivu na pia kuhakikisha nchi haiendi mrama kama si wewe. Washauri wangu watanishauri tu lakini kama sitokuwa na faraja kutoka kwako ni zero kabisa, ona Moses huyu ameamua kumsafirisha mke wake tu  kisa matatizo aliyokuwa nayo aliyajua tangu mapema kama yangemkabili. Mke wake amekuwa akimpa moyo sana na amekuwa yupo tayari arudi awe pmoja naye  lakini kutokana na uzito wa matatizo hayo amekataa kabisa, yule ni binti tu mdogo kwako mke wangu sasa jaribu kujifunza kutoka kwake kumpita umri haimaanishi umempita kimawazo wala kumpita kuolewa haimaanishi utakuwa unajua kila kitu kuhusu ndoa!" Rias Zuber aliongea kwa hasira
                       "lakini mume wangu watoto wale"
                       "Wamefanyaje?! Ndiyo wamekutuma uje kuniambia hivyo? Wao ndiyo wamekutuma uje kuniambia wako tayari baba yao niingie jela wakose malezi yangu waende shule? Sema basi!"
                        "Hapana"
                        "Inaonekana ni kiasi gani una unajali raha zadi ukisahau shida zitakuja muda wowote, sasa ni hivi jua wanajeshi wote waliokuwa wapo mbele kuizunguka ikulu wapo upande wangu na waliokuwa wapo nyuma ndiyo wapo upande wa msaliti wa nchi. Nikirudi madarakani utaenda kupumzika kwenu ili ujifunze nini maana ya ndoa"
                       "(Maneno hayo yalimshtua sana Mke wa Rias)Basi mume wangu, yasiwe hayo"

                        "Nikiweka uamuzi nimeshaweka sifuti naomba unipishe nina mjadala na kijana wangu juu ya hili linaloendelea"
                        "(Machozi yakimlenga)Mume wangu nisamehe"
                        "Nimesema nipishe niendelee na majadiliano na kijana wangu" Rais Zuber alipoongea maneno hayo alisimama kwenye kiti alichokuwa amekaa na kwenda kumshika mke mkno na kumtoa nje ya ofisi yake kisha akarudi ndani akakaa kwenye kiti chake huku viganja vya mikono vikiwa ipo kichwani mwake.

   Mke wake tayari alikuwa ameshamchanganya hadi muda huo aliokuwa amemtoa humo ndani kutokana na kukasirishwa naye, akiwa amekaa kwenye hicho kiti Moses  alifungua mlango na akarudi ndani kwa mara ya pili. Moses alienda kuketi kwenye kiti kilichokuwa mkabala na kiti cha Rais Zuber na akawa anamtazama tu  bila ya kuongea neno lolote. Hakutaka kuanza kumuongelesha neno kwa muda huo aliokuwa amechanganywa na kukata tamaa kwa mkewe na aliamua kunyamza tu, alikuwa akimtazama Rais Zuber jinsi alivyokuwa ameweka viganja vya mikono usoni mwake akionekana na mwenye kuchanganyikiwa kwa maneno ya mke wake.
                "Yaani hawa wanawake ni zero" Rais Zuber aliwadunisha wanawake wote kwa kosa alilolitenda mke wake kwa muda huo, wala hakuwa akifikiria kama miongoni mwa wanawake hao aliokuwa akiwadunisha mmoja wao ndiyo alikuwa amemleta ndani ya dunia hii, Moses hakuchangia kabisa maneno hayo yeye aliendelea kukaa kimya tu.

****

                 "Baba tumefanya nini mimi na binti yangu mpaka ukatuleta huku" Mke wa Mufti alikuwa akilalamika akiwa yupo ndani ya chumba maalum na Norbert ambaye alikuwa ameshatoa kanzu na ndevu za bandia alizokuwa amezibandika, Ilham alikuwa akilia tu baada ya kupata uhakika kuwa walikuwa wametekwa na mtu ambaye walidhani ni dereva mpya wa gari yao ya nyumbani ambayo hutumika ikiwa baba yake yupo ofisini na wana ulazima wa usafiri.

    Alikuwa akimtazama Norbert kijana aliyekuwa mtanashati ambaye hakufanana kabisa na kazi aliyokuwa akiifanya hadi akawatia nguvuni hadi muda huo. Walikuwa wamefungiwa ndani ya chumba cha kisasa chenye kila kitu ndani ya nyumba ya EASA, mazingira ya chumba hicho yaliyo mazuri bado hayakuwafanya wajione kama wapo mahali salama hasa kwa jinsi walivyoingizwa humo ndani ya nyumba hiyo.
            "Mume wako mama yangu ndiyo mwenye kosa wala si wewe hivyo mtakaa hapa hadi pale atakapokiri uzushi aliokuwa akiutoa kwenye hotuba ya leo, si Mheshmiwa Rais ndiyo kashinikiza kugawa viwanja vya waislamu kwa muwekezaji ili achimbe dhahabu baada ya maeneo hayo kubainika yana madini hayo. Akiendelea kukaa kimya kuhusu hili jua na wewe hautatoka" Norbert alimwambia.
            "Sasa Baba ninakutambua wewe ni mwandishi wa habari na hiyo ni kazi ya wanausalama  kama ilikuwa ni kweli au si kweli anasambaza uzushi, kwanini unaingilia kazi  isiyokuhusu baba yangu" Mke wa Mufti aliendela kumuambia, Norbert alipoyasikia hayo maneo hakujihangaisha kujibu badala yake alitumbukiza mkono mfukoni mwake na akatoa kitambulisho chake cha kikazi akampatia mke wa Mufti. Alikipokea kitambulisho hicho kilichokuwa kipo kama kitabu kidogo na akakifungua, alishtuka sana alipokifungua kitambulisho hiko na akakirudisha kwa Norbert ambaye alikuwa akimtazama tu umakini bila ya kuongea lolote.
              "Samahani baba yangu kwa kuingilia kazi yako" Mke wa Mufti aliomba radhi akiwa na hofu baada ya kubaini kuwa alikuwa akiongea na mwanausalama wa shirika la kijasusi la Afrika ya mashariki ambalo alikuwa akilisikia tu na hakuwahi kumuona hata mwanausalama mmoja wa shirika hilo, uoga juu ya wanausalama ambao aliwahi kuwasikia walikuwa ni hatari sana wakiwa kazini ndiyo ulimuingia muda huohuo.
             "Sina ubaya wowote nanyi naomba mtulie na mkae humu, ukifika muda wa kuachiwa mtaachiwa nyote" Norbert aliwaambia kisha akageuka nyuma akaufuata mlango wa chumba hicho walichopo hao, aliufungua mlango na akatoka. Norbert alitokea kwenye ukumbi mwembamba na mrefu uliopo ndani ya nyumba hiyo ya EASA , pembeni ya mlango huo alikuwepo Salum  yule kijana wake aliyefanya naye kazi kule Msasani ambaye alionekana alikuwa akimsubiri yeye tu atoke humo ndani ya chumba.
              "Vipi Salum mbona uko hapa?" Norbert alimuuliza
              "Mkuu taarifa mpya imeingia muda huu" Salum alimuambia
               "Enhee! Nipe ripoti" Norbert aliongea huku akianza kutembea na Salum alikuwa akifuatana naye.
                 "Mufti amedondoka kwa mshtuko ofisini kwake na hivi sasa amelazwa Aga Khan"
               "Nilitarajia hilo suala litatokea maana udhaifu wake ndiyo upo mikononi mwetu, sasa mwambie Eva aje nimpe ujumbe aende kule akampe huo ujumbe  ataoukuta akiamka tu"
                "Sawa mkuu"
                 "Mwambie aje ofisini sasa hivi leo hii siku ni hakuna kulala"
                  "Sawa mkuu"
   Norbert alipotoa amri hiyo alikaza mwendo kuelekea ilipo  ofisi ndani ya nyumba hiyo ya kijasusi, Salum alienda moja kwa moja kwenda kumuita Eva kama alivyokuwa ameagizwa na mkuu wake.

*MUFTI HOI MWENYE UDHAIFU UDHAIFU WAKE UPO MIKONONI MWA WENGINE
*NDANI YA ALASITI TU MASAA TAKRIBANI TISA YAMEBAKI MAPINDUZI YAANZE, JE YATAFANIKIWA?
*MKE WA RAIS AZIDI KUMCHANGANYA MUMEWE, NINI HATMA YAKE?

SEHEMU YA THELATHINI NA TISA NA KUENDELEA NDIYO ZINA MAJIBU YA HAPO USIKOSE KABISA YAANI






No comments:

Post a Comment