Thursday, December 1, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA KUMI NA NANE




RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________




SEHEMU YA KUMI NA NANE!!

    Majira saa kumi alasiri aliwasha simu yake ambayo aliizima kutokana na kazi zake, muda huo huo alianza safari ya kuiacha wilaya ya Karatu ili aende uwanja wa ndege wa Arusha aweze kurudi jijini Dar es salaam.



    Alikuwa yupo katikati pikipiki ya kukodisha ambayo ndiyo aliona ni njia pekee ya kumfikisha uwanja wa Ndege wa Arusha haraka sana, kutokana na mwendo mkali uliokuwa unatumiwa na dereva wa pikipiki hiyo alitumia saa moja na akawa tayari yupo katika uwanja wa ndege wa Arusha.


****

    Norbert aliingia ndani ya  uwanja ya ofisi za uwanja wa ndege wa ndege eneo la mapokezi akaizima kamera yake ndogo, hapo alikutana na sura ya msichana mrembo ambaye alimtolea tabasamu la kebehi tu baada ya kumuona. Norbert naye alirudisha tabasamu na akajongea katika dawati la mapokezi uwanjani hapo, alipofika aliegemeza  viwiko vya mikono juu ya dawati hilo akawa anamtazama huyo binti kwa tabasamu pana.

               "Loh! Mwanaume mbaya wewe" Yule binti alimuambia.

               "Haaaaaa! Bibie  ndiyo salamu yako hiyo" Norbert alimuambia yule binti.

               "Yaani hata hiyo hamu ya kukusalimia sina kwakweli, unaingia Arusha hadi sasa hivi najua unataka kuondoka bila kunipa taarifa" Binti huyo alimuambia Norbert huku akionekana kutopendezwa.

                "Fatma unajua nimekuja ghafla tu nisamehe mke wangu, ukininunia wewe dunia nzima chungu kwangu" Norbert alichombeza huku akimtazama usoni na binti huyo akaanza kuangalia kando.

                "We sema tu tiketi ya Dar jioni hii siyo kuniletea hizo ngonjera zako" Fatma aliongea huku akikwepa macho ya Norbert.

                 "Haaaaaa! Fatma maneno gani hayo kwahiyo mimi sipaswi kukuambia maneno mazuri tu lazima unihisi nataka kusafiri kupitia wewe unifanyie mambo marahisi, ok tufanye hivi ngoja niende ofisi za makampuni ya ndege zenyewe nitapata hata ya kesho asubuhi. Jioni njema bibie" Norbert aliongea maneno hayo kisha akaanza kupiga hatua taratibu kuondoka eneo la mapokezi akawa anaelekea nje, hakutaka hata kutazama nyuma kumuangalia Fatma.

    Alipiga hatua ndefu  kuonesha kwamba hakuwa amefurahia maneno ya Fatma, alipofikia mlango wa kutokea nje alivutwa mkono kwa nyuma. Alipogeuka alimuona Fatms akiwa ana uso wa huruma sana akiwa anatikisa kichwa kukataa jambo, Fatma alikuwa akikataa Norbert asiondoke na alikuwa akimtazama Norbert ambaye hakuonesha mzaha katika uso wake.

            "Fatma nini achia mkono wangu niwahi nikafanye booking unanichelewesha" Norbert alimuambia.

                "Norbert please nisamehe nimekosea" Fatma aliongea kwa huruma.

            "hujakosea Fatma sema mimi niliyekuja kuleta uhusiano kazini nimekosea ukaniumbua wacha niondoke nikafanye booking hujui nina haraka ya kiasi gani" Norbert aliongea huku akiutoa mkono wa Fstma na binti huyo chozi likaanza kumdondoka hapohapo, chozi lake liligeuka machozi akawa anamtazama mzee wa warembo huku akizidi kuyadondosha machozi.
  
    Hakika alikuwa hajiwezi kwake na kauli yake mbele ya haraka ya Norbert kuingia Dar es salaam aliiona chungu, hakujua Norbert alikuwa kaingia vipi Arusha alichojua yeye ni kuweka wivu mbele tu.

             "Nor please usiniumize naomba rudi nitakufanyia mpango uondoke na ya juoni hii" Fatma aliongea kwa uchungu pasipo kujali yupo katika eneo la kazi, upungufu wa watu jioni hiyo ambapo wengine walikuwa tayari wamepitiliza kwenda kuketi kwenye ndege kusubiri ndiyo ulifanya pasiwepo na mtu mwenye kupata faida juu ya maongezi hayo.

             "Rudi sehemu ya kazi" Norbert alimuambia.

             "Nor please usinikasirikie njoo nikupe tiketi nataka niondoke sasa hivi shift nishamaliza namsubiri mwenzangu aingie yupo anabadili nguo" Fatma alimuambia Norbett huku akiwa bado anatokwa na machozi.

            "Ok" Norbert alikubali kisha akarudi eneo la dawati mapokezi, Fatma alimpatia tikiti ya shirika la ndege la Precision, Norbert aliipokea ile tikiti kisha akaanza kuisoma halafu akaifunga akamwangalia Fatma usoni.

           "Bado nusu saa ndege iondoke" Fatma alimwambia Norbert, muda huo huo msichana mwingine wa mapokezi aliingia hapo kwenye dawati la mapokezi na Fatma akatoka akampisha.

    Fatma alienda hadi sehemu aliyosimama Norbert akamshika sehemu za juu za kiwiko chske huku akimtolea tabasamu.

            "Naweza kukusindikiza sasa hivi" Fatma aliongea huku akitabasamu akawa anajongea sambamba na Norbert.

            "Halafu Fatma hivi mbona una wivu hivyo hata safari ya kikazi ya ghafla unanionea wivu jamani" Norbert alimuambia.

            "Haaa! Babu wee mimi abiria hivyo kuchunga changu muhimu"

             "Siibiwi mama ila kazi yangu emergence nyingi huwezi amini yaani hata kamera za kazi nilisahau nikatumia simu kupiga picha"

              "Teh! Pole yako mume wangu ulikurupushwa inaonekana?"

             "Kama ulikuwepo vile nilikuwa Kibaha kwa anko sina hata vifaa vya kazi napigiwa simu nije  Arusha haraka sana, bahati nzuri nilipata ndege mapema uwanja wa ndege Dar. Yaani hata nyumbani kwangu sikurudi.

            "Pole sana mume wangu ndiyo kazi hiyo, safari njema mume wangu urudi  salama"

            "Sawa mke wangu"

    Walikuwa tayari wameshafika kwenye eneo la kuingia ndani ya uwanja, Fatma alimbusu Norbert mdomoni akiwa ametekwa kisawasawa na uongo aliopewa na Norbert kisha akamkumbatia kumuaga. Norbert naye alimuonesha uchangamfu kwa binti huyo kisha akaingia ndani ya uwanja akaelekea mahali ilipo ndege, aliingia ndani ya ndege akakuta tayari ndege ilikuwa imejaa na viti vichache ndiyo vilikuwa vimebakia. Akiwa na umakini wake wa kila siku alitembea huku na huko akiangaza kila pande  akaenda kuketi kwenye kiti chake akafunga mkanda, muda mfupi baadaye ndege aliyopanda ilianza kujongea taratibu kuelekea kwenye njia za kurukia.

    Iliinuka sehemu ya mbele baada ya kifika eneo la kurukia kuashiria ndiyo ilikuwa inaiacha ardhi ya Arusha kisha ikakaa sawa baada ya kufika angani. Norbert hapo alifungua mkanda wake wa kiti kisha akamtazama abiria aliyekuwa yupo siti ya pembeni, abiria huyo aliyemuona alimpa hamasa zaidi ya kutaka kumjua zaidi kwani muda huo alikuwa kalala na kavaa kofia aina ya hat iliyofunika uso wake kwa sehemu kubwa. Mikono ya abiria huyo ilikuwa ni ya mzungu lakini sura ambayo ilikuwa imefunikwa na kofia ilimzuia Norbert hakuiona  , alibaki akimtazama jinsi alivyozama kwenye usingizi hata ndege ilivyokuwa ikipanda angani hakuwa na dalili ya kuamka.

   Norbert alimpuuzia abiria huyo kisha akageuza macho kutazama nyuma kwa namna ambayo ingekuwa vigumu kwa mtu kumjua anatazama nyuma, huko napo aliwaona wazungu watatu waliovaa suti zinazofanana ya abiria aliyeketi jirani yake. Wazungu hao nao walikuwa wamevaa kofia aina ya hat nyeusi kama yule abiria aliyekuwa amelala pembeni yake, Norbert aliwatazama kwa umakini kisha akaachana nao akatazama viti vilivyo usawa nae kwa upande wa pili. Huko alimuona abiria mwingine aliyevaa nguo kama ya abiria aliyeketi pembeni yake, tofauti ya abiria huyo na huyu wa jirani ya Norbert hakuwa mzungu bali alikuwa ni mhindi mwekundu mwenye nywele ndefu alizozisokota kama mkia zikiwa zimeangukia mgongoni mwake.

    Mwili wa mtu huyu ulikuwa umejengeka kimazoezi zaidi tofauti na miili ya wazungu wale, shingoni hadi kidevuni alikuwa na mchoro unaofanana na mabaka ya chui ambao ulimfanya aonekane tofauti kabisa na shingo za wanadamu wengine. Mtu huyo alionekana kuwa siyo mtu wa kawaida kwa macho ya Norbert hadi muda huo, alionekana ni mtulivu kuliko kawaida akiwa hageuzi shingo pande yoyote ile lakini kwa Norbert bado aliendelea kumtilia shaka mtu huyo kutokana na muonekano wake.

   Norbert alibaki  akiwa ameelekeza uso wake mbele lakini macho yake yalikuwa yakimtazama mtu yule kwa wizi mkubwa ili mwenyewe asiweze kumtilia shaka yoyote, muda huohuo abiria aliyekuwa amekaa pembeni yake alianza kuamka kisha akapiga muayo mrefu na akafungua mkanda wa kiti. Abiria huyo alijinyoosha kwa uchovu na hapo kofia yake ikaanguka na sura yake ikaonekana dhahiri kwa Norbert, alikuwa amenyoa mtindo wa kijogoo kichwani mwake na sikio lililopo upande wa Norbert alikuwa amevaa hereni ndogo.

    Norbert alimtazama  yule mzungu na yeye akamtazama Norbert, tabasamu la ghafla la kusabahi ndiyo lilimtoka mzungu huyo na Norbert akarudisha tabasamu hilo.

              "Tanzanian(Mtanzania)" Mzungu huyo aliongea kwa kingereza chenye  lahaja ya kimarekani, Norbert alitabasamu kisha akatikisa kichwa kuitikia aliposikia kauli hiyo.

              "Woow! Nice, Thomas and you?( Wooow! Nzuri, Thomas na wewe?)" Mzungu yule aliongea huku akimpa mkono Norbert.

              "Kaila, also known as Norbert. Also You can call me Norbert Kaila (Kaila, pia najulikana kama Norbert.  Pia unaweza kama Norbert Kaila)" Norbert aliongea huku akipokea mkono wa Thomas.

              "Pleased to meet you(Nimefurahi kukutana nawe)" Thomas aliongea huku akimpa mkono na Norbert na yeye akampa mkono huku akisema, "pleased to meet you too (ninafuraha na kukutana na wewe pia)".

    Kimya kilifuata baada ya hapo kwa Norbert na Thomas, kila mmoja aliwaza lake liliopo kichwani kwake muda huo wakisubiri ndege iwasili jijini Dar es salaam walipokuwa wakielekea. Thomas alirudi katika hali aliyokuwa nayo awali baada ya kuamka kumsabahi mgeni wake, Norbert akiamua kutoa simu yake kuangalia kilichojiri tanguvwakati alipokuwa ameiweka kwenye mfuko wa suruali. Aliitoa akaperuzi akisubiri muda wa ndege kutua ufike, nusu saa baadaye sauti ya mhudumu akiwatangazia kuwa wafunge mikanda ndege ilikuwa ikikaribia kutua katika uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere ilisikika.

    Norbert alifunga mkanda akatulia na Thomas naye akafunga mkanda akatulia, abiria wote pia walifunga mikanda  na ndege ikaanza kuinama kwa mbele kidogo kuashiria ndiyo ilikuwa ikielekea kutua. Muda mfupi baadaye matairi ya ndege hiyo ambayo tayari yalikuwa yametolewa nje yaligusa ardhi ya uwanja wa kimataifa wa mwalimu Nyerere, ndege hiyo ilikimbia kwa kasi sana kisha ikapunguza mwendo ilipofika  karibu na eneo la kuegesha ndege. Ilisimama kabisa jirani na jengo lenye ofisi za uwanja, milango ya ndege hiyo ilifunguliwa kisha abiria mmoja baada ya mwingine akaanza kushuka kwa utaratibu hadi chini walipoikanyaga ardhi ya uwanja huo.

    Norbert alikuwa ni mmoja kati ya watu walioshuka ndani ya ndege hiyo  akiongozana na Thomas, Norbert alimuaga Thomas na akataka kuondoka lakini rafiki yake huyo waliyekutana ndani ya ndege alimuomba asubiri kidogo. Norbert alisubiri hadi pale waliposhuka wazungu wengine pamoja na yule mhindi mwekundu  ambao walivaa nguo sare na Thomas, Norbert alitambulishwa kwa watu hao ndipo naye akaondoka akiwa ameongozana nao hadi ndani ya jengo la uwanja huo wa ndege ambapo maalum kwa watu kusubiri wasafiri wanaowasili.

    Katika eneo hilo Norbert alimuona Benson akiwa amesimama akaenda kumsabahi, Norbert alimsabahi kwa furaha kwa lugha fasaha ya kiswahili lakini Benson huyu hakuwa akiongea kiswahili zaidi ya kutumbukiza maneno ya machache ya lugha ya kiswahili kwa kuchanganya na kingereza. Muda huo huo Thomas na wenzake wakaja kwa Benson wakasalimiana kwa furaha huku wakigongesha mikono, hawakujua kuwa walikuwa wakimpa wasiwasi juu yao na pia hawakutambua kama walimoa hamu ya kutaka kuwafahamu zaidi. Norbert hakutaka kubaki eneo hilo baada ya kujua watu hao walikuwa wapo karibu sana na mtu aliyekuwa karibu na Jack Shaw, aliamua kuondoka kwani vinyweleo vya mwili wake vilishaanza kumsisimka hasa alipomtazama yule mhindi mwekundu ambaye alitambulishwa kama Santos.

    Aliwaaga watu hao baada ya kubadilishana namba ya simu na Thomas kisha akachukua teksi uwanjani hapo, akili yake tayari ilikuwa imeshamuonya dhidi ya watu na aliamua kuondoka mapema kabla ya wao hawajaondoka. Alikuwa ni mwingi wa kutazama nyuma pindi tu teksi aliyopanda ilipoingia barabarani, Norbett kwa tahadhari zaidi aliketi koti cha nyuma kabisa na akawa anaangalia nyuma kila baada ya muda mfupi kwani vinyweleo vyake vyote bado vilikuwa vilikuwa vikimsisimka na moyo ukawa unapiga kwa hamasa ya kutomsahaulisha hatari. Teksi aliyopanda ilikuwa ipo katika barabara ya Mwalimu Nyerere na alipofika jirani na kampuni ya Scania tawi la Tanzania Norbert aliiona gari aina ya ford ikiwa ipo nyuma yake kwa gari tatu, gari tatu hizo zilienda zikahama njia ya kushoto katika barabara ya Mwalimu Nyerere ambao huwa na njia mbili.

    Pamoja na gari hizo kuacha nafasi kubwa baada ya kuhama njia bado ford hiyo haikusogea zaidi mbele, walienda hadi wakafika jirani na sehemu ambayo huwa yanaegeshwa magari mengi ya kubeba vinywaji baridi vya kampuni ya SBC Tanzania. Hapo katika uwazi ule lilioacha ile ford ilikuja kuingia basi la abiria la kampuni ya UDA, Norbert alipoona hiyo gari imekuja kuchomeka mbele alishusha pumzi halafu akawa yupo makini katika kutazama nyuma. Msafara wao huo ambao ulimtia kila aina ya shaka Norbert haukufika mbali, ulikomea kwenye foleni kubwa iliyopo kwenye mataa ya Tazara ambayo ilusababisha magari mengi yasimame. Hapo Norbert alimshika bega dereva teksi kwa kumuita, dereva teksi aligeuka nyuma kuitikia wito huo.

               "Kaka naomba fanya kama nitakavyokuambia, chukua hii hela yako yote ya kutoka Jeti Rumo hadi Temeke" Norbert alimuambia huku akimpatia hela yake yote

               "Kaka mkubwa mbona sikuelewi" Dereva teksi aliuliza.

               "Ni hivi nashuka hapa nimesahau kitu ila nakuomba nenda njia hiyo hiyo kama nilivyokuelekeza ya Temeke mimi utanikuta Vetenari nikiwa tayari nimeshachukua kitu nilichokisahau" Norbert aliongea huku akifungua mlango wa gari kidogo akaokota gunia kubwa lililojaa barabarani vumbi akaliingiza ndani, Norbert aliwasha kamera iliyokuwa kwenye kifungo cha shati lake akawa analiweka gunia vizuri.

                 "niwashukuru halmshauri kwa uchafu wao wa kutosafisha barabara leo hii wameniokoa" Norbert aliwaza huku akilitazama lile gunia chafu huku akitabasamu.

                 "Kaka gunia chafu hilo la nini humu" Dereva teksi aliuliza

                  "Hii siyo kazi yako mkubwa, sikia nimeghairi tena kupanda gari unaweza ukaenda kugeuza popote ukaendelee na kazi yako" Norbert alimuambia dereva teksi huku akilivaa gunia hilo chafu ambalo lilimchafua hata nguo zake lakini hata hakujali, dereva teksi alibaki akimshangaa sana lakini hakumjali hata kidogo.

     Alipomaliza alifungua mlango wa gari kidogo kishs akajipenyeza akatoka nje ya gari bila kuonekana kutokana na baadhi ya magari kuwa yamezima taa, alijipinda mgongo wake gunia hilo likawa limefunika hadi kiatu  chake. Kimuonekano hakuwa tofauti na ombamba wa barabarani, Norbert akiwa kajifunika gunia hilo ambalo kiukubwa ilikuwa ni sawa na gunia tatu za mkaa zilizounganisha alitembea hadi ilipo daladala ya UDA.

   Alinyoosha mkono juu kuomba katika madirisha ya daladala hiyo ya  UDA, alinyoosha  mkono wake uliochafuliwa  na vumbi la gunia hilo pamoja na weusi wa uchafu kuomba  huku akitetemeka mithili ya mtu mgonjwa. Baadhi ya abiria walimpatia senti zao huku baadhi wakifunga vioo vyao kutokana gunia hilo kunuka sana, Norbert alipitisha mkono hadi alipolipita daladala hilo sasa akaiendea gari aina ya ford aliyoitilia shaka ambayo ilikuwa ipo nyuma ya hiyo daladala ya UDA.

    Alipoifikia gari hiyo alikuta ina vioo vya kawaida visivyo na giza ambavyo vilikuwa vimepandishwa hadi mwisho, ndani ya gari hiyo Norbert alimuona Benson akiwa ndiyo dereva na wengine wote aliopanda nao ndege moja kutoka Arusha. Norbert aligonga kioo cha gari hiyo akiretemeka kama masikini mwenye ugonjwa au mwenye njaa kali sana, Benson alifungua kioo kisha akamtazama Norbert kwa chuki nyingi kutokana kukerwa na jinsi kioo kinavyogongwa.

             "Hey what are you want(Hey! Unataka nini?)" Benson aliuliza kisha akapandisha kioo haraka sana baada ya kuisikia harufu kali inayotoa gunia alilovaa Norbert, alimuonesha Norbert alama ya kidole cha kati huku wenzake wakiwa wanacheka.

      Norbert kwa kuona hali hiyo ilimbidi ajifanye mnyonge kisha akaanza kuomba  kwenye gari kadhaa zilizofuata nyuma, alipofika mbali na gari  waliyopanda kina Benson alitoka kando ya barabara akavua gumia hilo ambalo harufu yake ilimkera ingawa aliamua kuvumilia. Aliitazama kamera ndogo aliyokuwa ameichomeka kwenye shati ambayo muda wote ilikuwa ikirekodi matukio yote yaliyokuwa yakitendeka, aliporidhika ipo salama aliizima kisha akakunja lilw gunia ili ajiandae kulitupa lakini aliikuta akisukumwa kwa nguvu na mtu ambaye alikuja nyuma yake bila yeye kumuona.

     Norbert aliyumba kwa kusukumwa huko lakini alimudu kusimama kisha akajigeuza kwa haraka ili apambane na huyo aliyemsukuma, aligeuka akiwa amekunja ngumi lakini aliachia ngumi hizo baada ya kuona aliyemsukuma alikuwa ni masikini aliyevaa  nguo zilizochakaa na zenye kutoa harufu. Masikini huyo alikuwa ni mwanamke mtu mzima mwenye mwili mnene sana, Mwanamke huyo alikuwa akimtazama Norbert kwa chuki sana huku akihema kwa nguvu sana.

             "Huna adabu mwanakenda wewe, nimeweka gunia langu nililalie limepeperuka na upepo ndiyo ulichukue wakati nilikuwa nikilifuatilia lilipopeperuka nilirudishe. Nyinyi wapiga debe mnaovaa vizuri mkaibie watu kwenye daladala mna laana yaani hamunihurumii hata mimi sawa na mzazi wako nitalala vipi?" Mwanamke huyo aliongea huku akiweta kwa hasira, Norbert alilitazama lile gunia lililomfanya asukumwe na yule mwanamke anayefaa kumuita bibi yake kisha akasogea hadi mbele yake.

    Alimkabidhi lile gunia pamoja pamoja na peaa zote alizoomba kimaigizo ili tu awakwepe wabaya wake baada ya kuwa na wasiwasi, mwanamke alilivuta gunia kwa nguvu lakini alipoona pesa alikuwa mpole na akawa anamtazama Norbert kwa tabasamu badala ya hasira kama ilivyokuwa mwanzo. Norbert  hakujali tabasamu la yule mwanamke aliamua kuondoka lakini  aliitwa tena ikabidi aguke kumsikiliza, alisogea karibu kisha akamtazama yule mwanamke kwa umakini.

                 "Baba yule dereva teksi aliyekupa msaada uingie kazini kama ni rafiki yako kimbia atakutaja" Yule mwanamke aliongea akijua Norbert ni teja aliyeiba mavazi kwa jinsi alivyochafuka na alijua yule dereva teksi kamsaidia haoo pale kwenye mataa ili aje kuibia watu, mwanamke huyo aliamua kulipa wema wa kusaidiwa vijisenti kidogo na Norbert.

                  "Baba kuna wazungu wamemkaba, nilipokuwa nakufuatilia usiondoke na gunia langu nimewaona. Kimbia mwanangu" Yule mwanamke alimwambia na muda huohuo simu ya Norbert ikaanza kuita kwa kutoa mtetemo ndani ya suruali yake, Norbert alimtazama yule mwanamke kisha akaondoka eneo hilo kwa kasi ili tu amfanye mwanamke yule aamini kuwa yeye ni teja kweli aliyevaa tofauti.

     Harufu ya like gunia ambalo alijifunika ilimpa mwanamke uhakika wa kuwa Norbert ni teja na  aliamua ambakishe na mawazo hayohayo kutopokea simu yake ilipoita kisha akakimbia, simu yake ilikuwa ni ya kisasa na ya gharama kubwa sana na laiti kama angeipokea basi angempa mwanamke yule wasiwasi.

       Alipofika mbali kabisa na eneo alilokuwepo awali aliitoa simu yske akaipokea akaongea, "sema Thomas..... ila mmejitahidi sana kunifuatilia niwape hongera kwa hilo......karibuni ndani ya kidari poo" . Norbet alikata simu kisha akafungua mfuniko wa betri wa simu yake, alitoa betri na ndani kulikuwa na sehemu nne za kuweka kadi ya simu tofauti na simu nyingine. Alitoa kadi moja ya simu akaivunja kisha  akaitupa akafunga simu vile vile akaiwasha, baada ya hapo alienda kwenye kituo cha pikipiki akachukua  pikipiki ya kukodi akatoweka eneo hilo.

 ****
 

ILIVYOKUWA
     Sheikh Ahmed siku iliyopita alienda Musoma kuwachukua vijana wake, alirudi nao kwenye hoteli ya Singita kisha akawapa jukumu ambalo walitakiwa walitekeleze wakiwa nchini. Siku iliyofuata majira ya mchana vijana hao ambao ndiyo Thomas, Santos na wenzao watatu walipanda ndege katika uwanja wa kimataifa wa Serengeti uliopo maeneo ya Mugumu mkoani Mara.

      Kwa mipango iliyofanikisha kupenyeshwa kwa bahasha ya kaki(kuhonga), walifanikiwa kupata ndege binafsi katika uwanja huo iliwapeleka mpaka Arusha vijana hao. Huko Arusha tayari walikuwa wameshaandaliwa tikiti za shirika la ndege la Precision iliyokuwa inaondoka jioni ya siku hiyo, jioni ya siku hiyo walisafiri na Norbert pasipo kutambua wanasafiri na adui yao. Thomas alivutika sana kuongea na mwisho akaongea naye wakaunda urafiki papo, walipotua kwenye uwamja wa ndege  wa Mwalimu Nyerere walipokelewa na mtu ambaye Norbert alikuwa anamjua kuea ni Benson kumbe alikuwa ni pacha wake Benson anayeitwa Benjamin.

       Benson na Benjamin ni wahalifu  wa  kuaminika wa kundi hatari la Jack Shaw kutoka nchini Uingereza ambao walitangulizwa Tanzania wakiwa na kikundi kidogo walichokiita Cats Kingdom, kikundi hicho ndiyo kilichomteka Norbert akaja kutoroshwa na Norene. Benson na Benjamin ndiyo Panthers wenyewe waliokuwa wakiendesha mauaji mbalimbali, hawakuwa wakijulikana kama wapo mapacha kwa jamii bali walijulikana kwa watu wachache tu. Mapacha haea ndiyo walioshiriki mauaji ya Jenerali Kulika ambapo Benson ndiye mwenye alama ya mshono mkononi na Benjamin ndiye mwenye alama ya mchoro wa kipepeo, tofauti yao kubwa ilikuwa uongeaji wa lugha ya kiswahili tu na sio kufanana  kwani  walikuwa wamefanana kila kitu kinachoonekana.
Norbert hakuitambua tofauti hiyo na hata alipomsalimia wakati anakuja kupokea wenzake alimjibu kwa kuchanganya na lugha ya kingereza, bado Norbert hakuwa amehisi kitu tofauti.

    Norbert alipoondoka eneo hilo ndipo Benjamin alipowauliza wenzake juu ya kufuatana kwao na Norbert, Thomas alieleza jinsi alivyokutana ndani ya ndege na Norbert akiwa hajamjua ni nani. Benjamin alimsikiliza kwa umakini sana kisha akawaeleza wote juu ya uhalisia wa Norbert, tena akawaeleza ni mmojawapo kati ya watu wanaohitajika wauawe kabla mpango wao haujaingia Tanzania. Taarifa hiyo ilipofika  kwa vijana waliotumwa kuja kuongeza nguvu baada ya Cats kingdom kupungua ilikuwa ni kuitejeleza mara moja kazi yake, wote kwa pamoja waliingia ndani ya gari iliyowafuata wakaanza kuifuatilia teksi aliyokuwa amepanda Norbert.

     Hawakujua kama mpango huo  Norbert alishaujua tayari,  waliendelea kuifuatilia ile teksi lakini pia walifanya kosa jingine kubwa zaidi kwa kuiacha  basi ya abiria  ya UDA kukaa mbele yao wakawa hawaioni vizuri teksi aliyopanda Norbert. Foleni ilipoanza tayari giza liliingia na walikaa kidogo wasubiri hadi pale daladala la UDA lilipozima taa za mbele kwenye foleni hiyo, wajiandaa kushuka lakini kioo cha dereva ambaye ni Benson kikagongwa na Norbert waliyejua ni ombaomba. Harufu kali iliyoingia ndani ya gari iliwakera wote na Benjamin akapandisha kioo kuepuka hiyo kero, Norbert wanayemsaka wakamuangamize aliwakimbia namna hiyo bila wao kujua.

   Thomas na Santos walienda hadi kwenye ile teksi  wakaingia bila  taarifa, Thomas aliingia kiti  cha nyuma na Santos akaingia kiti cha mbele lakini hawakumkuta Norbert. Dereva teksi alibaki akiwashangaa wageni ambao walimtisha na alihitaji kujihami kwani ni kawaida madereva teksi kutembea na silaha kwa usalama wao, aliingiza mkono chini ya kiti chake atoe silaha kwa haraka lakini aliwahiwa na kabali ya Thomas iliyokuwa ya haraka kushinda haraka yake. Muda huo ndiyo yule mwanamke anayetafuta gunia lake lililochukuliwa na Norbert alipita akaona hilo tukio lakini aliondoka haraka kuepusha usalama wake.
 


TUKUTANE IJUMAA PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA



HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA YA MTUNZI




No comments:

Post a Comment