Friday, December 23, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI





RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA



______________+18__________________



SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI!!

    Huduma ya kwanza kwa Josephine ilianza kutolewa kwa haraka huku mawasiliano yakifanywa kwa wakubwa zao, ndani ya dakika kadhaa tayari walikuwa wameshasambaza mawasiliano kwa wenzao wote ingawa waligwaya zaidi katika kusambaza taarifa hiyo. Kugwaya kulitokana na Wilson kuipiga namba ya mzungu aliyekuwa yupo chini ya kina Norbert ili ampatie taarifa, maneno aliyoyasikia kwenye simu hiyo yalimfanya aibamize chini kwa nguvu simu yake ya kisasa aliyoinunua kwa gharama.

              "Aaaargh! N001 Tenaa!" Wilson aliongea kwa ghdhabu pasipo kuijali simu yake ambayo ilik
uwa ishagawanyika vipande, sauti yake ilimfanya Benson auachie mwili wa ndugu yake akasimama kwa ghafla aliposikia jina la muuaji wa ndugu yake linatajwa.

               "Yuko wapi?!" Benson aliuliza kwa hasira.


_____________
 ______________
_____________
    ________


                "Amepokea simu ya Golden pia" Wilson alimjibu Benson ambaye alikuwa tayari amechnganywa na kifo cha pacha wake, tarifa hiyo iliwachanganya pia kina Santos nao wakabaki wakiwa wamegwaya. Walitambua tayari walikuwa wamewahiwa na mjanja zaidi yao ambaye walikuwa wakimtambua kwa jina la     N001 badala ya kumtambua sura na jina lake halisi.

     Wote waliowahi kumtambua N001 kwa sura yake halisi tayari walikuwa ni marehemu na wachache waliomfahamu kama mpelelezi pasipo kumtambua kwamba ndiye huyo mpelelzi hatari kati ya wapelelezi watano wa daraja la juu wa EASA wenye majina yanayoanziwa na herufi 'N' akiwemo Norbert. Tayari kazi yao iliyowaleta ilikuwa imeshaingiliwa na adui yao mkubwa ambaye hawakumtambua ndiye waliyekuwa wakimuwinda wakamkosa,walichoka pasipo kuchokeshwa na walipagawa pasipo kupagawishwa na kitu  chochote.

    Benson alitoa ukelele wa hasira aliposikia taarifa hiyo kisha akapiga magoti kwa ghafla huku macho yake akiangalia lilipo dari la sebule hiyo, aliweka mikono ambayo ilikuwa imetapakaa damu usoni mwake baada ya tarifa ya uhakika ya kumpata Norbert ikiwa haipo. Matarajio ya Benson ilikuwa ni kwamba Wilson alikuwa amepata mahali ambapo Norbert alikuwepo, aliposikia taarifa ya kwamba alitumia simu ya Golden kuongea ilimfanya azidi kupagawa zaidi.

     Santos naye alipandwa na hasira zaidi akapiga ngumi hewani huku akiachia matusi mfululizo kutokana na taarifa hiyo,Thomas alijikuta kiketi kwenye sofa bila ya kupenda na mikono akaweka kwenye mashavu yake kama alikuwa amepokea taarifa ya msiba wa ndugu yake anayempenda.

                 "Hivi huyu N001 ni nani hasa mpaka atuchezee akiili namna hii' Santos aliuliza huku akiuma meno kwa hasira sana.

                  "ni very dangerous spy wa EASA na tusipokuwa makini basi tutaisha wote" Wilson aliongea

                  "Unasema nini Wilson  kwahiyo unamuhofia na wewe huyo mtu' Santos aliongea kwa hasira huku akimtazama Wilson.

                   "Santos cool down, akisemacho Wilson ni sahihi kabisa tuwe makini maana tunacheza mchezo na mtu tusiyemjua ambaye anatujua' Thomas aliongea kwa utaratibu huku akimtazama Santos ambaye alikuwa amezidi kuwa mwekundu zaidi hata ya rangi yake ya uhindi wekundu kutokana na jinsi alivyoona wanazidi kupungua kutokana na kazi ya N001 ambayo anaifanya kimyakimya.

                    "Come on Thoms hiyo ni ishara ya uoga kumpa sifa hivyo huyo mtu ambaye anazidi kutupa hasara na hata Don na Sir wakikusikia watakata kichwa chako" Santos alimuambia Thomas.

                    "Ok kumpa sifa ni ishara ya woga siyo, vipi kuendekea hasira katika kazi ambayo unatakiwa utulize kichwa ili uweze kuifanya ni ishara ya nini? Kushindwa" Thomas aliongea kwa msisitio zaidi huku akimtazma Santos kwa macho makali, Santos naye alibaki akimtazama  Thomas akiwa na macho makali baada ya kusikia kauli hiyo ambayo ilikuwa ya ukweli ndani yake lakini ilikuwa ina karaha katika moyo wake.

                    "Santos tunapambana na mtu mwenye kutumia akili zaidi kuliko nguvu vipi tutumie nguvu na hasira, fikiria kuhusu hilo Komandoo wa kuaminika miongoni mwa  makomando wa kuaminika wa Don Ahmed" Thomas aliendelea kumueleza Santos.

                    "Santos akisemacho Thomas ni kweli kabisa tusitumie nguvu wala hasira mbele ya huyu N001" Wilson aliongea huku akimtazama Santos ambaye alibaki akimtazama Thomas kwa macho makali kutokana na maneno  aliyokuwa akiyaongea ambayo aliyaona yalikuwa yakimdhalilisha alipoyasikia lakini aliyaona yanafaa baada ya Thomas kuzidi kumuelezea kwa mara ya pili na kusababisha jazba iliyokuwa ikimpanda kuanza kupungua taratibu ingawa haikuwa imepungua yote hadi muda huo, maneno aliyoyaongeza Wilson yalimfanya ageuze macho pia amtazame kwa umakini halafu akashusha pumzi.

    Macho yaliyokuwa yana dalili ya ukali ambayo yalipelekea uso wake kukunjika yalianza kurudi  katika hali ya kawaida taratibu, aliwatazama wenzake mmoja baada ya mwingine kisha macho yake akayahamisha kwenye kochi ambalo alikuwa amelazwa Leopard Queen baada ya kukutwa akiwa yupo chini tangu apoteze fahamu.

                 "Tupo pamoja" Santos aliongea huku akiachia tabasamu fupi halafu kamuinua Benson pale chini alipokuwa amepiga magoti tangu alipokuwa akilia, alimshika mabega huku akimtazam usoni kwa umakini sana.

                  "Benson hivi unahitaji kulipa kisasi kwa N001?" Santos alimuuliza Benson ambaye aliishia kutingisha kichwa kukubali.

                  "Sasa ukikaa chini ukiendelea kulia ndiyo N001 utafanikiwa kumjua ni nani na ukaanza kumtafuta na kulipa kisasi?" Santos alimuuliza swali jingine Benson kwa sauti ya ukali zaidi, swali hilo halikujibiwa na Benson zaidi ya kukaa kimya huku akimtazama Santos kwa mcho yaliyokuwa yamezongwa na machozi sehemu za mboni zake.

    Swali hilo kutojibiwa hakukumzuia Santos kuendelea kuongeea maneno ambayo alikuwa na uhakika yangemrudisha Benson katika hali yake ya kwaida na akaondokana na hasira iliyokuwa ikimkabili pamoja na uchungu wa kufiwa na kaka yake kipenzi. Santos alimuachia Bneson bega lake moja kisha akakunja vidole vyake vilivyokomazwa na mazoezi akiacha kidole kimoja ambacho ni cha shahada.

    Alikielekeza kidole hicho cha shahada katika upande ambao alikuwa amelala Leopard Queen akiwa hana fahamu pasipo kuongea neno lolote kwa sekunde kadhaa, Benson kwa taratibu aligeuza macho upnde kilipoelekea kidole hicho cha shahada na macho yake yakatua katika mwili wa msichan wa kazi mwenye urembo wa asili wa kila aina ambao ungeweza kumvutia mwanaume yeyote yule mwenye utimilifu katika viungo vyake visivyohitajika kuonekana.

                     "Atakayeweza kukusaidia kumpata N001 ni yule ambaye amelala pale kwenye sofa akiwa hajitambui my friend, lakini ambaye anayeweza kukusaidia kumpata N001 hawezi kuwa msaada kwako pasipo kupewa msaada yeye utakaomuwezesha kukupa msaada wewe" Santos alimuambia kwa sauti iliyojaa msisitizo zaidi

                      "Unamaanisha nini?" Benson aliuliza huku akijifuta machozi kwa kutumia kiganja chake cha mkono.

                      "Come on Benson huoni kwamba hana fahamu yule na hatujui alipatwa na nini hadi akawa katika hali ile, anahitaji first aid yule ili aweze kufumbua macho na kutupa msaada katika hili" Santos alimuambia Benson huku akimminya bega lake ambalo alikuwa amemshika, Benson aliinamisha uso wake akiwa anajifikiria baada ya kuambiwa maneno hayo.

                      "Kumbuka wewe ni pekee uliyebaki mwenye taaluma ya utabibu ukiondoa Benjamin ambaye tayari hayupo nasi kimwili, hivi unafikiri ukiendelea kulia hapa huyu ambaye atakuwa msada kwetu ataweza kutusaidia vipi tumjue  huyo mtu ambaye anatuharibia mipango yetu. Try to think buddy" Snatos alizidi kumuambia Benson.

      Maneno ya Santos yaliweza kuleta athari nyingine katika ubongo wa Benson na yalisaidia kwa kiasi kikubwa katika kumbadilisha kutoka katika hali ya kulia na kuwa katika hali ya kawaida ingawa huzuni haikuwa imetoka katika uso wake, aliutoa mkono wa Thomas katika bega lake kisha akapiga hatua kumsogelea Leopard Queen aliyekuwa amelazwa pale kwenye kochi. Alipomfikia alianza kumkagusa sehemu za juu za mwili wake huku wenzake wakimtazama kwa tabsamu hafifu baada ya kuona amerudi katika hali yake ya kawaida, alimkagua Leopard Queen kuanzia usoni hadi miguuni na alipomaliza akageuka kuwatazama wenzake akiwa na uso wenye jambo ambalo alipaswa kuwaambia. Wenzake nao walimtazama kwa macho yenye shauku ya kutaka kujua kile alichokuwa nacho moyoni Benson, aligeuza tena shingo kamtazam Leopard Queen sehemu ya begani halafu akawatazama wenzake kwa zamu.

                              "Amepigwa risasi begani" Benson aliwaambia wenzake.

                              "N001 Mtoto wa Mbwa wewe" Wilson aliongea baada ya kupokea taarifa hiyo ambayo ilimtia hsira sana.

     Benson hakuijali kauli ya Wilson aliamua kumgeuka Lepard Queen kisha akamgeuza akalala kifudifudi akazidi kumkagua kuanzia sehemu za kisogoni ambapo alifunua nywele zake, alimtazama kwa umakini sana sehemu hizo ambapo alishuhudia nundu likiwa lipo kisogoni. Alimchunguza zaidi sehemu nyingine za mwili wake na hakumkuta na jeraha lolote jingine ambalo lingeweza kuhatarisha afya ya binti huyo, baada ya kuridhishwa na ukaguzi wake alimrudisha Leopard Queen alivyokuwa amelazwa chali.

                           "Yupo salama huyu hana tatizo jingine lolote, inaonekana  alipigwa na kitu kigumu kama kitako cha bastola au chuma sehemu za kisogoni ambacho kimefanya apoteze fahamu hadi muda huu" Benson aliwaambia kisha akambeba Leopard Queen akwaambia wenzake, "mbebeni na kaka yangu tuelekee chumba cha first aid".

   Wilson na Thomas kwa haraka waliunyanyua mwili wa Benjamin baada ya kusikia kauli hiyo ya Benson, walifuatana na Benson ambaye alikuwa anatembea kwa taratibu kuelekea ilipo korido ndefu inayotenganisha vyumba katika nyumba hiyo huku Santos akiwafuata kwa nyuma.


****



   Wakiwa wapo katika ofisi ndogo ya kipelelezi iliyotengenzwa ndani ya nyumba ya kampuni, simu ya Golden ambaye ndiye yule mzungu aliyekuwa akiteswa na Norbert iliita kwa kutoa mtetemo ikiashiria ilikuwa imetolewa sauti. Norbert aliipokea simu hiyo kwa haraka baada ya kuona jina linalonekana kwenye simu ndiyo lile aliloliona kwenye simu ya Leopard Queen akalipiga. Ilikuwa ni simu ya Wilson ndiyo ilikuwa inapiga, baada ya kuiweka sikioni simu aliwaashiria wenzake wake kimya nao wakafanya vivyo hivyo.

               "Ni N001 kwa mara nyingine ewe unayejiita Nouther karibu kwenye mchezo" Norbert aliongea na maneno na simu upande wa pili ikakatwa ghafla ambapo aliishia kutabsamu tu, ilipokatwa simu iyo ulikuwa ndiyo muda ambao Wilson aliibamiza simu yake chini kwa nguvu baada ya kuisikia sauti ya Norbert kwa mara nyingine ikiwa ndiyo ileile aliyokuwa ameitumia kumpigia simu kwa mara ya kwanza akimuambia kuhusu janga aliloliacha nyumbani kwa Leopard Queen. Norbert alipokata simu hiyo aliangua kicheko sana akawatzama Moses na M.J Belinda ambao walikuwa wamekaa kwenye viti wakiwa wameizunguka meza moja, wenzake nao waliingiwa na matabasamu baada ya kusikia kile alichokuwa akikiongea Norbert.

                   "Na watakoma kuingia kwenye ukanda wa Afrika ya Mashariki uliomshinda Brown Stockman" Norbert aliongea huku akiifungua simu ya Golden sehemu ya  mfuniko seli kavu(betri) akatoa kadi ya simu akaivunja.

                    "Wameanza acha sisi tumalize, ok tuendeleeni na mpango wa kesho maana ndiyo mazishi ya General" Moses aliongea

                   "Kesho ni hivi mimi na Norbert tutahudhuria mazishi wewe Moses utabaki kisha tukitoka ndiyo tutaenda ikulu tukiwa pamoja" M.J Belinda aliongea.

                   "Mose usitoke au ukitoka badili uso huo ili usijulikane kumbuka wewe ni wanted hata raia wa kawaida wakikuona itakuwa ni kifo chako sasa epuka hili suala kabisa la kuonekana uso wako kwa mtu yoyote" Norbert alimuambia Moses.

                    "Ok nitafanya hivyo ila na wewe ukijogoo upunguze yasije yakukuta kama ya huyo Leopard Queen uliyetuambia" Moses naye alimuasa Norbert kutokana na tabia yake ya kupenda wanawake

                     "Usihofu wala nini sasa hivi nitamfuata yule sajenti anayemlinda Dorice mtoto wa General nafikiri siyo adui yule" Norbert aliongea kimasihara akasababisha Moses acheke kwa nguvu na M.J Belinda asikitike akiwa  anamtazama

                      "Khaa! Huyu mwanaume huyu anajifanya jogoo pori si uoe tu" M.J Belinda alimuambia Norbert.

                      "we mbona huolewi" Norbert naye alidakia.

                      "nyoooo! Haya uje unioe wewe basi nikuweke kibano usiku ucha mpaka uwe mstarabu uache hiyo tabia" M.J Belinda alimuambia Norbert huku akimtazama kwa jicho la madaha.

                      "Hey tuweni serious basi utani tupunguze" Moses aliwaambia kisha akaendelea, "Sasa na mimi sitokaa humu ndani bali nitatoka nikiwa na sura nyingine niende huko mazishini".

                      "Kwahiyo tutakuwa pamoja huko?" M.J Belinda aliuliza.

                      "Ndiyo maana yake ili nicheze na wabaya wangu bila ya wao kunijua" Moses alijibu.

                      "Ok kazi kwetu nafikiri Belinda urudi kwako ukajiandae kabisa kwani massa ndiyo yanakaribia inabidi utokee nyumbani" Norber alimuambia M.J Belinda.

                      "enhee jamani nimepata wazo" Moses alisema huku akiwa ameweka uso watabasamu baada ya kile alichokifiria kuwa ndiyo njia sahihi kwake, Norbert na M.J Belinda walimtazama kwa shauku sana kutaka kujua hilo wazo.

                       "Mnaonaje kesho nivae sura ya bandia pamoja magwanda ya jeshi niingie kinamna nyingine  hiyo kesho" Moses aliongea huku akiwatazama wenzake ambao walikaa kimya hawakuwa wameongea kitu, kimya chao kilimaanisha hawajamuelewa na ikabidi awape ufafanuzi zaidi.

                         "Yaani naingia kama dereva wa Belinda" Moses aliongea akawafanya wenzake watoe matabasamu katika nyuso zao baada ya kuuelwa mpango wake vizuri.

                          "wazo zuri sana hilo sasa msipoteze muda rudini Tabata haraka sana hakuna muda wakupotea sasa hivi nafikiri tunaelewana jamani" Norbert aliongea, Moses na M.J Belinda walinyanyuka kwenye viti vyao kisha wakampa ishara ya kumuaga Norbert na wakaondoka ofisini humo wakimuacha Norbert akiwa ameketi kwenye kiti akiwasindikiza kwa macho.



   ASUBUHI ILIYOFUATA
 (SIKU TATU KABLA MAPINDUZI YALIYOPANGWA)

     Majira saa nne asubuhi tayari magari yalishaanza kumiminika nyumbani kwa Jenerali Kulika kuja kuuaga mwili wake katika siku hiyo kabla ya kuelekea Pugu kajungeni kwa Mazishi, viongozi mbalimbali wa kisekali wakiongozwa na Rais Zuber Ameir ambaye ameamua aje kuhudhuria mazishi ikiwa anatambua wazi mwisho wa utawala wake ulikuwa umefika tayari baada ya kupigiwa simu siku tatu zilizopita Mnadhimu mkuu wa jeshi L.J Ibrahim.

    Rais Zuber alikuwa amekaa kwenye kiti kilichopo chini ya turuba la kisasa lililokuwa limeandaliwa kutumiwa na viongozi mbalimbali, ulinzi wake ndani ya eneo hilo ulikuwa umeimarishwa tofauuti na ilivyo kawaida kutokana na amri aliyowapa wanausalama wa ikulu. Alikuwa amekaa na viongoo mbalimbali wastaafu pamoja na waliopo madarakani waliokuja kuhudhuria mazishi ya komandoo wa kuogopeka, ndani ya eneo hilo pia Norbert alikuwa yupo akiwa amekaa katika kundi kubwa la waandishi wa habari akiwa na kamera yake ya kisasa mkononi ambayo ilikuwa ina uwezo mkubwa sana. Alikuwa akipiga picha mbalimbali za eneo hilo huku akiwatazama maadui zake kama wapo eneo hilo, akiwa na kitambulisho kilichokuwa na kamba ambacho kilikuwa kifuani mwake kilimfanya asihisiwe yupo tofauti kimalengo kwa waandishi wenzake ambao walikuwa wakimfahamu vyema kwa uhodari wake wakusaka habari na kuvumbua ukweli.

     M.J Belinda naye alikuwa yupo katika turubai maalum walilokaa viongozi mbalimbali wa kijeshi akiwa yupo pembezoni mwa L.J Ibrahim, alikuwa yupo amkini katika kutazama pande zote za eneo hilo. Alikuwa yupo katika safu moja na viongozi wakubwa wa kijeshi wenye vyeo sawa na yeye huku kati yao akiwa yupo Luteni jenerali akiyewazidi cheo wote, wote walikuwa wamevaa magwanda yenye kofia tofauti kutokana na vikosi walivyomo. Nyuma yao walifuatia wanajeshi wenye vyeo vya Brigadia jenerali na kuendelea.

     Wote walikuwa wametulia huku wakitazama mbele ambapo kulikuwa kuna jeneza  lenye bendera ya taifa lililowekwa picha ya Jenerali Kulika kwa juu, upande mwingine wa eneo hilo kulikuwa kuna turubai ambalo walikuwa wamekaa familia ikiongozwa na mjane wa marehemu pamoja na ndugu wengine wa marehemu. Upande huo ndiyo ulikuwa upande uliokuwa umetawaliwa na vilio  ambavyo viliongozwa na mke wa marehemu pamoja na watoto wake, huzuni ndiyo ilikuwa imetawala turubai hilo lililokaa familia na ndugu wa marehemu ambayo isingeweza kuelezeka kwa maandishi ikatimia kuieleza pasipo kuwa na mapungufu yoyote.

    Ndani ya eneo hilo pia Benson alikuwepo akiwa amevaa miwani nyeusi ambayo ilificha macho yake yaliyokuwa na huzuni sana, alikuwa yupo katika turubai ambalo lilikuwa limekaliwa na watu wa kawaida. Macho yake bado yalikuwa mekundu  kutokana na huzuni ya kufiwa na pacha wake, alikuwa amekaa jirani kabisa na Wilson ambaye anatambulika kama mfanyabiashara tajiri maarufu sana.


    Mnamo saa tano na nusu ibada ya mazishi ilianza hapo nyumbani ambapo iliongozwa na askofu wa kanisa katoliki nchini, misa hiyo iliongozwa hadi muda wa saa moja kisha msemaji mkuu wa jeshi akasimama akiwa ameshika karatasi akaelezea wasifu wa Marehemu Jenerali Kulika. Msemaji huyo alisoma wasifu huo wa marehemu uliochukua takribani nusu saa na ilipotimu saa saba kamili tayari alikuwa amemaliza, shughuli iliyofuata iliyokuwa ni mlo wa mchana nyumbani hapo kwa marehemu ambao ulichukua nusu saa hadi saa saba na nusu kisha taratibu za kutoa heshima za mwisho kwa marehemu ndiyo zikafuata

    Shughuli hiyo ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu ilianza kwa kutangulia viongozi mbalimbali wa kiserikali ambao walitoa heshima zao za kumuaga Jenerali Kulika akiwa yupo ndani ya  jeneza, baada ya hapo ndipo walifuata viongozi mbalimbali wa kijeshi wakifuatana kicheo.

    Viongozi wa kijeshi wakiwa mstari mmoja mbele yao alikuwa yupo L.J Ibrahim ambaye ndiye mhusika mkuu wa hayo yote akiwa ameweka huzuni ya kinafiki katika uso wake, L.J Ibrahim alifika mbele ya jeneza lenye mwili wa Jenerali Kulika akatoa saluti ya kinafiki  kwa mkubwa wake huyo ambaye ndiye amesababisha afariki. Alifuatiwa na  M.J Belinda halafu M.J Marwa akafuatia akiwa yupo nyuma yake, mameja jenerali wengine walifuatia katika mstari huo na walipoisha waliingia mabrigadia jenerali hadi viongozi wote wa jeshi walipomalizika.

    Ndugu wa marehemu ndiyo walifuata wakiongozwa na mke wa marehemu katika kutoa kuaga, akiwa yupo mbele kabisa akiwa ameshikiliwa na askari wa JWTZ mke wa Jenerali Kulika alijikongoja hadi lilipo jeneza la mume wake huku akilia sana akimuita mwanaume huyo aliyempenda ambaye muda huo hakuweza kuitikia witi huo. Alipouona uso wa mume wake ukiwa kama mtu aliyalala huku ngozi ys mwili ikienda kuwa kijivu ndiyo alizidi kulia huku akiwa anaishiwa nguvu, askari wa JWTZ aliyekuwa yupo pembeni  yake aliwahi kumzuia  asiende chini kisha akamuondoa eneo hilo.
 
    Watoto wake wakiongozwa na binti yake mkubwa nao walifuata wakiwa wanalia kwa uchungu wakiwa wameshikiliwa na maaskari wengine wa kike wa JWTZ  ambao walikuwa nao begabega hadi wanauaga mwili wa baba yao. Ndugu na jamaa nao walifuata katika kutoa heshima zao za mwisho kwa Jenerali Kulika, ndani ya dakika arobaini shughuli hiyo ilkamilika na jeneza likafungwa na wanajeshi wenye vyeo vya brigadia jenerali wakalizunguka wakiwa wamesimama kiukakamavu.

    Ilikuwa ni saa nane na robo mchana wanajeshi hao wenye vyeo vya brigadia wakiwa wamelizunguka jeneza la mkubwa  wao wa  kijeshi, sauti ya amri ilisikika na kwa pamoja maaskari hao wenye sare za kombati walifunika bendera ya taifa wakalinyanyua jeneza la Jenerali  Kulika kikakamavu zaidi. Maaskari hao walianza kutembea kwa mwendo wa pole kwa hatua zisizopishana hadi kwenye gari maalum la kijeshi lililoteuliwa  kuubeba mwili wa Jenerali Kulika kuupeleka katika eneo la maziko shambani kwake Pugu.

    Jeneza lilipandisha ndani ya gari kwa taratibu mno hadi katika eneo maalum la kuweka jeneza hilo katika gari la kijeshi ambalo halikuwa tofauti na magari ya wazi yatumikayo kuwaaga wanajeshi wastaafu.

    Misafara mbalimbali ya viongozi wa nchi hii iltangulia kuondoka eneo hilo ikiongozwa na msafara wa rais Zuber baada ya misafara hiyo kuondoka magari ya watu wa kawaida nayo yaliondoka na mwishoni kabisa ukaondoka msafara uliobeba mwili wa Jenerali Kulika kuelekea eneo la  maziko ambalo lilikuwa lina na mawindo ya watu hatari waliokuwa wanawindana.

    Majira ya saa tisa kasoro robo misafara hiyo tayari ilikuwa imeshawasili katika eneo la Pugu ambalo kulikuwa kumefungwa maturubai na viti kwa ajili ya kuketi viongozi mbalimbali, dakika kumi baadaye gari lililobeba mwili wa Jenerali Kulika liliwasili na watu aote walisimama wakati jeneza liliwa linashushwa ndani ya gari hilo. Maaskari wa JWTZ walewale wenye vyeo vya Brigadia jenerali yaani bibi na bwana pamoja na nyota tatu katika mabega yao walilibeba jeneza hilo kwa mwendo wa pole kuelekea katika eneo lenye shimo lililojengewa pamoja na kuwekea mbao juu. Walitembea kwa mwendo huo hadi walipolifikia shimo hilo la kaburi wakaweka jeneza juu yake katika mbao, maaskari hao walisogea pembeni  ya shimo hilo kikakamavu  kisha watu wakaketi katika viti vyao kusubiri taratibu zingine zinazofuata.


*Alazwe mahala pema komandoo wa nchi


TIKUTANE JUMATATU PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA




HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI






No comments:

Post a Comment