Friday, December 2, 2016

WAKALA WA GIZA SEHEMU YA KUMI NA TISA



 
RIWAYA: WAKALA WA GIZA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU: +255713776843
          +255762219759


WHATSAPP: +255713776843

SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA ULIMWENGU WOTE KWA KUNIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII NIKIWA NA AFYA NJEMA




______________+18__________________




    SEHEMU YA KUMI NA TISA!!
   Thomas na Santos walienda hadi kwenye ile teksi  wakaingia bila  taarifa, Thomas aliingia kiti  cha nyuma na Santos akaingia kiti cha mbele lakini hawakumkuta Norbert. Dereva teksi alibaki akiwashangaa wageni ambao walimtisha na alihitaji kujihami kwani ni kawaida madereva teksi kutembea na silaha kwa usalama wao, aliingiza mkono chini ya kiti chake atoe silaha kwa haraka lakini aliwahiwa na kabali ya Thomas iliyokuwa ya haraka kushinda haraka yake. Muda huo ndiyo yule mwanamke anayetafuta gunia lake lililochu
kuliwa na Norbert alipita akaona hilo tukio lakini aliondoka haraka kuepusha usalama wake.
 
****

   Kabali nzito ya mkono wa Thomas  ambayo uligeuka kua migumu baada ya misuli kukazwa, ilizidi kumfanya dereva teksi huyo asiwe na ujanja wowote akiwa anahangaika kutoa mkono huo. Thomas naye alizidi kumkaba kwa nguvu hadi sauti ikawa haimtoki kabisa Dereva wa teksi , nguvu ziliamza kumuishia dereva teksi huyo akawa hana uwezo wa kujitetea akabaki akiwa ameshikilia  mkono wa Thomas kama  alikuwa akiishinikiza iendelee kumkaba.

   Thomas naye hakutaka kumuachia aliendelea kumkaba kwa nguvu dereva teksi hadi akaanza kurusha miguu, mguu mmoja wa dereva huyo ulikanyaga sehemu ya kuongeza mwendo wa gari na kuifanya gati itoe mngurumo mkubwa lakini haikwenda popote kutokana na gia yake iliyo katika ipo mfumo moja kwa moja(automatic)  kuwa katika P yaani parking. Kulia huko kwa gari kuliwashtua  hata watu walioko mbele lakini hawakufanikiwa kuona chochote  kutokana na taa za ndani za gari hilo kuwa limezimwa.

    Santos aliingiza mkono chini ya kiti cha dereva akatoa jambia kubwa ambalo lilikuwa bado jipya kisha akamtazama dereva teksi kwa dharau, Santos kwa kutumia mikono yake yenye nguvu aliamua kumpiga dereva huyo kibao kimoja cha kifua. Kibao hicho kilimfanya dereva huyo aache kurusha miguu na akatulia huku akijaribu kukohoa kutokana na chachafya ya kofi lile zito la Santos, nafasi ya kukohoa nayo hakuipata kwani kabali imara ya mikono ya Thomas bado ilikuwa palepale ambayo ilamfanya abanwe kwenye sehemu ya kuegemea.

             "Abiria uliyemchukua Airport yupo wapi?" Santos aliuliza akisogeza jambia alilolipata chini ya kiti cha dereva jirani na koo la Dereva teksi hili, Thomas naye alimuachia kwa haraka na jambia hilo likagusa koo la Dereva wa teksi huyo. Santos alimkunja kwa nguvu huku akigusa koo lake kwa jambia hilo akimuacha akikohoa mara chache kisha akakandamiza jambia hilo kooni mwa dereva wa teksi, ncha kali ya jambia hilo ambayo haikumtoboa ngozi yake zaidi ya kuonesha dalili kutoboa ilimfanya Dereva teksi  huyo asiwe na namna zaidi ya kuongea ukweli.

               "Kashuka hapahapa na kavaa gunia  kaenda huko nyuma" Dereva teksi aliongea kwa tabu kisha akajaribu kukohoa tena lakini ncha ya jambia ilimkatisha kufanya hivyo kwani ingemtoboa ikiwa angekohoa koo lake likatikisika.

                "Damn! Ndiye huyo aliyekuwa anaomba kwenye hiyo gari hapo nyuma kabla hajasogea nyuma zaidi?" Thomas aliuliza akiwa haamini kama Norbert tayari alikuwa amewatoka, Dereva teksi aliishia kujibu swali hilo kwa kuchezesha nyusi kwani angetikisa kichwa kizima basi lile jambia lingemletea balaa jingine.

    Thomas alitoa simu kisha akabonyeza namba za Norbert walizopeana uwanja wa ndege, simu ya Norbert iliita kwa muda mrefu kutokana na muda huo ndiyo muda ambao Norbert alikuwa anakimbia ili asogee mbali na yule mwanamke aliyempa gunia ili ajue kama kweli alikuwa akikimbia baada ya kusikia Dereva teksi  alikuwa akikabwa na alikuja kuipokea baada ya kufika mbali.

     Thomas simu ilipopokelewa aliongea, "ndiyo unajifanya mjanja siyo kuliko Sungura.......tutakunasa tu"

      Alikata simu kisha akamtazama Santos akampa ishara baada ya muda huo kuwa tayari magari yalikiwa yameruhusiwa, Santos naye alilegeza mkono wake katika kukandamiza jambia halafu akampa nafasi ya kuendesha gari dereva huyo.

               "Ingia kulia haraka" Santos alitoaa amri na dereva huyo akaweka gia huku akikohoa akakanyaga mafuta gari ikaanza kuondoka kwa kasi ili waepuke lawama za watu ambao walikuwa na haraka wapo nyuma yao, walipokuwa wakikata kona kuingia barabara ya Mandela taa za magari yaliyosimamishwa zikamulika ndani ya gari hiyo hadi Askari wa usalama barabarani aliyepo katikati ya makutano hayo akaona kile ambacho kinafanyika humo ndani ambacho kilimshtua sana.

     Askari wa usalama wa barabarani alionekana mbele ya macho ya Thomas na Santos alihangaika kuitoa simu yake ya upepo kwa haraka sana, Santos alimuamuru Dereva teksi aongeze mwendo naye akatii.

       Dereva Tulsa alikata kona kuingia upande wa kulia ilipo barabara ya Mandela, walikuwa wanaelekea Vetenari. Mwendo wa gari ulikuwa mkali na  Thomas alitumia muda wake kuangalia nyuma kwa tahadhari, milio ya ving'ora vya poliai ilianza kusikika kwa  mbali walipokuwa wanakaribia jirani na makutano ya barabara yaliyopo jirani na kituo cha mafuta cha Oilcom.

      Santos  alifungua mlango wa gari kisha akatoa Jambia shingoni mwa Dereva teksi ambaye alibaki akishangaa sababu iliyomfanya Mhindi yule mwekundu amuachie kirahisi namna hiyo mshangao wake haukupata majibu akasikia mlango wa nyuma upande wa kushoto nao  ukifunguliwa. Dereva teksi alipoona hivyo pamoja na kusikia ving'ora vya magari ya polisi aliamua kuwakamatisha Santos na Thomas, akili yake ilimpa asilimia mia kwamba Santos na Thomas walikuwa wakiwakimbia  polisi.

    Aliazimia kukamyaga breki ya gari kwa nguvu ambayo itawafanya Santos wayumbe ili awazubaishe  polisi waweze kukaribia, Dereva teksi huyo hakujua kwamba hila yake tayari ilikuwa imegundulika baada ya Thomas kuuona mguu wake alipokuwa  akijaribu kuutoa kwenye kikanyagio cha mwendo aupeleke kwenye breki.

     Mguu wake huo haukufika kwenye breki tayari Thomas alishadaka kidovu chake kwa mkono wa kushoto na kisogo chake kwa mkono wa kulia , tendo hilo lilimshangaza Dereva teksi huyo akawa amesitisha kukanyaga breki bila ya kutarajia. Thomas naye hakutaka kupoteza muda alifanya tendo la haraka la kuzungusha shingo ya Dereva akaivunja kisha akaruka nje kwa mlango wa upande wa kushoto alioufungua, Santos naye aliruka nje na wote wakatumbukia kwenye mtaro wa maji machafu uliokuwa mkavu.

      Walitoka kwa haraka wakasimana kando ya pili ya mtaro huo kutoka barabarani bila ya kuonekana na mtu, walijikung'uta nguo zao huku wakisikia kishindo kizito kilichowawafanya watabasamu. Muda huo huo pikipiki zilizopakia askari wenye sare za kikosi cha kutuliza ghasia wenye silaha zilipita kwa kasi sana, wakielekea upande kiliposikika kishindo hicho ambacho waltambua ni cha ile Teksi baada ya kukosa muelekeo kutokana na Thomas kumuua dereva kwa kumvunja shingo.

     Baada ya kufanya tukio hilo walitembea hadi kituo cha daladala cha Tazara  wakakuta gari yao iliyowafuata ikiwa imeegeshwa kwenye kituo cha daladala, waliingia ndani wakiwa na sura za huzuni kutokana na kumkosa Norbert.

            "What(Nini)?" Benjamin aliuliza.

            "He escaped( Ametoroka) Thomas alijibu.

            "How(Kivipi)" Benjamin aliuliza kwa kuchoshwa na taarifa hiyo.

             "He knocked your window as a sluggard( Aligonga kioo chako kama mvivu)" Santos naye alidakia kisha akawatazama wale wazungu watatu akawaambia, "ni mtu  makini sana na sisi tuwe makini".

    Wazungu  hao waliitikia kwa kichwa tu  pasipo kuongea lolote kisha wakaonesha ishara ya dole gumba kwa Santos, Benjamin aliwasha gari kisha akaliingiza barabarani akaliondoa kwa mwendo wa wastani.

****

     Pikipiki aliyopanda  Norbert ilikuja kumuacha katika mtaa ambao alimuelekezaa dereva ampeleke, Norbert alishuka akamlipa dereva wa pikipiki hiyo ambaye alishukuru Mungu kwa kufika mwisho wa safari kutokana na harufu kali aliyokuwa nayo Norbert. Alikubali kumbeba Norbert hadi mitaa hiyo kutokana na kusaks noti tu, laiti ingelikuwa siyo noti basi asingembeba kutokana na harufu kali aliyokuwa akiitoa. Alipopewa pesa yake aliamua  kugeuza pikipiki yake na kuondoka kwa kasi kuepuka harufu hiyo, alimuacha Norbert akiwa amesimama palepale hadi pale alilipopotea katika upeo wa macho ya Norbert.

    Hapo Norbert ndiyo aliamua kutembea kusonga mbele huku akiwa makini kuangalia uwepo wa mtu anayemfuatilia, alitembea kwa mitaa takribani mitatu kisha akasogea jirani na geti kubwa jeusi ambalo lilikuwa na kibanda kidogo cha ulinzi. Aligonga geto hilo kisha akasubiri kidogo ambapo mlinzi alifungua dirisha dogo akachungulia nje, mlinzi alipomuona ni Norbert alifungua geti kwa haraka sana kisha akasogea pembeni huku akibana pua kutokana na harufu iliyokuwa inatoka mwilini mwa Norbert.

                 "Mh! Bosi mbona unanuka hivyo?" Mlinzi huyo  aliuliza.

                 "siyo kazi yako, mke wangu yupo?" Norbert alimuambia akiwa amelunja sura kutokana na kutopenda maneno ya mlinzi huyo.

                 "Madam yupo we pita tu" Mlinzi huyo alijibu na Norbert alipita pasipo kungeza neno jingine hadi kwenye mlango wa nyumba kubwa ya kisasa. Aligonga mlango  wa nyumba mara moja kwa kutumia vidole vitatu, mlango wa nyumba hiyo ulifunguliwa na Norene akaonekana akiwa amevaa nguo laini la kulalia.

      Harufu inayotoka mwilini mwa Norbert ilimfanya hadi yeye abane pua kisha akasogea kando ya mlango kumpisha aingie, Norbert aliingia ndani kisha Norene akafunga mlango wakabaki wakitazamana kama ndiyo wanaonana. Kicheko cha ghafla kilimpuka Norene alipomtazama Norbert usoni akaona uchafu mweusi ambao ulimfanya aonekane kituko, alibaki akiwa ameweka mkono mdomoni kutokana na harufu kali iliyokuwa inatoka mwilini mwa Norbert.

                   "Ulilala kwenye gari la taka nini?" Norene aliuliza huku akicheka.

                    "sasa unacheka nini?" Norbert aliuliza.

                     "Wacha nicheke tu umekuwa kama zimwi vile na unavyonuka kama ulijifukizia marashi yaliyotengenezwa kwa taka za dampo" Norene aliongea.

                    "Alaa! Kumbe sasa ngoja nikukumbatie tugawane hii harufu tuone utamcheka nani" Norbert aliongea akiwa na tabasamu huku akimsogelea Norene akiwa ametanua mikono amkumbatie, Norene alikimkwepa kisha akakimbia. Norbert alibaki akimfukuza nyuma huku akiwa ametanua mikono yake, Norene alikimbilia moja kwa moja chumbani kwake akaingia katika bafu la ndani huku akiwa anacheka kwa jinsi Norbert alivyokuwa anamkimbiza.

       Norene alikimbia hadi lilipo eneo maalum la kuogea lililotengenezwa kwa udongo mgumu, alipofika hapo alisimama mbele ya sinki kubwa la kuogea ambalo tayari lilikuwa limejaa maji akimuangalia Norbert kwa tabasamu pana.

                   "Yaani hapo tunaingia wote kwenye sink " Norbert aliongea huku akimsogelea Norene ambaye alikuwa alikuwa akimtazama kwa tabasamu tu.

                   "Toa madude yako ya mfukoni ndiyo uje tuingie wote" Norene alimuambia Norbert ambaye alitoa vitu vyake vyote vilivyokuwa na uwezo wa kuingia maji vikaharibika kisha akamfuata Norene kwa kasi akiwa ametanua mikono amkumbatie, Norbert alipomkaribia Norene hakufanikiwa kumgusa kwani alijikuta akitupwa ndani ya sink la kuogea akiwa na nguo zake baada ya Norene kutoa mtindo mmoja wa judo wa kujihami. Alimzoa Norbert kwa kumtegea mguu uliomfanya ajikwae akaingia ndani ya sinki hilo lililojaa maji pasipo kujigonga sehemu yoyote kutokana na utaalam alioutumia, Norbert aliangukia kwenye maji kifudikifudi na alipogeuka alimuona Norene akimtazama huku akicheka kwa nguvu.

                    "umeniweza leo" Norbert aliongea huku akijipangusa maji usoni mwake.

                    "leo mjanja mimi haya vua nguo zako mwenyewe uoge ndiyo mengine yatafuata" Norene aliongea

        Norbert alivua nguo zake ambazo tayari zilikuwa zimelowana, alioga akiwa anasimamiwa na Norene. Alipomaliza kuoga Norene alimpa taulo akajifuta maji kisha akampatia vazi maalum la kuvaa ambalo huvaliwa muda wa kulala.

                  "Nimekuweza  kweli yaani niliweka maji ya kuoga nikienda kulala nioge ila wewe umejileta umeyaoga" Norene alimuambia Norbert huku akitoka bafuni na Norbert akafuata nyuma yake.

****

       Gari walilopanda kina Thomas liliingia  katika nyumba yenye uzio mrefu pamoja na geti kubwa, gari liliingia eneo la maegesho na wote wakashuka wakakuta wenyeji walikuwa wakiwasubiri kwa hamu sana. Walikuta Mzee Filbert Ole akiwa na faili mikononi mwake , Wilson Ole, Benson, Leopard Queen na Kamishna wakiwa wanawasubiri kwa hamu, kitendo cha wao kufungua milango na kuikanyaga ardhi ya nyumba hiyo makofi ya ukaribisho yalipigwa na Filbert Ole ambaye ndiye ametoroshwa gerezani masaa machache yaliyopita.

             "Karibuni simba wetu" Filbert Ole alipngea akiwa na tabasamu pana usoni mwake, vijana wote wa kazi walioingia humo ndani waliachia matabasamu mapana katika nyuso zao kisha wakaenda kusalimiana na wenyeji wao kwa kushikana mikono.

              " ushindi nauona kila ninapowatazama" Filbert Ole aliongea.

               "hakika ushindi lazima, tumekuja kwa ajili ya kazi sasa tunaianza kazi" Santoa aliongea kisha akaivua kofia aliyoiva kichwani ambayo ilifanya mywele zake zionekane kwa wote, sura yake  isiyo na mzaha  ilionekana ambayo iliwafanya Filbert Ole na mdogo wake Wilson watabasamu.  Filbert Ole alimkabidhi faili Santos huku akisema,

                "usiku huu anatakiwa auawe M.J Belinda ambaye ndiye huyo wa kwanza kwenye file".

        Santos aliafiki kwa  kutikisa kichwa kidhs akasema, "bastola zetu zile nafikiri zimewasili tayari tutazihitaji kwenye kazi  hii".

                     "Ondoeni shaka kuhusu hilo  bastola tayari zimewasili cha muhimu ni kumuua huyo malaya tena muwe makini sana ni komandoo" Wilson aliongea.

                      "Komandoo mmoja mbele ya makomandoo hatapona ameshazidiwa uwezo" Thomas alidakia na wote wakaachia matabasamu usoni mwake.

                       "Anawasili kwake saa tatu usiku General kampatia kazi makusudi ili aingie muda huo, nyumbani kwake kwa sasa analala peke yake hivyo kazi hiyo itafanyika kwa urahisi" Kamishna alionges kwa msisitizo.

                      "sasa hivi ni saa mbili kamili hakuna muda wa kupoteza ni kuingia kazini"Benson aliongea huku akiitazama saa yake ya mkononi, vijana wa kazi watatu ambao ni wale wazungu walioletwa pamoja na kina Thomas waliachiwa kazi hiyo pamoja na usafiri, walipewa gari maalum inayotumia ramani kuwaelekeza ilipo nyumba ya M.J Belinda ili waende kummaliza.


****


              MLIMANI CITY
   Kazi nzito aliyopewa M.J Belinda na mkuu wake ilimfanya achelewe kutoka na hata pia achelewe kwenda kufanya manunuzi ya vitu muhimu vya nyumbani kwake atakavyovihitaji, ilikuwa ni masaa machache tu yamebaki ili iingie siku mpya ambayo ndiyo ndani yake  kutakuwa na mazishi ya Jenerali Kulika. Akitumia gari yake ya kazini yenye nyota mbili mbele na nyuma, gari hiyo iliingia katika eneo la Mlimani city hadi kwenye maegesho.

    Kawaida ya mwanajeshi akifika cheo chs brigadia jenerali basi gari yske huwekwa nyota moja, akiwa meja jenerali basi gari yake huwekwa nyota mbili, akiwa luteni jenerali basi gari yake huwekwa nyota tatu na akiwa Jenerali basi gari yake  huwekwa nyota nne. Nyota hizo zote huwekwa sehemu ya kuweka namba za usajili mbele na nyuma, gari hiyo ikionekana mahali popote kwenye kambi ya jeshi hutambulika aliyemo ndani ya gari ni nani kwa kuangalia idadi ya nyota zilizopo sehemu ya namba za usajili.

     Buti la kijeshi lilionekana likitoka ndsni ya gari aina ya Toyota landcruiser yenye rangi ya kijani iliyopauka, alionekana M.J Belinda mwanamke mrembo sana mwenye ngozi laini na umbo lililobeba mzigo mzito uliopo chini ya kiuno ambao uliweza  kumvuta mwanume yoyote mwenye tamaa abaki anamtazama. Ngozi ng'avu macho yake yaliyokaa kama  yanasinzia pamoja na nyusi zake nene zilizochongwa vizuri, zilimfanya atamaniwe na kila mwanaume mwenye kupenda kuwa na mwanamke mrembo lakini nguo zake za kazi zenye nishani tele pamoja na bawa moja la chuma lililopo juu ya sare vilitosha kuwafukuza wanaume wasimsogelee kabisa. Hakuna mwanaume ambaye angekuwa tayari kumfuata akiwa amevaa gwanda lenye cheo kikubwa kama hiko, umri wake na cheo chake vilikuwa vitu viwili tofauti.

    Akiwa na gwanda hizo aliingia ndani ya jengo la Mlimani city kwa ajili ya kununua vitu katika  maduka makubwa(supermarket)  ya hapo, aliingia ndani ambapo alikaa kwa robo saa akatoka akiwa amebeba  mizigo ambayo alienda kuiweka nyuma ya gari kisha akaingia ndani ya gari akaondoka eneo hilo ili awahi nyumbani kwake kupumzika.

    Aliliondoa gari hadi kwenye makutano ya barabara ya Mlimani city aliingia upande wa kulia kwenye barabara ya Ssm Nujoma, alienda na barabara hiyo hadi alipofika mwanzo wa barabara ya Shekilango. Aliiacha barabara ya Sam Nujoma akaingia barabara ya Shekilango, alienda na barabara hiyo hadi alipofika kwenye kituo cha daladala cha Kwa Manyola akahisi kuna hali tofauti ndani ya gari yake. Mlio wa makasha ya kiti cha nyuma ambayo hutoa mlio mtu akiwa anajigeuza aliisikia mlio wake alipotaka kugeuka kuangalia nyuma aliguswa na kitu cha baridi sehemu ya mwanzo wa shingo, msisimko ndani ya mwili wake ndiyo ulfuata baada ya kuguswa na kitu hicho cha baridi.

                           "Tulia hivyo hivyo Belinda" Alisikia ikitoka nyuma yake ikimpa amri.

                            "Moses nini unafanya sasa?" Belinda aliuliza baada ya kuibaini ni sauti ya Moses ndiyo ilimpa amri.

                             "Imenibidi ili nikufumbue macho" Moswa aliongea.

                             "sikuelewi" M.J Belinda aliongea, alipotaka kugeuka nyuma alisikia mlio wa kuondolewa usalama kwa bunduki ukisikika.

                             "Park gari hapo stendi haraka sana" Moses alitoa amri na muda huo tayari gsri iilikuwa imeshafika kituo cha Sinza Kijiweni, M.J Belinda alitii amri na akaegedha gari kituoni. Moses alimpatia simu yake ambayo ilikuwa  ina video iliyorekodiwa, M.J Belind aliipokea simu ya Moses akaitazama video hiyo hadi mwisho kisha akarudisha  simu kwa Moses huku akiwa amechoka kwa kile alichokiona.

                              "Benson ni muuaji wa General hadi sasa uamini hilo kwanza hadi uchunguzi mwingine utakapoendelea" Moses alimuambia.

                               "Umeipata wapi hii video?"  M.J Belinda aliuliza.

                               "Nor yupo kazini na ndiyo amebaini, unaweza kuendesha kwa sasa" Moses alimuambia na M.J Belinda akatii akaliingiza gari barsbarani akaondoka.


     Ndani ya dakika tano tayari walikuwa wamefika mtaa wa Megasiti ambapo ndiyo kwenye makazi ya M.J Belinda, gari lake lilisimama kwenye geti kubwa la mapambo ya mti M.J Belinda akapiga honi. Geti hilo  lilifunguliwa na mtu aliyevaa magwanda ya JWTZ ambaye ana jukumu la kuilinda nyumba nyakati za usiku, gari liliingia ndani na Moses akawa ana kazi ya kuwatazama wanajehi waliokuwa watatu walioanza kuifuata gari ya M.J Belinda.

     M.J Belinda aliipeleka gari kwenye maegesho akashuka na wanajeshi hao watatu wenye miili miembamba na mirefu wakasimama mbele yake, wote walitoa saluti kisha wakasimama kiukakamavu.

                            "Kuna mgeni yoyote aliyefika hapa?" M.J Belinda aliuliza lakini wale wanajeshi watatu hawakuongea chochote.

                            "Sajenti, Koplo na lensi Koplo inamaana swali langu hamulisikii?" M.J Belinda aliuliza lakini hakujibiwa zaidi ya wale wanajeshi kutazama kila mmoja, hali hiyo ilimkera sana M.J Belinda na akapiga hatua kusogea karibu kisha akawasukuma kila mmoja kwa hasira.

                            "Inamaana mna dharau siyo" Aliwaambia kwa hasira lakini ni kama alikuwa amewasha moto, Mwanajeshi aliyekuwa amesimama kati wenzake wawili alirusha ngumi ambayo aliikwepa kwa kuyumba upande wa kulia. Yule aliyekuwa  upande wa kulia alitupa ngumi ngumi ya uso ambayo aliinama ikapita kisha akajizungusha akakaa sawa, aliwatazama wale wanajeshi ambao walivua kofia zao wakazitupa chini na sura zao zikaonekana dhahiri kwa msaada wa taa kubwa  iliyopo uani. Walikuwa ni wazungu watatu waliojipaka  rangi nyeusi usoni wasionekane ni watu weupe, Belinda aliwajua kuwa ni wazungu kwa kupitia nywele zao ambazo zilikuwa kama singa lakini zilikuwa nyeupe zinazoelekea kufanana na mvi.

      Wazungu hao hawakumuacha hata M.J Belinda apate nafasi kujifikiria zaidi kuhusu wao, waliamua kumfuata M.J Belinda kwa mapigo tofauti. Yule aliyekuwa kati alimfuata kwa ngumi ambayo M.J Belinda aliikwepa kwa kuyumba pembeni, huko pembeni alipoyumba mwingine alimfuata kwa mateke mawili ya juu ambayo pia aliyakwepa kwa kupiga msamba yakapita.

     Mwingine alimfuata kwa mateke mawili ya kujirusha akiwa pslepsle chini kwenye msamba ambayo yalimpata barabara ya mgongo, M.J Belinda alitoa mguno wa maumivu kisha akaanguka chini na wazungu hao wakamzunguka huku wakidunda kama mabondia.
M.J Belinda aliamua ajikaze kisha akajiinua kwa sarakasi, hapo na yeye alianza kujibu mashambulizi kwa utaalamu wa juu akitumia mbinu zake za kikomandoo. Alitumia uwezo wake wote katika kupigana  huku akijua alikuwa akipigana na watu wenye uwezo sawa na yeye ambao walikuwa wamemzidi idadi, alijitahidi awezavyo lakini wazungu hawa walionekana kumzidi ujanja kabisa.

     Mpambano ulimzidia ingawa alikuwa ameshamjeruhi mmoja jicho na wawili wakamzidia nguvu, alipigwa mapigo mfululizo ambayo yalimfanya Moses atoke ndani ya gari na kuingilia.  Moses aliingia kwa kurusha mateke mawili yaliyowapata makomandoo wawili chini ya shingo zao wakaenda kusalimiana na ardhi katika upande aliopo M.J Belinda  ameanguka ambaye  alimshika mmoja akavunja shingo yake akafa kisha wa pili akampiga goti la uso.

     Mpambano uliwageukia wazungu hao kwa kupewa kichapo kizito mfululizo hadi mwingine akapoteza maisha, alibaki yule aliyepigwa goti la uso  tu ambaye alitiwa nguvuni akaingizwa kwenye chumba cha mateka katika nyumba  ya M.J Belinda.

****


     Muda ambao Moses na M.J Belinda wanafanikiwa kuwadhibiti makomandoo wa kizungu ndiyo muda  ambao Norbert alikuwa yupo ndani ya gari aina ya Toyota Noah akitoka nyumbani kwa Norene Tabata, akiwa ndani ya nguo nyingine kabisa aliamua kutoka akimdanganya Norene alikuwa akiingia kazini kumbe kulikuwa na jingine zaido ya hiyo. Ilikuwa ni siku maalum ya kukutana na Josphine tangu alipoagana naye kwa mara ya mwisho siku ya jumamosi, pia zilikuwa zimebaki siku tatu na masaa mawili nchi ya Tanzania iingie katika mikono ya kijeshi chini ya Luteni Jenerali Ibrahim.

     Siku hiyo Norbert aliamua aende katika nyumba anayoishi Josephine akiwa na akili nusu hofu nusu amani, alitumia  dakika shirini akawa tayari yupo ndani ya eneo la Keko Michungwani. Hapo alimpigia simu Josephine aje amfuate katika muda huo wa usiku kisha akatulia amsubiei Jospine aje baada ya kumpa taarifa.



JUMAMOSI NAYO NI SIKU TUKUTANE PANAPO UHAI NA AFYA NJEMA.



HAIRUHUSIWI KUNAKILI RIWAYA HII KWA NAMNA  YOYOTE PASIPO RIDHAA
YA MTUNZI


No comments:

Post a Comment