Monday, June 20, 2016

NSUNGI

RIWAYA:  NSUNGI
MTUNZI; HASSAN O MAMBOSASA
MAHALI: TANZANIA





       SURA YA KWANZA


******KIONJO*****


Nuru pekee iliyoonekana kuangaza anga ilikuwa ni Mbalamwezi kutokana na kuwepo kwa kiza kizito sana, ilikuwa ni majira ya usiku sana katika eneo la makaburini sehemu yenye mti mkubwa sana. Mti huo ulijenga mazingira  ya kutisha katika muda huo wa usiku , kutisha kwa mazingira hayo hakukuwafanya waliopo eneo hilo  kutishika na giza hilo la makaburini

 Watu hao  walikuwa wamekaa makundi manne wakitazama mbele alipo mzee wa makamo aliyekuwa kajifunga kaniki kama ilivyo wengine huku akiwa na shanga nyingi pamoja na hirizi ambazo hakuna mwingine aliyezivaa nyingi zaidi yake, hali ya amani ndani ya eneo hilo ilionekana kutibuka na hasira za waziwazi zilionekana katika nyuso za waliopo hapo kasoro huyo mzee. Kimya kizito kilikuwa kimetanda eneo hilo na wote walikuwa wakimtazama mzee huyo ambaye alikuwa kimya akizitazama pande zote nne zilizopo eneo hilo, mzee huyo alikuwa kimya muda wote huo akitafuta la kuongea.

   Kimya cha mzee huyo kiliibua minong'ono ya chini kwa chini miongoni mwa wahusika kutokana na kukosa subira ya kusubiri kile walichokuwa wakikisubiri kutoka kwa mzee huyo, hatimaye minong'ono hiyo iligeuka kuwa kelele baada ya mzee huyo kutokuongea.


    Subira ya kusubiri maneno kutoka kwa mzee huyo iliwashinda na hapo lawama za waziwazi kwa mzee huyo zikaanza, maneno ya lawama yalianza kurushwa kwa mzee huyo ambaye alikuwa ametulia kimya tu.
Kimya chake kilishindwa kustahimili lawama zao  na hatimaye akanyoosha mkono juu huku macho yakiwaka kama ya Paka, ghadhabu za waziwazi zilionekana zipo katika uso wake baada ya macho hayo kuwaka kama taa kisha yakazima. Kitendo cha kuwaka kwa macho hayo kilisababisha pande zote nne zikae kimya huku zikimtazama mzee huyo kwa umakini sana, wote kwa pamoja walikuwa wapo makini katika kutega masikio kusikiliza nini kitaongelewa na mzee huyo.

"Zindubaaaaa!" Mzee huyo aliongea kwa sauti kubwa huku akitazama pande zote nne kwa zamu.
"Heeee! Zinduuu" Wote kwa pamoja waliitikia kwa utiifu mkubwa.

"Zindubaaaaaaa!" Mzee huyo aliongea tena kwa sauti kubwa  huku akisimama akinyoosha mkubwa, sura ya jazba ndiyo aliyokuwa nayo akionekana hakufurahishwa kabisa na jambo fulani.

"Wana Zinduba, Zinduba jamii yetu ya toka mababu na mababu. Tangu sukuma, manyema, waha  na kerewe zilipoungana kwa mara ya kwanza kuiunda Zinduba iliyo na amani na upendo. Zinduba hii itaendelea kudumu milele na milele si Ntambwe mwenzangu wala nani atakayevunja jamii na sipo tayari kuiona Zinduba ikivunjika kisa Nsungi. Nasema sipo tayari niruhusu Nsungi awe ndiyo chanzo cha kuvunjika kwa umoja wetu uliodumu toka enzi za mababu. Zindubaaaaaa!" Mzee huyo aliongea kwa hasira sana kisha akamaliza kwa kutamka ishara ya salamu ya jamii ya Zinduba yenye nguvu sana upande wa kaskazini magharibi na magharibu mwa Tanzania.

"Heeee! Zinduuuuuuuu" Wote waliiitikia kwa sauti kubwa sana wakati mzee huyo akiwa anataja ishara hiyo ya salamu ya ukoo huo, mzee huyo alipomaliza hayo maneno hakuwa na la ziada na alirudi kuketi mbele kabisa kwenye mzizi mkubwa wa mti huo uliopo hapo makaburini kisha akaonesha ishara ya mkono iliyosababisha mzee mwingine wa makamo asimame.


   Mzee huyo aliyesimama alikuwa amejifunga kaniki nyeusi kama ilivyo wengine, mzee huyu alikuwa ametofautiana na wengine kwa kuvaa hirizi  iliyofungwa vyema kichwani ikiwa inaning'inia kwenye paji la uso. Mabegani alikuwa amevaa shanga nyingi zenye mchanganyiko wa simbi zilizoishia ubavuni, uso wake ulikuwa una mistari ya unga mweusi na mweupe ambao ulimfanya asiwe tofauti na sehemu ya ngozi ya pundamilia. Kusimama kwake mzee huyo kuliambatana pamoja na moshi mzito uliotoka sehemu ya makalio yake, macho yake pia yaliwaka mithili ya nyota mbili zilizopo pamoja angani. Mzee alitia ajabu jingine kwa kutembea mithili ya mtu aliyefungwa mashine miguu kusogea mbele  haraka aliposimama mzee mwenzake ambaye ndiye kuongozi wao, alipomfikia kiongozi wao alipiga goti moja akainama kwa heshima kisha akawageukia wenzake waliokuwa wamekaa makundi manne.


"Zindubaaaa!" Alitamka kwa nguvu hadi sauti yake ikaleta utetemeshi katika ardhi iliyopo eneo hilo, lilikuwa ni kama tetemeko ambalo halikuwapa wahka wanajamii hao wa kichawi wala halikutikisa mti mkubwa ambao walikuwa wamekaa chini yake.

"Heeeee! Zinduuuu!" Jamii nzima ya Zinduba iliitikia kwa pamoja, kuitikia huko kulimfanya mzee huyo asimame kimagambo zaidi na alitikisa kichwa kukubaliana na ushirikiano walioutoa wenzake katika kuitika huko.

"Zinduuuu! Bweeeee! Mkuu nafikiri mmemsikia enyi wana wa manyema, mkuu nadhani mmemsikia enyi wana wa Kerewe, mkuu nadhani mmemsikia enyi wana wa Uha pia mkuu nadhani mmemsikia enyi wana wa sukuma. Hakuna zaidi yake kitukuu cha mababu wa Ntambwe atakayepinga amri yake, Nsungi ni wa kwetu sisi na ataendelea kuwa wa kwetu sote siyo koo ya Manyema,Usukuma,Ukerewe wala Waha ni wetu sote. Zindubaa!" Mzee huyo aliongea kwa sauti kubwa sana.


"Heeeee! Zinduuu!" Wote kwa pamoja waliitikia kisha Mzee huyo akaendelea kusema, "muda wa kujiweka sawa Zinduba yote iwepo na Mnyunga vanza kuwaweka sawa wanazinduba".


   Mzee huyo alipomaliza kuongea maneno hayo aligeuka nyuma akatoa heshima kwa mkuu halafu  akatembea kwa mwendo uleule kama amefungwa mashine miguuni akarudi kukaa, muda huo wa kujiweka sawa ilikuwa inamaanishwa ni muda  wa wachawi kula nyama kwa pamoja ambapo ilihitaji wote kwa pamoja wajitokeze


 Eneo hilo la chini ya mti kulikuwa kukionekana kuna vikundi vinne pamoja na kiongozi wao lakini kiukweli kabisa kulikuwa kuna kundi kubwa la wachawi ambao  walikuwa hawaonekani kabisa na walikuwa wakijificha hivyo ili kuweka ulinzi katika eneo hilo na wengine kulinda vitu muhimu visiibiwe na wachawi wasiohusika, ukifika muda wa kula nyama ndiyo wachawi wote ambao huunda Zinduba huonekana kwa pamoja.

    Ndani ya muda huo mchawi mmoja baada ya mmoja  alianza kuonekana kutoka pande mbalimbali za eneo la makaburi hayo, ilipotimia nusu dakika wachawi mbalimbali waliovaa kaniki nyeusi wakiwa na nyuso zilizowafanya watishe walianza kuonekana. Walijitokeza kwa namna ambayo ingemshtua mtu wa kawaida kama angeweza kuwepo eneo hilo lakini kwa wachawi wenzao ilikuwa ni jambo la kawaida kabisa, eneo zima la makaburi lilikuwa limekaliwa na wachawi hao haswa makaburi yaliyojengewa ambayo yaligeuzwa viti kabisa. Makaburi yaliyojengewa hayakuweza kuonekana kabisa na yalikuwa yamefunikwa na wachawi hao kwa kuyakalia, misalaba pekee ndiyo ilionekana eneo hilo kuonesha eneo lilipo karibu.


    Muda huo nyimbo zisizoeleweka zilianza kusikika zikiimbwa na wachawi hao kwa nguvu  sana, wachawi wachache walikuwa wamesimama  wakigawa vipande vya nyama mbichi kwa kila mmoja huku nyimbo hizo zikiendelea. Shangwe na vigelegele ndiyo vilitawala eneo hilo wakati nyama hizo zikifika kwa kila mchawi, ndani ya muda mfupi kila mchawi alikuwa ameshika kipande cha nyama huku akila na hapo ndiyo na nyimbo nazo zilikoma huku paka weusi  wenye macho ya kung'aa wakionekana wapo kwenye kila kingo ya eneo la makaburini. Bundi wengi wenye rangi nyeusi nao muda huo  ambao wachawi walipojitokeza kwa pamoja walionekana wakipaa kuzunguka eneo la makaburini hapo, viumbe hao walikuwa wapo makini katika kuimarisha ulinzi wa hapo makaburini na hawakuwa viumbe wa kawaida kama ambao waliozoeleka kuonekana mchana. Viumbe hao walikuwa ni mizimu kutoka koo za nne hizi ambazo Zimeunda Zindiba, walikuwa ni vibaraka  wa mizimu mikuu ya koo zote nne ambazo ndiyo zilikuwa zimekaa kimakundi hapo awali zikuonekana hazina amani.


     Viongozi wa jamii hiyo ya kichawi ya Zindiba walikuwa wamejitenga peke yao wakiwa na vichwa vya bindamu, walikuwa wakivila vichwa hivyo kwa namna ya kustajaabisha kabisa mithili ya watu wanaokula vichwa vya ng'ombe vilivyopikiwa supu, kula kwao ilikuwa ni kwa pupa mithili ya watoto wanaokula chakula cha shughuli ambayo hawakualikwa.


****


  MTAA WA UZUNGUNI
           MBEZI
    DAR ES SALAAAM
 
     Muda huo ambao wachawi wa jamii ya Zinduba wakiwa wapo kwenye eneo la makaburini, ndani ya jiji la Dar es salaam maeneo ya Mbezi mtaa wa Uzunguni hali ilikuwa shwari kabisa katika usiku huo wenye kiza. Wakazi wa eneo hilo wote walikuwa wamelala isipokuwa binti mmoja aliyekuwa ameamshwa usingizini na kero ya takamwili, binti huyo alikuwa amebanwa na haja ndogo ambayo ilimlazimu kwenda katika chooni kilichopo humo ndani kuondoa takamwili hiyo. Alienda haraka katika choo ambacho kilikuwa kimejengwa ndani ya chumba chake, huko alitumia muda mfupi akawa ameshamaliza kuiondoa  haja ndogo iliyokuwa ikimkera na sasa akatoka chooni humo akasimama mlangoni.


  Uchovu wa mwili wake kuamka usingizini alianza kuusikia aliposimama hapo mlangoni baada ya takamwili  kumuondoka, alijikuta akiuegema ukuta kwa uchovu huo. Usingizi ulianza kumzidi kiwango na ikambidi apige  hatua kutoka kwenye mlango wa chooni aingie kwenye eneo la chumbani baada ya kivivua viatu vya choomi kwenye  ngazi moja iliyotengenezwa kwa marumaru zenye  mapambo yenye kupendeza. Alipoimaliza ile ngazi hiyo  iliyopo kwenye mlango wa choo cha chumbani kwakralikuwa akiikanyaga sakafu ya chumbani kwake, alipoweka mguu wake kuikanyaga sakafu ya chumbani kwake kiza kizito kilitanda humo ndani ambacho kilimtisha sana.

   Binti huyo baada ya kiza hicho kutanda alianza kusikia sauti ya wadudu mbalimbali wa porini, eneo alilolikanyaga ambalo alidhania ni sakafu ya chumbani kwake alianza kuhisi siyo sakafu bali ni machanga mwingi sana. Mshtuko ndiyo ulivamia moyo wa binti huyu kutoka familia yenye kujiweza, alipoangaza pande zote  alihisi yupo kwenye eneo la wazi ambalo lilikuwa limezungukwa na miti mingi. Akiwa katika  mshangao huo sauti za vicheko zilianza kusikika kisha eneo alilopo akahisi lilikuwa likizunguka, binti huyo alitoa ukelele wa uoga akakimbia huku akiita jina la mama yake. Hakufika mbali alijikwaa akaanguka hapo kelele hizo za vicheko zikabidilika kuwa  za popo kisha sauti ya  viatu vya farasi akikimbia ikaanza kusikika vikitokea nyuma yake, binti huyo aliamua kujikaza akajiinua pale alipoanguka akaanza kukimbia tena lakini hakufika mbali akajigonga pua kwenye nguzo nyeupe ambayo hakuiona. Sauti ya viatu hivyo vya farasi zilizidi kukaribia karibu, uoga nao ukazidi kuivamia nafsi ya huyo binti akajikuta akiishika ile nguzo ambayo aliiona ina rangi nyeupe na hakujishughulisha kuingalia ilikuwa ni kitu gani. Alisimama kwa msaada wa kushika nguzo hiyo kisha akakimbia kwa hatua tatu tu akajikuta akizuiwa na nyavu nyeupe iliyomuangusha hadi akaangukia mgongo  wake, alipotazama juu akiwa bado ana maumivu ya mgongoni mwake aliona Mtambaa panya mweupe uliofungwa nyavu ambazo zilikuwa zimepita katika eneo alilokuwa anakimbilia.

   Binti hakuelewa ule Mtambaa panya ulikuwa una mahusiano gani ma nyavu ile, alipoangalia kulia na kushoto ndipo alipobaini Mtambaa panya ule ulikuwa ni nguzo ya juu ya goli la uwanja wa mpira wa miguu. Hakuelewa amefikaje eneo hilo kwani alikuwa yupo ndani ya chumba chake cha kulala, kelele za viatu vya farasi nazo zilizidi kusikika kisha upepo ukaanza kuvuma kuelekea alipo.

"Huwezi kunikimbia hata siku moja wewe ni halali yangu" Sauti iliyojaa mwangwi ilisikika ambayo ilizidi kumtia woga na ikamfanya asimame kwa haraka kisha akaangalia upande aliokuwa anakimbilia, huko aliona nyavu ya goli la mpira ambayo imgemzuia kukimbia. Alipogeuka nyuma kwenye eneo litakalomuwezesha kukimbia aliona umbile la mtu likiwa limejengwa na vumbi baada ya upepo kuvuma kuvuma, umbile hilo lilinyoosha mkono mrefu ambao ulimfuata binti huyo kwa kasi ambao ndiyo kumtia uoga.

"Maaaaamaaaaaa!" Alipiga ukelele akarudi nyuma kwa kasi akakutana na kizuizi kilichomzuia sehemu za nyuma ya ugoko wa miguu yake, kizuizi hicho kilimfanya aangukie katika kitu kilaini akiwa ameziba macho kwa kiganja chake asiuone mkono ule uliojengwa na vumbi ambao ulikuwa ukija eneo alilopo. Aliendelea kupiga kelele kwa uoga akijua umbo lile la mkono lililojitengemeza kwa vumbi lilikuwa likimfuata, alijaribu kujinyanyuka kwenye kitu laini alichoangukia huku bado akipiga kelele lakini akakosa nguvu akarudi pale. Alipotoa mkono macho alinyamza kimya mwenyewe akabaki akishangaa kwa uoga tu baada ya kujikuta yupo ndani ya chumba chake, kitu kilaini alichokiangukia ilikuwa ni godoro lake. Kichwa kilianza kumuuma kwa nguvu akajikuta akikishika baada  ya maumivu kuwa makali, maumivu hayo yaliisha ghafla na hapo kumbukumbuza eneo alilokuwepo zikamuondoka.

   Muda huohuo mlango wa chumbani kwake ukafunguliwa akaingia mwanamke aliyekuwa aliyekuwa amevaa mavazi ya kulalia, mwanamke huyo alipomuona yule binti katika hali ambayo hakutarajia kumuona nayo  alibaki akiwa ameweka mkono kinywani mwake.

"Yesu wangu Maria kimekupa nini mwanangu" Aliongea mwanamke huyo huku akimkimbilia Maria pale kitandani alipokuwa amelala, alipomfikia alibaki akiwa ameweka mikono kichwani baada ya kumuona Maria alikuwa akitokwa na damu puani. Mwanamke huyo alipigapiga chini miguu yake kwa kuchachawa na hali ya Maria ambaye  hadi muda huo alikuwa amepigwa na bumbuwazi kutokana na mazingira aliyojikuta yupo. Kila alipomtazama Maria ambaye alikuwa anashangaa sana , mwanamke huyo alizidi binti yake ambaye bado  alikuwa amezubaa. Nguo za Maria nyeupe za kulalia zilizokuwa zimechafuka kwa vumbi zilizidi kumfanya mwanamke huyo ashangae, alipiga magoti katika eneo la jirani ya kitanda ambapo Maria alikuwa amekaa hadi muda huo kisha akamtazama.

"Maria! Maria! Maria mwanangu una nini niambie mama yako, mbona unatoka damu puani? Uwiii niambie mwanangu" Mwanamke huyo alizidi kupiga kelele hadi vishindo vya watu wakikimbia vikasikika vikikaribia humo chumbani, mlango wa chumbani humo ulikuwa wazi na hapo wenye kutoa vishindo vile walionekana dhahiri. Walikuwa ni vijana wawili wa kiume waliokuwa wamevaa bukta za jezi ya mpira pamoja na fulana zilizokatwa mkono, vijana hao ambao kiumri walikuwa wamepishana walikimbia  hadi pale jirani na mama yao aliyekuwa amepiga magoti akimtazama Maria aliyekuwa ameketi kitako kwenye kitanda huku miguu ikiwa nje huku akiwa anaonesha kutoelewa chochote kinachoendelea. Mmoja wa vijana hao ambaye alionekana ni mkubwa kuliko mwingine aliamua kumpiga vibao vya mashavu Maria huku akiliita jina lake, Maria alishtuka kwa ghafla halafu akawatazama  wote waliokuwa wanamshangaa.

"Kaka Kevi, Frank, Mama kuna nini mbona siwaelewi kuna nini?" Maria aliuliza huku akiwatazama kila mmoja akiwa na mshangao.

"Maria mdogo wangu huelewi nini? Mbona umechafuka miguu yako? Mbona una damu puani" Kijana ambaye ni mkubwa kuliko Maria anayeitwa Kevi alimuuliza, Maria aliposikia swali hilo alijitazama kwa haraka sehemu zote alizoambiwa akiwa haamini kama kweli yupo katika hali hiyo. Miguuni na kwenye nguo zake kweli  alikuwa yupo kstika hali hiyo, alipojishika puani akaangalia mkono wake alikutana na damu ambayo ilimfanya azubae tena.

"Maria mwanangu umekumbwa na nini?"Aliuliza Mama  yake, swali hilo halikusikika kwa Maria. Mwanamama huyo alibaki akimshangaa binti yake ambaye muda huo tayari alikuwa ameinamisha kichwa kwenye mapaja yake huku akiweka mikono masikioni akitetemeka, Maria aliacha kutetemeka kisha akanyanyua uso akawashanga kwa muda na hatimaye akaangukia mgongo  katika kitanda chake akiwaacha mama yake na ndugu zake wakimuamsha bila mafanikio.

 Maria alikuja kufumbua macho kwa mara nyingine baada kuhisi mgongo wake ukimuuma kutokana na kulala sehemu ngumu sana, alikutana na mwangaza mwekundu ukiwa unamulika eneo ambao ulizidi kumshangaza. Alipoangaza pembeni aliona amelala katika eneo lenye vitu mfano wa changarawe kubwa ambazo zilikuwa zimerundikwa sehemu moja, vitu hivyo havikuwa tofauti na uchafu uliokuwa umetupwa dampo. Moshi mzito mwekundu ulikuwa unatoka  chini kwenda juu ambao ulizidi kumshangaza sana Maria, moshi huo ulimpa hisia za kwamba alikuwa amelala jirani na moto na hivyo ilimpasa ajiondoe eneo haraka sana. Hapo alikurupuka kwa haraka kisha akaangalia eneo ambalo alikuwa amelaza mgongo wake, alibaki akishtuka akapiga kelele alipoangalia eneo hilo na akawa anahema kwa kasi ya ajabu sana huku akianza kurudi nyuma.

   Loh! Alichokiona kilikuwa ni kitu kisichoweza kustahimiliwa na binadamu mwenye moyo laini kama wake kukitazama, kasi yake kurudi nyuma ilizidi kwani alichokuwa amekuona hakikuwa kitu cha kawaida na hicho kitu alikuwa akiishia kukiona kwenye filamu tu za kutisha. Maria aliongeza mwendo wake wa kurudi nyuma huku  akiwa haamini kama kweli alikuwa amejilaza kwenye kifusi cha mafuvu  ya binadamu ambayo mwanzo  alihisi yalikuwa ni changarawe kubwa.

   Kasi yake ya kurudi nyuma iliongezeka na hatimaye ikawa mbio ambazo hazikufika mbali kwani alikutana na kizuizi kilichomzuia asikimbie, hakika alijikwaa kwenye kizuizi hicho kilichomfanya aanguke chini akaangulia mifupa ya watu mingi ambayo ilivunjika kutokana na uzito wa mwili  wake. Kipande cha mkono cha mifupa aliyoiangukia kiliruka juu kikatua tumboni mwake, Maria alijiinua kwa haraka alipoona kipande hicho cha mfupa na aliachia ukelele wa woga ambao ulipelekea sauti za vicheko vya kutisha zianze kusikika.

"Karibu sana katika makao makuu ya Ulimwengu wa pili binti" Sauti nzito ilisikika ikimkaribisha ambayo hakujua ilikuwa inatokea upande gani kwani ilikuwa ikivuma kila upande  katika pande zote, ilikuwa  ni sauti iliyosikika kama ilikuwa imetoka kwenye maspika ambayo yalifungwa pande zote nne.

"Karibu sana na tena sana, huku ndiyo makazi yako ya asili binti" Sauti hiyo ilimuambia kwa mara nyingine, moshi mzito mwekundu ulitanda eneo hilo kwa kipindi kifupi cha muda  kiasi cha kumfanya Maria ashindwe hata kuona popote. Moshi huo haukaa sana na hatimaye ulianza kupungua taratibu, ulipopungua  kiasi cha Maria kuona vizuri aliweza kuona maumbo mbalimbali yenye ncha mbili sehemu  za juu yakiwa yamemzunguka, ulipoondoka kabisa huo moshi Maria aliweza kuyaona maumbo yake yalikuwa ni fisi na ncha mbili zilizopo juu yao yaani kichwani yalikuwa ni masikio yao. Fisi hao walianza kumsogelea karibu huku wakiwa wameinamisha vichwa vyao chini na kuzidi kumtisha, Maria alizidi kuogopa na hapo akarudi nyuma lakini alisita baada ya kuona hata huko nyuma anapoelekea hao fisi wapo.

   Maria alibaki alitetemeka huku akiwaangalia fisi wale kwa hofu kubwa sana kwa jinsi wanavyomsogelea, fisi waliamua kuinua macho yao yaliyokuwa mekundu na ya kutisha kisha kwa pamoja wakaanza kumsogelea Maria kwa kasi ya ajabu sana huku wakiwa wamefungua vinywa vyao vilivyojaa meno marefu mithili ya meno ya Ngiri. Fisi hao walizidi kumtisha ambapo muda huo wote kwa pamoja walijirusha juu huku wakitanguliza vinywa vyao vilivyosheheni meno kumuelekea  Maria tena huku wakitoa mingurumo ya hasira sana.

"Mamaa! Nakufaaaa!" Maria alipiga makelele kwa nguvu akiwa amefumba macho akahisi akishikwa mabegani mwake na hapo alizidi kupiga kelele kwa woga huku akifurukuta.

"Maria hebu tulia mdogo wangu, Frank kamuite Dokta" Aliisikia sauti ya kaka yake ambayo ilimfanya aache kufurukuta akafumbua macho akiwa anahema kwa nguvu, aliangaza macho akajikuta yupo katika eneo jingine tofauti na alilokuwepo awali. Alipozidi kushangaa eneo hilo tofauti na lile eneo la kutisha alilokuwepo kichwa kilimuuma, alijishika kichwa chake kutokana na maumivu kumzidi kiwango. Kichwa hicho kilipoacha kuuma kumbukumbu yote ya tukio lililopita ilipotea ghafla na akawa anashangaa eneo hilo lenye rangi nyeupe ambalo alikuwa yupo muda huo, aligeuza shingo akishangaa akiwa haelewi yupo eneo gani kwa muda huo kutokana na kuchanganyikiwa.

NI  BINTI WA FAMILI YA UWEZO WA JUU ANAINGIA KWENYE MAJARIBU AMBAYO HAKUWA KUINGIA KWENYE MAISHA YAKE, YOTE KUTOKANA NA ASILI YA NASABA YAKE. UKAWA MWANZO WA KUHITAJIKA NA SHETANI KWA HALI NA MALI. HUO NI MWANZO WAKE


RIWAYA HII UTAIPA  KWA BEI NAFUU KWENYE EMAIL YAKO, WHATSAPP NA HATA FAEBBOK KAMA UKIHITAJI. CHA KUFANYA UNACHOHITAJIKA NIKUFANYA MALIPO KWA NJIA YA TIGOPESA, MPESA AU BENKI YA POSTA. UKIHITAJI GROUP LA SIRI LA WHATSAPP LA HII RIWAYA PIA UTALIPATA KWA 5000 KWA MWEZI AU 6000 KWA MWEZI INBOX


NAMBA ZA MALIPO NI;
O713776843(TIGOPESA) HASSANI MAMBOSASA

0762219759(MPESA)     HASSAN O MAMBOPSASA



00700013656(BENKI YA POSTA TANZANIA /TPB) HASSANI OMARI MAMBOSASA



MUHIMU: UKISHALIPA TAFADHALI TUMA UJUMBE WA MUAMALA KWENDA WHATSAPP NAMBA 0713776843 AU FACEBOOK KWENYE PAGE YETU YA RIWAYA MARIDHAWA.
PIA USEME UTUMIWE RIWAYA KWA NJIA GANI KATI ZILIZOAINISHWA HAPO JUU




KARIBUNI NDANI  YA MARIDHWA JUMBA LA RIWAYA


No comments:

Post a Comment