Tuesday, June 21, 2016

SHUJAA SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE

RIWAYA: SHUJAA


MTUNZI: Hassan O Mambosasa

SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE




SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE!!
Alibiringita hadi pembeni ya ukuta wa nyumba kisha akatulia gizani kwa nusu dakika akiangalia mazingira yalivyo, aliporidhika pako kimya akasogea taratibu ulipo mlango  wa kuingilia ndani kisha akanyonga kitasa cha mlango huo taratibu lakini ulionekana umefungwa kwa ndani. Mlango huo ulionekana ulikuwa umefungwa kwa ndani na ikamlazimu atumie ufunguo malaya kufungulia mlango huo kisha akaingia ndani baada ya mlango kufunguka, aliufunga vile kisha akaanza kutembea taratibu kwani ndani kulikuwa na giza kutokana na taa kuzimwa.


Norbert alipopiga hatua tano tu tangu alisikia sauti ikimuambia"karibu sana"  kisha akapigwa na kitu kigumu kisogoni hadi akapoteza fahamu hapohapo.

****

Alikuja kuzinduka baada ya kusikia sauti za milio ya ndege ikisikika katika eneo alilokuwepo na mwanga mkali ukawa unapita katika macho yake, alipofumbua macho alianza kuhisi maumivu sehemu ya kidogoni pia mikono yake alihisi imefungwa kwa nyuma kwa kamba ngumu sana. Alipoangaza maeneo ya karibu na pale alipo aliona ni eneo lenye uzio mrefu kuliko kawaida, upande mwingine wa lile eneo alimuona Brian akiwa amesimama na Jameson wakiwa wapo na  vijana wapatao sita wakiwa na silaha nzito mikononi mwao. Alipoangalia upande mwingine hakuona kitu chochote cha muhimu zaid ya jengo lililopo mita kadhaa kutoka pale alipo, aliyarudisha macho yake kwa Brian na Jameson ambao walikuwa wanatabasamu tu.

"ohoo! Norbert Kaila karibu katika mlango wa kuelekea kuzimu" Brian aliongea kwa dharau sana huku akimtazama Norbert pale alipo, Norbert aliposikia maneno yake ya kebehi alikaa kimya hakuongea chochote.

"nadhani umekutana na kiumbe mwenye  uwezo zaidi yako na hutotoka hai katika mkono wangu hata iweje jua upo katika mlango wa kuzimu" Brian aliongea kwa dharau kisha akamsogelea Norbert hadi karibu yake, alipomfikia alimshika kidevu halafu akamuinua  akawa anatazana naye kisha akamuambia "nataka ufe kifo cha kikatili kuliko hata uliyowaua vijana wangu". Norbert alipoambiwa hivyo hakuongea kitu aliishia kumtemea mate usoni Brian  akijaribu kurusha kichwa ili ampige puani lakini hakikumfikia Brian.

"nadhani humjui Brian Mcdonald vizuri" Brian aliongea kisha akaanza kumshushia kipigo kizito Norbert hadi nguvu zikamuishia ingawa bado aliendelea kuleta kiburi akiwa anavuja damu. Brian alimshika  shingo Norbert akawa anatazamana naye uso kwa uso halafu akamwambia, "nadhani umeshamjua Brian ni nani".

"mi nimemjua Brown Stockman gaidi anayetafutwa na dunia aliyevaa sura ya bandia akajiita Brian Mcdonald" Norbert aliongea hayo maneno huku akiugulia maumivu kutokana na kipigo kizito alichoachiwa halafu akamtemea mate usoni kwa mara nyingine. Brian alimpiga pigo la   kwenye utosi Norbert hadi akazirai tena kwa mara ya pili kisha akawaambia vijana wake, "mtupeni kwenye chumba cha mateka huyu hatakiwi kutoka mzima na wala kuuawa na mtu yoyote anatakiwa auliwe na mimi mwenyewe nikiwa nishajua kila kitu kuhusu yeye. Haiwezekani awe anajua mambo yangu ya siri kirahisi tu, Interpol wameshindwa kunijua yeye ndiyo anijue". Aliondoka akiwa pamoja na Jameson akiwachaa vijana wake wakimfungua Norbert ili wakamfunge katika chumba walichoambiwa.

****

   Norbert alifungwa kwenye chumba chenye mlango mgumu na imara ambao hauwezi kufunguliwa na binadamu wa kawaida hata mwenye nguvu gani, ilimchukua nusu saa kuja kurudiwa na fahamu na kujikuta yupo kwenye mazingira tofauti na aliyofungwa awali. Muda huo njaa ilianza kumsulubu kutokana na kutopata chakula kwa masaa kadhaa uchovu uliotokana na kipigo kizito alichopewa na Brian, yalipita masaa kadhaa tangu arudiwe na fahamu ndipo mlango ukafunguliwa na mmoja wa vijana wa Brian. Norbert alimshukuru mungu baada ya mlango huo kufunguliwa na hapo ndipo akajiona ameangukiwa na nyota ya jaa na aitumie ifuatavyo ili aokoke katika nyumba hiyo ambayo hakujua ipo upande gani wa Tanzania wala hakujua kama ipo nje ya Tanzania. Kijana wa Brian aliyefungua mlango alipoingia Norbert alijifanya bado hsjarudiwa na fahamu na hata yule kijana alipompiga teke ili amuamshe aliendelea kulala hivyohivyo kama vile hajitambui ingawa alipata maumivu kutokana na teke alilopigwa.

"Oya Oscar hebu njoo fasta huyu mbuzi nahisi kavuta maana hata kupumua sidhani kama anapumua" Yule kijana wa Brian aliyefungua mlango alimuita mwenzake aliyekuwa yupo nje ya chumba huku akitazama upumuaji wa Norbert, mwenzake naye aliingia baada ya kusikia wito huo.
"Una uhakika kavuta kweli sio tumtoe halafu mtu bado yupo hai, halafu unajua don katuonya juu ya huyo jamaa kasema ni mtu hatari sana" Oscar aliongea akimsogelea mwenzake aliyekuwa yupo karibu na Norbert.

"Mmh! Anapumua kwa mbali sema anaweza kutufia huyu au una.." Yule kijana alishindwa kumalizia kauli yske baada ya pigo kali liitwalo nukite ambalo hutumia vidole kutua katika koo lake na kuufanya mwili na roho yake vitengane hapohapo, Oscar naye akiwa bado hata hajapata mbinu ya kuitumia alijikuta akichotwa mtama na Norbert uliompeleka hadi chini kisha miguu ya Norbert ikamkaba kwenye koo lake kwa nguvu hadi alipoiaga dunia ndiyo aliachiwa.
 
   Baada ya kuwamaliza wote wawili Norbert aliwapekua akachukua bastola zao mbili kisha akachungulia nje huku bastola zote zikiwa mikononi mwake tayari kwa lolote litakalo mkabili mbele yake, macho yake yalikutana na korido  ya wastani baada ya kuchungulia ambayo ilikuwa tupu kabisa. Aliamua kuifuata korido ile kwa mwendo wa tahadhari hadi mwisho wake ambapo kulikuwa kuna ukumbi mdogo, alichungulia ndani ya ukumbi huo kwa makini akaona hakukuwa na dalili ya kuwepo mtu zaidi ya kuwepo kwa vifaa mbaliimbali vinavyotumika katika silaha. Kulikuwa kuna vibebea risasi, maboksi kadhaa ya risasi na viwambo vya kuzuia sauti vikiwa mezani, Norbert alichukua viwambo vya sauti vilivyopo mezani akavifunga kwenye bastola alizozichukua  kisha akatembea kwa mwendo wa tahadhari. Alitoka hadi nje ya jengo alilokuwepo ambalo lilikuwa kimya sana ingawa kimya hicho hakikuwa sababu ya Norbert kutoka kama mbuzi anayetoka zizini. Aliamua kujibanza na kuchungulia kila pande za jengo hilo ili kuona ulinzi uliokuwepo kwenye jengo hilo, lilikuwa ni jengo lenye ulinzi mkali na wa kimya kwani walinzi wake walikuwa makini kuliko kawaida. Norbert alipiga hesabu za kuwakabili walinzi hao ambapo katika hesabu zake aliona ni afadhali awavamie wa upande wa kulia waliokuwa wachache kuliko kwenda upande wa kushoto kwenye walinzi wengi wakati alikuwa ana bastola mbili katika kila mkono na zilihitajika kufanya kazi kwa pamoja. Aliamua kusogea hadi kwenye kona ya upande wa kushoto kisha akajibiringisha kuuvamia upande wa kushoto kwa ghafla ili kuwapa kiwewe walinzi hao, alifyatua risasi katika bastola zote akiwa anajibiringisha ambazo ziliwapata walinzi wote wakaenda chini bila hata kufyatua risasi zao. Alipohakikisha upande huo hajabaki mlinzi hata mmoja aliamua kuwasogelea akachukua vibeba risasi katika mifuko yao pamoja na visu, alipomaliza aliusogelea ukuta ambao umejengwa kama uzio kuzunguka jengo hilo akaupanda kwa taratibu hadi alipofika juu ndipo alipojikuta akiibua kizazaa kingine bila hata kujijua. Upande alioupanda ulikuwa na kamera ya ulinzi ambayo ni ya kujiendesha yenyewe ambayo imeunganishwa na kengele ya hatari iliyopo hapo ngsni ya jengo na ikimuona mtu asiyehusika na eneo hilo lazima ipige kengele ya hatari, kamera hiyo ilimuona Norbert na hapo ndipo kengele ya hatari ikawa inasikika ingawa aliwahi kuruka akatua nje katika pori asilolijua.
 
"katoroka huyo kila mtu achukue pikipiki arudishwe hapa, snipers pandeni juu ya minara mumtafute na mumtungue miguu huyu kabla hajafika mbali" Ilisikika sauti inayokwaruza ikipiga kelele ndani ya uzio wa jengo hili na milio ya pikipiki ikafuatia, muda huo Norbert alikuwa yupo mbio sana na alikuwa akijichanganya kwenye miti minene ya pori ambalo hakulijua lipo wapi. Alikimbia sana ingawa nyuma yske alisikia vishindo vya watu wakija pamoja na milio ya pikipiki ikisikika katika sehemu  ambayo barabara ilikuwepo, Norbert alizidi kukimbia sana katika pori hilo ambalo hakujua mwisho wako ni upi. Baada ya muda alihisi kuchoka kutokana na njaa aliyokuwa nayo kwani hakuwa amekula kitu, aliona akiendelea na mbio angekuja azirai njiani na hawa maadui zake wamuokote kama mzoga wamrudishe kule alipotoka aje kufa kama kuku akiwa bado anategemewa kwakuwa yeye ndiyo mpelelezi aliyepewa kazi ya kumnasa gaidi Brown Stockman. Hakutaka kukamatwa na hakutaka kukimbia tena kwa kuhofia hali yake na njaa aliyokuwa nayo atakuwa amejimaliza mwenyewe, aliamua kusimama kisha akazichomeka bastola sehemu ya kiunoni halafu akatoa visu alivyovipata kama ngawira.

"inabidi nitumie mafunzo ya hali ya juu ya uninja niliyojifunza kabla sijapewa kazi hii ya ujasusi" Norbert alijisemea kisha akapanda juu ya mti haraka kama nyani, alipofika juu alivunja sehemu ndogo ya matawi  ya miti akaichonga upande mmoja yakawa na nchi kali. Yalikuwa na ukubwa kama magongo ya ufagio wa chelewa wa kufagia nje, yalikuwa ni magongo madogo mawili yenye urefu kama mkuki ambayo aliyatengeneza Norbert kwa kutumia kisu.

"ama zangu ama zao" Norbert alisema huku akiuma meno yake kwa hasira akiwasubiri maadui zake juu ya mti katika matawi yaliyojificha, baada ya muda mfupi tangu apande juu ya mti alisikikia vishindo vya watu wakija kwa kasi na hatimaye akawaona wabaya wake wakiwa tayari wamefika pale chini ya mti alioukwea. Walikuwa wapo watano na walipofika pale chini ya mti wakasimama sehemu yenye majani mengi makavu, mmoja wao aliinama akaangalia sehemu ya njia ambayo ilijaa majani ya miti makavu yaliyoanguka.

" ni unyayo wake huu" Aliongea yule aliyekuwa anaangalia sehemu ile ya njia yenye ambapo kulikuwa kuna alama ya unyayo iliyobaki kwenye majani makavu kisha  haikuendelea mbele, yule mtu alipomaliza kuangslia ule unyayo aliinuka akawaambia wenzake " hayupo mbali na hapa huyu, wawili wapite kulia wawili kushoto peke yangu nitaangalia mazingira ya hapa karibu".
 
    Wakati anatoa maelezo hayo kwa wenzake alifanya kosa kutoangalia juu ya mti ambapo ndipo wanayemtafuta yupo, uzembe huo ndiyo ulikuwa ushindi mkubwa kwa Norbert kwani alijiachia kutoka juu ya mti huku akiwa na yale magongo madogo marefu aliyoyachonga. Alipotua chini tayari magongo aliyachoma kwenye shingo za wawili kati yao kisha akapiga sarakasi baada ya mwingine kufyatua risasi ambayo ilimkosa, alipotua chini kwa sarakasi ya kininja aliyopiga ile risasi tayari ilimpata mwingine aliyekuwa  yupo karibu yake. Wawili waliobaki aliwarushia yale magongo kama mkuki yakawatoboa nae wakaenda chini ingawa hawakufa , aliwafuata akawamaliza kwa kuwakanyaga shingoni kila mmoja kisha akakaa chini ya mti akawa anahema.

   Baada ya muda mfupi alinyanyuka kisha akaanza kukimbia kuelekea mbele akiwa anapita msitu hadi msitu, alikuja kusimama kwenye chemchem ya maji akanywa maji katika msitu huo, njaa ilipomzidi aliamua kula matunda ya porini hadi ilipomuisha kisha akaendelea kukimbia hakutaka kusimama hata kidogo. Baada ya nusu saa toka akimbie alitokea katika batabara ya Lami ambayo hakujua ipo wapi alipotaka kuvuka barabara hiyo alisikia mlio wa pikipiki aina ya Bajah ukitokea upande wa nyuma yake, Norbert aliamua kuchukua tahadhari na alijitupa pembeni sehemu yenye majani mengi kisha akasubiri hadi pikipiki hiyo ilipotokea. Pikiki hiyo ilikuwa unaendeshwa na mtu mwenye mwili mkubwa sana aliyebeba bunduki aina ya SMG mgongoni, Norbert akipomuona huyo mtu alitambua fika  kama ni mmojawapo wa vijana wa  Brian aliyekuwa anamtafuta. Yule mtu alipofika jirani na barabara alisimamisha pikipiki akawa anatazama pande zote ili aingie barabarani, Norbert aliitumia nafasi hiyo kumrukia na akamchoma kisu shingoni kisha akambana wakati anahangaika kukata roho hadi alipotulia ndiyo akamuachia. Alimpekua yule mtu akamkuta na kitita cha pesa katika mfuko wa koti akakichukua, alichukua simu yake ndogo ya kichina akatoa kadi ya simu akaitupa kisha  akaweka mfukoni. Alimsukuma kwenye majani yule mtu kisha akaisimamisha pikipiki yake ambayo bado ilikuwa inawaka, aliipanda akaingiza barabarani akatoweka eneo hilo.


****

  Kuanzia asubuhi ya siku iliyofuata hadi jioni inaingia Moses alikuwa anawasiliana na mpenzi wake tu huku akiwa hapokei simu za Annie wala kujibu ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwake, alikuwa ana kazi ya kuwasiliana na Beatrice tu na hakutaka kusikia habari za mwanamke asiyempenda mwenye ung'ang'anizi kama ruba. Majira ya saa tano baada ya kumaliza kujisomea aliamua kuchukua simu na akaendelea kuwasiliana na mpenzi wake kutokana na hamu aliyokuwa nayo na ya kumuona kipenzi cha moyo wake kwani siku chache ambazo hakuonana naye zilitosha kumfanya ataabike walau kuiona sura ya mpenzi wake, mawasiliano ya simu kati yake na Beatrice yalikuja kukoma baada ya muda kwenda sana na ikamlazimu alale.

  Asubuhi  ya siku iliyofuata aliamka akafanya mazoezi kama kawaida yake kisha akasafisha kinywa chake pamoja na mwili wake, alipata kifungua kinywa kisha akashika kitabu kwani alibakisha muda mfupi sana katika kipindi chake cha kidato cha sita. Hadi inafika saa sita alikuwa ameshamaliza kusoma na akawa anatumia simu yake kuperuzi mtandaoni, ilikuwa ni kawaida yake kila apatapo muda wa kupumzika ambao yeye huutumia kuperuzi mtandaoni au kulala.

   Muda huo wote alikuwa amekaa sebuleni kwenye kochi la kisasa akiwa kajilaza na mkononi ana simu yake, alikuwa kapachika spika za masikioni akisikiliza muziki mtandaoni  huku akiperuzi mambo mengine. Hakuweza kusikia ugeni wowote uliomjia kwa muda huo kutokana na kunogewa na muziki, alikuja kutambua kama mgeni baada ya spika aliyoiweka sikioni la kushoto kuvutwa.  Alikereka na uvutaji wa spika ya masikioni aliyoivaa na alipomuangalia mtu aliyefanya hivyo ndiyo akajikuta akikereka zaidi baada ya kumuona mtu ambaye ni kero hata kuitazama sura yake, alikuwa ni Amkie aliyefanya hivyo akiwa anaonekana amekasirika sana. Moses alimuangalia tu kisha akavaa tena spika ya masikioni kama vile hatambui uwepo wake hapo, Annie alipoona dharau  hiyo alizivuta spika hizo kwa nguvu hadi nusura aangushe simu ya Moses.

"unajifanya hunioni sio?!" Annie aliuliza kwa ukali, lakini Moses hakujibu chochote  aliishia kumtazama kwa kebehi.

"si naongea na wewe?" Annie alimuambia kwa ukali.

"hapa upo kwangu jeuri sitaki sema shida yako usepe na kama huna cha kuongea cha maana kilichokufanya unyanyue mguu wako kutoka huko ulipotoka hadi ukaja hapa ni bora uutumie mlango uliingia nao kutoka" Moses aliongea kwa dharau huku akiachia tabasamu lillozidi kumuudhi Annie

"unajifanya mjanja siyo? Sasa utanijua mimi ni nani?" Annie aliongea kwa shari zaidi.

"hata haina haja kukujua wewe  zaidi tayari nishakutambua kama ni malaya unayetaka kugawa kwa lazima" Moses alizidi kuongea kwa dharau.

"sasa huyo Beatrice wako unayemringia mimi naenda kuchafua kabisa si unakumbuka picha zako" Annie aliongea huku akimuwekea vitisho Moses.

"sio uchafue sema tuchafuane tuone nani zaidi, si mtoto wa waziri wewe sasa kaanze mi nimalizie" Moses aliongea huku akitabasamu kwa dharau.

"unasemaje wewe?!" Annie aliuliza kwa ukali, Moses badala ya kujibu swali la Annie aliamua kusimama halafu akatoa flash ya tarakilishi mfukoni akaichomeka nyuma ya luninga ya kioo bapa kubwa iliyofungwa ukutani sebeleni hapo. Aliiwasha luninga kisha akachukua kiongozi cha luninga(remote) akabonyeza sehemu ya kuonesha mafaili yaliyopo ndani ya flash, aliufungua mkanda wa video alioutengeneza Hilary akauacha ukiwa unaonekana halafu akasema "unataka kujua mimi nasemaje sasa mimi nasema hivyo".
Annie alipoona kile alichoekewa na Moses alijikuta anakaa chini kwenye zulia la sebuleni hapo bila kujitambua, alibaki akiwa anakodolea luninga huku akiwa haamini kwa kile alichokiona.

"vipi hizi sofa za hapa sebuleni ni invisible kwa macho yako nini mpaka ukae kwenye zulia?" Moses alimuuliza Annie kwa dharau, Annie alijikuta akitembea kwa magoti kumfuata Moses alipo huku uso wake ukiwa na hofu.

"dada siku hizi miguu yako haifanyi kazi mpaka utumie magoti" Moses alizidi kumuandama Annie kwa maneno ya kumchanganya.



ITAENDELEA!!


MWENYE KUIHITAJIA RIWAYA HII HADI MWISHO ANAWEZA KUWASILIANA NA MTUNZI KUPITIA NAMBA ZAKE HAPO JUU KWA NJIA YA UJUMBE MFUPI TU WA MANENO NA SI KUPIGA. HUKO UTAIPATA YOTE.



KWA RIWAYA ZAIDI LIKE UKURASA WETU WA FACEBOOK AMBAO NI:




      Riwaya Maridhawa
       Riwaya Maridhawa
      Riwaya Maridhawa
       Riwaya Maridhawa
        Riwaya Maridhawa

No comments:

Post a Comment