Monday, August 14, 2017

TENDAGURU SEHEMU YA TATU



RIWAYA: TENDAGURU
NA: HASSAN O MAMBOSASA
MAHALI: TANZANIA NA MAREKANI



<><><>SEHEMU YA TATU<><><>


"Nasa screenshot yake pamoja na ya gari lake hilo halafu play mwingine" Amri nyingine ilitoka na kijana alifanya kama alivyoagizwa, mkanda wa siku nyingine uliwekwa na mtu akiwa ni yuleyule anayemuona anakuja kupokea wageni uwanjani hapo.

"Piga screenshot kila mkanda wa siku ambazo anafika huyu mtu" Aliweka agizo jingine.




_____________TIRIRIKA NAYO
       Ilichukua kitambo kirefu kiasi cha muda kuweza kukamilisha kile killimchomleta hapo, alitazama  mikanda yote kwa umakini mkubwa hadi akamaliza na kuweza kuibuka na kitu muhimu kwa ajili ya kazi yake hiyo. Vitu vyote alivyoagiza vichukuliwe yeye aliviweka kwenye simu yake ya mkononi  ya kisasa, alitumia waya maalum kuvirusha vyote. Baada ya kumaliza hilo alimshukuru sana kijana aliyemfanyia huduma yote aliyokuwa akiihitaji na kisha alitoka humo ndani na kurejea kule ofisini kwa mwenyeji  wake. Alitoa  shukrani zote kwa kuweza kutimiziwa kazi hiyo  na  Mputa, alibadilishana naye machache baada ya kukamilisha kila kitu chake  na kisha alinyanyuka kitini na kuaga. Kutokana na ukaribu wao  uliyotokana na utambulisho wa siri ambao wanao kila mmoja, walisindikizana hadi eneo la mapokezi ambapo kulikuwa na wale wasichana wa awali  alipofikia kwenye dawati lao. Hata wale ambao mwanzo walimkalia kimya walimpa tabasamu alipofika hapo akiwa yupo na mtu wake  wa karibu, Missinzo kwa kujaliwa ucheshi pamoja  na sura iliyojaa bashasha ilitosha wazi kuwateka akili zao  kwa muda mfupi aliyosimama hapo kuongea nao. Hata alipoondoka walitamani haswa aendelee kubakia hapo lakini kutokana na huyu kuwa ni   mtu wa kazi, na awapo kazini haendekezi kitu kingine chochote.Ilikuwa ngumu kubaki hapo  kwenye eneo la kutafutia ugali kwa watu wengine, aliagana na kusindikizwa na rafiki yake hadi nje kabisa ya uwanja kwenye maegesho ya magari.

"Sasa Missinzo mimi ninaishia hapa si unajua bado nipo kibaruani" Mputa alisema.

"Kibaruani kwa maigizo siyo" Missinzo alimwambia.

"Sasa ndiyo kunapotuweka mjini unafikiri tutafanyaje sasa"

"Haya wewe kaendelee na kazi hiyo mimi ninaingia kwenye mchakamchaka wa siku mpya"

"Haina shida"

     Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maongezi yao kwa siku hiyo na kila mmoja alishika njia yake, Mputa alirudi ofisini na Missinzo aliingia garini na kuondoka eneo hilo akiwa  amenyaka vichache. Safari yake kutokana na kutokuwa na  la kuendelea baada ya kufikia hapo. Ilimbidi arejee kule nyumbani kwake kuweza kupitia kile ambacho amefanikiwa kukipata kwa siku hiyo, mwendo ulikuwa ni uleule wa kupita njia za mkato na hatimaye alifika nyumbani. Aliegesha gari mahali stahiki kisha akaingia ndani ya nyumba, alilakiwa na utupu wa nyumba hiyo kutokana na kutengana na mwandani wake ambaye walifunga pingu za maisha miaka kadhaa iliyopita.

        Ni mwaka sasa umepita tangu aanze kuishi maisha ya upweke baada ya kushindwana kiutuzima na yule aliyemfanya akalipe pesa nyingi ili amuweke ndani, hali hiyo hapo awali ilimtesa akiiona ni adhabu kutokana na kuzoea kulala naye kitanda kimoja kwa miaka takribani miwili. Lakini baadaye aliizoea na alielekeza nguvu zake  zote kwenye kufanya kazi,  ndiyo maana imemsaidia aweze kumudu walau kuishi namna hiyo bila ya mwenza kwenye nyumba yake kubwa aliyoijenga kwa jitihada zake mwenyewe. Si kwamba aliamua kujitoa kabisa kwenye suala la mapenzi  kabisa na kuwa mbali na hitaji tofauti, bado alibakia na kuwa Muonjaji asali tu na si Mchonga mzinga. Hayo ndiyo maisha mapya aliyoyazoea tangu awepo peke yake, kwake ni kawaida haswa hadi kufikia jira hilo.

      Missinzo alijibwaga kwenye kochi imara lililoweza kumudu uzito wake  pasipo kutoa walakini wowote, alilala kwenye kochi hilo pasipo kutoa viatu na akatoa simu yake ya mkononi ambayo aliipitia  kwenye vile vitu muhimu alivyokuwa amevipata alipoanzia. Kupitisha macho pamoja na kuipa kazi mpya tafakuri, kulimfanya hata ainuke hapo kochini na kuingia chumbani kwake moja kwa moja. Alihisi kitu ambacho alikihitaji zaidi  kwa  wakati huo kilikuwepo huko, hicho ndiyo kingeweza kuwa msaada kwake.


****


           JIJINI WASHINGTON DC, MAREKANI

       Wakati kukiwa ni saa kumi jioni nchini Tanzania nchini Marekani kwenye jiji la Washington Dc kulikuwa ni  saaa tatu asubuhi. Tofauti ya hii nchi na Tanzania ilikuwa inapishana masaa saba, daima barani huko ndiyo wapo nyuma kimasaa na huku barani Afrika kwenye nchi ya ukanda wa mashariki ilikuwa  mbele. Asubuhi hii kwa huku kipindi cha baridi kabisa  ambapo wakazi wengi huvaa nguo  za kujikinga  na baridi, alionekana kijana mmoja aliyekuwa na  asili ya barani Afrika akiwa anatoka kwenye lango la kuingilia kwenye hoteli ya nyota tano ya Hay Adams. Huyu alivaa suti nadhifu  ya rangi nyeusi , juu alivaa koti jingine jeusi ambalo lilifanana kila kitu na  na muundo wa  suti. Nguo hii ya nje aliiweka mahususi kwa kujikinga na baridi, mabegani alibeba mkoba mdogo.

        Aliongozana na  binti  mwenye asili ya kizungu huku wakitembea kwa pamoja wakiwa wameshikana mikono, walipofika eneo la  la mbele la hoteli hiyo. Kijana huyo alipiga mbinja moja matata    na kupelekea teksi  zenye wajibu wa kuchukua abiria ndani ya jiji hilo kusogea mita  kadhaa mbele yao. Walijitoma ndani ya gari wote kwa pamoja akitangulia binti wa kizungu na kisha akafuata yeye, mlango ulipofungwa safari ilianza kwa gari hiyo kuondoka hotelini hapo. Ilipita mitaa kadhaa na hatimaye ilikuja kusimama mahali ambapo kuna ghorofa refu ambalo hupangishwa wakazi, gari hiyo iliegeshwe pembeni ya barabaraba na kisha wote wawili walishuka. Kijana alitoa ishara  kwa dereva na kisha akajongea hadi lilipo lango la kuingilia ndani ya ghorofa hilo,  hapo alimuaga binti huyo kwa busu motomoto na kisha alirejea tena kwenye gari na kuondoka eneo hilo.

      Aliyekuwa amekaa nyuma ya usukani alijua kucheza na wajibu wake vilivyo kwa jinsi alivyokuwa akienda sambamba na amri za Mteja wake, yote ni kutokana na kutaka haswa bakshishi kutoka kwa Mtu aliyembeba aweze kusogeza siku zake za kuishi ndani ya jiji hio. Muda huu safari  yao ilikuja kuishia kwenye mtaa wa West End jirani kabisa na ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, hapo huyo kijana alishuka na kisha akalipa  malipo stahiki kwa Dereva. Alipoiacha  gari hiyo alitoa kitu cha plastiki akakibana kwenye koti la suti la ndani, kitu hiko hakikuwa kingine ila ni kitambulisho  chenye kumpa  utambulisho  wake awapo eneo hilo. Hapo alikaza mwendo kulisogelea lango la ubalozi wa Tanzania, walinzi waliyokuwa wapo langoni wakiwa a vifaa maalum wala hakuonesha kuwa na shka juu yao. Alipita langoni  kulipokuwa na ulinzi siku hiyo pamoja na idadi  ya watu tofauti na siku zingine pale alipomaliza kukaguliwa, akiwa hapo na kitambulisho chake muhimu alifungua begi lake na kutoa kamera. Alianza kupiga picha mahali hapo huku akiiingia ndani, kimuonekano alikuwa ni mwandishi wa habari aliyepo kazini, hilo halikuwa na shaka ni yupo wajibuni na hawezi kupingika.

         Aliingia ndani akiwa na dhima hiyohiyo hadi chumba maalum ambacho kilikuwa kimeandaliwa vilivyo ndani ya jengo hilo, alikutana na baadhi ya wanahabari wakiwa wamewasili humo ndani lakini bado hafla iliyokuwa ikifanyika humo haikuwa na dalili za kuanza. Alichukua eneo  lake aliloona lingemfaa kupiga picha na kisha akaweka kituo hapo, ilichukua takribani nusu saa ndani ya eneo hilo hadi pale wageni mbalimbali wakianza kuingia humo ndani. Ulinzi uliimarishwa haswa na ikiwemo wanausalama kutoka ikulu ya Marekani, hii ilionesha wazi kuna ujio wa kiongozi mkubwa ndani ya nchi hiyo hapo Ubalozini.

      Muda mfupi baadaye waliingia walinzi waliyokuwa wamevaa suti lakini hazikuwa zimefanana kabisa na zile za wanausalama wa FBI waliyoingia humo ndani.Hawa walipanga kwenye eneo lao la kazi. Baadaye kidogo watu waliyopo ndani ya  ukumbi huo mdogo walisimama  baada ya kumuona Rais wa Marekani akiwa ameongozana na Rais Zuber Ameir kutoka nchini Tanzania pamoja na balozi wa Tanzania nchini humo. Walipooanza kuingia watu hao kijana huyo alichangamka haswa kwa kufanya kazi yake ya kupiga picha, alitoa hata kitabu kidogo akawa ananakili matukio muhimu yaliyoandaliwa siku hiyo. Aliendelea na wajibu wake hadi Kiongozi mgeni na Kiongozi mwenyeji walipoongea machache na wageni maalum waliyopo nchini humo.

      Baada ya shughuli hiyo kuisha tayari ilikuwa ni saa sita mchana wageni walianza kutawanyika mmoja baada ya mwingine, Mwanahabari huyu alipotaka kuondoka tu hapo ubalozini kwakuwa hakuwa na la kumuweka zaidi.  Alijikuta akishindwa kuondoka  baada ya Rais wa Jmhuri wa Muungano wa Tanzania kumtia machoni akiwa kibaruani,  alikijindaa kutoka alipokea ujumbe wa kuhitajika ndani na mmoja wa vijana wa kazi kutoka nchini Tanzania. Hakuwa na  la kupinga zaidi ya kukubali tu kuonogozana na Mlinzi huyo hadi kwenye chumba maalum, huko alikutana na Rais Zubeir akiwa amekaa kwenye kiti kilichopo mkabala na upande aliyoingia ndani ya chumba hicho. Alisimamiwa na wanausalama wawili kwa upande wa kulia na upande wa kushoto, kitendo cha kuonekana mbele ya kiongozi wake alipokewa na tabasamua pana sana ambalo lilimpa kabisa amani ya wito wake eneo hilo.

"Norbert Kaila" Rais Zuber aliita.

"Mheshimiwa" Norbert Kaila ambaye ndiye mwanahabari mwenyewe aliitika.

"Nafurahi sana kukuona huku kijana  shupavu na Mzalendo mwenye sifa bila ya kujulikana sura"

"Nafurahi pia Mheshimiwa uwepo wako huku"

"Norbert ukiwa kama mwanahabari na upo huku kwenye kusaka habari, unaonaje kama ukiongozana na mimi kwenye ziara yangu nchini humu"

"Mheshimiwa ni jambo zuri sana kwani huniongezea habari na kunipa ugali, lakini kiupande mwingine ni hatari kwangu mimi na kwako"

"Kwanini?"

"Unatambua wazi kazi ninayoifanya  ya kufichua maovu nchini, hivi ikitokea wabaya ninawahabaribia habari zao wakaniona kwenye msafara wako ilihali sihusiki. Unafikiri watanipa jicho gani la umakini. Mwanzo wa kuishi kihatari ndiyo huu, hivyo Mheshimiwa sipo tayari kwa hilo tu nahitaji niwekewe macho ya kawaida tu ili niweze kufanya kazi  zangu kwa ufanisi"

"Hakuna shida kijana wangu uliyeniweka kwenye usalama, kila la heri na wajibu wako nafikiri tutaonana tena kwa mara nyingine kwenye siku ambayo nitaondoka hapa nchini. Ufike hapa ubalozini upatiwe Mwaliko na uongozane na vijana ufike pale White house kwenye hafla ya kuniaga nirejee Tanzania"

 "Hakuna shida Mheshimiwa"

"Unaweza kuendelea na harakati zako jijini humu watanzania wapate habari za huku kupitia wewe"

"Nashukuru Mheshimiwa"

     Walipeana mikono kwa pamoja na kisha Norbert alitoka humo akiwa ameongozana  na kijana ambaye aliingia naye, aliongozana naye hadi mahali jirani na mlango wa kutokea nje. Yule Mlinzi alirejea ndani na kisha   Mzee wa kazi alitoka nje ya lango mwenyewe akiwa na vitendea kazi vyote, alijongea akikatiza mitaa hiyo kwani akili yake haikumtuma kabisa kuweza kuchukua gari muda huo. Safari yake kupita mitaa ilikuja kuishia kwenye Mgahawa uliyopo kona kadhaa za mitaa kutoka ulipo Ubalozi, hapo aliketi na kuagiza  chakula cha mchana kwani tayari wasaa wake ulifika. Akivuta subira kwenye  kuagiza chakula hicho, alitumia kugeuza macho kila pande kwani haikuwa kawaida yake kukaa bila ya kuyajua mazingira aliyopo yapo vipi. Alipohakikisha usalama upo alipeleka macho kwenye luninga ya Mgahawani hapo, aliweka macho hapo hadi pale chakula kilipofika. Kuwasili kile akitakacho aliondoa macho na kuweka eneo stahiki huku akaanza mashambulizi hadi pale sahani ilipobaki tupu, hapo alinyanyuka na kulipa kisha akatoka nje kwani hakuwa na haja ya kunawa kutokana na kutumia vifaa vya kushikia. Alipofika mlangoni mwa Mgahawa baada ya kuufungua alikutana na binti mrembo sana ambaye alioenekana wazi ni mwenye haiba, Norbert alijikuta akiacha mdomo wazi akitazama binti huyo aliyekuwa akitaka kuingia humo ndani. Mlango alishaziba njia kabisa kwa kutotaka kabisa binti huyo ampite hivi, Bibie alibaki akimtazama tu na hapo akapewa tabasamu la mauaji.
"Hellow! Angel of the Earth" Norbert alitamka.


****


        Wakati bwana  afya  wa maungo akiwa amekutana na  Mrembo mlangoni, nchini Tanzania Missinzo  alikuwa bado hajatoka chumbani kwake na alikuwa yupo kwenye eneo la Tarakilishi. Ujuzi wake wote  wa kwenye  teknolojia na habari aliitumia hapo kuweza kutafuta kile ambacho alikihitaji, muda ambao Norbert bado yupo ndani ya ukumbi yeye alishafanikiwa kuingilia mtandao wote wa kampuni ya mapato  Tanzania.  Alikuwa ni muingiliaji mzuri haswa wa mitandao ya watu(Hacker), kiasi cha kuweza kupara taarifa zozote muhimu azitakazo ndani ya wasaa wowote ule bila ya kujulikana. Tarakilishi yake ilikuwa na ulinzi wa hali ya juu kiasi cha kwamba hata akiamua kufuatiliwa kwa kuingilia tovuti za watu wengine, ingekuwa ni ngumu kuweza kupatikana.

        Hadi majira hayo alishabaini  wamiliki wa gari ile iliyokuja pale uwanja wa ndege  kwa siku mfululizo kuchukua watalii, haikuwa gari binafsi wala iliyokuwa ikihusika na utalii. Ndiyo maana aliiwekea shaka na kuchukua picha zake, lengo kubwa ilikuwa apate namba za usajili. Hizo ndiyo zimemfanya hadi aingie kwenye tovuti ya mamlaka ya mapato(TRA) na kuweza kutafuta usajili wake, sasa ameupata na ameunakili kitabuni. Ilikuwa ni gari inayomilikiwa na kampuni ya kukodisha magari hapa nchini iliyo na makazi yake  makuu Kibaha mkoani Pwani na ofisi ndogo katikati ya jiji la Dar es salaam. Baada ya kupata hilo aliweza kuingia kwenye tovuti  ya kampuni hiyo ya ukodishaji magari iliyojitenga nje ya mji na kuipekua vilivyo, hii hakumaliza  kwani waliyopo kwenye maono yao waliweza kujua kuna mtu anapitia taarifa zao. Hapo mtandao mzima ulipotea hewani kimaajabu tena ukiwa umelenga na kuua Tarakilishi yake kabisa ikiwa namba muhimu zitajulikana za kifaa hicho, hilo lilishindikana kwasababu ni kifaa chenye ulinzi kupitiliza. Hivyo wakawa wamemnyima wasaa wa kuweza kiundani zaidi, kupitia kuingia kwa muda mchache aliweza kunasa vichache ikiwemo watu muhimu waliyopo nyuma ya uongozi wa  tovuti hiyo.

      Tayari alishaandika majina yao pamoja na anuani zao kwenye kitabu hicho, kilichokuwa kipo kichwani ni kuwaendelea kwa mwendo ambao si  wa kivita. Hakuwa na ujuzi nao hadi aingie kinamna nyigine kwao, alihitaji kuwaingia kwa namna ambayo ingemfanya weze kunasa vitu muhimu.

"Huu ni mwanzo tu nyinyi, tena ninaanza na wewe jioni ya leo" Alisema huku  akiweka alama kwenye jina mojawapo ambalo lipo juu kabisa ya karatasi yake, alipomaliza kuiweka tu hilo jina barua pepe iliiingia kwenye tarakilishi yake na kutoa mlio kutokana na kuiweka proramu maalum ya baruapepe.

"Enheee!" Alijisemea


ITAENDELEA!!







WAKATI  TUNAANZA KWA PAMOJA RIWAYA HII, PIA TUNAPENDA TUWAJULISHE YA KWAMBA, RIWAYA NYINGINE  YA NORBERT KAILA TOLEO JIPYA INAPATIKANA  NDANI YA PROGRM YETU PENDWA YA SIMU YA ANDROID IITWAYO HADITHIAPP. INAITWA RALOND NA DESMOND KWA BEI NAFUU TU, PIA RIWAYA YA  SHUJAA AMBAYO ILIWAHI KUKATISHA KWENYE  BLOGU YETU  IPO HUKO UTAUPATA MWENDELEZO WAKE KWA BEI NAFUU. KAMA NI MDAU  WA BLOGU MARIDHAWA, HAKIKISHA UNA  PROGRAMU HII UWEZE KUJISOMEA. KUJIPAKUA FUATA LINK HII>>>>> https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi

No comments:

Post a Comment